Rais Magufuli ameboresha uwekezaji wa kimkakati Tanzania

Oct 6, 2020
27
50

UONGOZI WA RAIS MAGUFULI UMELETA UWIANO KATI YA UWEKEZAJI WA KIMKAKATI NA HUDUMA ZA JAMII

Ni habari njema katika utekelezaji wa sera za maendeleo ya Taifa pale nchi yetu ya Tanzania inapoingia katika uchumi wa kati. Lakini habari ya kutia moyo zaidi ni kwa Uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuzidi matarajio ya malengo ya utekelezaji wa sera za maendeleo ya nchi hii kwa kuifanya nchi ifikie katika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda wa malengo kufikia. Kauli ya Hapa Kazi Tu, imeonyesha matunda, na ama kwa hakika, kazi inaleta hamasa zaidi kwa watekelezaji pale wanaposhuhudia matunda yake.

Lakini kwa Rais Magufuli na Serikali yake kazi hii haikuwa nyepesi. Siku za hivi karibuni tulisikia malalamiko yaliyochochewa na baadhi ya wanasiasa wakiutuhumu uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuendesha siasa za kujinyima na kujibana sana kiuchumi huku pesa zikielekezwa kwenye miradi wanayoiita white elephant projects yaani miradi isiyotekelezeka. Waswahili wana methali isemayo ‘akutukanaye hakuchagulii tusi’.

Lakini methali hii inarandana na msemo wa mtu anayekuchukia hakuchagulii jina maana atakuita jina lolote alimradi amekuudhi. Kwa maneno mengine watu hawa walishawishi tuikatae kaulimbiu ya HAPA KAZI TU na wakaanzisha ya kwao ya KAZI NA BATA. Lakini ukifanya tathmini ya kina utagundua kuwa kauli mbiu yao ya KAZI NA BATA ilikuwa propaganda za kisiasa tu. Makala haya yatadadavua kwa kina mapungufu ya propaganda hii na kuonyesha kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati, uongozi wa Rais Magufuli umewekeza katika maendeleo ya watu.

Kwanza nianze kwa ufafanuzi juu ya hii miradi mikubwa na ya kimkakati. Tanzania tunapaswa kujivunia uthubutu na uthabiti wa Rais Magufuli katika kuianzisha na kuitekeleza miradi hii. Kwa mfano, ujenzi wa reli kwa kiwango chaStandard Gaugeni mradi wa kimkakati ambao utachangamsha sana uchumi wetu. Kama nchi tumekuwa na utegemezi mkubwa sana wa barabara kusafirisha abiria na mizigo. Ndio maana ajali zinaongezeka, barabara zinaharibika sana kila leo na kuathiri uchumi wetu. Wakulima kule kijijini wamekosa faida katika mazao yao kwa kuwa miundombinu ya usafirishaji wa mazao na pembejeo ni finyu.

Reli ni suluhisho la kudumu kwa kero hizi. Lakini pia reli hii itasafirisha mizigo nchi jirani za Burundi, Rwanda, DRC na Uganda na kuleta hamasa kubwa ya matumizi ya bandari zetu. Watanzania wazalendo hatuna budi kumuunga mkono Rais Magufuli katika ujenzi wa Reli ya standard gauge ya Mtwara — Mbamba Bay na matawi ya Mchuchuma na Liganga sambamba na uboreshwaji wa bandari ya Mtwara ili kuwafanya watu wa Malawi, wapatao takribani milioni 19 watumie bandari yetu. Miradi hii ya reli ya kisasa ni uwekezaji utakaoleta faida kubwa kwa nchi yetu.

Pili, uboreshaji wa shirika la ndege (ATCL) kulikotokana na manunuzi ya ndege mpya na kuanzishwa kwa vituo vya ndege nje na ndani ya nchi ni jambo muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wetu na katika kuchagiza ukuaji wa sekta ya utalii nchini. Sote tunatambua kuwa Tanzania kwa hakika inaongoza barani Afrika kwa vivutio vya utalii. Hivyo kufufua shirika la ndege kumetufanya, kama nchi, tulikamate soko letu la ndani baada ya kuanzisha vituo vya ndege vya ndani 8 zaidi kufikia jumla ya vituo 13. Uwekezaji huu wa kimkakati unarahishisha huduma ya kusafirisha watalii nchini lakini pia kuwezesha usafirishaji wa haraka wa rasilimali muhimu na watu katika sekta zingine.

img-20190115-wa0038.jpg

Pamoja na uwekezaji mkubwa ambao Serikali inafanya katika ujenzi wa barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya kwa kiwango cha lami na madaraja makubwa hapa nchini; pia ukarabati wa reli za zamani; na ujenzi wa meli na vivuko vyote vikilenga kufungua na kurahisisha usafirishaji nchini, lakini msomaji wangu utakubaliana nami kuwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, ni wa kimkakati mno kwa masilahi mapana ya nchi yetu. Bwawa hili lenye uwezo wa kufua umeme wa MW 2,115 utaiwezesha nchi kupata umeme wa uhakika lakini pia utawasaidia wananchi kunufaika na huduma ya nishati hii muhimu kwa gharama nafuu. Lakini mwisho wa siku kama kauli mbiu yetu ya Tanzania ya Viwanda inavyohamasisha, upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa kutosha utasaidia kukuza uchumi wa viwanda vikubwa na vidogo.

Pamoja na uwekezaji huu mkubwa, wa kimkakati na wenye tija kwa ukuaji wa uchumi, bado Serikali ya Rais Magufuli imefanya uwekezaji katika huduma na maendeleo ya watu kwa mafanikio makubwa. Watu wanaodai serikali hii haijawekeza katika huduma za jamii wanapiga porojo tu. Kwa mfano, Mtakumbuka kuwa, ripoti ya Mkutano wa Umoja wa Kimataifa juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD, 2018) wanaofanya tathmini ya maendeleo ya nchi maskini zaidi duniani, yaani Least Developed Countries iliielezea Tanzania kuwa ilikuwa imeshavuka katika kigezo cha uhimilivu wa kiuchumi (yaani economic vulnerability Index) lakini bado nchi yetu ilikuwa imekwama katika vigezo viwili ambavyo ni pato la wastani la kila Mtanzania lililosimama kwenye Dola za Kimarekani 902 na kigezo cha ustawi wa rasilimali watu yaani Human Assests Index ambacho tulikuwa chini ya kizingiti cha kufikia lengo la kuingia katika uchumi wa kati.

Kazi ngumu na yenye kuhitaji fikra na upeo mkubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano imefanikisha kuleta mabadiliko makubwa katika vigezo hivi viwili vilivyobaki. Nataka niwakumbushe tu Watanzania kuwa, kwa mujibu wa UNCTAD, kigezo cha ustawi wa rasilimali watu kinagusa maeneo matano ikiwemo: vifo kwa watoto chini ya miaka mitano; uandikishwaji wa wanafunzi shuleni; kujua kusoma na kuandika kwa watu wazima; Vifo vinavyotakana na uzazi; na utapia mlo. Serikali imefanya uwekezaji wa kuridhisha katika huduma ya mama na mtoto ambapo vituo 487 vimejengwa nchi nzima.

Uwekezaji huu umeongeza idadi ya akina mama wanaojifungulia hospitali kutoka asilimia 64 mwaka 2015 hadi 83 mwaka 2020, na muhimu zaidi idadi ya vifo vya wachanga vimepungua kutoa 25 hadi 7 tu kwa jumla ya watoto 1,000. Katika kigezo cha utapia mlo, Serikali imetekeleza miradi ya lishe nchini kwa matokeo makubwa mno. Kwa mfano, hali ya udumavu kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano imepungua kutoa asilimia 34.7 hadi 31.8 wakati huo huo ukondefu umeshuka kutoka asilimia 3.8 hadi 3.5.

Ongezeko la uandikishwaji wa wanafunzi shuleni ni moja ya mafanikio makubwa ya sera ya elimu bure inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano na ongezeko hili linaanza na idadi za shule za msingi na sekondari lakini pia idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa mashuleni. Kwa mfano, kwa shule za msingi undikishwaji umeongezeka kutoka 8,298,282 mwaka 2015 hadi 10,938,156 mwaka 2020. Na kwa sekondari uandikishwaji umeongezeka kutoka 1,648,359 mwaka 2015 hadi 2,185,037 mwaka 2020.

Mbali na hivi vigezo vya Mkutano wa Umoja wa Kimataifa juu ya Biashara na Maendeleo, Serikali pia imesambaza umeme vijijini kupitia mradi wa REA kwa mafanikio makubwa kutoka vijiji 2,081 mwaka 2015 hadii vijiji 9,112 mwaka 2020. Lakini pia imesambaza huduma ya maji safi na salama mijini na vijijini kwa mafanikio makubwa na kuweza kupunguza magonjwa ya milipuko yatokanayo na ukosefu wa maji. Matunda ya wazi kabisa na yanayoonekana kutokana na jitihada za serikali kuwekeza katika maendeleo ya watu ni kupungua kwa umaskini wa mahitaji ya msingi. Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mijini umaskini ulipungua kutoa asilimia 21.7 hadi 15.8 na vijijiji umaskini ulipungua kutoka asilimia 33.3 hadi 31.2 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Takwimu hizi za kuvutia zinakuja kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Seriakli ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli.

Image for post

Kama Rais Magufuli angekuwa ni kiongozi wa kubana matumizi kama inavyodhaniwa, angeelekeza nguvu zaidi kwenye miradi ya kimkakati tu na siyo kuwekeza katika huduma za jamii na maendeleo ya watu. Labda sifa inayomfaa Rais huyu si ya kubana matumizi ila ya kuhimiza matumizi sahihi ya pesa za kodi za wananchi. Tukumbuke kuwa pesa nyingi zilikuwa zinatumika vibaya ikiwemo kuendesha semina siziso na tija kwa taifa. Kwa mfano, kuacha kutumia pesa za Sherehe za Uhuru mwaka 2015 kulitufanya tuboreshe huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini pia kulisaidia tupate barabara pana na bora ya Moroko-Mwenge, na kupunguza msongamano wa magari uliokuwa unatupatia hasara kubwa ya matumizi ya mafuta na muda.

Sasa katika muktadha wa uwekezaji huu wa miradi ya kimkakati na uwekezaji katika huduma za jamii na maendeleo ya watu, unajiuliza huyu anayetaka ‘Kazi na Bata’ angepewa uhalali wa kisiasa wa kuongoza nchi na kutekeleza sera zake angefanya nini zaidi ya alichokifanya Amiri Jeshi wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli? Kwa hakika Watanzania wanapaswa kuyaelewa maono ya mbali ya Rais wao na hawapaswi kuyumbishwa kwa propaganda zisizo na uelekeo kwa maisha yao na maendeleo ya Tanzania.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom