Taasisi ya Dido, Female Future Program wawawezesha wanafunzi wenye mazingira magumu Mtwara

Blasio Kachuchu

Senior Member
Sep 7, 2016
153
111

Mtwara. Kwa kutambua ugumu unaowakabili baadhi ya wanafunzi kukidhi mahitaji yao muhimu, taasisi ya Dido Mwanafunzi Initiative (DMI) kwa kushirikiana na Female Future Program Cohort 9 imetoa msaada wa sare za shule, madaftari na viatu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari mkoani Mtwara.

Msaada huo uliotolewa kwa Sekondari za Naliendele, Mikindani na Nanyamba pamoja na Shule za Msingi Mwenge na Mtawanya pia umejumuisha taulo za kike, vesti, mabegi ya shule na vifaa vya kujifunzia zikiwamo kalamu.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa DMI, Rehema Moses, amesema baada ya serikali kufuta ada na michango mingine shuleni uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza hata wale wanaojiunga kidato cha kwanza umekuwa mkubwa hivyo kuibua changamoto nyingine zinazohitaji ushiriki wa wadau kuzitatua.

“Serikali inajitahidi kukuza elimu nchini ila, familia nyingi haziwezi kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu hasa ya wanafunzi kama vile sare za shule, madaftari au taulo za kike vitu ambavyo havitolewi na serikali. Sisi tunayo programu ya mvishe aende shule inayolenga kusaidia kutatua baadhi ya changamoto hizi.

Leo tupo hapa Mtwara kesho tutakuwa mkoa mwingine,” amsema Rehema Moses.

Kwa upande wake, Rais wa Female Future Program Cohort 9, Maureen Njeri amesema wakati wanahitimu shahada ya juu katika Taasisi ya ESAMI (Eastern and Southern Africa Management Institute) mwaka 2022 waliona wanayo kila sababu ya kusaidia kutatua kero na changamoto wanazokabiliana nazo wanawake wenzao katika jamii hivyo kushirikiana na DMI katika kampeni ya Mvishe Aendee Shule.


“Leo ni mwendelezo wa juhudi tunazozifanya ili kuisaidia jamii. Vifaa tulivyovitoa vimetokana na michango tunayoitoa. Ni kidogo lakini tunaamini inasaidia kupunguza tatizo. Iwapo wadau wengine watajitokeza, tunaweza kumaliza baadhi ya changamoto zilizopo nchini, na kuunga juhudi za serikali katika kuimarisha elimu” amesema Maureen.

Female Future Program iliyozinduliwa mwaka 2016 na Rais Samia Suluhu Hassan kipindi akiwa Makamu wa Rais, ipo chini ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) ikisimamiwa na Shule ya Biashara ya ESAMI, inalenga kuwawezesha wanawake wengi zaidi kuingia kwenye nafasi za uongozi ili kushiriki kutoa uamuzi wa masuala mbalimbali.

“Lengo hilo halitowezekana iwapo mwanamke na mwanamme hawatoandaliwa tangu wakiwa wadogo. Elimu ndio msingi wa kila kitu ndio maana tunakwenda mpaka shule za msingi kusaidia kuwakuza wasichana na wavulana wenye changamoto za kijamii,” ameongeza Maureen.


Akipokea taulo za kike, Sofia Bakari, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Sekondari ya Mikindani amesema wasichana wasio na uwezo hushindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa kwenye siku zao hivyo kuwapa changamoto ya kukimbizana na wenzao ili wasiachwe nyuma.

“Kuna wasichana wanaopoteza mpaka siku saba kila mwezi kutokana na hedhi. Msaada huu ni muhimu mimi na wenzangu tulioupokea tunajua thamani yake. Tunawashukuru sana kwa kutukumbuka,” amesema Sofia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mikindani Sekondari, Yonas Boniface Mtimbati, amesema kuna wanafunzi wengi katika shule hiyo ambao wazazi au walezi wao hawana uwezo wa kumudu mahitaji yote ya watoto wao hivyo wanapojitokeza wadau kama DMI na Female Future Program kusaidia inaongeza moyo wa kujifunza kwa wanafunzi hao.


“Wapo wanafunzi wasio na viatu wengine hawana au wanavaa sare zilizochakaa. Wadau wa elimu wanahitajika kusaidia vifaa hivi ili kuwapa moyo wa kujifunza bila kuhisi kunyanyapaliwa na wenzao wenye mahitaji yote,” amesema Mwalimu Yonas.


Mkurugenzi wa Dido Mwanafunzi Initiative, Rehema Moses (kushoto) na Dkt. Riziki Suleiman, wakimvisha viatu mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwenge iliyopo katika Kata ya Naliendele mkoani Mtwara.


Rehema Moses, Mkurugenzi Mtendaji Dido Mwanafunzi Initiative, Doreen Dominic, Mkuu wa Kitengo cha Umma, Benki ya Stanbic na Maureen Njeri, Rais wa Darasa la Female Future Program Cohort 9 katika hafla ya kugawa mabegi, sare za shule, chupi na viatu vya shule kwa wanafunzi wakiume na wakike, katika kata ya Naliendele, mkoani Mtwara.

 
Taasisi ya nini? cocastic ufafanuzi tafadhali. Natambua fika wewe ni mzoefu sana kwenye aina hii ya taasisi.
 
Back
Top Bottom