Reuben: Mtanzania anayetamba anga za mitindo, filamu Uingereza

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126
Taaluma ya uandishi wa habari imesababisha nipende kusoma majarida mbalimbali, magazeti, magazeti tando(blog) na habari katika mitandao ili mradi kutaka kufahamu mambo yanayoendelea ndani na nje ya nchi.

Wakati natii kiu yangu ya habari mwaka jana, nilifungua mtandao wa gazeti tando hapa nchini, nikakutana na habari kuhusu kijana wa Kitanzania, Julius Reuben anayefanya kazi za mitindo nchini Uingereza. Habari hiyo ilinivutia na nilitamani kufahamu habari zake kwa undani na ikiwezekana nimwandike katika gazeti letu la HabariLeo Jumapili kwenye jarida letu la Nyota.

Jarida hili huandika habari mbalimbali za burudani na lina kurasa mbili maalumu kwa ajili ya makala ya mtu ambaye amefanikiwa katika shughuli zake au kujipatia umaarufu kwa ajili ya jambo fulani linaloweza kuwa mfano kwa jamii. Kwa kuwa katika habari hiyo ilikuwapo anuani ya tovuti ya kijana huyo, niliamua kuwasiliana naye kwa kumwandikia ujumbe, nikajitambulisha na kumweleza nia yangu.

Baada ya siku chache alinijibu akinieleza yuko tayari lakini aliniahidi kuwa angenitafuta, hata hivyo tangu wakati huo hatukuwasiliana na nilisahau kabisa kama niliwahi kuwasiliana na Reuben. Mwishoni mwa mwezi uliopita, alinipigia simu ya ofisini akanieleza kuwa yuko tayari kwa mahojiano lakini kwa kuwa yuko mbali, njia rahisi kuwasiliana naye ni kumtumia maswali na yeye ajibu kwa njia ya mtandao.

Dhamira ya kuwasiliana naye ilikuwa ni kuwafahamisha Watanzania kuhusu kijana Mtanzania anayeiwakilisha nchi kupitia sanaa na namna alivyofanikiwa katika fani ya mitindo wakati ni mwanamume kwa kuwa mara nyingi tumezoea akinadada wa Kitanzania ndio hujihusisha na masuala ya mitindo na urembo.

Reuben anasema aliondoka Tanzania miaka 12 iliyopita baada ya familia yake kwenda kuishi London, Uingereza na sasa ni muda mrefu tangu alipoondoka nyumbani (Tanzania). Ukweli mara nyingi sikuwa nikiishi Tanzania, nimekuwa nikitembea sehemu mbalimbali sehemu kubwa ya elimu nilipata nchini Kenya na muda mwingi wa mapumziko ya likizo nilikuwa nikisafiri, anasema.

Baada ya kumaliza masomo yake, mwanamitindo huyo mwenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro, aliamua kwenda kujiunga na familia yake ambao tayari walikuwa raia wa Uingereza lakini pia alikuwa na ndoto ama lengo la kutafuta maisha bora. Kama ilivyo kwa binadamu wengine, Reuben pia alikuwa na ndoto ya kuwa na fani fulani au kufanya kazi fulani. Alitamani kuwa padre lakini kumbe majaliwa yake yalikuwa katika fani ya mitindo.

Wakati tukiwa Tanzania, mama yangu alikuwa akifanya maonyesho ya mitindo katika miji mbalimbali nchini, mara kwa mara alikuwa akibuni nguo za watoto na alikuwa akinivalisha mimi, kaka yangu na binamu yetu. Baada ya kuzivaa tulipita katika majukwaa ya mitindo kuzionyesha, anasema. Reuben anasema kipindi hicho mama yake ambaye anamtaja kwa jina la Angel B, alikuwa akimiliki kampuni ya Angel Fashion ya Dar es Salaam.

Anasema, mama yake alilazimika kuacha shughuli zake hizo baada ya mtoto wake wa kike (dada yake Reuben ambaye hakutaka kumtaja jina) kuumwa, akaenda katika nchi mbalimbali kutafuta tiba ya binti yake huyo na kwa bahati mbaya hakufanikiwa na hivi sasa binti huyo ni mlemavu. Mama wa mwanamitindo huyo hivi sasa anafanya biashara ya kutengeneza na kupamba nywele, na ana biashara zingine pamoja na kumtunza binti yake huyo.

Pamoja na kuwa na ndoto ya kuwa padre kijana huyo anasema watu wengine waligundua kipaji chake cha kuwa mwana mitindo: uwanamitindo haikuwa ndoto yangu, nilitaka kuwa padre, lakini kama watu wanavyosema unachoona katika macho yako sio wanachoona ndani yako watu wengine... wakati nikiwa shule walipokuwa wanafanya maonyesho ya mavazi, walikuwa wakiniomba nishiriki lakini muda mwingi nilikuwa nikikataa.

Reuben anasema mpaka wakati anakwenda London, alikuwa na mtazamo wa kuwa padre lakini mambo yalibadilika baada ya kushirikishwa katika utafutaji wa wanamitindo ndipo alipopata dhana ya kujaribu shughuli za mitindo. Niliamua kushiriki katika utafutaji wa wanamitindo hapa London, nikafikiria labda naweza kufanikiwa kuwa mwanamitindokwa hiyo ilikuwa bahati yangu, kama unavyoona nimefanikiwa, anasema.

Reuben anasema kuthubutu kumemwezesha kupata matunda yanayoonekana sasa ikiwa ni pamoja na kufanya kazi zinazompatia kipato cha kuendesha maisha yake na kukaa na watu ambao hakuwahi kufikiria katika maisha yake angeweza kuwa nao karibu. Akizungumzia masuala ya lugha iwapo ni tatizo au changamoto kwa Watanzania au hata kwake kijana huyo anasema, mimi sijawahi kuleta upuuzi kwenye lugha...kama unatumia lugha yako ya pili, siku zote utakuwa na matatizo ya kutofautisha neno kwa neno.

Hatuna tofauti na nchi nyingine, kitu ninachoweza kufikiria kuhusu lugha yetu ni linganifu, yenye amani hasa kama unatoka Tanzania lakini Kingereza ni kinyume chake na hivyo tunapata ugumu kutamka baadhi ya maneno lakini sio mbaya kama inavyoelezwa. Kijana huyo anasema hajasahau asili yake hivyo bado anaikumbuka lugha ya Kiswahili.

Bado nakumbuka Kiswahili, ingawa kuna kipindi tulikuwa hatuzungumzi lugha hiyo kabisa lakini tangu bibi yangu asisitize tuitumie hivi sasa tunazungumza sana tunapokutana katika sikukuu za kifamilia, chakula cha usiku na tunapokuwa matembezini, anasema. Reuben hivi sasa hayuko katika masomo yoyote, anasema baada ya kumaliza kidato cha sita aliamua kuchukua mafunzo ya sanaa za maonyesho na akatunukiwa stashahada ya juu.

Anasema, kama mipango yake itakwenda kama alivyokusudia ana mpango wa kuchukua shahada ya kwanza ya fani hiyo. Kijana huyo anasema anafikiria kuja kuwekeza nyumbani (Tanzania) ingawa amesikia vitu vingi tofauti, vibaya na vizuri. Ndio nina mpango huo (kuwekeza nchini) lakini nimekuwa nikisikia vitu vingi tofauti lakini itabidi nije kujionea mwenyewe siku zote kuna changamoto sehemu yoyote nitakayokuwa lakini hiyo haiwezi kunizuia kutimiza malengo yangu, anasema.

Akielezea namna Watanzania wanavyoishi Uingereza, Reuben anabainisha kuwa baadhi ya Watanzania huishi pamoja kama familia na baadhi huishi wenyewe huku wengine wakiwa wamefika huko kwa njia zao binafsi lakini wote kwa pamoja wakiwa na mkakati wa kutimiza malengo yao katika maisha. Mwanamitindo huyo anasema angependa kusaidia vijana wengine wa Kitanzania wenye ndoto ya fani hiyo lakini anasema wengi ambao amekuwa akiwasiliana nao kwa njia ya barua pepe wanaweza kufanya kazi ya matangazo zaidi kuliko mitindo.

