Riwaya maridhawa

Hassan Mambosasa

JF-Expert Member
Aug 2, 2014
3,350
4,485
RIWAYA: KOSA

MTUNZI: HASSAN O MAMBOSASA

SIMU:+255713776843

+255762219759

WHATSAPP:+255713776843


SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI MWENYEZIMUNGU MUUMBA WA DUNIA NA VILIVYOMO KWA KUNIPATIA AFYA NJEMA ILIYONIWEZESHA KUANDIKA RIWAYA HII KWA MARA NYINGINE



ANZA SASA KUUFUATILIA MKASA HUU


SEHEMU YA KWANZA!!

Sauti ya kulalamika ilisikika ikitoka ndani ya chumba kimojawapo cha nyumba ya kifahari iliyopo katikati jiji la Tanga, ni ndani ya mtaa ambao una makazi ya watu wenye nazo katika jiji hili katika maeneo ya Raskazone. Kijana mmoja mwenye asili ya kisomali aitwae Hassan alikuwa akilalamika mbele ya pacha wake anayeitwa Hussein, machozi yenye kutiririka mithili ya chemchem ya maji ndiyo yalikuwa yamefunika mboni za macho yake hadi akawa anaona ukungu katika macho yake. Hussein alikuwa ana kazi ya kumbembeleza pacha yake huyo aliyelia akilitaja jina la msichana, kilio chake kilikuwa ni uchungu tosha kwa pacha wake aliyekuwa anambembeleza. Neno mapenzi ndiyo lilitawala kinywa cha Hassan muda wote aliokuwa analia, kupende ndiyo kulimliza kijana huyo. Muda wote mapacha hawa ambao wanapendana kwa dhati wakiwa wanabembelezana, hawakutambua kama waliacha wazi mlango wa chumba chao wanacholala zaidi ya mmoja kulia tu na mwingine akiweka mawazo yake katika kumbembeleza mwenzake.

"Hassan hebu nyamaza basi wanawake wapo wengi utapata mwingine tu" Hussein alimwambia pacha wake.
"Hussein unajua inauma sana yaani Jabir kaamua kumroga Mariam ili apendwe yeye inauma, inauma kuona mtu ninayempenda kwa dhati anachukuliwa na mtu mwingine ambaye ni rafiki wangu wa karibu" Hassan aliongea kwa masikitiko huku machozi yakimbubujika machoni mwake.

"hebu wacha fikra zako potofu, una uhakika gani kama kamloga Mariam. Kaka Mariam ndiyo kapenda pale, nakushauri tu uachane na fikra za huyo mwanamke. Tafuta anayekupenda" Hussein aliongea huku akiwa amemshika pacha wake bega.

"Mariam na urembo wake wote ule atampendaje masikini kama yule mwenye kusomeshwa na mfadhili tu halafu aniache mimi niliyekuwa nina uwezo wa kumlisha na kumvalisha" Hassan aliongea.

"kaka mapenzi si pesa wala mali ndiyo utayapata, mapenzi ni kuweza kuuteka moyo wa mtu ndiyo utayapata na moyo wa mtu hautekwi kwa pesa" Hussein aliongea.

"Hussein na wewe usinichanganye kabisa, nimekuambia namtaka Mariam na nitampata kwa gharama yoyote ile na hata ikiwezekana kuondoka na maisha ya mtu. Yaani kuogopa kwangu kumuambia kama nampenda ndiyo njia aliyoitumia Jabir kumpata yeye, nasema sikubali hata kidogo na Jabir nitamshikisha adabu kwa pesa tu. Mbele ya hela hakuna kinachoshindikana na hata mapenzi yanawezekana" Hassan aliongea kwa hasira kupingana na ushauri wa pacha wake.

"PWAA! PWAA! PWAA! PWAAA! PWAAA!" sauti ya mtu akipiga makofi ilisikika ikitokea mlangoni mwa chumba chao wanacholala. Wote kwa pamoja walishtuka kisha wakageuka upande ambao sauti hiyo imetokea, walishtuka zaidi baada ya kumuona baba yao akiwa amesimama katikati mlango akiwa anawatazama.

