Rais Samia usipite bila kusoma ujumbe huu

NAFIKIRE

JF-Expert Member
Sep 5, 2014
634
415
Mama Hongera tena hongera sana sana. Ninaamini bado sijachelewa sana kukupongeza kwa kazi kubwa uliofanya ndani ya miaka miwili iliyopita ya kuiongoza nchi yetu kwa uongozi wako uliotukuka. Hongera sana.

Mama ninakupongeza kwa kukamilisha miaka miwili ya uongozi wa nchi yetu ukiwa kama rais na amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama wa nchi yetu. Ama kweli umesimama imara na nchi ipo shwari na kazi inaendelea.Msemo maarufu wa siku hizi wanasema umeupiga mwingi mpaka umemwagika.

Mama umeupiga mwingi ndani na nje ya nchi yetu hongera sana .Watu waliowengi walidhani utakwama (mfume dume) ila umeweza tena umeweza sana; na watakaokataa ni wale wafurukutwa wa atake asitake tutaongeza muda -mimi ninasema mtake msitake mama ameifanyia haki nafasi yake na tupo nae mpaka 2030 mtake msitake.

Mama nasema tena hongera maana sasa wana wa Mungu wamepumua. Walipita kwenye kipindi kigumu mama miaka kadhaa iliyopita ,ni Mungu tu anajua maswaibu yaliowakuta nitakukumbusha machache mwishoni; ila ninaamini wameshasamehe na wapo na wewe wanasema ‘Kazi iendelee”

Mama nikupongeze kwa kusimama na watu wa Mungu,kweli ni wazi sasa wanapumua, mambo yao yanaenda, kazi zao na biashara zao zinaenda.Ama kweli hakuna kiongozi aliyesimama na wana wa Mungu akakwama.Ahsante mama kwa kuwaamini na kuendelea kuwapa nafasi.

Mama hongera kwa kuweza kusimamia miradi mikubwa iliyoachwa na baba Jesca; miradi inaendelea kwa kasi ile ile hongera sana. Mama nani asiyejua wasiokukubali walikuwa wanasubiri miradi hii mikubwa isimame waitumie kama fimbo yao ya siasa ila wazungu wanasema umewaprove wrong hongera sana.

Mama hongera kwa kudumisha na kuendeleza mahausiano ya kimataifa kwa viwango vya juu. Kwangu kwa upande huu umeupiga mwingi sana..Ninakumbuka hotuba yako kule umoja wa mataifa-mmh mama ngeli unaijua bwana-mnyonge mnyongeni haki yake mpeni..ulishuka mpaka nikasema kweli mama anaweza kweli kweli au nasema uwongo ndugu zangu

Mama hongera kwa uwekezaji mkubwa ulioufanya kwenye sekta za elimu na afya.Mafanikio ya matumizi mazuri ya fedha za UVIKO yameonekana.Kwa hili mama hongera sana..Niseme tu utake usitake tupo na wewe mpaka 2030 na ikiridhia tutaongeza muda

Mama wafanyakazi wa serikali huku mtaani wanatabasamu; wanasema hakuna kama mama-walimu na vishikwambi vyao ndio usiseme-wote wanasema kwa kauli moja kazi iendelee; uliyoyafanya kwao ni makubwa kwa miaka hii miwili.Waliopandishwa madaraja wanashangilia,(hapa kwenye kupandisha madaraja mama upaangalie vizuri-unaweza kukuta kunawaliopandishwa bila kukidhi vigezo-nasema wapo-fuatilia mjumbe auhuwawi); waliokuwa wamefukuzwa kwa vyeti feki wanasema nani kama mama, waliolipwa madeni yao nao wanashangilia ingawa wapo baadhi bado hawajalipwa madeni yao mama(angalia na hapa mama unaweza kukuta kuna madeni hewa).Waliopewa ajira serikalini wanasema mama mitano teno..Mama baba Jesca alifanya uhakiki wa vyeti vya watumishi na wewe fanya uhakiki wa watumishi waliopandishwa madaraja ujue kama kweli walistahili na waliolipwa madeni yao.

Mama kwa upande wa wafanyakazi kama ikikupendeza mama amia sasa kwenye ujenzi wa nyumba za wafanyakazi na kurahisisha upatikanaji wa vyombo vya usafiri kwa wafanyakazi wa serikali na mikopo isiyo na riba au yenye riba ndogo. Pia mama kuna wafanyakazi wa serikali hawakupita JKT na wanatamani kujiunga na jeshi hilo kwa mafunzo ya miezi mitatu ya kizalendo-naomba uwape nafasi mama kwa kuanzisha oeperesheni Samia kwa wafanyakazi wa serikali.

Mama jeshi la akiba la nchi yetu kwa maana ya askari mgambo wanafanya kazi kubwa sana ya ulinzi na usalama kwenye ngazi ya kijiji, mtaa, kata na hata wilaya. Ikikupendeza mama serikali yako ione sasa namna ya kuanza kuwalipa mishahara kama askari wengine.Pia mama ukianza kuwalipa wazee posho kama wenzetu wa visiwani utakuwa umeupiga mwingi sana; ebu litazame na hili.

Mama hongera kwa upande wa kilimo umefanya makubwa.Hasa hili la kutoa ruzuku ya mbolea hongera sana mama, vijana kupewa mashamba ya kulima hakika vijana hawatausahau uongozi wako.Ila mama hili swala la mfumuko wa bei za vyakula kusema kweli linatweza sana serikali yako..libebe hili mama upate mwarobaini wake. Mama kama tuna mamlaka ya kusimamia bei za mafuata na kupanga ; kwanini tusiwe na mamlaka (ewura) ya kupanga na kusimamia bei za vyakula sokoni bila kuingilia soko huru.Pia iwepo na mamlaka ya kusimamia bei ya vifaa vya ujenzi na vifaa vingine.

Mama hongera kwa upande wa utalii umefanikiwa sana.Wamiliki wa TOURS na hoteli za kitalii kule kaskazini, Zanzibar na sehemu nyigine za nchi kwa miaka hii miwili wamenufaika sana na biashahara hii ya utalii.Idadi ya Watalii wanaoitembelea nchi yetu baada ya ile filamu yako ya Royal tour imeongezeka mara dufu.Mama kwenye upande wa utalii kuna swala lilianzishwa kipindi cha baba Jesca la kuwa na maduka ya kuuza nyama za wanyama pori naomba liendelezwe-kwangu naona lilikuwa wazo zuri na sisi watanzania kwa kiasi Fulani tutanufaika na uwepo wa wanyama pori wengi ndani ya nchi yetu. Ila mama hili swala la vitalu vya kuwindia wanyama pori nalo ulitupie macho-unaweza kukuta tunapigwa sana upande huo. Mama pia hizi mbuga ambazo baba Jesca alikuwa anataka kuziinua viwango vyake; Burigi, Rubondo na Kigosi ebu mama uziangalie kwa macho mawili ili kuinua utalii ukanda wa Magharibi na kiwanja cha ndege Geita kipate wateja wengi.

Mama kwa upande wa nishati na madini tunakupongeza sana ulivyofanya kazi kubwa kwenye sekta hii kwa muda wa miaka miwili.Kubwa kabisa ni wewe kuendeleza mradi mkubwa wa bwawa la umeme la Mwl Nyerere na mabwawa mengine madogo kule kanda ya kusini na magharibi hongera sana mama.Ila mama mjumbe ahuwawi; hili swala la umeme kukatika mara kwa mara limekuwa doa sana kwenye serikali yako; litafutie nalo hili mwarobaini ninaamini katika; Tanzania ya umeme wa uhakika inawezekana chini ya uongozi wako mh rais.Mama ninakuomba kwa unyenyekevu mkubwa ebu hili swala la umeme kukatika mara kwa mara uliangalie tena kwa macho mawili; kwa mikoa ya kanda ya ziwa (hasa mkoa wa baba Jesca) limekuwa ni swala sugu. Mama tumia hata watu wako wa ulinzi na usalama kulichunguza hili labda kuna watu wanataka kuhujumu juhudi za serikali yako. Labda ndani ya Tinisco kuna masalia ya watu wa Kalimoni wanahukuhjumu uwezi kujua..Tena mama hawa tinisco huko kwenye mkoa wa baba Jesca wanasubiria wakati kunatukio kubwa labda la mechi ya Yanga na Mazembe ndio wanakata umeme..umeme kwa siku unakata zaidi ya mara kumi kama sio hujuma hii ni nini?(nasema uongo ndugu zangu)

