Rais Samia aleta ahueni ya maisha

Billal Saadat

Senior Member
Nov 30, 2022
169
356
SERIKALI imetangaza kushusha bei za baadhi ya vyakula na vifaa vya ujenzi nchini, lengo likiwa kupunguza makali ya maisha kwa Watanzania. Katika hatua hizo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pia ametoa kibali kwa wafanyabiashara wa ndani, kuagiza mchele tani 90,000 huku akiiagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kutoa chakula katika Maghala ya Serikali na kuuza kwa bei ya ruzuku kwa wafanyabiashara.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, alisema tangazo la ahueni ya bei hizo za bidhaa, litaanza wiki ijayo kesho kutwa Jumatatu.

Kwa mujibu wa Waziri Dk. Kijaji, lengo la Rais Dk. Samia ni kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na ujenzi ni kuinua uchumi pamoja na kipato kwa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla.

Alieleza kuwa, Rais Dk. Samia, ameonya ongezeko la bei ya vyakula vyenye uhitaji katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ikiwemo sukari na ngano kwa kuwa, hakuna uhaba wa bidhaa hizo huku akizitaja bidhaa na bei elekezi.

MAHINDI
Alisema bei ya bidhaa hiyo kwa mwezi Februari ni kati ya sh. 750 na 1,750 kwa kilo, huku bei ya chini haijaonyesha mabadiliko wakati bei ya juu, imepanda ikilinganishwa na ile ya Januari mwaka 2023, ambayo ilikuwa kati ya sh. 750 na 1,600.

Waziri Dk. Ashatu alifafanua kuwa, serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na ongezeko hilo la bei ikiwa ni pamoja na kufungua vituo vya kuuzia mahindi yake katika mikoa 15 na halmashauri mbalimbali nchi nzima kwa wastani wa bei ya sh. 680 hadi 900, ambapo hadi kufikia Januari 31, 2023 jumla ya tani 29,084 ziliingizwa sokoni.

“Bei hizo za chini zipo katika Mikoa ya Iringa, Songwe, Njombe na Ruvuma na katika maeneo yote ambayo Serikali imepeleka mahindi ya bei ya ruzuku, wakati bei ya juu ipo katika Mikoa ya Kigoma, Mara na Lindi.
Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na ongezeko hilo la bei ikiwa ni pamoja na kufungua vituo vya kuuzia mahindi katika mikoa 15 na halmashauri mbalimbali nchi nzima kwa wastani wa bei ya shilingi 680 hadi 900 kwa kilo, ambapo hatua zilizochukuliwa hadi kufikia Januari 31, 2023 jumla ya tani 29,084, zimeingizwa sokoni.

UNGA WA MAHINDI
Aidha, bei ya unga wa mahindi kwa Februari ni kati ya sh. 1,500 na 2,100 kwa kilo, haijabadilika ikilinganishwa na bei ya Januari mwaka 2023. bei ya chini ipo katika Mikoa ya Geita na Manyara na bei ya juu ipo Mikoa ya Kigoma na Mara.

MCHELE
Dk. Kijaji alisema bei ya mchele kwa mwezi Februari ni kati ya sh. 2,500 na 3,500 kwa kilo, hiyo haijabadilika ikilinganishwa na bei ya Januari mwaka 2023.

“Mikoa yenye bei ya chini ni Iringa, Simiyu na Tabora, bei ya juu ipo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Manyara ambapo serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ongezeko la bei ya mchele pamoja na kutoa vibali vya kuingiza mchele kutoka nje ya nchi, hadi kufikia Machi, 2023, jumla ya tani 90,000 za mchele zinatarajiwa kuingia sokoni, hivyo kushusha bei iliyopo.

MAHARAGE
Bei ya maharage kwa Februari ni kati ya sh. 2,300 na 4,000 kwa kilo ambapo bei ya chini, imeshuka ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa sh. 2,400 kwa kilo na bei hiyo, inapatikana katika Mkoa wa Songwe na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Shinyanga.

VIAZI MVIRINGO
Alitaja bei ya viazi mviringo kwa mwezi Februari ni kati ya Sh. 1,000 na 1,750 kwa kilo, bei ya chini imepanda ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Sh.800 kwa kilo, bei ya juu ya Viazi Mviringo imeshuka ikilinganishwa na bei ya mwezi Januari 2023 ambayo ilikuwa Sh.2,000. Alisema bei ya bidhaa hizo, zilikuwa chini katika mikoa ya Songwe, Tanga na Mbeya na bei ya juu, ipo katika Mikoa ya Manyara, Mara na Ruvuma.

