Sasa naona wazi kwamba Prof. Mwandosya ni tofauti sana na wengine

Synthesizer

JF-Expert Member
Feb 15, 2010
11,143
18,774
Nimekuwa nikifuatilia kwa makini yale wanayosema wale wanaotangaza uraisi, na mara nyingi nimesikitishwa na mambo yanayosemwa na watu ambao wanajitokeza tuwaone wanafaa kuwa viongozi wa nchi yetu. Hata nilisema katika posti moja kwamba watu wanafanya mzaha na hii taasisi ya uraisi, wakidhani kwamba wanaweza kuwa maraisi kwa kuangalia nani amewahi kuwa raisi au kujitokeza na kudhani kama hata yule amejitokeza basi hata mie ngoja nijitokeze!

Tofauti na wengine, Prof Mwandosya ameongea kwa namna ambayo inamtofautisha sana na wengine wanaojitokeza. Ame-balance vizuri sana kati ya masuala ya chama chake CCM na yale ya kitaifa. Pia amegusia mambo karibu yote muhimu, kutia ndani ulinzi wa Tanzania, jambo ambalo wagombea wengi sana huwa hawalikumbuki. Lililovutia hata zaidi ni jinsi ambavyo ameingiza katika hotuba yake suala la Zanzibar - just brilliant!

Kwa mtu yeyote mwenye kufikri, ataona huyu jamaa kweli akili inafanya kazi kichwani. Kuna mambo ya msingi ambayo mie binafsi ameni-impress sana katika hotuba yake;

  • anajua wakati huu si wa kulaumu waliopita bali kuwapongeza kwa waliyojitahidi kufanya, huku akiongelea atafanya nini kuendeleza pale walipofikia
  • hakishambulii chama chake cha CCM (CCM haiyumbi bali watu) na kukumbusha zile ahadi za CCM ambazo nadhani wengi hata ndani ya CCM wamezisahau au hawazijali
  • halaumu mtu kwa mapungufu tuliyo nayo bali mfumo tunaotumia (kuiwezesha Takukuru)
  • Anasema wazi uchumi kwanza uboreshwe ili kuimarisha elimu na afya, badala ya kutoa ahadi hewa isiyo na msingi
  • Anakumbushia umuhimu wa kuwa na viwanda, na kutoahidi vijana kazi bali kuwasaidia na kuwawezesha wajiajiri na au kupanua wigo wa kupata ajira nje ya Tanzania
  • Anaongelea kuimarisha kilimo kwa kubadili miundombinu ya kilimo
  • Anaongea kwa namna ya kuwafanya Zanzibar wajue tuko pamoja nao, kwamba wao ni muhimu katika Tanzania na wanaweza kuwa kitovu cha maendeleo ya nchi yetu
  • hajisifii kwa yale aliyotenda, bali anakubali aliweza kuyafanya pamoja na wengine
  • Amesema wanaotaka kujua alichofanya waulize watu wengine aliofanya nao kazi badala ya kumtaka yeye ajisifie

Hotuba yake kama ilivyoripotiwa katika mwananchi iko hapa chini.

Profesa Mwandosya aja na mambo 10 kuinua uchumi
Mbeya. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya jana alitangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kusema kesho atachukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

Profesa Mwandosya alisema atachukua fomu katika Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kesho saa nne asubuhi mjini Dodoma.

Akitangaza nia hiyo jijini Mbeya, Profesa Mwandosya alianza kwa vijembe, akisema alikuwa kimya kutangaza nia hiyo kama neema tu ya Mungu. Alisema katika maisha ni afadhali kuwa kimya kuliko kuwa mpayukaji na mwenye uamuzi wa papo kwa papo yenye hasara kwa Taifa.

"Mara nyingi katika maisha mjenga hoja na mtendaji makini ni bora kuliko mpayukaji mwenye maamuzi ya papo kwa papo na kusababisha hasara kwa Taifa,'' alisema.

Alisema kipindi cha mpito katika Serikali nyingi ni kigumu, hivyo misingi ya waasisi wa Taifa inachangia Watanzania kuendelea kuwa na furaha.

CCM haiyumbi, bali wanachama

"Wapo wanaosema CCM inayumba, lakini mimi nasema CCM haiyumbi isipokuwa baadhi ya wanachama wake ndiyo wanaoyumba mno baada ya kukiuka kiapo cha ahadi za CCM ikiwamo inayokataza rushwa,'' alisema na kuzisoma ahadi zote za CCM:

  • Ahadi ya kwanza inasema; ‘binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
  • ahadi ya pili; ‘nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, ya tatu; ‘nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma'
  • ya nne; ‘rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa'." Alisema na kueleza kwamba mbali ya ahadi hiyo, wengi wameikiuka na hivyo wanayumba.
  • Alitaja ahadi nyingine kuwa ni ya tano isemayo; ‘cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu,'
  • ya sita; ‘nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote,'
  • ya saba inasema; ‘nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu,
  • ya nane; ‘nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko na ya
  • tisa inasema; ‘nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.'

Profesa Mwandosya aliwaambia mamia ya wanannchi waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Mkapa kwamba wana CCM wengi wamekiuka ahadi hizo ambazo waliapa mbele ya Watanzania na Mungu na kwamba ndiyo maana wanayumba wao, lakini CCM ipo imara.

Sababu za kugombea

Alisema ameamua kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho ili kuhakikisha Dira ya Maendeleo ya 2025 ambayo alishiriki kuiandaa mwaka 2000, inatekelezwa na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati na hatimaye mwaka 2050 iwe nchi ya dunia ya kwanza.

"Sasa tutafikaje huko, wengi wanaweza kuuliza," alisema na kueleza kuwa ameandaa mambo 10 ya kutekeleza ili kufikia malengo hayo.

Profesa Mwandosya aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha kisasa na kisayansi kinachozingatia sifa zote za kilimo cha kisasa kwa kuboresha pembejeo na miundombinu yote ya shughuli za kilimo.

Alitaja suala la pili kuwa ni kupambana na rushwa kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia mapapa wa rushwa wasishughulikiwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

"Upo utaratibu kwamba kabla ya kuhojiwa, vigogo wala rushwa, lazima Takukuru wapate kibali, lakini kwa wala rushwa wadogowadogo wao wanakamatwa na kufikishwa mahakamani bila kizuizi hicho, sasa hilo ni kero,'' alisema.

Alisema akifanikiwa kupita na kuingia Ikulu, ataboresha sheria ili vigogo wa rushwa kubwa washughulikiwe kuliko wadogo ambao wataacha wenyewe.

Pia alisema akifanikiwa katika safari yake hiyo, atahakikisha vyombo vya kiuchumi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mifuko ya hifadhi inapewa uhuru zaidi wa kujisimamia na kwamba Serikali itakuwa mhimili wa uchumi ili kuwafanya Watanzania waone matunda ya kukua kwa uchumi.

"Serikali itakuwa injini ya kukua kwa uchumi kwa kuboresha mazingira ili sekta binafsi zifanye kazi kwa ufanisi na kulipa kodi nzuri kwa Serikali,'' alisema.

Profesa Mwandosya alisema uchumi ukizorota Serikali, haiwezi kutekeleza majukumu na kwamba zilizotangulia zilifanya kazi nzuri kwa kujenga misingi ya uchumi.

Alisema mambo mengine ya kutekeleza ni kuanzisha na kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuhimiza zaidi kilimo cha umwagiliaji ili nchi ijitosheleze kwa chakula na kuuza mazao yaliyosindikwa nje ya nchi.

Hatua nyingine ni kuondoa vizuizi vya uwekezaji kwa Watanzania na hata wa nje, kuimarisha sekta ya utalii wa ndani na nje kwa vile una fursa nyingi na pia kuhakikisha sekta ya utumishi inaboreshwa ili wafanyakazi waongeze bidii, uadilifu na kujituma kazini.

Profesa Mwandosya alisifia Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwamba imefanya mengi mazuri, lakini Watanzania wengi hawathamini wakati viongozi na watu mbalimbali wa nje ya nchi wanashangaa kwa ufanisi wa kazi hiyo.

Alisema Tanzania inaendelea vizuri katika kukua uchumi wake na kwamba yeye atasimamia kwa nguvu zote kuhakikisha uchumi unazidi kupanda chati hadi kuwafikia Watanzania wote.

"Baada ya uchumi kukua nitahakikisha elimu inaboreshwa kwa kuangalia sera na mitalaa na ikiwezekana elimu ya msingi itaanza darasa la kwanza hadi la kumi, lakini baadaye litakuwa hadi la 12,'' alisema.

Alisema katika hili, pia atasimamia kuboreshwa kwa masilahi ya walimu na taaluma yao. Pia, baada ya uchumi kukua atahakikisha sekta ya afya inaboreshwa kwa kusimamia zaidi kitengo cha kinga akisema ni bora kuliko tiba.

"Kwa kweli siku hizi maofisa afya hawaonekani mitaa lakini utafika wakati tutalazimika kuimarisha zaidi kinga.''

Profesa Mwandosya aligusia pia kwamba Serikali yake itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na kuhakikisha Watanzania wanakuwa wamoja.

Alisema ulinzi wa Taifa na wananchi ni suala la lazima na kwamba akifanikiwa Serikali itaendelea kuliboresha.

Kuhusu ajira kwa vijana, alisema wasomi wanaotembea na vyeti mikononi kutafuta ajira wanapoteza muda na kuwataka vijana wa aina hiyo wawe wabunifu na wenye mawazo ya kujiajiri.

Aliwataka vijana wenye mawazo na fikra za kutaka kufanya kazi ya kujiajiri wafike kwake na watasaidiwa kupata fedha, lakini siyo kuomba kazi.

"Vijana jitumeni, hata kama mnakosa kazi Tanzania, wasomi nendeni Uarabuni, Zambia na Malawi kutafuta kazi, jifunzeni lugha mbalimbali za kimataifa kikiwamo Kichina,'' alisema na kuongeza kwamba wasomi wengi wa Kenya, Uganda , Ghana na Nigeria wamejaa nchi za mbali kufanya kazi.

Profesa Mwandosya alizungumzia pia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akieleza kuwa ataudumisha kwa nguvu zote ili uwe wa kuigwa Afrika.

Alisema kwa kawaida visiwa vingi duniani ni chimbuko la maendeleo, hivyo anaamini Zanzibar inaweza kuwa kitovu cha maendeleo ya Tanzania.

"Zanzibar ikiwa na rasilimali watu, ikitumiwa vizuri itakuwa kitovu cha maendeleo ya nchi yetu,'' alisema.

Kuhusu sababu za kutangaza nia ya kuchukua fomu za urais jijini hapa Profesa Mwandosya alisema alizaliwa Mbeya miaka 68 iliyopita na kusoma Shule ya Msingi Majengo. Aliishi eneo hilo kwa kipindi kirefu.

Profesa Mwandosya alisema mbali na yeye kuishi jijini Mbeya pia Baba wa Taifa Marehemu Julius Nyerere alikuwa akifanya mikutano yake eneo la viwanja hivyo wakati alipokuwa akidai uhuru wa Tanganyika.

"Eneo hili enzi hizo lilikuwa likiitwa Welfare Center, hivyo Waafrika walikuwa wakikusanyika hapa kumsikiliza Mwalimu Nyerere,'' alisema.

Awali, watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya waliwasili na kuelezea matumaini yao kwa Profesa Mwandosya.

Wazanzibari watinga Mbeya

Katika hali isiyotarajiwa Wazanzibari zaidi ya 10 walitua jijini hapa wakiwa wamevalia fulana zilizoandikwa "Matumaini ya Zanzibar yapo kwa Profesa Mwandosya.''

Wazanzibari hao wengi wao wakiwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, walisema walifika Mbeya kwa vile wanamwamini Profesa Mwandosya kwamba anaweza kuisaidia Tanzania Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Pia, alikuwapo Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa ambaye alisema kwamba Profesa Mwandosya anafaa kuongoza Tanzania kwa kuwa ana uelewa na mtazamo wa maendeleo ya kweli.

Ajibu maswali

Alipoulizwa atawafanyia nini Watanzania ili kuwaongezea imani alisema Profesa Mwandosya alisema: "Nitasimamia utawala bora na kuishi kwa kufuata haki na amani. Siamini katika utajiri wa kuwagawia wananchi."

Kuhusu amelifanyia nini Taifa kwa kipindi chote alichokuwa mtumishi wa Serikali alisema: "Nimeyafanya mengi na wenzangu, sina nilichofanya peke yangu. Niliwahi kwenda kwenye shule moja ambayo niliichangia fedha nyingi na wakataka shule ile iitwe jina langu lakini nilikataa," alisema na kuongeza: "Nilikataa kwa sababu hata kama kiongozi anabuni miradi mbalimbali, utekelezaji ni wa watu tofauti."

Hata hivyo, aliwataka watu wanaotaka kujua zaidi mchango wake kwa jamii kwenda wizarani au kwenye taasisi mbalimbali alizowahi kufanyia kazi kuzitafuta na akawataka Watanzania wajenge desturi ya kujisomea vitabu ili kujua waliyofanya na watu tofauti.

Update: Membe atoa tamko Prof. Mwandosya ni namba moja kwa uadilifu na aina ya kiongozi anayetakiwa kwa Tanzania

Hii ya Membe imeniacha hoi. Kwa kifupi, amesema kwamba kama CCM haitampitisha kuingia tano bora, atampigia kampeni kwa moyo wa dhati Profesa Mark Mwandosya iwapo ataingia fainali ya kuwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais. Alisema unapozungumzia viongozi waadilifu nchini, Profesa Mwandosya ni namba moja, kwani amekuwa kiongozi mwenye maadili ya uongozi na mwenye upendo wa dhati kwa wengine.

"Natamka hili kwa moyo wangu wa dhati, jina langu lisiporudi ndani ya chama, nitampigia kampeni Profesa Mwandosya. Sina tatizo lolote hata wakisema mimi nimuachie Mwandosya nipo tayari, kwani ndiyo viongozi wanaotakiwa kama yeye kwa sasa kuongoza nchi yetu," alisema.

Source: Mwananchi


 
Nasahihisha hapa: "CCM HAIYUMBI ILA WANACHAMA" Hivi kuna chama bila wanachama? Tuseme wana CCM "wote " wakichana kadi zao na kukana uanachama bado kutakuwa na chama cha CCM? Napata shida kuelewa kabisa. Hizi ni kauli za kujifariji tu na kuepusha shari. Anajaribu kuepuka malumbano na wanaoharibu chama.
 
Nasahihisha hapa: "CCM HAIYUMBI ILA WANACHAMA" Hivi kuna chama bila wanachama? Tuseme wana CCM "wote " wakichana kadi zao na kukana uanachama bado kutakuwa na chama cha CCM? Napata shida kuelewa kabisa. Hizi ni kauli za kujifariji tu na kuepusha shari. Anajaribu kuepuka malumbano na wanaoharibu chama.

Gari haliyumbi ila ni dereva!
 
Slogan ya MBEYA KWANZA VYAMA BAADAE ndio inayomwangusha?
 
Nasahihisha hapa: "CCM HAIYUMBI ILA WANACHAMA" Hivi kuna chama bila wanachama? Tuseme wana CCM "wote " wakichana kadi zao na kukana uanachama bado kutakuwa na chama cha CCM? Napata shida kuelewa kabisa. Hizi ni kauli za kujifariji tu na kuepusha shari. Anajaribu kuepuka malumbano na wanaoharibu chama.

Mkuu, mie nimemuelewa sana hapa Prof Mwandosya. Anatumia organizational theory, kwamba "organizations are meant to outlive their members". Kwa hiyo ukitumia hiyo concept, kuyumba kunakotokea katika CCM kunakuwa ni kwa muda, na chimbuko lake sio misingi ya uundwaji wa taasisi, bali baadhi ya watu katika taasisi. Nadhani ndio maana alitoa zile ahadi tisa za CCM.
 
Hafai ana elements za kukumbatia mafisadi. Hata kuwa mkali kuinyoosha nchi bali legelege kulinda chama chake

Acha ushabiki, sema ukweli. Hebu linganisha aliyosema yeye na wagombea wengine wa CCM. Ukweli ni kwamba hadi sasa watu walioonyesha busara kwenye kueleza nia ni Lipumba wa CUF na Mwandosya wa CCM.
 
Nimekuwa nikimfatilia kwa karibu Prof Mwandosya.
Nadhani ana vigezo tunavyohitaji.
Ngoja tuendelee kumtathmini.
 
Huyu nae angejikalia kimya tu mambo yaishe ... watu wanakumbukumbu nzuri sana alichokifanya TTCL, CELTEL ...
 
Huyu nae angejikalia kimya tu mambo yaishe ... watu wanakumbukumbu nzuri sana alichokifanya TTCL, CELTEL ...

Tuacheni ushabiki jamani, tunatafuta kiongozi kwa maslahi ya nchi, sio ya kwetu binafsi tunaoshabikia watu au mtu fulani. Haipingiki kwamba kama tunataka kuwa na kiongozi mwenye vision, basi kwa kutumia hotuba wanazotoa hadi sasa Prof. Mwandosya anaongoza. Lakini ngoja tusubiri wengine, kutia ndani na vyama vingine, sio CCM tu.
 
Synthesizer

nothing new within ccm my friend they have been in the system for different occasions nothing have been done, so conclusively no body from ccm qualifies,they have failed totally!
 
Last edited by a moderator:
Anaongoza kwa kuwavalisha watu tshirt za Zanzibar? Kwa hoja ipi mpya? ... So far ameifanyia nini nchi hii zaidi ya Business as usual ? ....
Tuacheni ushabiki jamani, tunatafuta kiongozi kwa maslahi ya nchi, sio ya kwetu binafsi tunaoshabikia watu au mtu fulani. Haipingiki kwamba kama tunataka kuwa na kiongozi mwenye vision, basi kwa kutumia hotuba wanazotoa hadi sasa Prof. Mwandosya anaongoza. Lakini ngoja tusubiri wengine, kutia ndani na vyama vingine, sio CCM tu.
 
Nimekuwa nikiuliza watu wa jimbo la Mwandosya, wananiambia huenda Mwandosya ni mbunge pekee ambaye kwenye jimbo lake hata vyama vya upinzani vilikuwa vinamkubali kwa kutoweka mpinzani kushindania kiti cha ubunge katika jimbo lake. Kuna hii post iliwahi kutoka hivi karibuni. Sasa naelewa kwa nini.

Upinzani wambeba Prof. Mwandosya urais 2015

VIONGOZI wa Chama cha NCCR-Mageuzi na TADEA mkoani hapa, wamemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, kugombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba ni mtu mwadilifu.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mbeya, viongozi hao walisema wamechoshwa na tetesi na minong'ono iliyopo mitaani kuwa atawania nafasi hiyo huku yeye akiwa amekaa kimya bila kukata kiu ya wafuasi wake ndani na nje ya CCM.

Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Mbeya, Chifu Daimon Mwakatumbula, alisema wanamtaka Profesa Mwandosya kutangaza msimamo wake akiwa mkoani Mbeya ambako ni Mbunge wa Rungwe Mashariki.

"Tunamtaka Profesa Mwandosya aje Mbeya na atangaze akiwa huku kuhusu msimamo wake wa kuwania nafasi ya urais mwaka huu au la, na sisi akitangaza kuwania nafasi hiyo tutamuunga mkono maana ni mwadilifu," alisema Chifu Mwakatumbula.

Akizidi kumpigia debe, Mwakatumbula alisema katika wizara ambazo amewahi kuongoza Profesa Mwandosya hajawahi kuwa na kashfa na kwamba hana tabia ya kusaidia mtu mmoja mmoja bali anakuwa na masilahi mapana ya taifa.

"Sisi kama viongozi wa vyama vya upinzani, tunamtafuta rais wa nchi na wala siyo rais wa chama fulani, kwa sababu tunaamini katika kaulimbiu ya ‘Tanzania kwanza, vyama baadaye'," alisema Mwakatumbula.

Kiongozi huyo ambaye chama chake kimo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambao wanatarajia kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao, alisema mwaka 2010, hata Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba aliwahi kusema Mwandosya ndiye anafaa kuwania urais.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TADEA Mkoa wa Mbeya, Boniface Mwakibinga, alisema Profesa Mwandosya kabla hajawa Mbunge wa Rungwe Mashariki, alidhihirisha kuwa uongozi huanzia nyumbani baada ya kujenga shule na kupeleka maji katika jimbo lake.

"Profesa Mwandosya ni msikivu na ana heshima kubwa kwa wenzetu wa nje ya nchi kutokana na uadilifu wake, hivyo akipata nafasi ya urais hakika Tanzania tutakuwa tumepata kiongozi bora na sisi wapinzani tutampigia kura bila kujali itikadi zetu," alisema Mwakibinga.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, kupitia NCCR-Mageuzi, Policia Mwaiseje, alisema baadhi ya waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wana harufu mbaya za ufisadi.

"Maandiko matakatifu yanasema tafuteni kwanza ufalme wa mbinguni na mengine yote mtazidishiwa, lakini kwenye siasa ni kwamba tafuteni kwanza ufalme wa siasa na mengine yote mtayapata, hivyo mapinduzi ya kiutamaduni yanahitajika katika taifa ili tusonge mbele," alisema Mwaiseje.

Kuhusu yeye kuwania ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini, alisema hadi sasa hajafanya uamuzi ingawa atamuunga mkono mgombea yeyote atakayesimamishwa na Ukawa.

Chanzo:Mtanzania
 
Akiwa kama waziri asiye na wizara maalum amelifanyia nn taifa lake na huo uwaziri wa kuhongwa

Wewe kuku acha hizo. Tukianza kusema hivyo hakuna atakaesimama, au unaweza kukuta bado ni Prof. Mwandosya anaesimama. Hebu jaribu kuuliza swali hilo hilo kwa kila aliyejitokeza.....
 
Professor ungepumzika na siasa sasa. Nchi ilipofikia tunahitaji mabadiliko kwa kasi kubwa na fikra za kuambiana ukweli waziwazi, hili jema na hili baya. Halafu tutende na kwenda mbele.
 
Back
Top Bottom