Tanzania - Taifa la Wadanganyika Waliokata Tamaa na Wanaishi kwa Matumaini

Keil

JF-Expert Member
Jul 2, 2007
2,214
803
Mwanzoni mwa miaka ya 90 nikiwa pale UD, kuna siku majira ya saa mbili usiku, kulilipuka kelele za kushangilia ambazo zilitokea Hall 1, Hall 2, Hall 3 na Hall 5. Jirani yangu nae nilimsikia akishangilia; nilipomwuliza kulikoni Mlimani kumelipuka kwa shangwe? Boom limeongezwa? Jirani alisema dawa ya UKIMWI imegunduliwa hapa Kenya, kwa hiyo mambo swafi! Furaha hiyo ilidumu kwa muda mfupi, maana dawa ile haikuwa effective na hivyo watu waliendelea kupukutika. Leo ni karibu miaka 20 tangu niliposikia tangazo hilo, bado watafiti wanaendelea kutafuta tiba na chanjo, bahati mbaya watu wanaendelea kuteketea.

Shangwe ya siku hiyo, inanikumbusha Tanzania nzima ilivyolipuka kwa shangwe na nderemo siku Lowassa alipotangaza kuachia ngazi. Kilichomfanya atangaze kuachia ngazi si kingine bali ni ufisadi. Mawaziri wengine walioachia ngazi ni pamoja na Karamagi na Dr. Msabaha. Furaha waliyokuwa nayo watanzania ilikuwa kana kwamba kuondoka kwa Lowassa ndio ilikuwa mwisho wa ufisadi au Lowassa ndiye fisadi pekee ambaye alikuwa anafanya maisha ya wananchi yawe magumu sana.

Furaha hiyo haikudumu; Pinda aliyejinasibu kwamba yeye ni "Mtoto wa Mkulima" alishindwa kutekeleza karibu maazimio yote ya Bunge ya sakata la Richmond. Wabunge wa CCM walimaliza sakata hilo kiaina chini ya uongozi wa "mpambanaji" Anko Sam Six a.k.a Mzee wa Kasi na Viwango. Sakata hili ndio liliwaibua "wapiganaji" akina Mama Killango, ole Sendeka, Lembeli & Co. Walikuwa instrumental kwenye chaguzi ndogo ili ku-neutralize hoja ya ufisadi ya CHADEMA.

Mwaka jana baada ya CCM kugundua kwamba imepoteza mvuto baada ya JK kupata "ushindi" wa kuchakachua wa 61%, jukwaa la sanaa lihamishiwa kwenye Chama. Ikaja operation vua gamba iliyoambatana uteuzi wa vijana kuingia kwenye secretariat. Watanzania kama kawaida tulipata mhemko wa ajabu sana, ghafla matumaini yakarejea kwa kasi kubwa kwamba sasa CCM inabadilika. Secretariat mpya ikasema mafisadi wamepewa muda wajipime then waondoke wenyewe vinginevyo watang'olewa. Hivi sasa ni mwaka mzima tangu CC ilipovunjwa na kuundwa mpya pamoja na secretariat. Ufisadi ndio kwanza unazidi kuota mizizi na mafisadi bado wanapeta ndani chama.

Mvua za rasharasha za Arumeru Mashariki, Kiwira - Mbeya, Lizaboni - Songea, Kirumba - Mwanza na Tanga, zimewashitua wabunge wa CCM kwamba mwaka 2015 wanaweza wasirejee mjengoni. Wachezaji wa safari hii ilikuwa ni breed mpya ndani ya chama; Deo Filikunjombe, Esther Bulaya, Alphaxard Lugola & Co. wakisindikizwa na mkongwe mzoefu Bwana Zambi. Kwa mara nyingine tena watanzania kwa kipindi cha siku 3 zilizopita tumejawa na matumaini, tukishangilia kwamba sasa wabunge wa CCM imeamua kupambana na ufisadi, lakini furaha yetu itakuwa ni ya muda mfupi kama kawaida; ni furaha ya watu waliokata tamaa na wanaishi kwa matumaini kwamba mambo yatabadilika.

Tatizo la ufisadi hapa Tanzania ni la kimfumo; halihusiani na kubadilisha watendaji kwenye wizara na idara za serikali na/au mashirika ya umma. Hata akishuka malaika kutoka mbinguni kwa mfumo uliopo, ufisadi utaendelea. Mfumo huo unalelewa kwa ushirikiano kati ya serikali, wabunge wa CCM (maana ndio wanao-set agenda mjengoni kwa kuwa ni wengi na ndio maana kukiwa na issue hot/nzito huwa hawachelewi kuitana chemba ukumbi wa Msekwa) na CCM yenyewe. Hawa mapacha watatu ndio adui wakubwa wa watanzania. Wabunge wa CCM na Chama kazi yao ni kucheza mazingaombwe halafu serikali inafuata tune kulingana na response ya wananchi.

Kama swala ni kubadilisha watendaji, basi baada ya Lowassa kujiuzulu kusingetokea ufisadi mwingine. Lakini ufisadi uliojadiliwa siku mbili unatisha na kukatisha tamaa. "Marehemu" Ballali tulisema ni fisadi wa kujenga twin towers; stimulus package imeyeyuka na waliopewa wala si walengwa, Prof. Ndullu akachangamkia tenda ya kujenga nyumba ya gavana kwa gharama kubwa mpaka kila mtu anahoji kwamba ni nyumba ya aina gani. Pale Wizara ya Nishati na Madini, chini ya JK, tayari wameishapita watatu na wote wanatimka kwa kashfa ya ufisadi, ina maana hawajifunzi? Ina maana hawaogopi kwamba watatia kitumbua chao mchanga? Huu ujasiri wa kila waziri akienda hapo anafanya ufisadi halafu anaondoka, unatoka wapi? Kwanini hawa wanaoondolewa kwa ufisadi huwa hawachukuliwi hatua za kisheria? Alikuwepo mchumi Dr. Arthur Mwakapugi akaondoka na Richmond, akaja Jairo nae ameondoka na "mshiko wa kusaidia kupitisha bajeti". Wizara ya Fedha alikuwepo Mama Zakhia Meghji akaondoka na kashfa ya kufunika KAGODA. Sasa tuna jambazi mwingine ambaye anajifanyia analotaka. Madudu ya Mkulo yanapitia kwenye cabinet na ndio maana Zitto alilituhumu Baraza la Mawaziri kwamba lilihongwa, akaambiwa athibitishe, mpaka leo Spika hajawahi kuongelea uthibitisho huo. Kwa hiyo Spika wa Bunge aliamua kuilinda serikali.

Januari Makamba anasema ufisadi na rushwa ni swala la mtu binafsi/tabia, mimi nasema kwa Tanzania ni swala la mfumo unaolelewa na serikali ya CCM, wakisaidiana na wabunge wa CCM na CCM yenyewe. Jana viongozi wa CCM na Katibu Mkuu Kiongozi (Balozi Sefue) walikuwa mitaa ya Bungeni kupanga mazingaombwe nani atoke na nani abaki. Magazeti yameweka vyema kwamba mawaziri watakaojiuzulu ni kwa sababu ya kuinusuru CCM. Sio kwamba wanajiuzulu kwa kuwajibika, bali wanakinusuru chama. Dr. Mwakyembe, mwaka 2008 alisema kwamba Kamati Teule hawakusema/weka kila kitu kwenye report ili kuinusuru/setiri serikali. Ukiangalia hiyo pembe tatu, unapata "utatu usio mtakatifu" ['unholy trinity'].

Kwa hiyo hapa chama kinailinda serikali, serikali inawalinda wabunge wa CCM [kuchakachua matokeo ya uchaguzi majimboni maana wapo kibao ambao hawashindi kihalali na wengine wanashinda kwa rushwa lakini serikali haiwafanyi lolote], na wabunge wa CCM wanailinda serikali. Mawaziri na watendaji wa serikali wanapoondolewa kwa kashfa za ufisadi, serikali huwa haiwapeleki mahakamani. Wabunge wa CCM wakitishia kuivimbishia serikali, chama huwa kinaingilia kati na kuwaita kwenye caucus ambako huelekezwa wafanye ili "mazingaombwe yaweze kufanikiwa".