Reuben anasema yeye hushughulika na wanamitindo wa kiwango cha juu (high fashion models) ambao hawawezi kufanya kazi za matangazo ambazo hufanywa na watu ambao ni watanashati na warembo lakini katika tovuti yake kuna kampuni za uwakala wa wanamitindo ambao ni watanashati na warembo wenye vigezo vinavyotakiwa anaweza kuzitumia hizo kampuni. Anakiri kuna tofauti kati ya wanamitindo wa Tanzania na wale wa nchi za magharibi na kwa mujibu wa meelezo yake, Tanzania imefunikwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Anaongeza kuwa wanachotakiwa kufanya ni kutafuta sura inayoitambulisha Tanzania ambayo itawawakilisha Watanzania na si wanamitindo kwa ajili ya matangazo ya biashara. Ngoja nikufafanulie vizuri, wanamitindo wa matangazo ya biashara ni warembo na watanashati ambao mvuto wao hauwatofautishi na watanashati wengine , baadhi yao ni wale wanaoshinda mataji ya urembo na utanashati.

Wanaotakiwa katika fani hii ni wenye kiwango cha juu wanatakiwa kuwa wasichana wenye sura zenye mvuto unaofanana na mvulana, na mvulana mwenye mvuto unaofanana na msichanasio wazuri wala wabaya ila wanavutia kutazama, huwa wanawaita sculptured (wa kuchonga), anasema.

Kuhusu sifa zao Reuben anasema kuwa kwa msichana kutoka Afrika Mashariki basi anatakiwa kuwa na kifua saizi 34, kiuno saizi 24 nyonga (hips) saizi 34 na si zaidi ya hapo wakati urefu anatakiwa kuwa si chini ya futi tano na inchi nane ( 5"8). Anasema, wavulana wanatakiwa kuwa na kifua saizi 38-40, kiuno saizi 30-32 wakati urefu ni futi 6 hadi futi sita na inchi mbili (6"2 ) na si zaidi au chini ya hapo.

Sisi Watanzania tuna tatizo la utambulisho (kama nimeweka sawa). Unajua Msudan, Msomali, Mkenya, Muethiopia na mara nyingine Mganda unapomwona unaweza kutambua anakotokalakini sio Mtanzania, mara nyingi huwa wanatuchanganya na watu wengine kutoka nchi nyingine. hata mimi mara kwa mara wanafanya kosa kunitambua kwa sababu hatuna sura yenye nguvu ya kutuwakilisha kimataifa.

Watu wengi wananifahamu kuwa ni mwanamitindo wa Ufaransa, hilo ndio jambo baya, anasema. Mwanamitindo huyo anasema, tuna wasichana na wavulana ambao wanaweza kutuwakilisha vizuri lakini hawapewi nafasi kwa sababu ya udanganyifu nchiniwako tayari kumpa nafasi mtoto kutoka familia ya kitajiri kuliko mtoto kutoka familia masikini sana.

Reuben ambaye ana umri wa miaka 24, nywele nyeusi, macho ya kahawia, urefu wa futi sita na inchi sita, kifua saizi 38, kiuno saizi 30 na nyonga saizi 38 anasema hajaoa ila ana wazo hilo na kuongeza kuwa, familia bado, nahitaji miaka mingine zaidi. Mwanamitindo huyo aliyezaliwa nchini Tanzania aligunduliwa na Kampuni ya wanamitindo ya Flair Model Agency ya nchini Uingereza ambapo hivi sasa ndio makazi yake.

Mambo anayopenda Reuben ni kupanda farasi, mpira wa kikapu, mitindo, muziki na familia. Maonyesho ya mavazi aliyoshiriki hivi karibuni ni pamoja na London Fashion Week, La Dolce Vita Fashion Week na AFW 2008 lakini pia hivi karibuni alionekana katika vipindi vya televisheni vya Holby City, Hotel Babylon na MI High wakati ameshiriki katika filamu How To Lose Friends and Alienate People na Run Fat Boy Ru, pia hivi karibuni ameshiriki katika mchezo wa kuigiza wa Dust na video ya Last Night A DJ Saved My Life. Huyo ndiye Julius Reuben kijana aliyetamani kufanya kazi ya Mungu lakini akajikuta akidondokea katika majukwaa ya mitindo akipeperusha bendera ya Tanzania nchini Uingereza.
1592204437656.png
 
Back
Top Bottom