Sungusungu wa Shinyanga wapewa jukumu kuzuia ndoa za wahitimu la Darasa la 7

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,309
5,464
Jeshi la Jadi (Sungusungu) Manispaa ya Shinyanga na Wilaya ya Shinyanga limepewa jukumu la kuhakikisha hakuna ndoa ya utotoni ya mwanafunzi yeyote aliyehitimu darasa la saba mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko aliwakabidhi jukumu hilo juzi wakati wa kusimikwa viongozi wapya sita wa Jeshi la Jadi (Sungusungu) Tarafa ya Shinyanga Mjini.

Alisema wanafunzi waliohitimu darasa la saba wako majumbani wakisubiri matokeo ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, hivyo hataki kusikia wanafunzi hao wakiozeshwa ndoa za utotoni huku akilitaka jeshi hilo liwe mlinzi wa watoto hao.

"Sitaki kusikia mtoto ameozeshwa na ninyi Jeshi la Jadi mpo, zuieni ndoa hizi ili matokeo yakitoka ya kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, wakutwe wako salama na kuendelea na safari ya kutimiza ndoto zao kielimu.

“Fanye uchunguzi wa ndoa hizo na kuzidhibiti watoto hawa ni wetu sote lazima tuwalinde, ninawaomba na viongozi wa dini kemeeni matukio ya namna hii ya watoto kufanyiwa ukatili kwa kuozeshwa ndoa za utotoni, kunajisiwa na wakiume kulawitiwa ili jamii iwe salama," aliagiza.

Mkuu wa Wilaya huyo pia alilitaka jeshi hilo kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama katika mitaa yote pamoja na kudhibiti wimbi la vibaka mitaani ambao wamekuwa wakipora vitu mbalimbali zikiwamo simu na pochi za kinamama.

Ofisa Uhusiano na Umma kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Nsianel Gerald aliliomba Jeshi la Jadi kukomesha vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya maji ambavyo kwa sasa vimekithiri na kusababisha ukosefu wa huduma ya maji kwa wananchi.

Mwenyekiti Mpya wa Jeshi la Jadi Sungusungu Tarafa ya Shinyanga Mjini, Paulo Madale aliahidi jeshi hilo litafanya kazi zake kwa weledi kukomesha vitendo vya uhalifu mitaani.

Alisema kuwa fedha ambazo watakuwa wakitoza za faini kutokana nma makosa mbalimbali, zitakuwa zikipelekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Viongozi wapya wa Jeshi la Jadi (Sungusungu) Tarafa ya Shinyanga Mjini waliosimikwa ni Paul Madale (Mwenyekiti), Makamu wake, Juma Mipawa, Katibu Mkuu Ngaja Ngasa, Msaidizi wake, Lucas Shija, Kamanda Mkuu Thomas Mwita na Msaidizi wake Rashidi Ngoeji.

Source: Nipashe
 
Back
Top Bottom