Polisi adakwa akipokea rushwa 200,000/-

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Arusha , imemtia mbaroni na kumfikisha mahakamani askari Polisi Jamal Omari wa kituo kidogo cha Polisi cha ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa madai ya kupokea rushwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasomambuto, askari huyo alidakwa Mei 13 kwa madai ya kukutwa akiomba na kupokea rushwa ya Sh 200,000 katika Kijiji cha Kimba wilayani Ngorongoro.

Taarifa hiyo imedai kuwa, askari huyo aliomba rushwa ya Sh milioni moja kutoka kwa mfanyabiashara aliyemkamata Mei 6 mwaka huu, akiwa na viazi kwa madai kuwa alivilima ndani ya Hifadhi hiyo ya Ngorongoro kinyume cha sheria.

Hata hivyo inadaiwa mfanyabiashara huyo aligoma kutoa kiasi hicho cha fedha na kukubali kupelekwa kituoni ambako alilala mahabusu siku nne mfululizo hadi Mei 9 mwaka huu, alipotoka kwa dhamana ya Sh 50,000 baada ya kumpatia askari huyo rushwa.

Licha ya kuwa nje kwa dhamana, inadaiwa mtuhumiwa aliendelea kumdai mfanyabiashara huyo rushwa ili afute jalada la kesi alilomfungulia na alikubali kupunguza rushwa hiyo kutoka Sh milioni moja hadi Sh 500,000.

Kutokana na makubaliano hayo, inadaiwa mfanyabiashara huyo alitoa taarifa kwa maofisa wa Takukuru wilayani humo, waliandaa mtego na kufanikisha kumkamata mtuhumiwa akipokea Sh 200,000 ikiwa ni sehemu ya malipo ya Sh 500,000.

Mtuhumiwa amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Ngorongoro Mei 16 mwaka huu, na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu, Loshirari Raphael lakini alikana mashitaka na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30 mwaka huu.
 
Back
Top Bottom