Rais awe kwa ajili ya uhusiano wa kimataifa, tuwe na serikali mbili za ndani (edited)

KABERWA2013

JF-Expert Member
Feb 5, 2013
304
90
UTANGULIZI
Najitokeza kuandika walaka huu huku nikitambua ya kwamba Rais Nyerere alisema maadui watatu wa taifa ni ujinga, maradhi na umaskini lakini mimi Kaberwa nasema maadui wetu ni uvivu, uoga na njaa. Ukizaaa mtoto mwoga pia atakuwa mvivu, akikua anakuwa mjinga na mwisho wake ataishi na njaa matokeo yake atakuwa tegemezi ambao ndio unaoitwa umaskini na maradhi. Kama taifa litajikita katika kutengeneza mazingira ya kuwa na watoto wanaoweza kuthubutu basi taifa letu litakuwa limeweza uondokana na ujinga, umaskini na maradhi.

1. RAIS (kusiwe na makamu wa Rais)
Asitokane na vyama vya siasa bali agombee kwa aiba yake binafsi (mfano Rais wa Shirikisho la Ujerumani). Hatuitaji kuwa na Rais ambaye akiwa Ikulu anakuwa sultani maana familia na wapambe wake wanaona ni wakati wakupeta kwa kuanza kutumia madaraka vibaya, vimbwanga vya mtoto wa Rais ambaye kabla ya baba yake kuwa Rais hakuna aliyemfahahamu lazima vipingwe katika katiba mpya. Tuchague Rais watanzania kutegemea na mfumo wa dunia unaokuwepo, mfano katika kukabiliana na ugidi Wamarekani walimchagua Obama aliposema ataondoa majeshi ya nchi yao kutoka Afghastani, na mashariki ya kati kuondokana na vita vya Alkaida, na walimpa nchi ya Marekani kwa sababu alihaid kutumia diplomasia, tofauti na sera za Rais Bush ambaye wakati wake Wamarekani waliokua nje ya nchi walikuwa katika hatari ya vitisho vya kigaidi.

Bush alipeleka majeshi kupigana na magaidi lakini wakawa magaidi wakaanza kuwashabulia Wamerekani wa kawaida ilihali yeye akiruka na Airforce one huku wanzeke wakiwindwa kila kukicha popote walipo duniani. Kadhalika kuna huko USSR Rais Breznerv aliondolewa punde tu alipohudhuria kikao cha UN na kutishia Marekani kwa kiatu kugonga meza.

Katika swala la rais wetu tunahitaji kuchagua mtu ambaye kwa wakati fulani ataiweka nchi yetu katika diplomasia ya dunia kimataifa inayotawala kwa wakati huo. Rais wetu hatakuwa na hatimiliki katika kipindi chake madarakani kama ilivyo sasa hivi kwani tukiona diplomasia ya dunia imebadilika tunaweka rais mwingine inayeweza kuendana na dunia kwa wakati huo.

Wakati tunapompa mtu nafasi ya urais anatakiwa kujua kinachompeleka ikulu na kama akishindwa anakuwa tayari kujiondoa au kuondolewa. Watanzania kikatiba tutakuwa na haki ya kuweka na kuondoa rais wetu wakati wowowte bila kuulizwa na mtu wa n je. Katika utarartibu wa katiba tunayotaka kuiondoa rais wetu anapata miaka mitano ambayo hata asipofanya vizuri hakuna mtu wa kumuuliza na anajitahidi kuwa na urafiki binafsi na viongozi wa mataifa makubwa kama njia mojawapo ya kijiwekea kinga dhidi ya watu wake, anakuwa mungu Mtu. Tunataka madaraaka ya rais yasiingilie mihimili mingine ya ndani ya nchi. Rais ataishia kuwa mhimili wa amani na asijione na kuwa na wasiswasi kwa mambo yanayoendelea ndani ya nchi.

Wakati akiwa madarakani rais atashitakiwa iwapo atatumia madaraka yake vibaya na atahudhuria mahakamani kama mtu wa kawaida hadi mwisho wa kesi inayomkabili. Akipatikana na hatia atajiuzuru na nafasi yake itajazwa kwa utaratibu wa kawaida. Aidia hapa ni kwamba wakati akiwa katika madaraka yake rais hatapata muda wa kufanya makosa ya jinai au madai na kama itakuwa aliyafanya kabla ya kuwa rais sheria za uchaguzi zitakuwa zilimkataza na kama atakuwa aligushi sifa ambazo hakuwa nazo wakati wa uchaguzi basi atahukumiwa kwa kusema uongo. Lakini endapom atakiuka vifungu vya katiba ataweza kushtakiwa mahakamani akiwa
bado yu ofisini.

Rais baada ya kumaliza ngwe yake ataishi maisha ya kawaida akiwa na haki zote za msingi za raia na hatapewa ulinzi wa dola ataishi kwa pensheni kama watumishi wengine wa wakati huo na mshahara wa rais hautakuwa siri kwani siasa ni wito na si taaluma.Katika katiba ya zamani mishahara ya watumishi wa umma ni siri na hii inaongeza mianya ya kufanya ufisadi. Rais mstaafu atalazimika kulinda aiba yake katika jamii na akifanya makosa atashtakiwa kama raia wa kawaida. Hii imekuwa ikifanyika kwa wastaafu kama majaji, maaskofu, masheikh na watumishi wengine wa ngazi za juu.

Rais kama mhimili atategemea bajeti itakayopitishwa na bunge kutegemea na hali ya uchumi wa nchi. Katika hali ya katiba tunayoondoa kuna taasisi ambazo bajeti zake hazilingani na uchumi wa nchi. Kusema kuwa hata kama hali mya uchumi ni mbaya jeshi lazima wapate chao hata ikiwa ni pamoja na kulazimika kuacha vipaumbele vingine haitakubalika.

Aidha hapa ni kuwa na jeshi ambalo linaguswa na hali halisi ya maisha ya mtanzania nakujenga jeshi la kizalendo zaidi. Watu wanaweza kuogopa hii dhana ya kupunguza bajeti ya jeshi kwamba wanajeshi wanaweza kupindua nchi. Nataka kuwahakikishia kwamba katika dunia ya leo hakutakuwa na utawla wa kijeshi kwa vile hakuna mataifa ya leo yanayounga mkono tawala kama hizo na zimekwishatoweka (chukua mifano ya Komoro, Gaboni, Guinea hawa wanalazimika kufanya chaguzi za uongo ili waonekane ni tawala za kiraia).

Lakini pia uchumi wa nchi hautakuwa mikononi kwa rais kama ilivyokuwa bali utakuwa katika mikono ya wachumi kupitia BOT (nitaeleza majukumu ya BOT huko mbele) kutegemea na mwenendo wa uchumi wa dunia na hali ya uchumi wa nchi itakuwa inatolewa kwa watu wote kila mwisho wa mwezi. Aidia hapa ni kwa kila raia wa nchi yetu kuwa na fursa sawa katika kumiliki na kukuza uchumi na
kwahiyo hakutakuwa na wakulaumuwa Rais na taasisi zilizoko chini yake atakuwa msimamizi tu wa maadili katka kukuza uchumi na hawezi kuonekana kama sababu ya kuyumba kwa uchumi wa nchi.