Mama hivi karibuni nimekusikia ukiongea kuhusu kusomana kwa taarifa za tra na mamlaka ya bandari hili ni swala zuri sana mama..lifuatilie kwa nguvu zako zote..Kwa kufanya hivyo utaongeza makausanyo ya kodi pale bandarini sana..Pia mama ebu fuatilia kama risiti zinatolewa kwenye vituo vya mafuta zinasoma tra au ni ‘gosheni ‘..mama tumia vyombo vyako kufuatilia hilI na unaweza kukuta baadhi ya vituo vya mafuta vinavyotoa risiti hewa na vingi vinamilikiwa na wabonge wa bonge la januhuri. Mama una kazi; fuatilia hili anzia huko kanda ya ziwa, uende nyanda za juu kusini then Tanzania nzima.

Mama baba Jesca alianzisha mfumo mzuri sana wa masoko ya madini yanayochimbwa sehemu mbalimbali za nchi yetu. Naomba sana ulele msisitizo uliokuwepo mwazo wa biashara ya madini kufanyika ndani ya masoko haya uendelee. Ninaona kwa sasa kama msisitizo huo umedorora kidogo-Waziri wetu wa madini alisisitize hili kwa nguvu. Mama hii sekta ya madini bado unapoteza fedha nyingi sana; kuanzia kwenye uchimbaji mpaka kufika sokoni.Kuna vitozo vingi sana ambavyo kiukweli havifiki kwenye mfuko wa serikali vinaishia kwa maafisa madini na viongozi wengine wa huo mnyororo.

Ni wakati sasa mamlaka inayohusika na uchimbaji na biashara ya madini ikapunguza au kumaliza kabisa mianya ya upotevu na utoroshaji wa madini.Mama sekta ya madini ukiisimamia vizuri itaongeza pato la taifa kwa kiwango kikubwa sana.

Mama sina taarifa kama serikali imeshaanza kutunza madini ya dhahabu kwenye benki yetu kuu.Kama tayari hongera sana.Kama bado ninashauri serikali yako sikivu ianzishe mchakato wa kuweka akiba ya madini ya dhahabu kwenye benki yetu kuu..pamoja na madini mengine ikiwezekana.

Mama kwa upande wa sekta ya usafirishaji nikupongeze tena na tena kazi kubwa imefanyika..Kubwa kuendelea kwa mradi mkubwa wa reli ya mwendo kasi, hongera sana mama; pili ujenzi wa meli kubwa kwenye ziwa Victoria na maziwa mengine, tatu ujenzi wa daraja la busisi na ujenzi unaendelea wa bomba la mafuta kutoka Uganda mama hongera sana..Miradi yote hii mikubwa imeingiza fedha nyingi sana kweye mifuko ya watanzania na hata wageni kwa kuongeza mzunguko mkubwa fedha sehemu miradi hii inapofanyika..Eti mama ile stand ya mabasi kule nyumbani kwa baba Jesca mbona kama inasusua, sema neon mama stand hii ikamilike kama alivyokuwa anataka baba Jesca.

Mama kwa upande wa michezo hongera sana kwa kuleta hamasa kubwa kwenye mpira wa miguu-mchezo pendwa hapa Tanzania.Mama kama ikupendeza jenga viwanja vikubwa vya mpira wa miguu na michezo mingine kule Kigoma, Shinyanga au Mwanza, Tabora ,Mbeya au Katavi, songea, Lindi au Mtwara, Kilimanjaro na Dodoma ili ndani ya uongozi wako Tanzania iandae mashindano makubwa ya mpira wa miguu Afrika..Hili kwa uongozi wako linawezekana mama.

Mama sasa nikukumbushe baadhi ya mapito waliopitia watu wa Mungu siku wanazoziita za giza zilizopita..Mama nani asiyekumbuka wana wa Mungu walivyobomolewa nyumba zao kule Kimara na kuharibiwa biashara zao na mali zao nyingi.Mama uwawangalie hawa watu kwa jicho la huruma kama kuna hila yoyote iliyofanyika dhidi yao, basi wapewe fidia wanaostahili fidia.

Mama tunakumbuka mwana wa Mungu kule Tanga alikuwa boss wa katani mama aliteseka mahabusu mpaka akafariki.

