Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,331
- 33,147
Vyombo mbalimbali vya habari nchini, jana vilitanda kwa habari nzito na ya kustusha kwamba askari mmoja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wa kikundi cha wahalifu kilichokuwa kimejichimbia katika mapango ya Amboni mkoani Tanga.
Mbali ya kuuawa kwa askari huyo, pia askari wenzake wawili na polisi watatu walijeruhiwa katika mapambano hayo yaliyoelezwa kuwa yalidumu kwa takriban saa 48 katika maeneo ya maporomoko ya Mikocheni, kijiji cha Amboni umbali wa kilomita 10 kutoka jijini Tanga.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, alithibitisha kujeruhiwa kwa askari polisi watatu, askari wa JWTZ wawili na mmoja aliyefariki; na kwamba majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo.
Chagonja alisema askari wanaendelea na operesheni ya kuwatafuta watu hao wanaodaiwa kujichimbia kwenye mapango hayo ya Amboni.
Kwa mujibu wa Chagonja, hadi kufikia juzi walikuwa wamekamatwa watu watatu wakiwa na silaha za jadi zikiwamo mishale, pinde na mikuki.
Kwa hakika, hali hiyo siyo tu inaleta wasiwasi kwa wakazi wa eneo la Amboni, bali pia inaweza kuzua hofu kubwa kwa usalama wa maeneo mengine nchini. Ni imani yetu kuwa jitihada zinazoendelea sasa jijini Tanga kwa ushirikiano wa pamoja wa polisi na vyombo vingine vya usalama zitazaa matunda na mwishowe wahalifu wote watadhibitiwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Hata hivyuo, pamoja na imani yetu hiyo, sisi tunadhani kwamba ipo haja kwa jeshi letu la polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukulia tukio hili kuwa ni sehemu ya kutuzindua ili tuongeze nguvu zetu maradufu katika kukabili uhalifu nchini.
Hii inatokana na ukweli kuwa katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na matukio kadhaa ya vituo vya polisi kuvamiwa na majambazi, askari kuuawa na silaha kadhaa kuporwa, zikiwamo za kivita kama Sub Machine Gun (SMG).
Tukio la hivi karibuni lilikuwa ni la polisi wawili waliokuwa doria jijini Tanga kuvamiwa na majambazi wenye visu na kisha kuporwa bunduki mbili aina ya SMG zinazodaiwa kuwa kwa pamoja zilikuwa na risasi takriban 60. Taarifa zilieleza kuwa mmoja wa polisi waliokumbwa na tukio hilo alilazwa hospitali baada ya kuchomwa kisu na majambazi hao.
Siku chache kabla ya taarifa za tikio la askari kuporwa bunduki wakiwa doria jijini Tanga, kulitokea uhalifu mwingine wa kutisha kwenye kituo cha polisi Ikwiriri, Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Majambazi wanaokadiriwa kufikia 10 wakiwa na silaha za aina mbalimbali za moto na jadi, waliwaua askari wawili pamoja na kupora silaha saba na kulipua bomu katika kituo hicho.
Askari polisi waliouawa katika tukio hilo ni PC Judith Timoth na Koplo Edgar Mlinga. Na hadi sasa, hakuna taarifa za kina juu ya kukamatwa kwa watu waliohusika na uhalifu huo licha ya jeshi la polisi kuahidi zawadi nono ya Sh. milioni 20 kwa yeyote atakeyewezesha kukamatwa kwa majambazi waliotenda unyama hao.
Tukio hilo lilikuwa ni mfululizo wa matukio mengine mawili yaliyohusisha uvamizi kwenye vituo vya polisi katika kipindi kifupi kisichozidi miezi saba. Awali, Juni 11, 2014, watu wasiojulikana walivamia Kituo kidogo cha Polisi Mkamba kilichoko katika Wilaya ya Mkuranga na kuua askari polisi mmoja pamoja na mgambo. Askari aliyeuawa katika tukio hilo ni D 9889 Koplo Joseph Ngonyani huku mgambo akiwa ni Venance Francis, aliyefariki wakati akitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) huku askari Mariamu Mkamba, akijeruhiwa lakini alitibiwa na kupona.
