Rubada: Umeme wa uhakika 2014 Stiegler’s Gorge

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
picture-9.jpg

Na Alfred Lucas - Imechapwa 11 July 2012

Ndani ya Jamii

BAADA ya ahadi nyingi za upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, hatimaye Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (Rubada) imefanikisha mradi mkubwa wa ujenzi wa umeme wa nguvu ya maji.


Mradi huo maarufu kama Stiegler's Gorge unatarajiwa kuingiza katika gridi ya taifa megawati 2100 na hivyo kulifanya taifa kuwa na ziada ya megawati 500.


Tayari mamlaka hiyo imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo na kampuni ya Odebrecht International ya Brazil na unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili ijayo.


Mkurugenzi wa Rubada, Aloyce Masanja akiwa mwenye furaha ya hatua iliyofikiwa amesema, "Hadi Julai 2014 Tanzania tutakuwa na Megawati 2100 za umeme kutokana na maporomoko ya mto Rufiji."


Katika mahojiano na mwandishi wa MwanaHALISI Jumamosi iliyopita, Masanja anayesimamia shirika linahusika na sekta nne; kilimo, nishati, maji na mazingira, alisema mradi huo utatekelezwa kwa awamu tatu. Hatua ya kwanza ilikuwa kutia kusaini mkataba uliofanyika wiki iliyopita.


Alisema baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, awamu hii inatoa fursa kufanyika upembuzi yakinifu kupitia ule uliofanywa awali na kampuni ya Nor-Consult ya Norway miaka ya 1980 na kufanyiwa maboresho na baada ya miezi sita kampuni hiyo itakabidhi ripoti ya kwanza.


Halafu awamu ya pili, alisema itahusisha mkataba wa kibiashara kwa kuangalia maji, teknolojia itakayotumika, vyanzo vya fedha na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.


"Awamu ya pili ni ya kufanya upembuzi yakinifu huku serikali ya Tanzania ikifanya tathmini ya kimazingira ya utekelezwaji wa mradi huo na awamu ya tatu ni ujenzi wenyewe," alifafanua.


Alisema ni lazima kuangalia mazingira kwa vile mradi huo wa Stiegler's uko katika Hifadhi ya Selous. Bonde hilo pia ni muhimu kwa kilimo.


Masanja, ambaye alijiunga Rubada mwaka 1993 kama mchumi, aliongeza kuwa hatua ya tatu itakuwa ni kuanza ujenzi wa mradi wenyewe na matarajio ni kuanza baada ya miaka miwili kuanzia sasa ukigharimu fedha za Marekani bilioni mbili na kwamba utakamilika katika kipindi kisichozidi miaka miwili kuanzia sasa.


Mradi huu utachangia kuimarika kwa viwanda na hatimaye kukuza uchumi wa Tanzania. Kukamilika kwa mradi huo kutafanya Watanzania kusahau shida ya umeme kwa muda mrefu baada ya mateso ya mgawo wa umeme wa mara kwa mara.


Hatua mbalimbali zilizochukuliwa awali hazikusaidia na ahadi za kutatua tatizo hilo hazikutekelezeka.


Mathalani, mwaka 2003 serikali iliahidi kuondoa kero ya umeme kwa kutumia makaa ya mawe kutokana na ujenzi wa miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na Kiwira, lakini haikutekeleza.


Mwaka 2008, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliliambia Bunge: "Tatizo la umeme litakuwa historia," lakini wapi.


Mwaka 2009, Masanja, wakati huo akiwa Kaimu Mkurugenzi wa miradi ya Rubada alisema tatizo la umeme nchini kuwa historia ifikapo 2012 ukikamilika mradi wa Stiegler's Gorge. Alieleza kwamba kiasi cha juu cha uzalishaji kitakuwa megawati 2750.


Desemba 24, 2010 Ngeleja akaboresha porojo zake akisema mgawo wa umeme utakuwa historia ifikapo mwaka 2013. Akijua kwamba umeme wa uhakika ni kitendawili kisicho na majibu, Februari 15, 2011 Ngeleja aliliambia Bunge kuwa serikali inahitaji Sh. 300 bilioni ili kukamilisha miradi ya muda mfupi na mrefu, itakayokamilika kati ya mwaka 2013 na 2033.


Machi 26, 2011 Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal akasema kero ya umeme itamalizika mwaka 2015.


Juni 27, 2011 Ngeleja akadai umeme ni janga la taifa akataka wananchi wavumilie. Mei 4 Ngeleja akatupwa nje ya Baraza la Mawaziri, nafasi yake ikachukuliwa na Prof. Sospeter Muhongo.


Masanja anasema kuwa japokuwa wamelenga kuzalisha megawati 2100 "…bonde lina uwezo wa kuzalisha megawati 3696 za umeme kwa nguvu za maji na lakini mradi wa Stigler's Gorge, unaweza kuzalisha kiasi cha megawati 2100 peke yake," anasema.


"Huo mradi wa umeme wa Stigler's Gorge ni mmoja wa miradi mingi tuliyonayo," anasema. "Pia tuna Mnyera unaoweza kuzalisha megawati 485 na Mpanga megawati 160.


Mkurugenzi huyo anataja miradi mingine kuwa ni Ruhuji (mw 685); Lukose (mw 130); Iringa (mw 87); Kilombero Kingengenanas na Shuguli Falls (mw 464) ambayo inakamilisha jumla ya Mw 3,696.


Masanja anasema kabla ya mradi huo, Rubada iliwahi "kuporwa" mradi wa Kihansi uliochukuliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lakini huu akasema, "Huu si kama wa Kihansi bwana, huu ni wetu."


Anasema kwamba mvutano ule na TANESCO ulikwisha na kwamba sasa "tumefungua ukurasa mpya."


Aidha, Masanja anasema mradi huo ukikamilika utaleta faida nyingi baadhi zikiwa ni uboreshaji wa kilimo katika bonde hilo, hivyo kutoa chakula kitakachotosha kwa mahitaji ya nchi na kuweka akiba kwa matumizi ya baadaye.


Lakini pia, Taifa litapata chakula cha ziada kwa ajili ya kuuza kwa nchi nyingine zitakazokabiliwa na tatizo la uhaba.


"Tulinyimwa fursa kwa muda mrefu ya kuboresha bonde hili. Nashukuru sasa tumepata nguvu baada ya serikali kuridhia hadi kusaini mkataba huu," anasema.


"Zamani tuliona ni kama serikali imetususa. Imeisusa Rubada kwa kutotupatia kipaumbele."


Bonde la Mto Rufiji lina eneo la kilomita 177,000 za mraba, ikijumuisha mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na sehemu za mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mbeya.


Ndani ya mikoa hiyo, kuna mabonde manne yenye rutuba - Kilombero, Usangu, Ruwegu na Rufiji Chini – yaliyo chini ya usimamizi wa Rubada na yote yanafaa kwa kilimo cha mpunga.


Kutiwa saini kwa mkataba huo kumeiondoa serikali katika mlolongo wa lawama baada ya porojo nyingi juu ya mipango ya upatikanaji wa umeme.


Baada ya kujiunga na Rubada mwaka 1993 kama mchumi wa mamlaka, mwaka 1995 alikwenda Japan kwa mafunzo maalum ya kilimo na maji.


Alipandishwa cheo na kuwa Ofisa Mipango. Baadaye aliteuliwa Mkurugenzi wa Uchumi na Mipango hadi mwaka 2009 alipoteuliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu. Aliteuliwa mkurugenzi kamili mwaka jana.



 
Back
Top Bottom