Mama tunakumbuka mwana wa Mungu mwandishi-mtu wa huko kagera aliteseka mahabusu mpaka mama yake akafa na akashindwa hata kwenda kumzika.

Mama kuna mwana wa Mungu kule Dodoma alijipiga risasi –enzi februari akiwa waziri baada ya viroba vyake kuzuiwa kuingia sokoni. Jamani, nani asiyekumbuka sakata la vifaranga vya kuku kuchomwa moto kule mpakani.

Mama nani asiyekumbuka mwana wa Mungu kule Musoma, tajiri wa mabasi alivyopambana na watekaji waliokusudia kumpoteza.

Mama nani asiyekumbuka bosi wa timu kubwa hapa Tanzania alivyotekwa na baba yake kuomboleza kwa huzuni kubwa, ama kweli tulipita kwenye wakati mgumu.

Mama nani asiyekumbuka mwanaccm kindakindaki aliyepambana usiku na mchana na Comrade Kinana kuiweka ccm madarakani-Ndugu Nape alivyotishiwa kwa bastola mchana kweupe.

Mama nani asiyekumbuka mwana wa Mungu na kada maarufu wa chadema kule mkoa alikotoka baba Jesca alivyouwawa kwa ukatili mkubwa mchana kweupe. Rest in peace Mawazo. Mama ninakuomba uingalie familia ya huyu kamanda mawazo kwa jicho lako la huruma. Serikali imsomeshe mototo aliyeachwa.

Mama nani asiyekumbuka mwanasheria wa chadema alivyopona kufa kule Dodoma na mirisasi aliyomiminiwa na watu wasiojulikana. Siku ile ilikuwa giza kubwa kwa usalama wa nchi yetu. Ahsante tunakumbuka ulivyofika Nairobi kumjulia hali kiongozi wa makamanda. Hongera sana ule ndio utu.

Mama nani asiyekumbuka akina Ben Saanane na Yule mwandishi wa habari hawaonekani mpaka leo-mama zifute machozi familia za Ben saanane na mwenzake.Familia hizi zimepita kwenye huzuni kubwa sana ni Mungu mwenyewe anajua. kumbukwe pia na familia ya Akwilina Yule mwanafunzi wa chuo aliyeuwawa kwa risasi Dar..uifute machozi.

Mama nani asiyekumbuka wana wa Mungu wenye maduka ya kubadilisha fedha walivyoporwa fedha zao na maduka yao kufungwa kwa hila kubwa. Nikupongeza nimemsikia waziri Nape akisema umewarudishia fedha zao hongera sana mama

Mama nani asiyekumbuka Mr 2 moto chini alivyoteseka gerezani mpaka mama yake akafariki.. Mama ni mengi ila wana wa Mungu sasa wamepumua. Jina la Bwana libarikiwe.

Mama nani asiyekumbuka bustani ya kamanda wa anga ilivyoharibiwa kwa hila kule hai, na matajiri wa mabasi kutuhumiwa kwa tuhuma za uongo za kutaka kuhujumu miondombinu ya reli-hongera Hamduni kamanda wa polisi wakati huo ulilikataa hili mchana kweupe.

MAMA MIMI NI SHABIKI WAKO KINDAKINDAKI(AKA CHAWA WA MAMA SAMIA) NA NI RAIA MZALENDO WA TANZANIA NA NINAIPENDA NCHI YANGU. NINAKUPONGEZA SANA KWA KAZI YAKO NZURI ILIYOTUKUKA YA KUIONGOZA NCHI YETU .MUNGU AKULINDE, AKUJALIE AFYA NJEMA NA HEKIMA YA KIPEKEE UNAPOONGOZA WATU WA MUNGU WA TANZANIA.

MUNGU IBARIKI AFRIKA; MUNGU IBARIKI TANZANIA.

AHSANTE
 
MAMA MIMI NI SHABIKI WAKO KINDAKINDAKI(AKA CHAWA WA MAMA SAMIA)
Nimecheka sana🤣. Umechagua kiongozi akuletee maendeleo, wewe umeamua kuwa Chawa wake. Hivi kura yako ipo kwa kuwa Chawa? au ipo kwa kuchagua kiongozi mwenye kuleta maendeleo kwako na kizazi kijacho? kwa maendeleo ya watanzania wote?.
 
Back
Top Bottom