Taarifa ya Ngome ya Vijana ACT Wazalendo kuhusu changamoto katika zao la korosho 2021/2022

Abdul Nondo

JF-Expert Member
Oct 28, 2016
515
2,875
Ndugu Waandishi wa habari, sote tunafahamu ya kwamba zao la korosho ndio zao linaloongoza kwa kuingizia nchi yetu mapato ya fedha za kigeni kuliko mazao yote kwa ujumla. Na hili linasibitishwa kutokana na mapato ambayo nchi tulipata mwaka 2016 nchi yetu ilipata Dola million 271 baada ya kuvuna tani 265,238 na kwa mwaka 2017 nchi yetu ilinufaika zaidi kwa kupata Dola million 542 kutokana na zao la korosho baada ya kuvuna tani 313,826.

Lakini jambo la kusikitisha kuanzia msimu wa mwaka 2018 uzalishaji ulipungua hadi kufikia tani 206,719. Anguko hili limeendelea hata katika msimu huu wa mwaka 2021/2022 dalili zote zinaonesha uzalishaji utapungua zaidi. Kumekuwa na changamoto nyingi katika zao hili la korosho.

Changamoto hizi zimesababishwa na sera na maamuzi mabovu ya serikali katika zao hili dhidi ya wakulima. Serikali inapaswa kubeba mzigo wa lawama na kuwajibika kwa kusababisha uzalishaji wa korosho kushuka na bei kuporomoka katika msimu wa mwaka huu.

Hivyo serikali inachangia kumfukarisha mkulima wa korosho badala ya kumnufaisha. Tutafafanua katika taarifa hii.

1. Kushuka kwa Uzalishaji wa Korosho katika Msimu huu mwaka 2021/2022.
Ndugu waandishi wa habari, katika msimu huu wa korosho mwaka 2021/2022 kuna dalili zote kwamba uzalishaji wa korosho utaporomoka na kushuka kwa kiwango kikubwa sana kutokana na upatikanaji hafifu wa Pembejeo/Viwatilifu/Dawa ya unga yaani Sulphur na kwa gharama kubwa mno ikiwa pamoja na kucheleweshwa kuwafikia wakulima.

Serikali inaongopea wakulima kwamba tatizo ni Corona. Tunajiuliza, kwani Corona imeanza leo? Corona ina miaka 3 sasa hivi haiwezi kuwa sababu ya uhaba wa pembejeo ikiwa serikali yenyewe ndio iliahidi.

Ukweli ni kwamba changamoto ya uhaba na kucheleweshwa pembejeo na bei ya pembejeo kuwa kubwa ilisababishwa na serikali yenyewe kwa sababu serikali kupitia wizara ya kilimo iliahidi kutoa pembejeo bure. Ahadi hii ya serikali kugawa bure pembejeo kwa wakulima ilifanya wauzaji wa pembejeo hasa Salfa wa mara zote kuagiza pembejeo kidogo kuepuka kupata hasara. Matokeo yake serikali ikapeleka pembejeo kidogo sana kwa kuchelewa na ambayo ilikuwa haitoshi.

Jambo hili lilipelekea kuwe na uhaba mkubwa wa pembejeo na mahitaji kuwa makubwa yaani DEMAND AND SUPPLY. Hivyo kusababisha pembejeo chache iliyokuwepo kuuzwa kwa bei kubwa kutokana na mahitaji kuwa makubwa.

Mfano, mfuko mmoja wa salfa ulipanda kutoka Tsh.35,000 kufikia Tsh.50,000 hadi Tsh. 75000. Jambo ambalo sio wakulima wote waliweza kumudu gharama hizi.

Hivyo wakulima wengi hawakutumia pembejeo na dawa ya Salfa. Hii ni dalili tosha uzalishaji katika msimu wa mwaka huu utapungua sana. Hivyo serikali lazima iwajibike katika hili kwa kusababisha zao la korosho kuporomoka.

2. Kuporomoka kwa bei ya Korosho katika msimu huu wa mauzo ya korosho mwaka 2021 /2022.

Ndugu waandishi wa habari, katika msimu huu wa mauzo ya korosho 2021 /2022 bei ya Korosho imeendelea kuporomoka maradufu kupitia minada mitatu ya mwanzo ambayo tayari imefanyika. Mnada wa kwanza wa korosho ulifanyika tar 8 Oktoba katika wilaya ya Newala, Mtwara bei ya juu ya korosho kwa kilogramu ilikuwa Tsh. 2,445, mnada wa pili ulifanyika tarehe 9 Oktoba Mkoa wa Lindi, Nachunyu Halmashauri ya Mtama. Bei ya juu ya Korosho ilikuwa ni Tsh. 2,275 na chini Tsh. 2,020 katika mnada huu wakulima waligoma kuuza Korosho zao tani 1,895 na mnada wa tatu umefanyika jana tarehe 15 Oktoba, mkoa wa Mtwara wilaya ya Tandahimba ambapo bei ya juu ilikuwa Tsh. 2,401 na bei ya chini ni Tsh.2,225.