Majukumu ya rais ni pamoja na kuhakikisha kuwa raia wote wanaielewa katiba ya nchi, haki zao za kikatiba na wajibu wao kwa maendeleo ya nchi. Hatutaki rais anayekuwa juu ya sheria na hakivunja katiba watu wananyamaza tu. Katika katiba iliyopo rais anaweza kuuza mlima Kilimanjaro alafu asiulizwe wala kufanywa lolote, hii inatokana na wapambe na washauri wake kumshinikiza ,angalieni
migodi ya madini.

Kwa walosoma shule za bweni mtakumbuka kwamba wanafunzi wengi hupenda kuwa viongozi wa bwalo la chakula badala ya kuwa viongozi wa mabweni kwa sababu kule kwenye mabweni kuna kusimamia usafi, kuripoti wanaokwenda disko usiku kazi ambazo ni za lawama ilihali kule bwaloni kuna uwezekano wa kula chochote wakati wowote. Katika katiba 1977 urais ni sawa na kazi ya bwalo kila mtu mlafi anataka kukimbilia huko.

Katika katiba hii rais wa namna hii watu wote watajiona sehemu ya rais wao kwa vile hatatokana na chama. Watu watakuwa tayari kumsaidia kulinda maliasili za taifa. Katika katiba ya 1977 watu wanakaa kimya au wanashiriki kuhujumu maliasili za taifa kwa kushirikiana na na wageni kwa sababu watu wanadhani kulinda maliasili ni kazi ya idara ya usalama wa taifa. Wanauona usalama wa taifa kama watoto wa ndoa na wao ni watoto wa kambo kwa hiyo jukumu la nchi si lao. (Hata usalama wa
taifa nao wanajiona ni watanzania zaidi ya wengine) hizi ni fikra fikara.

Katika katiba ya 1977 rais anakwenda ulaya bila kutumwa na nchi anajiamlia mwenyewe tu anachokwenda kufanya huko watu hawakijui na anatumia fedha za umma kusafiria kwa ajili ya mambo yake binafsi.

Watanzania si mali ya rais, rais ni mali ya watanzania na kumbukeni katika katiba ya 1977 vijana wanajitokeza kutaka kugombea uongozi. Naonya kwamba katika mfumo huu siasa ni mkusanyiko wa wat uwavivu wa kufiri ambao wako tayari kutumiwa na wenzao kwa manufaa Fulani kwa wakati Fulani na wakati ukipita watu hao wanawaacha solemba na kutafuta washirika wengine na kama wewe ni kijana utajikuta unapoteza muda wa kuzalishamali wakati bado una nguvu za kufanyakazi. Je, ni vyeme kuzalishamali ukiwa mzee ilihali huna nguvu za kutosha? Vijana msitekwe na jinamizi la siasa.

Katika katiba mpya siasa haitakuwa ajila bali utumishi wa wito kwa sasa ukiwa mwanasiasa ili utajirike lazima utumie nafasi yako kufisidi nchi na hilo halitakuwepo. Wafanyakazi katika idara ya Rais lazima wasifungamane wala kujuhususha na vyama vya siasa kwa
namna yeyote ile. Chini ya Rais kutakuwa na idara zitakazoongozwa na wakurugenzi watendaji kama ifuatavyo.


Diplomasia na mambo ya nje

Mwanasheria mkuu

Usalama wa taifa (atateuliwa na rais)

Jeshi la wananchi (atateuliwa na rais)

Polisi, magereza na uhamiaji

Elimu na Utamaduni (Muundo wa Elimu)

Maliasili na utalii na mazingira

Maadili ya umma

Nishati na madini

PPRA

Pensheni kwa wazee


Tume ya ajira na maslahi ya watumishi. Watendaji hawa wataomba ajira kwa tume maalumu ya ajira za juu katika taifa na utendaji wao
utaratibiwa moja kwa moja kwa wananchi. Tume ya ajira itafanya usaili wa wazi kwa waombaji wote na matokeo yanaweza kupingwa mahakamani na raia yeyote bila woga.

Katika kipindi cha bajeti mkuu wa kila idara atawasiliasha makadirio ya idara yake kwa bunge katika staili ambayo ataitetea mbele ya bunge. Kuhusu diplomasia na mambo ya nje tutakuwa na balozi pale panapolazimu kufanya hivyo. Katika mazingira ya sasa ambapo nchi karibu zote za ulaya zinatumia paspoti moja kuna haja gani ya kuedelea kuwa na ofisi za kibalozi katika kila nchi ya ulaya ikiwa mtu anaweza kutoka Swedeni akenda kufanya kazi Denmark bila kuulizwa kwanini asihudumiwe na ubalozi ulioko katika nchi mojawapo. Kuna haja gani ya kuwa na ubalozi nchini Kenya au Uganda, Rwanda, Zambia, DRC, Malawi, Msumbiji wakati hawa wako mipakani na kama kuna Mtanzania anaishi huko tatizo likitokea simu zinapigwa nchini na anashughulikiwa na uhamiaji mipakani kwetu.

2. MHIMILI WA HABARI
Utaundwa na vyombo vyote vya habari kwa weledi watakaojiwekea ambapo kila aina ya chombo kinachoeneza habari kitatambuliwa yakiwemo magazeti,televisheni, redio, simu, intanet, blogu nk na vyombo hivi vitahusika katika mhimili huu. Kutokana na umuhimu wake mhimili huu utakuwa na sheria zake ambazo zitaelekeza namna ya utoaji habari za ndani na nje ya nchi.

Aidia ni kupata waandishi wa habari ambao hawatafungamana na mlengo wowote wa kisiasa. Hakutakuwa na chombo cha habari cha serikali. Vyombo vyote vitakuwa na nguvu sawa na vitapata maslahi kutegemea na jinsi vitakavyokubalika katika jamii. Kazi kubwa ya mhimili huu ni kuelekeza taifa katika malengo ambayo yatakuwa vipaumbelea na namna ya kuyafikia. Vipaumbele vya nchi sio mali ya wanasiasa au mtu mmoja binafsi bali ni sera ya nchi nzima bila kujari nani au chama gani kiko madarakani. Katika hali ya sasa mtu akiamka asubuhi atakuta muziki wa bongofleva katika televisheni au taarabu katika redio.

Miaka ya nyuma tunamkumbika S.S. Mkamba kwa kile kipindi cha mazungumzo baada ya habari ambacho kilikuwa na mafundisho makubwa, kumbuka michezo ya redio ama maigizo ya pwagu na pwaguzi ni vipindi ambavyo vilitumika kulea maadili ya jamii ya Kitanzania. Katika igizo la ngapulila vijana walihaswa kuacha kufikiria kuzamia meli kwenda ulaya jambo ambalo lilishamiri wakati ule, leo taifa lina janga kubwa la matumizi ya madawa ya kulevya lakini mhimili wa habari umetumika kwa kuwango cha chini sana kudhibiti hali tuliyonayo ya madawa haya.

Hatuwezi kusahau simulizi za mama Sango Kipozi katika mama na mwana ambazo kwa baadhi yetu zimebaki ni zana za maarifa kwa
mambo yetu ya kila siku, zamani mabibi na mababu walitumika kufunza jamii, kwa dunia ya leo baada ya kushindwa kuishi maisha ya kufunzwa na mabibi na mababu ni wakati sasa mhimili wa habari kuchukua nafasi ya kulea jamii, tusiache kazi hii kwa viongozi wa madhehebu ya dini tu. Kutokana na kukosa mhimili wa habari ambao una dira kila kitu sasa kinatoka na kuingia katika jamii yetu bila
kuchujwa.

Tunahitaji kuwa na waandishi wa habari watafiti kwa maendeleo ya taifa letu katika nyanja zote. Kila chombo cha habari kitakubalika kutokana na habari kinazotoa. Kuna vyombo vya habari vitazungumzia uchumi, kilimo, biashara, masoko, fedha , utamaduni na michezo n.k au tasnia zote kwa pamoja. Kwa sasa tuna magazeti mengi ya michezo na yote yanaandika habari za ulaya, timu za Liverpool na Manchester zinafahamika kuliko kiwango cha mauzo ya riba katika soko la hisa , au bei ya nishati ya mafuta au bei ya dola katika burea ni change au bei ya mazao katika masoko makubwa ya taifa letu.

Uhuru wa habari tulionao umeliamisha taifa kutoka katika misingi yake halisi na kila mtu anatamani kuwa kama mtu aliyeko ulaya na wengine wanafikiria kwenda huko. Leo kuna magazeti yanayomilikiwa na watawala na yanatumiwa kuuhadaa umma kuhusu mambo nyeti ya taifa na hakuna hatua za kuchukua. Katika katiba mpya hakuna mwanasiasa, wala mfanyabiashara wala taasisi za dini zitakazoruhusiwa kumiliki vyombo vya habari na kuvitumia kwa manufaa yake binafsi na yenye athari kwa jamii. Tunataka vyombo huru vya habari visivyo na maslahi kwa kundi fulani.

Viwe vinafichua na kuelezea mambo yote ya nchi kwa uwazi kadili inavyowezekana.Vyombo vya habari havitakuwa na mipaka katika maswala ya nchi. Kutokana na uweledi watakaojiwekea watakuwa wanajua nini cha kuandika na kipi kiachwe. Nafikiri mambo ya siri yatabaki ni yale yanayohusu ulinzi wa mipaka ya nchi nchi yetu na katika hili tuna JWTZ na tumewapa kazi ya kutulinda. Mambo mengine yote yatakayoitwa siri yatakuwa na nia mbaya kwa matumizi ya rasilimali za nchi yetu.

Uhuru wa vyombo vya habari unaweza kupatikana tu ikiwa na vyenyewe havitamilikiwa na watu au taasisi zenye maslahi binafsi badala ya taifa na kwa hiyo havitatumiwa na makundi hayo, lazima viwe huru kama mahakama. Mtu anaweza kumiliki vyombo vya habari lakini kuvitumia kwa maslahi yake ya kisiasa au kibiashara yatahesabika ni makosa na kuvunja katiba. Lazima tuwe na vipindi vya keleimisha jamii mfano ni kipindi cha vioja mahakamani kinachorushwa na KBC kinafundisha watu jinsi ya kushiriki katika mwenendo wa kesi katika mahakama.

3. MHIMILI WA FEDHA
Huu utakuwa mhimili huru kabisa ambao utashirikisha asasi na taasisi zote za fedha.Gavana wa fedha atachaguliwa na wachumi wenzake baada ya kuomba na kusailiwa na Tume ya ajira za juu ya taifa katika utaratibu ambao wachumi wataona unafaa na hatakuwa mteule wa rais. BOT lazima iendeshwe na kuwa benki kubwa kama IMF, ADB, au WB kwa kutumia rasilimali zetu hata iweze kutoa mikopo kwa nchi nyingine punde uwezo ukiruhusu kwa manufaa ya taifa. Hii inawezekana kwa sababu mfumo wa BOT ni sawa na wa benki zingene isispokuwa tofauti ni kwamba wateja wa BOT ni mabenki badala ya watu binafsi.Kama CRDB inakopesha wateja wake kwanini BOT isikopeshe nchi kama Komoro na ikatoza riba.

Aidia hapa nikuipa uhuru BOT ili kuiwezwesha kumiliki uchumi moja kwa moja bila kuingiliwa na na wanasiasa. Uganda walipata kuwa na rais Idd Amin ambaye alimwamuru gavana wa benki ya Uganda print more money. Hapa Tanzania rais Nyerere ambaye hakuwa mchumi alikataa kugeuka jiwe aliposhauriwa na gavana Edwin Mtei kuhusu kukubali kushusha thamani ya shilingi dhidi ya dola ya
Kimarekani ili kukabiliana na uchumi uliokuwa umeathiriwa na vita ya Kagera. Laiti gavana Mtei angekuwa na nguvu za kikatiba yote haya yasingetokea na kama ungefanya makosa kwa kushusha thamani ya shilingi bila weledi angeadhibiwa kikatiba. Katiba hii mpya impe gavana madaraka ya mwisho kuamua mambo kama hayo na mahakama peke yake yaweza kutumika kuhoji uweledi wa
maamuzi yake.

BOT itatoa kwa uwazi mwenendo wa uchumi wetu kila baada mwisho wa mwezi. Itakusanya kodi zote kubwa zenye VAT, itasimamia kodi zinazitokana uwekezaji toka nje kama utalii, biadhara za kimataifa, mahoteli makubwa, bandari,biashara za ndege, meli, madini yote, uwindaji. Katika katiba ya 1977 baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakishirikiana na wawekezaji na kuwakingia kifua ili kuwawezesha kupora uchumi wa taifa. Kampuni moja simu za mkononi inabadili jina kila inapoona kipindi chake cha msamaa wa kodi kinakaribia kumalizika, BOT itakomesha mianya ya namna hii.

Mimi nikiwa mzalendo wa kisasa ninaamini kabisa kuwa nchi yetu inao wataalamu wa uchumi wazuri ambao tukiwapa uhuru wa kutenda kwa weledi watapeleka uchumi wetu kwa kasi ya ajabu kimaendeleo.Wanazo au kama hawana waweke sheria zao za weledi na mchumi akiteteleka anadhibiwa kisheria.

Biashara zote za kununua rasilimaliagizwa (import goods) ambazo Mungu akuijaria nchi yetu zisimamiwe na BOT moja kwa moja. Bidhaa kama petrol badala ya kuachwa kwa kuagizwa kibiashara na watu binafsi na kuilangua kwa wananchi ziwekwe katika kundi la bidhaa muhimu kwa taifa na zisimamiwe na BOT kutegemea na hali ya uchumi wa nchi.Nchi kubwa kama Marekani zimejiwekea utaratibu wa kuzipiga vita nchi za kiarabu na kuzipora mafuta na wala si mabepari na mabwanyenye wa huko walioachiwa kuagiza mafuta.Hii inasaidia kumonita bei ya mafuta ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi kwa nchi zinazotumia nishati hiyo.Vivyohivyo rasilimali zote ambazo hazipatikani Tanzania hazitakuwa sehemu ya kujitajirisha kwa watu wachache badala yake ziratibiwe na BOT moja kwa moja kutegemea na ukuaji wa uchumi wetu.

Ushuru wa forodha (bidhaa toka nje ya nchi) ni kazi ya BOT. Mikataba yote ya kimataifa kuhusu fedha, mikopo, misaada ya fedha toka nje ya nchi na mifoko ya fedha ya kimataifa zisimamiwe moja kwa moja na BOT kutegemea na uhcumi wa nchi.Hakuna mwanasiasa atakaeruhusiwa kwenda nje ya nchi kuomba misaada kama tunavyoona marais wetu walivyofanya. Rais wa nchi unakwenda kuomba msaada kwa niaba ya watu wako bila ridhaa yao ni kuidhalilisha nchi.

Mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi iandikwe kwa lugha ya Kiswahili na wageni walazimike kujua lugha hiyo. Mikataba yote ya aina hiyo itangazwa kwenye vyombo vya habari ili kila mwananchi ahoji uhalali wa masharti ya mikataba.

4. MHIMILI WA UWAZIRI MKUU WA TANGANYIKA /UWAZIRI KIONGOZI WA ZANZIBAR( HIZI NI SERIKALI ZA NDANI AMBAZO HAZITATAMBULIWA KIMATAIFA)

Mhimili huu ndio utakuwa mhimili wa wanasiasa ambao utajihususa moja kwa moja na mkate wa kila siku wa watu wetu.Maswala yote ya kuboresha maisha ya ndani ya nchi kama Haya yatakuwa chini ya hawa wanasiasa. Wazii mkuu/Kiongozi watapatikana kupitia uchaguzi wa vyama vya siasa kwa kila upande. Kila upande utakuwa na vyama vyake vya siasa na mfumo wake wa uchaguzi na hakutakuwa na uhusiano wowote wa kiutawala baina ya serikali hizi.

Serikali hizi kila moja itakuwa na akaunti ya katika BOT kama wateja wengine zinaweza kukopa kutoka BOT ili kutimiza ilani zao za uchaguzi na zitalipa mapato yao kutokana na kodi za ndani. Serikali hizi zitakusanya kodi za ndani ( tofauti na zile za BOT) ili kuweza kuendesha mambo yake. Asipotekeleza ahadi anaondolewa mara moja. Katika mfumo wa sasa watu wanapeana madaraka ya serikali/umma bila kujali uadilifu na uwajibikali wa mtu. Hata wasiofaa wamo kwa mfano tunaweza kuwa na waziri wa
uvuvi ambaye ni mmasai wakati hata hajui maisha ya samaki na si chakula kule anakotoka je mtu kama huyo ataipenda kazi hiyo.

Katika mfumo tulionao wa katiba ya 1977 kuna walaji wengi kuliko wazalishajimali, kuna wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halimashauri, wakuu wa mikoa, watendaji wa mitaa n.k ambao ukujumlisha nguvukazi iliyomo katika ofisi hizo na kulinganisha utendaji na gharama za uendesheji wa maofisi hayo ni hasara kwa nchi. Nguvu kazi yote hii inasubiri mshahara bila uzalishaji na kama ikibadilishwa kuwa wazalishaji katika ajira binafsi kama kilimo, uvuvi, ufugaji,viwandani n.k kadhalika hakika tutakuwa mbali. Matatizo ya serikali kushindwa kulipa mishahara katika muda muhafaka yanasababishwa na uwepo wa watumishi wengi wasiozalisha ambao wanakula bure mithili ya malikia wa nyuki na sisi wengine tunakuwa kama askari wanyuki kazi yetu kuwazalishia wale.

Wafanyakazi wengi katika mfumo wa sasa rutini zao ni kupokea taarifa/habari toka ngazi moja na kupeleka ngazi nyingine, na tarehe zikifika akaunti zao zinajaa siku zinasonga mbele. Huu ni mfumo unaotengeneza watu wavivu wanaokula bure na ndio sababu tuna njaa. Kuna watu wako katika ofisi za aina hii kwa sababu ya mfumo walioukuta na iwapo watapewa fursa wanaweza kuzalisha lakini sikatai kuwa kuna wengine wavivu ambao wanapenda kubaki katika mfumo huu wa kufanyakazi kidogo na kulipwa mshahara mkubwa. Lazima tufikirie kupunguza ajira za aina hii zisizo na tija kwa taifa. Mfumo huu wenye wafanyakazi wengi wa aina ya malikia wa nyuki sijui nani aliuanzisha unatengeneza waganyakazi wengi ridandanti na ndio maana wengi huwezi kuwakuta maofisini baada ya saa saba. Lakini pia kazi ya kusafirisha habari toka ngazi moja hadi nyingine kwa kutumia miguu umeondolewa na teknolojia ya kisasa TEKNOHAMA.

Maofisi haya sasa yanatakiwa kuajiri watu ambao kazi yao ni kutolea maamuzi maswala ya kiserikali yanayoletwa na wananchi na sio kutunza mafaili ambayo yanasubiri mtu mmoja kuja kutolea maamuzi maswala hayo na hii itaondoa urasimu wa mtu fulani tu kuwa ndiye mtendaji tu kwa mambo yanayohusu uhusiano wa jamii na serikali yake.Hata wale wanaopenda kuwa malikia wa nyuki waangalie mifano ya wenzao waliostaafu katika mfumo huu wanaishi maisha gani baada ya kustaafu kama si watu wa chini kwa sasa, walidanganywa na mfumo matokeo yake ni kuzalisha tabaka la wazee masikini lenye athari kwa uchumi wa taifa.

Ili kuunda mhimili huu vyama vya siasa lazima viwe na watu madhubuti wenye nia hasa ya kuwatumikiawananchi na wala visiwe vyama vyenye mitandao mikubwa mpaka mashina ya nyumba kumikumi ambayo hayana tija kwa taifa zaidi ya kujenga chuki za kisiasa za kuwagawa watanzania. Matokeo ya mashina ya nyumba kumi ni watu kuogopa kuzungumza maswala yanayoligusa taifa lao. Unakuta
chama kina mtandao na ndani ya mtandao kuna mtandao ambayo watu wazima wanakaa kuchimba mambo ya wenzao kwa majungu ambayo hayana tija kwa taifa. Vyama vya aina hii vinatumika kama vichaka vya kuficha waovu hasa vinapokuwa madarakani.Mitandao katika vyama vya aina hii inashiriki katika mapinduzi ya ndani ya chama ili kuhodhi madaraka na mali.

Inashangaza badala ya watu kufungua mashina ya maendeleo ya kufundishana namna nzuri ya kufanya ujasiriamali watu wanafungua mashina ya wakereketwa ambayo chini ya bendera wanajazana vijana wavivu, mateja wasio na dira ambao tangu asubuhi hadi jioni kazi ni kusifia chama chao huku wakikaba wapiti njia ili kupata chochote na polisi hawawezi kuchukua sheria wanaogopa bendera ile.
Mhimili huu utakuwa na kazi zifuatazo na viongizi wake watakuwa makatibu wakuu(si mawaziri)


Kilimo na chakula, mazao na masoko ya ndani

Afya na matibabu

Usambazaji maji safi na uondoaji majitaka

Barabara na usafirishaji

Biashara za ndani (ondoa zile za BOT) afya,

miundombinu,

mfumko wa bei za bidhaa n.k

Maslahi ya wafanyakazi

Maslahi ya walimu na wanafunzi

Biashara za ndani

Maslahi ya wakulima na ushirika Mambo hayo hapo juu yanawezwa kuachwa mikononi mwa wanasiasa ili washindanishe sera zao na
waonyeshe umaili na ubunifu ili kuinua maisha ya watu.

5. MHIMILI WA DINI
Tanzania itakuwa nchi inayotambua kwama MUNGU yupo. Itazitambua imani za tatu yaani madhehebu ya ukristo, uislamu na dini asilia. Kila mtu atakuwa na uhuru wa kuabudu dini hizi bila kuhathiri haki za binadamu. Katika uhuru wa dini wa sasa kuna madhehebu ambayo yanamwabudu Mungu tangu asubuhi hadi jioni na mengine ni hadi usiku wa manane. Madhehebu ya namna hii yanateka fikra za watu na kuwafanya kuacha kazi za uzalishajimali kwa vile muda mwingi unatumika katika ibada. Athari za madhehebu ya aina hii ni kuwa na walaji wengi kuliko wazalishajimali. Mwenyezi Mungu anasema aseyefanya kazi na asile kwani ata yeye alifanykazi siku sita ya saba akapumzikakuna. Kuna umuhimu wa kuwa na mhimili wa dini kuliangalia jambo hili kwa kina na kuweka utaratibu wa ibada ambao
unatoa nafasi kwa watu kupata muda wa kuzalisha mali badala ya kusihnda na kulala kwenye ibada kwa kutumia kisingizio cha kesheni mkiomba.

Waumini wa dini za asili wanazingatia sana swala la ibada na uzalishaji. Imefika wakati muafaka kwa viongozi wa dini kuhusia watu kuzalisha mali kwa kufanyakazi kwa bidii badala ya kufichama kwenye majengo ya ibada kwa kisingizio cha kumtafuta Mungu wakati ni muda wa kazi, kwangu mimi naona kuna uvivu ndani ya hilo jambo. Dini zitoe mafundisho yenye mifano ya jinsi mitume walivyokuwa
wachapakazi hodari ili watu washawishike kufanyakazi. Mifano kama ya uhodari wa ufugaji wa Nabii Ibrahim, Yusufu aliyeuzwa Misri jinsi alivyosimamia kilimo wakati ule wa ukame na mifano mengine ya namna hiyo inaweza kuamsha jamii kutoka kwenye mapokeo ya sasa yaliyojikita katika kuitafuta mbingu na ahera badala ya kufanyakazi za uzalishajimali.

Vitabu vyetu vya dini za Kikrsisto na Uislamu vina chimbuko la Uajemi ambapo pamejaaliwa mafuta mengi bila ardhi ya kilimo. Watu wa uko ni rahisi kushinda katika bao na karata bila kuzalisha na kisha jioni wakapata mkate kwa sababu ya mafuta yao je sisi kwa ardhi tuliyonayo tunaweza kukaa kwenye ibada bila kulima kisha tukakuta ndizi, maharage, mchele mashambani mwetu au tukakaa kwenye
karata na jioni tukaenda kwenye zizi tukakuta mifugo imejichunga yenyewe na tunachinja na kula nyama na kukamua maziwa au nyuia wamechonga mzinga kwa maarifa yao na sisi tunakwenda kulina na kuondoka na asali tu?. Kwa Uajemi hayo yote yanawezekana na ndio maana wanaweza kukaa katika nyumba za ibada na muda wa ibada usiathiri uzalishaji mali.

6. MHIMILI WA BUNGE
Wawakilishi wa watu bungeni wapatikane bila kupitia vyama vya siasa na watakwenda bungeni kutetea maslahi ya watu na si maslahi ya vyama au makundi binafsi ya kimaslahi. Watapigiwa kura katika majimbo ya uwakilishi na watagharimiwa na wananchi moja kwa moja kwa utaratibu watakaojiwekea. Watatumwa na wananchi moja kwa moja. Aidia hapa ni kupata wabunge ambao watakuwa wawakilishi wa kweli wa maslahi ya wananchi na si kuwa na watu ambao wanakwenda majimboni na pesa zao kugombea na wakishapata ubunge wanapotea hadi baada ya mhula wao kuisha. Katika mfumo mpya watu wataweza kumuondoa mbunge/mwakilishi wao kila wanapoona inafaa, wanaweza kuitisha uchaguzi kabla ya miaka mitano au wakaamua kutofanya uchaguzi kama wataona anafaa. Lengo ni kumfanya mwakilishi ajue matatizo ya wananchi wake.

Katika mfumo wa katiba ya 1977 mtu anaweza kuishi Dar es Salaam anakwenda kugombea Bukoba akishapata anarudi kuponda raha Mbezi beach anawaacha watu wake wakiwa yatima hawajui watampata wapi uwakilkishi gani huu wa kisanii? Kama unataka kuwakilisha watu kaa nao kunywa nao, kula nao ndipo utajua matatizo yao na utakuwa na feeling na utapenda kuwasaidia.

Kuwe na ofisi ya bunge ambayo bajeti yake itajadiliwa bungeni itakayokuwa chini ya spika na katibu wa bunge. Wafanyakazi wataouhusuka na bajeti hii ni watumishi wa kuajiriwa wa bunge, katibu na spika. Katibu wa bunge ataajiriwa kwa utaratibu wa usaili na idara ya ajira za utumishi wa umma. Bunge litafanya vikao viwili kila mwaka ambavyo ni kikao cha bajeti kwa ajili ya kupitisha matumizi ya mhimili wa Rais, BOT, Mahakama, Waziri mkuu /kiongozi na ofisi ya bunge.Kikao kingine kitakuwa ni bunge la kutunga sheria kama zitakavyowasilishwa na mwanasheria mkuu. Miswada mipya ambayo itatakiwa kujadiliwa na bunge itawekwa wazi kwa umma miezi mitatu kabla, mikataba inayohusu rasilimali za taifa kwa wawekezaji pia itajadiliwa na bunge ili itawekwa wazi mieazi mitatu kabla.

Katika muda huu wa miezi mitatu wawakilishi wataitisha mikutano katika majimbo yao ili kuelezea miswada hiyo na kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuyasema bungeni. Spika wa bunge atachaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge na asiwe na rekodi ya kuwa shabiki wa chama filani cha siasa. Atakaimu urais wakati iwapo rais hayupo. Chini ya bunge kutakuwa na idara zifuatazo ambazo wakuu wake wanaajirirwa kwa usaili na idara ya ajira za umma, hawa ni

Takukuru

Mkurugenzi wa mashtaka wa umma DPP

Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za umma

Jengo la ukumbi wa bunge lazima lionyeshe pande mbili yaani upande wa serikali na wabunge katika mpagilio wa viti kama vile mabunge Uingereza na Kenya. Katika ukumbi wa bunge ulioko Dodoma haujilikani wapi ni upande wa serikali na wabunge , ukumbi umejengwa kwa ajili ya chama kimoja hata viti vyake ni laini hadi kumfanya mwakilishi kusahau mataizo ya kule alikotoka.Lazima viti hivi vibadilishwe viwekwe vile vinavyomfanya mwakilishi asijisahau na kulala usingizi pindi awapo bungeni. Wawakilishi wote kwa wakati mmoja watakuwa wapinzani wa serikali hadi pale watakapopiga kura kuunga mkono hija za serikali.

