Tunataka Kujenga Taifa la Wote, kwa Maslahi ya Wote

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Hifadhi ya jamii kwa wote (Pensheni, mikopo na bima ya afya) - Mawazo ya ACT Wazalendo

Huduma mbovu za Afya ni chanzo kikubwa cha umasikini wa Watanzania. Kwa mujibu wa tafiti za Benki ya Dunia, watanzania wengi wapo juu kidogo au chini kidogo ya mstari wa umasikini. Hivyo, Wakipata changamoto za afya walio juu ya mstari wa umasikini hurudi chini na walio chini huenda chini zaidi.

Bima ya Afya ni nyenzo muhimu sana kuzuia watu kudumbukia kwenye umasikini. Mfumo wetu wa Bima ya Afya wa sasa ni mfumo wa kitabaka ambao unatoa huduma kulingana na uwezo wa mtu badala ya kulingana na mahitaji yake. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeweka utaratibu wa vifurushi ili wenye uwezo kifedha walipe zaidi wapate Huduma bora na wasio na uwezo mkubwa wapate Huduma zenye ubora wa chini. Mfumo huu unaimarisha matabaka nchini na kujenga mataifa 2 ndani ya Nchi moja katika Huduma za Afya.

Bajeti ya Serikali ya mwaka huu 2023/24 haijalitazama tatizo hili na kutenga fedha ili kuweka mfumo mzuri na endelevu wa kufadhili Bima ya Afya kwa Watanzania wote. Sisi, tumekuwa na msisitizo wakati wote wa kuitaka Serikali kuwekeza fedha kwenye Mfumo utakaoimarisha afya ya watanzania kwa kuwezesha kugharamia matibabu kwa watu wote nchini bila kuweka matabaka.

Mfumo ambao tumekuwa tukipendekeza ni ule wa Bima ya Afya iliyofungamanishwa na Mfumo wa Hifadhi ya Jamii.

Tunataka mfumo unaomfanya mtu alipe bima kulingana na uwezo wake lakini apate huduma kulingana na mahitaji yake. Hali ya sasa katika upatikanaji wa huduma bora za afya kwa sehemu kubwa umekuwa ukitegemea uwezo wa kifedha wa Mwananchi kununua huduma hiyo badala ya uzito wa ugonjwa.

Hali ya watanzania kuhusu Hifadhi ya Jamii na Bima ya Afya kwa Mujibu ya takwimu rasmi zinaonyesha kama ifuatavyo;

Watanzania watu wazima milioni 1.8 tu ndio wapo kwenye mfumo wa hifadhi ya jamii (Wanachama wa NSSF na PSSSF) wanaohudumiwa na bima ya afya. Wanachama wa NSSF wanapata Fao la SHIB na Wanachama wa PSSSF hupaswa kukatwa 3% ya mishahara yao kulipia NHIF ili kupata Bima ya Afya.

Watanzania Watu wazima milioni 7.4 wapo juu kidogo ya mstari wa umaskini na wapo kwenye sekta isiyo rasmi. Baadhi yao wanajilipia Bima ya Afya, Lakini wengi licha ya kuwa na kipato hawana Bima hivyo wakitikiswa kidogo wanaangukia chini ya mstari wa umasikini.

Watanzania Watu wazima milioni 8 wapo chini ya mstari wa umaskini ambao baadhi yao wapo kwenye mfumo wa kunusuru kaya maskini (TASAF). Hawa hawana Bima ya Afya kabisa wala Akiba katika Hifadhi ya Jamii

Pendekezo la ACT Wazalendo ni kuanzisha Mfumo wa Hifadhi ya Jamii ambapo utapanuliwa kutoka kwenye kundi dogo la watu wazima milioni 1.8 hadi Watu milioni 17.2 kwa sasa ili kuhakikisha watanzania wote wanakuwa na bima ya afya.

Mfumo huu endelevu wa Hifadhi ya Jamii utakaofungamanishwa na Bima ya Afya kwa Wananchi wote unapendekezwa kujengwa kwa namna ifuatayo;

i. Kwa wananchi Karibu milioni 1.8 ambao sasa ni wanachama wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii: Asilimia 20 ya michango yao kwenye mifuko ya NSSF au PSSF itapelekwa NHIF kwa ajili ya Bima ya Afya. Wanachama wa PSSSF hawatakatwa tena makato ya NHIF kutoka mishahara yao bali mchango wao kwenye mfuko huo huo utawapa Fao la Matibabu.
Wanachama wa NSSF watapata Fao la SHIB kupitia NHIF.
Hivyo kadi ya NSSF/PSSSF itakuwa ni kadi ya NHIF.

ii. Kwa wananchi ambao wapo kwenye sekta isiyo rasmi ambao wana vipato vya kuweza kuchangia (hawa wanakadiriwa kuwa watanzania milioni 7.4 ): Serikali itoe motisha kwa kuwachangia shilingi 10,000 Katika Shilingi 30,000 ya mchango wa kila Mwezi. Hivyo Mwananchi atajiwekea Akiba ya Shilingi 20,000 kila Mwezi na Serikali itamwongezea Shilingi 10,000.

iii. Kwa wananchi ambao ni maskini, wanaoishi chini ya mstari wa umasikin (watanzania milioni 8), Serikali iwachangie kwa asilimia 100 kwenye Mfumo wa Hifadhi ya Jamii, Shilingi 30,000 kila Mwezi.

Kupitia pendekezo letu, kitakwimu tunaenda kuwa na matokeo yafuatayo;

Jumla ya Watanzania watu wazima Milioni 17.2 watakuwa wanachama wa Mfumo wa Hifadhi ya Jamii na moja kwa moja watanufaika na Fao la Bima ya Afya.

Watanzania wote milioni 61 watapata bima ya afya kwa kanuni ya kawaida ya mchangiaji mmoja na wategemezi watano (Mwenza na wanufaika).

Mfumo ya Hifadhi ya Jamii utakuwa na jumla ya michango ya Shilingi trilioni 8.5 kwa mwaka kwa mchanganuo ufuatao.

o Shilingi trilioni 2.7 kutoka kwa wanachama wa sasa waliopo kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

o Shilingi trilioni 2.9 kutoka wanachama watakaojiunga kwa utaratibu wa hiyari (wanachama milioni 7.4)
o Shilingi trilioni 2.8 kutoka kwa wanachma wanaochangiwa asilimia 100 na Serikali (Watanzania milioni 8)

20% ya michango ya Hifadhi ya Jamii itaenda kugharamia Bima ya Afya Sawa na Jumla ya shilingi trilioni 1.7
Serikali itatumia shilingi trilioni 3.88 kila mwaka kugharamia Hifadhi ya Jamii

Kwahiyo, ili kutekeza hili Serikali inapaswa kutenga fedha sawa na 2.5% ya Pato la Taifa kugharamia Mfumo wa Hifadhi ya Jamii kwa wote ambao una Fao la Matibabu kwa wanachama wake.

Kwa Mfumo huu kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya isiyo na matabaka wala ubaguzi. Hapatakuwa na vifurushi vya Bima. Kila mtu atapata Huduma ya Afya ya ubora wa Juu kabisa bila kujali hali yake ya kipato.

ACT Wazalendo inataka kujenga Taifa la wote kwa Maslahi ya wote.
 
Back
Top Bottom