Mara nyingi minada ya mwanzo bei huwa inapaswa kuwa nzuri sababu namna minada inavyoendelea ndio bei huwa ina shuka ila kwa msimu huu imekuwa tofauti minada ya mwanzo imeanza na bei mbaya ni wazi kama hatua hazitachukuliwa mapema tutegemee bei ya korosho kuendelea kuporomoka maradufu.

Kuporomoka kwa bei ya korosho katika msimu huu wa mauzo ya korosho 2021/2022 Serikali haiwezi kukwepa lawama na inapaswa iwajibike kwani imesababisha bei ya korosho kuporomoka kwa kiwango kikubwa.

Serikali inaishia kujificha katika kichaka cha bei ya soko la dunia. Ni kweli, bei ya soko la dunia inaweza kuathiri lakini sio soko la dunia tuu inaweza athiri bei. Maamuzi mabovu ya serikali ndani ya nchi dhidi ya zao la Korosho, sera mbovu za serikali ndani ya nchi dhidi ya zao la Korosho na mifumo mibovu ya serikali ndani ya nchi dhidi ya Korosho imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa bei ya Korosho katika msimu huu.

Namna serikali ilivyosababisha kuporomoka kwa bei ya korosho.
 Utitiri wa Tozo katika zao la Korosho.
Wingi wa tozo umezidi kuchangia kuporomoka kwa bei ya korosho.

Mwaka baada ya mwaka tozo mpya zisizo na msingi zinatengenezwa na hii imekuwa kama njia ya watu wachache kula na kujinufaisha katika mfumo huu wa stakabadhi ghalani kupitia zao la korosho na jasho la mkulima bila kujali ya kwamba utitiri huu wa tozo una muathiri mkulima na kumuongezea mzigo mkubwa sana.

Tozo zinazotozwa kupitia zao la korosho zipo aina mbili;

a) Tozo anayotozwa mnunuzi ambayo ina muathiri mkulima katika mjengeko wa bei.

 Mnunuzi anatozwa Tsh. 64.48 kwa kilogram kwa ajili ya gunia na kamba.

 Mnunuzi anatozwa Tsh. 38 kwa kilogram, kwa ajili ya kuhifadhi korosho ghalani.

 Mnunuzi analipa Tsh.110 kwa kilogram kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho.
Jumla ni Tsh. 212.48

 Lakini pia jambo la kushangaza mnunuzi anatozwa tena tozo ya Export Levy na TRA USD 160 kwa tani sawa na Tsh.368,800 na kwa kilo moja sawa na Tsh.366 . Lengo la tozo hii kwa mujibu wa sheria ya Cashew Nut Industry Act Na.18 ya Mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho 2018 ilikuwa ni kuendeleza zao la korosho. Tozo hii bado inatozwa kwa mnunuzi lakini vilevile mnunuzi bado anatozwa tozo ya Tsh.110 kwa lengo mahususi la aina moja na export levy anayotozwa. (double taxation).

Hata hivyo Serikali haijawahi kutoa majibu ya wapi inazipeleka fedha hizi za export levy tangu 2018 walipozipokonya baada ya kubadili sheria na kuchukua 100% yote badala ya 35% ambapo 65% ilikuwa ina kwenda Bodi ya Korosho kwa ajili ya kusaidia kuendeleza zao la Korosho.

Msimu wa 2018 serikali ilipokonya takribani tsh.bil. 200 za export levy hadi sasa tangu 2018 haijawahi rejesha export levy kwa mkulima.

Tozo hizi hazimuathiri mnunuzi bali zina muathiri mkulima katika mjengeko wa bei. Kiasi anacholipa mnunuzi kulipia tozo hizi hakiwi nje ya fedha aliyopanga kununua korosho kwa mkulima bali fedha hiyo ya tozo inakuwa ndani ya kiasi cha fedha alichopanga kununua korosho, hivyo akilipa fedha hii kulipia tozo hizi lazima iathiri kiasi cha fedha ambacho mkulima angepata kutoka kwa mnunuzi kama tozo hizi zisingekuwepo.

Hivyo tozo hii analipa mkulima pasi moja kwa moja yaani indirectly.Hivyo lazima bei iwe chini ili kufidia gharama alizolipia tozo.

b) Tozo anayolipa mkulima mwenyewe kutoka katika kila kilogram ya Korosho anayouza.

Mfano,
 Mkulima analipa gharama za uendeshaji wa vyama vya ushirika AMCOS-chama cha msingi na UNION –chama kikuu Tsh.100 kwa kilogram.

 Mkulima analipa usafiri wa korosho kwenda ghala kuu kutoka chama cha ushirika Tsh,45 kwa kilogram

 Ushuru wa Halmashauri tsh.56.69 kwa kilogram

 Gharama za usimamizi wa tasnia ya korosho tsh.25 kwa kilogram kwenda Bodi ya korosho. CBT.

 Chuo cha utafiti zao la Korosho , Chuo cha TARI-Naliendele.Tsh 25

Tozo ya usimamizi wa tasnia ya korosho inayolipwa CBT na tozo ya Chuo cha utafiti TARI -Naliendele zipaswa kuchukuliwa kutoka kwenye Exporty Levy sababu ndio sababu mahususi ya kuanzisha export levy ni kwa lengo la kuendeleza zao la korosho badala yake serikali imekwapua na kuiba fedha za export levy za wakulima na serikali bila huruma imempa mzigo mkulima kulipa fedha hizo kupitia tozo katika fedha zake kidogo alizopata kutokana na bei duni ya korosho.Matendo haya ni ya kufukarisha wakulima.

3. Masharti Magumu na ya Kisiasa ya Serikali kutaka wanunuzi wa korosho kusafirisha Korosho kupitia Bandari ya Mtwara.
Serikali ilifanya maamuzi ya kisiasa kwa kuwataka wanunuzi wa Korosho kusafirishia Korosho kupitia Bandari ya Mtwara bila kujali kiasi gani maamuzi hayo yataathiri bei ya Korosho katika msimu huu. Miaka yote wanunuzi wamekuwa wakinunua Korosho na kuzisafirisha kwa gari kutoka Kusini hadi Bandari ya Dar es salaam.

Hii ilikuwa rahisi sababu ya unafuu wa gharama ya kusafirishia mzigo kwani bandari ya Dar es salaam kuna wepesi wa upatikanaji wa meli za mizigo zinazoshusha mizigo na kupakia mizigo kwa ajili ya safari. Ila bandari ya Mtwara hakuna hizo meli za mizigo hivyo inahitaji mnunuzi kuleta meli maalumu na makontena katika bandari ya Mtwara kwa ajili ya kubeba Korosho tuu.

Jambo hili linaongeza gharama kwa mnunuzi wa Korosho na namna ambayo mnunuzi anaweza kufidia gharama hizi ni kwa kununua Korosho kwa bei ya chini zaidi kutoka kwa mkulima. Hii ni moja ya sababu iliyosababishwa na Serikali kuporomosha bei ya Korosho. Serikali imefanya maamuzi ya kisiasa kutaka kulazimisha Bandari ya Mtwara kutumika katika msimu huu wa Korosho bila ya kutatua changamoto za kimiundombinu na uwekezaji utakaofanya nchi za Zambia, Malawi na Msumbiji kutumia Bandari ya Mtwara badala ya Bandari ya Dar es salaam.

Tunaishauri Serikali isome Study Report ya JDI –Japan Development Institute inaitwa Tanzania Mtwara Development Corridor, Mtwara Port and Economic Development Zone EDZ Development Plan of March 2009. Taarifa hii imeelezea kwa uzuri namna ya kufanya Bandari ya Mtwara kufanya kazi tofauti na ivyofanywa na Serikali sasa kutaka kulazimisha.

Maamuzi haya ya Serikali yameondoa ushindani kuwa mkubwa sababu wanunuzi wanaojitokeza ni wachache kutokana na masharti magumu ya serikali. Maamuzi haya yameongeza gharama za usafiri kwa mnunuzi ndio maana hadi sasa hakuna makontena yoyote ya kupakia Korosho Mtwara sababu jambo hili ni ghali na gumu. Ngome ya Vijana tuliwasiliana na watu wa Shipping Line na Mawakala kutaka kujua changamoto zilizopo.

Taarifa tuliyopewa ni kwamba ni gharama kubwa sana kuibadilishia ratiba meli kuipeleka Mtwara kubeba Korosho. Serikali haiwezi kukwepa lawama kusababisha bei ya Korosho kushuka katika msimu huu.


