Simulizi - change (badiliko)

CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+


MUHTASARI MFUPI....

Jitihada zote ambazo Namouih aliweka katika kumchunguza Draxton hazikuwa zimefanikiwa, na bado alikuwa anahofia kwamba huenda siku moja mwanaume yule angekuja kumuumiza vibaya sana rafiki yake, lakini ni kama Blandina alikuwa amepofushwa na upendo aliokuwa nao kumwelekea kuona hilo. Kwa hiyo akawa ameamua jambo moja tu; kuupata ukweli kutoka kwa Draxton kwa njia ya lazima. Yaani angemfata na kutumia njia fulani ambayo ingemlazimu mwanaume yule aseme kila kitu yeye mwenyewe, na hiyo ilikuwa kumtisha kwa kutumia bastola ya mume wake.

Alimfata mwanaume huyo, lakini akakutana naye njiani akiendesha gari kuelekea upande fulani wa jiji bila ya yeye Draxton kuwa amemwona. Mwanamke akaamua kulifatilia gari la jamaa, Kufatilia gari la Draxton kulimfikisha Namouih kwenye maeneo ambayo hayakuwa na makazi, ikiwa ni kama msitu, na Draxton akasimamisha gari lake na kushuka kisha kuelekea upande wenye miti zaidi. Namouih hangekaa kukisia jibu la swali lake kuhusu ni nini kilikuwa kimempeleka mwanaume huyo huko, naye akaikoki vizuri bastola yake na kulisogelea gari hilo na kuanza kulichunguza, lakini hakupata jambo lenye kuridhisha haja zake.

Akajitoa hapo na kuangalia huku na kule kuona kama Draxton alikuwa anarudi lakini hakumwona. Wazo la kwamba ingefaa zaidi kama angemfatilia jamaa huko huko alikoenda alikuwa nalo, lakini isingekuwa rahisi kumpata sasa hivi maana alikoelekea hakukujulikana. Akawaza tu kuondoka hapo upesi kisha angetumia fursa nyingine kumfatilia jamaa moja kwa moja, au aje huku wakati mwingine ili atafiti eneo hili yeye mwenyewe. Akarudi usawa wa gari la Draxton na kuufunga mlango wake, na hapo akashtuka sana baada ya kumwona mwanaume huyo akiwa amesimama nyuma yake! Yaani kupitia kioo cheusi cha mlangoni aliweza kumwona kwa nyuma, na kwa haraka akageuka na kumtazama pia.


★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA MBILI

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Draxton alikuwa amesimama huku akimwangalia mwanamke huyu kwa umakini uliopitiliza, naye Namouih akavikaza viganja vyake vilivyoshikilia bastola kwa chini, akiwa ameingiwa na hofu kiasi lakini akijitahidi kuonyesha ujasiri. Ni suala la ni jinsi gani mtu huyo alifika nyuma yake ghafla namna hiyo wakati hakuonekana sehemu yoyote ile sekunde chache nyuma.

"Unafanya nini?" Draxton akauliza kwa umakini.

"Naonekana kama nafanya nini?" Namouih akajibu lakini kwa swali.

Draxton akaiangalia bastola aliyoishika mwanamke huyo, naye Namouih akaikaza vizuri zaidi na kujiweka tayari kumshambulia nayo endapo kama angejaribu kuleta mzaha mbaya, akiwa hajasahau pia kwamba kifaa chake kidogo cha kurekodi sauti kilikuwa kinafanya kazi yake.

"Hii itakuwa ni mara ya kwanza na ya mwisho kukwambia hivi. Achana na mimi," Draxton akamwambia kiutulivu.

"Nimekushika wapi?" Namouih akauliza kwa ujasiri.

"Kaa mbali na mimi wewe mwanamke..." Draxton akasema kwa uthabiti.

"Kwani tatizo ni nini attorney? Unaficha nini huku? Huwa unakuja kuzika wafu au?"

"Haikuhusu. Ninakuomba uingie kwenye gari lako uondoke."

"Ah-ah subiri. Tuongee kidogo. Sisi... mimi na wewe... we're cut out from the same cloth... kwa hiyo kama kuna siri, basi naweza kukusaidia kuitunza..." Namouih akaongea kikejeli.

Draxton akainamisha uso wake kuonyesha amekerwa.

"Niambie kama una tatizo lolote tusaidiane," Namouih akasema.

"Utanipatia msaada gani? Kunipiga kwa risasi?"

"Oh, kwa hiyo unasema kwamba ndiyo, una tatizo..."

"What's it to you? Kwani we' unataka nini?"

"Nataka tu nikusaidie...."

"Sihitaji msaada wako!" Draxton akamkatisha kwa ukali.

Namouih akabaki kumtazama.

"Nenda. Nakuomba uende," Draxton akamwambia kiutulivu.

"Hapana. Siondoki. Siondoki mpaka uniambie wewe ni nani..."

"Nini?"

"Wewe ni nani? Wewe ni mtu wa aina gani? Unagongwa kwa gari haufi? Unaingia kwenye kesi siku moja tu tayari umeshajua fact zote za mambo ambayo hata mtuhumiwa wako unayemsimamia hajui?"

"Kwani... unaongelea nini, sikuelewi...."

"Ukiguswa tu kidogo na mwanamke unachemka kama pasi na kukimbia, ni kwa nini?"

Draxton akakaza sura na macho yake kimaswali.

"Na unakuja huku msituni kufanya nini? For a guy anayejifanya kuwa mnyoofu sana una mambo mengi yanayokutia mashakani..." Namouih akamwambia.

"Why are you so obsessed with me?"

"Sina muda wa kuwa obsessed nawe. Umeingia kwenye maisha ya rafiki yangu na kuanza kuyarusha danadana kama vile hayana thamani, na hilo linaniathiri mimi pia. Ukiingia mahakamani unajifanya unajua sana kutetea haki, lakini kila kitu kukuhusu ni question mark inayotakiwa kutafutiwa majibu haraka sana, la sivyo utayaharibu maisha ya...."

"Mimi siyo mmiliki wa maisha ya mtu! Huyo rafiki yako nimemfunga mikono? Wanaume wameisha duniani au? Na kwani maisha yake binafsi yanakuchoma vipi wewe mpaka unakosa kutumia busara na kunifatilia mimi? Inakupa faida gani?" Draxton akaongea kwa ukali.

"Siyo kuhusu rafiki yangu tu...."

"Nimekwambia ondoka. Ondoka sasa hivi..."

"Au utanifanya nini? Na mimi utanikata tumbo kama hao wasichana unaowapoteza na kuwaua?"

Draxton akakaza macho yake na kuishika shingo ya Namouih ghafla sana! Namouih alitaka kutenda kwa uharaka ili amfyatulie risasi mguuni, lakini mkono mmoja wa Draxton ukaishika mikono yake iliyoshikilia bastola na kuikandamiza kwa nguvu, hivyo Namouih akashindwa kuielekeza kwa jamaa. Draxton akamsukuma na kumkandamiza kwenye gari lake, huku akimwangalia kwa hasira sana, naye Namouih akawa anapumua kwa kasi lakini kwa shida.

"Niachie.... niache...."

Namouih akajaribu kutoa sauti lakini ikawa kavu mno kutokana na jinsi alivyokazwa shingoni. Draxton akaubamiza mkono mmoja wa mwanamke huyu kwenye gari uliokuwa umeshikilia bastola, na Namouih akaidondosha chini. Kisha jamaa akaacha kumkaba na kubaki amemwangalia tu, naye Namouih akaanza kukohoa sana.

"Kalia kimya kile usichokijua. Narudia tena, hii iwe mara ya mwisho unanifatilia. Ninakuomba uondoke," Draxton akamwambia kwa mkazo.

Namouih alikuwa amejishika shingoni sasa huku akimtazama, na kwa hasira akampiga Draxton sehemu za siri kwa goti lake ili amuumize kutokana na jinsi alivyomtendea. Lakini akashangaa sana baada ya kufanya hivyo na mwanaume huyu kutoonyesha dalili yoyote ya maumivu. Ikamwingia akilini kuwa inawezekana kweli jamaa hakuhisi maumivu kwa kukumbukia usiku ule walipomgonga mtu mwenye tattoo kama yake, na huenda ilikuwa ni huyu huyu ingawa walitofautiana kwa kadiri fulani.

Mwanamke akataka kuiokota bastola yake upesi ili aitumie tena, lakini Draxton akaushika mkono wake huo, sehemu ya chini ya kiganja (wrist), akiukaza kwa nguvu sana. Namouih akawa anajaribu kuutoa mkono wa Draxton lakini akashindwa. Draxton ni kama alikuwa anaongeza nguvu ya kuukaza mkono wa mwanamke huyu ingawa hakuonyesha jitihada yoyote hata usoni kwake, akimtazama Namouih kwa njia ya kawaida tu. Kadiri alivyoendelea kuukaza ndivyo jinsi Namouih alivyohisi kudhoofika, naye akalegea na kupiga magoti huku sura yake ikionyeaha namna alivyohisi maumivu.

"Aaih... mamaa... unaniumiza...."

Namouih akanena hivyo kwa sauti kama ya msichana anayelia, naye Draxton akawa anamwangalia kutokea juu kwa njia fulani yenye huruma kiasi. Akaulegeza mkono wake uliomkaza mwanamke, naye Namouih akautoa wake na kumsukuma kidogo kwa mwingine, akionyesha kukasirika bado. Akawa amejishika mkono wake wenye maumivu huku akimtazama kwa mkazo, naye Draxton akajishika kichwani kwa kiganja chake kama vile kuonyesha kinamuuma. Akakaza meno yake kwa nguvu, kisha akaichukua bastola ya Namouih na kumnyanyua kwa nguvu mpaka akasimama.

Mwanaume huyo akaanza kumvuta kwa lazima kuelekea gari lake (Namouih), halafu akamwingiza na kumfungia mlango kwa nguvu baada ya kuirushia bastola yake siti za nyuma. Namouih akawa anamwangalia tu kwa hasira mpaka jamaa alipoanza kuondoka na kulifata gari lake, kisha akaligeuza na kuondoka eneo hilo. Namouih akiwa amebaki hapo, ndani ya gari lake, alikuwa akiangalia sehemu ile ya mkono Draxton aliyomkaza kwa nguvu. Ilikuwa nyekundu hasa kutokana na ngozi yake nyeupe kuwa laini, na bado msuguo aliohisi uliendelea kumpa maumivu kiasi.

Pamoja na kwamba alijitahidi kuonyesha ushupavu wake mbele ya mwanaume huyo, hakupata chochote cha maana katika uchunguzi wake huu zaidi ya kuambulia maumivu tu. Lakini alikasirishwa sana na kitendo ambacho Draxton alikuwa amemfanyia, na hiyo ikafanya aazimie hata zaidi kufichua yale yaliyokuwa yamefichwa na mwanaume huyo mwenye uajabu wa hali ya juu. Akawasha gari lake na kuondoka huko pia.

★★

Alifika nyumbani kwake tena kwenye mida ya saa kumi na mbili na nusu jioni. Alikuta gari la mume wake likiwa hapo tayari, na hicho ni kitu ambacho hakutarajia, yaani Efraim Donald kurudi mapema bila kumwambia. Akaelekea ndani na kumkuta sehemu ya sebule ya chini, akiwa amekaa kwenye sofa huku akitazama mechi kwenye TV yao kubwa sana ukutani, naye akaelekea usawa wake na kumsalimu. Alikuwa amejishika sehemu ile ya mkono wake ili Efraim asione ulivyotiwa alama nyekundu.

"Ulifika saa ngapi?" Namouih akamuuliza.

"Muda siyo mrefu sana. Nilikuwa tu nimewahi mechi hii kuiangalizia huku," Efraim Donald akamwambia.

"Oooh... kombe la dunia kweli. Sawa. Ngoja nikajimwagie halafu nishuke..."

"Ulikuwa wapi?" Efraim akauliza.

Namouih akamtazama kimaswali, kisha akasema, "Nilikuwa ofisini, unauliza nilikuwa wapi tena?"

"Nimepita kwa Edward wakati nakuja, nikakucheki hukuwepo. Na Esma ameniambia ulifika hapa kwanza halafu ukaondoka. Ulikuwa ofisi gani?"

"Ahah... Efraim ngoja kwanza nikaoge, nitakwambia. Nimechoka...."

"Umechoshwa na nini?" Efraim akauliza.

Namouih akaangalia pembeni.

"Namouih... njoo ukae hapa," Efraim akamwambia.

"Efraim... siko fresh... nahitaji..."

"Nimesema njoo ukae hapa," Efraim Donald akamwambia kwa utulivu.

Namouih, akionekana kutoridhia, akaelekea alipoketi mume wake na kukaa pia. Efraim Donald alikuwa anamtazama kwa umakini sana, na Namouih akawa ameangalia chini tu huku amejishika mkono wake.

"Umefanyaje mkono?" Efraim akauliza.

"Sijafanya kitu," Namouih akajibu kama ameudhika.

Mume wake akauchukua mkono huo kwa lazima na kuutazama, naye Namouih akakunja uso kuonyesha anaumia kiasi.

"Hii alama imetoka wapi?" Efraim akauliza.

Namouih akabaki kimya tu.

"Sema Namouih," Efraim Donald akaongea kwa uthabiti.

Namouih akautoa mkono wake kwake na kusema, "Kuna mtu tu nimekorofishana naye, ndiyo aka...."

Kabla hajamaliza maneno yake, Efraim akasimama na kuifata rimoti mezani, kisha akazima kabisa runinga kuonyesha kwamba alitaka umakini wake wote uwe kwa mke wake. Akarudi kwake akiwa amevuta kiti kidogo cha sofa cha kuwekea miguu kilichokuwa pembezoni mwa meza hiyo, naye akakikalia; sasa akiwa anatazamana uso kwa uso na mke wake.

"Nataka uniambie ni nani amekufanya hivi, na kwa nini," Efraim Donald akasema kwa utulivu.

Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Ni Draxton."

Efraim akarudisha uso wake nyuma kidogo, akiwa ameshangaa kiasi. "Attorney Draxton?" akauliza.

Namouih akatikisa kichwa kukubali.

"Kwa nini akufanye hivi?"

"Ni kuhusu ile ishu nilivyokwambia. Yule kaka hajakaa sawa, ni wa ajabu sana. Ninahisi anahusika kabisa na mambo ambayo Felix amekuwa akichunguza kuhusiana na vifo vya wasichana wengi kwa muda mrefu, na ninahofia anaweza kumuumiza Blandina. Lakini naye hasikii, amemng'ang'ania tu wakati mtu hata haonyeshi kumpenda... leo alikuwa ameenda msituni huko, sijui kufanya nini. Ana pigo za kichawi yule siyo wa kumwamini... ni kama...."

Namouih akaishia hapo baada ya kutambua kwamba mume wake alikuwa anamwangalia tu, kwa njia iliyoonyesha haamini mashaka ya mke wake.

"Mbona unaniangalia hivyo?" Namouih akauliza.

Efraim Donald akashusha pumzi, kisha akauliza, "Kwa hiyo... umemfatilia leo... mpaka huko msituni... kumuuliza ikiwa ni yeye ndiyo anawaua hao wasichana, au... ikiwa yeye ni mchawi?"

"Unataka ku-imply nini Efraim?"

"No, no, usiniulize swali, nipe jibu. Umeenda ukamhoji... ndiyo akakufanyaje... akakupiga?"

"Hapana hajanipiga. Nilikuwa namuuliza anieleze ni kwa nini anafanya vitu ambavyo.... akakasirika, ndiyo akanikandamiza mkono..."

"Yaani akukandamize mkono kwa sababu tu umemuuliza? Namouih nakujua, umefanya nini kingine?"

Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Nili... nilimtishia kumpiga kwa bastola."

Efraim akashangaa. "Bastola? Umetoa wapi bastola?"

Namouih akabaki tu kumtazama machoni.

"Oh my God... Namouih!" Efraim Donald akasema hivyo baada ya kuwa ametambua kwamba mke wake alimaanisha bastola yake yeye Efraim.

"Efraim nisikilize. Instinct zangu zinaniambia kabisa kwamba huyo kaka ni mtu mbaya. Siku ile tulipomgonga yule mtu sijui kiumbe gani, niliona tattoo ambayo...."

"Halafu mje kusema wanaume hatuwakililizi, lakini mkiongea ni vitu pointless," Efraim akamkatisha.

Namouih akamkazia macho na kuuliza, "Unamaanisha nini? Unasema kwamba nakudanganya?"

"Namouih nilikwambia hayo masuala achana nayo. Unamsumbua kaka wa watu kwa sababu tu umeota ndoto za kutisha?"

"Efraim...."

"Siyo watu wote watakuwa jinsi unavyotaka Namouih, na kama haufurahishwi na mtu fulani achana naye... siyo kuanza kumsakama. Hii yote kwa sababu ulipoteza kesi dhidi yake? Na tena na hapo ni yeye ndiyo alikuwa sahihi. Haya masuala ya wasichana kuuawa, Namouih, waachie maaskari. Usijiingize huko. Hata kama mimi ndiyo ningekuwa Draxton ningekasirika maana umeanza kumsakama kijana wa watu tokea mara ya kwanza alipofika hapa, na hata hajawahi kuonyesha ubaya. Kuna watu wangapi kwenye hii nchi wa kushuku kwa sababu ya hayo mauaji unayoongelea halafu wewe umemkazania Draxton tu?"

Efraim Donald aliongea hayo kwa uthabiti kabisa, naye Namouih akainamisha uso wake kidogo. Alionekana kuhuzunika sana mpaka machozi yakaanza kumlenga, naye Efraim akaketi kwenye sofa tena na kupitisha mkono wake begani kwa mke wake ili ambembeleze kidogo.

"Sikia Namouih. Mimi sitaki uingie matatizoni kwa sababu ya vitu kama hivi. Wewe ni muhimu sana hapa. Mambo yaliyo nje ya kazi yako yasikuumize kichwa, na usikazane kuchunguza maisha ya watu mpaka kufikia hatua za namna hii. Leo umekwanguliwa mkono, kesho ukinyofolewa kichwa je? Umeshafikiria mama, Sasha, na Nasma watasonga vipi bila wewe?" Efraim akamwambia kwa upole.

Namouih akajitahidi kuikaza midomo yake ili asilie. Efraim Donald akakilaza kichwa cha mke wake usawa wa kifua chake, akimpa kumbatio hilo ili kumtuliza. Alimdekeza sana.

"Niambie hautafanya jambo kama hili tena honey," Efraim akasema.

Namouih akatikisa kichwa kukubali, kisha akakinyanyua kichwa chake kutoka kifuani kwa mumewe na kuketi sawa.

"Nitaongea na Draxton kuhusu suala la yeye kukukaza mkono..." Efraim akamwambia.

"Hapana, haina shida. Uko sahihi. Sikuwa nimetambua kwamba nimevuka mipaka. Sitarudia," Namouih akasema.

"Oh honey, sipendi kukuona namna hii. Okay, you know what? Nenda kajisafishe, vaa vizuri halafu tutoke, sawa? Twende uagize chochote unachotaka," Efraim akamwambia ili kumchangamsha.

Namouih akatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kukubali, kisha Efraim Donald akambusu shavuni na kumwambia airudishe bastola kule kule alikoitoa maana ingeweza kuwa hatari kwake, na Namouih akaanza kuzifata ngazi ili apande kuelekea juu. Dada wa watu akaenda mpaka chumbani na kuingia bafuni bila kukawia ili kutoa uchovu mwingi na kuweza kujiandaa kutoka na mumewe. Bado tukio la awali kule msituni liliendelea kuzunguka kichwani kwake, lakini akajitahidi kutoliacha limharibie "mood" yake aliyotaka kuifanya iwe nzuri kwa ajili ya mume wake. Hii haingemaanisha kwamba suala hilo angelipuuzia kabisa, kwa kuwa tayari alikuwa ameshafikiria njia mbadala ya kujua ukweli kumhusu Draxton.


★★★


Tunaelekea mpaka upande mwingine wa jiji ambako kuna mtu muhimu sana kwa Namouih. Huyu si mwingine ila mdogo wake kipenzi, binti mpole na mrembo sana aitwaye Sasha. Huku ndiko alikokuwa anaendelea na masomo yake ya vidato, na kwa wakati huu ndiyo alikuwa anatarajia kuingia kidato cha sita. Tokea alipojiunga na shule yake kuendelea na masomo, aliishi bwenini, yale mabweni ya shule yanayokuwa yamejengwa eneo tofauti na shule yenyewe, lakini si mbali sana. Kwa vipindi ambavyo wangekuwa na likizo, Sasha hakurudi nyumbani kwao kabisa, bali angekaa kwenye chumba cha kupanga pamoja na rafiki yake aliyesoma pamoja naye, lakini yeye akiwa siyo wa bweni. Rafiki yake aliitwa Sabrina, aliyekuwa na miaka 20.

Wakati huu Sasha alikuwa pamoja naye, zikiwa zimebaki wiki kadhaa kabla ya masomo kuanza rasmi, naye alikuwa amepatwa na shida fulani iliyomkosesha amani sana, tena sana. Alikuwa na mawazo mengi mno. Kila mara ambapo kungekuwa na likizo, angetumia muda mwingi pamoja na Sabrina kutembelea maeneo mbalimbali, kujifurahisha kwa njia nyingi pamoja na rafiki zao wengine waliokuwa huku, na kuwa pamoja na mpenzi wake aliyeitwa Shomari, mwanaume kijana aliyefanya shughuli ndogo tu ya uuzaji wa bidhaa mbalimbali za madukani na za kisasa. Alianza mahusiano na kijana huyo mwenye sura nzuri mwanzoni kabisa alipofika jijini kuanza kidato cha tano, na alimpenda sana kwa sababu alikuwa mtaratibu na mchapakazi.

Lakini kilichokuwa kimemkosesha amani Sasha kwa wakati huu ilikuwa ni huyo huyo Shomari, na sababu ilikuwa ni kubwa sana. Kwa wiki mbili mfululizo, Sasha alionekana kukosa raha kabisa, na kila mara ambayo Sabrina alimuuliza tatizo lilikuwa nini, binti aligoma kusema. Mwishowe, jioni ya siku hii baada ya Sabrina kutoka mizunguko na kurudi ndani ya chumba walichopanga, alimkuta Sasha akilia kabisa kitandani, na hilo likamtatiza sana. Alitaka kujua nini hasa kilichomsumbua mwenzake, hivyo akalazimisha sana kumfanya aseme mpaka Sasha alipolegeza na kufunguka hatimaye.

Akiwa anajikaza kulia, Sasha akasema, "Ni Shomari."

Sabrina alikuwa ameketi naye kitandani huku akimwangalia kwa umakini, naye akauliza, "Shomari amekufanya nini?"

Sasha akabaki kimya kwa ufupi.

"Niambie Sasha, amekufanyaje? Ameku-cheat? Au amekupakazia maushenzi?" Sabrina akauliza tena.

Sasha akatikisa kichwa kukanusha. Sabrina akaendelea kumtazama akisubiri jibu.

"Nilimpa Shomari hela... nilimkopesha. Lakini sasa hivi kila nikimtafuta simpati... sijui ameenda wapi?" Sasha akasema huku machozi yakitiririka.

"Umempa hela? Umempa shi'ngapi?"

"Laki tisa..."

"Laki tisa? Sasha umempa mwanaume laki tisa?!" Sabrina akashangaa.

Sasha akatikisa kichwa kukubali huku akijifuta machozi na mengine yakiendelea kumtoka.

"Kwa nini umempa laki.... umezitoa wapi?"

"Hhh... alinipa dada..."

"Za nini?"

"Ada."

"Eh Mungu wangu!" Sabrina akashangaa zaidi na kujishika shavu.

Sasha akaendelea kulia bila kutoa sauti ya juu.

"Sasha jamani! Kweli unampa mtu hela ya ada, aifanyie nini?"

"Alisema angeirudisha. Mara zote huwa anarudisha... hata hii nilijua... ahhh...." Sasha akashindwa kuendelea.

"Mara zote? Unamaanisha huwa una kawaida ya kumpa hela?"

"Akiwa anahitaji ya haraka kama ninayo nampa... hhh... halafu anairudisha kila tarehe aliyo-promise..."

"Ndiyo umpe laki tisa? Kwanza... dada yako si huwa analipia ada moja kwa moja kwa akaunti ya shule? Imekuwaje akakupa wewe?"

"Zamu hii alinipa nije kulipia ya mwaka mzima mpaka tukimaliza cha sita... na ya matumizi yangu pia. Sasa... ahh... me... aliponitumia niliona nisubirie mpaka tukikaribia kuanza Ili ndiyo nikalipie. Lakini Shomari aliniomba nimsaidie, halafu angeirudisha... ndiyo nikatoa hicho kiasi kwenye ya ada. Ni kawaida... tumeshafanya hivyo sana nyuma nilipokuwa natoa kwenye za matumizi ila sa'hivi kwa kuwa aliomba kubwa kidogo ndiyo nikatoa kwenye ya ada. Sijui tu sasa hivi ime..imekuwaje... labda amepatwa na matatizo huko aliko...."

"Acha kuwa mjinga Sasha. Huyo amekuibia. Amekuibia, kakutapeli, mwanaume tapeli tu huyo!" Sabrina akasema kwa uthabiti.

"Lakini mbona..."

"Hakuna cha lakini Sasha, tumia akili. Hizo mara... hicho kipindi cha nyuma ulikuwaga unampa laki tisa?"

"Hapana. Nimempa laki, tisini, hamsini, laki mbili, na zote angerudisha...."

"Oooh... yuko wapi sasa sasa hivi umempa laki tisa? Alikwambia angeirudisha lini?"

"Tarehe ya wiki iliyopita..."

"Ai jamani! Sasha..." Sabrina akasikitika.

Sasha akaendelea kulia.

"Siku hizi mambo ya kuaminiana kwenye mapenzi mpaka unampa mtu hela ndefu namna hiyo hayapo. Hayapo Sasha. Watu... ah... watu siyo jinsi wanavyoonekana rafiki yangu, siyo kabisa. Ameshakutia hasara sasa. Laki tisa... dada yako alikupa shi'ngapi?"

"Hhh... milioni moja na nusu..."

"Jamani!"

"Yaani sijui nitafanyaje Sabrina... Namouih ataniua mimi..."

Sabrina akamwangalia kwa huruma sana. "Umemtafuta huyo mbwa kila sehemu hujampata?" akamuuliza.

"Hayupo. Pale alipopanga hayupo, dukani hayupo, kwa simu simpati, yaani aah... nahisi dunia imenilemea jamani... sijui nifanyeje..." Sasha akasema kwa huzuni.

"Sasha... futa machozi. Futa machozi, twende polisi sasa hivi!" Sabrina akamwambia.

"Hapana Sabrina!" Sasha akakataa.

"Hapana nini?"

"Nikienda polisi Namouih... Namouih... Namouih ataniua Sabrina..."

"Kwa hiyo ukiendelea kukaa hapa kulia hizo pesa ndiyo zitarudi? Unajua usipofanya lolote dada yako ndiyo atakuua vizuri zaidi? Twende polisi, waambie hiyo hela huyo mshenzi amekuibia... hata dada yako akijua ataona kweli umeibiwa... Sasha..."

"Hapana Sabrina. Namouih ana akili sana. Atajua tu nilimpa me mwenyewe, na atajua alikuwa mpenzi wangu wakati ni kati ya vitu alivyoniambia niepuke kwanza kwa wakati huu. Ni ujinga wangu tu mimi. Kujaribu kuonyesha nampenda mtu halafu nimeangukia pua... oh Allah... nitafanya nini?"

Sasha aliongea kwa majonzi sana mpaka Sabrina akaingiwa na simanzi.

"Sasha... nisikilize. Ni lazima kuwe na kitu cha kufanya. Hauwezi kukaa tu kusubiri muujiza, na ninaelewa jinsi dada yako alivyo mkali. Hiyo ni hela nyingi sana, na sasa hivi maisha ni magumu kucheza na pesa na kuiacha ipotee tu hivyo," Sabrina akasema ukweli.

"Najua. Uko sahihi. Yaani natamani muda ungerudi nyuma... sijui itakuwaje. Namouih... amenipigania kwa vitu vingi sana... ataumia mno akijua nimeivunja trust aliyonayo kwangu. Sikutegemea yaani Sabrina... kumuumiza dada yangu ni kitu ambacho sitaki, na sijawahi taka kitokee kabisa... lakini ndiyo nilichokifanya... aahh... labda itakuwa bora tu kama akiniua kabisa...."

"Hawezi kufanya hivyo bwana..."

"Ndiyo najua... najua. Sabrina ni kujua kwamba hataniua kihalisi ndiyo kutafanya nihisi kama ameniua... kwa sababu atanichukia sana," Sasha akaongea kwa uchungu.

"Hatakuchukia... wewe bado ni mdogo wake. Dada yako anakupenda sana..." Sabrina akajaribu kumtia moyo.

"Atanichukia Sabrina... sana... amefanya mengi... atachoka... aahh..." Sasha akasema hivyo na kuufunika uso wake kwa viganja huku akilia kwa huzuni.

Sabrina alimtazama rafiki yake sana, akitafakari kuhusu nini afanye ili kumsaidia. Hangeweza kujizuia kuwaza kwamba haya yote yalikuwa ni makosa ya Sasha mwenyewe, na malipo ndiyo yalikuwa hayo. Ila kumsaidia lilikuwa jambo la muhimu sana hasa kwa sababu alimpenda kama dada yake wa damu. Akakaa kutafakari kwa kina kuhusu njia mbalimbali za kumsaidia rafiki yake, na hatimaye, wazo fulani likamjia. Hakuwa na uhakika ikiwa Sasha angekubaliana na hilo wazo, lakini akaona ajaribu kumwambia kwa sababu lilionekana kuwa suluhisho la haraka na pekee ambalo halingemtia matatani, endapo tu kama angekubali kulifanya, na kulifanya kwa umakini.

Akamshika rafiki yake kwa upendo na kuulaza mwili wake kwake, kisha akamwambia amepata wazo mbadala kumsaidia apate pesa za kufidishia kile alichoiba Shomari. Sasha akajifuta machozi na kuweka umakini wake kwa Sabrina, akisikiliza kile ambacho angesema, na rafiki yake akaanza kumpanga kuhusu ni nini afanye ili kuliondoa tatizo hilo bila Namouih kujua. Lilikuwa ni jambo zito kiasi kwa Sasha kuafiki, lakini alijua pia kwamba hakukuwa na njia zingine za haraka za kusuluhisha tatizo lake, hivyo akakubali kulifanyia kazi, na ambacho kingebaki ingekuwa kulitekeleza, kumwachia Mungu, na kusubiri matokeo.


★★★


Wanandoa Efraim Donald na Namouih walirejea nyumbani usiku baada ya kutoka matembezi yao jijini. Angalau wakati huu Namouih alikuwa akijihisi uchangamfu kwa kuwa Efraim alimfanyia mambo mengi yenye kufurahisha na kumnunulia vitu vingi sana. Kwa hiyo walipofika, mwanaume akaona aingie bafuni kujimwagia ili akilala alale vizuri, naye Namouih akamwambia kuna kazi fulani alitaka kwenda kuiweka kwenye laptop yake, iiyokuwa ndani ya ofisi yake ndogo kule chini. Efraim akamwambia asichukue muda mrefu maana bibie alipenda mno kazi, naye Namouih akatoka na kuelekea chini baada ya kuvaa nguo ya kulalia.

Ilikuwa ni mida ya saa sita na nusu usiku sasa. Taa za ndani ya nyumba nzima zilikuwa zimezimwa, isipokuwa ndani ya chumba cha ofisi alichokwenda Namouih. Alikuwa akihamishia ile rekodi ya sauti yake na Draxton aliyorekodi leo kutoka kwenye kile kifaa kidogo na kuiweka kwenye laptop yake ili kuitunza humo, na karibu na miguu yake chini ya meza alilala Angelo. Palikuwa kimya sana, kama vile kuna mtu alibonyeza kitufe cha "mute" kwenye rimoti iliyoendesha sauti zozote ndani ya nyumba hii.

Akiwa anaendelea kubofya kwenye laptop yake, taswira fulani ndani ya akili yake ikamwingia kumfanya atambue kwamba Angelo hakuwa amelala. Alipomtazama chini hapo, akamwona sasa akiwa amesimama, masikio yake yakiwa yamelala nyuma ya kichwa chake, na hata sauti ya mbali ya kuunguruma ilisikika kutoka kwake. Umakini wake ulielekea sehemu ya mlango wa kuingilia ndani ya ofisi hiyo, naye Namouih akatazama huko pia.

Ilimshangaza kiasi kuona kwamba mlango ulikuwa umeacha uwazi mdogo, ingawa alikumbuka kwamba alikuwa ameufunga alipoingia humo muda si mrefu. Hata kama ungekuwa umefunguliwa tena angesikia, lakini kwa kufikiria ni Esma labda, akaona aite.

"Esma... Esma..."

Kimya. Alikuwa ameita kwa sauti isiyo kubwa sana lakini kama kungekuwa na mtu mlangoni basi angesikia, lakini hakupata jibu lolote.

"Efraim..."

Akajaribu kuita na jina la mume wake, lakini hakupata jibu. Alipomwangalia Angelo tena, bado alikuwa ameweka mkao wake ule ule wenye kuonyesha ukali, kisha ghafla paka huyu akaingia zaidi katikati ya miguu ya Namouih kama anajificha. Namouih alipotazama tena mlangoni, akaanza kuona kitu kama kivuli kidogo kikitokea nje ya mlango na kuingia ndani humo taratibu kwenye sakafu. Kilikuwa na umbo dogo, kama vile kidole mwanzoni, lakini kadiri kilivyoingia kiliongezeka upana na kuchukua umbo kama pembe tatu, lenye ufanano na sikio la paka.

Msisimko mkubwa sana ukamwingia mwanamke huyu, ambaye alihisi mwili wake ukianza kutetemeka, hofu ikiwa inajijenga ndani yake, lakini akaendelea tu kutazama jambo hilo. Kadiri kivuli cha "sikio" hilo kilivyozidi kuingia, ndiyo na mlango ukawa unafunguka taratibu, kama vile unasukumwa kwa upepo, au kitu fulani.

Namouih akaifunga laptop yake na kusimama taratibu, kisha akajaribu tena kuita "Efraim" bila kupata itikio lolote. Ilikuwa ni kama "kivuli" hicho kwenye sakafu "kilisikia" alipoita hivyo, kwa kuwa hapo hapo kikaanza kupungua, yaani kikiishia na kutoka ndani ya ofisi hiyo. Ilimfanya Namouih awaze kwamba kulikuwa na kitu fulani kimesimama hapo na kuondoka, na hii haikuwa kwamba labda ni akili yake tu ndiyo inayomchanganya kwa sababu hata Angelo alikiona na kuonyesha kuogopa.

Namouih hakujua ni jinsi gani alipata ujasiri wa kuibeba laptop yake na kutoka ndani ya chumba hiki cha ofisi. Sehemu yote kuanzia hapo ilikuwa na giza, la kawaida tu kwa sababu mambo mengi yalionekana kiasi kutokana na mwangaza wa taa za nje pia, lakini kuvuka hapo na kuanza kupanda ngazi bila kugeuka nyuma ilikuwa ni jambo lililohitaji ujasiri wa hali ya juu. Mapigo ya moyo wake yalidunda kwa nguvu sana kila hatua aliyopiga kuelekea juu zaidi, akihisi ni kama yuko kwenye nyumba ngeni kabisa kwa sababu hakutaka hata kugeuka nyuma kwa jinsi alivyoogopa.

Akafanikiwa kukifikia chumba chake, naye akawasha taa na kuufunga mlango kwa funguo upesi sana huku mikono yake ikitetemeka. Ni hapa ndiyo alihisi kama moyo wake unataka kupasua kifua kwa hofu iliyomwingia baada ya kuhisi kitu fulani kikiugusa mguu wake kwa chini, naye akarusha mguu wake kwa nguvu na kujibamiza mlangoni. Alipoangalia vizuri sasa akawa amemwona Angelo, paka wake, akiwa amerukia upande mwingine, naye akaelewa kuwa mnyama huyo alipanda kuja huku pamoja naye bila yeye kutambua. Alikuwa anapumua kwa kasi kiasi kutokana na woga uliomwingia, lakini akaingiwa pia na huruma baada ya kutambua alikuwa amempiga Angelo kwa nguvu.

Paka wake akamfata tu tena miguuni na kuanza kujisugua taratibu, naye Namouih akatembea haraka kukielekea kitanda huku akimwita. Akaweka laptop yake pembeni na kupanda kitandani, naye Angelo akalalia kigodoro chake kidogo kwa chini. Hakuwaza hata kumshika Efraim na kumsemesha, kwa sababu ilionekana tayari mume wake huyo alikuwa ameshapitiwa na usingizi. Namouih akajifunika kwa blanketi na kulala huku taa ikiwaka. Hakujua ikiwa hata angeweza kupata usingizi, lakini mwishowe akasinzia.

Mwanamke huyu hakuwahi kuogopa giza kabla, lakini baada ya hiki kitu kilichokuwa kimetokea muda mfupi nyuma, alihisi ni kama asingeweza kuja kutazama tena gizani, kwa sababu sasa alitambua kwamba giza lilikuwa linamtazama yeye.



★★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★★


Usikose sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali ya CHANGE. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Itakuwa ikiruka hapa siku za Jumamosi na Jumapili. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.

WhatsApp no: +255 787 604 893

e-mail: eltontonny72@gmail.com
 
Aisee story kali kinoma. Ila unabana sana, angalau ungekuwa unaweka episode hata 2 kila j1 na j2
Anafeli fuatilia hizi hapa story iko bomba sana
 
Aisee story kali kinoma. Ila unabana sana, angalau ungekuwa unaweka episode hata 2 kila j1 na j2
Na hii
 
Anafeli fuatilia hizi hapa story iko bomba sana
Mkuu sio vizuri ku share link ya simulizi yako kwenye simulizi ya mtu mwingine. Anzisha na wewe
 
Okay nimewaelewa. Ratiba mpya itakwenda namna hii; nitakuwa narusha episode moja kwa kila siku za Junatatu, Jumatano, na Ijumaa. Nathamini mnavyoonyesha upendo kwa hadithi hizi ila kupost mara moja moja ni muhimu kwa kuwa episode zangu ni ndefu na ninafanya mauzo pia, ikiwa nitapost kila siku hakutakuwa na faida yoyote kwa upande wangu.

Kumradhi kuwasubirisha. Wacha nishushe episode moja now. 😉
 
CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+


MUHTASARI MFUPI....

Baada ya visa vingi kutokea vilivyomhusisha mwanasheria Draxton katikati ya kila jambo, ni Namouih pekee ndiye aliyetambua hilo, naye anafikiria kukusanya ushahidi kwa njia yake baada ya wiki nzima kupita bila kupata chochote; na njia hiyo ni kutumia bastola ya mume wake kumshurutisha mwanaume huyo aseme ukweli wa matendo yake. Namouih anapojaribu kumtishia, Draxton anakasirika sana na hata kumuumiza mkononi, akimsisitiza akae mbali naye kabisa. Mwanamke huyu anarejea nyumbani na kumweleza Efraim Donald yaliyotokea, na hata mume wake huyo anamwambia aache kujiingiza kwenye mambo ambayo yanaweza kumsababishia akaumia. Ili kumpoza roho kidogo, Efraim Donald akamtoa mke wake kwa ajili ya matembezi.

Upande mwingine wa jiji hilo, Sasha, mdogo wake Namouih, anapatwa na shida fulani ambayo ni mzito sana. Amepoteza pesa nyingi baada ya kumpatia mpenzi wake aliyeahidi kuzirudisha kupotea tu, na zilikuwa ni pesa alizopewa na dada yake kwa ajili ya kulipa karo ya shule kwa mwaka mzima. Anasononeka sana na kuogopa mno kumwambia Namouih maana anaelewa jinsi alivyo mkali ingawa ni mwenye kujali, na rafiki yake aitwaye Sabrina anajaribu kumtuliza, kisha anampa ushauri wa kufanya jambo fulani ambalo litadaidia kufidishia pesa hizo bila dada yake kujua kilichotokea.

Efraim Donald na Namouih walirejea nyumbani usiku baada ya kutoka matembezi yao jijini. Namouih alitaka kwenda kuiweka ile rekodi ya sauti yake na Draxton aliyorekodi kutoka kwenye kile kifaa kidogo ili kuitunza kwenye laptop yake, iiyokuwa ndani ya ofisi yake ndogo kule chini. Akiwa anaendelea kubofya kwenye laptop yake, akaanza kuona kitu kama kivuli kidogo kikitokea nje ya mlango na kuingia ndani humo taratibu kwenye sakafu, na kadiri kilivyoingia kiliongezeka upana na kuchukua umbo kama pembe tatu, lenye ufanano na sikio la paka. Msisimko mkubwa sana ukamwingia mwanamke huyu, ambaye alihisi mwili wake ukianza kutetemeka, hofu ikiwa inajijenga ndani yake. Kadiri kivuli cha "sikio" hilo kilivyozidi kuingia, ndiyo na mlango ukawa unafunguka taratibu, kama vile unasukumwa kwa upepo. Akajaribu tena kuita "Efraim" bila kupata itikio lolote, na hapo hapo kikaanza kupungua, yaani kikiishia na kutoka ndani ya ofisi hiyo.

Namouih hakujua ni jinsi gani alipata ujasiri wa kuibeba laptop yake na kutoka ndani ya chumba hiki cha ofisi mpaka chumbani kwake. Mapigo ya moyo wake yalidunda kwa nguvu sana kila hatua aliyopiga kuelekea juu zaidi, akihisi ni kama yuko kwenye nyumba ngeni kabisa kwa sababu hakutaka hata kugeuka nyuma kwa jinsi alivyoogopa. Akaweka laptop yake pembeni na kupanda kitandani. Hakuwaza hata kumshika Efraim na kumsemesha, naye akajifunika tu kwa blanketi na kulala huku taa ikiwaka.

Mwanamke huyu hakuwahi kuogopa giza kabla, lakini baada ya hiki kitu kilichokuwa kimetokea muda mfupi nyuma, alihisi ni kama asingeweza kuja kutazama tena gizani, kwa sababu sasa alitambua kwamba giza lilikuwa linamtazama yeye.


★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA TATU

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Kukucha kukakucha. Ikiwa imetimia saa tatu asubuhi siku hii ya Jumamosi, Efraim Donald akaamka na kujigeuza kitandani hapo taratibu ili amwangalie mke wake. Akakuta Namouih akiwa amelalia ubavu wake huku amejifunika kwa blanketi mpaka kichwani, akiacha sehemu ndogo ya uwazi kwenye uso wake. Alikuwa ameikunjia mikono yake kufikia usawa wa shavu, na macho yake yalikuwa yamefunguka huku yakiangalia chini tu kwa njia fulani yenye huzuni. Efraim akajigeuza vizuri na kulalia ubavu wake pia, sasa akiwa anatazamana uso kwa uso na mke wake kwa ukaribu, naye akapitisha mkono wake ndani ya blanketi hilo na kuanza kuzishika nywele laini za mke wake kwa njia ya kuzichezea.

"Good morning," Efraim akasema.

Namouih akamtazama tu machoni.

"Vipi... unajisikiaje sa'hivi?" Efraim akauliza tena.

Lakini Namouih akaendelea kumwangalia kwa njia iliyoonyesha mfadhaiko mwingi, na hilo likafanya Efraim Donald atambue kwamba mke wake hakuamka vizuri.

"Namouih what's wrong?" Efraim akauliza kwa kujali.

Tena, na hapa Namouih akashindwa kusema lolote na kubaki ametulia tu, naye Efraim Donald akamshika kwenye paji la uso kuona kama alikuwa anaumwa, ila akakuta joto lake liko kawaida tu. Akajinyanyua na kuketi, kisha akatumia nguvu kiasi kumvuta Namouih ili naye akae pia, na akafanikiwa kwa hilo. Namouih alionekana kuchoka yaani, uso wake haukuonyesha hisia yoyote ya furaha kama alivyokuwa jana usiku walipotoka kwenda matembezi, naye Efraim akataka kujua ni nini tena kilikuwa kinamsumbua.

Akamshika shingoni na kumtazama kwa ukaribu, kisha akauliza, "Umeota ndoto mbaya tena?"

Namouih akatikisa kichwa kukanusha.

"Tell me honey. Nini tatizo?" Efraim akauliza tena kwa kubembeleza.

"Yaani sielewi kwa kweli. Nahisi kuchanganyikiwa Efraim...."

"Shida ni nini? Ni haya mambo yaliyotokea jana au?"

"Yaani sijui. Sijui ikiwa mambo yaliyotokea jana ndiyo yanasababisha nakuwa naona hivi vitu, au ni nini yaani...."

"Vitu gani?"

Namouih akafumba macho yake.

"Namouih nielezee..." Efraim akamwambia.

"Jana... kabla sijapanda kuja kulala, nilikuwa huko na Angelo... tukaanza kuona kama kivuli Efraim... kilikuwa kama kinaufungua mlango kabisa... niliogopa sana yaani sijui tu ni nini kilichonisaidia nikaweza kufika huku lakini... hii hali inanitisha mno..." Namouih akaongea kwa hisia.

"Kivuli?"

"Ndiyo. Mara nyingi nikiota ndoto za kutisha huwa naona vitu kama vivuli... ila jana haikuwa ndoto Efraim. Sikutanii... kuna kitu hakiko sawa..."

"Usijali Namouih, nakuamini. Pole sana. Ungeniambia hiyo jana, labda kuna mtu alikuwa ameingia hapa..."

"Hamna, hakukuwa na mtu kabisa. Ahh... nakwambia kila mara nikifanya tu interaction na Draxton ni lazima nitaota ndoto mbaya au kuanza kuona vitu vya ajabu. Ni kama kipindi kile ambacho unanichumbia unakumbuka nilikwambiaga kuna wakati nilikuwa naona mtu fulani wa ajabu, mara ananifatilia, mara anitokee dirishani...."

"Ndiyo nakumbuka Namouih, nakumbuka..."

"Ni kama hivyo yaani. Hayo yaliacha lakini ni kama tena na sasa hivi yameanza... I don't know... sijui tu Efraim nimefanya nini kustahili kupatwa na haya yote..." Namouih akasema kwa huzuni.

"Namouih... naelewa unakuwa na mambo mengi akilini, na inaonekana ndiyo kati ya mambo ambayo...."

"Hapana Efraim, nina uhakika hii siyo tu kwa sababu ya kuwa na mambo mengi akilini..."

"Sasa inaweza kuwa nini? Kuna mwanaume yeyote ambaye labda... anakuchokoza-chokoza labda kimapenzi au...."

"Nini?"

"Yaani, labda kuna mtu anayekuchokonoa vibaya ndiyo maana...."

"Efraim nakwambia kuhusu mkazo naopata kwa sababu ya haya mambo ya ajabu halafu wewe unaniambia masuala gani tena hayo?"

"Am sorry... nilikuwa tu najaribu kuangalia labda kuna shida hapo. Mtu anaweza hata akakutupia madude mabaya kwa mambo kama hizo, ni muhimu sana kuwa mwangalifu, ndiyo nachosema tu..."

"Agh, me kiukweli ninachoshwa sana na haya mambo. Itabidi nikaonane na shehe..." Namouih akasema.

"Au labda tukupeleke kwa Mwamposa?" Efraim Donald akasema kiutani.

Namouih akamwangalia na kushindwa kujizuia kutoa tabasamu ingawa kweli alikuwa amefadhaika.

"Ahahah... pole honey, pole. Jitahidi tu kufanya vitu hivi. Achana na masuala yale tuliyozungumzia jana, ni moja kati ya mambo yanayokupa huo mkazo. Halafu... labda itakuwa vyema kama usipoenda kazini leo maana hata hivyo ni Jumamosi..." Efraim akamwambia.

"No, kwenda ni muhimu. Nitakuwa sawa. Hili jambo lilinitikisa sana jana lakini... nitakuwa sawa," Namouih akasema.

"Una uhakika?" Efraim akamuuliza.

Namouih akatikisa kichwa kukubali.

Basi, Efraim Donald akambusu mke wake kwenye paji la uso wake na kumwambia yeye anaingia bafuni kuoga, naye akamwacha kitandani hapo akiwa bado na mawazo mengi. Kulikuwa na hilo suala la Draxton, ambalo akili yake ilimwambia kuwa lilihusiana kwa njia fulani na hili suala la mambo yenye kuhofisha yaliyokuwa yakimpata. Usiku waliomgonga yule kiumbe na yeye kuiona ile tattoo, aliota ndoto mbaya. Siku aliyoona tattoo ile mgongoni kwa Draxton, akaota ndoto mbaya. Jana ndiyo alimfata Draxton na kumuuliza kwa ujasiri kabisa kuhusu mambo yote ya ajabu kumhusu, halafu usiku akaona kitu kile chenye kutisha. Sasa kilikuwa kimebaki nini?

Alielewa kwamba wengine wangeona maoni yake kuwa kama ya mtu aliyepandwa tu na jazba, lakini bado hakutaka kukata tamaa ya kujua na kufichua mabaya ya mwanaume yule. Akajiondoa kitandani hapo na kwenda kuoga pia baada ya Efraim kutoka bafuni ili naye ajiandae kwenda kazini.

★★

Muda mfupi baadaye, Namouih akawa ofisini kwake akishughulika na mambo machache kwa siku hii. Kwa sababu ilikuwa Jumamosi kweli hakukuwa na mambo mengi, hata mume wake alikuwa amekwenda kazini lakini hakungekuwa na mambo mengi sana labda tu kwa sababu yalikuwa ya lazima kufanywa. Mpaka inafika saa tano, Namouih hakuwa ametoka kwenye kiti chake wala kupata kiamsha kinywa, na ndipo rafiki yake kipenzi akaingia muda huo kwa kuwa hawakuonana tokea alipofika.

Blandina aliingia akiwa na shauku yake ya kama kawaida, jambo lililoonyesha kuwa sasa alikuwa sawa kihisia, lakini Namouih akawa wa baridi tu, akionekana kuwa makini na kile alichoandika kwenye kompyuta yake.

"Steplar yako ina pini?" Blandina akauliza.

"Ndiyo, yako haina?" Namouih akamuuliza pia bila kumwangalia.

"Imeishiwa, nipe yako nikaitumie..."

"Chukua."

Blandina akasogea karibu na meza ya Namouih ili kuichukua, kisha akauliza, "Umeshapiga breakfast?"

Namouih akatikisa kichwa kukataa.

"Well, mambo kati yangu na Draxton yako vizuri sa'hivi, ali-apologize jana, tuka-spend muda pamoja," Blandina akasema huku akitabasamu.

"Okay. Hongera Blandina," Namouih akasema hivyo bila hata kumwangalia usoni.

"Niliona picha uliyopost Insta uko na Donald jana usiku. Mlienda wapi?"

"Kuzurura."

"Mmm... si useme wapi kabisa, short answer za nini sasa?"

Namouih akamwangalia, kisha akasema, "Tulienda kutembea town, tukatembea kuzungukia sehemu mbalimbali, tukala dinner, tukaingia mall, tukanunua vitu kama saa, cheni, mikufu, mkaa, pemba, vijola... tukatoka hapo tukaenda park ile yenye rollercoaster, tukanunua ice cream, akanilisha, akaniambia mimi ni mrembo sana, nikacheka, akanibusu, tukabembea, akanibeba, tukarudi nyumbani baada ya kupiga picha, ndo' nikapost... halafu tukalala."

Blandina akabaki kumtazama tu, kisha akasema, "Una makusudi sana."

"Nini sasa, si ndiyo jibu refu ulilokuwa unataka?"

"Yeah, lakini hujagusia na ile part ya lala nikupandilie."

Namouih akairudia kompyuta yake na kusema, "Tulikuwa tumechoka kwa hiyo... hiyo haikutokea."

"Aisee! Unatia huruma sana best..."

"Na mimi nisemeje kuhusu wewe?"

"Angalau kuna sababu upande wangu, wewe mommy hupewi sababu yoyote... no offence," Blandina akasema.

Namouih akabaki kimya tu, akionekana makini sana.

"Umefanyaje mkononi, mbona umeweka plasta?" Blandina akauliza.

"Mtu wako ndiyo amenifanya hivi" ni jibu ambalo lilitaka kumtoka Namouih, tena kwa hasira, lakini akaishia tu kumwangalia rafiki yake usoni.

"Nini sasa?" Blandina akauliza.

"Niliumia tu kidogo, siyo kitu kubwa," Namouih akaficha ukweli.

"Okay, inaonekana unahitaji kuachwa kwanza la sivyo utameza mtu..."

"Hey... kila kitu kiko fine kati ya me na wewe, usifikiri labda...."

"Usiwaze honey, nakujua vyema. Chochote unachopitia jua kwamba itakuwa rahisi zaidi kukishinda ukishusha chai kidogo na kaushauri kutoka kwa rafiki... ukikahitaji unajua pa kunipata," Blandina akamwambia.

Namouih akatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kukubali.

"Okay, baadaye," Blandina akaaga na kuanza kuondoka.

Namouih akawa anamtazama tu rafiki yake, akihisi ni kama hakutenda haki kutomwambia alichofanya jana, lakini ikiwa angesababisha audhike tena isingekuwa jambo zuri, hivyo kutomwambia ikaonekana kuwa kitu cha busara. Blandina ndiyo alikuwa ameukaribia tu mlango ili atoke pale ulipofunguliwa na msaidizi mwingine wa kampuni hiyo. Akasimama tu na kumwambia Blandina kwamba mwanasheria Namouih alikuwa na mgeni, naye Blandina akasema amruhusu kuingia. Msaidizi huyo akapisha kidogo, na mgeni huyo akaingia hapo.

Blandina akaachia tabasamu la furaha baada ya kumwona Draxton, akiwa amefika bila kutarajiwa. Alikuwa amevalia koti lenye rangi ya blue-nyeusi juu ya T-shirt nyeupe, suruali nyeusi, na viatu vyeusi vya kisasa vyenye muundo kama raba. Baada ya Namouih kumwona, akaacha alichokuwa anafanya kwenye kompyuta yake na kubaki amemtazama tu, kwa sababu uwepo wake wa ghafla hapo ulimaanisha bila shaka kuna jambo halikuwa sawa. Hangeweza kujizuia kumtazama kwa hisia kali, lakini akajitahidi kutofanya hilo lipite kiasi.

"Draxton!" Blandina akaita kwa shauku.

Draxton akasimama mbele yake, kisha akamtazama Namouih pale alipoketi. Namouih akarudi tu kuitazama kompyuta yake. Msaidizi yule akaondoka.

"Hukuniambia kama unakuja babe," Blandina akasema.

"Aa... nimekuja kumwona Namouih," Draxton akamwambia.

"Okay. Si umeshamwona sasa?"

Draxton akatabasamu kwa mbali, kisha akasema, "Nina mazungumzo naye kidogo. Nitaku-check tukimaliza."

"Okay, utanikuta kwa ofisi yangu..."

"Poa."

Blandina akamgeukia Namouih, na sasa mwanamke huyo alikuwa anamwangalia pia hivyo akampungia vidole kwa njia ya kusema kwa heri, halafu akatoka hapo. Mwanaume akaanza kuelekea mpaka kufika usawa wa meza ya Namouih na kusimama tu mbele yake. Namouih hata kumwangalia hakumwangalia, akiendelea kuonyesha yuko bize na kazi.

"Habari yako Namouih?"

"Unataka nini?"

"Nimekuja kuzungumza nawe kuhusu jana. Nina... ninahitaji kuomba samahani kwa... kukutendea bila..." Draxton akaishia tu hapo.

Namouih akamwangalia na kuuliza, "Bila nini, heshima? Utaweza vipi kutenda kwa heshima wakati ni kitu ambacho huna?"

"Ndiyo maana nakuomba samahani. Nimekuja tu kuomba samahani..."

"Halafu?"

"Sitarajii chochote. Nilichokufanyia hakikuwa sawa... nilijutia. Hakuna kitu cha namna hiyo kitatokea tena ikiwa sote tutaheshimu mipaka yetu dada."

"Kwa hiyo huwa una kawaida ya kuwasukuma au kuwaumiza wanawake wakivuka mipaka yao kwako eh?" Namouih akauliza.

Draxton akaangalia pembeni.

"Unafikiri Blandina atakuona vipi nikimwambia jinsi ulivyonifanyia jana?" Namouih akamuuliza.

"Itakuwa jambo zuri ukimwambia. Kwa sababu nimeshajionyesha kuwa mbaya kwako, ninaweza kuja kuwa mbaya hata kwake pia. Kwa hiyo ni bora ajue nilikuumiza ili naye akae mbali nami... asije kuumia," Draxton akamwambia.

Namouih akamkazia macho yake, akiwa ameshangazwa kiasi na kauli hiyo.

"Ona... ifike tu mahali ambapo muda utapita na sote tutasahau kwamba hii iliwahi kutokea. Ningesema hauna sababu yoyote ya kuwa na mashaka juu yangu lakini sitakulazimisha unione kwa njia yoyote ile. Hayo yatabaki kuwa mawazo yako. Narudia tena kuomba samahani kwa kilichotokea jana," Draxton akasema.

Mwanaume huyu aliyasema maneno hayo kwa njia iliyoonyesha kwamba aliyaamini kabisa, yaani yalikuwa yanatoka moyoni, na Namouih akawa anamtazama tu kama vile anamtathmini.

"Uwe na kazi njema," Draxton akamwambia hivyo, kisha akaanza kuondoka ofisini hapo.

Namouih akamwangalia tu mpaka alipokuwa ameufikia mlango, kisha akasema, "Subiri."

Draxton ndiyo alikuwa ameshika kivutio cha mlango, lakini akageuka kumwangalia baada ya kuambiwa hivyo.

Namouih akanyanyuka kutoka kwenye kiti chake, naye akaanza kutembea taratibu kumwelekea jamaa. Kuna kitu kuhusu mwonekano mzuri sana wa mwanamke huyu kilichofanya Draxton abaki kumtazama tu kama amezubaa, lakini hakuwa na wazo lolote la uvutio kumwelekea. Namouih akamfikia karibu zaidi, na kama ile kawaida, Draxton akafumba macho taratibu na kuinamisha uso wake. Bado jambo hilo lilikuwa moja kati ya mambo yaliyomfanya Namouih aone uajabu ndani ya mwanaume huyu, lakini kwa sasa akaamua tu kulipuuzia. Draxton akanyanyua tena uso wake na kumwangalia machoni, na wote wakawa wakitazamana sawia.

"Unaujua ule msemo wa nimekusamehe ila sitakusahau?" Namouih akamuuliza.

"Ndiyo," Draxton akajibu.

"Well, mimi nimekusamehe kwa kilichotokea jana, na nitasahau kabisa mambo hayo ikiwa tu utaniahidi jambo moja..."

Draxton akabaki tu kumwangalia, kama kumwambia anamsikiliza.

"Usimwambie Blandina. Haitakuwa na faida yoyote nyie mkikatisha mahusiano yenu eti kisa tu ulinikaza mkono," Namouih akasema.

"Si ni wewe ndiye uliyesema utamwambia?"

"Ndiyo, nilikuwa nakujaribu. Nataka tu kuhakikisha kwamba wewe hautamwambia lolote."

Draxton akatazama pembeni.

"Nisikilize. Mimi pia nahitaji kukuomba samahani kwa kila kitu nilichofanya, nili-panick tu. Blandina anafurahia sana kuwa nawe na mimi sitopenda kuona chochote kinamnyang'anya hilo. Nakuomba tu pia usahau mambo yote niliyosema jana. Ninatumaini next time tunakutana itakuwa ni companionship nzuri... ikiwezekana hata tuwe marafiki. Unaonaje?"

Namouih aliyasema maneno hayo kwa uhakika kabisa, naye Draxton akawa anamwangalia tu kama vile bado anataka kuendelea kumsikiliza.

"Vipi... litakuwa jambo zuri au halitafaa?" Namouih akauliza.

"Hapana, ni wazo zuri. Nashukuru kwa kunionyesha msamaha," Draxton akajibu kikawaida tu.

Namouih akatabasamu, kisha akasema, "Sawa. Cheer up. Mimi siyo mbaya sana kama navyoonekana."

"Yeah, wewe siyo mbaya. Unataka tu kuhakikisha kwamba kila kitu na watu unaowapenda wanakuwa sawa, na hilo linakufanya unakuwa imara unapohitaji kusimama kwa ajili yao," Draxton akamwambia.

Namouih akatulia kidogo, kisha akasema, "Asante. Basi... tutaonana nafikiri. Acha niendelee na kazi."

"Yeah, sawa."

"Kaonane na huyo dogo asije kunitafuna kwa kukuchelewesha," Namouih akatania.

"Okay. Jitahidi kula pia. Tumbo lako linaunguruma kama trekta," Draxton akatania pia.

Namouih akapandisha nyusi kuonyesha mshangao, naye Draxton akatoa tabasamu hafifu na kisha kuuvuta mlango na kuondoka.

Mwanamke huyu akavuta pumzi ndefu na kuishusha huku akiwa amefumba macho yake, akijipa utulivu baada ya pindi hiyo iliyokuwa imemfanya ajione kuwa mnafiki wa hali ya juu. Kwa nini? Kwa sababu ni kweli alikuwa akifanya unafiki. Akarudi mezani kwake na kupiga simu kwa mtu muhimu sana, ambaye hakuwa mwingine ila rafiki yake mpelelezi Felix Haule mwenyewe. Akamwambia kuna jambo la muhimu sana alitaka wazungumzie, hivyo wakutane ana kwa ana ili ampe taarifa zote mubashara.

Felix kama Felix hakukwaza, akimwambia rafiki yake kwamba hata akipenda basi wakutane mida hiyo hiyo, naye Namouih akasema wakutane saa saba mchana sehemu isiyo maalumu kikazi. Baada ya hapo, mwanamke huyu akakata simu na kuendelea na mambo mengine kwanza, akiwa ameshauweka tayari mpango wake wa kumhusisha Felix kwenye utata kumwelekea Draxton, ili mpelelezi huyo amsaidie kumnasa jamaa katika maovu ambayo Namouih aliamini ni Draxton ndiye aliyehusika kuyatenda.


★★★


Upande wa bwana Efraim Donald. Mzee wa kazi tu alikuwa ofisini kwake siku hii, kama kawaida akifanya mambo ya kiofisi. Ubize mwingi ni kitu ambacho kilikuwa cha kawaida sana kwake kila siku ambayo aliingia ofisini au kutoka kushughulika na mambo ya kikazi, hivyo kwa leo pia alijikuta amemezwa na kazi nyingi ingawa ilikuwa Jumamosi.

Lakini mwanaume huyu alikuwa amekusudia kuwahi kumaliza mambo yake ili ampitie na mke wake, waende sehemu fulani pamoja kisha waelekee nyumbani, au kama Namouih angehitaji kuendelea na kazi basi yeye Efraim atangulie nyumbani. Aliona ingefaa kufanya hivyo hasa kutokana na jinsi mambo mengi yalivyoonekana kumchanganya sana mke wake siku za hivi karibuni, naye akajitahidi kuzihimilisha kazi vizuri ili kufikia saa saba mchana asiwe na mambo ya lazima ya kufanya kisha ndiyo amtafute mke wake.

Ilipofika mida ya saa sita hivi, akapigiwa simu na rafiki yake wa karibu zaidi, aliyeitwa Mr. Godwin Shigela. Huyu kwa Efraim Donald ndiyo alikuwa "best friend," kwa sababu walijuana kwa muda mrefu na walisaidiana kwa mambo mengi. Mwanaume huyo alikuwa mtu mwenye pesa nyingi na mafanikio mengi pia, hivyo yeye na Efraim Donald walikuwa kama timu ya mapedeshee wawili tu. Efraim akaipokea simu huku akitabasamu kwa kuwa alifurahi sana kuipata simu ya rafiki yake.

"Kaka kaka," Efraim Donald akasema.

"Vipi kijana wangu?" Godwin akauliza kutokea upande wa pili.

"Ah ujana ushapita, naelekea ukongwe sasa..."

"Hahahaha... za huko?"

"Nzuri tu. Uko wapi sasa hivi?"

"Nimeingia Nairobi juzi kati hapo."

"Mh... wewe si ulisema ukitoka kisiwani unakuja moja kwa moja huku?"

"Yeah, change of plans. Kama ujuavyo mambo yetu bwana, kidogo tu uko hapa au pale, hupumziki yaani..."

"Dah, fanya utoke sasa huko brother, mwezi wa saba huu sijaliona lisura lako..."

"Haaaahahah... nishakuwa babu mandevu. Nitakuja tu... ndiyo nilikuwa nimekupigia kukujulisha niko huku kwa hiyo kama ulikuwa umeniandalia party itabidi mgeni rasmi abadilishwe..."

"Ahahah... pesa za mgomo, party wapi kaka?"

"Aa kwenda zako."

Simu ya mezani ofisini kwake Efraim ikaanza kuita, lakini akaipuuzia.

"Huko mshiko unakamatika eh?" Efraim akaendelea kuongea na Godwin.

"Kama vumbi la mpunga..."

"Usinambie! Dah, kweli maisha mazuri sana usipokuwa loser..."

"Hahahaha... wazogaji watuachie sisi tufurahie pepo ndani ya hii dunia iliyo kama jehanamu," Godwin akasema.

Efraim akacheka kidogo.

"Vipi bi mkubwa yuko poa?" Godwin akauliza.

"Yuko poa. Umri unaenda lakini hazeeki," Efraim akamwambia.

"Hah... je mrembo wetu?"

"Nani, shemeji yako?"

"Kwani kuna mwingine?"

"Ahahahah... yupo poa tu. Bado hakuna anayeufikia utajiri wa sura nzuri kwake..."

"Hahahaha... unapenda kumringia sana bwege wewe. Vipi lakini lile suala la ndoto? Bado zinamsumbua?"

"Yeah, nilikwambia imekuwa ikiendelea kutokea, sa'hivi ameanza hadi kuona mambo ya vivuli yaani... ila anasema atakuwa sawa."

"Well, unajua itakuwa problem kama akiendelea hivyo. Mlete kwangu basi..."

"Hahahah... kichwa chako! Ila hapana, haitakuwa na shida wala usijali..."

"Una uhakika? Uchizi ndiyo unaanzaga hivyo hivyo, anapiga kelele, anakimbia kimbia, mwisho wa siku hauko naye tena. Na we' ni kama umepuuzia hilo rafiki yangu, ile mali siyo ya luiacha iteseke namna ile..."

"Ahah... brother, inaonekana unatamani sana kuja kuupeleka moto kwa mke wangu siku moja eeh?"

"Ahahahah... kweli umeoa mwanamke anayejielewa. Ungechelewa kidogo tu...."

"Ungefanyaje? Unajua kwamba nina pistol ndani?"

Godwin akacheka na kusema, "Huko sitafika, we' enjoy tu hilo kombe. Piga hadi na watoto sita kabisa."

Simu ya mezani ikawa imeacha kutoa mwito baada ya kuita kwa muda mrefu.

Efraim akaendelea kuongea, "Heheheh... bwege wewe. Anita hajambo kwanza?"

"Anita yupi tena? Yule tuliyekutana naye kwenye boti?"

"Hamna, yule kibibi mweupe anayependa cocktail sana..."

"Unaongelea yule anayevaa vimini zaidi, jicho la kusinzia?"

"Achana na hilo jimama. Aisee, kaka umewapanga kama ndoo za maji hahahah..." Efraim akasema huku akicheka.

"Aaa... kama ujuavyo, hakuna kuremba. Wakijileta ni kuwafumua tu..."

Efraim Donald akiwa anaendelea kuongea na rafiki yake, msaidizi wake akaingia ofisini humo na kumfata kisha kusimama mbele ya meza yake.

"Hey kaka, subiri mara moja..." Efraim akamwambia hivyo Godwin, kisha akaishusha simu kwa ufupi. "Vipi Lucy?" akamuuliza msaidizi wake.

Msaidizi huyo, mwanamke mzuri na mweupe aliyevalia kwa unadhifu wa kiofisi, akasema, "Una mgeni."

"Nani? Sina mipango ya kukutana na mtu yeyote leo hapa," Efraim akasema.

"Anasema ni mdogo wako," Lucy akamwambia.

"Mdogo wangu? Nani?"

"Anaitwa Sasha."

"Sa.... oooh Sasha! Mdogo mdogo, mweupe?"

"Ndiyo."

"Okay. Mwambie aje. Mwambie aje ndani."

Lucy akatikisa kichwa kukubali, kisha akaondoka ofisini hapo taratibu.

"Hey Godwin..." Efraim akairudia simu.

"Nilikuwa namsikia hawala yako hapo anaongea," Godwin akasema.

Efraim akacheka kidogo, kisha akasema, "Acha zako. Nina mgeni asiye rasmi hapa, nitakucheki mida baadaye."

"Wala hata usijisumbue, we' piga tu mambo yako hayo yasiyo rasmi," Godwin akamwambia kiutani.

Efraim Donald akatabasamu na kuagana naye, kisha akaketi sawa akisubiri ujio wa dada mdogo wa mke wake.

Mlango wa kuingilia hapo ukafunguliwa tena, naye Lucy akaonekana kusimama hapo kama anapisha mtu, na hatimaye binti Sasha akaingia. Alikuwa amevalia shati jeupe la kike lenye mikono mirefu, sketi iliyoishia magotini yenye rangi fulani ya kijivu hivi, na viatu "simple" vilivyokuwa rahisi kutembelea. Alisuka mtindo wa rasta nene zilizolazwa kuelekea nyuma ya kichwa chake lakini zikiishia shingoni tu, fupi yaani, naye alibeba kimkoba cha rangi nyeusi mkononi. Alionekana kama mtu wa ofisini zaidi kuliko mwanafunzi, hasa kutokana na kuwa mrefu karibu na urefu wa dada yake. Lucy akaufunga mlango na kutoka, akimwacha Sasha amesimama huku anamwangalia kaka-mkwe wake usoni.

Efraim akaachia tabasamu lililoonyesha jinsi alivyofurahi sana kumwona, kisha akasema, "Sasha. Karibu. Karibu sana."

"Asante kaka," Sasha akajibu kwa sauti yake nyororo.

"Njoo... njoo ukae," Efraim akamwambia.

Sasha akatembea taratibu kuielekea meza ya Efraim, kisha akaketi kwenye kiti cha upande wa kushoto kutokea pale alipotazamana naye mezani.

"Aisee... karibu sana mdogo wangu. Yaani umeni-surprise," Efraim Donald akasema.

Sasha akatabasamu na kuendelea tu kumwangalia.

"Habari za shule?"

"Nzuri tu kaka."

"Ndiyo unaingia form six eh?"

"Ndiyo."

"Hongera sana. Masomo vipi?"

"Safi tu."

"Ulichukua combi gani?"

"PCB."

"Wow! Unaenda kuwa daktari kumbe!"

Sasha akatabasamu tu.

"Safi. Safi sana. Komaa haswa..."

"Ndiyo, nitakomaa..."

"Very good. Ila... niseme pole kidogo Sasha. Mimi na wewe hatujawahi kukaa kuzungumza mengi. Mambo yanakuwa tight sana..."

"Usijali kaka, ninaelewa. Una majukumu mengi."

"Yaani! Kazi mpaka basi. Ila nashukuru umekuja kunitembelea. Ni kitambo eeh... tokea mara ya kwanza tumekuja huku na Namouih, sikudhani hata kama ungepakumbuka..."

"Siwezi kupasahau. Kampuni yako ni kubwa yaani hata siyo rahisi kupotea."

"Ahahah... nafurahi sana. Karibu. Sijui... kuna jambo fulani umekuja kuzungumzia au ni ili kunipa hi tu?" Efraim akauliza.

"Aa... vyote. Kwanza samahani kaka kwa kuja bila kutoa taarifa..."

"Ondoa shaka mdogo wangu. Unakaribishwa muda wowote, ila ni kama tu ukinikuta maana mara nyingi sikai tu hapa..."

Sasha akatabasamu tu tena na kuangalia chini.

"Mambo yanasemaje?" Efraim Donald akamuuliza.

"Nilikuwa nimekuja kuongea nawe kuhusu jambo fulani. Yaani tu... sijui hata nianzie wapi..."

"Usijali Sasha. Unaweza kuniambia chochote. Jisikie huru kabisa."

"Okay. You see... nina rafiki yangu ambaye... ana tatizo fulani baya sana. Limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu, na... linatakiwa kutafutiwa suluhu haraka la sivyo... atakufa," Sasha akasema.

"Oh Sasha, hiyo ni mbaya. Pole. Pole kwa rafiki yako pia..."

"Asante."

"Anasumbuliwa na nini?"

"Saratani."

"Aaa... sawa. Unasoma naye?"

"Hapana. Yeye hasomi. Alikuwa tu anafanya biashara ndogo ndogo, lakini sasa hivi yuko hospitali. Alikuwa ameanza kupata matibabu... ila kuna njia nzuri zaidi zinazohitajika kufanywa ili wamsaidie kuiondoa..."

"Kuiondoa kabisa?"

"Ndiyo... a... apone kabisa."

"Okay... sawa. Ungependa nikusaidie vipi mdogo wangu?" Efraim akauliza.

"Wangemfanyia... yaani... wangempa hiyo tiba ila sema, gharama yake ni kubwa na... alikuwa amebakiza kiasi fulani kumalizia lakini kufikia sasa bado hajapata. Anahitaji, ametafuta na kutafutiwa za kuongezea lakini hajapata. Nataka sana kumsaidia ila nashindwa," Sasha akaeleza.

"Amebakiza kiasi gani?" Efraim akauliza.

"Laki tisa," Sasha akajibu.

"Oh sawa. Umejaribu kuongea na Namo...."

"Hapana!" Sasha akamkatisha upesi.

Efraim Donald akaendelea tu kumwangalia kwa utulivu.

"Na..namaanisha... dada ndiyo... ndiyo alikuwa ametoka kunilipia ada ya mwaka mzima, na... najua kuna mambo mengi anashughulikia... nahisi kumwomba anisaidie kwa hili itakuwa kama... yaani kama mzigo kwake... halafu..."

"Okay Sasha, usihofu. Nimekuelewa. Usijali," Efraim akamtuliza.

Sasha akaangalia chini tu, akionekana kuwa na wasiwasi kiasi.

"Usijali Sasha nitakusaidia. Utampatia rafiki yako kiasi kilichobaki ili atibiwe, sawa?" Efraim akasema.

Sasha akamwangalia, kisha akasema, "Nashukuru sana kaka. Yaani... sijui niseme nini tu..."

"Nashukuru uliyosema inatosha," Efraim akamwambia.

"Hapana, naona kama haitoshi. Kaka nikija kuanza kazi nitahakikisha nakulipa kwa sababu ya msaada unaonipa... namaanisha... kwa ajili ya rafiki yangu..."

"Ondoa shaka Sasha. Usiwaze kabisa. Subiri..."

Efraim Donald akamwambia hivyo na kuchukua kijitabu fulani kidogo, kisha akaanza kuandika juu ya kikaratasi kimoja ndani yake.

"Unajua kutoa pesa kwa mfumo wa cheque?"

"Ndiyo," Sasha akajibu.

"Okay."

Efraim Donald akamaliza kuiandikia karatasi hiyo na kuichana kwa uangalifu kutoka kwenye kitabu hicho, kisha akampatia binti, ambaye aliipokea kwa mikono miwili. Sura ya Sasha ikakunjamana kimaswali baada ya kusoma kilichoandikwa, naye akamwangalia kaka-mkwe wake kwa mshangao.

"Kaka... mbona... mbona umeandika milioni mbili?" Sasha akauliza.

"Ndiyo ni milioni mbili. Au ulikuwa hujui kwamba we' ni wa gharama?" Efraim akamwambia.

Sasha akaganda kwa kumtazama kama vile hamwelewi kabisa.

Efraim Donald akacheka kidogo na kusema, "Nakutania tu. Unaweza kufanya unayohitaji sasa. Msaidie rafiki yako, na we' jihudumie kwa chochote unachotaka."

"Lakini kaka, hiki ni kiasi kikubwa... siwezi kukubali hii yote..."

"Sasha take it easy. Relax. Unaniheshimu kama kaka, si ndiyo? Nakuomba uichukue tafadhali. Sitamwambia Namouih lolote. Nimefurahi sana kwamba umekuja kwangu badala ya kuamua kutafuta njia za mbali au kulibeba hili mwenyewe. Kwa hiyo... uwe na amani. Muda wowote ukihitaji nikusaidie usisite kuniambia, umeelewa mdogo wangu?" Efraim akamwambia kwa upole.

Sasha akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa. "Asante sana kaka Donald," akasema.

"Karibu."

"Yaani... ahah... sikutegemea kabisa kama..."

"Usiwaze... hapa ni anytime. Be free."

Efraim akamwambia hivyo, kisha akakunja kiganja chake na kumnyooshea mkono. Sasha akatabasamu na kufanya hivyo hivyo pia, nao wakagonga tano kirafiki.

"Umekuja huku kwa usafiri gani?" Efraim Donald akauliza.

"Kutokea kule karibu na hostel nilichukua mwendokasi. Nilipofika maeneo ya huku nikachukua gari za abiria mpaka hapa."

"Mmm... na foleni?"

"Haikuwa kubwa... ahah..."

"Umejitahidi. Piga picha kama ungekuta sipo sasa," Efraim akasema.

Sasha akacheka kidogo.

"Unatakiwa urudi mapema? Au... unapanga kuonana na dada?"

"Ninataka kuwahi. Sikuwa nimepanga kuonana na Namouih... sikutaka hata ajue nipo huku," Sasha akasema kwa sauti ya chini kidogo.

"Aaaa sawa. I got you," Efraim akamwambia na kumkonyeza kirafiki.

