Serikali kuanza kutoa tuzo kwa waandishi mahiri wa riwaya nchini kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/23

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Serikali imeunda kamati maalum inayoongonzwa na Prof. Penina Mlama kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kutambua na utoaji tuzo kwa waandishi mahiri wa riwaya nchini kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/23.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) wakati wa tamasha la Elite Mjue Mtunzi lililofanyika mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam ambapo amesema lengo la kuwa na tuzo hizo ni kuhamasisha uandishi na usomaji wa vitabu miongoni jamii.

Kiongozi huyo, amesema tayari wizara yake katika bajeti ya Mwaka wa fedha 2022/23 imetenga fedha kwa ajili ya utoaji wa tuzo hizo kama zawadi kwa mshindi. Amesema fedha zitatumika kwa ajili ya uchapishaji na usambazaji.

"Katika bajeti yetu ya Mwaka 2022/23 tumeshatenga Shilingi Bilioni Moja ambazo watapatiwa washindi kwa ajili ya kuchapisha na kusambaza riwaya watakazokuwa wameandika na zikashinda," amesema Prof Mkenda

Ameongeza kuwa Serikali imeamua kusaidia waandishi katika hatua hii ili kuwawezesha kufanya tafiti nzuri kabla kuanza kuandika riwaya ambazo zimekuwa zikitunza historia ya nchi pamoja na kukuza uzalendo nchini.

Aidha, Prof Mkenda ameupongeza Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (WARIDI) kwa kuanzisha Tamasha hilo na kwamba Serikali itaunga mkono kwa kufadhili matamasha hayo ili kuongeza hamasa kwa washiriki wengi zaidi, huku akiwataka wadau vikiwemo Vyuo Vikuu vya umma na binafsi kuona umuhimu wa kushiriki na kufadhili tamasha hilo.

Mdhamini wa Tamasha hilo utoka Elite book store, Hemes Damian amesema Kampuni yake itaendelea kufadhili tamasha hilo kwa kuwa kupitia usomaji wa vitabu watu wanapata historia ya nchi kwani maandishi yanabaki kwa vizazi na vizazi.

Damian ameongeza kuwa kutokuwa na vitabu na simulizi kuhusu matukio mbalimbali ya nchi itasababisha vizazi vijavyo kutokuwa na historia kitu kitakachopelekea kukosa uzalendo.

Katika hatua nyingine Damian ameeleza kuwa mwaka 2020 walianzisha daftari la kudumu la wasoma riwaya kwa lengo la kuwa na takwimu za wasoma vitabu pamoja na kuanzisha maktaba mtandao.

Kwa upande wake Rais wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (WARIDI) Hussein Tuwa amemwambia Waziri kuwa lengo Umoja huo ni kuhakikisha wanapeleka mbele fasihi kwa kuzingatia maadili, nidhamu, uzalendo na lugha ya Staha.

Akizungumzia kuhusu Tamasha hilo la Elite Mjue Mtunzi linalenga kuendeleza utamaduni wa kusoma na kuandika vitabu miongoni mwa wanachi na wadau na kuondoa dhana ya kuwa watanzania hawapendi kusoma vitabu.

Katika Tamasha hilo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amezindua vitabu vya Riwaya vilivyoandikwa na waandishi wapatao watano pamoja na kutoa ngao kwa msomaji bora wa riwaya.

IMG-20220704-WA0005.jpg
IMG-20220704-WA0006.jpg
IMG-20220704-WA0007.jpg
 
Back
Top Bottom