UNGA WA NGANO
Dk. Kijaji alisisitiza kuwa, bei ya unga wa ngano kwa Februari ni kati ya Sh. 2,000 na 2,500 kwa kilo, bei ya juu ya unga wa ngano imeshuka ikilinganishwa na bei ya Januari mwaka 2023 ambayo ilikuwa sh. 3,200 kwa kilo na bei hizo zipo katika maeneo mengi nchini na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Songwe.

SUKARI
Aidha, sukari kwa Februari ni kati ya sh. 2,700 na 3,000 kwa kilo na bei hiyo, imeonyesha uhimilivu ikilinganishwa na Januari, 2023 hali ambayo inatokana na jitihada zinazoendelea za kuvutia uwekezaji na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa sukari nchini ambapo bei ya chini, ipo katika mikoa ya Morogoro, Mwanza, Pwani na Singida na bei ya juu ipo, katika mikoa ya Ruvuma, Manyara na Lindi.

MAFUTA YA KUPIKIA
Waziri Dk. Kijaji aliongeza kuwa, bei ya mafuta ya kupikia ya Alizeti kwa Februari ni kati ya sh. 4,750 na 7,800 kwa lita. Vilevile, bei ya mafuta ya kupikia ya Mawese (Korie na Safi) ni kati ya sh. 4,500 na 7,250 kwa lita, aidha bei hizo zimeonesha uhimilivu ikilinganishwa na Januari, 2023 na bei ya chini ya mafuta ya kupikia ya Alizeti, ipo katika mikoa ya Manyara, Morogoro na Singida na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Mara.

1. MWENENDO WA BEI ZA VIFAA VYA UJENZI
Akizungumzia mwenendo wa bei za vifaa vya ujenzi kwa mwaka 2023, alisema zimeendelea kushuka kutokana na kuimarika kwa uzalishaji wa ndani wa bidhaa hizo, pamoja na usimamizi madhubuti wa mwenendo wa soko la bidhaa uliofanywa na Wizara na taasisi zake.

SARUJI
Alisema bei ya saruji kwa Februari ni kati ya sh. 14,750 na 23,500 kwa mfuko wa kilo 50 na bei hiyo, imeshuka ikilinganishwa na ile ya Januari 2023. Mikoa yenye bei ya chini ni Tanga, Dar es Salaam, Mtwara na Pwani, bei ya juu ipo katika mikoa ya Mara, Kigoma na Katavi.

NONDO
Kuhusu nondo, Waziri Dk. Ashatu alieleza bei ya nondo milimita 10 kwa Februari, ni kati ya sh. 16,100 na 25,000 ambayo imeshuka ikilinganishwa na bei ya Januari 2023, ambayo ilikuwa sh. 17,500. Bei ya juu ya nondo imepanda ikilinganishwa na bei ya Januari mwaka 2023 ambayo ilikuwa sh. 23,000.

“Bei za chini zipo katika mikoa ya Kilimanjaro, Iringa, Mwanza na Tanga na bei ya juu, ipo katika Mkoa wa Lindi huku bei ya nondo milimita 12 kwa Februari ni kati ya shilingi 22,000 na 28,000, ambapo bei ya chini, imeshuka ikilinganishwa na ile ya Januari 2023 ambayo ilikuwa shilingi 23,000 kwa nondo. Bei za chini zipo katika Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, za juu zipo katika Mkoa wa Katavi,” alisema.

BATI

Dk. Ashatu alitaja bei ya bati nyeupe ya geji 30 kwa Februari ni kati ya sh. 22,000 na 30,000, bei ya chini ya bati imepungua ikilinganishwa na ile ya Januari, mwaka 2023 ambayo ilikuwa sh. 22,500, bei ya chini ipo katika Mikoa ya Tanga, Songwe, Kilimanjaro Singida na Ruvuma na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Njombe.

2. SABUNI
Alisema Serikali inatambua umuhimu wa bidhaa kama sabuni, hivyo sabuni aina ya Jamaa, White wash na MO kwa Februari ni kati ya sh. 2,500 na 4,000, kwa mche na bei ya chini ipo katika Mkoa wa Simiyu na bei ya juu ipo katika Mkoa wa Mbeya.

“Bei ya Sabuni aina ya Takasa, kiboko na Kuku kwa Februari ni kati ya sh. 1,200 na 3,250 kwa mche na bei ya chini, ipo katika Mkoa wa Mara na bei ya juu ipo mikoa ya Ruvuma na Tanga.
“Sabuni za Magadi kwa mwezi Februari ni kati ya sh. 1,000 na 3,250, sabuni zipo aina mbili nazo ni miche miembamba na miche minene, bei ya chini ipo katika Mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma, bei ya juu ipo katika Mikoa ya Dodoma na Mara.

