RC Makalla aagiza shule inayopakana na Makaburi ijengewe uzio ili kuwapa amani Wanafunzi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,121
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni, Hanifa Suleiman kujenga ukuta kuzunguka Shule ya Msingi Boko Mtambani ili kuleta amani na usalama shuleni hapo.

Shule hiyo imejengwa karibu na eneo la makaburi yanayodaiwa kuwa na matukio ya mauzauza.

Alitoa maagizo hayo jana alipofika shuleni hapo kukagua ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa na ndipo kupokea kero hiyo kutoka kwa uongozi wa shule.

Makalla alisema hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa za kujenga uzio utakaotenganisha shule hiyo na eneo la makaburi ili kuzuia wanafunzi kuathirika kisaikolojia pale wanapoona wafu wakizikwa.

“Ninaamini katika mkakati wangu wa kujenga uzio katika shule zote za Mkoa wa Dar es Salaam, hii shule ndiyo itakuwa ya kwanza,” alisema Makalla.

Hata hivyo, alipongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa wilayani humo na kusema Rais Samia Suluhu Hassan alitoa Sh bilioni 12.3 mkoani humo kwa ajili ya ujenzi wa shule huku Kinondoni ikipewa Sh milioni 200.

Aliwapongeza viongozi wilayani humo kwa kusimamia ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa na huku Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ikitoa fedha pia na kuamua kujenga majengo ya ghorofa.

“Uongozi ni kufanya maamuzi siyo kulalamika. Rais Dk Samia alifanya uamuzi mgumu wa kutoa fedha hizi. Alitusaidia. Zamani kipindi kama hiki ingekuwa ni hekaheka ya kuwachangisha wazazi na walezi fedha za kujengea madarasa lakini sasa wazazi watakuwa na majukumu ya kununua vifaa vya watoto wao huku Serikali ikijenga shule na madawati,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe, alimhakikishia Mkuu huyo wa mkoa kwamba ifikapo Januari 9, 2023 ujenzi huo wa madarasa utakuwa umekamilika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Suleiman, alisema Novemba 8, 2022, halmashauri ilipokea Sh milioni 200 kutoka serikali kuu kujenga madarasa 10.

Alisema kutokana na ufinyu wa maeneo waliomba kibali Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kujenga ghorofa ambapo Kinondoni iliongeza madarasa 10.

Mwenyekiti wa bodi ya shule, Zainabu Mbilo pamoja na Mkuu wa shule hiyo, Agustina Magana, wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema uwepo wa makaburi katika eneo la shule ni kero.

Walisema wakati mwingine wanafunzi wakiwa darasani hushuhudia maziko, huku watu wakiimba na wengine wakilia.

HABARI LEO
 
Huu ni upumbavu. Hayo makaburi yalikuwapo kabla ya shule kujengwa?!

Au makaburi yamekuta shule tayari imeshajengwa?!

Kuna mambo ni kuendekeza kuchekeana. Ni nani aliyehusika katika utoaji vibali vya ujenzi au shule nataka kufahamu nini kilianza hapo ndipo tutajua shida imeanzia wapi.
 
Back
Top Bottom