4. Ukiritimba Unaofanywa na Vyama vya Ushirika, Bodi ya Korosho kwa kushirikiana na Wanunuzi dhidi ya Mkulima.

Vyama vya Ushirika na Bodi ya Korosho vilianzishwa mahususi ili kumlinda mkulima. Lakini hivi sasa vimegeuka na kuwa chanzo cha kumnyonga mkulima. Kuna ujanja ujanja mkubwa kutaka kila mtu ale kupitia huu mfumo wa stakabadhi ghalani ambao unajiendea endea bila utaratibu mahususi.

Katika suala la kupanga bei kumeonekana kuna usiri mkubwa na mienendo ya ulaji na makubaliano ya gizani kati ya vyama vya ushirika na wanunuzi.
Utaratibu unaotumiwa katika Stakabadhi Ghalani unatengeneza mianya ya walaji katika mnada. Chama cha Ushirika kinakuja na sanduku ambalo limefungwa na funguo wanazo wao, kisha wanafungua mbele ya wakulima kusoma bahasha moja moja za wanunuzi wa korosho zilizoandikwa bei ya kununua korosho.

Mfumo huu una hila na usiri mkubwa kati ya vyama vya ushirika na wanunuzi. Lakini mfumo wa stakabadhi ghalani huenda sambamba na bei elekezi kutoka serikalini. Lakini kwa sababu serikali nayo inahusika kuporomosha bei ya korosho haiwezi kuwa na uhalali wa kupanga bei.

Mapendekezo yetu kwa Serikali:

1. Serikali itengue maamuzi yake ya kulazimisha wanunuzi kusafirisha Korosho kwa kutumia Bandari ya Mtwara kwani huongeza gharama kwa mununuzi na kumvuja moyo.

2. Serikali irejeshe fedha za Export Levy kwa wakulima ili zitumike kuendelezea zao hili la korosho. Hii itaondoa utitiri wa tozo kwa mkulima na mnunuzi zinazojirudia rudia. Au, Serikali ikiona ni ugumu kurejesha fedha hiyo ili kusaidia kuendeleza zao hili la korosho basi kodi ya export levy iondolewe kwa miaka kadhaa ili kuondoa mzigo huo kwa mnunuzi na hivyo fedha hiyo iwe inarudi kwa mkulima kupitia bei nzuri.

3. Tozo zinazotozwa kwa mkulima na mnunuzi ziwe zinarekebishwa kulingana na bei ya mwaka husika. Tozo haiwezi kuwa ileile kila msimu bila kuangalia bei iliyopo kwa mkulima. Jambo hili linaumiza na kumnyonya zaidi wakulima.

4. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani unapaswa kuangaliwa upya, ufanyiwe marekebisho ya msingi hasa kupunguza mnyororo wa walaji kupitia zao la Korosho na jasho la mkulima.

5. Mfumo wa Stakabadhi Ghalani lazima uende sambamba na bei elekezi ya Serikali kuliko kumuacha mnunuzi kuja na bei yake katika sanduku linalobebwa na Vyama vya Ushirika.

6. Serikali iwe inathibitisha tozo ambazo Vyama vya Ushirika vinatoza kwa Wakulima ili kumlinda mkulima dhidi ya utitiri wa tozo.

Mfano, AMCOS ya Namikango inamtoza mkulima ushuru wa Halmashauri Tsh. 56.69 halafu hapo hapo inamtoza mfuko wa elimu Tsh. 30 na Ushuru wa Kata Tsh. 30. Haiwezekani vyama vya Ushirika kutoza wakulima wanavyoona inafaa. Lazima kuwe na udhibiti na utaratibu mzuri kumlinda mkulima anayevuja jasho katika kilimo.


Mwisho, Swali:
Serikali inapelekea wapi fedha za Export Levy ? Tunahitaji kupata majibu.



Imetolewa na:

Abdul Omary Nondo
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT Wazalendo Taifa.
16 Oktoba, 2021.


IMG-20211016-WA0326.jpg
 
Hili andiko si kwa ajili ya waafika, watanzania.

Pili mnada wa mwanzo kwa kawaida huwa bei ndogo. Kwasababu korosho za mwanzo kuvunwa nyingi huwa ni za daraja la pili.

Bei nzuri ni baada ya wiki mbili kupita.


Kwa ufupi hatuhitaji uwingi, bali tunahitaji soko bora.

Soko bora lipo, wasimamizi hawajali kwa kuwa si miongoni mwa wakulima na si wenyeji wa mikoa inayolima korosho.
 
Back
Top Bottom