Alisisitiza kuwa, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaendelea kufanya tathimini ya mwenendo wa bei za mazao ya chakula na bidhaa muhimu nchini, kwa lengo la kutoa taarifa na kufanya uamuzi utakaochangia kukuza uchumi na kipato katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla.

“Wizara inaendelea kuratibu ukusanyaji wa takwimu za bei za mazao na bidhaa muhimu kama vile vyakula na vifaa vya ujenzi kutoka katika masoko yaliyopo katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kupitia wakusanya taarifa za masoko (market monitors) na maofisa biashara wa mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, takwimu hizi husaidia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), katika ukokotoaji wa kiwango cha mfumuko wa bei kila mwezi na kuweza kufanya tathmini ya upatikanaji wa mazao na bidhaa nchini.

Dk. Kijaji alisema Serikali itaendelea kulinda maslahi ya wadau wakiwemo wazalishaji, wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa husika na kuwataka wafanyabiashara kuendelea kuzingatia misingi ya ushindani wa haki; kuunga mkono jitihada za ukuaji wa uchumi kwakuwa wizara kupitia Tume ya Ushindani (FCC), itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 na Kanuni za Ushindani za mwaka 2018, kwa lengo la kumlinda mlaji na kushajihisha ushindani.

“Nitoe rai kwa wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuongeza jitihada za uzalishaji wa bidhaa kwa ubora unaohitajika sokoni. Kumekuwepo na malalamiko ya watuamiaji wa bidhaa zetu za viwandani kuhusu ujazo na hata ubora wa bidhaa hizo. Niwatake Wakala wa Vipimo Tanzania kufanya Ufuatiliaji wa karibu juu ya malalamiko haya na hatua madhubuti zichukuliwe kwa wote watakaopatikana na kosa la kuzalisha bidhaa chini ya kiwango na ujazo unaohitajika ulioonyeshwa kwenye vifungashio.

KUELEKEA RAMADHAN

Alisema katika kuelekea na kuanza kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Kwaresma, ni matarajio ya Serikali bei ya bidhaa zote zinazotumika kwa wingi katika kipindi hicho hazitopanda, hivyo amewataka wazalishaji wa sukari kuzingatia agizo hilo.

“Tumekuwa na vikao vya pamoja na kwa umoja wetu, tumekubaliana tuna sukari ya kutosha ndani ya nchi yetu, hivyo hatutarajii kuona bei ya sukari inapanda pia bei ya unga wa ngano imeonyesha kushuka ndani ya miezi hii miwili, hivyo hatutarajii kuona ikipanda tena kwani Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwa na bidhaa hii ya kutosha ndani ya nchi yetu,” alisema.

Aliongeza kuwa, yapo maeneo ndani ya nchi yameanza kuvuna maharage hivyo serikali haitarajii kuona bei ya bidhaa hiyo muhimu ikipanda tena.

DK.SAMIA ATOA VIBALI VYA MCHELE

Kuhusu mchele, Waziri Kijaji alieleza Rais Dk. Samia, ametoa vibali vya kuingiza nchini tani 90,000 ambazo zitaanza kuuzwa kwa bei elekezi ya Serikali ndani ya mwezi ujao, hivyo katika bidhaa hiyo, wanatarajia itashuka ndani ya wiki mbili zijazo.

“Niendelee kuwahakikishia Watanzania wote kwamba, Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti katika maeneo yote ambayo yanaonekana kuchangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ili tuendelee kubaki kwenye wigo wa mfumuko wa bei tuliokubaliana ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika,”alisema.

Alisema ni muhimu jamii kutambua mwenendo wa bei za bidhaa za vyakula kwa nchi jirani kutokana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake katika mavuno ya mazao muhimu ya chakula; kama mchele, mahindi, maharage na viazi mviringo, kwani bidhaa hizo katika nchi jirani yamekuwa makubwa kuliko uzalishaji hivyo, kuchangia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula nchini na nchi jirani.

Alisisitiza, bei za vyakula katika nchi nyingi duniani zimepanda hivyo, mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ukilinganishwa na nchi jirani, ambapo kwa Tanzania kiwango cha mfumuko wa bei ni asilimia 4.9 kwa Januari mwaka 2023 ikilinganishwa na asilimia 9.1 ya kiwango cha mfumuko wa bei nchini Kenya, asilimia 10.4 nchini Uganda na asilimia 21.7 nchini Rwanda kwa Januari, 2023.

#MamaYukoKazini
 
Kumbe huwa wanafanya makusudi kutukaanga huku wenyewe wakila na kunywa buree
Kweli CCM ni wachawi sana
 
Back
Top Bottom