Taasisi za dini zina wajibu wa kuikosoa Serikali

Magobe T

JF-Expert Member
Mar 19, 2008
4,621
2,567
+Zisikubali kunyamazishwa!

Baada ya Kanisa Katoliki kutoa waraka kuhusu Uchaguzi Mkuu 2010, kumezuka mjadala mkubwa nchini huku baadhi ya Watanzania wakiunga mkono vipaumbele 7 vilivyopendekezwa na waraka huo vifanyiwe kazi na wengine wakipinga kwamba Kanisa linachanganya dini na siasa.

Mpaka sasa badala ya kutoa mawazo au elimu ya uraia kuhusu Uchaguzi Mkuu, wakosoaji wengi wamekuwa wakisema waraka una nia ya kuleta udini na kuwahamasisha Wakatoliki kuwachagua viongozi wa dhehebu lao. Yote haya yamekuwa yakisemwa bila kuonyesha ni kipaumbele kipi kina mlengo wa udini au kuwachagua Wakatoliki!

Serikali kwa upande wake inatafuta njia ili kama taasisi za dini zitakuwa na kitu, basi ziwasiliane na Serikali ili kupata njia nzuri ya kutoa mwongozo kama huo hapo baadaye.

Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Nne (2005) katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 18 inasema kila mtu:

a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kuelezea fikra zake;
b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi;
c) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake; na
d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.

Swali langu ni hili: kama kila mara taasisi za dini zikitaka kutoa changamoto kwa Serikali au kuifanya jamii iwe na msimamo thabiti kuhusu mwelekeo fulani (maana ni vizuri kujua 'subject' ya Mamlaka ya Nchi ni kutunga sheria, kusimamia haki na utekelezaji wake - kutawala - na taasisi za dini ni kusimamia/kufundisha maadili - spiritual/religious/moral values), je taasisi hizo zitakuwa zikitimiza tena wajibu wake?

Hii ina maana kama kitu kinatakiwa kisemwe leo ili jamii ikifahamu itabidi Serikali ione ni lini inafaa kisemwe (hata kama ni baada ya miaka kumi). Je, taasisi za dini zitakuwa na maana tena Tanzania?

Ni vizuri Serikali na taasisi za dini zikafanya kazi kwa kushirikiana ndiyo (kama inavyofanyika katika huduma za jamii) lakini inapoonekana Serikali inafanya kinyume na maadili ya jamii ni vizuri taasisi hizo zionyeshe kuwa ni tofauti na Serikali na hapo ndipo changamoto inapotakiwa kutolewa.

Nionanvyo mimi, Serikali inatafuta njia ya kuzinyamazisha taasisi za dini hasa pale zinapokuwa na changamoto za kufanyiwa kazi. Na ikitokea hivyo, Serikali inaona aibu kukosolewa na ili kukwepa hiyo aibu, inatafuta njia za kuzifunga mdomo au kuzifanya ziseme pale tu Serikali itakaporidhia kufanya hivyo!

Ni kama Serikali inataka kuziambia taasisi za dini "mnatakiwa mseme hivi..." na kufanya hivyo, je ndivyo Katiba inavyosema?

Kwa maoni yangu, taasisi za dini zikiogopa kuikosoa Serikali zitakuwa hazina maana tena katika jamii yetu na kufanya hivyo ni kushindwa wajibu wake!

Uhuru wa kutoa maoni ubakie palepale... Maana kitu kinaweza kusemwa na kuleta mtafaruku na kuleta mtafaruku siyo lazima kisemwe vibaya au kitu chenyewe kiwe kibaya. Inategemea tafsiri ya kitu chenyewe au upotoshaji unaofanywa makusudi na baadhi ya watu ili ujumbe wake usieleweke vizuri. Tangu lini haki au ukweli ukawapendeza watu wote?
 
Last edited:
Back
Top Bottom