Riwaya: Hatia


RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya
SEHEMU YA KUMI NA SABA

Mzee Keto na upendo wake atanielewaje?? Alijiuliza Mariana, mara bila kutegemea, ule uasili wa kabila lake uasili usioaminiwa na watu wengi lakini ni uasili wa asili, uasili wa kurithi kutoka kwa chifu Mkwawa, ‘kuliko kudhalilika heri kufa!!!', Mariana akajikuta akiwaza kujiua tena kwa kujinyonga. Maneno machache yalichafua karatasi, kanga yake ilimtosha kabisa muhehe huyu, Mariana akajinyonga chumbani mwake!!!
Hasira, mfadhaiko na uasili ukawa umemuua Mariana. Hatia yake ilikuwa nzito kujibu kuliko kuikwepa. Mariana kitanzini akapanda na hatia yake.

*****

Kundi dogo la vijana lilikuwa limemzunguka kijana mwenzao ambaye alionekana kuwa katika hali tofauti kidogo ya maisha, walikuwa wanakunywa pombe huku wakilikubali kila jambo ambalo alikuwa akilisema kijana huyu.
Alikuwa amevaa nguo zilizoonekana kuwa mpya lakini kwake hazikumkaa vyema, tumbo lake liliinyanyua shati yake na kuifanya kuwa fupi jambo ambalo liliruhusu mgongo wake kuonekana. Nywele zake zilizotoka kunyolewa siku kadhaa nyuma zilikuwa zinameremeta. Alikuwa anatoa noti kadhaa na kumlipa muhudumu, vijana wenzake walinyanyua glasi zao juu na kuzigonganisha ishara ya kumsifia, hakuna ambaye alikuwa amelewa.
Mfukoni alikuwa na shilingi laki moja na nusu, elfu hamsini pungufu ya pesa alizokuwa amekuja nazo eneo lile la Villa Park akiwa ametokea nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amehamia.
Huyu alikuwa ni Defao akiwa ameisahau familia yake, akiwa amemsahau hadi Minja aliyekuwa amempa dili hilo. Defao alikuwa anaijaribu ladha tamu ya pesa, hakika ilikuwa tamu sana na ni ladha hiyo ambayo ilimuweka jijini Mwanza kwa siku kadhaa mbele.
Heshima yake katika eneo la Villa Park ilikuwa juu sana, siku hiyo hiyo alipata mpenzi, akaondoka na kwenda kulala naye katika chumba alichokuwa amefikia. Ladha hiyo ya umaarufu ikamsahaulisha mengi akaisahau hatia yake ya kumdhulumu Minja mgao wake, pia hatia ya kuitelekeza familia yake ilikuwa imeenda likizo hakumkumbuka mgonjwa aliyekuwa mahututi. Defao alipachikwa jina la Papaa Defao na wanamuziki wa bendi baada ya kuwa amewatunza mara kwa mara katika nyimbo zao.
Sifa zikaongezeka akapata wapambe.
Kila penye wengi kuna jambo!!!
Na hakuna rafiki mbaya kama rafiki anayepatikana wakati mtu ana pesa.


****



Alidamka asubuhi akajikwatua na vipodozi mbalimbali akiwa mbele ya ‘dressing table', akajigeuza huku na huko akauthaminisha urembo wake, akatabasamu.
Alikuwa amependeza!!!
Honi iliyopigwa ndio ilimkurupua kutoka pale na kuchukua mkoba wake mbio mbio akaanza kwenda nje, alipoifikia gari aliifuata ‘side mirror' ya upande wa kulia mwa gari akautazama uso wake ambao ametoka kuuangalia sekunde chache mbele ya kioo kikubwa.
"Mh!! Wasichana mna mambo?? Sasa huko ndani hujakiona kioo au" alizungumza kwa utani mwanaume huyu huku akiungurumisha injini ya gari yake, msichana huyu akajibu kwa kucheka huku akiweka sawa papi za mdomo wake kwa kuziumauma.
Baada ya hapo mwanaume huyu aliyekuwa amejiwekea hifadhi yake ndani ya suti nyeusi iliyokuwa ya hadhi ya juu alimfungulia mlango binti akajitosa ndani ya gari na kuubamiza mlango ukawa umejifunga.
Kabla yule binti hajafika marashi ya yule mwanaume yalitawala ndani ya gari lakini kufika kwa yule binti kulivunja utawala wake, utuli wa yule binti ukachukua nafasi. Geti likafunguliwa John Mapulu akawasha gari, ilikuwa ni safari ya kumpeleka Joyce Keto kliniki ambayo aliamua amuandikishe hospitali ya Agha Khan ya jijini Mwanza kwani huduma zake zilikuwa nzuri sana tofauti na hospitali za serikali.
Zoezi hilo liliwachukua muda wa nusu saa baada ya kufika. Joyce akapewa ratiba ya kuwa anahudhuria kliniki. John akaahidi kuwa anamleta kila siku iliyopo kwenye ratiba. Joyce akashukuru wakarejea nyumbani.
Wazo la Joyce kuwatafuta ndugu zake halikuwepo hata kwa mbali, sumu aliyokuwa amepandikiziwa na John ilikuwa imeathiri akili yake na kujihisi hapo alipo ndio mikono salama zaidi na si kwingine.
"Mh!! Mhehe ajiua, hawa nao kwa kutuandama!!!" alisema Joyce wakati huo gari ipo kwenye foleni, baada ya muuza magazeti kupitisha katika dirisha lililokuwa upande wake.
"Hah!! Kumbe muhehe wewe mh!!" aliuliza John, Joyce hakujibu!!!
Alitoa noti ya shilingi elfu tano, muuza magazeti hakuwa na chenji hiyo, na John naye hakuwa na pesa ndogo, mataa yakawa yameruhusu gari likaondoka.
Joyce hakufanikiwa kununua gazeti lile, alitegemea atanunua mbele ya safari, akasahau hadi wakafika nyumbani.
John akamuaga Joyce wakaahidiana kuonana jioni!!
Laiti kama angefanikiwa kuisoma habari iliyokuwa kwenye gazeti basi angetambua kifo cha mama yake mzazi katika harakati za kumwokoa.


*****


Penzi alilopewa Adrian na Matha kwa mara ya pili lilikuwa bora kuliko lile la kwanza alisahau kabisa suala la ndoa yake na Monica, akawa ameamua kujizatiti kwa mpenzi wake huyu wa zamani hizo.
Na ili ampate ilikuwa lazima na yeye amdhulumu John Mapulu. Atamdhulumu vipi?? Hilo ndio lilikuwa swali gumu.
Nina pesa!!! Pesa ndio kila kitu!!! Nitamrejesha Matha kwangu. Alipata muafaka Adrian. Wakati huo alikuwa amerejea nyumbani kwake baada ya polisi kuwa wamekamilisha upelelezi wao dhaifu kama kawaida na siku hiyo hakuwa ameenda kazini kwani msaidizi alikuwa ametangulia tayari.
Hatia ya kumsababishia Monica kubakwa ilikuwa imesahaulika, sasa alikuwa anaingia katika jaribio la kurejesha kile kilicho bora kwake.
Adrian akafikiria kutumia pesa aliyokuwanayo kumpa John onyo, kumpa maumivu makali kama ambayo aliyapata yeye baada ya John kumpokonya tonge mdomoni. Hasira ikamsababishia kukihesabu alichotaka kukifanya kuwa kisasi halali.
Akanyanyua simu yake akapiga namba fulani simu ikapokelewa.
"Za siku kaka!!!"
"Poa ndugu yangu, nina shida kidogo"
"Nini tena??"
"Namuhitaji Nunda"
"Kuna mshenzi gani amekusumbua??"
"Yupo mpuuzi nahitaji kumpa somo!!!"
"Tuonane mchana dukani kwako"

Adrian alikubali na kukata simu, akasimama na kuongoza mwili wake bafuni, akaoga kisha akajiandaa akaelekea Makoroboi kwa usafiri wa daladala.
Mida ya mchana akafika rafiki yake wa shule ya msingi aliyeitwa Mark ambaye aliacha shule kitambo na kujiingiza katika vitendo vya kihuni. Alikuwa ameambatana na mwenzake.
Adrian alitoa maelekezo yote, akaeleweka, kisha akawatajia jina la muhusika kuwa ni John Mapulu.
"Nahitaji apigwe na apewe onyo la kuachana na mke wake!!"
"Laki tano unusu!!" alitaja bei
Adrian akakubaliana nayo akatanguliza nusu.
Akawa ameingia rasmi katika vita ya kumgombea Matha!!!! Msichana aliyeamini kuwa aliumbwa kwa ajili yake.

****

Baada ya siku mbili Adrian alipigiwa simu na Mark kuwa mambo yanakaribia kuiva hivyo wanatakiwa kukutana kwa ajili ya makubaliano ya mwisho baada ya utafiti.
Adrian alijiona mshindi katika vita hii, akaacha shughuli zake na kufuata maelekezo, walikutana maeneo ya Nata, Adrian akaelezwa kwamba alitakiwa akutane na Nunda mwenyewe ili aweke kiapo cha siri. Adrian hakusita akakubali, hamu yake ilikuwa kumuona Matha akiwa huru ili aweze kumtambulisha kwa wazazi wake badala ya Monica.
Walipanda daladala zinazoelekea Nyakato Sokoni ndani ya jiji la Mwanza, kila mtu alikuwa kimya hadi pale abiria mmoja aliposhtuka na kupiga kelele kuwa ameibiwa simu yake. Alikuwa ni mwanamama aliyekuwa na heshima zake kabisa kila mtu alimuamini, na jambo la kushtua zaidi ni pale walipojaribu kuipiga namba yake ikaita mara moja na kisha simu ikazimwa.
"Sikubali mimi simu ya mume wangu jamani halafu mwizi yupo hapa hapa ndani sikubaliiiiii…." Alilia kwa uchungu yule mama kila mmoja akawa anamuonea huruma.
"Dereva ingiza gari kituoni huu ushakuwa ujinga sasa!!! Mnawachekea sana na mnawajua" abiria mmoja aliyekuwa kimya muda mrefu alitoa tamko hilo, akaungwa mkono na wengi, taratibu daladala ikakata kushoto ikaingia kituo cha polisi maeneo ya mabatini. Abiria wasiokuwa na hatia walilalamika sana kupotezewa muda lakini je utajuaje huyu ana hatia na huyu yu salama.
Gari lilipofika pale alishuka dereva peke yake, akaenda mapokezi na kutoa shtaka hilo, askari wawili wa kiume na watatu wa kike walipewa jukumu hilo la kukagua kila mmoja ili simu iweze kupatikana.
Mark hakuwa na wasiwasi alikuwa akizungumza na Adrian kwa sauti za kunong'oneza, wote walikuwa na furaha.
Askari aliamuru abiria wote kutelemka, likaanza kusachiwa gari, hakikupatikana kitu, baadaye abiria mmoja baada ya mwingine, wasichana kwa askari wa kike na wanaume kwa askari wa kiume. Zoezi halikuwa gumu sana kwani wengi wao hawakuwa na vifurushi. Na waliokuwa na vifurushi hawakuwa na dalili ya kuwa wezi wa hiyo simu, ndio hivyo alivyochukuliwa Adrian, kati ya abiria waliokuwa nadhifu basi alikuwa ameongoza. Kuanzia juu mpaka chini alikuwa anashawishi macho kumtazama.
Kifurushi chake kidogo kilipekuliwa kwa wepesi. Askari hakuamini alichokiona, yeye pamoja na mwenzake wakajikuta wakihamaki, kutoka katika begi dogo la Adrian tofauti na uwepo wa pesa kulikuwa na risasi nne. Adrian hakuwa akiifahamu risasi ilivyo hivyo alibaki kutabasamu tu, harakaharaka akashangaa amerukiwa na askari mmoja akamnasa vibao halafu akamtia pingu mikono ikiwa kwa nyuma.
Abiria waliruhusiwa kuondoka.
Simu ilikuwa haijaonekana.
Mark kama vile hamjui Adrian na yeye alitoweka!!
Adrian matatani!!!

Adrian aliingizwa katika chumba cha mahabusu akiwa haelewi nini kinachoendelea, safari yake aliyotegemea ya kwenda kumkomoa John Mapulu sasa ilikuwa imemgeukia yeye. Wasiwasi ukamtawala, ilikuwa mara yake ya pili kuingia katika mahabusu tena mara ya kwanza ilikuwa utotoni ambapo walikamatwa siku ya mkesha wa sikukuu ya krismasi wakiwa wanazurura. Hapo ilikuwa baada ya kuwa wametoroka kanisani.
Asubuhi waliruhusiwa kurejea makwao. Hapakuwa na kesi na wala hawakupigwa makofi kama aliyokumbana nayo hapa.
Wasiwasi ukazidi nguvu ushujaa wake, akafadhaika!!!
Baadaye sana aliruhusiwa kupiga simu nyumbani kwao. Mzee Mhina akaipokea, akapewa taarifa, kama kawaida akawa mbinafsi hakumshirikisha mke wake japo alipaliwa na mate baada ya kupewa taarifa hiyo. Hakuyapenda mambo ya polisi kwani aliutambua usumbufu uliopo kule.
Hakutaka kuendesha gari yake binafsi bali alipanda taksi hadi akafika pale kituoni.
"Bunduki ya mwanao ipo wapi" askari mpelelezi wa kesi hiyo alimuuliza mzee Mhina wakati akijiweka sawa katika kiti kilichokuwa katika moja ya ofisi.
"Bunduki!!! Bunduki gani" alihoji huku akishindwa kukaa vyema, alikuwa amekumbwa na mshawasha. Askari hakujibu lolote aliendelea kupeleleza mafaili yake huku na huko, na kupiga mluzi ambao haukuwa wa nyimbo yoyote ile bila shaka alikuwa ameutunga ghafla ili kumburudisha Mhina.
"Kwani mwanangu amekamatwa kwa kosa gani??"
"Jambazi!!"
"Jambazi nani Adrian??" alihamaki. Askari hakujibu akakaa na faili mkononi akamkazia macho mzee Mhina kisha akajilazimisha kutabasamu.
"Jambazi mwanao ilete hiyo bunduki tumalizane!!" alirudia maelezo yale askari huyu ambae alijulikana kwa jina la Moa. Baada ya kuhamaki sana na kulalamika kuwa hatendewi haki zake za msingi kama mzazi wa mtuhumiwa, Moa alisarenda akamueleza kinagaubaga kila kitu kilivyokuwa na baadaye akaitwa Adrian.
Alikuwa peku peku, suruali kiunoni ilipakataa na shingo yake ilikuwa imerefuka, kwa masaa kadhaa Adrian alikuwa amekonda!!
Hakukumbuka kumsalimia baba yake kutokana na hali iliyokuwepo. Aliamriwa kukaa chini kisha akaanza kuulizwa maswali akajieleza kila kitu kilivyokuwa huku akimtaja mara kwa mara Mark!! Lakini hakuisema njama aliyokuwanayo yeye na Mark dhidi ya John Mapulu!!
Baada ya maelezo kuandikwa alirudishwa rumande dhamana ilikuwa haijatimia kimasharti.
Kwa siku nyingine akawa amelazwa tena mahabusu.
Siku iliyofuata ilikuwa jumamosi, mpelelezi wa kesi alikuwa na udhuru hakuja kazini, na siku ya jumapili si kawaida yake kuja kazini.
Adrian akawa amesalia ndani ya kachumba kadogo ka mahabusu hadi siku ya jumatatu ambapo dhamana ilipitishwa akawa huru.
Hewa ya uhuru iliyeyusha hofu aliyokuwanayo, japokuwa alinuka sana hakujali alifurahia kuwa huru.
"Usimweleze mama yako chochote!!!" baba alimwambia mwana, lilikuwa neno la kwanza tangu awe huru!!!
Adrian alijibu kwa kutikisa kichwa juu na chini mara kadhaa. Macho yake yalikuwa yamevimba bila shaka alipigwa kidogo na wakorofi wa jela aliowakuta pale mahabusu. Mzee Mhina akawasha gari wakaelekea nyumbani kwa Adrian.
Baada ya kuoga na kupata chai nzito ya maziwa hatimaye kilikuwa kikao cha dharula.
Baba na mwana!!
Adrian alimueleza baba yake kila kilichotokea lakini hakutaka kuonekana mjinga mbele ya baba yake huyo aliyemuamini sana. Hakudiriki kumtaja John wala Matha katika mlolongo wa maelezo yake.
"Una uhakika kuwa hujui lolote kuhusu zile risasi"
"Nikwambie mara ngapi baba??" alihamanika Adrian, mzee Mhina akashusha pumzi kwa nguvu zote kisha akajiegemeza kichwa chake katika sofa.
"Nitamalizana na yule mpelelezi japo anahitaji pesa ndefu sana kinyume na hapo ni mahakamani kisha hukumu kwenda jela" Adrian akapaliwa na chai aliyokuwa anaifurahia ladha yake mdomoni!!! Alikohoa sana kabla ya kukaa sawa.
"Baba mpe hizo pesa mambo ya mahakamani tena aah!!" alilalamika Adrian. Mzee Mhina hakujibu kitu akawa ameaga na kuondoka!!
Adrian hakuendelea tena kunywa chai, akaingia chumbani akajifungia na kuanza kumlaani Mark kwa kitendo cha kinyama alichokuwa amemfanyia.
Ina maana alitaka nikafie huko huyu jamaa!!! Alijiuliza huku akikifinyafinya kitanda chake kwa kutumia makucha yake yasiyokuwa na urefu wa kutisha.
Alilaani kwa kila namna na mwishowe fikra za ajabu ajabu zikaanza kumvaa akamwona Mark kama mnyama tena mnyama wa kutisha aliyefanya mbinu ili ammeze bila taarifa, mnyama asiyekuwa wa kufugwa, alimfikiria amfananishe na simba akagundua ni yeye alikuwa akiitwa simba na baba yake. Akaona jina lake haliwezi kufanana wala kutumiwa na mtu kama Mark.
Mwishowe akaamua kumfananisha na JITU. Jitu lisilokuwa na utu, jitu ambalo linaipoteza amani kama ukilichekea lakini mwisho wa jitu ni kutumia makali ya upanga.
Adrian akawa amejawa na fikra za kumteketeza Mark ambaye alikuwa amepewa jina la JITU.
Wakati huo Matha alikuwa amesahaulika kidogo na John hakuwa kwenye fikra zake.


*****

John baada ya kuachana na Joyce tu, wazo lisilompendeza kabisa lilirejea kichwani mwake, wazo juu ya Adrian Mhina lilimkaba koo. Akasogeza gari pembeni ya barabara akazimisha, akatoa sigara katika koti lake akaipiga kiberiti na kuanza kupuliza moshi hewani kwa fujo, alikuwa anajaribu kukabiliana na ghadhabu iliyokuwa inachukua nafasi yake kwa kasi.
Uso wa furaha aliokuwanao wakati yupo na Joyce ulikuwa umepotea, chuki ikachukua nafasi.
John Mapulu akataharuki!!!
Namuua huyu (……!`~) akamtukania mama yake!!!

John alikuwa katika hasira zilizomaanisha alikuwa ameamua kumpotezea mbali Adrian kwa jambo alilohisi anafanyiwa naye. Hakuwa mtu wa kuweka ahadi asiyoitimiza.
Alifanya mikakati yake na kamati yake ndogo. Aliamini kuwa Adrian hakuwa na haki ya kuyaonja mauti bali alitakiwa atikisike kwanza na iwapo ataleta ubishi ndipo iwe adhabu ya mwisho.
Kwa kumtumia mama mtu mzima aliyekuwa anafanya shughuli za ukahaba pale mjini Mwanza John aliweza kuufanikisha mtego aliopanga kuuweka na aliamini kuwa utanasa.
Kijana wa kazi Joram alikuwa kazini na mama huyu, walimfatilia Adrian siku hii kwa kila hatua aliyokuwa anaenda moja baada ya nyingine. Walimshuhudia tangu alipotoka nyumbani kwake na kuelekea hadi Nata ambapo walipanda daladala, ni katika mlolongo huo huo Joram alicheza kamchezo kadogo sana kakumzongazonga Adrian kisha kutumbukiza risasi tatu katika mkoba wake uliokuwa umeachia uwazi kidogo.
Baada ya zoezi hilo ilikuwa zamu ya mama wa mjini kufanya maigizo ya kuibiwa simu, igizo lake likapata mashabiki wengi, gari ikaamuliwa kuingia kituoni.
Adrian akawa ameingizwa hatiani!!!
John akaendelea kuwa mshindi.
Lawama zote zikamwangukia Mark.

Mark alishindwa kabisa kuelewa ni namna gani Adrian atamchukulia kutokana na tatizo lililokuwa mbele yake, lakini katikati ya mawazo akaanza kumuogopa Adrian akiamini kuwa ni mtu hatari sana kwake.
Anamiliki bunduki!!! Hatari sana mtu huyu, alitaka kuniua au kumteka Nunda?? Mbona kizungumkuti!!! Alijiuliza Mark. Kisha akawasha redio kwa sauti ya juu kidogo ili iingilie kati mawazo yake yaliyomzonga kichwani. Haikuwezekana, akainuka na kutoka katika chumba chake akaenda katika baa iliyokuwa jirani akaagiza na kuanza kunywa moja baada ya nyingine.
Lazima nifanye kitu hapa kabla ya hatari!!!


***ADRIAN anahisi kuwa MARK ni mtu mbaya kwake...MARK naye anahisi ADRIAN ni mtu hatari anayemiliki Bunduki...wote hawajui kama kuna kichwa chenye jina la JOHN MAPULU katika mkasa huu......
****Mimba ya Matha bado ipo katika riwaya hii ya HATIA ....kumbuka ni mimba hiyo imeyaleta yote haya.....nini hatma yake.....NA VIPI YULE MCHUNGAJI FEKI?????

Mr Rocky NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila
 
Last edited by a moderator:
john mapulu anaakili kama mbwa wa police lakini kashidwa kumkamata michael...
 
Casuits shusha madini kwa sana escrow ishazimwa kiintelijensia. Weka madini tujipoze
 
yani akishindwa kabisa kumkamata michael nafunga safari hadi Mwanza kumueleza ukweli.. lol

ohoooooo...unaitafuta hatia ya pili..asije kata kichwa chako akatembea nacho mfukoni kama pochi bule...au laa uangukiw kwenye mikono yakina joram mbona utachezea kichapo usahau mpaka jinsia shauli yako..mim sitaki kuwa shaidi.
 
ohoooooo...unaitafuta hatia ya pili..asije kata kichwa chako akatembea nacho mfukoni kama pochi bule...au laa uangukiw kwenye mikono yakina joram mbona utachezea kichapo usahau mpaka jinsia shauli yako..mim sitaki kuwa shaidi.

aisee.. siendi tena mana nimeghairi
 
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA KUMI NA NANE


Mark alishindwa kabisa kuelewa ni namna gani Adrian atamchukulia kutokana na tatizo lililokuwa mbele yake, lakini katikati ya mawazo akaanza kumuogopa Adrian akiamini kuwa ni mtu hatari sana kwake.
Anamiliki bunduki!!! Hatari sana mtu huyu, alitaka kuniua au kumteka Nunda?? Mbona kizungumkuti!!! Alijiuliza Mark. Kisha akawasha redio kwa sauti ya juu kidogo ili iingilie kati mawazo yake yaliyomzonga kichwani. Haikuwezekana, akainuka na kutoka katika chumba chake akaenda katika baa iliyokuwa jirani akaagiza na kuanza kunywa moja baada ya nyingine.
Lazima nifanye kitu hapa kabla ya hatari!!!


*****


Defao alizidi kujisahau na kujilinganisha na wafanyabiashara wenye majina makubwa jijini Mwanza, alikuwa hashikiki alitamani kuzimaliza kumbi zote za starehe na pia wanawake wote aliona kuwa ni haki yake kuwamiliki si mke wa mtu ama machangudoa wote alikuwa anawamezea mate na kisha mwisho wa siku alikuwa anatumia pesa zake na kuwapata.
Alikuwa na wapambe wengi sana ambao walimuheshimu kutokana na pesa aliyokuwanayo, pesa iliyomsahaulisha kuhusu mgonjwa aliyemuacha nyumbani, pesa iliyomfanya amsahau kabisa Minja ambaye ndiye alikuwa amemchorea dili hilo!!!
Defao akawa mwingine kabisa!!!!
Defao akawa Defao kweli!!!
Defao akiwa katika chumba cha kulala akiwa amesaliwa na takribani milioni moja na nusu alijikuta katika dimbwi zito sana la mawazo kumbukumbu mfululizo zikawa zinapita kichwani mwake baada ya kuwa ameangalia filamu katika luninga iliyokuwa imepachikwa katika ukuta wa chumba alichokuwa analala, filamu hiyo iliyoigizwa na masanii mashuhuri nchini Tanzania ilikuwa inazungumzia mapenzi bora lakini yanayoingia doa baada ya binti kupata ujauzito, ujauzito unakuwa karaha kwa mwanaume anaamua kuukataa. Aliukataa kwa sababu ya maisha yake magumu hakuwa anaweza kumuhudumia mtoto na mama yake.


Defao akajikuta kwa mara ya kwanza anamkumbuka Joyce Keto, akakumbuka jinsi alivyombaka kisha akakimbia na kujificha. Akajutia nafsi yake akajiona yu hatiani. Nafsi ikamsuta akajihisi yupo dhambini, akawa amefikiria kutubu dhambi yake, dhambi iliyotiwa chachu na tabia zake za kubadili wasichana jijini Mwanza, akafikiria pia kutubu kwa Minja.
Defao akawa ameamua kurejea mjini Singida. Aliamini kwa kiasi alichonacho Minja atamuelewa japo atalaumu sana. Pesa hiyo itatumika kiasi fulani kwa ajili ya matibabu ya mgonjwa. Je itatosha?? Hilo ndio likawa swali. Ghafla alipojiuliza hivyo akamkumbuka John Mapulu, akatamani kumwendea tena ili kudai kiasi kingine cha pesa.
Defao akamchukulia John kuwa ni ----- asiyejitambua katika mapenzi, akamdharau sana kwa kudanganywa na mpenzi wake halafu akamcheka kwa kuwa mwepesi sana kutoa milioni kadhaa kumshukuru yeye kwa kumuibia siri juu ya mkewe.
Akamsikitikia sana kwa kuwa John hakuwa na uwezo wa kuzaa, aliinama chini kisha akajisemea huu ndio wakati muafaka wa kuvuna tena kutoka kwa John!! Nitavuna kwa kuutumia udhaifu wake. Siri yake ya uhanithi itanipatia pesa zaidi ya hizi.
Siendi Singida kwanza!!! Alifikia maamuzi ambayo aliyaona kuwa ni sahihi.
Defao akawa ameamua kumfuata tena John Mapulu!!!
Akapitiwa na usingizi akiwa na maamuzi hayo.




*****


"Puuuuu" gari aliyokuwa anaendesha Joyce Keto ilipitia bonde katika njia iliyokuwa ya kushangaza, bonde lile lilikuwa wazi sana.
John akashangazwa sana na hali hiyo, Joyce alikuwa amefanya kosa kwa kukosa umakini barabarani, japo hakuwa na leseni ya kuendesha gari lakini alikuwa na uwezo mzuri wa kuendesha. Cha kushangaza tukio hilo Joyce alikuwa hajalitilia maanani, alionekana kuwa na hofu iliyojaa tele usoni mwake. Aliendesha gari kidogo kisha akaipaki.
"Vipi Joyce!!!" John alimuuliza.
"Mh!! Yule kama nani yule mh!!! Ila sio yeye" Hakueleweka alichokuwa akiongea Joyce, John akabaki anashangaa.
Ilikuwa ni siku yao ya saba kwenda kliniki na siku hiyo Joyce aliendesha kuanzia safari ya kwenda na kurudi kwa uangalifu mkubwa kama kawaida yake lakini hapa palipokuwa wazi kabisa amefanya kosa ambalo John Mapulu alibaki kulishangaa.
Joyce aliamini kile alichokiona kisha akaikataa imani yake!!! Hakuamini kama ni kweli.
Baada ya dakika kadhaa Joyce aliondoa gari hadi wakafika nyumbani!!
"Bosi kuna kijana amekuja kukutafuta anasema unamfahamu!!!"
"Anaitwa nani?" John aliuliza huku akishusha kioo vizuri.
"Amesema unayo namba yake lakini kama umeipoteza yeye anaitwa….nani…nani…Mafao sijui" mlinzi akawa amesahau jina la mgeni wa John. Joyce akacheka kusikia jina hilo, John naye akatabasamu akaitwaa namba akaingiza kwenye simu yake. Haikuwa imehifadhiwa hapo kabla akaihifadhi kwa jina la Mafao huku akitabasamu!!!
Wakaingia ndani!!
Huyo Mafao alikuwa ni Defao alikuwa amemfuata John nyumbani kwake badala ya kupiga namba yake , siku hii alikuwa amependeza sana na alifikia hatua ya kujilinganisha na John mwenyewe na pengine kumzidi.
Hakumkuta akawa ameacha maagizo pamoja na namba za simu.
Wakati anarejea mjini ndipo alipishana na gari ambayo ilikuwa imewapakia John na Joyce, Joyce akawa amemfananisha Defao, lakini hakuwa na uhakika kama alikuwa sawa ama la, ni wakati huo ambao alichengana na mahesabu ya kupunguza mwendo ili aweze kulivuka bonde.
Defao hakulitilia gari hilo maanani yoyote akaendelea na shughuli zake.
Alikuwa anasubiri simu kutoka kwa John!!!
Kama kawaida akaingia katika baa mojawapo jijini Mwanza akaanza kupata moja baridi moja moto.


Defao alipochangamshwa na zile pombe alizokuwa amegida kwa fujo kidogo, aliitazama simu yake hakuna mtu yeyote aliyekuwa amepiga simu.
Dharau!!!! Akawaza Defao, kisha akabonyeza tena namba za simu alizoamini kabisa kuwa zilikuwa za John, John Mapulu, hazikuwa zinapatikana kama awali. Akawaza kurejea tena nyumbani kwa John lakini akaionya nafsi yake kwani ni kama alikuwa anaharakia sana mambo kuliko kuituliza akili yake na kuisuka mipango yake taratibu.
Defao akajenga tabasamu lilioonyesha kukereka, akanyanyua chupa ya bia aliyokuwa anapiga katika mfumo wa tarumbeta. Akaipeleka mdomoni lakini akagundua kuwa ilikuwa imemalizika, akairejesha chupa kwa kasi ikakutana na meza ya mbao ikatoa mlio ulioshtua wachache. Akatazama kushoto na kulia akasimama na kuzinyanyua hatua zake kuuelekea mlango ulipo. Akawa ametoka nje.
Hakuwa na pakwenda ambapo ni rasmi!!!
Akaamua kurejea nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amefikia!!!!




*****




Nia ya Matha ilikuwa kuuondoa uhai wa Joram ili amuepushie zogo la kuwa anamtumia kimwili bila mkataba maalum wa lini mchezo huo mchafu utafikia kikomo. Joram alikuwa ameiongeza idadi ya wanaume wanaoufaidi mwili wa Matha kutokea kuwa watatu na sasa walikuwa wanne, Joram alikuwa amejihalalisha kuungana na Michael, John Mapulu na Adrian Mhina.
Matha akawa anamtazama Joram katika hali ya tofauti kabisa, alimchukulia kama mdhalilishaji, asiyekuwa na utu hata kidogo. Matha alikuwa anaamini asilimia zote kuwa Joram alikuwa ameshikilia mpini na yeye alikuwa upande wa makali. Joram alikuwa na silaha kubwa sana silaha ya siri!!! Jambo hilo lilimuumiza sana Matha ambaye hakutaka kuwa mtumiwaji kiasi hicho. Matha alikuwa anamzidi karibia kila kitu Joram, nguvu, cheo, ujanja na hata pesa. Tatizo lilikuwa moja tu!!! Siri!!
Matha akawa ameamua kuua
Kumuua Joram!!!
Lakini wazo la kuua likawa mtihani mgumu sana.
"Nitakuwa sijamkomoa kwa jambo analonifanyia kumuua ni adhabu nyepesi sana, atakufa mara moja……hapana lazima na yeye aumie" alibadili maamuzi Matha.
Wazo lake likawa kumkomoa Joram.
Akapiga akili kidogo tu akapata jawabu na hakutaka kupoteza muda sana kwani siku hii Joram alikuwa anahitaji penzi la Matha tena katika nyumba ya kulala wageni.
Matha alifika kwa wakati eneo husika akiwa amevalia kama kawaida baibui lake kuweza kujificha kwa watu kisha alipofika chumbani aliliondoa na kusalia na nguo zenye kupendeza machoni hasahasa chumbani. Joram alimkumbatia kisha akambwaga kitandani.
"Nina kiu Joram!!!" alisema Matha huku akiviondoa viatu vyake miguuni.
"Nimeagiza chakula bila shaka muda si mrefu kitafika na maji pia nimeagiza. Alijibu Joram!!
Baada ya dakika kadhaa mlango uligongwa, Joram akaenda kupokea chakula hicho.
Matha akafakamia maji na kuyagida ipasavyo, Joram alitoka na kwenda kunawa mikono bafuni alitaka ale ashibe kwanza kabla ya kumnyanyasa Matha kijinsia.
Alipotoka kwenda kunawa mikono ilikuwa nafasi ya kipekee kwa Matha alizama katika pochi yake akatoa unga mfano wa ndimu ya kusagwa akamimina katika chakula cha Joram.
Bila wasiwasi wowote Joram aliporejea alichukua chakula kile na kutaka kumlisha Matha.
"Mi siwezi bwana nimeshiba sana maji!!!" alikataa Matha. Joram akamuelewa akatupia pande lile la nyama mdomoni kwake.
Matha akaanza kumuhesabia dakika, zilipofika tatu chambo katika ndoano ikaanza kuliwa na samaki.
Matha akaanza kuhisi dalili za ushindi!! Ungaunga wa ‘doromee' ukaanza kutenda kazi katika mwili wa Joram, Joram akalainika na kisha kuangukia kitandani.
Ni wakati huo Matha alitoa taarifa kwa timu yake aliyokuwa ameiandaa kwa kazi moja tu kumuadabisha Joram bila kumuondoa uhai!!!!
Shughuli ikaenda kama alivyopanga.
Baada ya siku mbili jiji likatawaliwa na taarifa juu ya kulawitiwa kwa Joram!!!!!
Ilikuwa ni taarifa iliyotapakaa sana jijini Mwanza kuhusu kulawitiwa kwa kijana mtanashati na mwenye nguvu. Taarifa hiyo ilisambaa upesi kutokana na mazingira ambayo muhusika alikutwa, ni jirani na mabweni ya shule ya sekondari!!!
Joram alikutwa humo akiwa hajitambui kabisa, alikuwa yu uchi wa mnyama na pembeni yake palikuwa na pakiti za kondom zilizokwishatumika tayari. Wanafunzi makundi kwa makundi walizisambaza habari hizo katika hali ya ucheshi na wengine katika hali ya majonzi.
Joram alichukuliwa na kupelekwa hospitali ambapo aligundulika kupewa madawa makali ya usingizi yenye athari kwa muda wa masaa ishirini na nne.
Daktari baada ya kumpima aligundua kuwa hakuwa ameingiliwa kimwili yaani hakuwa amelawitiwa.
Nguvu ya sauti ya daktari haikutosha kuwashawishi walioshuhudia tukio hili hivyo vyombo vya habari vikachukua ya daktari na wananchi wakibaki na mawazo yao ambayo kwa nafasi kubwa yalichukuliwa kuwa ni ukweli!!!




******




Ilikuwa ni taarifa ambayo ilipokelewa kwa shangwe zote na Matha. Aliamini kwa skendo hiyo lazima Joram asalimu amri kwa mambo aliyokuwa anamfanyia.
Ilikuwa kama alivyokuwa anafikiria, Joram alipozinduka na kupewa taarifa hizo za udhalilishaji alijidai kuwa hazijamshtua kumbe kichwani mwake alikuwa amechukua maamuzi mazito tayari.
Joram akiwa na hatia yake moyoni hatia iliyoambatana na siri nzito juu ya John Mapulu na mpenzi wake Matha, alinyata usiku wa manane kutoka katika hospitali ya rufaa ya Bugando. Akatoroka kama vile anarejea baada ya muda mfupi.
Haikuwa muda mfupi Joram akatoweka moja kwa moja bila kumuaga John wala Matha.
Baada ya utafiti wa siku kadhaa taarifa kutoka hospitali zilikiri kuwa Joram ametoroka na haijulikani alipo. Taarifa hizo zilidumu kwa wiki kadhaa hadi pale jeshi la polisi wilaya ya Magu jijini Mwanza lilipotangaza kupatikana kwa mwili wa Joram ukiwa umeshambuliwa na wanyama lakini baada ya utafiti ilifahamika kuwa Joram alikufa kwa kunywa sumu.
Hatimaye simulizi tamu ya kusisimua juu ya Joram ikawa imeishia hapo, Joram akawa ameiaga dunia.
Matha aliipokea taarifa hii kupitia kwa mpenzi wake (John Mapulu). Usoni alisikitika huku moyoni akicheka, kicheko kikubwa sana kicheko cha ushindi. Ushindi wa chee!!
Matha alikuwa amemuua Joram kiwepesi kabisa.
Kifo cha kizembe!!!! Ni tafsiri aliyoifanya Matha.
Hakika Joram aliuwawa kizembe.
Matha akasalia na John, Michael na Adrian, huku tumbo lake likimkumbusha kuwa kuna kiumbe mwingine, kiumbe hatarishi zaidi anayetegemewa kuleta zogo kubwa zaidi.
Mimba!!!!!






******




Jambo ambalo mzee Keto hakutaka kulichukulia wepesi ni kifo cha mkewe mpenzi mama Joyce aliyezaliwa na kuitwa Mariana.
Kujinyonga??? Hapana haiwezekani!! Alikataa kuamini kuwa mkewe aliweza kujinyonga kiwepesi kiasi hicho, hawakuwa wamegombana katika siku za karibuni wala watoto wao hawakuwa wamewakera.
Alijaribu kuvuta kumbukumbu ya mazungumzo ya mwisho kati yake na mkewe, yote yalikuwa mazuri yaliyotawaliwa na upendo na amani tele. Hakupata kumbukumbu yoyote ile ya makwazo kati yao. Ndiyo Mariana alikuwa ni kutoka kabila la wahehe lakini hiyo haikuwa sababu tosha ya yeye kujiua.
Ujumbe ujumbe ujumbe!!!! Akili yake ikakumbuka ujumbe alioucha Mariana. Ujumbe uliochukuliwa na askari. Akili ikapata ahueni ya kupata jawabu, akasimama wima akajisachi na kujikuta na senti kadhaa zilizokuwa zinatosha kwa nauli ya kumfikisha kituo cha polisi. Aliwapita watoto wake pamoja na watu wengine waliokuwa wamehudhuria msiba huo.
Aliwasili kituo cha polisi Magomeni, na moja kwa moja akafikishwa kwa mpelelezi wa kesi yake hiyo isiyokuwa na mtuhumiwa.
"Kuna ule ujumbe ningependa kuuona huenda una msaada wowote"
"Sidhani maana una mafumbo matupu" alijibu yule mpelelezi huku akimpatia kikaratasi kilichokuwa na ujumbe.
"Nimedhalilishwa nikiwa katika harakati za kumtafuta mwanetu bora nife!!!" aliyakariri maneno yale kwa sauti ya chini kama mara tatu huku akikiweka mezani kile kikaratasi.
"Kweli hakuna maana yoyote!!!" aliunga mkono hoja, wakazungumza mawili matatu mzee Keto akaaga na kuondoka zake.
Alifika na kujilaza kitandani, alikuwa amedhoofika sana na hakutaka kuzungumza na mtu yeyote. Akilini bado alikuwa anaimba ule wimbo aliousoma katika kile kikaratasi. Mara katikati ya wimbo akaikumbuka siku ambayo mkewe alishawishika kumtafuta mtoto wao kupitia katika imani za maombi ya kidini. Hapo hapo kama radi akamkumbuka mchungaji JK, alimkumbuka kwa kuwa alitangazwa sana katika magazeti mbalimbali ya jijini Dar es salaam. Kama vile ameshtuka kutoka katika ndoto ya kutisha Mzee Keto alisimama na kukaa kitako.
Akachukua simu yake akataka kupiga lakini akagundua aliyetaka kumpigia yupo hapo hapo msibani.
Alikuwa ni mama yake mdogo na marehemu mke wake. Ni huyo ndiye aliaga anaenda kwake kwa mara ya mwisho.
"Huyu mwanamke alimfanya nini mke wangu!!!" alijiuliza mzee Keto. Hakutaka kuisumbua akili yake zaidi akasimama wima akatoka nje akasogea hadi jirani na yalipokuwa makundi ya kinamama. Akanyoosha mkono wake kisha akavikunja viganja mara kadhaa kumaanisha kuwa anamuita mtu, muhusika aliiona ishara hiyo akajinyooshea kidole kama ni yeye anaitwa, mzee Keto akatikisa kichwa kwamba hajakosea. Yule mwanamke akaacha kazi ya kuchagua mchele aliyokuwa anaifanya akajifuta mikono yake, akatafuta viatu vyake hakuviona akaamua kutembea pekupeku kumfuata mzee Keto, watu waliacha kufanya mambo yao wakaanza kumsindikiza mama yule kwa macho hadi alipomfikia mzee Keto.
"Shkamoo mama!!!" alisalimia kikabila Mzee Keto
"Marahaba!!" alijibiwa.
"Samahani sana mama, Mariana alipokuja kwako mligombana chochote!! Na alifuata nini kwako usiku ule??" aliuliza kwa kujiamini.
"Mimi?? Kwangu?? Lini baba" aliuliza kwa woga kidogo huku akijipiga piga kifuani.
"Mh!! Kwani amekuja lini kwako??" aliuliza kimakosa kwani ni yeye alikuwa ameulizwa hilo swali.
"Tangu mje wote siku ile hajawahi kuja tena kwangu??" alijibu yule mama safari hii kwa sauti tulivu.
"Ina maana alienda wapi sasa?? Mh!! Hebu njoo ndani tuzungumze!!" aliamua kuituliza akili yake Keto.
Mama yake mdogo Mariana akafuata kwa nyuma.
"He baba wapi tena huko??" mama huyu alimshtua Mzee Keto baada ya kugundua kuwa alikuwa anampeleka chumbani kwake. Mzee Keto akashtuka akapatwa na aibu kisha akabadili uelekeo wakaenda sebuleni.
Walizungumza mengi katika hali ya utulivu, Mzee Keto akazidi kufunguka akili yake. Mariana hakuwa amejiua kwa sababu ndogo.
Wamemuua mke wangu!!! Aliwaza






********




Furaha kubwa aliyokuwanayo Matha kwa kumteketeza Joram na ujanja wake katika njia nyepesi kiasi kile, Matha hakuridhika peke yake na ile furaha aliwafikiria Michael na Adrian katika jambo hili. Baada ya kuwa amempigia simu John Mapulu ili awe naye siku hiyo na John kukataa kata kata katika hali ya dharau. Baada ya hapo akawa na maamuzi mapya.
Kwanza alitaka kupiga simu kwa Michael lakini akaghairi kwani alikuwa na safari ya kwenda kuonana na Bruno nyumbani kwa John maeneo ya Mecco, akaamini ataonana na Michael huko huko, kuhusu Adrian ilikuwa ni lazima ampigie simu ili aweze kujua kama wanaweza kuonana ama la.
Alibonyeza namba za Adrian Mhina, simu ikaita haikupokelewa, akapiga tena ikakatwa na alipojaribu kwa mara ya tatu haikuwa inapatikana.
Wivu!!! Akajitupa kitandani kwa nguvu, akaivurugavuruga shuka aliyokuwa ameitandika kitandani. Akatamani kulia machozi yakawa mbali sana, ile hali ya kutaka kulia na kukasirika kwa pamoja ikaifanya sura yake ikawa kama kinyago kilichochongwa kwa maksudi ya kuchekesha.
Akiwa katika hali hiyohiyo mara simu yake ikaita, akawaza aidha ni John Mapulu, ama Adrian Mhina, akaichukua kwa haraka haraka akaitazama alikuwa ni Michael Msombe.
Nini tena na huyu argh!! Akasonya akakata simu. Aliamini atapata kero nyingine tena. Wakati anairudisha ikaita tena, akaipuuzia akiamini kuwa ni Michael tena, ilipokatika ikaita tena, akaiendea kwa lengo la kuizima kabisa akakumbana na namba mpya. Akaitazama akaipokea bila kuongea mpaka upande wa pili ulipoanza kuzungumza. Ilikuwa sauti ngeni kwake.


"Nakayange Mutukula naongea!!!"
" Nani?? Unasemaje??"
"Mke wa John Mapulu!!" uliuliza upande wa pili akasita kujibu Matha badala yake akauliza.
"Kwani vipi??"
"Ningependa sana kuonana na wewe"
"Ili iweje na kwa misingi ipi??" aliuliza kwa kiburi Matha. Upande wa pili haukutetereka.
"Kwa ajili ya ndoa yako"
"Ndoa yangu!!!" alihamanika Matha, sauti yake ikasikika ikianza kutetemeka.
"Lini na wapi??" hatimaye alilegea.
"Kesho mahali tutafahamishana" ilijibu kwa majivuno sauti nzito iliyotulia upande wa pili.
"Umesema unaitwa??"
"Eeeh!! Nakayange Mutukula" alijibiwa.
Simu ikakatwa baada ya utambulisho.
Mfuasi wa Joram, Joram hakufa na siri yangu!!! Alilalamika Matha huku akizungukazunguka chumbani mwake, alikuwa kama anayekaribia kuchanganyikiwa akatazama simu yake kwa hasira kama anayesubiri imjibu kitu. Mshtuko alioupata kwa simu hiyo ulisababisha ajihisi kama amepigwa teke na kitoto kilichoanza kukamilika tumboni. Maumivu matamu yakasikika kisha yakawa makali akakimbilia chooni!!
Mpambano mpya kabisa!!!! Matha majaribuni!!




****NAKAYANGE MUTUKULA ni nani tena???? Na ameijulia wapi siri hii inayomtesa Matha!!!
****JORAM amekufa!! Kumbe hajaondoka na ile SIRI!!!!!.......
****MZEE KETO haamini kama mke wake amekufa hivihiv anahisi kuna namna...je? atafuatilia na kupata jibu!!!!


Mr Rocky NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwiDonatila
 
Utunzi umekaa kiakili mno.
Ila John kaharibu sana akili ya Michael hadi namuhurumia Michael.
 
defao kwisha habari yake.. john mapulu photocopy amekufa sasa anakutana na john mapulu orijino!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom