Sababu Muswada wa Bima ya Afya kwa wote kukwama tena Bungeni

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC), ambao kwa miaka zaidi ya mitatu umekuwa ukikwama kuwasilishwa bungeni, kwa mara nyingine umegonga mwamba kujadiliwa na kupitishwa kwa kile kilichoelezwa kukosekana kwa chanzo cha fedha kitakachowezesha utaratibu huo kuwa endelevu.

Muswada huo ulitegemewa kuwasilishwa juzi kwa mara ya pili bungeni Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu baada ya Septemba 23 mwaka huu kusomwa kwa mara ya kwanza na kufuatiwa na ukusanyaji wa maoni ya wadau uliofanyika Oktoba 19 na Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge, muswada huo ulipangwa kuingia bungeni Novemba 2, lakini ukasogezwa hadi jana kabla ya kuondolewa kwenye ratiba za shughuli za Bunge.

Jana asubuhi baada ya dua kabla ya kikao kuanza, Spika Dk Tulia Ackson alisema hati iliyokuwa iwasilishwe na Waziri wa Afya, ya muswada huo haitawasilishwa tena mezani kwa sababu Serikali na Bunge wanaendelea na mashauriano.

“Sasa hati hii haitawasilishwa leo (jana) mezani kwa sababu Bunge pamoja na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri,” alisema bila kueleza zaidi.

Alisema Bunge hilo halitautazama muswada huo tena na badala yake wataendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na wabunge, wadau waliojitokeza katika kamati na nyingine za Serikali.

Alisema Serikali inaendelea kuangalia namna bora ya kuwahudumia wananchi kwenye eneo hilo na kwamba utapelekwa bungeni watakapokamilisha mashauriano hayo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, miongoni mwa mambo yaliyosababisha muswada huo kutojadiliwa jana ni kukosekana kwa chanzo endelevu cha kuhudumia watu wasio na uwezo wa kumudu gharama za bima.

“Nchi kama Ghana wamefanikiwa kwa kuwa na bima ya afya kwa wote endelevu kwa sababu wana chanzo endelevu kutoka kwenye VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo,” alisema mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka kutajwa jina.

Novemba 3, mwaka huu wakati wa semina ya wabunge iliyofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa, Waziri Mwalimu alisema tathimini waliyoifanya imebaini watu milioni 15 wameonekana kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo za bima.

…maeneo tisa

Akizungumza na Mwananchi jana katika viwanja vya Bunge, lililotaka kujua kilichokwamisha muswada huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo, alisema sehemu zote tisa za muswada zilionekana kuwa na shida, hivyo kunahitajika mashauriano zaidi na Serikali.

Alipoulizwa kama suala la uendelevu ni miongoni mwa mambo yaliyofanya muswada huo kutojadiliwa bungeni, Nyongo alijibu kwa kifupi “na hilo ni miongoni mwao.”

Hata hivyo, Waziri Ummy alipoulizwa ni mambo gani yamesababisha muswada huo kukwama hakuwa tayari kueleza.

Kauli ya mwenyekiti huyo wa kamati iliungwa mkono na Wakili Fulgence Massawe wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), aliyesema waliuchambua muswada huo na kuuona una upungufu, hivyo wakashauri ufanyiwe maboresho na hakukuwa na haja ya kuwahi kuupitisha na changamoto zilizopo.

“Mfano muswada ulishindwa kuainisha chanzo cha mapato kwa ajili ya watu wasiokuwa na uwezo na pia haikutoa tafsiri mtu asiye na uwezo ni nani.

“Pia muswada ulikuwa unanyima watu huduma nyingine muhimu, mfano kupata kadi ya Utambulisho wa Taifa (NIDA), sasa ajabu ili kusajiliwa huduma za bima lazima uwe na namba ya NIDA, kwa hiyo kwa kipengele hicho tu sheria ilikuwa haitekelezeki,” alisema.

Ni takribani miaka mitatu sasa Serikali imekuwa ikieleza kuupeleka muswada huo bungeni, lakini unakwama. Novemba mwaka jana katika mkutano wa Bunge, aliyekuwa Spika, Job Ndugai alisema suala hilo linapaswa kushughulikiwa haraka.

Alisema hayo baada ya muswada huo uliokuwa uwasilishwe na aliyekuwa waziri wa Wizara ya Afya wakati huo, Dk Dorothy Gwajima kukwama, licha ya Novemba 17 mwaka jana kueleza ulikuwa tayari kufikishwa bungeni kwa hatua zaidi.

“Bima inagusa Watanzania wengi, hususan wa kipato cha chini, huu ni muda mwafaka kwa muswada kufikishwa, ili itungwe sheria. Ni muhimu Serikali ikasema kama kuna mkwamo mahali, ili Bunge lisaidie,” alisema Ndugai wakati huo akiwa spika kabla ya Januari mwaka huu kujiuzulu.

Septemba 11 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya kilele cha kusherehekea miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) zilizofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam alisema muswada huo ungepelekwa katika mkutano wa Bunge wa mwezi huo.

“Nataka niwape habari njema kwamba Bunge litakalokaa mwezi huu wa tisa, linakwenda kupitisha muswada wa sheria ya bima ya afya kwa Watanzania wote,” alisema Rais Samia.

Mkuu huyo wa nchi alisema kuwa bima ya afya kwa wote itasaidia wananchi kupata matibabu kwa wakati.

“Niwaombe sana ndugu zangu, tutakapopitisha sheria hii, Watanzania twendeni tukajiunge na mifuko ya bima ya afya,” alisema.


Uamuzi sahihi

Kukwama kwa muswada huo kumewaibua wadau, akiwemo Rais wa Chama cha Optometría Tanzania, Dk Asha Mweke aliyesema wameipokea hatua hiyo kwa mikono miwili kwa kuwa hawakupewa muda wa kutoa maoni yao, licha ya kufanya juhudi zinazohitajika.

“Naunga mkono alichofanya Spika wa Bunge, ukisema bima ya afya kwa wote ina maana ijumuishe huduma zote, sio anakuja mtu mwenye shida ya macho bima inashindwa kumhudumia, hii inakuwa haina maana.

“Pia huduma kwa watoa huduma wote iingizwe kwenye bima. Hawa watu wanaotoa huduma za afya ngazi ya jamii wanahudumia watu wa huku chini, hadi mtu apewe rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) tayari ni hatua nyingine, watoa huduma hawa wajumuishwe nao ili watoe huduma bora kwa wananchi,” alisema.

Alisema mtoa huduma za afya ngazi ya jamii anayeshughulikia matatizo ya macho hatambuliki kwenye bima ya afya na anapomhudumia mgonjwa fomu ya bima anayopaswa kujaza hajazi, badala yake anayejaza ni mtu mwingine ambaye hakumhudumia mgonjwa huyo na kupatiwa malipo asiyostahili.

“Optometric (mtaalamu wa macho) anamuona mgonjwa mpaka dakika ya mwisho, lakini kusaini ile fomu ya bima anapelekewa daktari mwingine ambaye hajamhudumia mgonjwa akasaini, jambo ambalo sio sahihi,” alisema.

Dk Asha alisema kabla ya muswada huo kuwasilishwa kwa mara nyingine bungeni, huduma zote za afya kwa ujumla hazipaswi kukosekana.



Walichokisema wabunge

Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichwale alisema kutojadiliwa kwa muswada huo kutawasaidia kuusoma zaidi na pia kwenda kuwashirikisha wapigakura wao zaidi.

“Hadi Januari mwakani tunaweza kuja na mawazo mengine mapya ya namna ya kuboresha muswada huu, kwa sababu sisi tunasema kile ambacho wananchi wetu wanatuagiza kusema,” alisema.

Japhet Hasunga, mbunge wa (Vwawa-CCM), alisema Serikali imefanya vizuri kuahirisha mjadala wa muswada huo na hivyo itawapa nafasi kushauriana na wadau, ili kuja na muswada ambao ni timilifu utakaosaidia nchi pamoja na wananchi.

“Wameahirisha kwa sababu kuna baadhi ya vifungu ambavyo inabidi Serikali ifanye mashauriano ndani, lakini itafute vyanzo vingine vya kugharamia matibabu hayo,” alisema.

Hasunga ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) alisema kutafutwa kwa vyanzo vingine vya fedha kunatokana na muswada ulivyo hivi sasa kuwafanya wananchi wengi kuona ni mzigo mkubwa kujiunga na bima hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, sheria hiyo ikipita familia ya watu sita, wanapaswa kulipia Sh340,000 kwa mwaka.

Jesca Msambatavangu, mbunge wa Iringa Mjini (CCM) alisema haoni vibaya uamuzi uliofikiwa kwa sababu kwa hatua yoyote jambo linapoonekana halijaeleweka vizuri huwa linaahirishwa.

“Nchi ni ya kwetu tunapanga wenyewe, mambo ni ya kwetu, nyumba ni ya kwetu, kwa nini tufanye jambo tuharakishe lije lilete utata kwa wananchi? Naishukuru Serikali kwa sababu ni sikivu kwa mambo mengi,” alisema.

Alisema kuna wakati walipitisha mambo ya tozo za miamala, lakini yakaleta tatizo, jambo ambalo liliwafanya kurejesha tena bungeni kurekebisha.

“Kwenye muswada wa bima ya afya tuweke mazingira yawe salama, ili tunapowapa watu wetu kusiwe na vikwazo ama malalamiko. Naipongeza Serikali kwa hatua ya ujasiri kwamba wanaona wanaweza kwa hatua yoyote kufanya marekebisho kwa maslahi ya Watanzania,” alisema.



ACT-Wazalendo, Chadema

Makamu mwenyekiti wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu alisema uamuzi huo ni wa busara kwa sababu muswada huo si jambo dogo, hivyo ni vema likapata muda wa kutosha na mikakati ikawa imara na madhubuti.

“Kwa sababu jambo hilo likianza likaja kufeli mbele ya safari athari zake kwa Taifa kiuchumi na kijamii zitakuwa ni kubwa kweli kweli. Ni jambo jema hakuna mtu anayekataa bima ya afya kwa wote na limekuja kwa wakati sahihi,” alisema.

Alisema jambo kubwa linalohitajika ni kuendelea kutathiminiwa, kuendelea kupangwa vizuri, ili watakapoanza malengo yanayotakiwa bila kuleta taswira yoyote hasi katika jamii ama katika uchumi wa Taifa.

Hata hivyo, Mwalimu alisema kurudishwa kwa muswada huo kusiwe kufungia katika makabati.

Kauli ya Mwalimu inaungwa mkono na makamu mwenyekiti wa ACT-Wazalendo-Bara, Dorothy Semu aliyesema hatua ya kutojadiliwa kwa muswada huo bungeni ni sehemu ya maoni yao.

“Tulisema muswada huu unaharakishwa na tuliomba usitishwe, ili uendelee kupata mjadala mpaka kwa Watanzania na tupate suluhisho la kudumu, bima ya afya kwa wote ni kitu kizuri, lakini mifumo ambayo Serikali ilikuwa ikipendekeza ilikuwa imefeli kabla ya kuanza,” alisema.

Alisema wao wametoa suluhisho la jinsi ya kugharamia bima ya afya kwa wote na wanapendekeza wananchi wote kuelekezwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii ambapo bima ya afya kwa wote itakuwa ni sehemu ya fao la hifadhi ya jamii.



Yaliyomo kwenye muswada

Miongoni mwa mambo yaliyomo kwenye muswada huo ni kuzitaka mamlaka nane zinazotoa usajili, vibali, hati au leseni kwa waombaji kuzingatia kigezo cha uwepo wa uthibitisho wa uanachama katika skimu ya bima ya afya.

Mapendekezo hayo yamewekwa kufanyika kwa kuzingatia sheria zilizotungwa na Bunge, mamlaka zinazohusika na usimamizi au utoaji.

Muswada huo unazitaja mamlaka hizo ni zinazotoa leseni ya udereva, bima za vyombo vya moto, utambulisho wa mlipa kodi, usajili wa laini za simu, leseni ya biashara, hati ya kusafiria au viza, uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha tano, kidato cha sita na vyuoni na utoaji wa kitambulisho cha Taifa.

Kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa katika kanuni, mwajiri katika sekta ya umma na sekta rasmi binafsi atapaswa kumsajili mwajiriwa katika skimu ya bima ya afya ndani ya siku 30 tangu kuanza kwa mkataba wa ajira.

Kwa madhumuni ya upatikanaji wa kitita cha mafao ya msingi, kila mwajiri chini ya sekta ya umma na sekta binafsi atawasilisha katika skimu asilimia sita ya mshahara wa mwajiriwa na yeye atachangia nusu ya kiwango.

Muswada unaeleza waziri kwa kushauriana na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, ataainisha viwango vya uchangiaji kwa ajili ya sekta isiyo rasmi.

Pia ulipendekeza waziri, kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika, na kwa kupitia kanuni, ataweka utaratibu na namna ya utambuzi wa watu wasio na uwezo.

MWANANCHI
 
Hii haiwezekani, walitegemea kuongeza tozo baada ya kelele za Watz, wameanza kughairi... Bima ya afya kwa wote Budget yoote ya wizara ya afya nayo haitoshi
 
Kwa sasa tu ikiwa ya watu wachache nanga zinapaa huduma si ya kuridhisha sembese ikiwa Kwa wote?!
 
Back
Top Bottom