Sasha akatabasamu na kusema, "Shukrani sana kaka Donald. Sana."

"You're welcome. Sana. Ukipenda naweza kukufanyia mpango wa usafiri ukupeleke hadi kule hostel moja kwa moja," Efraim akamwambia.

"Aa, hapana, haina shida. Nitachukua tu usafiri kama nilivyokuja. Msaada ulionipatia ni mkubwa sana kaka kukuomba mwingine..."

Efraim Donald akatabasamu na kutikisa kichwa kuonyesha ameelewa.

"Basi, ngoja me nikuache uendelee na kazi kaka. Na sijasahau kuhusu kuja kukulipa. Nitakulipa tu, upende usipende," Sasha akasema na kumfanya Efraim acheke kidogo.

Baada ya hapo, binti akanyanyuka na kumuaga tena kaka-mkwe wake, ambaye naye akamuaga kwa kusema wangeonana tena. Efraim alikuwa anataka kunyanyuka ili amsindikize Sasha nje, lakini binti huyu akasisitiza kwamba haikuwa na shida; yeye angeondoka tu upesi kwa hiyo kaka mkubwa aendelee na kazi zake. Akaanza kuondoka huku akihisi furaha kiasi moyoni, hasa kwa kupewa kile ambacho kilipita matarajio yake, na jinsi Efraim alivyomtendea kwa heshima na ukarimu. Akawa anaiingiza karatasi ile ya cheki kwenye mkoba wake mdogo huku akitembea kuelekea mlangoni, nayo ikadondoka chini kabisa. Aliiona, na katika tendo la haraka la mwili wake, akachuchumaa ili aikote upesi. Alipoifikia tu chini, akawa ametambua jambo fulani lililotokea bila yeye kutazamia.

Kuchuchumaa kwake kulifanya shati lake lijivute kiasi kwa kupanda juu kutokea nyuma, na hivyo sehemu ya kiuno kwa nyuma ikafunuka. Sketi yake ilikuwa kwa usawa huo huo pia, lakini nguo yake ya ndani, chupi nyepesi ya rangi ya pink, ilikuwa imepita kwa juu kiasi kutokea kwenye mstari uliotenganisha mashavu ya kalio lake, hivyo kwa uwazi huo ikawa wazi kwake kwamba ilionekana vizuri kwa nyuma. Akaiokota karatasi upesi na kusimama, akilivuta shati lake chini kujisitiri, naye akageukia nyuma yake kuangalia kama Efraim aliona jambo hilo lililomtamausha binti huyu kwa kadiri fulani. Lakini ndiyo kwanza Efraim Donald alikuwa bize na kompyuta yake, akionekana makini kuandika mambo fulani, naye Sasha akashusha pumzi ya utulivu na kuufikia mlango, kisha akatoka hapo hatimaye.

Mwanadada huyu alihisi furaha sana. Kutoka na milioni mbili halikuwa jambo alilotazamia kabisa. Kwa upande mwingine, alijihisi vibaya kwa kadiri fulani, kwa sababu ingawa alikuwa anaihitaji pesa hiyo, aliipata kwa njia ya uwongo. Huu ndiyo uliokuwa ushauri ambao rafiki yake, Sabrina, alikuwa amempatia baada ya Sasha kumwelezea kisa chake cha jinsi mpenzi wake alivyotoweka na kiasi cha laki tisa alizompa. Kwa kuwa Sasha aliogopa kusema lolote kwa Namouih, Sabrina alimpa ushauri wa kumwomba shemeji yake amsaidie bila kumjulisha dada yake, kwa sababu alijua kuhusu namna ambavyo mwanaume huyo mkarimu alijitoa kusaidia kuokoa maisha ya baba yao kipindi cha nyuma, yaani mzee Masoud, ingawa baadaye alikufa.

Kwa hiyo Sabrina alimsaidia rafiki yake kubuni hadithi hii ya rafiki kuumwa saratani, ili Sasha apate pesa ya kufidishia kile ambacho mpenzi wake mshenzi aliiba. Mpaka wakati huu, bado huyo Shomari hakuwa amepatikana. Kiukweli, haikuwa jambo rahisi kwa binti huyu kumdanganya shemeji yake, lakini mwisho wa siku akawa amefanikiwa, na ambacho kingebaki tu kwa sasa ilikuwa ni Namouih kutokujua lolote, maana aliuelewa moto wa dada yake vizuri.


★★★


Muda wa saa saba ulipofika, Namouih akaondoka ofisini kwake ili kwenda kukutana na Felix hatimaye. Walikuwa wameshapanga kukutana kwenye mgahawa fulani wa kisasa, na mpaka kufikia muda huu Namouih hakuwa ameweka chochote tumboni mwake, hivyo angeitumia nafasi hiyo kupata chakula pia. Akaelekea huko baada ya kuagana na Blandina, aliyemwambia kwamba alikuwa na mipango na Draxton pia jioni ya siku hii, bila kujua kwamba rafiki yake alikuwa na mpango wa kumweka mpenzi wake huyo shabaha ya kumfatilia kisiri, na ndiyo alikuwa anaenda kuiweka sawa mipango hiyo.

Namouih akafika kwenye mgahawa huo na kumkuta rafiki yake mpelelezi akiwa hapo tayari. Wakasalimiana kwa kukumbatiana, kisha Felix akamwongoza bibie mpaka kwenye meza aliyokuwa amekwishachukua mapema. Ilikuwa kwa sehemu ya nje ya jengo la mgahawa huo maridadi, kukiwa na meza kadhaa hapo zenye watu pia waliopata milo na maongezi. Namouih akaketi, naye Felix akamwita mhudumu aliyekuwa karibu ili waagize msosi na vinywaji. Kila mmoja akaagiza chakula chepesi tu na sharubati za maembe, kisha wakaanza kuzungumzia mambo mbalimbali ya kirafiki mpaka Felix alipogusia kile ambacho Namouih alisema angemwambia.

"Yeah, nilikuwa nataka kushiba kwanza ndo' nikurushie mzigo sasa," Namouih akamwambia.

"We' urushe tu. Unaweza ukasubiria tushibe, ukaurusha, njaa ikarudi tena," Felix akasema.

"Mhm... kweli Felix ni jambo zito kiasi nalotaka kukuomba..."

"Nini, mechi au?"

"Ahahah... acha mambo yako..."

"Kama kuna boya amekuzingua vibaya jua hii ndiyo sehemu sahihi ya kufikia," Felix akasema.

"Asante, lakini... si kihivyo. Kuna mtu... Felix kuna mtu nahisi ana-connect na vifo vya hao wasichana uliokuwa ukifanyia upelelezi."

"Come again?"

"Ni instinct tu, sina uhakika sa...."

"Nani?" Felix akamkatisha.

"Draxton."

"Ndiyo nani?"

"Boyfriend wake Blandina..."

"Acha masihara basi!"

"Kweli. Unamfahamu?"

"Namsikia. Si ndiyo yule aliyekufanya ukaipoteza kesi ya Agnes?"

"Ndiyo, na tena na hapo najua alitumia uchawi... hata kama Agnes ndiyo alikuwa na hatia..."

Felix akacheka kidogo.

"Ninahisi kabisa kuna kitu anaficha."

"Kweli?"

"Kweli. Hayuko poa yule mwanaume... na Felix, mimi nahofia...."

"Usalama wa Blandina," Felix akamalizia maneno yake.

"Ndiyo."

"Nini kimekufanya ufikiri ni yeye, au ana-connect vipi na hii ishu?" Felix akauliza.

Vyakula vikawa vimeletwa, nao wakasubiri mpaka mhudumu alipomaliza kuwawekea kwa sehemu zao na kuondoka, kisha wakaanza kula taratibu huku Namouih akimwelezea Felix mambo aliyofikiria. Akamwambia kuhusu usiku ule walipomgonga mtu fulani wa ajabu aliyekuwa na mchoro wa tattoo mgongoni ambayo alikuja kuiona mgongoni kwa Draxton pia; ikiwa ni maneno yale yale. Akamwambia kuhusu usiku ule Agnes aliouawa, jinsi ambavyo alimwona Draxton hapo na gari lake kisha akaondoka upesi kabla ya maaskari kufika, na namna ambavyo mwanaume huyo alimtendea siku ya jana alipomfata na kumuuliza ikiwa alihusika na vitu vibaya vilivyokuwa vinaendelea.

"Mambo unayosema yana-make sense, lakini bado najiuliza ni kwa nini alikuacha tu hiyo jana. Ikiwa yeye ni serial killer usingekuwepo hapa sasa hivi," Felix akasema.

"Na leo kanifata ofisini eti kuniomba samahani kwa kilichotokea. Ni huyu huyu ambaye jana niliposema tu kuhusu kuwaua wasichana alinikaba nusu kuniua, halafu leo anajifanya malaika. Sijui anataka kuthibitisha nini?" Namouih akaongea kwa kuudhika.

"Labda atakuwa mgonjwa wa akili. Ninajua watu ambao huwa wanaonekana kuwa sawa kwa nje lakini vitu wanavyofanya gizani ni vibaya mno," Felix akasema.

"Na jinsi alivyo vizuri kwenye kazi zake unadhani kuna mtu ataamini hilo? Nimemwambia Efraim jana lakini hakuniamini..."

"Ahahah... bwana mkubwa akakuona kama wacko..."

"We' acha tu," Namouih akasema hivyo na kuendelea kula taratibu.

"Hmm... okay. Nitamchunguza huyu jamaa. Ikiwa anahusika kweli nitahakikisha anakuja kupata adhabu ambayo hakuna mtu aliwahi kupata kabla," Felix akaongea kwa uhakika.

"Unaweza ukakuta anashirikiana na watu wengine."

"Nikigundua anahusika kweli nitamtumia atuongoze kwa wenzake. Natakiwa nianze ku-monitor nyendo zake haraka, na wewe pia jitahidi kuigiza kwamba kila kitu kiko normal ili asishtukie lolote. Blandi ndo' hana clue kabisa?"

"Yaani utafikiri amerogwa! Hatanisikiliza kabisa na anaweza akawa anajiweka hatarini," Namouih akasema.

Simu yake Namouih ikaanza kuita.

"Nitaharakisha uchunguzi. Umefanya vizuri kuniambia, utapaswa tu kusubiri sasa," Felix akasema.

Namouih akaangalia simu yake na kukuta ni mume wake ndiyo anapiga, akamwonyesha Felix kwamba mwenye mali ndiyo alikuwa anapiga, naye Felix akatabasamu na kuendelea kula. Efraim Donald alikuwa anamuuliza mke wake ikiwa alikuwa ofisini muda huo ili ampitie na labda waende kupata chakula sehemu fulani kisha waelekee nyumbani, lakini Namouih akamwambia alikuwa ameshakula na alitoka ofisini kwenda sehemu nyingine kukutana na mtu ili azungumze naye mambo ya kikazi, hivyo yeye Efraim atangulie tu. Efraim hakuwa na neno, naye akaagana naye vizuri kisha simu zikakatwa.

"Bwana mkubwa anaku-mind sana," Felix akasema.

"Kivipi?"

"Ahah... una gari lako mwenyewe lakini bado anataka kukupitia ili mwende wote home..."

"Aaa... anapenda kunipeti, si unajua me kwake 10 ya 10?"

Felix akacheka.

"Mara nyingi akinipitiaga gari huwa naliacha tu kazini, then siku inayofuata ananipeleka kwa lake," Namouih akamwambia.

"Mmm... una raha sana. Kila ndoa ina matatizo lakini we' ni kama hayakupatagi kabisa. Siwezi kusema ulimnywea dawa maana sura tu hiyo ni mwisho...."

Namouih akacheka, akiwa amewaza namna ambavyo Felix hakujua kihalisi kwamba hata yeye alikuwa na mikazo kwenye ndoa yake, na marafiki hawa wakaendelea kuzungumza huku wakimalizia vinywaji na chakula. Walipomaliza, Felix akalipia ingawa Namouih alitaka kufanya hivyo badala yake kwa kuwa mkutano huu aliuitisha yeye. Wakatoka hapo, Felix akitembea kwa ukaribu na Namouih mpaka walipolifikia gari la bibie na kusimama wakimalizia maongezi, kisha wakakumbatiana na kuagana. Namouih akaingia ndani ya gari lake baada ya Felix kumfungulia mlango kiutani wa kirafiki, naye mrembo akaliwasha na kuondoka eneo hilo.

Hakungekuwa na yeyote kati yao ambaye angetambua kwamba tokea Namouih alipofika hapo kukutana na Felix, walikuwa wakitazamwa. Mwanzo mpaka mwisho. Na tena siyo kuangaliwa tu kwa kawaida ile ya watu kumtazama sana Namouih kwa sababu ya urembo wake, bali walikuwa wakiangaliwa kwa hila kabisa. Felix akaanza kulielekea gari lake pia, huku aliyekuwa anawatazama akiendelea kumwangalia mpaka alipoingia ndani ya gari lake na kuondoka, na mtu huyu akaondoka eneo hilo pia.



★★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★★


Usikose sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali ya CHANGE. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.

WhatsApp no: +255 787 604 893

e-mail: eltontonny72@gmail.com
 
Kweli maana inafika mda sitor inapoteza utamu kabisa sababu ya kusubiri sana
Soma hii hapa chini stor kali na mtunzi hana mbambamba
 
Soma hii hapa chini stor kali na mtunzi hana mbambamba
Anzisha uzi wako sio kuweka kwenye uzi wa mwenzako
 
Soma hii hapa chini stor kali na mtunzi hana mbambamba
Acha kuwa mpuuzi wewe. Nimekaa kimya usidhani sioni ujinga unaofanya humu. Heshimu kazi za wenzio, umeshaona nakuja kwako huko kukuvurugia mambo yako? Iwe mwanzo na mwisho
 
CHANGE

Story by Elton Tonny

Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha

R-rated 18+

TANGAZO: Nimebadili namba ya WhatsApp, sitapatikana kwenye ile ya mwanzo tena, bali sasa nitapatikana kwenye hii +255 678 017 280. Karibuni.

Enjoy!

★★★★★★★★★★★★★★★★★

SEHEMU YA KUMI NA NNE

★★★★★★★★★★★★★★★★★


Baada ya Namouih kuwa ameachana na Felix muda mfupi nyuma, sasa mwanamke huyu alikuwa mwendoni kuelekea nyumbani, na leo ingekuwa ni mapema tu anarudi nyumbani hasa kwa kuwa alijua mume wake angekuwa ameshafika huko. Alihisi kujiamini zaidi wakati huu kwa sababu alijua baada ya maongezi yake na rafiki yake mpelelezi, Felix hangemwangusha hata kidogo katika kumchunguza Draxton na hatimaye angeweza kufichua mabaya ya mwanaume yule na kumpa alichostahili.

Akafika nyumbani ikiwa ni saa tisa alasiri, naye akamkuta Efraim Donald akiwa zake chumbani amejipumzisha kwa kusinzia kabisa kitandani. Akaweka mkoba wake pembeni na kuanza kubadili
mavazi, kisha akaingia bafuni kujimwagia maji kwanza. Akiwa bafuni, taswira ya tukio la jana usiku
ikaanza kumwingia akilini tena, akikumbukia jinsi kivuli kile kilivyokuwa kinapenya kuingia ndani ya ofisi yao ya hapo nyumbani na mlango ukifunguka taratibu, kisha kilivyoondoka ghafla tena. Akafumba macho yake na kuendelea kuruhusu maji yaumwagikie mwili wake kwa muda mrefu, kisha akatoka humo na kurudi chumbani.

Kwa kuwa Namouih alikuwa ameshakula, akavaa tu nguo za kawaida na kwenda chini kuonana na Esma, akaongea naye mambo kadha wa kadha yaliyohitajika hapo nyumbani na kucheza na Angelo
kidogo, kisha naye akapanda juu tena na kwenda kitandani kulala. Akawa amewasiliana na mama
yake mzazi, Zakia, kumjulia hali yeye na mdogo wake, yaani Nasma, kisha ndiyo akautafuta usingizi wa mchana. Hakupata shida kusinzia mpaka alipokuja kuamka na kukuta Efraim akiwa ameketi tu kitandani kwa kumpa mgongo huku akisoma vitu fulani kwa simu yake, naye akamgusa mgongoni ili kumjulisha kwamba alikuwa ameamka.

Efraim Donald akageuka na kusema, "Vipi?"

"Safi," Namouih akajibu.

"Unalala kama umekufa yaani..."

"Kwa nini?"

"Hakuna hata sauti ya mkoromo."

"Mhmhm... me huwa sikoromi. Wewe sasa..."

"Ahah... unakuwa uchovu. Ulikula?"

"Ndiyo, si nilikwambia nilitoka kukutana na mtu? Nilikula huko."

"Sawa."

"Saa ngapi?"

"Saa kumi na moja. Ona, kuna sendoff leo ya rafiki yangu wa kazini... tutaenda saa mbili," Efraim
akamwambia.

"Iih! Yaani hata nilikuwa sijajiandaa Efraim..."

"Kwani unahitaji nini, nguo si zipo? We' twende bwana... nimeshalipia double."

Namouih akatabasamu tu, naye akauliza rafiki yake huyo alikuwa nani na alimuoa nani. Efraim Donald akaanza kumwelezea kuhusu sherehe hiyo ambayo alipokea mwaliko wake mapema leo na kufikiria kwenda pamoja na mke wake huko, hivyo kama ni kuanza kujiandaa wangetakiwa waanze mapema maana Efraim alitaka mke wake amsaidie kumtengeneza vizuri kwa ajili ya hafla hiyo. Kweli Namouih akamchagulia mume wake mavazi mazuri na kumnyooshea, naye pia akatafuta vazi zuri sana lenye rangi ya maziwa (cream) ambalo angelivalia na kinguo chepesi kama ushungi wa kichwani lakini kisichofunika kichwa chake chote, yaani kingening'inia kutokea
nyuma ya nywele zake alizozibana. Efraim hakusema lolote kwa mke wake kuhusu ujio wa Sasha
ofisini kwake mapema ya leo.

Walikuja kukamilisha mitoko yao na kuendelea kukaa hapo nyumbani mpaka inafika jioni, kisha
wakaondoka kuelekea huko kwenye sherehe. Ilikuwa ni mwendo mrefu kiasi kufika huko lakini walitumia dakika chache tu hasa kwa kuwa dereva wake Efraim, yule Suleiman, ndiyo alikuwa anawaendesha kwa ustadi wake mwingi kwa hivyo hawakukawia. Walipofika wakaelekea moja kwa moja ndani ya ukumbi, uliokuwa mkubwa na uliopambwa vyema. Walipoingia ndani, baadhi ya watu waliofahamiana na Efraim Donald wakawa wanasalimiana naye na kupata kumjua mke wake
pia, na kama kawaida Namouih alisifiwa kwa urembo wake na kupendeza. Wakaelekea kukaa kwenye meza ambayo ilizungukwa na viti kadhaa, nao wakaletewa vinywaji. Hapo kulikuwa na wanawake wengine wawili na mwanaume mmoja, nao wakawa wanaongea pamoja na wanandoa hawa kwa njia ya kirafiki.

Namouih aliweza kutambua kwamba kuna baadhi ya watu kuzunguka sehemu ya ukumbi huo walioongea kwa njia ya umbea kumwelekea, tena
waziwazi kabisa, lakini akajitahidi kuwapuuzia tu. Muda haukupita sana na bibi harusi akafika hapo. Kama kawaida ya taratibu za sendoff MC akawa anafanya yake ili sherehe isonge mbele, naye Efraim Donald akawa amepigiwa simu na kwenda nje kuzungumza kwanza. Mwanamke mmoja kati ya wale wawili waliokuwa wamekaa meza moja na Namouih akawa ametambua kwamba mwanamke huyu aliishiwa pozi kwa sababu fulani, na tayari alikuwa ameshajua kwa nini. Akakishika kiganja cha Namouih, naye Namouih akamwangalia machoni.

"Hao wanaokuongelea sana ni washakunaku tu, hawakujui, huwajui, kwa hiyo wasikuvurugie usiku
wako kabisa sawa mpenzi?" mwanamke huyo akamwambia kwa sauti ya chini lakini iliyosikika
vyema kwa Namouih.

Namouih akatabasamu tu kwa mbali na kutikisa kichwa chake kukubali.

Mwanamke huyo alikuwa
na umri mkubwa kiasi kumzidi, kwa hiyo kulikuwa na heshima ya mwanzo kumwelekea kutoka kwa
Namouih. Ni wakati huu ndipo Efraim Donald akawa amerejea na kuketi pembeni ya mke wake.

"Namouih... kuna suala limezuka. Ninahitaji kwenda kukutana na kiongozi wa Cargo, ameniita mara
moja," Efraim akamwambia.

"Sasa hivi?" Namouih akasema.

"Ndiyo, yaani kuna mkataba mpya nilikuwa mbioni kusaini pamoja na kampuni yao, sasa hajapata muda na nini lakini sasa hivi ndiyo anataka tukutane ili tuongee vizuri... honey, sitachelewa. Tukimaliza tu narudi, okay?" Efraim akasema.

"Je ikitokea ukachelewa?"

"Hapana, sitachelewa. Na ikiwa kama dharura ya kunichelewesha sana itatokea basi nitamwambia
Suleiman aje akuchukue," Efraim akamwambia.

Namouih akaangalia pembeni.

Efraim Donald akambusu kwenye shavu mara mbili na kukishika kiganja chake, kisha akaondoka
hapo haraka ili awahi huko.

"Ni jambo zuri sana kwamba mume wako anakupenda... anaonyesha hilo waziwazi," yule mwanamke akamwambia Namouih.

Namouih akamtazama na kusema, "Ndiyo. Ni jambo zuri lakini sijui kwa nini kwa wengine huwa ni
dhambi."

"Agh, achana nao. Hakuna hata mmoja kati yao anayejua maisha yako kwa hiyo maneno yao
yasikubabaishe kabisa," mwanamke huyo akamwambia.

"Asante. Naitwa Namouih..."

"Naitwa Salome. Nakufahamu dada. Wewe ni mwanasheria mzuri sana, na kinachowafanya hao pakashumi wapige domo mno ni kuwa umewazidi kwa mambo mengi mno, na bado unazidi
kung'ara..."

Namouih akatabasamu na kusema, "Maneno ya watu hayajawahi kunipa shida. Sema, sipendi tu
hivyo wanavyoninyooshea-nyooshea vidole makusudi tu ili nijue wananisema. Inakera. Lakini
nikinyanyuka kuwafata me ndiyo nitaonekana mpuuzi... haina faida yoyote."

"Ni kweli. Mimi nilijifungua mtoto mlemavu miaka mingi nyuma, na nilisontewa vidole sana na watu... wakaongea mengi mno yaliyonikosesha amani. Lakini nilikuja kujua ukiwaonyesha kwamba
haujali wanachosema, wanakuacha, ila ukiwaonyesha kwamba unajali ndiyo wanakuwa kama wameshinda. Ni kupuuzia tu, maana ukibishana na chizi...."

"Na wewe utaonekana chizi," Namouih akamalizia maneno ya Salome.

"Ndiyo hivyo," Salome akasema.

"Unasema kweli. Pole pia kwa...."

"Aa... usijali. Mwanangu hakuwa mkamilifu kwenye kutokukamilika lakini nilimzaa mwenyewe.
Hakuna aliyenisaidia kumzaa... alikuwa wangu. Hilo lilitosha," Salome akasema.

"Alikuwa?" Namouih akauliza.

"Alikufa miaka mitatu iliyopita. Na wale wale waliokuwa wananisema vibaya ndiyo wakaja kulia pamoja nami. Ahah... dunia hii..."

"Masikini... pole sana Salome..."

"Nilishapoa. Wewe una mambo mengi mazuri, na umesaidia wengi, kwa hiyo hao watu wasikukoseshe raha kabisa..."

"Hivi unafikiri hata nawajali? Ni basi tu yaani hizi siku chache kumekuwa na mambo mengi yenye kukwaza halafu na hawa mbwa hata hawanijui wanakaa kunisontea tu vidole," Namouih akasema
na kusonya.

Salome akacheka kidogo.

"Umeshasikia maneno wanayosema kunihusu?" Namouih akauliza.

"Ndiyo. Huwa nasikia wanakuongelea sana kwamba unaringa mno kwa sababu ya sura yako... una pesa lakini mchoyo sana, ndiyo maana eti Mungu amekufungla usiweze kuzaa," Salome akasema.

Namouih akacheka kidogo kwa mshangao.

"Na hasa ile juzi maneno yalikuwa mengi ulipopoteza kesi ya yule msichana aliyekufa... mara sijui
ulimwahidi kushinda ndiyo maana aliposhindwa akajikuta anabebwa na malaika wa kifo.... yaani dada, we' acha tu," Salome akasema.

"Ahah... ina... inahuzunisha na inakera sana. Lakini angalau inafariji kujua kwamba kuna watu kama
wewe wanaonielewa vizuri," Namouih akasema.

"Kabisa, tena wako wengi tu. Usifikiri vitu vinavyokuzunguka vinakuwa mbali nawe, unakuta viko hapo hapo ulipo. Cha muhimu ni kujua tu jinsi ya kuishi vizuri ndani ya duara la dunia yako mwenyewe hata kama wanaokuzunguka wanataka kuiporomosha, na unafanikiwa katika hilo kwa kuishi namna uishivyo siyo kwa kuridhisha mtu, ila kwa kuridhika wewe mwenyewe," Salome
akamwambia.

Namouih alipendezwa sana na maneno ya mwanamke huyu, naye akasema, "Asante Salome.
Nampa Mungu marks za asilimia mia kunikutanisha nawe leo."

Salome akacheka kidogo na kusema, "Asante."

"Wewe ni..."

"Ni daktari... nimebobea sanasana kwenye mambo ya ushauri na saha," Salome akamwambia.

"Ooh... sawa. Ndiyo maana una maneno mazuri."

Namouih akaendelea kukaa hapo na rafiki yake mpya wakiongelea mambo ya hapa na pale huku
sherehe ikiendelea taratibu, naye kiukweli alikuwa amejihisi vibaya moyoni baada ya kujua kwamba
watu walizungumzia suala lake la kutokuwa na watoto kwa njia mbaya sana. Hakuwahi kukazia fikira sana suala la kuwa na watoto, lakini kisa cha Salome cha kumpoteza mtoto wake aliyekuwa mlemavu kilimgusa sana kiasi kwamba akaanza kutamani kuijua furaha iliyopo ya kuwa mama. Akaendelea kutulia tu akimsubiri mume wake arejee kwa sababu tayari sehemu kubwa ya sherehe hiyo iliyomboa sana ilikuwa imekwisha.

★★

Upande wa Blandina. Mwanamke huyu alikuwa ametoka pamoja na mpenzi wake kwenda matembezi kama walivyokuwa wameahidiana kufanya baada ya Draxton kukutana na Namouih mapema ya leo, na wapendanao hawa walikuwa wametumia muda mrefu wakiwa pamoja. Walitembelea sehemu nyingi na kufurahia maongezi na vitumbuizo, ndipo mida ya saa nne
wwakaelekea kwenye kumbi moja ya starehe ili kupata chakula na vinywaji. Yaani Blandina aliagiza
chakula nje ya kumbi hiyo, kisha ndiyo wakaingia kule ndani na kuketi kwenye meza yenye viti virefu na kuletewa vinywaji. Blandina yeye akachukua vileo vinne na Draxton viwili tu, kwa sababu mwanaume huyu hakunywa sana vilevi.

Blandina alikuwa ameketi karibu sana na Draxton kwa kupitisha mkono wake ndani ya mkunjo wa
kiwiko cha mpenzi wake, mara kwa mara akimnong'oneza maneno mazuri sikioni, naye Draxton
angemwambia vitu vilivyomfanya mrembo acheke sana. Kulikuwa na watu wengi kiasi, wengine
wakicheza muziki na wengine wakitazama runinga za hapo, bila kukosekana walevi walioongea
kwa sauti kubwa sana. Blandina akawa anamwangalia Draxton na kuona jinsi ambavyo alitazama
watu kwa njia ya kutojali, na hilo likamfanya atambue kuwa mwanaume huyu hakupendelea sana
sehemu kama hizi. Kulikuwa na wanawake ambao walimtazama sana Draxton lakini yeye hakuwa
na muda nao kabisa, vile vile na Blandina aliyeangaliwa sana na wanaume kadhaa.

"Panakuboa hapa?" Blandina akamuuliza Draxton kwa kunong'oneza.

"Mm?"

"Pamekuboa? Tutafute sehemu nyingine?"

"La... haina haja. Si tumeshaingia?"

"Yeah, ila naona kama hujapapenda..."

"No, pamechangamka. Besides, umeshaagiza na chakula so...."

"Lile pale lidada linakuangalia sana natamani nilifate nikalikoe!" Blandina akasema.

Draxton akatabasamu na kunywa tu kinywaji chake.

"Ah... sss!" Blandina akatoa sauti hiyo kama ameumia na kuutoa mkono wake kwa Draxton.

"Vipi?" Draxton akauliza.

"Sijui... kuna mbu amening'ata," Blandina akasema huku akijiangalia mkononi.

"Pole..."

"Yaani midude mingine mpaka unajiuliza sijui kwa nini iliumbwa tu..."

"Ahah... unajua kuna mtu anaweza kusema umekufuru."

"Hata kama bwana, yanakera. Halafu midude yenyewe huwa inaishi kwa siku moja na nusu tu... yaani inasumbua, mikelele nyooo... afu' inakaa siku moja tu," Blandina akaongea na kusonya.

Draxton akacheka kidogo na kumwangalia sehemu hiyo iliyong'atwa.

Blandina akahisi bega lake likishikwa kutokea nyuma, naye akageuka upesi kumwangalia aliyemshika. Tabasamu la furaha likamtoka baada ya kumtambua haraka.

"Hee... Felix!" Blandina akasema.

"Vipi wewe panya buku, upo?" Felix akamwambia kiutani.

"Sura kama kiroboto wewe!" Blandina akamwambia kiutani pia.

Wawili hawa wakakumbatiana kwa furaha, Blandina akiwa bado amekaa, lakini kuna jambo likawa
limemkera Draxton haraka. Felix alikuwa ameshika sigara katikati ya vidole vyake, hivyo alipomkumbatia Blandina hakuushikisha mkono ulioishika sigara mgongoni kwa Blandina, kwa hiyo ukawa hewani, lakini kwa kuwa Draxton alikuwa karibu sana na Blandina hiyo ikafanya sigara hiyo iguse T-shirt aliyokuwa amevaa. Draxton akaitazama sigara hiyo na kumwangalia Felix, ambaye alikuwa anamtazama pia huku akitabasamu kwa furaha, na ikawa wazi kwa Draxton kwamba mwanaume huyo alifanya hivi makusudi kabisa. Kisha....

"Oh, samahani, so sorry bro..." Felix akasema hivyo na kumwachia Blandina.

Blandina alipomwangalia Draxton akakuta anajiangalia kwenye T-shirt yake, ambayo sasa ilikuwa imebakiza alama ya majivu kiasi kutokana na sigara kuigusa, lakini haikuwa imechoma kabisa.

"Aaa... Felix mambo gani? Unaniharibia moment bwana..." Blandina akamwambia.

"Pole kaka, excitement ya kukutana na huyu nikajisahau. Pole sana," Felix akamwambia Draxton.

