Shairi: Nyuki Mfia Ua

Amani Dimile

JF-Expert Member
Jul 27, 2022
243
395
Mtunzi: Amani Dimile

Sina jipya la kusema, yote nimeshamaliza
Maisha yaenda vyema, Mungu ametujaliza
Pendo lafanya nahema, nafurahi napendeza
Mimi pombe ye mgema, wallah! ameniweza

Ametiririsha huba, huba lake maridhawa
Kabobea kwenye tiba, mgonjwa napewa dawa
Pishi lake ninashiba, na mengi naongezewa
Kaniganda kama ruba, mwenzenu nimezidiwa

Amekosha nafsi yangu, na kufuriza hisia
Yeye ndie fungu langu, Mwenyezi kanijalia
Zileteni hizo pingu, kifuatacho ni ndoa
Ua alopenda Mungu, hukua bila mvua

Acheni nifarijike, kupendwa raha jamani
Nafsi yangu iridhike, daima iwe mwangani
Hi safari nisishuke, hadi mwisho kituoni
Na tukifa tujizike, tuwe wote kaburini

Mi nyuki mfia ua, pendo langu maridadi
Sina mashaka najua, zitatimia ahadi
Nafsi nimeshaitoa, hisia zataradadi
Nampenda anajua, hata mbingu ni shahidi

Nalinda hisia zake, sababu kaniamini
Najali uwepo wake, sababu kanithamini
Yeye wangu mie wake, nadumisha tumaini
Siri zangu zote zake, aniue Samsoni

Nitabeba dhambi zake, ye abaki na thwawabu
Shida zake nijivike, kamwe asipate tabu
Hata msalaba wake, acheni nijisulubu
Sitaki ye ateseke, afurahi aghalabu

Nitampa jina langu, aitwapo niitike
NItampa mema yangu, mabaya yake nishike
Nitampa pendo langu, kamwe asisusurike
Nitamtunza wa kwangu, akipita asifike

Kutwa nitamtungia, mashairi ya mapenzi
Na nitamhadithia, hadithi za toka enzi
Nyimbo nitamuimbia, kumfariji mpenzi
Kwake nimeweka nia, ye ni wangu mkufunzi

E Mungu tupe sayari, tukaishi si wawili
Duniani kuna shari, hakufai tanawali
Tujalie kila kheri, maisha tuyakabili
Nampenda Lasabari, ndo mana ninamjali



InShot_20230825_103712745.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom