Semeni, msiogope, Rais lazima ang’oke/Raia Mwema, Septemba 25, 2019

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
BARAZANI

Semeni, msiogope, Rais lazima ang’oke

Na Ahmed Rajab

JUMAPILI Mei 21, 2017, marais wawili walikutana. Wote walikuwa wamepiga suti nyeusi, mashati meupe na tai za samawati. Walivaa viatu vyeusi vilivyofanana. Ila viatu vya mmojawao viking’ara zaidi ya vya mwenzake. Muda si muda, baada ya kupeana mikono na kutabasamu, wakaanza kupakana mafuta kwa mgongo wa chupa.

Aliyeanza alikuwa Abdel Fattah al Sisi wa Misri aliyemsifu mwenzake, Donald Trump wa Marekani, kwa kumwambia kwamba ana haiba ya kipekee na ana uwezo wa kulifanya lisilowezekana likawezekana. Al Sisi alimfanya Trump ajihisi kuwa ni mtu wa miujiza.

Kwa upande wake, Trump alimwambia al Sisi kwamba alivipenda viatu alivyovaa vilivyokuwa viking’ara zaidi ya vyake. Wakuu hao walikutana Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, ambako Trump aliwahutubia viongozi wa nchi zaidi ya 50 zenye wakaazi wengi walio Waislamu.

Wakati huo al Sisi alikuwa mkukuu madarakani. Ilikuwa miaka mitatu baada ya kumpindua Mohamed Morsi, Rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia. Trump alikuwa ndo kwanza anayaonja madaraka lakini tayari akionesha kiburi cha madaraka.

Wakati huo utawala wa al Sisi ulikuwa ukinuka kwa namna ulivyokuwa ukifanya mambo kimabavu na kwa kuzikiuka haki za binadamu. Utawala huo ulikuwa umekwishawaua watu wasiopungua elfu moja waliokuwa wakiandamana kupinga kupinduliwa kwa Morsi

Al Sisi alikuwa akiyafanya aliyoyafanya bila ya kukemewa na Marekani. Na walipokuwa wakipakana mafuta, al Sisi alijigamba kwamba nchi yake ilikuwa salama na thabiti kwa “ushirikiano” wa Marekani.

Wamisri walikuwa wameshamchoka. Ilikuwa kama si wao waliompigia vigelegele aliponyakua madaraka kwa kumpiga pute Morsi. Badala ya kuendelea kuonekana kama mwokozi, al Sisi aligeuka sura na kuwa dikteta.

Lakini kila aliyemwita dikteta hadharani alikiona chake. Hiyo ni tabia ya madikteta. Haikushangaza ila ilisikitisha kumuona mtu aliyeingia madarakani akipokewa kwa wema na wananchi wenzake baadaye akawageukia kwa kuwaumiza.

Alizidi kuzibirua taasisi za kidemokrasia na kuzifanya zimtumikie yeye. Taasisi moja aliyoitumia vibaya ni mahakama na mfumo mzima wa sheria nchini Misri. Matokeo ya hayo ni kwamba wapinzani wake wasiopungua 60,000 wako jela na wengi wao wamehukumiwa kunyongwa.

Sambamba na kuwaumiza wakosoaji wake kwa kuwatumbukiza jela na kuzikaba haki zao za kiraia, al Sisi amekuwa pia akiuendesha vibaya uchumi wa Misri, nchi kubwa yenye wakaazi wasiopungua milioni 90 wengi wao wakiishi maisha ya dhiki. Kwa kubana matumizi ya serikali, al Sisi ameiondoa misaada ambayo serikali ilikuwa ikiwapa wananchi kwa mfano katika ununuzi wa mafuta ya petroli au kwa upande wa bei za vyakula, hasa mikate.

Al Sisi alianza kuzichukua hatua hizo za kubana matumizi mwaka 2016 zikiwa miongoni mwa masharti aliyowekewa na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, ili Misri ipewe mkopo wa dola za Marekani bilioni 12.

Vijidikteta sampuli ya al Sisi huwa haviitalii na kuisoma vizuri historia. Inashangaza kumuona al Sisi akiwa hivi alivyo kwani alikuwa na fursa nzuri ya kuitalii vilivyo historia ya karibuni ya nchi yake na ya jirani zake. Angelifanya hivyo angeweza kuliepusha hili janga linalomkabili sasa nchini mwake na linaloweza kumzoa na kumtupa kwenye jaa pamoja na madikteta waliomtangulia.

Al Sisi alikuwa na pengi pa kujifunza. Angeliweza kuangalia namna Rais Hosni Mubarak alivyotawala na jinsi alivyong’olewa madarakani na umma wa Misri. Au namna Rais Zine el Abidine Ben Ali wa Tunisia (aliyefariki Alhamisi iliyopita akiwa uhamishoni Saudi Arabia) alivyoangushwa kwa maandamano. Au namna maandamano yalivyowaondosha madarakani Rais Abdel Aziz Bouteflika wa Algeria na Rais Omar Hasan al Bashir wa Sudan.

Si bure kwamba Wamisri wanamuelezea al Sisi kuwa ni kibaraka wa Netanyahu (waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu) na wa Mohamed bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia na anayefikiriwa kuwa ndiye mwenye kushika usukani wa uendeshaji wa taifa hilo. Viongozi aina ya al Sisi ama hupachikwa madarakani na madola makubwa ya nje au huvumiliwa na madola hayo ilimradi wawe hawayadhuru maslahi ya madola yanayohusika. Mara nyingi huwa wanayatumikia maslahi ya madola hayo.

Hivyo ndivyo al Sisi anavyofikiriwa na wengi, nje na ndani ya nchi yake, kwamba ni kibaraka wa Israel, Marekani na Saudi Arabia. Mwezi uliopita Trump mwenyewe wakati wa mkutano wa G7 huko Biarritz, Ufaransa, alimtaja al Sisi hadharani kuwa ni “dikteta nimpendaye”. Ndio maana mwishoni mwa wiki iliyopita kuna Mmisri mmoja, Iyad al Baghdadi, aliyempelekea Trump ujumbe kwenye Twitter akimwambia: “dikteta wako umpendaye yuko njiani anakuja New York. Muweke huko huko. Wamisri hawamtaki.”

Al Sisi alikuwa anakwenda kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambao alitarajiwa kuuhutubia leo Jumatano. Hii ni mara yake ya sita tangu awe kiongozi wa Misri kuhudhuria mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Mwaka huu nusura aivunje safari yake kwa sababu ya maandamano makubwa yaliyozuka jijini Cairo na katika miji mingine kadhaa nchini humo dhidi ya utawala wake na yenye kumtaka aondoke madarakani. Maandamano makubwa yalifanywa katika medani ya Tahrir huko Cairo na pia katika mji wa Suez.

Maandamano yote hayo yalikumbusha yale yaliyofanywa dhidi ya Mubarak na yaliyomtaka aondoke madarakani. Mwishowe Mubarak hakuwa na hila ila kuyaacha madaraka.

Maandamano dhidi ya al Sisi yalikuwa maandamano ya mwanzo makubwa tangu kiongozi huyo ashike madaraka miaka sita iliyopita. Mengi yamepita nchini Misri katika muda wote huo. Kubwa kati ya hayo ni jinsi al Sisi alivyozidi kujizatiti katika madaraka kimabavu, jambo ambalo ni dhahiri Wamisri wengi wamechoka nalo.

Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyowafanya waandamanaji wasiogope tena ukandamizi wa polisi na wanajeshi wa Misri na wakawa tayari kuihalifu sheria ya mwaka 2013 yenye kupiga marufuku maandamano. Sheria hiyo iliwekwa baada ya jeshi chini ya al Sisi kumpindua Morsi.

Tukiyaangalia yaliyopita katika nchi nyingine tunaona kwamba sheria kama hizo za kuwazuia watu wasiandamane pamoja na nguvu kubwa zinazotumiwa na vyombo vya ulinzi kuyazima maandamano hufanikiwa kwa kipindi fulani tu.

Baada ya muda umma unaodhulumiwa haki zao za kidemokrasia kwa kukandamizwa huwa sugu. Wananchi huwa hawauogopi tena utawala. Husema “naliwe liwalo” na huwa tayari kupambana nao utawala mpaka unapoanguka. Kwa sasa, kuna dalili kwamba Wamisri wako tayari kwa mara nyingine kumpindua Rais wao kama walivyompindua Mubarak 2011.

Safari hii waandamanaji wanahamasishwa na Mohamed Ali, mkandarasi wa majenzi na mwigizaji wa sinema, anayedai mitandaoni kwamba al Sisi pamoja na wanajeshi wenzake wameifisidi nchi kwa ubadhirifu wa kutumia mamilioni ya dola za Marekani kujijengea majumba ya kifahari, hoteli na kasri mpya ya al Sisi. Ali anasema kwamba al Sisi akitaka kasri mpya ijengwe kwa sababu mkewe hakutaka kulala katika jumba alilokuwa akilala mkewe Mubarak, Suzanne.

Ali, anayeishi uhamishoni Uhispania, amewataka Wamisri wampindue Rais wao na pia amemsihi waziri wa ulinzi, Mohamed Ahmed Zaki, amkamate al Sisi. Mwaka 2013, al Sisi alikuwa waziri wa ulinzi alipomkamata na kumpindua Rais Morsi.

Kwa upande wake, al Sisi amezikanusha tuhuma zote hizo kuwa ni za uwongo na ni uzandiki mtupu.

Wananchi wa kawaida wa Misri wanaoishi maisha magumu wanaziamini. Wameingiwa na ghadhabu wakijitazama na kuyaona maisha duni wanayoishi na wakisikia jinsi al Sisi na wenzake wanavyotumia fedha za umma kuishi maisha ya kifahari.

Maandamano haya ni kitisho kikubwa kwa utawala wa al Sisi. Waandamanaji, wengi wao vijana, wamekuwa wakitiana moyo kwa kuambizana wasikae kimya, wasiogope kuendelea kudai kwamba al Sisi lazima ajiuzulu.

Tunasikia kwamba si wananchi wa kawaida tu wenye hasira naye. Inasemekana kwamba kuna wakuu wa jeshi na wa baadhi ya taasisi za serikali wanaomuona al Sisi kuwa “mzigo” kwa taifa. Wamekaa chonjo wanasubiri wakati muwafaka wa kumuangusha.

Miongoni mwa shutuma za ufisadi anazoshutumiwa al Sisi ni hatua yake ya kuwateua mwenyewe majaji wakuu wa nchi hiyo, wakiwa pamoja na majaji wa Mahakama Kuu ya Kikatiba. Hii ni mara ya mwanzo katika historia ya Misri kwa Rais kuwateua binafsi majaji wakuu. Kwa kufanya hivyo, kuna hatari kwamba mahakama hayatokuwa huru.

Kadhalika al Sisi anatuhumiwa kuwa sababu ya kupandishwa cheo mwanawe, Mahmoud, kwenye ngazi za juu za Idara ya Ujasusi ya Misri, GIS. Wakati huo huo watumishi wengine wa idara hiyo walilazimishwa wastaafu.

Tutaweza kuupima vizuri mustakbali wa al Sisi siku ya Ijumaa, siku ambayo pametolewa wito wa kufanywa maandamano zaidi nchi nzima. Lakini hata kama maandamano hayo yatakandamizwa na majeshi ya ulinzi na polisi, al Sisi hajihisi tena kuwa yuko salama. Iko siku lazima ataanguka kama walivyoanguka madikteta waliomtangulia nchini mwake na katika nchi za jirani,


Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
 
Kuna simulizi ukizisoma unaweza kujikuta mwenye mikono salama bila kujijua
 
Back
Top Bottom