Sheria ya mifuko ya jamii moto

OSOKONI

JF-Expert Member
Oct 20, 2011
10,965
5,336
VUGUVUGU la kupinga mabadiliko ya sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2012 limechukua sura mpya baada ya wabunge kutaka kuifanyia marekebisho mengine.
Wabunge hao wameitaka serikali kuipeleka tena bungeni sheria hiyo ili ikidhi mahitaji ya wafanyakazi ambao wameyakataa marekebisho yaliyofanywa Aprili mwaka huu.
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ilitoa taarifa juu ya marekebisho hayo kwamba mwanachama hataruhusiwa kuchukua mafao yake kwa sababu yoyote mpaka hapo atakapofikisha miaka 55 au 60.

Bungeni

Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo (CCM), mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, aliomba mwongozo wa Spika akitumia kanuni ya 47 (1) mpaka (3) akitaka Bunge lisitishe shughuli za kujadili hoja za serikali na badala yake lijadiliwe jambo la dharura.
“Mheshimiwa mwenyekiti nimesoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kuhusu sakata la wafanyakazi linaloendelea huko nje wakilalamikia sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii inayowanyima fursa ya kulipwa mafao yao hadi wafikishe miaka 55.

Jambo hili limekuwa tete huko nje, wafanyakazi wameanza kuacha kazi sasa naomba Bunge lijadili na kutafuta muafaka…mheshimiwa mwenyekiti naomba kutoa hoja,” alisema Jafo na kuungwa mkono na wabunge wengi.
Akitoa mwongozo wa jambo hilo, Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, alikubali hoja hiyo kwa madai kuwa inagusa maslahi ya watu wengi lakini akamuomba mbunge akakusanye taarifa zaidi kujua ni kitu gani kinalalamikiwa ili wabunge waweze kujadili kwa kina.
Mara baada ya kutoa mwongozo huo, mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, na Tundu Lissu wa Singida Mashariki (CHADEMA), walimshauri mwenyekiti kulipeleka jambo hilo kwenye Kamati ya Uongozi likachanganuliwe kwa kina.

Hata hivyo, mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM), aliwapinga wenzake kwa kudai kuwa hawapaswi kuungana na wafanyakazi kulalamikia sheria hiyo kwa sababu wao (wabunge) ndiyo walioyapitisha.
“Hapa wa kulaumiwa ni sisi wabunge kwa vile hatukuwa makini katika kupitisha hii sheria, hivyo leo tusijigeuze na kuanza kulalamikia sheria tuliyoitunga wenyewe,” alisema.

Hata hivyo Lugora, alipingwa na Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, ambaye alisema sheria wanazozitunga si msahafu kwani zinaweza kubadilika kulingana na matakwa ya wananchi.

SSRA yafafanua

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji cha SSRA, imefafanua kuwa sheria hiyo imeshaanza kutumika na maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi muongozo mwingine utakapotolewa.

Ilibainisha kuwa lengo la kusitisha maombi ya kujitoa uanachama ni mamlaka na mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa elimu kwa wadau ambao ndio wanachama wa sekta hiyo.

Taarifa hiyo ilisema wamesitisha fao la kujitoa si kwa sababu ya serikali au mifuko ya hifadhi kufilisika kama baadhi ya watu wanavyodai bali inalenga kuboresha maslahi ya wanachama.

“Tunapenda kuwahakikishia wanachama kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii ni thabiti na michango yote ya wanachama iko salama.
“Tunawaomba wanachama na wadau wote wa sekta ya Hifadhi ya Jamii kuwa na utulivu mchakato huu ukiwa unaendelea kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya wanachama,” ilisema.
 
Back
Top Bottom