Katika tukio hilo, majambazi yalipora bunduki mbili aina ya SMG, tatu aina ya shotgun na magazini 30 zilizokuwa kwenye ghala la muda zikisubiri kupelekwa kwenye kituo kikubwa chenye ghala kuu la silaha.
Kwa mara nyingine, Septemba, 2014, majambazi yalivamia Kituo Kikuu cha Polisi kilichoko katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na kuwaua askari wawili na kuwajeruhi wengine watatu.
Vilevile, majambazi hayo yalifanikiwa kupora bunduki 10 aina ya SMG, risasi ambazo idadi yake haikutambulika na pia mabomu ya kutupa kwa mkono.
Kutokana na mfululizo wa matukio haya, NIPASHE tuliwahi kuhoji katika tahariri yetu ya ........ kwamba je, kulikoni hivi sasa uvamizi huu umehamia kwenye vituo vya polisi? Kulikoni vituo hivyo vinavyotegemewa kuwa kimbilio la wananchi kwa ajili ya usalama wao na mali zao vigeuzwe kuwa dango la majamabzi kujitwalia silaha kwa ajili ya shughuli zao za kihalifu?
Tulieleza hofu yetu kwamba isije ikawa mfululizo wa matukio hayo ni ishara ya kuwapo kwa kikundi fulani cha watu, wenye malengo fulani ya kihalifu, wangali wakijipanga kwa kujikusanyia silaha hizo nzito za polisi kwa sababu wanazozijua wao.
Sisi tunaamini kwamba kwa muda wote wa kuibuka kwa vitendo hivi vya kihalifu, bado kuna mahala tutakuwa hatujapafanyia kazi vizuri. Ni dhahiri vile vile kuwa zipo dalili za kuwapo na mwanya kwa wahalifu kutenda watakayo huku sisi tukiendelea kutoa majawabu mepesi.
Tunafikiri kwamba jeshi la polisi na vyombo vingine vinavyohusika moja kwa moja na usalama wa raia na mali zao kujipanga zaidi ili kutuhakikishia usalama wetu.
Kwa mfano, sisi tunadhani kwamba Mkuu wa Jeshi la Polisi ana wajibu wa kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kuongeza uwajibikaji wa askari wetu. Taarifa za majamabzi kuwapora askari silaha nzito za moto kwa kutumia visu haziashirii mwelekeo mzuri.
Tunaingiwa hofu kwamba pengine, silaha zile zile zilizoporwa kwa askari wetu zinaweza pia kuangukia mikononi mwa wahalifu kama hawa waliobukia Amboni Tanga na kutishia usalama wa raia na mali zao.
Ni kwa kuzingatia yote hayo, ndipo tunapoona kwamba sasa, tukio hili la Tanga lichukuliwe kama sababu ya kutufungua macho katika kuhakikisha kwamba usalama wetu uanendelea kuwa wa uhakika na kamwe hatubabaishwi na wahalifu wa aina yoyote ile.
Mathalan, tumeelezwa kwamba katika tukio la Amboni (Tanga), taarifa za kuwapo kwa silaha kwenye mapango hayo zilitolewa na raia wema kwa polisi na ndipo vyombo vya dola vilipofuatilia na kuanza kuchukua hatua.
Sisi tunajiuliza, silaha zote hizo zilipita vipi hadi kufikishwa katika mapango hayo ya Amboni pasipo vyombo vyetu vya usalama kuzibaini na kuwakamata wahusika kungali mapema? Ni baadhi ya maswali yanayopaswa kuwa chanzo cha kuongeza umakini.
Pamoja na yote yanayotokea, sisi tunaamini kwamba bado taifa letu lina vyombo imara vya kutuhakikishia ulinzi na usalama. Isipokuwa, ni wazi kwamba kuna mahala tumeteleza na hivyo ni wajibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama na wadau wengine kuangalia kwa kina ni wapi pana tatizo na kutafuta majawabu ya kweli yatakayoondosha tishio lolote la usalama.
CHANZO: NIPASHE