Rushwa yaendelea kuisakama CCM hadi Chipukizi

Magezi

JF-Expert Member
Oct 26, 2008
3,359
692
Mwandishi Wetu, Morogoro

TATIZO la rushwa katika chaguzi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), linaonekana kuzidi kukua baada ya uchaguzi wa viongozi wa chipukizi taifa kukumbwa na matukio ya utoaji takrima kwa wajumbe wa mkutano huo.

Habari zilizopatikana kutoka katika mkutano huo uliofanyika mjini Morogoro, Desemba 29 mwaka jana, zinaeleza baadhi ya wapambe wa wagombea waligawa pesa hadharani na wengine kukutana nao usiku wa manane.

Utoaji wa rushwa kwa wajumbe ulianza siku moja kabla ya uchaguzi huo ambapo wapambe wa wagombea hao watoto wadogo wa miaka kumi, walipita kwa wajumbe wakiomba kura na kutoa takrima mbalimbali zikiwamo pesa.

Katika uchaguzi huo ambao watoto wa vigogo ndani ya chama hicho waliibuka washindi, unaelezwa kuwa ni ishara mbaya kwa CCM kwa vile sasa hata watoto wadogo wa miaka 10, wanafundishwa kutoa na kupokea rushwa.

Wajumbe wa mkutano huo ni wenyeviti wote wa Chipukizi wilaya ambao ni watoto wa miaka 10 hadi 13, na makatibu wa Chipukizi na uhamasishaji wa wilaya ambao huwa ni vijana wakubwa.

Pia uchunguzi huo umebaini kuwa makatibu wa mikoa wa UVCCM ndio waliotumiwa na vigogo ndani ya CCM kupanga mkakati wa kuwawezesha watoto wao, kushinda katika uchaguzi huo.

"Hilo si siri kweli tuliitwa na baadhi ya watu ambao walijitambulisha walitumwa na kigogo na kupewa msimamo wa kuhakikisha kijana anashinda, tusimwangushe," alisema mjumbe mmoja wa mkutano huo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Morogoro, Jonas Nkya alikanusha hayo akisema uchaguzi ulifanyika vizuri na yeye binafsi alishuhudia hakukuwepo vitendo vyovyote vya rushwa. Kigezo kingine ambacho Nkya alikichukulia kama sehemu ya uchaguzi kwenda vizuri ni kutokuwepo na malalamiko.

"Hadi sasa hakuna kiongozi wala mgombea ambaye amewasilisha malalamiko kuulalamikia," alisema Nkya huku akitoa wito wa yeyote ambaye hakuridhika na uchaguzi huo kutosita kuwasilisha malalamiko yake.

Baadhi ya wajumbe wengine wa mkutano huo, waliiambia Mwananchi Jumapili kwa masharti ya kutotajwa majina kuwa uchaguzi huo uligubikwa na rushwa kuchafuana majina miongoni mwa kambi hali iliyosababisha watoto wa vigogo kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo.

Walisema pamoja na kuweka msimamo wao mwanzo wa kuhakikisha hawawachagui watoto wa vigogo, msimamo huo ulishindikana kutokana na shinikizo la viongozi wa juu na kulainishwa kwa rushwa.

"Kwa kweli sisi wajumbe tulishaweka msimamo wetu baada ya kuona nafasi nyeti zote katika umoja wetu zinachukuliwa na watoto wa wakubwa na hivyo, kupendekeza tuwachague walalahoi wenzetu," alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Kanda ya Ziwa.

Baadhi ya wajumbe hao walidai msimamo huo uliwashtua baadhi ya viongozi wa juu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) taifa waliokuwepo mkoani hapa na kuamua kumshauri mmoja wa wagombea wa uchaguzi huo, Halfan Kikwete asitokee katika uchaguzi huo kwa kukwepa aibu ya kushindwa.

Waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Gabriel Makala ambaye ni mtoto wa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Taifa, Amos Makala kuwa Mwenyekiti mpya wa chipukizi taifa baada ya kupata kura 300 kati ya kura 357 zilizopigwa na hivyo kuwashinda wagombea wenzake saba waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Mbali na Makala pia mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, Halfan Kikwete alichaguliwa kuwa mjumbe wa baraza kuu kutoka Tanzania bara kwa kura 301 bila kuwako ukumbini hali mbayo iliwashangaza wafuatiliaji wengi wa uchaguzi huo.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika uchaguzi huo, uliohudhuriwa na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Emanuel Nchimbi, mshauri wa rais January Makamba, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM taifa, Amos Makala pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya ulibaini kulikuwepo na mazingira ya rushwa.

Mwandishi wa habari hii aliyekuwepo katika chuo cha ualimu Kigurunyembe siku moja kabla ya uchaguzi huo saa 7:00 usiku, alishuhudia vigogo mbalimbali wakiwaamsha wajumbe katika vyumba vyao na kugawa fedha kuwashawishi wawapigie kura wagombea wao.

Hata hivyo, habari zingine zimedai kuwa makatibu wa Chipukizi na Uhamasishaji waliitisha mgomo siku moja kabla ya uchaguzi huo wakidai posho waliyopewa ni ndogo na hivyo hata wakipiga kura hawatawachagua watoto wa vigogo.

Hatua hiyo ilimfanya kiongozi mmoja wa CCM kunusuru jahazi kwa kuwapa sh 30,000 kila mmoja na hivyo uchaguzi ukafanyika.
Source: Mwananchi Jumapili
 
Kwa mwendo huu CCM mnatuharibia nchi na watoto wetu kuwafundisha wizi
 
Umuhimu ni upi wa uchaguzi huu jamani na hao watoto wanategemewa kufanya maamuzi gani ? Je watoto wa Isamilo, Rorya , Tarime, Bunda , Tandahimba, Iringa nk walikuja ama ilikuwaje mie sielewi haya mambo
 
Siku hizi experiences zitajengwa na kutafutwa kwa pesa....ili baadae ukiingia mwenzangu na mie uambiwe bado hujaiva kichama!!
 
Inaoneka uchaguzi huu nao umegharimu mipesa kibao.KUNAFAIDA GANI HAO watoto kuingia kwenye uchaguzi?
Je hao watoto wanafahamu nini maana ya siasa hasa za vyama vingi?
Je anayonafasi ya kujifunza uongozi kweli kweli?
Je wanawakilisha kundi gani na kwa utaratibu upi?
Maoni yangu:Tuache watoto wasome tusiwaingize ktk vurugu za kisiasa na kuwakomazi wangali wadogo.
Mashuleni watajifunza uongozi ktk ngazi zao na kwa upeo wao eg KIRANJA,M/kiti TYCS,BAKWATA etc pia kuna Rais,mawaziri,wabunge kwa level ya chuo kikuu.
 
Makapi yamezaa makapi!!!!!!!!!!

Fikiria endapo bidii hiyo ya kuwaingiza watoto katika rushwa ingebadilishwa wakafundishwa UZALENDO na kujitolea kwa ajili ya ukombozi wa kweli wa nchi yao.
Viongozi wa CCM na wanachama wake wamepoteza kabisa hisia za utaifa na hakika CCM itatumaliza.

CCM mama wa rushwa na umasikini wa nchi yetu!!
 
wale walongi wanakumbuka ule
wimbo uliopigwa marufuku wa western jazz
ambao ulikuwa na sehemu inasema "chenyewee
kimejibanza..." nadhani wimbo huu ungefaa sana
wakati huu.
 
Tumefikia hatua mbaya sana. Hawa jamaa wameona mbinu mpya ya kuingiza watoto wao kwenye uongozi ni kwa kupitia vikundi kama hivyo, ili baadaye waseme wana historia katika chama. Hebu tujiulize hao watoto wanaelewa kweli wanachokigombea? Badala ya kuwasisitizia wasome wapate ufahamu wa mambo wanafundishwa namna ya kutoa rushwa. Hizi ni dalili za wazi kabisa za kufilisika kimawazo.
 
How about ule msemo wa tahadhari kabla ya hatari; hapa tena imeshekuwa too late uchaguzi ndio umeshapita na matokeo tumeshapewa.

Time ya kulalamika na kuhakikisha uchaguzi wa haki unatendeka ulikua wakati ule thread ya kwanza ilipokuja mtoto wa Kikwete achukua form.

Labda muanzilishi wa hile mada alikua na nia ya kutuambia wenye uwezo akikisheni haki hapo inatendeka au kama kuna namna tayari leteni tujue wapi amna lolote.

Sasa hapa cha ajabu wala sioni kwa jinsi tunavyo ifahamu Tanzania na kwa level hii ya uchaguzi wala amna haja ya kumpeleka mtoto hata kwenye huo uchaguzi hata shinda tu.

Hivyo wala sioni sababu ya kulalama hapa tusubiri na huyo mwingine aliebaki anatafutiwa nini cha rika lake kuongoza. Huyo ndio JK anajua vya kunyonga tu vya kuchinja awezi; kama yeye alivyopachikwa tu.
 
Jamani mabadiliko yanaanza kwako! Ukikataa kuipigia kura ccm mwaka huu utasaidia sana kuondoa haya matatizo yanayojitokeza haya. Hawa jamaa wanataka nchi iendeshwe kichif. Kibaya zaidi afadhali machif walikuwa na vision wenyewe ni sifuri
 
Wanawafundisha watoto wao uzuri wa rushwa katika kupata madaraka. Kama mtoto akikua anajua kuwa rushwa ni nzuri, basi itakuwa ni vigumu sana kumfanya apambane nayo. Ni kama mtu aliyekua kwa kula ugali, huwezi kumshibisha kwa kumpa sandwich au Pizza.
 
Kwa nini Makala alikwenda kwenye Uchaguzi ambao mtoto wake ni mgombea?

Je Makala alitumia rushwa, ahadi, takrima na vitisho vya namna gani mtoto wake akapata kura nyingi kiasi hicho na kuwashinda wale wagombea wengine saba?

Je watoto wenye umri chini ya miaka17, ambao walilipiwa nauli, mahali pa kulala, chakula na mengineyo, iweje walalamike kuwa wanataka posho? na zaidi kuwa posho waliyopewa haikutosha?

Kwa nini Nchimbi, January, Makala, Guninita na Machibya walikwenda kwenye huu uchaguzi? Je umashuhuri wao na wagombea waliowataka wao kuliathiri vipi matokeo ya uchaguzi huu?

Ikiwa CCM inapanda mbegu chafu ya kuona kuwa Takrima ni kitu sahihi na haki, iweje Watanzania waendelee kuamini kuwa CCM ndio chama mbadala na pekee kitakachoweza kuivusha Tanzania kutoka umasikini, dhuluma na hujuma na kuwa na jamii iliyo endelevu, fanisi na fikra huru?
 
Back
Top Bottom