Porojo na Uhalisia Katika Kashfa ya Ndugai

IslamTZ

JF-Expert Member
Nov 22, 2010
309
182
Abuu Kauthar
ndugai2.jpeg

Siku hizi kila jambo linalotokea ni hoja ya kudai katiba mpya. Ni hivyo hivyo imekuwa katika kashfa ya Job Ndugai ya kuipinga serikali na chama chake hadharani, jambo lililopelekea hasira za wana CCM na kulazimika kujiuzulu.

Limezungumzwa sana suala la mihimili ya utawala kuikingiliana, hususan serikali kulidhibiti bunge na kukandamiza uhuru, uwezo na haki ya taasisi hiyo ya wawakilishi wa watu kusimamia. Imedaiwa kuwa yaliyotokea kwenye sakata la Ndugai linathibitisha udhaifu wa katiba, na hivyo kuyapa madai ya katiba mpya. Lakini je hoja hizi zina mashiko?

Lipi kosa la Ndugai?
Ndugai alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka CCM, chama tawala; na ni mjumbe wa kamati kuu ya chama chake.

Kuna nafasi, fulani ukishikilia, unapoteza uhuru wa kutoa maoni yako binafsi kwenye yanayoenda kinyume na taasisi unayoiwakilisha hadharani, hasa kwenye jambo ambalo lishafanyiwa uamuzi. Kwa nafasi yake, Ndugai ana majukwaa yake ya kutoa maoni, sio mtaani. Jukwaa la Ndugai ni kwenye kikao cha juu kabisa cha chama, Kamati kuu, ambako yeye ni mjumbe. Maoni nje ya hapo ni kutengeneza sintofahamu na kuonesha kuwa chama kimegawawanyika.

Kama alivyoeleza vema Mchungaji Josephat Gwajima, Ndugai alikuwa na nafazi ya kueleza maoni kwenye Bunge lililopita ambalo lilijadili mkopo huo au kwenye Kamati Kuu ya chama ambayo ilikutana wiki au siku chache zilizopita. Iweje tena akosoe serikali nje ya vikao hivyo na kutengeneza taswira ya chama chenye mgogoro?

Ni haki ya kila mtu kuwa na maoni yake na kuyawasilisha apendavyo bila masharti yoyote. Ni haki pia ya mtu yoyote kugombea nafasi ya uspika wa bunge. Hata hivyo, kuna tofauti ya hizo haki mbili.

Ile haki ya kupiga kura ni hivyo ilivyo, haina masharti, haitegemei chochote. Lakini ile haki ya kugombea, kuchaguliwa na kuhudumu kama spika (na nafasi nyingine za kisiasa) zina kanuni na masharti kuanzia wakati wa kugombea hadi wakati wa kudumu. Kwanza, spika, lazima adhamniniwe na chama, pili lazima awe mtii kwa chama na tatu, lazima akiri na kufuata kanuni ya uwajibikaji wa pamoja. Hali iko hivyo duniani kote na ndio maana vyama hutafuta namna ya kuhakikisha spika anatoka kwao ili kudhibiti bunge.

Katika watu wote, Ndugai alipaswa zaidi kujua kanuni hizi za siasa za uspika kwa sababu kwanza ni mwanasheria, pili ana uzoefu mkubwa katika uongozi na tatu katembea duniani – hadi Galilaya (kwa Yesu na mkewe kafika). Kama aliona uhuru wake binafsi wa kutoa maoni wadhifa wake wa uspika, alipaswa tu kuachia ngazi mapema. Waswahili mshika mawili, moja humponyoka.

Kuna wakosoaji wa Rais Samia wanasema hii ni dalili nyingine ya udikteta. Kama ndivyo, basi huu ni udikteta wa kidemokrasia kwa sababu nchi karibu zote ziko hivi kwenye masuala haya. Kote duniani, inategemewa chama tawala kidhibiti bunge. Kote duniani, wabunge wa chama tawala (na spika wao) hushirikiana na serikali yao kuhakikisha sera, bajeti, miswaada ya serikali, ambayo ni sera za chama tawala, zinapita bungeni.

Kusema hasira za Rais Samia ni za kuchukia kukosolewa si sahihi. Wangapi wanamkosoa kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kwa lugha kali zaidi na hachukii? Shida ya Ndugai si udhaifu wa hoja zake za masuala ya mkopo bali ni uwajibikaji wa pamoja, kichama.

Watanzania inabidi turejee historia ya vyama hapa Tanzania, CCM na wapinzani, na tutadhihirikiwa na ushahidi mwingi kuwa vyama vyote vimewahi kuwajibisha viongozi kwa kutoa maoni tofauti hadharani – kuanzia CCM, Cuf hadi Chadema. Na ukiacha ‘siasa ndogondogo’ ukweli ni kwamba hakuna chama kwenye kingekuwa nafasi ya CCM kingemuacha Ndugai.

Kuna hoja imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuwa sakata hili linaonesha kuwa serikali ni dhaifu kwa sababu hili ni tukio ambalo halijawahi kutokea kwa maspika wote waliopita huko nyuma. Lakini Lissu anasahau kuwa hii ni mara ya kwanza pia kwa Tanzania kuwa na rais mwanamke, na hivyo ni jambo linalotegemewa wanaume kuhisi wanaweza haki na uwezo wa kumdhibiti kiongozi mwanamke kama wanavyodhibiti wake zao majumbani.Pili, Lissu mwenye amekiri mara kadhaa kuwa huyu ndiye spika wa hovyo zaidi kuwahi kutokea. Ajabu nini hapa hadi ionekane kuwa huo ni udhaifu wa Rais Samia?

Ikumbukwe kuwa hii si mara ya kwanza Ndugai kumchocha kidole machoni mama. Huko nyuma, aliwahi kutoa kauli ambazo ni wazi zilimlenga Rais Samia pale alipowaambia wanawake eti waache kujinasibisha na uanauke! Ndugai alisema: “Na ajenda ya kusema, ‘Mimi kama mwanamke’ achana nayo. Nani hajui? We DC, RC, mbunge songa mbele. Kila dakika, ‘Oh mi mwanamke, sisi wanawake, kwani nani kakwambia kuna shida gani?”

Katika hotuba ile, nakumbuka, alifikia hadi kusema eti wanawake wanaosema hivyo wanawaharibu hadi viongozi wakuu wa nchi, bila shaka akimaanisha rais. Kwa hiyo rais kaharibika!?

Ndugai hateteeki, Rais alikuwa sahihi na hao wanaodai mhimili unaingiliwa rekodi zao zinaonesha kuwa ndio vinara wa kutimuana kwenye vyama vyao huko.

Isipokuwa, katika sakata hili, jambo moja tu nililolifurasha, katika porojo za kumtetea Ndugai: Ni wazi kuwa kadri demokrasia yetu inavyozidi kukua, matumizi ya sayansi ya mikakati ya kisiasa inazidi kuonekana kutumika. Chadema wameona adui yao mkubwa Ndugai anaporomoko, hana tena mashiko hivyo kuendelea kumkandamiza hamna tija tena kisiasa. Tija iko wapi? Ni katika kumteta ili kwanza kuendelea kuchochea mtafaruku ndani ya CCM na pili, Ndugai amekuwa sasa silaha ya kumpigia Rais Samia.

Na hili Baraza jipya ambalo lina maajabu kadhaa, ikiwemo mkoa wa Pwani kutoa watu watano, mawaziri na manaibu mawaziri, Chadema ni kama wameokota dodo uwanjani. Mkakati ni: Chochea moto ili 2025 ma CCM yawe yameishiwa nguvu kwa kupambana wenyewe.
 
Back
Top Bottom