Tatizo la Ugumba kwa wanaume la zidi kuwa kubwa

kbm

JF-Expert Member
Oct 5, 2012
5,222
1,670
Moshi. Kama unadhani tatizo la ugumba ni la wanawake zaidi unajidanganya, kwani kliniki iliyoanzishwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, sasa inapokea wagonjwa kati ya 25 hadi 30 kwa wiki, wakiwamo wanaume.

Dk Thomas Kakumbi, ambaye ni mkuu wa kitengo maalumu kinachoshughulikia matatizo ya uzazi, anasema wanaume wasijidanganye kuwa kama wanaweza kufanya tendo la ndoa kwa muda mrefu basi hawawezi kuwa na tatizo la kutungisha mimba.

“Unaweza kufanya tendo la ndoa hata mara tano kwa siku bado mbegu zako zinaweza zisiwe bora kutungisha ujauzito,” anasema.

Dk Kakumbi, ambaye ni daktari bingwa katika matatizo hayo ya uzazi alibainisha hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi, akisema tatizo hilo ni kubwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Manyara na nchi jirani.

“Tatizo la mbegu na kutungisha mimba linachangiwa na makundi yote, mume na mke. Sisi wanaume hatujui tunachangia sawa kabisa na wanawake kwenye changamoto hii, labda kwa sababu tu ya uvivu wa wanaume kufanya vipimo, kwa wale wengi tuliowafanyia vipimo, inatuonyesha changamoto ni kubwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema wanaume wengi hawafahamu au hata kukubaliana na tatizo hilo, wakidhani kutungisha mimba ni kuwa na uwezo wa kufanya tendo la ndoa tu.

Kiini cha tatizo la ugumba

Kwa mujibu wa Dk Kakumbi, tatizo la ugumba lina sababu nyingi ambazo zinaweza kusababisha utasa, kwani utasa ni mtu hawezi kabisa kutungisha mimba ila ugumba anaweza.

“Maneno ugumba na utasa yanatumika kwa kuchanganywa na mara zote yanajaribu kumaanisha kitu kimoja wakati si kweli. Ugumba ni mtu kushindwa kupata ujauzito baada ya kuwa amekaa kwa muda usiopungua miezi 12 akishiriki tendo la ndoa bila kinga yoyote.

“Utasa ni mtu ambaye hawezi kabisa kubeba ujauzito, hawezi kabisa kutungisha ujauzito. Kwenye changamoto za uzazi hatumchukui mtu mmoja peke yake. Tunawachukua kama wanafamilia mke na mume.”

Anasema ili kuweka urahisi zaidi wa kuzijua sababu, zinagawanywa katika makundi matatu au manne.

“Kundi la kwanza ni sababu zinazomhusu mwanamke peke yake. Aina ya pili ni ile ambayo inatokana na mwanamume kama hana uwezo wa kutungisha.

“Aina ya tatu ni ile ambayo mwanamke ana sababu kadhaa zinasababisha ugumba na mwanamume ana sababu kadhaa zinazosababisha ugumba au wote kwa pamoja wanachangia kwenye changamoto ya kupata ujauzito na kundi la nne tunaita halielezeki,” anasema.

Anasema katika kundi hilo, mtu anakuwa amepima vizuri na kuonekana hana changamoto yoyote, lakini bado wanashindwa kupata ujauzito.

Ukubwa wa tatizo

Akizungumzia ukubwa wa tatizo, Dk Kakumbi anasema tatizo la ugumba ni kubwa na takwimu zilizochapishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) Aprili 13, 2023 zinaonyesha kwa kila familia sita, moja imeathiriwa na tatizo hilo.

Tatizo hili linaenda mbali zaidi kwa sisi tunaokaa kliniki na kuona na hiyo ni kwa ujumla kwa watu wote kwa jamii nzima.

“Lakini kwa wale ambao wanapata nafasi ya kuja kumuona daktari kwa matatizo ya uzazi kwa siku za karibuni, kwa kila wagonjwa watano, walau wawili au watatu kati yao wakati mwingine wanaweza kuwa na tatizo la kutopata mtoto.”

Ameshauri kufanyika kwa utafiti zaidi ili kujua undani wake na kwamba katika hospitali hiyo wameanzisha hospitali maalumu kwa ajili ya utafiti huo baada ya kuongezeka kwa watu wenye tatizo hilo.

“Unakwenda kliniki kwa siku unaona wagonjwa 15, kulingana na uasili ama utaratibu ambao unatumika kupata maelezo ya mtu mwenye tatizo la uzazi, inahitaji muda, uvumilivu, usiri na daktari uwe na muda mtu akuelezee mahangaiko yake.

Tiba inayopatikana KCMC

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mojawapo ya matibabu kuna aina kadhaa za matibabu na akaziweka katika makundi makubwa matatu.

“Kundi la kwanza ni matibabu yanahitaji tu ushauri. Kuna watu ambao wanakuja unazungumza nao unagundua hawakuwa na ufahamu ni siku gani baada ya mzunguko wa hedhi anatakiwa akutane na mwenzake ili kupata ujauzito.

“Kwa sababu kitaalamu ziko siku takribani tano tu ndani ya mwezi mzima ambazo unaweza kupata ujauzito.

“Wengine wanahitaji vidonge vya kupevusha mayai kujaribu ku balance homoni zao ili zikae vizuri. Lakini wengine tunaenda mbali zaidi na kufanya upasuaji, kitaalamu tunaita diagnostic laparoscope,” anasema Dk Kakumbi.

Anasema njia hiyo inatumika katika maeneo mawili kuweza kuangalia mirija iliyoziba kama mojawapo ya changamoto na pia inatumika kutibu kwa sababu wakati unapoangalia mirija iliyoziba kuna uwezekano pia wa kufanya jaribio la kuzibua.

Kwa wanawake wenye uvimbe kwenye kizazi, anasema huwafanyia upasuaji wa kuutoa na wanaweza kupata watoto kabisa.

Upandikizaji mimba KCMC

Kwa mujibu wa Dk Kakumbi, ambaye ni mbobezi katika matatizo ya uzazi katika hospitali hiyo ya KCMC, anasema njia ya tatu ni upandikizaji mimba kiteknolojia.

Kuhusu upandikizaji wa kuweka mbegu zilizosafishwa vizuri kwenye mji wa mimba, anasema zaidi ya asilimia 45 ya mbegu za kiume zinazotolewa zinaweza kuharibiwa kwa sababu tu ya mazingira kutokuwa rafiki kwenye via vya uzazi.

“Asilimia zilizobakia ndio hufanikiwa na kutungisha ujauzito. Sasa kwa wale wenye changamoto hii tunachokifanya sisi ni kuchepusha (by pass) hii njia ya kupitisha kwenye njia ya kawaida ya kupita kwenye uke, njia ya kizazi, mji wa mimba, ipite kwenye mirija mpaka ikute yai,” anasema.

Akifafanua zaidi, anasema wakati mwanamke ameshatengenezewa uwezo wa kutengeneza mayai mengi yaliyopevushwa, mbegu za mume zenye changamoto, ikiwamo ya kusafiri haraka husaidiwa ili kuzisafirisha haraka.

“Unaposaidia kuzipeleka kwa staili hiyo inakuwa umekwepa walau ile asilimia 30 hadi 40 ambazo zingeweza kukwapuliwa kwa sababu ya immunity ya via vya uzazi wa mwanamke vikidhani pengine ni ugonjwa vikaishia pale,” anasema.

Ametaja pia njia ya upandikizaji inayohusisha kuchukua mayai ya mama yaliyokomaa na mbegu za baba zilizokomaa, kuingia nazo maabara na kupandikiza na kutengeneza kiini tete chenye mtoto, tunaita kijusi chenye walau siku moja maabara. “Kinapopitia huo mchakato wa ukuaji walau kwa siku tatu mpaka nne na tano, kinarudishwa tena kwenye mji wa mimba wa mama ambaye anakuwa ameandaliwa sasa na homoni za ujauzito,” anasema.

Anasema hospitali ya KCMC kwa sasa iko katika hatua za mwisho kuanza kutoa huduma hiyo kwa ukamilifu kwa sababu inahitaji vifaa vingi, bora, wataalamu na inahitaji uwekezaji mkubwa.



Umri, mitindo ya maisha kiini

Dk Kakumbi anasema umri pia unachangia kwa watu wote wawili kwa sababu umri unahusishwa moja kwa moja kitaalamu na ukuaji wa viungo, pia hata mwili hupungua nguvu mtu anapofikisha umri wa miaka 50 au 60 na kuendelea.

“Viungo vya ndani kwa mwanamke na vyenyewe vinazeeka au kupoteza uwezo ule wa awali.

“Akiba ya mayai kwa mwanamke ikipungua maana yake nguvu yake ya kubeba ujauzito itatofautiana na binti mwenye miaka 18 ambaye yuko kwenye prime na muda mzuri zaidi wa yeye kubeba ujauzito,” anasema.

Halikadhalika Dk Kakumbi alisema mojawapo ya sababu kadhaa zinazochangia kwa wote mwanamume na mwanamke ni mtindo wa maisha.

“Ndio maana tunapowaona hawa wateja wetu kliniki kitu cha kwanza katika matibabu huwa tunasisitiza hasa kuhusiana na kubadilisha mtindo wa maisha.

“Uzito uliopitiliza, kutokufanya mazoezi, kutumia vyakula ambavyo vitafanya uwezo au mwili wako uwe na mafuta mengi, BMI yako iwe kubwa.”

Anataja matumizi ya vileo kupitiliza au uvutaji wa sigara, shisha, tumbaku, ugoro kuwa miongoni mwa mambo yanayoathiri uzazi.

Mwananchi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom