Tumeweza uvumilivu, Tunahitaji Ujasiri!

Mbelwa Germano

JF-Expert Member
May 7, 2011
789
289

Tumeweza uvumilivu, Tunahitaji Ujasiri!


Kutambua ukweli ni moja ya msingi muhimu kabisa wa maendeleo. Kimsingi maendeleo si tu kuwa na mali, katika ngazi ya mtu mmoja mmoja maendeleo ni pamoja na kuwa na maarifa,ujuzi,uhuru,ubunifu,heshima,uwajibikaji na utu.

Kutopenda kuambiana ukweli hupotosha wajibu tulio nao wa kutumikia fikra zetu kufuatana na ujuzi halisi wa mambo na hali ya mazingira yetu. Jambo la muhimu tunalopaswa kutambua ni kwamba, kila binadamu anafanya makosa lakini hatupaswi kujiridhisha na makosa yetu bila kutumia fikra zetu kutafuta ufumbuzi mkubwa kusahihisha makosa yetu. Ukweli hautaki kupuuzwa hivyo tusijidanganye wenyewe na kujiridhisha kana kwamba matatizo na shida zetu hazihitaji fikra za juu zilizojaa hekima, ubunifu, uadilifu na busara.

Lakini, ieleweke kwamba ukweli haupatikani bure, lazima jamii ijenge utamaduni wa kupenda kupata taarifa kwa maana ya kupata maarifa na hili linawezekana kama tutakuwa na uhuru wa kifikra na utashi wa kutokuwa na unafsi.

Ipo mitazamo mbambali kuhusu maana ya neno siasa kulingana na makundi mbalimbali katika jamii yetu. Wapo wanaotazama siasa kama porojo, uzushi, kejeli na usanii. Si ajabu kusikia kijana mtaani anamwita mwenzake “acha siasa zako” akiwa na maana acha uongo au uzushi, hii inatokana na matendo ya wanasiasa wetu kuhubiri maneno yasiyoendana na matendo. Wapo wanaohusisha siasa na uchawi, ikiwa na maana bila uchawi hakuna siasa, “siasa mchezo mchafu”, kwa sababu wanasiasa wanafanya siasa kwa ajili ya matakwa yao na si ya jamii inayowazunguka. Kinachofanyika ni kufanya mabadiliko ya juu juu (cosmetics changes) kujaribu kuziba mirija ya ufahamu ya wananchi.

Lakini mara nyingine siasa hizi zina uhusiano wa moja kwa moja na kuwa na jamii dhaifu ambayo haipendi kutambua ukweli juu ya matatizo yake ili kuweka mipango inayotekelezeka. Na jamii hii inaweza kusambaratishwa kifikra kwa kutumia wingu la udini, ukanda, ukabila. Lakini vilevile tuna wasomi wenye akili timamu ambao hupotosha maana halisi ya siasa, wanachoshindwa kutambua ni kwamba siasa ni elimu, maarifa na ujuzi ambao hutoa msimamo na msingi wa jamii, kila jamii huwajibika kufuata misingi iliyowekwa katika maisha ya kila siku, hivyo matokeo na maamuzi ya kuchagua, kulinda, kuhifadhi mfumo mbovu au mzuri wa utawala ni matokeo ya jamii husika. Baadhi ya wasomi ambao tunaamni kabisa wana nyenzo muhimu (elimu) ambayo inaweza kuleta mapambazuko ya kifikra, kisiasa na kiuchumi katika jamii wanatumikia zaidi matumbo yao kuliko mahitaji ya jamii inayowazunguza.

Katika miaka ya hivi karibuni Taifa letu limekuzwa katika propaganda na kuwafanya watu waishi kwa matumaini katikati ya mateso ya unyonyaji ndani ya taifa hili. Babu zetu walidanganywa na wakoloni weupe kwa kupewa vitu vidogovidogo na kuuza ardhi ya bara hili ambayo imekombolewa kwa damu nyingi, wakoloni weusi wanadanganya raia wenzao kwa vitenge, kofia, maneno mepesi n.k. Swali la muhimu tunalopaswa kujiuliza: Je, tunapaswa kuendelea na utamaduni huu katika kukidhi changamoto za nyakati? Je, viongozi wa Taifa hili wameamua kuasi maadili ya uongozi, kutofuata utawala wa sheria na kuunda azimio la rushwa lisilo rasmi? Je, viongozi wa Taifa hili wameamua kuua baadhi ya mashirika ya umma, wameuza viwanda, ili kusubiri bomu la ajira kwa vijana lilipuke? Je waliuza nyumba za serikali ili kupunguza au kuongeza gharama za serikali?

Labda tujiulize maswali mengine ya ziada; Kwa kuwa bei za vyakula zinazidi kupanda kila siku, je lengo la kilimo kwanza lilikuwa ni kupandisha gharama za vyakula au kupunguza? Kwa kuwa kilimo ndiyo sekta muhimu inayoajiri vijana wengi Tanzania, tumeamua kudidimiza kilimo kwanza ili bomu la ajira lilipuke?

Ndugu Msomaji jambo la kufurahisha zaidi, taifa letu la Tanzania lina bahati ya kupata viongozi wenye akili timamu ambao wanapima ubora wa elimu kwa kuzingatia wingi wa vitendea kazi au kujua kuongea Kingereza. Watu hawa wenye akili timamu baadhi yao wamepelekwa kwa kodi za wananchi masikini wa Tanzania kwenda kusoma ulaya, Je, kwa kuwa asilimia zaidi ya 80% ya wanafunzi wa kidato cha nne wanafeli, wingi wa shule za kata ulilenga kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofeli kidato cha nne au kupunguza? Au bomu litakapolipuka tuseme tulijua ila tulijisahau?

Ikiwa umechagua fedha kuongoza taifa letu la Tanzania badala ya watu wenye fikra pevu, uadilifu na busara je, unapaswa kuvumilia maamuzi yako? Ikiwa uliweza kupiga makofi na vigelegele kupuuza hoja za watetezi wa haki za msingi za raia, je unapaswa kuendelea kulalamika hovyohovyo? Kama tumepuuza msingi wa kufanya michakato ya kupata viongozi bora na kuchagua pesa kutuchagulia viongozi, je unapaswa kuendelea kulinda maamuzi yako.

Naomba nimalize kwa kusema maneno yafuatayo; kutambua ukweli ndio njia ya kuamsha fikra na kuamini matendo chanya, kukubali ukweli wa maisha na kupambana kubadilika kuelekea kwenye mafanikio zaidi. Lazima kwanza tukiri kwamba tuna matatizo makubwa na sio changamoto na tunapaswa kubatiza Taifa letu upya na kupata viongozi wenye upeo, maono na uadilifu. Taifa letu linahitaji fikra za mabadiliko kuanzia kung’oa mfumo wa utawala unaolinda mafisadi kuelekea fikra za uzalendo zinazong’oa dhulma ya uharibifu wa mali za umma, uhuru ulio huru unaozingatia haki za raia kulinda tunu za taifa na uwajibikaji, kueneza fikra na njia mwafaka zenye tija (practical and workable solutions) pamoja na kujenga jamii yenye filkra pana.


Nawakilisha.
 
Back
Top Bottom