Simulizi: Msegemnege

JBourne59

JF-Expert Member
Jan 17, 2020
941
8,549
JF huwa ni moja ya sehemu zangu za kujiburudisha hususani kwa ‘ID’ hii. Kwa kuwa nimepata muda kidogo wa kuandika na tarehe ya leo ni kumbukumbu yangu ya siku ya kuzaliwa, nimeona nianze kuwaletea simulizi iitwayo “Msegemnege”.

MSEGEMNEGE

Ni simulizi ya kubuni.
Haina uhalisia wowote.
---



Msegemnege

Tupio la I – Alex.


Alex alikuwa akiishi na wazazi wake nyumba za mamlaka ya bandari eneo la Masaki, Tour Drive, mita kadhaa kabla ya kufika Sea-Cliff Hotel. Lakini baada ya wazazi wake kufariki alifukuzwa kwenye nyumba hiyo ya Masaki, yeye na dada yake wakahamia uswahilini Manzese kwa ‘mfuga mbwa’ sehemu ambayo iliendana na hali yao wakati huo na palikuwa jirani na chuo alichokuwa akisoma Alex.

Alex ni kijana asiye na majivuno wala maringo hata wakati wa uhai wa wazazi wake ambao walikuwa wana ukwasi wa kutosha kibongobongo, hakuwa mtu mwenye kujikweza. Mama yake alikuwa mfanyakazi wa mamlaka ya bandari na baba yake alikuwa mfanyabiashara. Baba yake na mama yake waliuwawa katika tukio la ujambazi. Ujambazi ambao uliacha maswali mengi kwa kitengo cha upelelezi cha Polisi kwani kwenye gari waliokuwa wakitokea mjini kurudi nyumbani walishambuliwa eneo la makutano ya ‘tour drive’ na ‘Tumbawe road’ na katika upekuzi kwenye gari walilokuwa wakitumia marehemu, kulikutwa kiasi fulani cha hela kwenye droo ya gari pamoja na vitu vingine vya thamani kwenye kiti cha nyuma ikiwemo tarakirishi mpakato Hp moja na vishikwambi viwili aina ya ‘Surface’. Hii iliashiria kuwa halikuwa tukio la ujambazi wa kawaida bali kuna jambo lipo nyuma ya tukio hilo. Hii ilikuwa ni takribani miaka mitano iliyopita na upelelezi ulikuwa bado haujakamilika.

Alex alikuwa ni mtoto wa kiume pekee wa mzee Jonathan na Miriam ambao katika maisha yao ya ndoa walibahatika kupata watoto wawili, wa kwanza akiwa wa kike aitwaye Queen ambaye habari zake tutaziona huko mbele, lakini kwa upande wa Alex yeye alikuwa anapenda mambo ya urubani na kufanya wazazi wake wampeleke kuanza mafunzo ya urubani katika chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT) ambapo akiwa mwaka wa pili ndipo wazazi wake wakafariki na kukatisha masomo yake miezi kadhaa baadaye kwa kukosekana kwa ada na hela za kulipia mafunzo kwa vitendo.

Alex hakuwa na jinsi bali kujiingiza katika biashara ndogo ndogo za kimachinga. Aliuza vocha, akauza karanga, akauza viatu vya ‘kulenga’, aliuza matunda ya msimu ili mradi kila alichoona kinafaa yeye alifanya ili aweze kujikimu. Kwa kuwa alikuwa anapenda kusoma, alikusanya fedha na kudahiliwa tena chuo cha IFM kwa masomo ya usimamidhi wa fedha na kwa bahati nzuri alipata mkopo kwa asilimia mia moja. Pamoja na kusoma lakini pia hakuacha kufanya biashara ndogo ndogo akiwa Chuoni IFM.

Kama ilivyo kawaida ya vijana wa vyuo, Alex naye alikuwa na rafiki wa kike ambaye wanafahamiana kwa muda mrefu tangia Alex alipokuwa akiishi Masaki ingawaje alimuacha madarasa matatu nyuma wakati huo. Walipo kutana IFM wakaanzisha uhusiano wa kimapenzi na walikuwa wanapendana ingawaje sasa Alex hakuwa kama vile alivyokuwa wakati wazazi wake wakiwa hai. Alikuwa anavaa kawaida tu siyo kama zamani, hakuwa na chombo cha usafiri, kwa ujumla maisha yalikuwa ya kuunga-unga.

Miezi michache baada ya uhusiano wao, Emilia aliona bora atafute mwanafunzi mwingine ili aachane na Alex maana Emmy alikuwa na marafiki zake ambao mabwana zao walikuwa vizuri kiasi cha kumfanya Emmy kuanza kumdharau Alex licha ya kujua historia yake.

Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Emilia ndiyo ilikuwa chaguo zuri kwake kumuacha Alex mbele ya marafiki zake kwenye sherehe fupi iliyofanyika kwenye bustani ya moja ya Hotel Kubwa maarufu iliyopo jirani na hapo chuo.

Neema, Rachel, Margareth, Lidya, Zaituni na Laura ndio walikuwa marafiki wa Emilia ambapo tayari walikuwa viwanja vya Hyatt Regency pamoja na mabwana zao ambapo Emmy sasa alikuwa na bwana mpya aitwaye John.

SMS

“Alex, uko wapi?” – Aliandika Emmy

“Nipo Library” – Alijibu Alex.

“Chukuwa boda fasta njoo hapa Hyatt Regency Hotel” - aliandika tena Emmy.

“Dakika sifuri” – alijibu Alex asijue hili wala lile, kumbe maskini ndio anaenda ‘kupigwa kibuti mubashara’ mbele za watu.

Baada ya dakika chache Alex akawa Mapokezi pale hotelini, akamtumia text msg Emmy, “Upo room ipi mie nipo hapa receiption”

“Hapana sipo room, zunguka huku uwanjani kuna party fupi, umesahau leo ni birthday yangu?!”

Kutokana na mchanganyiko wa mambo tangia Alex apoteze wazazi wala hakuwa tena anakumbuka tarehe ya kuzaliwa ya Emmy. Hivyo ni kama alishtukizwa tu.

Alex akaenda moja kwa moja hadi huko uwanjani ambako alikuwa watu wakifurahi na kunywa huku kila mmoja akiwa amekaa na mpenzi wake ‘including’ Emmy.

