Uchaguzi Wa Masoko Mahalia (Local Real Estate Markets)

Aliko Musa

Senior Member
Aug 25, 2018
156
240
Utangulizi
Soko mahalia ni jumla ya shughuli za kununua na kuuza viwanja, mashamba na majengo ndani ya eneo husika. Soko mahalia la wilaya ya Mbeya mjini hutofautiana na wilaya yoyote iliyo nyanda za juu kusini.

Soko mahalia kwenye wilaya moja ni tofauti kabisa na soko mahalia kutoka wilaya zingine ndani ya mkoa mmoja. Ukweli huu unasisitiza juu ya kufokasi kwenye soko mahalia lako bila kuzingatia uzoefu ulionao kutoka katika wilaya zingine.

Rafiki yangu, haiwezekani kujenga utajiri bila kufahamu kwa undani kuhusu soko lako mahalia. Hapa nina maana kuwa kama unawekeza katika wilaya ya Mbeya jiji, unatakiwa kujifunza soko lake kwa vitendo.

Katika kila mkoa kuna fursa nyingi za uwekezaji wa ardhi na majengo ambazo zinaweza kukutoa kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine nzuri zaidi.

Usijisumbue kuwekeza mikoa ya mbali hasa kama bado uwekezaji wako haujafikia hatua ya kuingiza kiasi kikubwa cha kipato endelevu.

Usitake uwekezaji mbali (long-distance real estate investment) ukiwa unaanza. Ukifanya hivi uwezekano wa kushindwa ni mkubwa sana ukilinganisha na uwekezaji wa kushinda.

Kwanini Uwezekano Wa Kushindwa Ni Mkubwa Unapowekeza Mikoa Ya Mbali?.

Jibu; sababu ni moja tu. Sababu yenyewe ni kujenga na kupata timu bora sana.

Ili uweze kujenga utajiri au kutunza utajiri kupitia ardhi na majengo ni lazima uwe na timu bora na mtandao wa watu sahihi. Hii kitu ni lazima na kipo ndani ya uwezo wako.

Lakini kuwekeza kwenye soko zuri sana sio lazima na kulifanya soko liwe zuri ipo nje ya uwezo wako.

Hebu nikukumbushe kitu kimoja muhimu sana kwenye safari yako ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Kumbuka: Timu bora na mtandao wa watu sahihi ni jambo la muhimu sana kuliko hata kuchagua soko la linalolipa sana.

Hii ni kwa sababu timu bora na mtandao sahihi utakusaidia kupata kiwanja au jengo linalolipa hata iwe kwenye wilaya yenye hali mbaya ya soko mahalia.

Lakini, timu mbovu na mtandao wa watu wasio sahihi haiwezi kukusaidia kupata kiwanja au nyumba inayolipa hata iwe mnawekeza kwenye wilaya yenye hali nzuri ya soko mahalia.

Hatua 3 Za Kuchagua Wanatimu Wako
1.
Orodhesha mambo yote ambayo unayafanya au utafanya kwenye mchakato wote wa kuwekeza kwenye ardhi na majengo.

Orodhesha kila kitu. Hii ni muhimu sana kulifanya.

2. Orodhesha madhaifu yako yote na maeneo ambayo wewe ni bora sana. Orodhesha kila jambo kwenye eneo hili. Kuwa mkweli wa nafsi yako rafiki yangu.

3. Tofautisha mambo unayopenda kufanya na mambo ambayo hupendi kufanya.

Muhimu: ongeza watu ambao watakuwa bora sana kwenye kufanya mambo ambayo ni madhaifu yako na hupendi kufanya.

Kwanini Unatakiwa Kufokasi Kwenye Wilaya Moja Au Kata Moja Tu?.

Kwa sababu urahisi wa kujenga timu bora sana na mtandao wa watu sahihi. Kumbuka mtandao wa watu sahihi na timu bora ni muhimu sana kuliko hata soko zuri la ardhi na majengo.

Unapowekeza wilaya nyingine ndani ya miaka miwili au mmoja toka umiliki kiwanja cha kwanza au nyumba ya kwanza unajiweka kwenye hatari kubwa. Hatari ya kujenga timu bora sana na mtandao wa watu sahihi ndani ya wilaya unapotaka kuwekeza kwa sasa tofauti na mwanzo.

Mambo 3 Ya Kuzingatia Kwenye Uchaguzi Wa Kata Ya Kuanza Kuwekeza

Sababu 3 muhimu zaidi zinazoathiri hali ya soko mahalia katika kata unayotaka kuanza kuwekeza ni kama ifuatavyo:

1. Hali ya ajira
Ajira za kudumu kwa miaka mitano (5) au zaidi. Hii ni kwa sababu mbinu ya kujenga utajiri kupitia ardhi na majengo ni kumiliki ardhi au majengo kwa muda mrefu (angalau miaka 10) bila kuuza.

Mbinu nyingine (kununua na kuuza viwanja, kununua na kuuza majengo, n.k) zinaweza kukusaidia kujenga utajiri. Lakini mimi Aliko Musa, mbobezi kwenye ardhi na majengo ninaamini kwenye kumiliki ardhi au majengo kwa angalau miaka 10 ndiyo njia bora sana ya kujenga utajiri kupitia ardhi na majengo.

Ajira unazoweza kuziangazia ni miradi ya ujenzi wa barabara, ujenzi wa viwanda na umeme, miradi ya kilimo cha muda mrefu kama kilomo cha mpunga huko Usangu jijini Mbeya. Miradi mingine ni ujenzi wa viwanja vya ndege na viwanja vya mpira wa miguu endapo vitachukua muda wa zaidi ya miaka mitano.

Pia, uchimbaji wa madini katika wilaya tofauti tofauti. Lakini iwe inachukua zaidi ya miaka mitano. Ajira hizi hupelekea ongezeko la uhamiaji wa watu kutoka katika maeneo mengine ya nchi.

Watu wanapofuata ajira katika kata unayotaka kuwekeza, hupelekea ongezeko la uhitaji wa nyumba za kupangisha. Hii hupelekea uwepo wa fursa za kumiliki nyumba za kupangisha zinazolipa sana.

2. Idadi ya nyumba za kupangisha zilizopo
Uwepo wa idadi ndogo za nyumba katika kata unayotaka kuwekeza hupelekea uwepo wa fursa kubwa sana kwa nyumba za kupangisha.

Kwa sababu chanzo cha wapangaji kitakuwepo kwa zaidi ya miaka mitano, unaweza kujenga nyumba ya kupangisha na ikakulipa. Hii inakuwa ni kweli endapo utaweza kutumia kanuni ya 2%.

3. Nyumba za gharama nafuu.
Unatakiwa ufanye tathmini endapo kuna idadi ya kukidhi mahitaji ya wapangaji kulingana na wastani wa kipato chao.

Ili uweze kulifahamu kwa undani zaidi soko lako unatakiwa kwenda mtaani kutafuta taarifa zinazoweza kukusaidia.

Acha kukaa kwenye kompyuta masaa kumi ukisoma makala zangu au vitabu vyangu.

Weka uwiano sawia katika kujifunza kwa vitendo na kujifunza kutoka kwenye makala, vitabu na masomo. Haiwezekani kufahamu hali ya soko mahalia ya kata yako kwa kusoma kutoka katika makala, semina za mtandaoni na vitabu vya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Hii ndiyo sababu ninasisitiza kwenye kutumia kanuni za uwiano za 100:10:3:1 na 30:10:3:1. Rafiki yangu, naomba uzingatie haya mambo ya muhimu sana kwenye safari yako ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo mengine.
 
Back
Top Bottom