Kama wabunge wa CCM wana nia ya dhati ya kupiga vita rushwa na ufisadi, wapitie sheria zote zenye matobo yanayosaidia kufanya ufisadi halafu mtu akibainika anaachiwa kwa kuwa sheria ni bomu. Wampe meno CAG ili awe anawaburuza mahakamani wale wote wanaokutwa wamefanya ufisadi. Kwanini hawatungi sheria za kuwabana? Kwanini serikali haiweki kanuni za uwajibikaji ambazo ziko wazi? BoT iko chini ya Wizara ya Fedha, kuna mambo kibao yanafanywa na Gavana wa BOT bila Wizara ya Fedha kuwa na taarifa. CEO wa shirika la umma anakuwa appointed na Rais, halafu unataka awajibike kwa Waziri, bado hapo hapo kuna Board ambayo ina Mwenyekiti [mteule wa Rais] na wajumbe [wateule wa waziri] bodi nzima haiko responsible kwa mtu yeyote. Unategemea nini hapo? Shirika lipate faida au hasara, who cares? Sakata la twin towers Liyumba pekee ndo alifungwa ilihali decisions zote zilikuwa zinapita kwenye bodi, kazi ya bodi ni nini? Je, bodi ikisababisha hasara au wakasaidia management ya shirika kufanya ufisadi, bodi inachukuliwa hatua gani?

Tutaendelea kujifariji kwa furaha za muda mfupi na kushangilia kila tunapoona "mazingaombwe". Lakini hatutaweza kutoka kwenye lindi la ufisadi ambako CCM, wabunge wa CCM na serikali yao wanajitahidi kuhakikisha tusitoke huko. Bahati nzuri JK alishasema kwamba 70% ya watanzania ni "bendera fuata upepo" alishagundua tumekata tamaa na tunaishi kwa matumaini na hivyo ni rahisi kutudanganya kwa kutumia wacheza mazingaombwe tofauti, leo atacheza Sam Six, Mama Killango & Co, kesho atakuja Nape, Makamba Jr, Nchemba & Co, baadaye atakuja Pinda na kulialia kwamba yeye ni mtoto wa mkulima anaelewa madhara ya ufisadi na jinsi yanavyowaumiza walalahoi, watakuja akina Dr. Hoseah na mbwembwe kibao kwamba kuna case 10 za rushwa na ufisadi zitakazotikisa hii nchi, baadaye itakuja breed mpya ya "wapiganaji" wabunge wa CCM akina Filikunjombe, Bulaya, Lugola & Co. Wote hawa, hakuna ambaye ana dhamira ya kuondoa mfumo wa kulinda ufisadi, kauli zao ni za kutupa matumaini na sisi tunabweteka kusubiri wabunge wa CCM wamalize ufisadi kwa maneno matupu bila kutunga sheria kali na kuhakikisha vyombo vya dola vinawajibika ipasavyo. Tunakaa tunasubiri serikali ijifunge kengele yenyewe, nani anapenda ku-commit suicide? Tunasubiri CCM iwateme mafisadi, so what? CCM yenyewe ni mnufaika wa ufisadi, unategemeaje ipige vita ufisadi? Ndio maana CCM inapigana kufa kupona ili kuongoza mabaraza ya madiwani, maana wasipoongoza "ulaji" kwenye majimbo na wilayani unakuwa mdogo na hawawezi kuchota. Kama baraza lina wajumbe wengi wa upinzani hawawezi kukubali ugeni wa ki-CCM uhudumiwe na fedha za halmashauri, wakati mwingine halmashauri hizo hizo huwa zinatoa magari yake yanabandikwa namba bandia za kiraia na yanakwenda kupiga kampeni. Wananchi wakiangalia wanaona ni mashangingi ya watu binafsi, na kumbe hapo kuna mafuta na dereva wanalipwa kutoka mafungu ya halmashauri!

Njia pekee ya kuondoa mfumo wa kulindana, ni kuondoa majority ya CCM kwenye Bunge, Hizi nyingine zote ni "areeeee towaaaaaaa?" watazamaji wanajibu "towaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaaa" Jamaa anajifanya kubadilisha karatasi na kuwa noti ya elfu kumi, ukimuuliza kwanini anatoza kiingilio kwenye mazingaombwe wakati ana uwezo wa kubadilisha karatasi kuwa noti ya shilingi elfu kumi, anakosa majibu na anakuwa mkali, "kama huamini, shauri yako!"
 
Back
Top Bottom