Si kweli kwamba Watanzania ni wavivu wa kufikiri

MwanaHaki

R I P
Oct 17, 2006
2,401
705
Nimesoma mahali fulani kwamba kuna mwanasiasa fulani amedai kwamba Watanzania ni wavivu wa kufikiri. Hoja yake hii haina mashiko hata kidogo. Watanzania wengi ni watu wenye ujasiri mkubwa wa kufikiri na uthubutu wa kufanya mambo makubwa, lakini kutokana na kwamba Watanzania wanatawaliwa na chama chenye sera kandamizi, CCM, kisichotaka daima kuwaona Watanzania wanapevuka kiuchumi, Watanzania hawa wananyimwa, tena kwa makusudi kabisa, fursa za kupevuka na kuimarika kiuchumi: msingi wa maendeleo yao.

Serikali ya CCM ilileta mikakati ya MKUKUTA na MKURABITA ambayo imebainika kuwa kiinimacho dhahiri kutokana na kuwa na malengo yaliyojificha zaidi ya kuwa wazi. Kwa mfano, MKURABITA ililenga Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania, mojawapo ikiwa ni kutoa Leseni za Makazi ambazo zingewawezesha wananchi, hususan wale wanaoishi na kumiliki kwenye mazingira yasiyopimwa na kupewa HatiMiliki, lakini wananchi hao, kila walipojaribu kwenda benki na hati hizo waligonga mwamba kutokana na ukweli kwamba serikali haikurekebisha Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha, kuweza kuzitambua Leseni za Wakazi. Naufananisha MKURABITA kuwa sawa na ujanja wa panya anapotaka kumnyofoa mnyama anayefugwa au hata mwanadamu usiku, ambapo kabla ya kumng'ata kwa meno yake anapuliza hewa baridi mahali alipolenga kisha anaanza kupatafuna. Huu unaitwa mtindo wa kupuliza na kuuma. Leseni za Makazi zikatolewa, kwa kulipiwa kwa kuwa ni leseni, wananchi wakiaminishwa sana kwamba wanaweza kupata mikopo ya masharti nafuu benki. Kumbe Leseni za Makazi ni sawa na, ashakum si matusi, karatasi za kuchambia msalani!

Kiinimacho kingine ni sera mfu ya kilimo iliyoleta majinamizi ya Vocha za Pembejeo, Vyama vya Ushirika na Stakabadhi Ghalani. Majinamizi yote haya yamekuwa na malengo ya kuwashawishi wakulima kuwa wazalishaji wakubwa wa mazao mbali mbali, lakini wasio na umiliki kamili wa masoko ya mazao yao ikiwemo pamoja na kupanga bei za mazao yao kwa mujibu wa, kwanza, kufidia gharama za uzalishaji na kupata faida ya jasho lao, na pili, kwa kuzingatia suala la bei za masoko mbali mbali ya bidhaa za mazao ya chakula na biashara, ya ndani na nje ya nchi. Ni nadra sana kusikia kwamba kundi fulani la zao la chakula na/au biashara limefanikiwa kupata soko kubwa la ndani na/au nje ya nchi, lakini ipo mifano michache ambayo kwa makala haya sitaizungumzia kwa kuwa si mahala pake. Kutokana na wakulima hawa kushurutishwa kujiunga na vyama vya ushirika vinavyoratibiwa na Idara za Kilimo za Halmashauri za Wilaya, ambapo uongozi wake umekuwa wa kupangwa na watendaji wa serikali kwa maslahi yao binafsi, vyama hivi vimekuwa vya kinyonyaji zaidi kuliko kuwanufaisha wakulima. Uongozi wake umekuwa ukiwapangia wakulima bei za kuuza mazao yao, haswa kwa mazao ya biashara kama vile korosho, pamba, chai, kakao, n.k. na pale ambapo mazao ni ya chakula kama vile ufuta, watendaji wa vyama hivyo hushirikiana na watendaji wa halmashauri kuwapangia bei wakulima pindi wanapopata wateja wao wenyewe na kupatana bei. Inasikitisha kuona kwamba watendaji hawa dhalimu, si tu kwamba wanainyima serikali kuu mapato yake kwa kuwashushia bei ya mazao yao wakulima hawa na hivyo, kwa upande wa serikali, kuufanya ushuru unaokusanywa kuwa mdogo, na kwa upande wa wakulima kuwafanya kupata faida ndogo inayowazuia kusonga mbele kimaisha. Huku ni kuwakatisha tamaa wakulima na kuhatarisha usalama wa chakula, kwani hakuna kinachowazuia wakulima kuweka zana zao chini na kutafuta shughuli mbadala za kufanya. Wakulima, kimsingi, wamekuwa wakidhulumiwa na si tu na watendaji wa vyama vya ushirika na halmashauri za wilaya, lakini bali pia na serikali yenyewe kupitia mpango wa Stakabadhi Ghalani, ambao sasa unatishia kuwafanya wakulima wa nafaka kama vile mahindi na mpunga, nao pia kuweka zana zao chini na kutafuta shughuli mbadala. Tumesikia yaliyotokea Lindi na Mtwara kuhusu Stakabadhi Ghalani kwa upande wa zao la korosho. Huenda tumefichwa makusudi kuelezwa yanayojiri Morogoro na Mbeya kuhusu mahindi na mpunga ili tusihamanike na kufadhaika. Wahenga walisema: Lisemwalo lipo kama halipo laja!