Ghafla Emmy akamuacha John na kwenda kumpokea Alex na kumbusu kiaina na kumkaribisha kwenye party.

Hakuna katika rafiki zake Emmy aliyekuwa anajuwa kuwa Alex ameitwa ili apigwe kibuti mbele zao.

Watu walikuwa wanendelea kuburudika na vinywaji na mziki kwa mbali kisha sauti ikasikika…

“Jamani nina tangazo…” Emmy alisema.

“Nina furaha kutimiza miaka kadhaa leo (aliitaja) na kwamba leo ninatengana rasmi na Alex na kuanza rasmi uhusiano na John…”

Alex alipigwa na butwaa, akaachama mdomo wazi, na kupata ububu wa ghafla…

Rafiki zake Emmy wote nao wakashangaa na mmoja akasema…

“Emmy, unafanya nini !!??” – Zai alisema kwa kumshangaa Emmy.

Emmy naye akajibu kuwa ndiyo hivyo kama mlivyosikia, kisha akamfuata John na kumkumbatia na kumbusu.

Wakati huo Alex bado alikuwa ameduwaa asijue la kufanya huku mikono yake akiwa amejishika kichwa.

“We Emmy, kwa nini unamfanyia hivi Alex?, Alex anakupenda sana, na unajuwa jinsi anavyo kupambania, unajua fika kuwa pato lake sasa hivi ni dogo lakini amepambana na kukufanyia mengi makubwa na hivi karibuni amekununulia simu nzuri latest…” Alisema Laura.

“Simu ndio nini, kwa nini ning’ang’anie Samsung wakati nimepata Iphone, chukuwa lisimu lako hili…” Emmy alijibu na kumtupia simu Alex ambapo kwa kuzubaa ilimpiga kifuani na kuanguka chini.

Alex hakuiokota. Akageuka na kuanza kuondoka huku akiwa na mawazo tele.
---


Alex alitarajia kumuoa Emmy, ilikuwa ni faraja yake maana wanafahamiana kwa muda mrefu na kwamba Emmy alikuwa anajuwa historia ya Alex na hali aliyokuwa nayo mwanzo, hivyo Alex alidhani amepata wa kumfariji.

Aliondoka huku machozi yaki mlenga-lenga na alikuwa amejiinamia huku anatembea alitoka mle hotelini ili achukue bodaboda kuelekea IFM.

Huku nyuma Zai aliiokota ile simu na kuanza kuikagua…

“Mmmmh, lakini wewe Emmy wewe,…” alisema Zai.

“Wewe nini!, kama unamtaka wewe mfuate…” alimaliza Emmy.

Zai akaangaliana na bwana ‘ake kisha akamtupia tena maneno Emmy…

“Kumbe ulishaifuta kila kitu, lakini ona sasa umeipasua kioo…”

Emmy alionekana kuto kujali na kuendelea kugigida kinywaji na ‘party’ iliendelea japo si kwa muda mrefu tena baada ya pale.

Ilikuwa siku ya Ijumaa mida ya alasiri, Alex akiwa Hostel za IFM kwa rafiki yake Boniface, akiwa amejilaza kwenye kitanda akitafakali kilichotokea, mara ghafla meseji ikaingia kwenye simu yake. Hakutaka hata kuifungua…

Alimshirikisha Bony suala hilo na Bony alimtia moyo na kumshauri amfute moyoni mwake na ndio itakuwa tiba ya kuvunjika kwa moyo alikokupata baada ya tukio lile.

Bony ndiye aliyekuwa rafiki yake mkubwa Alex pale chuoni, na ‘alimbeba’ kwa malazi (hostel) siku amabazo Alex alikuwa hawezi kurudi nyumbani kwake Manzese.

Sasa kabla ya kumuaga Bon ili arudi home Manzese, aliamua kusoma ile sms na kukuta imeandikwa hivi…

Ndugu Alex Jonathan na bi Queen Jonathan, shauri lenu la mirathi limefikia hitimisho, hivyo mnatakiwa mfike bila kukosa Mhakama ya Mwanzo Sinza siku ya Jumatatu saa mbili asubuhi bila kukosa kwa ajili ya kukamilisha taratibu zingine. – Hakimu Mkazi, Mahakama ya Mwanzo Sinza.

Ghafla sura ya Alex ikakunjuka na furaha moyoni ikarudi, maana ni zaidi ya miaka minne shauri lao linazungushwa na Mahakama na hawakuwa na ‘connection’ wala fedha za kuhonga kitu kilichofanya shauri lao kupigwa kalenda kila siku wakienda na kisha ‘kupotezewa’.



Inaendelea…
 
Tupio la II - Queen

Queen mwezi mmoja tu baada ya kuhamia Manzese alihama tena na kuhamia sinza, maana alichagua maisha ya kulala mchana na kutembea usiku kwenye kumbi mbalimbali za starehe akibahatisha riziki kwa njia ya kuuza mwili wake. Mawasiliano ya Alex yalikatika na kila mmoja alikuwa akiishi kivyake.

Alex alivyofika nyumbani Manzese alianza kumtafuta dada yake kwenye simu. Namba yake haikuwa ikipatikana. Akaamua kuanza kumtafuta kwa njia ya marafiki zake. Alianzia kwenda Sinza ‘Kumekucha’ ambako ndipo alipofikia wakati akitoka Manzese. Lakini ajabu akaambiwa na pale alihama na hawajui alipo, lakini ajaribu kumtafuta katika kumbi za starehe mbalimbali…

“Kwa kuwa leo ni Ijumaa bila shaka unaweza kumbahatisha huko...” Sauti ya dada mmoja ilisikika.

Hapo Sinza kumekucha kulikuwa na ‘ghetto’ la rafiki yake Queen aitwaye Mayasa waliokuwa wakisoma wote chuo cha elimu ya biashara (CBE). Mayasa alikuwa hajatulia hata kidogo, tangia chuoni yeye alikuwa akijiuza mdogo mdogo ilia pate kujikimu maana ‘boom’ likikuwa halitoshi. Urafiki wao ulidumu hata baada ya Queen uondokewa na wazazi wake. Mayasa aliamua kukaa na Queen Sinza kama vile akijaribu kulipa fadhila kwa Queen wakati wakisoma chuo maana alifadhiliwa sana kwa hali na mali.

Alex ndipo alipata kujuwa kuwa dada yake aliamua kuishi maisha ya ‘upaka pori’ ili kuweza kujikimu. Ijumaa hiyo hiyo ilipofika majira ya saa moja jioni alianza kumtafuta dada yake kwa kutumia bodaboda. Hadi saa tano za usiku ndipo akabahatika kumpata, bahati nzuri hakuwa amebadilisha jina, bado alikuwa anatumia Queen.

Kitambaa cheupe Tabata ndipo alipo mkuta akiwa amelewa na yupo katikati ya wanaume wawili ambao walikuwa wakinywa na kufurahia pamoja. Alex akamuita mhudumu, akampatia karatasi ili ampelekee Queen maana kwa hali ile aliyo mkuta nayo alishindwa kumsogelea.

“Samahani, chukuwa hii karatasi mpelekee yule dada paleeee…” alisema Alex akimuonesha yule mhudumu sehemu alipo Queen.

“Yule pale Kwini?” aliuliza yule mhudumu…

“Ndiyo, kumbe unamfaham?” alishangaa Alex.

“Nani asiye mfahamu Kwini baa hii…” alitabasamu yule mhudumu.

“Nawe nikuletee nini…” aliuliza mhudumu.

“Eeee niletee club soda…” alijibu Alex huku akimuangalia dada yake.

Moja kwa moja mhudumu alienda kumchukulia Alex, ‘crest water soda’ na kuja kumpatia kisha akaelekea upande alipokuwa Queen.

Mziki nao ulikuwa umekolea kiasi cha kufanya kusikilizana kuwe tabu.

Muda wote Alex macho yake yalikuwa yamemlenga dada yake ili waonane macho kwa macho.

“Samahani Kwini, kuna ujumbe wako kutoka kwa yule mkaka paleeee…” Mhudumu alimpatia Queen ile karatasi.

Bila kuangalia sehemu ilipotoka Queen akaifungua ile karatasi na kuisoma.

“Shauri limekamilika, tunatakiwa Mahakamani, - Alex, mwisho namba ya simu”

Ghafla, Queen akasimama na kuangaza huku na huku kama anatafuta kitu, bila shaka alikuwa anamuagalia mhudumu ili amuulize aliye mpa karatasi yuko wapi.

Akawaaga wale jamaa alio kuwa nao kisha akasimama na kuelekea eneo la kaunta na kabla hajafika Alex kwa kuwa alikuwa anamfuatilia akamwita alivyokuwa karibu naye…

“Da Queen!!” Aliita alex.

Pamoja na kelele zile lakini Queen hawezi kuisahau sauti ya nduguye, akageuka upande alipokaa Alex, akamuona kisha akamfuata…

Alex akasimama…

“Jamani Alex mdogo wangu…” wakakumbatiana.

“Oyaa kijana, vipi tena! Queen, huyu ni nani? Unatusaliti siyo…” wale jamaa wawili waliongea kwa kuchangia maneno huku mmoja akimvuta Queen na mwingine akimvuta Alex…

“Jamani ‘G’ huyu ni mdogo wangu kabisa baba mmoja mama mmoja, niache kwanza…”

Waliposoikia vile wale jamaa wakatulia.

“Sikiliza Alex, andika namba hii (akaitaja) kesho mchana nitafute tuongee vizuri, muda huu hatuwezi kuelewana kama unavyo niona nimelewa…” Alisema Queen.

Alex akafanya ishara ya kuomba simu ya dada yake, akapewa kisha akajipigia kutokea simu hiyo na namba akaipata.

Wakaagana, Alex akaondoka hata bila kuimaliza ile soda, Queen akaendelea na starehe zake. Muda huo saa sita kasoro usiku, na hadi kufikia kumpata Queen tayari alishatumia pesa nyingi sana kwa boda boda maana alitembelea “viwanja” vyote alivyoelekezwa kuanzia pale ‘Ambience’ ambapo ndipo alipoanza kupata maelekezo ya viwanja vya Queen.
---


Siku ya pili Alex aliamka kama Kawaida na kuwahi chuo kujuwa kinacho endelea, ilipofika saa saba, alimpigia Queen na siku ikapokelewa.

“Hallow..” – Queen aliongea.

“Shikamoo Dada, mimi ni Alex, uko wapi nikufuate tuongee..” alijibu Alex.

“Marhaba, kwani wewe muda huu uko wapi?” Queen aliuliza.

“Nipo Chuo Dada..” alijibu Alex.

“Basi kama ni hapo NIT nitakuja muda si mrefu nita ‘request bolt’ nije chap!” – Queen alisema.

“Siyo NIT dada, kule niliacha masomo, sasa nasoma IFM, hivyo nipo huku mjini Posta” – Alisema Alex.

“Okay, nitakuja muda si mrefu” alijibu Queen na kukata simu.

Baada ya kama saa moja hivi simu ya Alex iliita. Alipokea na kuambiwa na Queen kuwa yeye keshafika na yupo KFC Diamond plaza hivyo amfuate hapo.

Dakika chache baadaye Alex akafika KFC na baada ya kusalimiana wakaanza kuzungumza.

Walizungumza vya kutosha kuanzia pale Queen alipohamia Sinza na maisha yake kwa ujumla hadi sasa. Ilikuwa ni huzuni, na furaha pia baada ya ndugu kukutana tena.

Alex: “Nilikuwa sikupati kwenye simu,…”

Queen: “Line niliivunjavunja na kusajili mtandao mwingine,…”

“Sasa ni muhimu sana ni kurudisha line yako ya simu ya zamani…” alisema Alex kisha akamwita mmoja wa wasajili line wale wanaotembea na kufanya sim swap ilia pate ile line ya zamani ya Vodacom.

Baada ya dakika chache ile line ikawa tayari na kwa kuwa Queen alikuwa na line moja tu ya tigo kwenye simu yake, akaichomeka ile line mpya yenye namba yake ya zamani na punde si punde meseji zikaanza kutiririka.

Nyingi zilikuwa za lawama hapatikani, nyingine za kutongozwa nyingine na matangazo ya mitandao ya simu pasipo kuyahitaji ili mradi kulikuwa na vurugu za meseji kuingia.

“Dada, ziache ziingie kwanza, zikitulia kuingia ndipo uanze kusoma vizuri.” Alisema Alex alipo muona dada yake anakazana kuzisoma sms zile.

Kweli, baada ya muda text message ziliacha kuingia na simu ikawa na utulivu. Kisha Alex ndio akamwambia tafuta meseji za jana maana kuna ujumbe muhimu kutoka mahakani.

Baada ya kuperuzi kwa sekunde kadhaa akafikia kwenye eneo la meseji za jana na ndipo alipo kutana na ule ujumbe uliotoka Mahakamani. Ujumbe ulisomeka kama vile ulivyosomeka kwenye simu ya Alex jana kwamba Jumatatu wanatakiwa wafike mahakamani Sinza kwa ajili ya kukamilisha utaratibu juu ya shauri lao la mirathi.


Inaendelea…
 
Tupio la III – Jonathan family

Familia ya Mr. & Mrs. Jonathan ilikuwa ikiishi maisha fulani hivi kama ya kujitenga. Mzee Jonathan kutoka Songea - Ruvuma na Bi Miriam kutoka Mpwapwa - Dodoma walioana miaka ishirini na mitatu iliyopita, ilikuwa na ndoa ya Bomani na wala haikuhudhuriwa na watu wengi maana ndugu zao ni kama vile waliwatenga.

Maisha yao yote wakiwa Masaki hawakutembelewa na ndugu yoyote si kwa upande wa baba wala upande wa mama, walikuwa wakiishi wao tu ingawaje maisha yao yalikuwa mazuri. Familia yao ilihusisha mbwa mmoja kama mlinzi msaidizi, kijana wa kazi za bustani, mlinzi wa nyumba pamoja na dada wa kazi za ndani akitokea nchi jirani Malawi.

Walikuwa na gari moja zuri Nissan Patrol (Y61) ambalo lilikuwa likimpeleka Mrs. Jonathan Kazini kule bandarini na kisha Mr. Jonathan akilitumia kwa shughuli zake za biashara. Gari la Mrs. Jonathan, Honda CRV lilipata ajali ya kugongwa na kuharibika vibaya lakini pasipo na madhara kwa binadamu na halikuwa na bima kubwa hivyo lilikuwa limefunikwa tu nyumbani kwao hapo Masaki.

Baada ya msiba, ambapo marehemu walizikwa makaburi ya Kisutu Jijini Dar es Salaam, Queen na Alex waliamua kuyauza yale magari ili kuweza kumudu maisha hasa pale walipopewa notisi ya kuhama nyumba ya mamlaka ya bandari.

Hela zile zilimsogeza Alex hadi mwaka wa pili chuo na Queen ambaye alikuwa ameshamaliza kusoma chuo cha biashara CBE zilimsaidia katika kuendesha duka lake aliliofungua maeneno ya Namanga Oysterbay lakini halikudumu, akaamua kulijumlisha kwa mmoja wa wateja wake.

kuhamia Sinza ilikuwa kwa ushawishi ya rafiki yake aitwaye Mayasa ambaye alipanga chumba mtaa wa ‘kumekucha’ na akajikuta ameanza maisha ya ‘kudanga’ huku na huku ili ajipatie riziki.

Mirathi walifungua shauri mwaka mmoja baadaye kupitia Mahakama ya Mwanzo Sinza na shauri hilo lilipigwa danadana hadi walipokata tamaa baada ya miaka miwili na kuacha kufuatilia na kila mmoja akaendelea kupambana kivyake na ugumu wa maisha.

Kumbe maafisa wa Mahakama ‘walichungulia’ nyaraka na kung’amua kulikuwa na ‘mpunga’ mrefu benki pamoja na rasilimali zingine sehemu zilizotajwa kwenye wasia.

Kama bahati kumbe Mzee Jonathani pia aliuhifadhi wasio huo Benki Kuu (BoT) ambapo Gavana wa wakati huo alikuwa rafiki yake na pia Mahakama kuu ambapo pia alifahamiana na Jaji kiongozi wa wakati huo.

Mahakama ya mwanzo Sinza ilipiga danadana shauri hilo hadi lilipoingiliwa na nguvu mpya kutoka benki kuu ambapo iliambatana na memo kutoka kwa Jaji kiongozi ikitaka shauri hilo lifikie tamati na warithi wapewe haki zao.

Hiyo nguvu mpya iliyokuja ndiyo iliyafanya Alex na Queen kupata jumbe zile kwa kuwataka wafike Jumatatu Mahakamani kukamilisha taratibu.

Polisi nako jalada la upepelezi wa mauaji yale yalifufuliwa kwa shinikizo la Jaji mkuu ili kutaka kujuwa rafiki yao alifikwa na nini. Kumbe lile jalada lilikwamia ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makossa ya jinai kanda maalum ya Kipolisi Dar es Salaam, lakini baada ya vikao kadhaa na ofisi hiyo Jaji kiongozi aliridhia suala hilo liishie kama lilivyo kama tutakavyo kuja kujua huko mbele.
---


Mahakamani Sinza…. Anaelezea Alex.


Tukiwa tumekaa kwenye benchi tukisubiri zamu yetu kuitwa, mara akaja mtumishi mmoja wa Mahakama akaita Alex na Queen, nifuateni.

Tukasimama tukaanza kumfuata. Tukaingia kwenye ofisi ya Hakimu Mkazi na kukaribishwa.

“Ninyi ndio Alex na Queen sio?” sauti ya hakimu yule ilisikika bila kutuangalia huku akisoma kutoka kwenye faili lake.

“Shauri lenu limekamilika, mnatakiwa kuweka sahihi zenu hapo chini” alisema yule hakimu na kutupatia karatasi za kusaini, hakika tulisaini bila hata kusoma nini kilichoandikwa.

“Eeeee, sasa sisi tutazipeleka nyaraka hizi benki ya NMB, nini nawashauri baada ya wiki moja muende makao makuu ya NMB kule Posta mkamuone Meneja wa Benki” alisema yule Hakimu.

“Nilitaka kusahau, nipeni namba zenu za simu ili baada ya wiki moja niwatafute nione kama mmepata changamoto yoyote…” alisema huku akiwa kama anatabasamu hivi.

Tukamtajia naye akaandika kisha akatupatia business card zake mbili kwa ajili yetu.

“Sasa tukifika kwa meneja wa benki tumuambieje!?” aliuliza Queen kwa shauku.

“Eeee semeni mmetokea Mahakama ya Mwanzo Sinza na mimi ndiye niliye waelekeza mfike hapo kuhusiana na shauri la mirathi ya Mr. Jonathan Joel Ngonyani na Bi Miriam Kalunju Chikoko” aliongea kwa kujiamini huku akikaa vizuri kwenye kiti.

Baada ya maongezi mawili matatu tukaaga na kuondoka huku tukiwa na furaha la shauri hili kufikia hatua za mwisho ili tupate haki zetu.

Mimi na Dada yangu Queen tulitoka pale mahakamani na kuelekea nyumbani kwangu Manzese kwa ‘mfuga mbwa’ ambapo dada aliandaa chakula cha mchana huku tukiwa tunaongea maana ni chumba na sebule na jiko hapo hapo. Mazaga –zaga yote yalikuwepo nyumbani na tulivyotoka Mahakamani tulipitia buchani maeneo ya Shekilango tukanunua nyama kilo moja na nusu kwa ajili ya kitoweo cha mchana na jioni.

“We nae sasa uoe, wifi ndio anipikie…” Dada alisema kwa kunichagiza

“Wifi yako juzi Ijumaa ndio amenikataa rasmi mbele ya rafiki zake eti mimi ni masikini sina mbele wala nyuma siwezi kumtunza…” nilijitetea na kuendelea…

“Eksi wifi yako mwenyewe unamjua, si kale katoto ka mzee Mosha….” Nilisema, kisha yeye akadakia..

“Nani, Juliana?” aliuliza.

Juliana alikuwa dada yake Emiliana ambaye sisi tulizoea kumwita Emilia na wengi humwita Emmy.

“Hapana, ni yule mdogo wake, Emilia, tupo naye chuo IFM mwaka mmoja” Nilijibu.

Nikamhadhithia historia nzima ya jinsi alivyonipiga kibuti.

“Kha!, Emilia ndio amekuwa na kiburi kiasi hicho!” dada alishangaa, maana Emmy aliyekuwa anamjuwa yeye wakati ule alikuwa mdogo na leo hii amenipiga kibuti.

Stori za hapa na pale ziliendelea na wakati tunaanza kula mara simu yangu ikaita…

“Hakimu hapa, leo saa moja jioni tukutane Serena Hotel upande wa Restaurant tupate dinner pamoja, muhimu sana, usikose” alisema kisha akakata simu.

Sekunde kadhaa baadaye simu ya Dada ikaita na Hakimu yule yule akamwambia Da Queen kama alivyo niambia.
---


Katika kuzungumza Da Queen akaniambia kuwa alihama Sinza Kumekucha baada ya mwenzake Mayasa kuanza kumuonea wivu kazini na pia alikuwa ana madeni ya miadi na watu kadhaa (hakunificha maisha yake) ndipo akabadili na namba ya simu na ile laini ya awali akaivunja-vunja. Muda huu anaishi Tabata Barakuda ambapo amepanga nyumba nzima yeye na rafiki yake mwingine na maisha yake kwa ujumla hayakuwa mabaya sana kiuchumi ingawaje si ya kuridhisha kimaadili.

Akiwa na rafiki yake mpya aitwaye Jacquelene, waliamua kwenda Hospitali ya Sinza Palestina baada ya kushauriwa na rafiki zao wa ‘Ambience’ kuwa waende pale wapate ushauri, kupima vvu pamoja na kuanza kutumia vidonge vya kujikinga na maambukizi ya vvu.

Queen na Jacky kwa bahati nzuri walikuwa hawana maambukizi hadi muda huo. Lakini baada ya ushauri nasihi walipewa vidonge fulani viitwavyo ‘pre exposure prophylaxis’ (ARV fulani hivi) ambavyo huwasaidia watu wanaofanya ngono mara kwa mara wasipate maambukizi na hutakiwa kumeza vidonge hivyo kila siku kama vile watu wenye vvu wanayomeza.

Katika mazungumzo yetu nikamwambia kuwa asiache kupitia kila ujumbe mfupi ulioingia kwenye simu yake kwenye laini ya voda ilia one kama kuna ujumbe muhimu mwingine usije ukawa umempita.

Akanijibu kuwa alishafanya hivyo ila kuna ujumbe mmoja tu ambao ndio hajauelewa lakini hakufafanua vizuri ingawaje alisema hauhusiani na mambo ya mahakama.

Maisha yetu mimi na dada yalikuwa yale ya kuwa huru, hatufichani kitu na tuko wazi kuambiana mambo. Hii ilitokana na mfumo wa maisha ya pale nyumbani Masaki.

Yule ‘house maid’ tulimrudisha Mikocheni kwa wakala aliyetutafutia, Mlinzi tulimlipa stahiki zake zote baada ya kuuza gari, kwa ujumla wasaidizi wote tuliwapa stahiki zao vizuri baada ya kuuza gari na mali nyingine, mbwa tulimpigia mtoto wa Bahresa akaja kumchukuwa maana yeye ana kituo cha kuhifadhia mbwa walio telekezwa ama wasiotakiwa na wenyewe. Kisha ndio tukahamia Manzese.

Tulikumbushana maisha ya Masaki na tukawa mara tunafurahi mara tunahuzunika ili mradi dada alikutana na kaka yake basi familia ikarudi na maumivu ya kuachwa na Emmy yalipotea mazima.


Itaendelea…
 
Tupio la IV - Vailet

Vailet ni binti aliye lelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama yake. Baba yake hajulikani maana mama yake alibeba ujauzito wakati akifanya biashara ya kuuza matunda barabara kuu ya Morogoro – Dododma ambapo siku moja alikutana na dereva wa lori wakashiriki ngono kisha hawakukutana wala kuwasiliana tena.

Bi Mariam alilea mimba yake na kufanikiwa kuzaa mtoto wa kike katika Hospitali ya mkoa wa Morogoro, mtoto akampewa jina la Vailet. Alimlea kwa tabu sana kwani pato lake lilikuwa linategemea kuuza kwake bidhaa barabarani, lakini kwa msaada wa majirani aliweza kumlea binti yake huyo hadi akawa mkubwa kiasi cha kutembea naye barabarani akiendelea kuuza biashara zake ndogondogo.

Mariam ambaye sasa ni marehemu, ni mmoja wa wanawake waliopitia hatua za kufanya kazi katika nyumba kama msaidizi wa kazi za ndani (house girl), alipitia manyanyaso mengi sana na kuhama hama nyumba za kufanya kazi hadi alipofanikiwa kupata nyumba yenye ‘mabosi’ wenye roho nzuri na kufanya kazi hapo kwa zaidi ya miaka mitano.

Kwakuwa alikuwa bado kigoli, yeye hakupata unyanyasaji wa kingono hadi mwaka mmoja baada ya kuwa ‘mwari’ ambapo kulitokea jaribio la kutaka kuingiliwa kwa nguvu na bosi wake wakati mkewe akiwa safarini lakini aliweza kufunga mapaja yake vizuri na zoezi halikufanikiwa licha ya purukushani kubwa na watoto wa mwenye nyumba walivyo rudi kutoka shuleni ndio ikawa salama yake, akajifungia chumbani siku hiyo hakutoka.

Siku chache baadaye mama mwenye nyumba alirudi, akamueleza kilichotokea lakini alishangaa kesho yake akiambiwa atoke kwenye nyumba hiyo na asirudi tena. Alifungasha nguo zake chache na kuelekea stedi ya Msamvu asijue aende wapi maana huko alipotoka maeneo ya Songambele Kongwa hakuwa na baba wala mama. Wazazi wake walifariki kwenye tukio la ajali ya gari (lori) la mnadani lililohusisha vifo vya watu kadhaa. Alilelewa na majirani hadi alipofikia umri wa kuweza kusonga ugali ndipo alichukuliwa na wakala kwenda Morogoro mjini kufanya kazi za ndani ambapo hakudumu katika nyumba moja bali alihama huku na huku baada ya kudhulumiwa hela zake na mabosi zake hadi alipopata nyumba hiyo ambayo nako akapata kunyanyasika kingono na kufukuzwa.

Hapo Msamvu siku hiyo alilala hapo na kesho yake bado hakujuwa afanye nini, lakini kwa bahati alikutana na mama lishe mmoja wakati alipoenda kuomba kuosha vyombo ili ajipatie chakula cha mchana ndipo akapata na kibarua hapo cha kusaidia kuhudumia wateja. Kwa jinsi hiyo akapata sehemu nyingine ya kujihifadhi ingawaje maisha ya huyo mama lishe nayo yalikuwa ya kuuga-unga tu na alikuwa akiishi maeneo ya Kihonda Magorofani Morogoro.

Biashara ya mama lishe yule haikudumu sana lakini wakati huo tayari Mariam alikuwa ameshajikusanyia hela kiasi na akaanzisha biashara ya kuuza ndizi barabara kuu. Pia alipanga chumba chake maeneo huko huko Kihonda ingawaje ilikuwa mbele – mbele kidogo mbali na Magorofani ambapo alipata chumba cha bei nafuu.

Alianza maisha kwa kutandika kilago chini kama kitanda chake(kitu kama mkeka hivi) na baada ya miaka miaka mitatu ya dhiki na kujituma sana akafankiwa kujenga jirani na eneo alilopanga, kijumba cha vyumba viwili na kuhamia kwake. Mtaa mzima walijua bidii za bi Mariam ambapo kwa wakati huo alishafikisha umri wa miaka 18. Alijibidiisha katika kazi zake hadi siku hiyo alipopata bwana ambaye alimpa ujauzito kwa kulala naye siku moja, ambapo siku hiyo ndiyo pia ilikuwa siku ya kwanza kuingiliwa na mwanaume tangia avunje ungo.
---

Bi Mariam alifariki miaka 19 baadaye, akimuacha binti yake Vailet aliyekuwa akisaidiana naye katika biashara za kuuza matunda barabara kuu. Wakati huo tayari alishaiboresha nyumba yake na kuwa kubwa tu yenye vyumba 4 sebule jiko la nje na choo cha nje pia, nyumba haikuwa na uzio.

Vailet alikuwa mwenye bidii ya kazi kama mama yake, na miezi michache baada ya kuondokewa na mama yake alipata ujauzito kwa njia kama aliyoipata mama yake, lakini yeye alibahatika kiasi maana yule bwana alikuwa kila akipita Morogoro alikuwa akilala kwake na akimsaidia mambo kadha wa kadha hadi alipopotelea Burudi ambapo alipata ajali mbaya sana ya lori akiwa dereva na alizikwa huko huko maana mwili uliharibika kabla ya kugundulika chini ya milima mirefu.

Miezi tisa baadaye Vai alijifungua mtoto wa kiume, akampa jina la Onesmo Junior. Onesmo lilikuwa jina la baba wa mtoto huyo. Vai ilibidi atafute wapangaji katika nyumba aliyoachiwa na mama yake ili kuondoa upweke na pia kujipatia kipato fulani kitakachoweza kumsaidia kulea mtoto wake Junior. Kwa bahati nzuri alipata mpangaji mmoja mwanamke ambaye naye hakuwa na mume, wakawa wanaishi vizuri tu hadi siku maajabu yalipoanza kujitokeza katika nyumba hiyo.

Siku hiyo usiku, Junior alikuwa analia sana, hakulala. Muda wote alikuwa analia, Vai alijitahidi kumbembeleza lakini wapi, jirani yake naye ilibidi aamke kuja kumsaidia lakini haikusaidia.

“Au na homa?” aliuliza yule mpangaji

“Hapana, nimemgusa mashavuni na shingoni wala hana homa” Alijibu Vai huku akionesha kukata tamaa.

“Basi huenda itakuwa joto, hebu mtoe nguo zote…” alishauri yule mpangaji.

Ikafanyika hivyo lakini kilio hakikukoma. Mwisho Vai akaamua aingie chumba alichokuwa anatumia mama yake, ambapo sasa hakikuwa na kitanda wala samani yoyote, bali mkeka tu ambapo mida ya mchana hutumia kumuweka Junior humo acheze (maana alikuwa ameanza kukaa) na yeye Vai anapata wasaa wa kupumzika ama kufanya kazi nyingine za nyumbani.

Alitandika vizuri khanga ili amlaze mtoto kisha akamwacha yeye akarudi chumbani kwake ili achukue chandarua aje mafunike huku akiendelea kumbembeleza, lakini alivyofika chumbani kwake tu akajiengesha kitandani na kupitiwa na usingizi. Hakusikia tena kelele za mtoto maana alikuwa amelala.

Mpagaji naye kwa kuwa aliingia chumbani kwake baada ya zoezi la kumbembeleza mtoto kugoma naye akapitiwa na usingizi maana mida hiyo ilikuwa ni usiku wa manane. Usiku wa usingizi mzito. Si Vai wala mpangaji wake ambaye alijua kilichoendelea hadi asubuhi.


Inaendelea…
 
Tupio la V – Onesmo Onesmo

Ilipoishia…

Alitandika vizuri khanga ili amlaze mtoto kisha akamwacha yeye akarudi chumbani kwake ili achukue chandarua aje mafunike huku akiendelea kumbembeleza, lakini alivyofika chumbani kwake tu akajiengesha kitandani na kupitiwa na usingizi. Hakusikia tena kelele za mtoto maana alikuwa amelala.

Mpagaji naye kwa kuwa aliingia chumbani kwake baada ya zoezi la kumbembeleza mtoto kugoma naye akapitiwa na usingizi maana mida hiyo ilikuwa ni usiku wa manane. Usiku wa usingizi mzito. Si Vai wala mpangaji wake ambaye alijua kilichoendelea hadi asubuhi.


Sasa endelea…

Saa kumi na moja alfajiri Vaileti akashtuka kutoka usingizini, akapapasa kama anamuangalia mtoto alipo, hola!

“Jamani mwanangu!” Alipiga kelele na kuamka kutoka kitandani.

Kelele hizo pia zilimuamsha mpangaji naye akatoka kutaka kujuwa kulikoni. Vai akakumbuka kuwa alimuweka mwanae kile chumba cha mama yake na kukimbilia huko.

“Jamani mwanangu…” alisema Vai safari hii sauti ikiwa ile ndogo ya kufurahi baada ya kumuona mtoto wake akiwa amelala pale chini lakini uchi na wala hakufunikwa na net (chandarua).

Mama Rose naye akawa amefika na kuuliza… “Kulikoni mama Junior!?”

Ndipo Vai akaanza kumueleza kuanzia pale usiku mpangaji wake mama Rose alipoingia chumbani kwake.

“Haa! Ulimuacha mtoto alale peke yake, tena uchi bila nguo wala neti!!?” mama Rose alishangaa na kuhoji.

“Hapana mama Rose, sikudhamiria, nilivyoingia tu chumbani nikapitiwa na usingizi mzito hadi muda ule napiga kelele ndio niliamka.

Waliendelea kumkagua mtoto lakini alikuwa anahema kawaida na alikuwa bado amefumba macho kwa maana ya kulala.

Mtoto alivyoamka, wote mama Rose na mama Junior walikuwepo nyumbani, waliendelea kumkagua kutafuta kama kuna hitilafu yoyote lakini mtoto alikuwa salama isipokuwa sehemu mbili tu ambazo inaonekana aliumwa na mbu, hivyo palikuwa pamevimba kidogo.

“Ajabu, mbu wa maeneo haya lakini ameumwa sehemu mbili tu!” alisema Vai.

“Labda kwa vile jana mvua kubwa ilinyesha ndio maana mbu hawakuwepo wengi…”

Waliendelea kuongea pale huku wakiwaandalia watoto wao uji kwakuwa hata Rose naye alikuwa si mkubwa sana ingawaje yeye alikuwa natembea.

Maisha yaliendelea hadi wakasahau tukio lile ndipo tukio lingine likatokea.

Ilikuwa jioni wakati Vai akimlisha uji mwanawe, maziwa pekee yalikuwa hayamtoshelezi, ambapo yule mtoto kwa bahati mbaya akakwamwa na kitu fulani hivi kama ‘plastic’ ambacho kilikuwa katika ule uji bila Vai kujuwa.

Junior akaanza kukohoa ili kile kitu kitoke, Vai akawa anampiga piga mgongoni kama anamsaidia, lakini wapi. Junior akaanza kukosa hewa na kuanza kuhema kwa tabu huku akijitahidi kama kukohoa ili kile kitu kitoke lakini wapi!

Vai na mama Rose ‘waliimba nyimbo zote’ za ‘mapambio’ lakini wapi. Lakini kwa bahati nzuri mama Rose akakumbuka kitu akasema…

“Hebu tumpeleke kule chumbani kwa bibi yake tumwache peke yake kwanza…”

Hii ilikuwa ni hatua ya kukata tamaa maana hawakuwa na hela ya kuita teksi wakati huo na zahanati palikuwa mbali.

“Kweli, ngoja nimpeleke…” alisema akiwa amekata tamaa kabisa na mtoto nguvu ya kukohoa ilikuwa imeanza kufifia huku bado akihema kwa tabu.

Vai alifunga mlango kwa kumucha mtoto wake chumbani na akatoka huku analia akibembelezwa na mama Rose.

Punde si punde wakasikia sauti ya Junior ya kulia, “ng’aaaaa, ng’aaaa, ng’aaaa…”

Vai akaacha kulia na wote wakaingia mule chumbani na kukuta Junior bado analia lakini kile kiplastic kimetoka…

“Lo, Mungu ni mkubwa!” alisema mama Rose kwa kushangaa.

Vai akamnyakuwa mtoto wake na kuanza kumbembeleza huku naye machozi yakimlenga-lenga.

Baada ya Onesmo Junior kutulia, Vai wakaangaliana na mama Rose na kujiuliza kwa mshangao, hivi ni nini kinachoendelea juu ya mtoto huyu!?

Siku ikapita, maisha yakaendelea hadi matukio kadhaa mengine ya kustaajabisha yakatokea.

Ni kwamba, kuna siku Vai baada ya kutoka katika mizunguko yake ya biashara alirudi akiwa amechoka, hivyo alilala mapema. Kama kawaida ya Vai ili kubana bajeti, mtoto alikuwa anavalishwa nepi za khanga muda mwingi mchana isipokuwa usiku tu ndio alikuwa anatumia zile nepi nyeupe. Na alikuwa anaamka usiku kumbadilisha nepi hadi mara nne siku nyingine. Lakini siku hivyo kutokana na uchovu aliokuwa nao, alijikuta amepitiliza kulala hadi alfajiri saa kumi na moja ndipo aliposhtuka na kumkagua mtoto.

Lo, alimkuta amebadilishwa nepi mara 3, maana zilizotumika aliziona kwenye beseni zikiwa zimelowekwa kama ilivyo kawaida yake na hiyo aliyovaa mtoto ilikuwa bado haijalowa kabisa, yani kavu.

Akastaajabu sana, akaangalia mlango wa chumba chake bado ulikuwa umefungwa na komeo, kwa maana ya kwamba mlango wake haukufunguliwa.

“Labda niliamka na kumbadilisha na nimesahau…” alijisemea kwa kujifariji.

Tukio hili hakumshirikisha mama Rose, alitaka ajiridhishe kwanza.

Akapanga kwamba usiku huu wa leo, atafanya makusudi ili asimbadilishe mtoto nepi. Zoezi halikuleta majibu kama alivyotarajia, saa kumi usiku aliposhtuka alimkuta mtoto amelowa chapachapa, ikabidi ambadilishe tu na kuhitimisha kuwa huenda kweli ni yeye alimbadilisha na kusahau.

Siku chache zikapita, lile tukio la mtoto kubadilishwa nepi likjirudia, na safari hii nepi zilifuliwa maana hakukuwa na zingine kwenye sanduku la nepi zaidi ya hiyo aliyoveshwa mtoto usiku huo, tayari alishabadilishwa nepi mara tatu kwa usiku ule na nepi zote kukutwa zimefuliwa lakini hazijaanikwa bali zimekamuliwa na kutandazwa kwenye beseni jingine pana kama vile zikisubiri kwenda kuanikwa.

Safari hii ilibidi amshirikishe mama Rose. Baada ya majadiliano marefu waliamua Jumapili inayofuata wote waende kanisani kusali.

“Inabidi twende kwa kweli, maana matukio haya siyo ya kawaida, labda tunakumbshwa kwenda kanisani…” Alisema Vailet.

Siku hiyo ilikuwa Alhamisi, na ilipofika Jumapili walijiandaa wao na watoto wao ili waende Kanisani. Bahati mbaya, mama Rose alikuwa ni dhehebu la Katoliki na Vai alikuwa Mlutheri. Wakakubaliana misa ya kwanza waenda kanisa la ‘Roman’ kisha wawahi misa ya mwisho katika Kanisa la Kilutheri.

Ibada zote katika makanisa mawili zilienda vizuri, wakawa na Amani waliporudi nyumbani. Maisha yakaendelea na waliendelea kuhudhuria Kanisani lakini sasa kila mmoja akienda kwenye dhehebu lake.

Kama ilivyo kawaida kwa wanawake, yale matukio walijadili pamoja na waumini wenzao kanisani kila mmoja kwa wakati wake bila kumshirikisha mwingine. Kwa upande wa Roman, kundi la wana-maombi likapanga limtembelee mama Rose alipo na kwa upande wa Vaileti, alialikwa kwenye ibada za kufanya ufunguzi (deliverance)

Mama Rose alikuwa wa kwanza kumshirikisha mama Junior kuwa Jumamosi inayofuata kutakuwa na wageni kutoka Kanisani kwake, akafunguka pia alilipeleka suala la Junior kwa wana-maombi ndipo wakapanga waje kumtembelea na kusali pamoja.

Vai naye akasema…

“Hata mimi nimelifikisha Kanisani na nikaambiwa kila siku ya Jumapili jioni katika kanisa hilo kuna ibada ya maombezi ya kufungua vifungo mbalimbali…”

“Basi, Jumamosi tuwakaribishe wanamaombi na Jumapili jioni tuende huko kwenye kufungua vifungo…” alimaliza Vailet.

Siku hazigandi, Jumamosi ikafika na saa ‘kumi na mbili unusu’ asubuhi wageni wakakaribishwa. Baada ya utambulisho ibada ikaendelea kisha watu wakatawanyika bila kuwa na jambo lolote la ajabu kujiri.

Ikawa jioni, ikawa asubuhi Jumapili kila mtu akaenda kanisani kwake na jioni ndipo wakaenda kanisani kwenye ibada za ‘deliverance’ KKKT.

Kama ilivyokuwa jana yake, maombezi yalifanyika weee, kuna watu walianguka, wengine kutoa shuhuda na ikafika kipande ambacho mama Junior alitakiwa aende mbele kwa ajili ya maombezi na ukemeo wa mapepo!

Maombezi yalifanyika ‘kwa sana’ bila hata Vai kuyumba ama kuonesha tofauti yoyote yeye pamoja na Junior, Pastor alijitahidi hata kumsukuma kidogo kiaina lakini wapi, Vai hakuanguka na wala hakukuwa na tofauti zaidi ya yeye pia kuwa alikuwa anasema maneno ya kuabudu, kusifu na kukemea akifuatisha wengine wasemavyo, alishindwa tu kusema yale maneno mfano “…roborobo shakashaka…” . (kunena kwa lugha)

Maombezi yaliendelea na kupitiliza muda wa kawaida wa ibada hiyo lakini hapakuwa na jambo la kustaajabisha kwa Vai wala mtoto wake ingawaje kuna waumini ambao walianguka na kugalagala. Hatimaye ibada ikaahirishwa hadi Jumapili nyingine jioni ambapo pia mama Rose pamoja na mama Junior walitakiwa wafike bila kukosa.

Mama Rose na Vai walirudi nyumbani kwao huku wakiwa na amani kiasi fulani maana wametoka Kanisani na hapo nyuma walikuwa wavivu sana kufanya ibada za Jumapili Kanisani.

Wakiwa njiani, Vai alikuwa anashauriana na mama Rose kuhusu mustakabali wa maajabu ya matukio yake ambapo mama mmoja akiwa nyuma yao alisikia walichokuwa wakiongea, akakaza mwendo na kuwaambia kuna sehemu amesikia kuna mchungaji ana huduma nzuri sana, hivyo kama watapenda basi atawapeleka.

“Ni hapa hapa Kihonda, mchungaji ni mwanamke na ana huduma nzuri tu, basi nitawasiliana naye ili atupangie siku ya kufanya maombezi…” alisema yule mama.



Itaendelea kesho panapo majaaliwa…
 
Back
Top Bottom