Tume huru ya uchaguzi
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ataajiriwa kwa kufuata mfumo wa ajira kila baada ya miaka saba na anaweza kuajiriwa tena bajeti ya ofisi yake itapitishwa na bunge kutegemea na aina ya uchaguzi inaotarajiwa kusimamia.

7. MHIMILI WA MAHAKAMA
Utakuwa mhimili huru kwa wananchi wote pasipokujali madaraka ya mtu.Utapata mgao moja kwa moja toka BOT baada ya kutetea bajeti yake bungeni. Hakutakuwa na waziri wa sheria kushughulikia mambo ya mahakama kama ilivyo sasa.Jaji mkuu atachaguliwa na wanasheria wenzake na si kuteuliwa na rais, wakiamua kuwasha moshi mweupe kama vatikani hiyo ni juu yao.Katika mfumo wa sasa
mahakama ina mishahara midogo kiasi cha kuchochea rushwa na upindwaji wa haki za raia. Tunaishi kwenye nchi yenye sheria lakini isiyokuwa na haki. Aidia ni kuondoa hali hii.

MAMBO MENGINE YA KUZUNGUMZA VYAMA VYA USHIRIKA
Kutakuwa na vyama vya ushirika vitakavyoanzishwa na wakulima wenyewe kwa kufuata muundo wa zamani ambavyo vitakuwa na kazi ya kutetea maslahi ya wakulima. Ili kutetea maslahi ya wakulima viongozi katika vyama hivi hawataruhusiwa kuwa na maslahi katika vyama vya siasa. Vitakuwa vyama vyenye nguvu vinavyojitegemea bila kuingiliwa na serikali yoyote. Vitakuwa na kazi ya kuendeleza kilimo na kutafuta masoko na kutetea bei za mazao ndani na nje ya nchi. Vitahusika na pensheni za wakulima wastaafu. Vitakuwa na akaunti katika BOT na vitaanzisha benki ya kukopesha wakulima kwa kadili ya muundo utakaokubalika. Si kazi ya serikali kuanzisha benki kwa ajili ya wakulima wakati wenyewe hawashirikishwi.

VYAMA VYA WAFANYAKAZI
Vyama hivi vitaanzishwa na wafanyakazi wenyewe kwa malengo ya kutetea maslahi ya wafanyakazi wa sekta zote yaani sekta za umma na binafsi.

VYAMA VYA SIASA
Vyama vya siasa havitakuwa vya muungano. Kila upande wa muungano utakuwa na vyama vyake na mfumo wake wa uchaguzi.Kama inavyofanyika kuweka serikali ya mapinduzi kwa upande kuwa na chaguzi zake huru ndivyo itakavyokuwa kwa Tanganyika na vyama vitasajiriwa upande mmoja tu wa muungano. Kama majina yatafanana tutaongeza herufi T na Z ili kutofautisha pande za chama
kinapotoka.

Kila raia anahaki ya kuanzisha chama chake siasa na kunadi falsafa zake ambazo kama zikikubalika atapata wafuasi na kuchaguliwa na kuwa kiongozi katika jamii inayomzunguka. Anaweza pia kunadi sera zake kama mgombea asiye na chama.Muundo wa vyama utaanzia katika ngazi ya tarafa hadi taifa. Katika muundo wa sasa vyama vimekuwa na mashina ya nyumba kumukumi yasiyo na tija kwa
taifa badala yake yamekuwa vyanzo vya chuki katika jamii na kuwa vijiwe vya porojo na majungu na unazi wa kisiasa badala ya watu kuongelea sera nzuri za wanasiasa.

Muundo wa aina hii umesababisha CCM na CUF kule Zanzibar kuishi kwa uhasama usiokwisha watu wakiamka asubuhi wanakwenda kunywa ulojo wengine maskani ya CCM na wengine ya CUF matokeo ni kuzungumza ya jana badala ya kupanga mambo ya kesho. Katika muundo wa tarafa tutaondoa siasa za chuki na tutajadili sera za vyama bila ubaguzi kama tunavyojadili mpira wa Simba na Yanga bila chuki. Uzoefu unaonyesha kwamba muundo wa vyama kuanzia kwenye mashina umesababisha baadhi ya familia kujiita kwamba ni za chama fulani bila kujari manufaa ya vyama hivyo kwa taifa.

Katika mundo wa vyama vya siasa itakuwa ni marufuku kwa watoto chini ya miaka kumi na nane kujihusisha na siasa. Katika siasa za sasa kuna watu wanaitwa chipkizi wanabatizwa bila ridhaa yao kuwa wanachama watarajiwa wa vyama fulani , huu ni muundo uliopitwa na wakati wa kulazimisha mambo kwa ulaghai na hauna tija kwa taifa.Muundo wa nyumba kumikumi ulikwekwa ili kuwezesha watawala wa zama zile kudhibiti wageni kuingia kiholela ndani ya nchi yetu. Kwa sasa tunazo teknolojia
za kutambua wageni wanaoingia nchini bila kuhitaji wajumbe wa nyumba kumi.

Hakuna chama kitaruhusiwa kuwa na bendera zenye rangi zinazofanana na rangi za bendera ya taifa au za vilabu vya Simba na Yanga.Katika siasa za sasa kuna watu wengi wanaopumbazwa na rangi hizi badala ya watu kuchagua sera wanachagua chama chenya rangi za Simba au Yanga wanadanganywa na wazushi kwamba chama chenye bendera ile ni cha timu fulani.Kwa kuwa timu ya Yanga ni kongwe kuliko CCM, chama hiki itabidi kitafute rangi zingine endapo Katiba mpya itaruhusu vyama vilivyopo kuendelea kuwepo ingawa mimi napendelea tuanze siasa zetu kwa kuunda upya nyama vyetu hata kama majina yanaweza kuwa yaleyale lakini rangi za bendera na muundo lazima vibadilike.

Endapo chama kitashinda chaguzi mfululizo na kukaa madarakani kwa zaidi ya miaka kumi na nane kitasimamishwa kushirirki uchaguzi utakaofuata kwa muda wa miaka mitano ili kupisha kizazi kingine kushika madaraka.Wanasiasa wa chama kilichosimamishwa hawataruhusiwa kuhamia vyama vingine. Aidia hapa ni kuzuia chama Fulani kutawala vizazi zaidi ya kimoja mfululizo.

Muundo wa vyama usiangalie tofauti za umri wala jinsia kama ilivyosasa. Sioni kama kuna haja ya kuwa na jumuia za vijana au kina mama huu ni ubaguzi.Kiongozi katika chama apatikane kwa aiba yake. Mfano ni kule Ujerumai ambapo ilimchukua Chansela Angela Mekel muda mrefu kugombea na kupata kiti katika chama chake cha CDU lakini wakati ulipofika watu walimchagua.Ubaguzi wa aina ya umri uliigawa CCM mwaka 1995 kati ya Kikwete ambaye alikuwa chaguo la vijana na wagombea wengine waliokuwa na umri mkubwa. Tunataka tuondoe hali hiyo. Pia viongozi wastaafu wanapaswa kutoshawishi viongozi wapya ili kupisha fikra mpya za viongozi wapya wanaochaguliwa.

VILABU VYA MICHEZO NA BURUDANI
Katiba hii itazitambua timu za Simba na Yanga pamoja na bendi za Sikinde na Msondo kama nembo za taifa. Nembo hizi ni tunu ambazo bado zipo na kuna haja ya kutumia rasilimali zetu kuzidumisha kama sehemu ya urithi wa taifa katika Nyanja ya utamaduni na michezo.

JINSI YA KUFANYA KAMPENI WAKATI WA CHAGUZI
Itakuwa ni marufuku kwa vyama kugawa nembo za vyama vyao wakati wa uchaguzi. Ili kufanya kura kuwa kweli ni siri ni vizuri tusjue nani anakwenda kushinda. Katika mfumo wa sasa kuna vyama vinagawa nembo wakati wa chaguzi ili kudanganya umma kuwa vina wafuasi wengi na hivyo vinatabili kushinda hata kabla ya siku ya kura na kweli siku Ya kupiga kura vinashinda, kama hivyo ndivyo kuna aja gani ya kupiga kura si tungekuwa tunagawa nembo za vyama na tunaangalia chama kilichogawa nembo zaidi tunakipa ushindi bila kupoteza rasilimali kupiga kura.

Kila mgombea atapeleka ratiba yake ya kampeni kwa tume ya uchaguzi ambayo itapeleka kwa vyombo vya habari ili vipange ratiba ya kurusha kampeni hizo hewani. Siku hizi ni kawaida kwa wanasiasa waliofilisika kwa hoja kujibambika mazuri yaliyofanywa na Nyerere
utawasikia wakisema hata mwalimu alisema. Kutumia hekima za Nyerere ili kuiteka adhira iwe ni marufuku wakati wa kampeni za wanasiasa tunataka kushindanisha vipaji vipya na mawazo mapya hatuwezi kuendelea kuishi kwa mawazo ya watu waliopita hii inakinza kuibuka kwa fikra za kizazi kipya.

George Washington na Abraham Linciln ni marais maarufu sana katika nchi ya Marekani kama ilivyo kwa Winston Churchil kwa uwaziri mkuu nchini Uingereza, licha ya kwamba hawa watu wanaheshimiwa sana lakini fikra zao hazitumiki wala majina yao hayatajwi katika siasa zao huko kama njia ya kujitafutia uharari.Hotuba za Nyerere za kusema kuwa bila CCM madhubuti nchi itayumba zisiruhusiwe kutumika katika kampeni au wakati wowote maana zinabagua watanzania wengine ambao si wana CCM ama vinginevyo tukubaliane kwamba Nyerere si baba wa taifa bali ni baba wa CCM.

Itakuwa ni lazima kila mgombea katika nafasi yoyote ya uongozi kushiriki katika mdahalo wa wazi utakaotayarishwa na vyombo vinavyohusika kama vyombo vya habari, wanaharakati n.k. Katika mdahalo mgombea atakayehisi kuhujumiwa kwa vyovyote atakuwa na haki ya kusimamisha uchaguzi na ikithibitika hujuma ilikuwa ni kweli basi waliohusika na hujuma watashitakiwa mahakamani na
kufungwa jera ili kulinda heshima ya demokrasia. Hakuna chombo cha habari kitakachoruhusiwa kutumika kufanya propaganda za kisiasa hatutaki kujenga siasa za udaku ambazo hazina tija tunataka sera.

Siasa za mambo ya mtu na mahawala zake au mke wake hazina tija kwa taifa, tunahitaji kutumia bongo za watu kuendeleza nchi yetu. Tabia binafsi za mtu zisizungumzwe katika majukwaa ya siasa endapo mtu anahisi mgombea umeenda kinyume na maadili ya uchaguzi atalazimika kumwekea pingamizi kabla ya kuidhinishwa na tume kuwa mgombea. Akishakuwa mgombea atapingwa kwa hoja za sera zake ni si mambo yake ya kibinafsi. Kutumia mambo binafsi ya mtu kama sehmu ya kampeni itakuwa ni hujuma
na hukumu ni kifungo gerezani.

Wagombea wa nafasi za juu kama Urais na Uwaziri mkuu/Kiongozi lazima wafahamike miezi kumi kabla ya uchaguzi ili jamii ipate kuwafahamu na kujua wataleta neema gani kwa taifa.Wakati wote baada ya kufahamika watakuwa na fursa ya kutumia vyombo vya habari kuzungumza na wananchi ili wafahamike.

Vyama vinaweza kuunganisha sera na kufanya kampeni kwa pamoja Viongozi wa kimila wasishirirki kufanya kampeni za majukwaani kwani kama walivyo viongozi wa dini hawa nao ni watu wanaoongoza imani za watu na hivyo wanaweza kupotosha dhana ya
wagombea kunadi sera zao.

MFUMO NA AINA YA ELIMU
Kama ningewafufua na kuwauliza wazee wetu mfumo huu wa elimu waliuiga wapi nadhani wangesema haupo kokote duniani zaidi ya Tanzania. Mfumo huu unasaidia kutengeneza matabaka yasiyoyalazima katika jamii. Tuangalie mfumo wa elimu ya mjerumani ambayo lengo lake kubwa ni kuzalisha mafundi ambao wanaweza kujiajiri mara wanapomaliza masomo. Mfumo tulionao labda unafanana na wa Kingereza unapandikiza watu kuwa tegemezi wakiamini kwamba kila aliyesoma lazima aajiriwe na serikali au watu binafsi. Tunahitaji kuchagua mfumo na aina ya elimu ambayo kila anayeipata anaondokana na fikra za kuwa tegemezi na kuomba ajira. Kwa haraka naweza kuchagua mfomo wa elimu ya kijerumani hata kama tutatumia lugha za Kiswahili na kiingereza kufundishia.

MATIBABU YA VIONGOZI
Viongozi wote watatibiwa katika hospitali za ndani isipokuwa kama itathibitika kuwa ugonjwa huo hauwezi kutibiwa hapa nchini na safari za matibabu ya viongozi zitapata kibari kutika kwa mganga mkuu wa taifa.

HUDUMA ZA AFYA
Kuna matatizo ya kiafya ambayo itakuwa kazi ya serikali kuyatatua. Magonjwa kama haya yatatibiwa bure na hospitali zote zikiwamo za binafsi na serikali itagharimia kwa taratibu zitakazowekwa. Haya ni magonjwa yote yanayotokana na ajali, magonjwa ya mlipuko, Kifua kikuu na malaria.

MAKOSA MAKUBWA
Rushwa
Ujangili
Wanyamapori kama tembo, twiga, chui, mbuni, vifaru na wengine wanaohitwa nyara za taifa ni marufuku kuvunwa kijangili. Tutatoa adhabu kali kwa wote watakaopatikana na makosa hayo.

Biashara ya madawa ya kulevya Ili kuokoa taifa na madhara yanayotokana na mihadharati kuna haja kama taifa kuweka katika katiba
hii adhabu ya watu wanaohusika na biashara ya madawa ya kulevya.Je sisi kama taifa tutoe adhabu
gani kwa watu hawa?

JANDO NA UNYAGO
Tumekuwa wazembe kama taifa katika kuendeleza mila na tamaduni zetu za jando na unyago. Kwa kutumia jando na unyago tunaweza kuendeleza kizazi cha taifa letu kuliko inavyotokea katika kipindi tulichonacho. Vijana wa kileo hatujui hata kutunza ndoa zetu, ili nalisema kwa vijana wa kiume na kike kwa vile hatukufundishwa na wazee kutokana na taifa kukosa uelekeo juu ya mila hizi. Si siri leo hii vijana wengi hatujui ni nyakati gani na kwa ukaribu upi tunahitaji kukaa na wenzetu katika ndoa li tuweze kupata watoto katika ndoa zetu badala yake tunalazimisha kutafuta watoto hata wakati ambao haiwezekani au ni jinsi gani wanandoa wanapaswa kufanya maandalizi wakati wa kutafuta watoto. Mila zetu zilikuwa zimeendelea hata kufikia kuchagua jinsi ya mtoto wanayetaka yaani wa kiume au wa kike.

Napendekeza kuweko na utaratibu utakaoruhusu wanafunzi wanapofikisha umri unaoruhusu mambo ya jando na unyago waruhusiwe kuhudhuria ili kujifunza mambo ya familia vinginevyo kizazi chetu kitatoweka na kile cha wageni kitashamili na kuijaza nchi kama huamini jiulize familia zetu nyingi zina watoto wangapi.

WADHIFA WA UBABA WA TAIFA
Nimekuwa nakitafakari sana kuhusu matumizi ya neno baba wa taifa kama kitangulizi au heshima kwa rais wa kwanza wa taifa letu. Nimegundua kwamba sio sahihi kumuita Nyerere baba wa taifa. Heshiima hii alianza kupewa miaka sita tu baada ya Uhuru na watu wlioshirirki kuamua kumheshimu walikuwa watu wa TANU na wala hayakuwa maamuzi ya taifa lote. Hata katika hali ya kawaida haiwezekani kizazi kimoja kikafanya maamuzi kwa ajili ya vizazi vyote ni jukumu la vizazi vijavyo kumpa heshima hiyo mtu ambaye baada ya kulinganisha na wengine vizazi hivyo vitaona hasa panastairi kuwepo na heshima hiyo na nani apewe. Kwa sasa si busara kutoa heshima hiyo kwa Nyerere nashauri historia za viongzi wetu ziandikwe vizuri kwa kuonyesha mazuri na mabaya yao na vizazi vijavyo ndivyo vitaamua nani anastahiri heshima hiyo.

MJI MKUU WA TAIFA LETU
Nimekuwa nikitafakari iwapo bado kuna haja ya kuhamia Dodoma na mimegundua kwa sasa hakuna tena sababu kufuatia maendeleo makubwa ya teknolojia ya habari. Napendekeza mji mkuu huendelee kuwa Dar es Salaam ambao ndio jiji lenye uchumi mkubwa kuliko yote. Wakati serikali inamua kuamia. Dodoma chumi za miji yoye miwili hazikupishana sana lakini kwa sasa uchumi wa Dar es Salaam ni zaidi ya mara elfu moja ya ule wa Dododma.

WATOTO WA MITAANI NA WATU WENYE MAHITAJI MAALUMU
Iwepo taasisi ya serikali ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na watu wenye mahitaji maalumukama vile wazee na walemavu ambayo itaratibiwa na ofisi ya Bunge. Hawa watoto ndio taifa lenyewe waendelezwe katika fani za michezo na utamaduni ndio hawa wanaweza kuwa wanamichezo bora wa taifa letu.

ADHABU YA KIFO
Kwa watu wengi huu utakuwa ni mjadala ambao wangenda sana kuukwepa kwa sababu wanaogopa kujibu iwapo wanaunga mkono adhabu hii au hapana. Kwa upande wangu naunga mkono uwepo wa adhabu ya kifo. Napendekeza iendelee kuwepo kwa vile naamini kila mtu ana haki ya kuishi na kulindwa uhai wake. Iwapo tutaondoa adhabu hii tutakuwa tunakaribisha mauaji ya kutengenezwa kwa watu wetu. Wauwaji wana njama nyingi zikiwemo kupitia huduma za afya, ajari za barabarani n.k. lazima sheria iwabane sana kuepuka vitendo kama hivyo.
 
Habari zenu wanajukwaa, naomba msome haya maoni yangu msiogope kwa kuwa nimeandika kurasa ndefu. Jamiiforum kama lilivyo jina lake ni home of great thinkers kwahivyo sitarajii great thinkers msione mapungufu katika maoni yangu.
 
Kaka nakupongeza,kwani umejitahidi,ili kuikuza n'nchi yako,japo sikumaliza kusoma maoni yako lakini naomba kukurekebisha pale nimeona sivyo. Kwanza mabalozi, umelenga tu! kwa wageni wasafiri,bali ubalozi unikazi nyingi sana,kuimarisha biashara kati ya n'nchi na n'nchi.mikakati ya usalama baina ya majirani, na kadhaalika.

Pili ah! nimesahau hapo kidogo, lakini sisi nimajirani, ningewashauri watanzania,wapiganie serikali ya majimbo,maana n'nchi yenu ni kubwa sana na kuna umuhimu huduma siwafikie wanan'chi walioko mashinani, rasilimani za majimboni pia ziwafaidi wenyeji, badala ya kila kitu ni Dar, ona utata wa gesi, machimbo ya dhahabu,na mengineo, ingekuwa muhimu kwanza wenyeji wafaidike, muwe na magavana ambao watakuwa ni kama marais wa majimbo,na bila shaka lawama nyingi munge epukana nazo, mana jimbo lingekuwa na uwezo wakuekeza maendeleo kivyake, hivyo ingeleta ushindani wa kimaendeleo baina ya majimbo, na Tanzania ingeruka juu zaidi kimaendelea hata zaidi ya kenya. Kwani kenya tumeachiwa ukabila na ubinafsi. Watanzania hamuna hayo, Mungu awabarikini wabongo wote.alamsik.
 
Gambera nkushukuru sana mkuu kwa maoni yako juu ya nilichoandika. Nilikuwa kimya mua mrefu kusubiri maoni ya wengine lakini hadi leo ni wewe tu ulechangia. Tena umesema wewe ni mkenya. T seems JF ina mada nyingi sana kuzidi uwezo wa wanajamvi kuzivisit zote. Nashauri jambo lifanyike ili uondoa hali hii. People are not discussing issues badala yake wanasigana kwa vitu vidogo binafsi.thats not great thinking.
 
Back
Top Bottom