Sera nyingine kandamizi na kiinimacho ni elimu, ambayo kadri siku zinavyokwenda inazidi kujidhihirisha kwamba serikali haina nia wala mpango wa kuwanufaisha Watanzania, baya zaidi, madhumuni halisi ni kuwa na taifa la wajinga wasio na uwezo wa kupambanua kwa kina masuala yanayohusu mustakabali wao, haswa kwa upande wa vijana. Kuna mtu aliandika mahali, kana kwamba ni mtabiri, kwamba: Itafika wakati nafasi zote za ajira nzuri na fursa nzuri za kunufaika kiuchumi zitakuwa zimeshikiliwa na watoto wa vigogo serikalini, wa wafanyabiashara wakubwa na wageni. Watakaobakia, watoto wa wakulima halisi tulionyimwa elimu kutokana na wazazi wetu kutokuwa na fedha za karo, tutageuzwa manamba wa kufanya kazi mbovu na hatarishi, kwenye mashamba ya wageni wanaokuja kuwekeza, migodi ya madini, na wale watakaokuwa na bahati ya kujipenyeza mijini wataishia kuwa vibarua wa kulipwa ujira wa kutwa au wa wiki, kwenye supermarket za wazungu na viwanda vya wahindi.

Nasikitika kuwaambia kwamba utabiri huu tayari umeshatimia. Hauhitaji mjadala. Yote yaliyosemwa yamekuwa ya kweli.

Ndugu Watanzania, msidhani kwamba serikali yenu ya chama tawala imeanza majuzi kuchakachua elimu. La hasha. Ilianza zamani.

Miaka ya 70 serikali ilianzisha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ambayo ipo mpaka leo. Lengo lilikuwa kuwapumbaza kiakili wazee, haswa wazee, vijijini ili hatimaye waichukie elimu na wasione umuhimu wake. Ikaanzisha kile kilichoitwa Elimu ya Kufuta Ujinga maarufu kwa jina la ngumbaru. Chini ya miti, bila ya kujua kwamba wanatumika kwenye mchezo mchafu, walimu walipewa Stahili za Mazingira Magumu, na kupelekwa kwenye vijiji, ambapo chini ya miti hiyo, wazee, wake kwa waume, na wale wote ambao hawakuwa na elimu ya kusoma na kuandika, walifundishwa.

Enzi hizo kukiwa na vijiji vya Ujamaa, ufisadi ukiwa unazaliwa rasmi, watu walichangamkia kweli kweli fursa hizi za kuufuta ujinga wao. Wakaiona serikali yao kuwa inawajali mno kwa kuwaletea walimu, wengi wao wakiwa mabinti warembo kweli kweli. Watendaji serikalini waliwachagua walimu wasichana warembo ambao walijua kwamba wangekuwa na mvuto mkubwa kwa wazee hao, lengo likiwa kupata washiriki wengi ipasavyo. Siasa mchezo mchafu.

Walimu waliagizwa kuwatahini wanafunzi hao na wale walioonekana kuwa na uwezo mkubwa waliteuliwa kuwa walimu wasaidizi ambao walipewa majukumu ya kuwafundisha wenzao, jambo ambalo liliwajengea heshima kubwa mbele ya wenzao na ambalo walilifanya kwa ufahari mkubwa. Badala ya kuitwa Walimu Wasaidizi kama ilivyowastahili, wakaitwa Walimu.

Mojawapo ya vishawishi walivyopewa ili kuifanya kazi hiyo ni ahadi za kulipwa masurufu ya kutosha kujikimu kila mwezi, jambo lililowafanya kuipenda mno kazi yao hiyo. Hawakujua kwamba serikali haikuwa na nia thabiti ya kuendeleza mpango huo mchafu. Mosi, serikali haikuwa na nia ya kuendesha mpango wa Elimu ya Ndumbaru kwa zaidi ya miaka 3, na pili, haikuwa na nia ya kujenga maktaba katika vijiji vyote vilivyofikiwa na mpango huo. Ni takriban asilimia 10 tu ya vijiji ndivyo vilivyofanikiwa kujengewa maktaba hizo, huku kukiwa na shamrashamra, hoihoi, nderemo na vifijo ikiwa ni sherehe zilizohudhuriwa na viongozi wa chama na serikali, wote wanaume, wale wa chama wakiwa wamevalia mashati ya mikono mirefu au mifupi ya rangi za kijani, skafu na kofia za njano, huku wale wa serikali wakiwa wamevaa Suti za Kaunda au "Chou En Lai" za rangi nyeusi, kijivu au nyeupe. Hakika walipendeza kwani picha zilipigwa na kusambazwa vijijini humo kama kumbukumbu na wale ambao hawakuwa na uwezo wa kufika ili kushuhudia uzinduzi wa maktaba hizo walipata nafasi ya kushiriki kupitia matangazo ya moja kwa moja ya Redio Tanzania Dar es Salaam Idhaa ya Taifa, wakati huo akina Danstan Tido Mhando, Sekione Kitojo, Jacob Tesha na wengineo wakitangaza kwa mbwembwe zote ili kuifikisha patashika hiyo ya nguo kuchanika kwa wasikilizaji. Wanavijiji wa jirani baada ya kusikiliza redio zao walishawishika kuchukua baiskeli zao na kukimbilia sherehe hizo huku wale wasiojua kutumia baiskeli wakilazimika kuazima au kukodi baiskeli ili kufika, potelea mbali kuanguka na kuumia, majeraha yanatibika.

Enzi hizo serikali na chama kweli vilipendwa.

Lakini masurufu yalipokoma ghafla na kuwafanya "Walimu" Wasaidizi kufuatilia hadi kuchoka na kukata tamaa, wanafunzi wao waliokuwa na ari ya kuendelea kujifunza nao walikosa pa kujifunza, hatimaye kila mtu akaanza kuichukia elimu. Walimu wale, kwa kupewa pesa zile nyingi kwa wakati ule, waliweka chini zana zao za kilimo na kujenga nyumba bora za kisasa, na kuweka wake ndani ya nyumba. Hata mke wa Mwalimu aliheshimiwa na kuitwa Mama Mwalimu, hata kama alikuwa na watoto, ambapo angeitwa Mama Peter, Mama Hadija au Mama Wawili kwa mwanamke aliyezaa mapacha.

Ngumbaru ilipokoma ghafla walimu hao walilazimika kuyakumbuka majembe yao na wale waliokuwa wameweka akiba kidogo walinunua ng'ombe wa maksai na majembe yao.

Itaendelea.
 
Ndugu yangu Manyerere Jackton ukishamaliza ile kazi tuliyotumana, hebu njoo uanzie na makala haya hapa. Copy and paste kaka.

Ukishamaliza niambie nitakuonesha Part 1 na Part 2.
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom