Serikali imeanza vita itakayoshindwa kabla jogoo hajawika

Tukwazane Taratibu

Senior Member
Dec 20, 2012
195
537
SERIKALI IMEANZA VITA ITAKAYOSHINDWA KABLA JOGOO HAJAWIKA, KULAZIMISHA WAMILIKI WA BLOGU, MAJUKWAA YA MITANDAONI, REDIO NA TV ZA MITANDAONI KUJISAJILI “TCRA”NI KWENDA VITANI BILA KUJUA UWEZO WA ADUI WAKO.


Na Josephat K. Nyambeya

Kanuni ya 4 ya maudhui ya mitandaoni ya mwaka 2018 (The electronic postal communications (online content) regulations, 2018) unawataka wamiliki wote wa Blogu, majukwaa ya mitandaoni, televisioni na redio za mitandaoni kusajili vyombo vyao hivyo “TCRA”. Tangazo hilo limekuja juzi jumamosi baada ya siku kadhaa za uvumi uliokuwa ukidai kwamba jambo kama hilo linakuja.

Kwa siku za karibuni nchini kwetu kumeibuka ugonjwa wa kuichukia sana mitandao ya kijamii. Ugonjwa huu umelikumba sana tabaka tawala na hata baadhi ya watawala, nawaita watawala kwa sababu hawana sifa za kuitwa viongozi wamekuwa wakisikika mara kwa mara wakionyesha hasira zao juu ya mitandao ya kijamii.

Ikafikia hadi wengine wakasikika wakisema wanatamani malaika washuke waizime mitandao hiyo kwa maana eti inachelewesha maendeleo, very fun. Mitandao ya kijamii ni mjumuiko wa Blogu, Tovuti, Majukwaa ya mitandaoni n.k

Baadhi ya majukwaa ya mitandaoni (Jamii Forums) yenye watembeleaji (visitors) wengi sana nchini yamekumbwa na kesi mahakamani kwa madai ya kwamba eti waligoma kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pale jeshi hilo lilipotaka kupatiwa taarifa za siri za baadhi ya watumiaji wa jukwaa hilo, kitu ambacho mimi naamini ni kwenda kinyume na taratibu za faragha (privacy) za mtumiaji mitandao.

JamiiForums walilazimishwa kutoa taarifa hizo kwa kutumia sheria ya makosa ya mitandao (cyber crime act, 2015) ya mwaka 2015. Kosa lingine waliloshitakiwa nalo ni kushindwa kwao kusajili jukwaa lao kwa kutumia rajisi ya Tanzania kwa kingereza tunaiita .co.tz domain, kosa ambalo halina nguvu kisheria na kiutalamu. Kesi bado iko mahakamani.

Zimetungwa sheria mbalimbali zenye lengo la kuwadhibiti watumiaji wa mitandao na mitandao yenyewe lakini zimeshindwa kufikia lengo.

Kanuni hii ya maudhui iliyoletwa kwetu na wizara ya michezo chini ya mwanasheria msomi Harrison Mwakyembe (PhD) inazidi kuonyesha nia ya watawala dhidi ya mitandao hii ya kijamii.

JE KANUNI HII INASEMAJE?
Kanuni hii ya maudhui ya mitandaoni ina vipengele kadhaa lakini kipengele kikubwa ni kile cha kuwataka wasimamizi (moderators, admins, owners) kusajili blogu, majukwaa yao TCRA. Kanuni inawataka wamiliki wote walipe shs 100,000 kama gharama ya kuomba usajili TCRA, hii naweza kuiita “application fee” ambayo hairudishwi na baada ya maombi yao kupitiwa watarudishiwa majibu.

Kama maombi yako yamekubaliwa kwa wale wenye Blogu watatatikiwa kulipa kiasi cha shs Mil 1 kama gharama ya usajili na kiasi hicho kitatakiwa kulipwa kila mwaka kwa TCRA. Na kwa wale wenye TV na Radio za mitandaoni (hizi ni zile TV za Youtube kama Ayo TV, Ngassa TV, Muungwana TV n.k) watahitajika kulipa kiasi cha shs laki 2 kama gharama ya usajili na pesa hiyo hiyo itatakiwa kulipwa kila mwaka.

Ukiipitia fomu ya maombi iiyotolewa na TCRA utakuta vipengele kadhaa ikiwemo kuwataka wamiliki wa mtandao husika kuweka wazi asilimia zao za hisa kwenye blogu, au jukwaa husika, kuonyesha namba yao ya TIN ya TRA n.k

Naomba nizungumze kiufupi ni kwa jinsi gani sijaridhika na kanuni hii.

1. BLOGU
Kwanza kabisa Blogu ni moja kati ya majukwaa maarufu yanayotumika kwa ajili ya kuwapa watumiaji uwezo wa kufikisha habari kupitia mitandao. Hapa Tanzania, blog nyingi sana zimepata umaarufu kupitia blogpost. Kuna blog kama Issa Michuzi, Mjengwa blog na nyinginezo zimekuwa chachu sana kwa wana habari na kuwafanya nao kuanzisha blog zao.

Blogu ina faida nyingi, ikiwemo urahisi wa utumiaji, kutokuwa na gharama ya uendeshaji kwa matumizi ya kawaida, hakuna gharama ya hosting na vinginevyo vingi. Mara zote blog huwa ni maalum kwa ajili ya kuzungumzia na kujadili maada husika (Ufundi, habari, Mapishi, Kilimo, Teknolojia n.k).

Kwa dunia ya sasa Blogu imekuwa ikitumika kama chanzo cha kipato kwa wamiliki kupitia makampuni ya matangazo na matangazo ya watu binafsi pia. Hii imeongeza chachu ya kuongezeka kwa wamiliki na waanzishaji wa blogu duniani kote.

Kwa sasa wahitimu wengi wa vyuo ndio wamiliki wa Blogs ili kuweza kushindana na soko la ajira, kwa sababu kupata ajira limekuwa jambo gumu wengi wa vijana wameamua kujiingiza kwenye biashara ya utoaji wa habari kwa njia za blogu ili kuweza kupunguza makali ya njaa ya kukosa ajira.

Kupitia matangazo mmiliki wa blogu anaweza kuingiza kiasi cha fedha kuanzia Dola 100 za Kimarekani hadi kiasi chochote kwa kadri ya jitihada zake kwa mwezi. Wapo wanaoingiza dola 100, 200, 800 na hata zaidi ila kwa uzoefu wangu kwenye idara hiyo kwa sasa biashara hiyo imedorora sana ukilinganisha na zama za nyuma kwa sababu mbalimbali za kibiashara kutoka kwenye makampuni makubwa ya matangazo ya Google, Propeller Ads n.k

Kwa sasa vijana hawapati sana kipato kutokana na kazi hiyo, kumtaka mmiliki wa blogu alipe kiasi cha shs laki moja kwa ajili ya kuomba usajili TCRA ni jambo la ajabu sana na lililokosa ushauri wa kitaaluma na kitaalamu. Kwa sababu blogu nyingi hazijulikani wamiliki wake achilia mbali hizi zinazojitambulisha kwa majina ya wamiliki akina Michuzi blog, Mjengwa blog, Le Mutuz, Millard Ayo na wengine wanaojitambulisha kwa majina yao halisi . Kutojulikana kwa wamiliki wa blogu nyingi kunalifanya zoezi hili lisifanikiwe kwa asilimia kubwa.

Blogu nyingi zina rajisi ya .blogspot.com mfano “kulakwene.blogspot.com” usajili wake wa rajisi unatolewa bure na kampuni ya Google yenye makao makuu yake California, Marekani. Google wanatoa free registration of blogspot ili mradi tu uwe na email ya Gmail iweje leo kitu kinachotolewa bure na kampuni ya Google ambayo TCRA hawana hata chembe ya uwezo wa kuifikia wala kuomba taarifa za watumiaji wake eti wakadai wao wasajili.

Kama ni kulipa gharama ya usajili Google ndio wenye haki ya kudai malipo hayo na si TCRA , blogger ni huduma ya bure inayotolewa bure kwa kila mmiliki wa akaunti ya Gmail ya Google, basi TCRA waanze kutoza gharama kwa kila huduma inayotolewa na Google kwa watumiaji wake ikiwemo Google drive na nyingine wasiishie tu kwenye huduma ya Blogger. Wanasikitisha hawajui wakitendacho

Usajili wa blogu unatosha tu kuidhinishwa na Google na ni bure iweje TCRA watudai sisi fedha huku hawahusiki hata kidogo na kutu control? Tumekuwa chanzo cha mapato ya serikali? Je wamiliki wa Blogu wakipata matatizo kwenye hizo blogu zao wanaweza tatuliwa maatizo yao na TCRA? Jibu ni HAPANA kwa sababu TCRA hawana uwezo huo, uwezo huo ni mkubwa sana kwao.

Ukipata shida inamalizwa na Google wenyewe. TCRA wangefurahi na wangekuwa na uwezo na uthubutu wa kusema kama blogu zingekuwa na domain registration ya Tanzania kwa maana ya .co.tz mfano kulakwene.co.tz… Ila kwa sasa watulie tu wasituchanganye, hii ngoma ni nzito.

Pia zoezi hili la usajili wa Blogu litakuwa gumu kwa sababu hata usipoisajili TCRA bado utakuwa na uwezo wa kuitumia blog yako kama kawaida bila shida na bila kutambulika eneo unakotolea taarifa zako.

Kingine kinachokatisha tamaa kwenye usajili huu wa blogu ni ile shillingi Millioni moja ambayo mmiliki utatakiwa kulipa kila mwaka kwa TCRA , nadhani kama ni kosa basi hapa ndipo lilipo kosa kubwa . Mil moja? Hivi mnajua wamiliki wa blogu wanapata shillingi ngapi kwa mwezi hadi muwapangie kiasi hicho kikubwa cha fedha?

Na wakishalipa hizo fedha zinaenda wapi? Zinaenda kufanya nini? Kuna watu wanapata Dollar 100, 200 kwa mwezi ili mradi tu kufuta futa njaa za mtaani , haingii akilini unampangia atoe Mil 1. Wizara ya vijana na michezo haijakaa na wamiliki wa blogu ili kuweza kukubaliana na hoja zao hizi walizozileta kwenye kanuni hii mpya ya maudhi ya mitandoni, iweje wao wakae maofisini wapange kiasi hicho kikubwa cha fedha?

Mimi nihangaike kukesha kusoma vitabu, majarida na mitandao mbalimbali kuhusu kitu fulani cha teknolojia ili nije nikiandike kwenye blogu yangu, au mathalami blogu yangu ni ya kufundisha wanafunzi wa sekondari, nikishakiandika unataka tena nikulipe kwa andiko hilo, this is not fair hata kidogo. Blogging is no that easy.

Ukiangalia kati ya walengwa wote hawa wa Blogu ndio wamepewa kiasi kikubwa cha fedha sijajua ni kwa nini. Wanaweza sema wanataka kudhibiti zile blogu zinazotoa maudhui ya ngono na picha za utupu niwaambie tu hii siyo njia ya kuzidhibiti blogu za aina hiyo. Mtafute njia nyingine ya kitaalamu na mfanye utafiti mtaipata.

Natambua ugumu wanaoupata bloggers, kuanzia kutafuta habari, kuiandika na hata kuisambaza ili isomwe na upate pesa, hakika ni kazi ngumu sana, unaweza kupoteza masaa 16 kwa siku mtandaoni ukisaka maudhui ya kuwafurahisha wasomaji.

Halafu uambiwe uyalipie mil moja hahahaahah na huku unajua hata usipolipia hawana uwezo wa kukukamata. Kwa hili la blogu mzee Mwakyembe nikuhakikishie tu ya kwamba huwezi, utawapata hao wachache niliowataja hapo juu walioandikisha blogu zao kwa majina yao ila wale walioandikisha kwa majina yasiyojulikana mzee huwawezi hata kiduchu.

Njia pekee inayoweza kuzifunga blogu ni kwa kuufunga mtandao wa Google na WordPress ndani ya Tanzania basi vinginevyo haiwezekani. Na kuifunga Google hamuwezi.

2. USAJILI WA REDIO NA TELEVISIONI ZA MITANDAONI.

Kwa siku za karibuni tumeshuhudia ongezeko kubwa kwa hizi TV za mitandaoni (online TVs), TV hizi za mtandaoni kwa wingi zinarushwa kupitia mtandao wa Youtube ambao nao pia ni sehemu ya kampuni ya Google, Youtube inamilikiwa na Google japo kuna baadhi ya TV zinarushwa kupitia tovuti mbalimbali .

Usajili wa TV hizi nao umetakiwa kulipiwa shs laki moja kuombewa usajili pia kama utakubaliwa utahittajika kulipa kiasi cha shs laki 2 kila mwaka kama gharama yako ya kuruhusiwa kufanya kazi hiyo nchini Tanzania. Kama ilivyo kwenye blogu hizi chaneli za mitandaoni nazo ni chanzo kizuri cha mapato kwa vijana walioamua kujiajiri huko. Hupokea matangazo ya kibiashara kutoka kwenye makampuni ya kibiashara hususani Google ili kuweza kurusha kwa wateja na watazamaji.

Nyingi za video zinazorushwa kwenye channneli hizi za mitandaoni zina haki miliki (copyright) hivyo si rahisi kurusha video ya mwenzako, mara nyingi itakubidi utafute video zako halisi ili uweze ku survive kwenye gemu ya online TVs. Na hii ndio sababu ambayo inanifanya niamini ndio maana hawa wamiliki wa chaneli hizi wameshushiwa gharama ya malipo kwa mwaka japo wao ndio kwa sasa wanaingiza fedha nyingi sana zaidi ya wale wamiliki wa blogu na tovuti.

Usajili wa hizi chaneli za mitandaoni nao una changamoto zake, usajili wa chaneli ni bure na unahitaji hatua chache sana kuukamilisha. Na pia unaweza kutumia “ghost names” bila ya kutambulika na ukaweza kufanya biashara hii, hivyo kuwepo ugumu wa kutambulika na TCRA, kwa upande huu bado ninaamini TCRA watawakamata wale wenye chaneli zenye majina yanayowatambulisha kama Ayo Tv, Global TV Online n.k ila wale wenye majina yasiyojulikana TCRA waandike maumivu ya kuwakamata na kuwatoza kiasi hicho kikubwa cha fedha walichopanga wizara bila ya kuwasiliana na wadau. Mimi naamini Teknolojia haidanganyi hivyo bado Google ndio wanazo haki zote za watumiaji wake.

3. WAMILIKI WA MAJUKWAA YA MITANDAONI (ONLINE FORUMS).

Majukwaa ya mitandaoni yamekuwa ni chachu kubwa sana ya uibukaji mbalimbali katika jamii. Majukwaa haya yamekuwa yakitumiwa na watu mbalimbali kuibua masuala mbalimbali ya kiserikali, kijamii. Kwa siku za karibuni yamekuwa ni mwiba mkali dhidi ya serikali ya Tanzania. Kama nilivyotangulia kusema hapo juu serikali imekuwa ikitafuta namna mbalimbali ya kuya hold majukwaa haya bila ya mafanikio.

Walikuja na utaratibu wa kutaka kuyalazimisha majukwaa haya yote yajisajili kwa rajisi ya Tanzania ili iwe rahisi kwao kwa TCRA kuyafunga ila hilo limeshindikana kwa sababu usajili wa rajisi ya jukwaa au tovuti yeyote ni maamuzi ya msajili/mmiliki na hii iko kote duniani.

Huwezi kunilazimisha nilisajili jukwaa langu kwa rajisi ya Tanzania huku lengo langu ni kupata watumiaji kote duniani na kufahamika kwa wengi kiurahisi. Mfano wa majukwa ya mitandaoni kwa hapa nchini ni Jamii Forums, Mwanahalisi Forum, Facebook, Twitter n.k japo hizi 2 za mwisho hawana uwezo wake na wamiliki wake hawawezi.

Lengo kubwa la usajili huu linalotajwa na kanuni ya maudhui ni kuiwezesha TCRA kuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua wamiliki ikiwemo jukwaa lenyewe endapo litaonekana kukukiuka kanuni. Kwa kadri ya muonekano unaondelea kujengwa na watawala kwetu tunaamini hili siyo lengo zuri bali wanalo lengo la kuziba mianya ya serikali kuzodolewa, kusemwa na hata kuibua makosa yake mitandaoni, maana njia pekee iliyobakia kwa Watanzania kusema ni kupitia haya majukwaa ya JamiiForums, Mwanahalisi Forums.

Ni imani yangu baada ya serikali kushindwa kuwalazimisha kusajili rajisi zao nchini wameamua waje na njia hii ya kanuni ya maudhui. Wamiliki wa majukwaa haya wanajulikana na itakuwa rahisi kwao kuwapata endapo itahitajika.

TCRA hawana uwezo wa kuzifunga hizi Jamii forums wala mwanahalisi forum bali kwa kanuni hii mpya watakuwa na uwezo wa kuzizuia zisipost chochote, hawana uwezo wa kupata taarifa za watumiaji wa mitandao hiyo, wanaloweza kufanya ni hilo hapo juu tu kwa kuwa tu wamekuja na kanuni hii mpya.

Kwa upande wangu naamini kwamba kanuni hii imekuja mahususi ili kuweza kuwadhibiti Jamii Forums, Mwanahalisi Forums magazeti yanaoandika habari zake mitandaoni kama vile Raia Mwema. Ni muda muafaka sasa Watanzania tukaiga nchi ya Ethiopia kwa kuanza kuwa watu wa kutazama sana udaku mitandaoni badala ya kusoma vitu vya maana kwa ajili ya taifa letu, sote tuhamie Millard Ayo, Dizzim Online, Jonijooo n.k ili tukaharibu bongo zetu huko kwa udaku uliotukuka.

JE, SERIKALI ITAWEZA HII VITA?

Kwa maelezo yangu hapo juu serikai yetu haitaweza kuifikia adhima yake iliyodhamiria bali itaibua akaunti nyingi feki mitandaoni na hata chaneli feki za TV za mitandaoni, hili likiwa ni lengo la kukwepa kiasi kikubwa cha fedha za usajili kilichopangwa na kile cha kila mwaka.

Katika dhana ya uandishi na utoaji wa habari mara nyingi siyo vizuri kujulikana ili kukwepa shari pale unaposhindwa kuikwepa, sote tunajua watoa taarifa za mitandao ni binadamu na binadamu anakosea, ni nani aliye tayari kuwa charged kwa sababu ya kurusha mandamano mfano ya kisiasa ambayo serikali inaweza kusema yalikuwa si halali? Nani? Hakuna? Kama hauko tayari basi hautakuwa tayari kujisajili TCRA ili kulinda usiri wako.

Inachotakiwa kufanya serikali ni kushirikiana na haya makampuni makubwa kama Google ili kuweza kuzifunga akaunti zile ambazo zinaonekana kupotosha jamii kwa uchochezi, chuki na hata kimaadili kwa kuziripoti akaunti za namna hiyo na si kutaka kuzisimamia akaunti za mitandaoni kitu ambacho ninarudia tena hawakiwezi.

JE, WAMILIKI WA MAUDHUI YA MITANDAONI WAFUNGE BIASHARA ZAO?

Huu ndio mda sahihi sasa wa kuonyesha kwamba hakuna binadamu anaeweza kushindana na teknolojia. Mbinu mpya za kutoa mawazo yetu kupitia majukwaa, blogu na TV za mitandaoni ziibuliwe ili kuweza kukabiliana na kigingi hiki bila ya kuvunja sheria za nchi yetu ikiwemo katiba.

Katika ubunifu huo ikumbukwe kwamba lengo kuu ni kupeana elimu, habari na mwishowe kujipatia kipato ili kuweza kukidhi mahitaji. Watu wasitoke kwenye mistari na kuanza kujipendekeza na kusahau misingi ya uwazi na ukweli.
 
Wanakata tawi walilokalia... Hakuna watu wanapenda kiki za mitandaoni kama hao viongozi..
 
Acha serikali ishindwe vita, lakini blogs ,mitandao ya kijamii isajiliwe tu. Woga wa nini?

Unajua Madhara ya Kutumia mitandao ya kijamii in a negative way?
 
Nini kitatokea kama watu wakifungua hizo chaneli feki za TV mitandaoni? Kama TCRA inataka watu wajisajiri it means wanayo mechanism ya kutambua aliyelipa na ambaye hajalipa bado. So it will be easy kufungia yule asiyetaka kulipia.

Hayo ni mawazo yandu lakini.
 
Ahsante Mkuu, ni vigumu sana kupambana na teknologia, hizi zote ni mbinu za kutotaka kusikia wasichotaka kukisikia kutoka kwa wananchi. Naisihi serikali kwa dhati ikubali kuwaacha watu waseme kwa uhuru ili mradi wasivuje sheria. Kwani katika kuwasikiliza wasemacho huwenda ukakijua ambacho haukutazamia kukijua. Unaweza kumsikiliza kichaa na ukapata jambo ambalo kwako ni geni. Kwani hata professor anaweza kufundishwa kuwasha moto wa kuni.
 
Nini kitatokea kama watu wakifungua hizo chaneli feki za TV mitandaoni? Kama TCRA inataka watu wajisajiri it means wanayo mechanism ya kutambua aliyelipa na ambaye hajalipa bado. So it will be easy kufungia yule asiyetaka kulipia.

Hayo ni mawazo yandu lakini.
Chaneli feki za nini ndugu? Hakuna anayelazimishwa kutazama chaneli. Ukiingia youtube unatanzama kile unachovutiwa nacho. Kama tukianza kulipa, tutaanza kulipia kila kitu.
 
Acha serikali ishindwe vita, lakini blogs ,mitandao ya kijamii isajiliwe tu. Woga wa nini?

Unajua Madhara ya Kutumia mitandao ya kijamii in a negative way?
Hii nchi imekwisha. Wakipatikana vijana wenye mawazo kama wewe, basi tena Yesu aje atuchukue watu wake basi maana hakuna kitakacho fanyika.
 
KITAKACHO TOKEA, MAKAMPUNI YA SIMU YATALAZIMISHWA KUPUNGUZA DATA BUNDLES ILI KUDISCARAGE MATUMIZI YA MITANDAONI.
 
Ukifika wakati wa kampeni wataanza kuwapigia magoti na kujifanya wanawajali.

Yaani hata hizi tozo hawatazifuatilia lakinI wakifanikiwa kurudi madarakani watazidai kwa nguvu na faini juu.

CCM sio watu!!
 
Nini kitatokea kama watu wakifungua hizo chaneli feki za TV mitandaoni? Kama TCRA inataka watu wajisajiri it means wanayo mechanism ya kutambua aliyelipa na ambaye hajalipa bado. So it will be easy kufungia yule asiyetaka kulipia.

Hayo ni mawazo yandu lakini.

mechanism wataipata wap? ikiwa google ndyo mmiliki na hatokuwa radhi kutoa taarifa za wateja wao...kukurupuka kubaya sana
 
Back
Top Bottom