Draxton akatikisa kichwa chake tu kuonyesha haikuwa na tatizo, naye Blandina akawa anampangusa kwenye T-shirt yake.

"Haujaachaga tu kuvuta hayo madude?" Blandina akamuuliza Felix.

"Nina muda. Ila sema leo niliona tu haitakuwa mbaya kupiga pafu moja hahahah..." Felix akasema.

"Uko poa babe?" Blandina akamuuliza Draxton.

"Yeah," Draxton akajibu.

"Huyu ni rafiki yangu, anaitwa Felix, tumesoma wote. Felix, huyu ni Draxton. DRA-X-TON," Blandina
akasema.

"Nimesoma bwana, we' naye vipi? Hahah... nashukuru kukufahamu kaka. Pole tena kwa hiyo ajali ndogo," Felix akamwambia Draxton.

"Haina shida. Ni vizuri kukufahamu pia," Draxton akamwambia kikawaida tu.

"Za siku?" Blandina akamuuliza Felix.

"Aah mambo mengi... unyama mwingi. Tokea kwa Mwantum mpaka now hatujaongea eti?" Felix akasema.

"Eee we' si uko bize sana... lazima unyama uwe mwingi," Blandina akasema, naye Felix akacheka.

Ni wakati huu ndiyo vyakula ambavyo Blandina alikuwa ameagiza vikaletwa, na vilikuwa vyakula
vizuri sana vyenye kutamanisha mdomo mpaka kuijaza mate.

"Dah, safi sana. Mambo ya makamuzi hayo..." Felix akasema.

"Karibu. Kaa basi," Blandina akasema.

"Oh, no, nilikuwa napiga mbili tatu tu hapo ndo' nataka kukimbia sasa hivi... nyie mji-excuse tu. Aa...
mnafanya kazi pamoja?" Felix akaongea hivyo.

Blandina akamlalia Draxton begani na kusema, "My only one love."

Felix akacheka kidogo na kusema, "Sawa kabisa. Mko vizuri pamoja. Hivi ndiyo Draxton huyu
aliyempiga chini Namouih kwenye kesi eeh?"

Draxton akamtazama kwa macho yake makini.

"Ndiyo huyu. Habari zinasambaa haraka kumbe... hahahah..." Blandina akasema hivyo na kucheka.

"Dah, hongera sana kaka. Yule alikuwa hakamatiki kwenye kesi ila ukamweka sehemu yake, vizuri
sana. We' ni mtu wa wapi?" Felix akauliza.

Draxton akaacha kumwangalia na kubaki kimya tu.

"We' si ungekaa bwana, umeanza na upelelezi wako sasa... kaa ndiyo tuongee vizuri Ili uju...."

"We' ni mpelelezi?" Draxton akamkatisha Blandina kwa kumuuliza Felix swali hilo.

"Ndiyo. Rank za juu mpelelezi. Kwa kuwa sisi ni marafiki na Blandina ingekuwa poa mimi nawe
tukijuana vizuri zaidi au siyo?" Felix akasema.

"Yeah," Draxton akajibu huku akimtazama kwa umakini.

Blandina alikuwa ameshaanza kula, naye akasema, "Vipi tukipanga kesho tukutane sehemu nzuri?
Ni Jumapili. Sisi wote na Namouih, na Donald, na Oprah? Kwanza mke wako huyo hajambo?"

"Ahahahah... yuko poa. Itakuwa jambo zuri, au siyo... Draxton?" Felix akaongea hivyo huku anamwangalia usoni kwa umakini.

Draxton akamtazama kwa ufupi, kisha akatikisa kichwa kukubali.

"Haya, tutaongea badae'... nyie wawili mw-enjoy... kaka tutaonana," Felix akawaaga na kuondoka.

Blandina alikuwa anatabasamu, naye akamwangalia Draxton na kusema, "Ni rafiki yetu sana huyo me na Namouih. Tunao wengi lakini, Felix yuko tight sana. Tumetoka mbali."

"Anaonekana yuko rafu," Draxton akamwambia.

Blandina akacheka kidogo, kisha akaanza kuongelea mambo mengi kuhusiana na maisha yake ya
zamani pamoja na hao rafiki zake, bila ya mwanamke huyu kutambua kwamba lengo la Felix kufika hapo lilikuwa kumchunguza mpenzi wake kwa kadiri fulani. Akaendelea tu kuzungumza kuhusu namna alivyotaka kuanza mazoezi ya viungo ili kuupa mwili wake umbo zuri zaidi kwa wakati huu kama jinsi Namouih alivyokuwa. Draxton akawa anamwambia kwamba umbo lake lilikuwa zuri na hakutakiwa kujilinganisha na mtu yeyote yule, lakini Blandina aliona bado alihitaji kuuchangamsha mwili wake ili asijikute anafikia manyama uzembe.
Ni kati ya mambo yaliyofanya Draxton amfurahie sana mwanamke huyu kwa kuwa Blandina
alikuwa mtu mwenye kujiachia sana akiwa pamoja naye. Wawili hawa wakaendelea kupata chakula na vinywaji taratibu huku wakifurahia maongezi.

★★

Upande wa wanandoa Efraim Donald na Namouih. Mambo ya chereko yaliendelea vyema ndani ya sendoff ya rafiki yake Efraim ambapo mwanaume huyo alikuwa ametoka kidogo baada ya kupigiwa simu kwa dharura fulani ya kikazi, na sasa ikiwa imeingia saa sita usiku ndiyo mwanaume huyo akawa amerejea. Alimkuta Namouih akiwa pamoja na Salome; wawili hawa wakiwa wamepatana sana hadi ikawa ni kama Namouih amemsahau kabisa mume wake ingawa alichelewa.
Efraim akafurahi kukuta Namouih yupo kwenye hali ya uchangamfu, naye akasema kama ikiwezekana waendelee kukaa ili wazungumze zaidi na kupata vinywaji. Lakini tayari maharusi walikuwa wameondoka, na Salome alisema alihitaji kufika nyumbani haraka pia. Efraim Donald
alikuwa ametoa kama ofa ya kumpa lifti Salome lakini mwanamke huyu alikuwa na gari pia, kwa hiyo wakaachana baada ya Namouih kumpa mwanamke huyo namba za simu ili waendelee
kuwasiliana.

Wanandoa hawa wakaelekea nyumbani huku Efraim akiomba radhi kwa kumwacha Namouih mwenyewe, lakini mke wake hakuona shida sana kwa kuwa alipata rafiki mpya aliyepatana naye vizuri sana kimawazo. Wakafika nyumbani hatimaye, na baada ya Suleiman kuingiza na kuegesha gari ndani, geti likafungwa na mlinzi, yule Alfani, ambaye alikuwa macho muda wote kulinda sehemu hiyo.
Namouih na Efraim Donald wakashuka huku mwanamke huyu akimwambia mume wake kwamba
ingependeza sana kama wangebadili geti la nyumba hii liwe la mfumo wa kuendeshwa kwa rimoti,
naye Efraim akasema angelifanyia kazi suala hilo. Walipofika ndani walimkuta Esma akiwa
amesimama karibu na mlango wa kuingilia kama anawasubiri, naye akawasalimu vyema na
kusema kweli alikuwa anangoja warejee. Namouih akamwambia hakupaswa kufanya hivyo hasa
kwa kuwa muda ulisonga sana, naye akamwambia aende tu kupumzika.

Ikiwa ni mida ya saa saba ya saa nane usiku sasa, wanandoa hawa wakaingia chumbani na kuanza
kuondoa mavazi yao mwilini ili wavae mepesi kwa ajili ya kupumzikia. Namouih alikuwa
anamwangalia sana mume wake aliyekuwa kimya tu mpaka alipomaliza kuvua nguo zake na
kubaki na boksa, naye akaanza kumfata na kumkumbatia kutokea nyuma; yaani Efraim akiwa amempa mgongo. Mwanamke akawa anavitembeza taratibu viganja vyake kwenye kifua cha mume wake huku kucha ndefu kiasi kwenye vidole vyake laini zikimtekenya kwa mbali, na akimbusu shingoni, naye Efraim akawa ametulia tu. Kisha Namouih akaushusha mkono wake
kufikia sehemu ya siri ya Efraim na kupagusa, na hapo akasisimka baada ya kuhisi namna
palivyovimba sana, kuonyesha kwamba alifanikiwa kumpandishia mume wake hamu ya kimahaba.

Lakini mara Efraim akaushika mkono wa Namouih na kuushikilia kwa pembeni, ikiwa kama ameutoa hapo kwa kusudi, naye akamgeukia na kumtazama machoni. Namouih sasa alikuwa amebaki na sidiria nyeupe na chupi laini nyeupe pia, mwili wake mzuri uliotamanisha sana ukiwa
wazi mbele ya mume wake, naye akawa anamtazama tu Efraim Donald kwa hamu na matumaini.

"Namouih..." Efraim akaita.

"Bee..." Namouih akaitika kwa sauti ya chini.

"Tungelala tu mpenzi... ni saa nane sasa hivi..."

"Me sina usingizi... we' una usingizi? Si tulilala wote mchana?"

"Yeah, but ni uchovu tu. Kulikuwa na mambo mengi huko nilikoenda kwa hiyo...."

Namouih akatikisa kichwa kuonyesha ameelewa, kisha akatoka mbele ya mume wake na kuelekea
kabatini. Efraim Donald akabaki kumtazama tu jinsi alivyoanza kuzitoa nguo za kulalia na kuzirusha
kitandani kwa njia iliyoonyesha hasira, naye Namouih akavaa nguo yake nyepesi ya kulalia na
kubana nywele zake nyuma ya kichwa, kisha akachukua mto na kuanza kuelekea mlangoni. Efraim
akakunja uso kimaswali na kumfata upesi, kisha akamzuia kutembea kwa kumshika mkono na kusimama mbele yake ili asiufikie mlango.

"Unaenda wapi?" Efraim Donald akauliza.

"Guest room," Namouih akajibu.

"Unaenda chumba cha wageni kufanya nini?"

"Kulala."

"Kwa nini?"

"Kwa sababu sihitajiki humu."

"Namouih em' acha basi. Sa'hivi ni usiku, hakuna muda wa kuanza maigizo...."

"Maigizo? Anayefanya maigizo ni mimi au wewe?"

"Unamaanisha nini?"

"La 'usadiq hadha!" Namouih akaongea kwa kiarabu akiwa amekerwa sana.

Efraim akabaki kumtazama tu.

"Yaani Efraim... umekuwaje sijui... hii ni ndoa au maigizo?"

"Namouih..."

"Nini?"

Efraim akabaki kimya.

"Naomba unipishe," Namouih akasema.

"Hauwezi kwenda kulala huko... kitanda chako hicho hapo..."

"Kitanda gani? Hilo ni pambo tu Efraim. Unanisifia sana, unanitendea vizuri, unaniambia mimi ni wa
muhimu hapa, lakini kwa lipi? Nimekaa kuwa kama mdoli tu hapa..."

"Namouih ni kwa nini unaongea hivyo? Kila kitu unacho Namouih. Unataka nifanye nini... unataka
nikupe nini zaidi ili kukuonyesha kwamba nakupenda?"

"Ah! Are you seriously asking that? Nachokitaka ni wewe Efraim!" Namouih akasema hivyo na
kumpiga kifuani na mto.

Efraim Donald akatazama chini.

"Kuna mambo mengi yametokea... na kwa muda fulani, ndiyo... nilihitaji wakati upite. Lakini inaonekana kama unafanya hivi kunikomoa. Yaani unanifanyia hivi ili sijui nikome au.... au labda
unaishi kwa masharti Efraim?"

Efraim akamwangalia na kusema, "Namouih ni maneno gani hayo unaongea?"

"Unataka nifikiri nini sasa? Efraim... unajua watu wanasema nini kutuhusu? Kwamba sisi tunaringa
sana na tunaishi kwa masharti ndiyo maana bado uko nami ingawa eti siwezi kuzaa. Hawana uhakika kuhusu hilo lakini kwa jinsi mambo yalivyo inaanza kuonekana kuwa kweli," Namouih akaongea kwa hisia.

"Toka lini umeanza kujali yale watu wanayosema?"

"Agh, this is not about them! Hii ni kuhusu sisi Efraim! Hatujawahi hata kukaa kuzungumza ikiwa tunataka kuwa na watoto. Ni kazi, visingizio, kazi, visingizio, mpaka lini? Au unataka nije nitoke huko nje nikutane na limtu litakalotimiza haja zangu?"

"Usije kuthubutu tena kuongea hivyo Namouih!" Efraim akasema kwa hisia kali.

"Kwa hiyo unataka nifanye nini ikiwa wewe kama mume wangu mwenye haki zote unashindwa
kunipa nachohitaji? Niendelee kuwa pambo lako tu humu ndani si ndiyo? Una nguvu nzuri, una mke
mzuri, unapendwa, una... unahitajika Efraim... kwa nini huoni hilo? Kwa nini... just... kwa nini?" Namouih akasema kwa hisia mpaka machozi yakaanza kumtoka.

Efraim akataka kumfuta machozi lakini Namouih akarudisha uso wake nyuma.

"Namouih nisikilize..."

"Ndiyo nakusikiliza..."

"Nakuahidi... nitarekebisha hili. Nipe muda kidogo tu..."

"Ohoh... crap..." Namouih akasema hivyo kuonyesha hamwamini.

Efraim Donald akawa anataka kumshika mabegani, lakini Namouih akamfata mdomoni na moja
kwa moja kuanza kumbusu kimahaba. Alikuwa akimpa huba kwa kasi na kushika sehemu yake ya
siri lakini Efraim akamshika kwa nguvu kiasi na kumzuia, jambo lililofanya Namouih abaki
kumwangalia tu huku akitikisa kichwa kwa kufadhaika.

"Namouih..."

Namouih akanyanyua kiganja chake juu kumzuia asiendelee kuongea, naye Efraim akabaki kimya.

"Huo muda kidogo ukiisha, ndiyo nitarudi kulala humu. Keep me posted," Namouih akamwambia.

Efraim Donald akabaki tu kimya na kuendelea kumtazama mke wake usoni. Namouih akajifuta machozi na kuuokota mto wake ili atoke, lakini simu yake ikaanza kutoa mlio wake wa kuita. Akawa amekumbuka hakuwa ameichukua, hivyo akaifata ili atoke pamoja nayo, na Efraim akabaki kumtazama tu. Alipoishika simu yake, Namouih akaona kwamba aliyekuwa akipiga ni Blandina, naye akajipa utulivu na kuipokea huku akianza tena kuondoka.

"Hallo Blandi..." Namouih akasema.

"Namouih...."

Mwanamke huyu akasimama baada ya kusikia sauti ya rafiki yake ikitaja jina lake kwa njia iliyomwambia kwamba Blandina alikuwa analia. Uso wa Namouih ukakunjamana kwa njia ya kuonyesha maswali, naye Efraim akamsogelea karibu.

"Blandina... nini tatizo? Mbona unalia?" Namouih akauliza.

"Hhh... Namoouih... kuna... tumefiwa Namooouih...."

"Nani? Nani ame...."

"Felix ameuawa Namouih!" Blandina akaongea hivyo.

Namouih alihisi mtetemo ukipita ghafla kwenye mkono wake uliosababisha aidondoshe simu yake
kutoka sikioni!


★★★★★★★★★★★★

ITAENDELEA

★★★★★★★★★★★★


Usikose sehemu za mwendelezo wa hadithi hii kali ya CHANGE. Ni story nzuri na ndefu sana. Waweza ipata nakala yote kwa gharama nafuu sana. Itakuwa ikiruka hapa siku za Jumatatu, Jumanne, na Jumatano. Karibu WhatsApp au kwa E-mail yangu.

WhatsApp no: +255 678 017 280

e-mail: eltontonny72@gmail.com
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom