EMT
Platinum Member
- Jan 13, 2010
- 14,483
- 15,308
Waziri wa Afra na Ustawi Dkt Haji Mponda (aliye juu ya pikipiki) akizundua jana jijini Dar es salaam Pikipiki maalum iliyotengezwa na Kampuni ya E Ranger ya Afrika Kusini kwa ajili ya shughuli za kubebea wagonjwa ili kudhibiti vifo vya mama na watoto. Pikipiki hizo kila moja imegharimu Dola za Kimarekani 5,900.
Mmoja wa madereva walipata mafunzo ya matumizi ya pikipiki maalum za kubebea wagonjwa akionyesha jana jijini Dar es salaam jinsi ya kumsafirisha mgonjwa kwa kutumia usafiri huo huku akiwa na muuguzi nyuma.
Serikali imeagiza pikipiki maalumu 400 kwa ajili ya kubebea wagonjwa katika hospitali za rufaa, zahanati na vituo vya afya. Waziri wa afya na Ustawi wa Jamii Dokta Hadji Mponda amesema katika awamu ya kwanza Serikali imenunua pikipiki 30 zenye thamani ya dola za kimarekani 177,000 ambapo Mkoa wa Pwani utapatiwa pikipiki 7, Morogoro 7, Rukwa 6, Mbeya 5 na Dodoma 5.
Waziri Hadji amesema lengo la kununua pikipiki hizo ni kutekeleza mpango mkakati wa kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi na watoto. "Serikali imejizatiti kufikia malengo ya Milenia ambayo yanalenga katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili na vifo vya kinamama vinavyotokana na uzazi kwa robo tatu ifikapo mwaka 2015"alisema na kufafanua kuwa, tafiti za mwaka 2009/10 zimeonyesha kuwa vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi ni akinamama 454 kwa kila vizazi hai laki moja kutoka vifo 578 kwa kila vizazi laki moja mwaka 2004/5.
Alizitaja sababu zinazochangia kwa vifo vya kina mama wajawazito ni pamoja na kutokwa kwa damu nyingi kabla na baada kujifungua, uzazi pingamizi, uambukizo na shinikizo la damu linalosababishwa na ujauzito na matatizo ya kuharibika kwa mimba. Sababu nyingine ni pamoja na ugonjwa wa Malaria, Ukosefu wa damu na maambukizo ya virusi vya UKIMWI, kuchelewa kufanya maamuzi katika ngazi ya familia ikiwa ni pamoja na kuchelewa katika kituo cha kutolea huduma.
Waziri Mponda alisema Serikali imeona kuwa ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kiwango kikubwa imeboresha muundo maalumu wa pikipiki ambao utawezesha kuboresha huduma katika maeneo mengi kwa mara moja.
Alisema kuwa pikipiki hizo zimeonyesha mafanikio makubwa katika nchi za Kenya, Malawi, Afrika Kusini, Sudan Kusini, Ethiopia na Guinea. Bibi Zuhura Ahmed Mkazi wa Dar es Salaam ameipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kusema kuwa itawasaidia kina mama wengi na hasa wa vijijini wanaokufa kwa kukosa usafiri wa uhakika. Aidha Serikali inatarajiwa kupokea pikipiki zingine 370 ifikapo mwezi nne mwaka huu kutoka kampuni ya eranger iliyopo nchini Afrika ya Kusini.
from: Srikali yaagiza pikipiki maalumu 400 za wagonjwa -