Riwaya: Hatia

RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA KUMI NA NNE

Injini za gari zilizimwa mbali kidogo na nyumba aliyokuwa anaishi Adrian kwani umati ulikuwa mkubwa sana, Adrian alikuwa anatetemeka sana lakini mzee Mhina ukongwe ulimsaidia aliweza kupambana na presha ile.
"Mungu Wangu sijui kama ni mzima yule" walisikika watu wakizungumza. Adrian aliyasikia hayo, mzee Mhina akawa makini amemshika mkono kwani aliamini kuwa kuna tatizo kubwa ambalo mwanae hawezi kulihimili.
Na kweli hakuwa amewaza vibaya mzee huyu, punde tu baada ya kuuona mwili wa mpenzi wake Monica ukiwa umezungukwa na damu pande zote lakini ukiwa umesitiriwa kwa upande wa kanga Adrian alilegea na kupoteza fahamu palepale. Likaanza zoezi la kumpepea pasipo mafanikio.
Baada ya polisi kumaliza utafiti wao na kutoa PF3 , mwili wa Monica ulipelekwa hospitali kwa kujaribu kuokoa maisha yake. Mzee Mhina alichukua jukumu lote la kusimamia shughuli hii kwani aliamini kuwa mwanae atazinduka baadaye bila wasiwasi wowote.
Hospitali ya Sekoutoure (Seketule) ndiyo ambayo ilisimamia kidete kupambana na Israel asiitwae roho ya Monica. Juhudi zao zilizaa matunda kwani Monica alipata nafuu baada ya kuongezewa maji na damu mwilini huku akipumua kwa kutumia mtambo maalumu wenye hewa safi ya oksijeni.
Mzee Mhina alikuwa makini sana na jambo hili, kwa kuwa aliambiwa mgonjwa anaendelea vizuri hakutaka kumfikishia taarifa mkewe alihofia kuvuruga amani nyumbani maana mkewe alikuwa muoga sana.
Saa mbili usiku Monica alikuwa amerejewa na fahamu na alikuwa anapumua bila kutumia msaada wa mashine.
Mzee Mhina alikuwa katika chumba cha daktari ili aweze kupokea maelekezo. Daktari alizungumza mengi ya kumtia moyo mzee Mhina kisha akafikia mahali akamweleza mzee Mhina jambo la kushtua.
"Tunasikitika kwamba mimba yake imetoka"
"Mimba!!! Mimba gani tena??" alihoji mzee
"Mgonjwa alikuwa na mimba changa nadhani ni ya hivi karibuni labda wiki mbili hadi tatu"
Mzee Mhina hakuwa na swali la kuuliza zaidi ya kumshukuru daktari kwa msaada wao mkubwa.
Suala la Monica kuwa na mimba lilimshangaza sana mzee Mhina, kimoyomoyo akaanza kumlaumu Adrian kwa kumficha jambo hilo, alimchukulia kama mbinafsi sana. Aliamini ni yeye alimzuia Monica asimueleze kuhusu hilo.
Ghadhabu ikampanda akaidhibiti kwa kupiga mluzi usiokuwa rasmi.
"Monica mwanangu pole sana ni nini kilitokea" Mhina akamhoji mtoto wake huyo huku akimpapasa kiganja cha mkono wake wa kuume.
"Adrian baba!!!"
"Adrian…amefanyaje??"
"Kwa sasa siwezi kuzungumza" alijibu Monica. Baba akamuelewa!!!!


Adrian alikuwa katika hali ya kawaida baada ya kuwa amepewa muda wa kupumzika kidogo.
Sasa walikuwa, baba yake Adrian, Adrian na wazazi wa Monica. Wote walikuwa pale hospitali kumchukua Monica baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali. Lilikuwa jambo jema kuwa Monica hakuwa ameambukizwa magonjwa ya zinaa.
Adrian alikuwa kimya muda wote akijiuliza ni nini kimemsibu mke wake huyo mtarajiwa.
"Adrian nahitaji mazungumzo na wewe" Monica alimnong'oneza kwa sauti ya chini. Adrian akatikisa kichwa kuashiria kukubali.
Mzee Mhina alikuwa makini na usukani huku nyuma gari ya baba yake Monica ikifuata. Safari hii iliishia nyumbani kwa akina Monica, Adrian alimkokota Monica hadi chumbani kwake. Hapo ndipo walikuwa huru kuzungumza.
"Ulilala wapi Adrian" swali likatua katika kichwa cha Adrian, alikuwa hajajiandaa kujibu akaulizwa jingine tena, "Na ulilala na nani??" swali hilo likawa gumu zaidi ya lile la kwanza. Adrian akavuta pumzi ndefu huku akilitafuta jibu kwa jitihada zote.
"Nililala kwa rafiki yangu mmoja hivi haumfahamu"
"Ulilala naye?"
"Nililala kwake kwani vipi??"
"Adrian unanisaliti!!!" alisema Monica na kuanza kulia kilio cha kwikwi. Adrian akawa anambembeleza lakini akiwa na aibu kubwa sana, hatia ilikuwa inamsulubu ni kweli alikuwa amemsaliti Monica.
"Yaani kweli Adrian mimi wa kunifanyia hivyo, nimekukosea nini??"
Adrian hakuwa na la kujibu akamsisitiza Monica apumzike. Kabla monica hajakubaliana na ombi la Adrian kuwa alale, simu ya Adrian iliita, alikuwa ni Matha, akasita kupokea lakini hatimaye akapokea.


******


Matha alikuwa ameufurahia sana usiku aliolala na Adrian. Alipata wasaa wa kukumbuka mengi ya nyuma enzi za utoto wake. Ilikuwa kumbukumbu ya kipekee. Baada ya kulala kutwa nzima usiku sana aliamua kumpigia simu Adrian.
"Mambo baby Wangu"
"Safi hali vipi…nipo na hebu nipigie baadaye kidogo" alijibiwa na simu ikakatwa. Akajiongeza kiutu uzima Adrian alikuwa na mpenzi wake.
Wivu ukamshambulia lakini hakuwa na la kufanya. Akajifalagua hapa na pale hadi akalala tena.
Adrian aliendelea kuzungumza na Monica hadi akaelezewa mkasa mzima ulivyokuwa.
Akashindwa kumshuku mtu yeyote lakini kwa jinsi alivyozidi kuelezewa umbo la nje la muhusika akili yake ikahamia kwa John, John Mapulu.
Alijiuliza amejuaje juu ya uhusiano wa ghafla aliokuwa nao yeye na Matha, akakosa jawabu. Akaondoa hisia zake potofu juu ya John.


****
John hakurejea nyumbani baada ya tukio la kumbaka Monica, alielekea lilipokuwa eneo la tukio lao la wizi kwa kutumia silaha maeneo ya Imalaseko.
Alishukia mbali sana na eneo la tukio bila kuwapa taarifa wenzake ambao waliamini kuwa alikuwa anaumwa.
John akiwa na bunduki yake kiunoni ikiwa imefunikwa na shati kubwa alilovaa alikuwa na ghadhabu sana. Hasira yake alitamani kuimalizia kwa mwanadamu yeyote yule atakayekatiza mbele yake.
Baada ya kumkosa Adrian nyumbani kwake ambapo alikuwa amepanga kumuua sasa alikuwa na shida na kichwa chochote kile.
Alijibanza sehemu iliyokuwa na kigizagiza kidogo, mahali palipokuwa na kibanda ambacho mchana hufanya shughuli za kuuza nguo. Aliwashuhudia wenzake kwa jinsi walivyokuwa wanaingia ndani ya supermarket. Wawili walibaki nje kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, wakati huo walinzi wa sehemu hiyo tayari walikuwa katika foleni ya kusubiri kusomewa dhambi zao juu mbinguni. Tayari walikuwa wafu!!
John alikuwa makini sana, jicho lake lilishuhudia gari ikija na kupaki mbali kidogo na supermarket, wakashuka watu kama kumi. Aliamini mambo yanaharibika, alitamani kupiga kelele lakini alikuwa anahatarisha maisha yake. Risasi mbili ziliwapata barabara wenzake waliokuwa wanaangalia usalama wa nje.
Waliokuwa ndani hawakujua lolote kutokana na bunduki walizokuwa wakitumia maadui kuwa na viwambo vya kuzuia sauti.
John akaamua kuiponya nafsi yake akatoweka eneo hilo kimya kimya.
Hakika mambo yalikuwa yameharibika kwani siri ilikuwa imevuja na askari waliwahi eneo la tukio kwa ajili ya kuwakamata wezi.
Haikuwa kazi rahisi lakini mwisho wa mchezo ni askari wawili na jambazi mmoja waliofanikiwa kubaki hai.
Kituo cha polisi jijini Mwanza cha MWATEX ndipo alipohifadhiwa muharifu huyu. John alizisikia taarifa hizo kupitia vyombo vya habari siku iliyofuata. Hofu ya kutajwa na huyo mwenzake aliyesalia ilimtawala, John akawa si mtu wa kukaa nyumbani kwake tena wasiwasi ukawa ndiye rafiki yake. Alikuwa mzoefu wa kukamatwa na kuwekwa jela lakini hakupapenda hata kidogo hasa hasa kwa wakati huu ambao yupo katika vita ya kupambana dhidi ya wezi wa penzi lake.
Hatia ikazidi kuzaana katika mwili wa John, hatia zote zilikuwa zinasubiri maamuzi yake. John hakuwa na maamuzi!!!
Alikuwa anasikitisha sana!!!
Michael aliigundua hali ya hofu aliyokuwanayo John, lakini siku aliyotaka kumuuliza ndio siku hiyo hiyo naye John alikuwa ameamua kumueleza Michael. Alimueleza juu ya suala moja tu la kuhusu wasiwasi wake juu ya kukamatwa na polisi wakati wowote.
"Kwa hiyo sasa hapo tunafanyaje??"
"Nahitaji unisaidie kama utaweza!!!"
"Nitafanya nini sasa hapo kaka"
"Nataka uende kule polisi ufatilie kama kweli Julius Machanya amehifadhiwa pale!!" alijieleza John.
Michael alikuwa bado ana uoga lakini John alimtoa hofu, alimweleza jinsi ya kujua kama yuko pale. Michael alipata ahueni baada ya kuambiwa kuwa si yeye ambaye ataenda moja kwa moja bali na yeye atamtumia mtu!!
Michael akatii siku hiyo hiyo akapata jawabu kuwa Machanya yupo pale kituo cha MWATEX.
John hatimaye akawa amedhamiria kuzipunguza Hatia, hatia ya kwanza ilikuwa hii inayomtia wasiwasi hatia ya kutafutwa na polisi kwa kosa la wizi wa kutumia silaha.


*****
Adrian bado alikuwa anamuwaza Matha.
Akiwa ndani ya gari kuelekea nyumbani kwao Kirumba alikuwa anafikiria ni jinsi gani atamtwaa Matha jumla jumla. Aliutambua upendo aliokuwa nao Monica kwake lakini kitendo cha kubakwa kilikuwa kinaanza kumuumiza kichwa.
Laiti kama isingekuwa ujauzito!!!! Alisema kwa sauti ya chini Adrian.
Alifika nyumbani na kumkuta baba yake akiwa bado hajalala.
Mzee Mhina hakuwa amechangamka, na Adrian aliamini lazima iwe hivyo.
"Adrian!!! Mbona ulinificha!!"
"Nini baba??"
"Kuhusu ujauzito wa Monica!!" alijibu huku akiwa amemkazia macho mwanae, Adrian akajihisi kufadhaika akainama chini akijidai kufikiria, alidhani Monica alikuwa amemweleza baba mkwe wake juu ya hilo. Alimlaani kwa kitendo hicho!!
"Mony ndo kasema??"
"Hapana sio yeye, ni daktari amenambia!!" alijibu mzee Mhina.
"Unajua baba aaah!!! Mh!!! Nisamehe lakini ilikuwa bahati mbaya na hatukutaka wazazi wafahamu lakini aah!!!" alishindwa kujieleza.
"Hilo sio tatizo…tatizo ni kwamba aliyembaka mkeo amesababisha mimba itoke" alitoa kauli hiyo huyo mzee. Kauli ambayo ilimshtua sana Adrian, kwanza alifurahia taarifa hiyo halafu baada ya kugundua kuwa damu yake ndio imepotezwa alianza kujiona mjinga. Akajihisi yupo katika hatia, hatia ya mauaji. Mauaji ya mtoto wake ambaye ilikuwa bado miezi mingi aweze kuzaliwa!!!
Adrian akainama kwa muda mrefu!! Mzee wake akafika na kumpigapiga mgongoni kisha akamwacha sebuleni peke yake, yeye akaenda zake kulala.
"Wamemuua mwanangu!!! Lazima nimsake muuaji!!!" aliwaza


******


Hali ya hewa ya Singida ilikuwa imetulia sana, basi la Zuberi lilikuwa limesimama katika stendi ya Singida, abiria waliokuwa wamefika mwisho wa safari walikuwa wakiteremka kwa kufuata utaratibu usiokuwa maalum, kila mmoja alitaka kuwahi kushuka kabla ya mwenzake.
Minja ambaye alikuwa ni mtu wa kulala safari nzima huku akiwa amejifunika usoni kwa kofia yake kubwa, aliwatazama jinsi abiria walivyokosa akili ya kujiongeza. Wakati akiwaona wenzake ni wajinga kwa kugombania kushuka garini, mara jicho lake likatua kwa mtu ambaye alikuwa mwenyeji wake katika mji huu wa Singida, haraka haraka alianza kuwapangua watu ili aweze kushuka kabla yao, wazo alilokuwa anawawazia likasahaulika na yeye akakubali kuwa mjinga.
Jitihada zake zilizaa matunda japo aliwakera sana abiria wengine.
"Aaaah!!! Defaooo!!!" alipiga kelele za furaha Minja baada ya kumuona rafiki yake ambaye alijipatia umaarufu kwa jina la Defao, kutokana na unene aliokuwa nao, unene ambao haukuwa wa utajiri bali unene wa kuzaliwa nao. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Gervas!!.
"Ahh!! Minja huyooo!!! Karibu kijijini kwetu!!" alijibu katika hali isiyokuwa ya kuridhisha, Minja aliligundua hilo lakini akamsogelea na kumkumbatia.
Walitumia sekunde kadhaa kushangaana kabla ya Defao kumuongoza Minja hadi katika daladala ambayo iliweza kuwafikisha nyumbani kwa akina Defao maeneo ya Saba saba, nyumba ilikuwa imepooza sana. Nje walikuwepo watoto watatu hata wao nyuso zao zilikuwa zimejawa na simanzi huku macho yao yakitangaza njaa kali sana.
Minja hakuhitaji Defao amvute pembeni kuweza kumtangazia dhiki iliyokuwa pale, mazingira yale yalimkumbusha hali iliyokuwepo katika familia ya marehemu rafiki yake bwana Rashid, mazingira aliyoyashuhudia siku chache kabla ya kifo chake. Kumbukumbu ya kifo ikawa imefanya shambulizi katika akili yake, ile hatia aliyoamini kuwa haikupanda gari ambalo alipanda kwa safari ya kwenda Singida sasa ikawa imeibuka, alikuwa amesafiri na hatia yake!!! Uso ukajawa na wasiwasi.
"Vipi Minja….usisikitike rafiki yangu yaani nimepitia mengi ndugu yako…yaani afadhali umekuja" Defao alimweleza Minja huku akimpiga piga bega, hakujua kama Minja ameshtushwa na hatia inayomkabili.
Minja hakujibu kitu, alitikisa kichwa kuonyesha kusikitika. Walipoingia ndani walipokelewa na harufu ambayo haikuwa ya kupendeza, kidogo Minja azibe pua zake lakini alisita akajikaza.
"Karibuni!!" sauti ya mwanamke aliyekuwa na mvi hapa na pale katika kichwa chake iliwakaribisha akina Minja na Defao. Yule alikuwa ni mama yake na Defao.
"Mama huyu ni Minja yule rafiki yangu niliyekupa taarifa zake!!"
"Karibu baba, karibu tuuguze!!!" Alisema yule mama kinyonge, uso wake ulikuwa umepauka na alionekana kuwa na msongo wa mawazo.
Minja alipata jawabu kuwa hapo ndani kulikuwa na mgonjwa.
"Mama vipi amelala???" Defao aliuliza, mama akajibu kwa kichwa kuashiria kukubali!!
Defao akamwongoza Minja wakatoka nje.
"Minja ndugu yangu we acha tu, maisha yamenipiga kiukweli, hapa ndo nyumbani kwetu na yule ni mama yangu, hivyo vitoto hapo nje ni vya dada zangu walizalishwa wakiwa hapa hapa nyumbani ndo hao watoto tunalea!!!" alianza kujieleza Defao.
Minja akawa msikilizaji!!!
"Pale ndani mshua anaumwa…si baba yangu ni kaka yake na mama, nishasahau kumwita mjomba tulizoeshwa hivyo" aliendelea. Bado Minja alikuwa anasikiliza.
"Sasa hapa mzigo wote juu yangu!! Na sina hata kibarua maana kuna msala niliufanya hapa naishi kama digidigi tu!!!" alimaliza Defao kwa kumueleza Minja juu ya msala wa kumbaka binti wa mzee Bushir mzee ambaye alikuwa ni bosi wake wakati huo alikuwa ameajiriwa kama mlinzi.
"He!! Ndio maana na wewe dada zako wakajazwa mimba!!!"
"Hapana kaka si hivyo ila nilibaka!!! Yule mtoto hakika alinitega nikisema kunitega nadhani unanielewa, mimi unanifahamu huwa si mwepesi lakini kwa yule mtoto nilitenda unyama huo, ni hatia inayonisonga hadi leo kaka, maisha yangu yamekuwa magumu sana" alijieleza kwa sauti iliyoielezea kweli hatia yake, hatia iliyohitaji muafaka lakini muafaka wake ukawa mgumu sana.
"Pole sana kaka, yametokea hayo tugange mengine sasa" alisema Minja huku na yeye akiikumbuka hatia yake, hatia ya mauaji ya rafiki yake Rashid.
"Aaah!! Joyce nisamehe popote ulipo!!!" Defao alisema huku machozi yakimtoka, hakika alikuwa anajutia.
"Joyce ndo nani tena??"
"Ndiye msichana niliyembaka, anaitwa Joyce Keto. Sijui hata alipo kwa sasa!!" alijibu Defao, huku akizidi kububujikwa na machozi. Minja akamsihi ajikaze, akafanikiwa kumtuliza!!!
Minja alikuwa bado anajiuliza juu ya hali ngumu aliyoikuta katika mji huo wa akina Defao. Hakika hali ilikuwa ni mbaya sana na hata pesa aliyokuwa nayo aliamini kuwa isingedumu kwa kipindi kirefu sana ingeisha na angeanza kuishi maisha ya kubangaiza. Ugeni wake katika mkoa huo ulimwogopesha zaidi.
"Nitapata vipi pesa, udalali!! Umachinga!! Kuchimba mitaro!! Au au au…….yeah!!!" alikurupuka na kupiga kelele Minja. Deo akawa anashangaa, wakati huo alikuwa amenyamaza kabisa kulia.
"Defao!!! Pesa pesa nje nje!!!" alisema Minja kwa furaha.
"Pesa uipate wapi hapa Singida??" aliuliza Defao.
"Pesa pesa kaka!!!! Nimeikumbuka pesa" aliendelea kusema Minja, furaha yake haikuwa ya utani. Defao alilisoma na kulielewa hilo.
"Tulia basi unieleze!!"
Minja alitulia na kuanza kumpa mkasa mzima Defao, alimpa mkasa uliosababisha yeye awe katika mji huo ghafla kiasi hicho. Alimueleza juu ya siri iliyopo kati ya John Mapulu na mpenzi wake Matha Mwakipesile. Minja hakusahau kumuelezea Defao juu ya pesa ambazo John anaweza kuwa anamiliki.
Defao alipagawa baada ya kusikia habari hiyo, kutokana na shida alizokuwanazo aliamini huo ndio ulikuwa wakati muafaka wa yeye kufanikiwa tena kimaisha.
Siku hiyo hiyo Minja alimpa maelekezo yote Defao jinsi ya kufika Mwanza na jinsi ya kumpata aidha Matha ama John Mapulu.
Minja alikuwa anamchukulia John Mapulu kama mume mwema wa kawaida tu kamwe hakuwa anaufahamu upande wake wa pili.
"Ukifika anza na yule John, yule ndo atakupatia pesa nyingi, huyo mke wake baadae, John akishatoa pesa tunamalizia na kwa mkewe" alieleza Minja.
Harufu ya pesa ikatawala.
"Tukizipata hizo tufungue hapa mtaani banda la Mpesa na Tigo pesa yaani hakuna kabisa hapa jirani kitu kama hicho halafu yanalipa hayo" Defao akiwa amechangamka kabisa alimueleza Minja. Kwa pamoja wakakubaliana.
Siku hiyo walikunywa pombe kidogo, na nyumbani wakapeleka nyama. Ulikuwa mlo ambao ulikuwa umehadimika katika nyumba ile!!!!
"Huyu ndiye mzee wangu anaitwa Sajenti Kindo" Defao alimtambulisha mjomba wake kwa Minja.
"Kabla ya kuugua alikuwa ni sajenti huko Mwanza kwenu" Alimalizia Defao huku akificha juu ya suala la mjomba wake kukamatwa na kuwekwa ndani kwa kosa la kutoroka kwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi jijini Mwanza.
Mzee Kindo alitolewa kwa msamaha wa raisi lakini alifutwa kazi kulingana na sheria na kanuni.
Wazo lake la kumkuta mwanaye Joyce Kindo akiwa hai lilifutika baada ya kugundua kuwa tayari alikuwa anaitwa marehemu. Ni tatizo la ugonjwa wa moyo na shinikizo la damu lilikuwa limemuweka kitandani, mshtuko alioupata ulimletea madhara makubwa. Huyu ndiye alikuwa Sajenti Kindo. Sajenti aliyekuwa zamu siku ambayo John Mapulu na Michael walipotoroka rumande.
Minja aliachiwa jukumu la kuihudumia familia ya Defao wakati yeye (Defao) aliposafiri kwenda Mwanza, kwa lengo la kuonana na John Mapulu, lengo la kuvuna pesa bila jasho!!!
Defao akaagana na Minja akapanda gari na kuondoka!!! Laiti kama angeyajua maovu na unyama wa Mapulu ni heri angebakia katika shida zake!!!!
Hatia ya kumbaka Joyce Keto nayo ikapanda naye ndani ya gari.
"Nikizipata hizi pesa nitampatia Minja fungu lake halafu namtafuta Joyce Keto, kama yupo hapo Singida nitatangaza ndoa..pesa ndo kila kitu!!!!" aliwaza Defao akiwa katika siti ya dirishani akihesabu miti jinsi inavyorudi nyuma kwa kasi!!!!
Safari ya kwenda jijini Mwanza!!!


****




***DEFAO anauziwa dili na MINJA....dili la kwenda kumkabili JOHN MAPULU ama MATHA!!! Kumbuku ni huyu DEFAO aliyembaka JOYCE!!!.....na kumpatia mimba!!!
ITAKUWAJE WAKIONANA!!!!......Defao hamjui kabisa JOHN MAPULU!!! Anadhani mchezo ni mwepesi!!! ANAPIGIA MAHESABU PESA AMBAYO HAJAIKAMATA BADO....


***ADRIAN anagundua kubakwa kwa MONICA...anaapa kumtafuta aliyembaka..hajui kiuhakika kama ni JOHN wa MAPULU!!!! ...Nini mwisho wa harakati hizi


***MATHA katika uhusiano na wanaume watatu...kila mmoja kwa wakati wake!!! Nini hatma ya mchezo huu......


NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila
 
  • Thanks
Reactions: ram
Aahahahahhahhhh.... karibuni sana
Yaani naona raha kuona maeneo ninayoishi yakitajwa humu, I wish niwe namjua huyo John

nasubili hadithi itakayo simulia maeneo ya MAKETE NJOOOOOMBE...SIJUI ITAKUWEO KWELI DAAAH...
 
  • Thanks
Reactions: ram
Mkuu Casuist huu utaratibu wa kuweka story kila siku ni mzuri,sio mambo ya wiki hadi wiki.
 
Last edited by a moderator:
RIWAYA: HATIA
MTUNZI: George Iron Mosenya


SEHEMU YA KUMI NA TANO


Minja aliachiwa jukumu la kuihudumia familia ya Defao wakati yeye (Defao) aliposafiri kwenda Mwanza, kwa lengo la kuonana na John Mapulu, lengo la kuvuna pesa bila jasho!!!
Defao akaagana na Minja akapanda gari na kuondoka!!! Laiti kama angeyajua maovu na unyama wa Mapulu ni heri angebakia katika shida zake!!!!
Hatia ya kumbaka Joyce Keto nayo ikapanda naye ndani ya gari.
"Nikizipata hizi pesa nitampatia Minja fungu lake halafu namtafuta Joyce Keto, kama yupo hapo Singida nitatangaza ndoa..pesa ndo kila kitu!!!!" aliwaza Defao akiwa katika siti ya dirishani akihesabu miti jinsi inavyorudi nyuma kwa kasi!!!!
Safari ya kwenda jijini Mwanza!!!

****

Daladala inayokwenda Igoma jijini Mwanza ilisimama katika kituo cha Mwatex, akateremka mwanaume aliyekuwa amevaa miwani nyeusi. Kofia yake iliweza kuiziba miwani yake kidogo, alikuwa ni mrefu aliyekuwa na mwili uliothibitisha kuwa anafanya mazoezi, hakuwa akitabasamu wala hakuwa amenuna!!! Alilipa nauli yake kamili.
Daladala ilipoondoka alitazama kushoto na kulia akavuka barabara na kuelekea kilipokuwa kituo cha polisi. Hakukiendea kituo moja kwa moja bali alipinda kidogo kushoto akakutana na uchochoro, akaangaza tena pande zote kisha akakaa chini. Akaunyoosha mguu wake ukawa umeiziba ile njia nyembamba. Akatoa sigara akaitia mdomoni akataka kuiwasha akagundua kuwa alisahau kiberiti nyumbani. Akaiacha kwa muda mdomoni kisha akaitoa tena na kuitupa, akajilaza katika majani akawa anasubiri kitu. Ilimchukua dakika takribani tano kupata jawabu la swali lake. Alihisi mguu wake uliokuwa njiani ukiguswa.
Akasimama kwa ghadhabu, akaitoa miwani yake. Jicho jekundu likaonekana.
"Samahani kakangu!!" sauti ya mwanamke ikamsihi mbabe huyu. Maneno yale yakamchefua akamsogelea alipo akamnasa kibao kimoja kisha kipigo cha nguvu kikafuatia, yule mama akapiga mayowe raia wema wakafika kumsaidia. Muharifu huyu bado alikuwa anataka kumpiga lakini wanaume wakamdaka na kumvuta kuelekea kituoni.
Mwanamke alikuwa anavuja damu huku akigumia kwa maumivu!!! Wananchi wale wenye hasira wakajua wamefanya jambo la msaada sana kumkamata mbabe huyu ili sheria ichukue nafasi.
"Unaitwa nani???" afande alimuuliza baada ya kuwa amemnasa vibao viwili.
"John Daud!!!" alijitambulisha kishari shari!!!
Akaamriwa kuvua mkanda, kofia, miwani ikachukuliwa, akavua soksi na viatu, akasachiwa akakutwa na shilingi elfu hamsini na tano, zikaandikwa katika kikaratasi (PPR) akapewa hicho kikaratasi na kuongozwa kuingia rumande.
Alipoingia alitabasamu, tabasamu kutoka moyoni alikuwa amefanikiwa kirahisi sana kufika eneo la tukio kwa wakati. Mpango alioutaka ukawa umetimia. Safari ya kuingia rumande.

Huyu hakuwa John Daud kama alivyojitambulisha huyu alikuwa ni John Mapulu. Alikuwa amefanikiwa kuingia rumande, lengo lake likiwa moja tu kummaliza rafiki yake ambaye alikuwa amekamatwa katika tukio la wizi Supermaket!! Aliamini kwa kumuua huyu atakuwa amejipunguzia hatia, inayomkabili.
Hakuwa na wasiwasi wa kushtukiwa kuwa yeye ni John Mapulu aliyetoroka rumande katika kituo cha kati, kwanza alitambua kuwa wale askari waliokuwa zamu wote waliswekwa rumande na kama hiyo haitoshi, tatizo la takwimu Tanzania lilimpa hali kujiamini.
John Mapulu akaichukua nafasi yake akakaa huku akiwa ameuficha uso wake, waliojifanya wenyeji walimzodoa lakini hakuwajibu chochote aliendelea kuinama hadi hapo kigiza kilipoanza kuingia.
Punde baada ya kuhesabiwa idadi ya waliopo rumande kwa siku hiyo alihesabu muda kidogo mbele akaunyanyua uso wake, kisha mwili mzima akapiga hatua kuelekea chooni, akazuga kujisaidia haja ndogo, kisha akarejea na kupitia vyumba kadhaa, uzoefu wake katika maeneo kama hayo ulimpa ujasiri mkubwa. Ndani ya muda mfupi akawa amemuona Julius Machanya, ni huyu aliyekuwa anamtafuta!!!
John alishuhudia jinsi alivyokuwa katika hali mbaya, alikuwa amezungukwa na damu zilizotokana na kipigo. Akamsogelea na kujilaza jirani naye!! Mahabusu wengine walikuwa wamekikimbia chumba hicho!! John akatumia mwanya huo kuikutanisha mikono yake miwili katika shingo ya July akaikaba kiujasiri akauondoa uhai wake. Kama jambo la kawaida kabisa!!!
Hatia moja ikawa imepunguzwa kwa kufanya mauaji!!!
Baada ya kumaliza shughuli hiyo John alienda hadi mlangoni na kumuita afande mmoja aliyemuingiza hapo ndani.
"We mpumbavu unalala humu wakati una pesa?" afande akamweleza John!!!
John akajidai kufikiri kisha akamuita tena.
"Tuigawane basi!!!"
"Haya hebu subiri!!! Unakaa kaa tu humu ndani wakati hakuna aliyekuja kukushtaki? Acha kuwa mjinga wewe, au unataka ukasimame na yule hawara yako mahakamani" alijibiwa, baada ya muda ulifunguliwa mlango akaruhusiwa kutoka akapewa shilingi elfu ishirini na tano nyingine askari wakaigawana.
John Mapulu akawa huru tena!!!
Hatia ya kwanza ikazikwa. Akajihisi yupo huru.
Sasa ni zamu ya huyu mjinga Adrian ambaye anathubutu kunigusia Matha wangu!!! Alisema John huku akiwasha simu yake aliyokuwa amerejeshewa baada ya kutolewa rumande!!
Akampigia Matha, wakapeana salamu na utani wa hapa na pale hadi salio likaisha. John akajisikia fahari!!! Chuki dhidi ya Adrian ikaongezeka hakutaka mtu yeyote amuibie mpenzi wake.

***

Matha alikuwa ameanza kuipata amani ya nafsi baada ya Minja kuwa ameenda mbali na jiji la Mwanza. Aliamini kabisa hatia ya kubeba mimba nje ya uhusiano wake na John Mapulu ilikuwa imefichwa na Michael peke yake, kwani hata yule daktari aliyempima na kugundua kuwa yu mjamzito hakufahamu kama ile ilikuwa hatia bali alijua ni salama.
Kukutana na Adrian Mhina na kufanya naye mapenzi kisha wote kuondoka wakiwa na furaha lilikuwa jambo jingine lililompa faraja na kuamini kuwa ameua hatia mbili kwa wakati mmoja. Akajisikia amani sana kuishi bila hatia, ilibaki hatia moja tu ambayo nayo haikumtesa sana kwani hakuwepo mtu ambaye amemshuku, hatia hii ilikuwa ni ujauzito aliokuwa ameuhifadhi katika mfuko wake wa uzazi. Hatia hii alijua itavuta subira kwani tayari alikwishagundua kuwa ana mwili mzuri ambao hauonyeshi ujauzito mapema, na pia hakuwa mtu wa kichefuchefu mara kwa mara.
Mara akakumbuka hisia zilizokuwa zinajengeka haraka haraka juu ya Adrian, kwa hali halisi hazikuwa hisia za haraka haraka kwani hapo awali Adrian aliwahi kuwa mpenzi wake japo hawakuwahi kushiriki katika tendo la ndoa hadi pale walipofanya hivyo siku chache nyuma, tena kwa kuiba kwani Matha tayari alikuwa kwenye uhusiano na mwanaume mwingine.

Matha alijaribu kupanga majina ya watu watatu ambao wote walikuwa naye katika uhusiano alijaribu kuzitafakari hisia zake kwa makini kwa kila mmoja. Alianza na John, akayakumbuka mema yote ambayo John Mapulu alimtendea, akahesabu maisha mazuri aliyonayo, bila John asingekuwa hapo alipo, akaupima upendo wa John akagundua ni upendo wa dhati kwani kamwe hakuwahi kumfumania wala kumhisia kwamba ana mahusiano na msichana mwingine.


John ananipenda sana!!! Lakini John hazai!!! John hawezi kunipatia mtoto na mimi napenda sana watoto!!! John amenibadilisha na kuwa mrembo mkatili, John amenifanya niwe muuaji, John si mtu mzuri!! Ni kwangu tu ndo ananionyesha upendo, John alitaka kumuua Minja, John ameua watu wengi!! John hanifai japo ananipenda. Alifanya takwimu hiyo Matha akiwa kitandani kwake, akapiga kite cha hasira akakodoa macho yake kuiangalia picha ya John iliyokuwa ukutani akaitukania ile picha mama yake mzazi!!!


Michael, huyu naye ni mimi nilimpenda, nadhani ni kile kifua chake, mwili wa mazoezi na tabasamu zuri ambalo huzaa vidimples, yupo nadhifu sana Michael, halafu ni mpole na anajua sana kunifanya nifurahie kuwa naye faragha, Michael hana pesa lakini Michael ana uwezo wa kuzaa, Michael amenipatia zawadi ya maisha yangu. Lakini Michael alitaka kunikimbia, Michael ni baba mbaya sana kwa nini alitaka kumkimbia mwanae, huyu hana mapenzi ya kweli, nadhani vitisho vyangu ndo chanzo cha kumpata kaka huyu. Michael wewe ni ---- sana hujui kuwa John alinifanya kuwa muuaji naweza kukuua dakika yoyote??? Laiti kama nisingekuwa na mimba yako!!!!!! Alimaliza Matha kwa kukiendea kioo na kujitazama akalishika tumbo lake akajilazimisha kutabasamu, akaliendea jokofu dogo lililokuwa pale chumbani akachukua chupa ya maji akanywa.


Adrian, Adrian, Adrian!!!! Sina la kusema juu ya uvumilivu wake. Alinivumilia hakuwa na papara ya mapenzi, tazama alikuwa na upendo wa dhati. Na hadi sasa hapo amesema kuwa hajaingia katika ndoa. Maisha yake ni mazuri sana, amejipanga. Hana roho mbaya kama ile ya John na ni mvumilivu sio kama Michael. Adrian ndiye mwanaume sahihi, lakini je ataweza kuwa nami na hii mimba??? Lilikuwa swali zito. Sitaki kuitoa na kamwe sitaitoa!!!! Aliapa Matha. Kisha akachukua kalamu na karatasi akaamua kupata jibu sahihi kwa kuwapanga kiherufi, Adrian, John, Michael. Adrian akawa ametangulia kwa kila hali. Matha akacheka peke yake kama mwendawazimu kisha akakichana kile kikaratasi, akakirukia kitanda akajilaza.

*****

Defao alifika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza, alikuwa makini sana hakutaka kuunda urafiki na mtu yeyote bali alifuata maagizo aliyopewa na Minja. Shati yake iliyokuwa imechomekewa kwenye suruali mpya aliyokuwa amenunuliwa na Minja pamoja na kiatu kilichong'aa aliwashawishi madereva wa teksi kumkimbilia na kumpa heshima za kumuita bosi. Defao hakuwajali aliziendea daladala zilizomfikisha hadi Mkuyuni karibu na gereza la Butimba, huko ndipo palikuwa na nyumba za kulala wageni zilizokuwa za hadhi nafuu ya Defao. Maelekezo haya alipewa na Minja.
Alipata chumba cha bei nyepesi sana akalipia, akakikagua chumba kisha akatoka na kutafuta chakula cha bei nyepesi akaitibu njaa yake kisha akanunua vocha na kurejea katika chumba alichokuwa amelipia.

Akavua nguo zake na kubakiwa na pensi, akaingia kitandani, akajaribu kuishusha chandarua lakini akagundua kuwa ilikuwa ina matundu mengi pia ilikuwa ina vumbi, akaghairi akakitupa kilipokuwa, akajilaza akachukua simu yake na kupiga namba alizohakikishiwa kuwa ni za John Mapulu, akaachia tabasamu pana baada ya kusikia simu inaita. Tabasamu lililojaa tumaini!!!
"Nani mwenzangu!!!"
"Defao….naongea na John Mafuru" Defao akakosea jina John hakung'amua hilo.
"Eeh!! Unasemaje kwanza namba yako mpya huku"
"Nina shida kubwa ya kuonana na wewe kwa siku ya kesho nina jambo la msingi nahitaji kukueleza"
"Jambo gani??"
"La msingi" alijibu Defao.
"Nakupigia baada ya dakika tano ngoja niangalie ratiba"
Defao akaikata simu na kusubiri apigiwe. Alifarijika kuisikia sauti ya John.


John alikuwa amelala mapema sana siku hiyo, baada ya kuwa amezungumza mambo mawili matatu na Joyce Keto juu ya suala la kumuanzishia Kliniki ya mimba yake. John alikuwa amekubaliana na ombi hilo akaahidi kuwa atakuwa anampeleka.
Simu aliyopigiwa ndiyo ilimuamsha kutoka usingizini. Akakaa akamfikiria huyo mgeni aliyetaka kuonana naye, akapatwa na wasiwasi kwani alikuwa na maadui wengi sana jijini Mwanza. Hakutaka kumfuata alipo bali alitaka huyo mgeni amfuate kwake ili aweze kupambana naye kama ni mtu mbaya. Baada ya kupata muafaka huo alimpigia huyo mtu simu na kumuelekeza jinsi watakavyoonana.
"Lakini mkeo asiwepo!!!" alisema Defao baada ya John kuwa amemaliza kutoa maelekezo.
Neno hilo lilimshtua John lakini akahisi ni mbinu ya kucheza na akili yake.
Akatabasamu akazima simu akalala!!!


Asubuhi aliwaandaa vijana wake watatu, vijana aliowaamini kabisa kuwa ni vijana mashuhuri na wana roho mbaya lakini kubwa zaidi walikuwa wanamuheshimu sana. Alimuandaa mmoja kuwa ndiye awe John Mapulu wakati wengine wawe walinzi wa kuhakikisha kama huyo mtu ni mbaya basi waweze kutoa shambulio ikiwezekana kummaliza kama atajibu mashambulizi ama kumchukua mateka ili aweze kuwaeleza ni nani amemtuma.
Saa sita mchana, Defao alifika Nyasaka jirani na shule ya Jerry's kama livyoelekezwa na John, akampigia simu , akapewa maelekezo ya mwisho akaiona nyumba.
Lile jambo la kuiona nyumba ile lilimtia wasiwasi akaanza kumuogopa John, aliamini hakuwa na pesa za kawaida kama aliyesimuliwa na Minja mkoani Singida. Defao akairekebisha suruali yake akalisogelea geti, akabonyeza kengere kama alivyoelekezwa punde mlango ukafunguliwa.
"Wewe nani??" mlinzi aliuliza.
"Naitwa Defao ni…"
"Nakutambua!!! Na nina taarifa zako" alimkatisha kisha akamfungulia mlango akaingia, wasiwasi ukazidi kumtawala Defao, akaanza kuwa muoga. Akachukuliwa na kupelekwa mahali palipokuwa na bustani ya kupendeza, akaiangalia ile bustani akatamani ingekuwa yake, akawaza kupata pesa nyingi bila jasho akapanga kuwa na yeye atafanya mambo ya kuvutia kama haya anayoyaona.

Tamaa zikamuingia akaanza kufikiria jinsi ya kuchukua kiasi kikubwa zaidi ya Minja. Tamaa ikamshambulia ikamfanya ajione ana haki ya kupata mgao mkubwa. Wazo la kumchinjia baharini Minja likatulia tuli katika ubongo wake.
Akiwa katika mawazo hayo, akatokea mwanaume mrefu mwenye suti iliyomkaa vyema katika mwili wake, haikuwa kubwa wala ndogo bali iliendana na mwili wake. Mkononi alikuwa ameshikilia glasi iliyokuwa na pombe kali. Alijongea hadi akamkaribia Defao.
"Salama kaka, karibu sana!!!" alisalimia mwanaume huyu ambaye alijitambulisha kama John Mapulu.
"Naitwa Defao!!!"
"Hawajakuhudumia kinywaji??" aliuliza
"Aaah!! Usijali bosi usijali" alijibu.
Mwanaume huyu akakaa kitako, hakuwa John Mapulu bali Joram, huyu ndiye alikuwa ameagizwa na John Mapulu ili aweze kumtambua huyo mgeni.
Joram hakuwa na wasiwasi, alikuwa amezungukwa na walinzi ambao walikuwa wamejificha na bunduki zao viunoni.
"Ndio Defao…nakusikiliza!!" alisema Joram. Defao akaliweka koo lake sawa akajaribu kuzungumza kwa kujiamini lakini akawa anatetemeka sauti.
Maelezo yake yalikuwa yamenyooka sana kama alivyokuwa ameelezwa na Minja. Joram alikuwa makini sana kumsikiliza Defao hadi pale alipomaliza.
"Asante sana kwa taarifa kaka, asante sana tena sana….sasa chukua namba yangu hii nyingine nitakutafuta jioni, asante sana"
"Lakini ni biashara hii ndugu yangu!!!" Defao alisema.
"Kwani tulielewana bei gani kwa taarifa hii??" alihoji huku akidhani kuwa Defao alikuwa amewasiliana na Minja tayari kuhusu malipo.
"Bado hatujazungumza!!"
"Basi jioni nitakutafuta tuzungumze, kwa sasa hebu subiri kidogo" alinyanyuka Joram kisha akarejea na kibahasha kidogo akampatia Defao wakaagana kwa miadi ya kukutana jioni.

"Vipi alikuwa na ishu gani huyo??" John alimuuliza Joram.
"Aah!! ----- tu huyo alikuwa anamuulizia Julius Machanya, nadhani ni ndugu yake" alidanganya Joram.
"Mpuuzi aende akamuulizie kwa Mungu huko" alisema kwa jeuri John huku akimshangaa huyo Defao kwanini alitaka mkewe asiwepo wakati wa wao kukutana. Akapuuzia akaifuta namba yake!!!

Joram alikuwa amepata siri nzito sana ambayo ilimsukumia kupata ujasiri wa kufanya jambo ambalo hakuwahi kuliota, baada ya kuondoka pale nyumbani kwa John alimpigia simu Defao kabla ya jioni wakakutana mahali akampatia milioni tatu, akijumlisha na zile za asubuhi jumla inakuwa milioni tatu na laki moja na nusu.
Kwa Defao ilikuwa shangwe sana hakutegemea kupata pesa hizo kwa wepesi kiasi hicho, akazifunda katika suruali yake huku akimuahidi Joram ambaye yeye aliamini kuwa ni John Mapulu kwamba hataitangaza siri hiyo.
Siku ya Defao ikapendeza sana akahama nyumba ya kulala wageni Mkuyuni akaenda zile za gharama ya juu kidogo. Upendo wake kwa Minja ukaanza kupungua hatua kwa hatua akaingiwa na pepo la dhuluma.
Hakutaka kurudi Singida kwa wakati, akawatamani samaki wa Mwanza aina ya sato na dagaa watamu wa ziwa Viktoria. Miamba mikubwa mikubwa ikawa inazidi kumvutia machoni. Akapaona Mwanza patamu.
Akaendelea kukaa!!!
Jiji la miamba!!!

*****

Matha alikuwa anazungumza na Michael kwa njia ya simu ni siku nyingi zilikuwa zimepita bila wao kuonana. Yalikuwa majira ya saa nne usiku, wawili hawa walikuwa wanafurahia huduma za punguzo la bei katika mitandao ya simu hivyo walikuwa wanazungumza hata yasiyokuwa na maana.


Mlango wa Matha uligongwa, akasogea akiwa na simu mkononi akaufungua, kipande cha mwanaume kikakingia ndani.
Matha akakata simu ghafla, akamshangaa mgeni wake. Huyu alikuwa ni Joram!!! Kiuhusika alikuwa ni shemeji yake, lakini kikazi alikuwa ni jambazi mwenzake japo walipishana ngazi. Joram alikuwa wa kumuheshimu Matha kila siku!!! Lakini badala ya kumuheshimu ni mara nyingi Joram alipokuwa anabaki peke yake na Matha alikuwa akimtamkia maneno yaliyoonyesha kuwa alikuwa katika penzi zito.
Matha hakuwa na hisia hata kwa mbali kwa mtu huyu!!!


Harufu ya pombe ilimaanisha kuwa Joram alikuwa ametokea bar kunywa na kufika katika chumba cha Matha akiwa amelewa
Joram alimsogelea Matha na kumkumbatia kwa nguvu, japokuwa alikuwa amelewa lakini bado alikuwa na nguvu. Matha hakuwa legelege alijitoa katika mikono ya Joram na kujiweka pembeni, Joram akamsogelea tena, machale yakamcheza Matha akaamua kujilinda. Mwilini mwake alikuwa amevaa kanga moja na ndani akiwa na chupi pekee, kifuani alikuwa na sidiria.
Alimtazama machoni Joram kisha akaichokonoa kanga yake ikaanguka chini akazungusha mguu wake kama anavyofanya muigizaji wa filamu za mapigano Jean Claude Van damme. Mguu usiokuwa na kiatu ukatua barabara katika shavu la Joram akayumba lakini hakwenda chini. Matha hakulemaa akajirusha tena teke jingine safari hii Joram akaliona akakwepa lakini tayari mkono wa Matha nao ulishafika na kupangua kibao alichokuwa amekirusha Joram. Wakali wa mapigano ana kwa ana!!
Kengere ya hatari ikalia katika kichwa cha Joram akahofia kuchafuliwa sura na mwanamke huyu, akaamua kuzungumza.
"Matha!!! Achaaa"
Matha akatulia akawa amejisahau kuwa chupi ipo hadharani.
"Matha kuna jambo hapa!!! Kwanza vaa kanga" alisema Joram huku akitweta, Matha akavaa haraka haraka kanga yake.
"Nisikilize kwa makini kwanza samahani kwa kuja usiku kwako lakini ilikuwa lazima iwe hivyo" alisita akavuta pumzi kisha akaendelea, "Unajua kwamba siri yako kidogo itoke leo??"
"Siri gani??"
"Kuwa u mjamzito!!!" alitamka maneno ambayo kwa Matha yakawa na ladha tamu ya mkuki kwa nguruwe….akakodoa macho.
"Nani ana mimba nani kakwambia kama ni John anatania" alipagawa binti huyu, nguvu zikamwisha akajikuta anaogea ilimradi tu!!
"Wala si John!!! Hata huyo John hajui, hapa nafahamu mimi, wewe, na aliyekupa mimba basiii!!!" alijibu kwa utulivu Joram. Matha alikuwa anamkubali sana Joram kwa kuficha siri, hivyo alimuamini pale pale. Joram alielezea picha yote ilivyokuwa. Kipindi hicho chote Matha alikuwa anatetemeka. Hakutegemea kama tatizo limeibuka upya!!
"Kwa hiyo tunafanyaje Joram!!!" Matha akajaribu kuunda urafiki.
"Nadhani unajua tunafanyaje, bila shaka unaamini kuwa mimi ni mtunzaji mzuri wa siri"
"Nakuamini asilimia zote" alisema Matha, Joram akacheka kisifa sifa.
"Safi sana nilidhani imani yako imeshuka!!!"
"Kamwe haiwezi kushuka!!"
"Basi hata siri ya kuwa mimi ni mpenzi wako wa siri nitaitunza!!" aliongea kimajivuno huku akiyanyanyua mabega yake juu, Ngoma za sikio la Matha zikataka kufyatuka kwa kusikia maneno hayo makali ya Joram.
"Unamaanisha nini Joram?"
"Kwani unadhani nimemaanisha nini?"
"Yaani uwe mpenzi wangu"
"Ooh!! Samahani sio mpenzi bali mzinzi mwenzako maana mpenzi ninaye" aligandamiza msumari mwingine Joram, Matha akaiuma midomo yake kwa ghadhabu, hofu ikachukua ubabe wake wa kurusha mateke. Akawa dhaifu!
"Sidhani kama una maanisha Joram!!"
"Aah!! Basi kama simaanishi ngoja niende, lakini wamuonaje John wewe, una hamu ya kufa?? Si unajua kufa hakujaribiwi" alisema huku akigeuka aondoke.
"Joram!!!"
"Yes!! Darling" alijibu Joram, Matha akataka iwe ndoto yeye kuitwa hivyo na Joram lakini ilikuwa ni hali halisi. Joram alikuwa anataka penzi, kichefuchefu kikachukua hatamu!!! Akakimbia bafuni akatapika kidogo.
"Hivi ina miezi mingapi??" aliuliza Joram kwa mbwembwe. Huku akitabasamu.
"Joram usizungumze na John lolote nitakupigia simu" alisihi Matha.
"Jitahidi iwe kabla ya kesho jioni" alisema na kuondoka bila kuaga.


******


***HATIA ya usaliti na hatimaye kupata mimba inayomkabili MATHA inampa faida JORAM kujipatia penzi la burebure...JE MATHA ATAINGIA KATIKA UHUSIANO NA MWANAUME WA NNE????.....Hatia itajibu!!!!


***DEFAO analifurahia jiji la Mwanza na sasa anafikiria kuendelea kubaki.....TAMAA inachukua mkondo....Je? atakuwa salama kwa muda gani!!!....kibaya zaidi anadhani amekutana na JOHN MAPULU!!!


***ADRIAN, MICHAEL, MINJA ....wote wana hatia zao.....

NYIRO master09 Khantwe KABERWA2013 mbalu Honey Faith Sangomwile Jullie Z mugaru VAN HEIST binti kiziwi Donatila


 

Similar Discussions

Back
Top Bottom