"sijaona mtoto wangu mwenye akili na mwenye kutoa ushauri mzuri na wenye manufaa kama wewe Hussein na sijaona mtoto asiye na akili na mwenye kudanganywa na pesa za baba yake kama wewe Hassan" Baba yao aliongea huku akitembea kusogea mahali walipo Hassan na Hussein hadi alipowafikia kisha akaendela kuongea, "pesa si chochote si lolote ndani ya dunia hii wanangu hasa kwenye mapenzi, yaani we Hassan nilidhani kukaa chuo miaka miwili utakuwa umekua kiakili kumbe bado huna akili hata za kufikiria. Kakuambia mwanamke analogwa ili kumpenda mtu ndani ya dunia hii, mwenzako kauteka moyo na usitake utende kosa kama nililotenda mimi baba yako ambalo ninalijutia hadi leo".

"kosa!, kosa gani hilo baba?" Hussein aliuliza huku uso wake ukionesha kutomuelewa baba yake, Hassan alibaki akimtazama baba yake anavyoongea.

"wanangu sikuwahi kuwasimulia kuhusu kilichowahi kunipata kipindi cha nyuma nilipokuwa kijana kama nyinyi kwasababu ya ujinga ambao hata Hassan anataka kuufanya, Hassan mwanangu pamoja na wewe Hussein tambueni tu kuwa na pesa si kupata kila kitu ndani ya dunia hii" Baba yao aliongea huku macho yake yakiwa yana dalili za kutoka machozi, hal hiyo ilisababisha hata Hussein na Hassan wamuonee huruma baba yao.

"baba tueleze" Wote waliongea kwa pamoja walipomsogelea baba yao wakiwa wamekaa pembeni yake, Hassan alikaa upande wa kulia na Hussein alikaa upande wa kushoto. Mapacha hawa walimpenda sana baba yao na kitendo cha baba yao kuonekana ana dalili za kutokwa na machozi, kwao ilikuwa ni huzuni tosha.

"nisubirini hapahapa narudi sasa hivi" Baba yao aliinuka akaelekea nje ya chumba hicho kisha akarejea akiwa ameshika shajara(diary) kubwa mkononi, aliwapatia shajara hiyo kisha akasema "someni hii nadhani itawapa fundisho na pia mtatambua kosa nililolifanya". Hassan na Hussein waliipokea shajara hiyo kwa haraka, waliifungua ukurasa wakawa wanaanza kusoma huku baba yao akiwa anatoka nje ya chumba chao.

"tukianza asubuhi hii hadi jioni tutakuwa tumemaliza yote kwani kuna maelezo marefu" Hussein aliongea.
"tulia basi tusome maneno ya nini?" Hassan aliongea kutokana na kukereka na maneno ya Hussein.

****

"Pesa unaweza ukawa nazo lakini usiwe na kitu ukopendacho ndani ya dunia hii, unaweza ukafanya chochote unachotaka bila kujali kama unakosea au unapatia. Hii ni pesa ilinifanya mimi Abdulhafidh nifanye vitu pasipo kufikiria, utajiri wa baba yangu ambaye ni raia wa Somalia ndiyo ulinipa kichwa mpaka nikajiona nina uwezo wa kufanya chochote. Mpaka sasa najuta kwa hili jambo nililolifanya bila ya kuelewa uzito wake na matokeo yake, yote haya yalianzia baada ya kufanya jambo lililonifanya nijutie nafsi yangu.

Ilipita miaka kadhaa nikiwa nimelisahau jambo hilo nililolifanya na nikaamua kuwa mlevi ili kutuliza mawazo ya kumkosa yule ninayempenda ambaye amenikataa hata nilipotumia ushawishi wangu wote, nakumbuka vizuri ilikuwa ni jumapili tulivu nikiwa natoka klabu ya ya usiku ya bilicanas nikirejea nyumbani kwangu Masaki, nilikuwa nipo ndani ya gari yangu ya kifahari na pembeni yangu yupo changudoa niliyemuokota kwenye klabu hiyo kama ilivyo kawaida yangu kila mwisho wa wiki. Niliamua kununua machangudoa na kustarehe nao kwani sikutaka kuwa na mwanamke yoyote baada ya kukataliwa na Huwaida msichana mwenye asili ya kisomali kama mimi.

Nilifanikiwa kufika nyumbani nikiwa salama pamoja na changudoa niiliyemchukua usiku huo kwa ajili ya kustarehe ili kutuliza mihemko ya mwili wangu kutokana na kuathirika kitendo cha kukataliwa na Huwaida tangu naanza chuo kikuu hadi muda namaliza na hadi naanza kuendesha makampuni ya marehemu baba yangu, usiku hu kabla sijaanza kustarehe na binti huyo nilianza tabia yangu kupenda kunyonya matiti ya wanawake. Kitendo cha mimi kulinyonya titi la changudoa niliyemchukua nilihisi kichwa kizito na hatimaye nikaanza kupoteza nuru katika macho yangu, hali hiyo nilijitahidi kuizuia nikajua ni dalili ya kuumwa lakini nilishindwa na hatimaye fahamu zikanitoka.

Nilikuja kugutuka baada ya kuhisi upepo mwanana ukiupiga uso wangu, nilipofumbua macho nilikumbana na anga murua lenye wingu pamoja na dalili ya kunyesha mvua. Sauti za ndege ndizo zilizo nikurupusha na nikaona hali tofauti na eneo nililolala usiku uliopita.

Niljaribu kuvuta kumbukumbu ili kubaini kama nililala eneo hili lenye mchanga mwingi karibu na ufukwe wa bahari. Kumbukumhu zangu za mwisho zinaonesha sikuwa eneo hilo na nilikuwa nipo kitandani pamoja na changudoa niliyemchukua klabu ya Bilicanas. Nilibaki nimechanganyikiwa nisijue nimefikaje eneo lisilo na nyumba wakati usiku nilikuwa kitandani kwangu katika nyumba yangu, mwisho wake niliamua kuinuka na nikaanza kuzunguka maeneo ya eneo ambalo ni ngeni ili niweze kulitambua. Nilikuja kujua nipo kwenye kisiwa kidogo chenye kukaribiana na ukubwa wa nyumba yangu ya kisasa, hali ya kuchanganyikiwa ilinipata kuanzia muda huo na nikawa ninatembea kuzunguka kisiwa nyasi pamoja na miti kadhaa. Mwisho nilichoka na nikaamua kupumzika kwenye gogo nililoliona lipo katikati ya nyasi zilizopo kisiwani hapo, njaa na kiu nilianza kuhisi zikitafuna tumbo langu.

Nilikuwa nahema kwa nguvu kutokana kuchoka nilipokuwa natembea kukizunguka kisiwa bila muelekeo, gogo nililokalia nilihisi likianza kusogea kwa taratibu. Nilipotazama upande wa kulia kwangu niliona nililodhani ni gogo likijikunjakunja huku likisogea mbele hadi nikawa naogopa, sikutambua kama nimekaa mgongoni mwa nyoka mkubwa ambaye hivi sasa kichwa chake kimeshaingia baharini.

"Mamaaaaa!" Nilijikuta nikitoa ukelele wa uoga kisha nikaanza kukimbia kuelekea upande wa pili wa bahari kwenye kisiwa hicho kisha nikajitupa kwenye maji, nilianza kuogelea kuelekea nisipopajua hadi nikawa nimepotea katikati ya maji na nguvu zikawa zimeniisha.

Uzoefu nilionao katika kuogelea ndiyo ulinisaidia ndani ya siku hiyo, ndiyo maana hata nilipojitupa ndani ya maji sikuwa na hodu ya kufa maji na nilijua nitaweza kuogelea hadi niitafute nchi kavu. Sikuweza kutambua kutoka hapo nilipo hadi nchi kavu kuna umbali gani na pia sikutaka nikate tamaa na nife kirahisi wakati maisha bado nayapenda. Niliendelea kuogelea kwa taratibu nikiwa sina nguvu hivyohivyo hadi nilipouona mtumbwi kwa mbali ukiwa katikati ya bahari, kitendo cha kuuona mtumbwi huo kwangu ilikuwa ni tumaini jipya na nguvu mpya.

Niliongeza nguvu katika kupiga mbizi hadi nikaufikia mtumbwi huo, niliupanda nikidhani nitapata mwiko wa kupigia kasia ili nisogee lakini sikuukuta zaidi ya kukuta karatasi yenye maandishi haya, 'MTUMBWI HUU NDIYO SALAMA YAKO, UKITAKA KUISHI BASI INABIDI UUPANDE NA UTULIE'. Hadi nilipomaliza kuisoma karatasi hiyo tayari nilikuwa nipo ndani ya mtumbwi huo nikiwa nimekaa tu nikihema kutokana na kuchoka, sikuweza kuongoza mtumbwi huo na ikanibidi nitulie hivyohivyo nikiwa nimejilaza ndani yake.

Baada ya muda mfupi mtumbwu huo ulianza kutetemeka chini kuashiria kuna mashine, ulianza kuondoka kwa mwendo wa kasi kuelekea upande nisioujua kwa mwendo wa masaa kadhaa. Nilianza kuuona ufukwe wa bahari kwa mbali wenye mitumbwi mingi ya wavuvi ikiwa mitupu kwa muda huo wa mchana niliofika mahali hapo, mtumbwi niliopanda uliacha kusogea baada ya kukaribia ufukweni hapo kisha ukazama ndani ya maji kwa ghafla na kunifanya ninywe maji ya bahari bila kupenda hadi nilipoanza kuogelea kuelekea ufukweni. Kule ufukweni baadhi ya wavuvi waliona mtumbwi ukizama na walifika hadi kwenye maji kisha wakanitoa nje baada ya kuishiwa nguvu nilipofika kwenye maji yenye kina kifupi.

"is jy okay?(upo sawa)" Mmoja wa watu walionitoa kwenye maji aliniuliza kwa lugha ambayo nilikuwa siijui.

"is jy pyn(umeumia)?" Mwingine alishambulia kwa swali jingine ambalo nilikuwa silijui pia, nilibaki nikiwatizama kisha nikaanza kutazama mazingira ya eneo hilo nililolijua kwa umakini. Macho yangu yalitua kwenye kibao kilichopo kwenye barabara inayoingia eneo hilo, kibao hicho kiliandikwa maneno ya lugha ya kingereza niliyoyasoma 'WALVIS BAY'. Nilizidi kuchanganyikiwa zaidi na sikutambua nipo ndani ya nchi gani kwani Tanzania nilipozaliwa na kukulia hapakuwa na sehemu inayoitwa hivyo wala ufukwe wa namna.

"where am I?(nipo wapi)" Nilijikuta nikiwauliza wale watu walionitoa nje ambao kimuonekano walionekana ni wavuvi, watu hawa walitazamana kisha mmoja akaniuliza kwa tabu, "can you speak Afrikaas(unaweza kuongea kiafrikaas)?". Hapo ndipo nilipotambua nilipotambua kuwa watu hawa wanaongea lugha ya afrikaas inayoongelewa na watu wa kusini mwa Afrika, hivyo niliamua kutikisa kichwa kuonesha sikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha hiyo.

"who are you and where are you from(we ni nani unatokea wapi?)" Yule mmoja wao aliniuliza tena huku akinitazama kwa huruma. Swali hilo nilishindwa kulijibu kutokana na kuhofia usalama wangu, neno pekee nililolitamka ni, "help me(nisaidie)" kisha nikapoteza fahamu baada ya kuhisi kichwa kimekuwa kizito.

Nilipokuja kuzinduka nilijikuta nipo kwenye kitanda kikukuu katika chumba chenye mwanga hafifu sana, dari la nyumba hiyo lilikuwa ni chakavu kuliko kawaida. Nilipoangaza pembeni yangu upande wa kulia nilikuta bakuli kubwa lenye uji likiwa lipo kwenye stuli iliyochakaa sana, nilipoangaza pembeni yangu upande wa kulia niliona mlango wa kuingilia katika hicho. Mazingira ya chumba hicho yalionesha wazi kuwa ni katika kijiji ambacho sikuweza kukitambua hadi muda huo, yalikuwa ni mazingira ambayo sikutegemea kama nitakuja kukaa walau hata kwa saa moja kutokana na maisha niliyokulia toka utotoni. Sikutegemea hata kama nitakuja kulala kwenye kitanda kichakavu ambacho kinaumiza mbavu na mgongo kama hicho, mtoto wa kitajiri niliyekulia kwenye utajiri na ninaishi kitajiri nije kulala mahali kama hapo nilipojikuta nimelala baada ya kurudiwa na fahamu.

Ni ndani ya chumba ambacho nilikuwa nikiviona kwenye televisheni vikilaliwa na watu wenye hadhi ya chini ambacho kwangu nilikuwa nakiona kama choo, ewe mtoto wa kitajiri kama mimi usiombe ukalala kwenye chumba kama hicho kwani utajuta. Baada ya muda mfupi mlango wa chumba hicho uliojengwa na mabati ulifunguliwa kwa taratibu huku wakiingia watu watatu ambao wawili ni wanaume na mmoja ni mwanamke, watu hao walisogea hadi kitandani nilipolala huku wakingea lugha ya kiafrikaas. Sikuwaelewa kutokana na kutokuwa mzungumzaji wa lugha hiyo, watu hawa walizungumza kwa muda mfupi kisha wakanigeukia wote kwa pamoja wakawa wananitazama kwa tabasamu la matumaini baada ya kuniona nikiwa nimerejewa na fahamu. Kunitazama kwao huko kulisababisha niulize swali kwa lugha ya kiswahili pasipo kutambua nipo eneo lisilo na waswahili, "hapa nipo wapi?".

Wote waliposikia lugha niliyozungumza walishtuka sana kisha mmoja wao akatoka nje kwa haraka sana akiwaacha wenzake ndani wakiwa wananitazama tu pasipo kuongea chochote. Baada ya dakika kadhaa ule mlango chumba nilichokuwemo ulifunguliwa tena, yule mtu aliyetoka aliingia na mwanaume mwingine ambaye baadaye nilikuja kumtambua ni mmoja kati ya wale watu waliokuwa kule ufukweni. Mtu huyu ndiye aliyekuwa ananiuliza maswali kwa lugha ya kingereza huku wenzake wakinilulza kwa lugha ya kiafrikaas, mtu huyu aliwaambia wale wenzake "ekskuuz(samahani)" huku akiwaonesha ishara ya wao kutoka nje ya chumba hicho. Wote walitoka nje ya chumba akabaki yeye pamoja na mimi, aliamua kuja kuketi kitandani nilipolala huku akinipa mkono wake.

"habari yako" Alinisalimia kwa kiswahili fasaha kabisa hadi nikamshangaa kutokana na lugha waliyokuwa na wanaongea wenzake, salamu yake hiyo nilishindwa kuijibu kutokana na mshangao niliokuwa nao muda huo.

"usishangae sana kuniona naongea kuswahili, mimi ni mtanzania niliyekimbia maisha ya Tanzania, Jonas naitwa nani mwenzangu" Aliniambia ili kuniondoa hofu niliyokuwa nayo moyoni mwangu kisha akajitambulisha jina lake.

"hapa ni wapi kwanza na nimefika vipi?" Nilijikuta nikiuliza swali badala ya kutoa utambulisho wangu kama alivyotoa wa kwake.

"hapa ni eneo la ghuba ya Walvis kijijini katika mkoa wa Erongo" Jonas alijibu swali huku akizidi kuniacha njia panda kutokana na kutoijua sehemu anayonitajia. Nilizidi kumuuliza zaidi, "Erongo?! Nchi gani?". Jonas baadaya kusikia swali langu hilo alinitazama kwa umakini kisha akasema,"Namibia". Nilijikuta nikishtuka sana baada ya kutajiwa nchi hii iliyopo Kusini mwa bara la Afrika ambayo niliwahi kufika maeneo ya Windhoek kibiashara na nilikaa katika hoteli ya nyota tano iliyopo katikati ya jiji la Windhoek.

"kwanza hujaniambia hata jina lako ndugu, pia hujaniambia ulifika pale kwenye ufukwe wa ghuba ya Walvis" Jonas alinisemesha kwa upole sana.

"naitwa Abdul" Nilijitambulisha kwa kutaja jina langu kwa ufupi kutokana na mazoea niliyokuwa katika kulitumia jina langu kwa namna hiyo kisha nikamueleza kutoka mwanzo hadi nilipojikuta kwenye kisiwa asubuhi. Maelezo yangu yalimfanya Jonas anitazame kama mtu niliyechanganyikiwa hasa nilioomuambia kwamba nililala kwenye kitanda changu cha kifahari nikaja kuamka nikajikuta nipo katika mchanga wa ufukwe wa kisiwa nisichokijua, Jonas alitikisa kichwa kwa masikitiko kisha akainuka huku akitoa bahadha ya kaki mfukoni mwake halafu akanipatia.

"hiyo bahasha imeletwa na mtoto mdogo aliyetuambia amepewa na mtu ailete, tumeitambua kuwa inakuhusu wewe kutokana picha yako kuwa juu ya bahasha. Kunywa uji huo upate nguvu mi nakuacha upumzike na uangalie kilichomo ndani ya bahasha hiyo" Jonas aliongea huku akielekea mlangoni akiniacha mimi nikiwa njia panda zaidi kutokana na mambo yaliyonikuta ndani ya maisha yangu kwa muda mfupi toka nilale na changudoa ndani ya nyumba yangu, muda mwingine nilidhani kuwa utajiri niliokuwa nao ilikuwa ni ndoto na sasa nimeamka usingizini kwenye mazingira yangu halisi ya maisha yangu ya kila siku. Nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa na nilihisi naelekea kuwa kichaa kwa hayo yaliyonikuta ndani ya maisha yangu ndani ya muda huo, tajiri mkubwa kama mimi ambaye anamiliki kampuni kadhaa nchini Tanzania nipo kwenye nyumba mbavu za mbwa.


****

"Mmmh hivi ni kweli" Hassan alijikuta akimuuliza Hussein baada kuumaliza ukurasa wa kwanza wa shajara waliyopewa na baba yake.
"ebwanaeh utaniulizaje mimi tena, wa kuulizwa ni mshua" Hussein alimwambia Hassan huku akinyanyuka kitandani walipokuwa wamekaa halafu akasema, "muda wa msosi huu twende tukale". Wote kwa pamoja walitoka chumbani kuelekea kwenye ukumbi wa kulia chakula, walimkuta baba yao yupo mezani tayari akiwa anakula. Walijumuika naye mezani hapo huku wakimtazama sana usoni.
"hivi baba yale ni matukio ya kweli?!" Hussein aliuliza.

"kwa sasa siwezi kuwajibu mpaka mmalize kusoma yote" Baba yao aliwajibu.

"ni kisa chenye kuvutia sana" Hassan aliongea akiwa na tabasamu usoni hata kile kilio chake kilichokuwa kinamsumbua sana alikisahau kutokana na kuvutiwa na ukurasa wa kwanza wa maelezo yaliyomo ndani ya Shajara ya baba yake.
"malizeni kula kwanza ndiyo mengine yatafuata, kama kuongea basi ongeeni mkimaliza kula" Baba yao aliwaambia.


*JE NDANI YA BAHASHA YA KAKI ALIYOPEWA ABDUL KUNA NINI?

*JE KOSA HILO NI LIPI?


YOTE HAYO UTAYAPATA UKENDELEA KUFUATILIA MKASA HUU WENYE KUFUNDISHA
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom