Peniela (Story ya kijasusi)

PENIELA
SEASON 1
SEHEMU YA 24
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Hatukuwa tumetegemea shambulio kama lile lililotokea kwa kitendo cha kufumba na kufumbua kwa hiyo tulijikuta tukipoteza kikosi kizima na ni mimi peke yangu niliyefanikiwa kutoka salama.Mpaka leo ninaamini nilifanikiwa kutoka katika shambulio lile kwa maongozi ya Mungu tu. Kila mara picha ya shambulio lile ikinijia mwili wote husisimka.Siwafichi ndugu zangu ni miaka kadhaa imepita sasa lakini mpaka leo hii nikikumbuka kilichotokea usiku ule huwa ninaogopa sana.Ni picha ambayo ni ngumu hata kuielezea” Akanyamaza kidogo na kuinama halafu akasema
“ Nilipofanikiwa kutoka salama eneo lile nilikimbia moja kwa moja hadi nyumbani kwangu lakini nikakutana na kitu cha ajabu ambacho mpaka leo hii picha yake haiwezi kunitoka kichwani.Nyumba yangu ilikuwa ikiteketea kwa moto.Familia yangu yote ilikuwa imeteketea katika moto ule mkubwa” Mathew akashindwa kuvumilia akainama na kuangusha chozi

ENDELEA……………………………………..

Nilichanganyikiwa baada ya kuona nyumba yangu ikiteketea kwa moto.Nilitamani hata kujitupa ndani ya moto ule ili nami niteketee pia pamoja na familia yangu.Mara walitokea watu wawili ambao sielewi walitokea wapi ambao nilidhani walikuwa ni miongoni mwa majirani zangu,wakaniingiza katika gari na kuniwekea bastora kichwani wakinitaka nisifurukute bali nifuate kila watakachonielekeza.Kwa wakati huo nilikuwa kama mtu niliyechanganyikiwa na sikuwa nikiogopa chochote,nilianza kupambana nao na walipoona nimewashinda wakaamua kunitupa nje na kukimbia huku nikiwa nimejeruhiwa kwa risasi begani.” Mathew akavua shati na kuwaonyesha akina Anitha kovu mahala alikopigwa risasi
“ Nilikimbia na kujificha chini ya daraja,nikampigia simu mkurugenzi na kumfahamisha kilichotokea.Dr Wilbert Augustino mkurugenzi wa idara ya ujasusi aliyekuwapo wakati ule alifika mara moja mahala nilipokuwa nimejificha na kunichukua akanipeleka katika nyumba fulani kubwa.Akawapigia simu rafiki zake wawili madaktari wakafika na kunitoa risasi ile niliyopigwa begani.Nilijaribu sana kumuuliza mkurugenzi kama anafahamu chochote kuhusiana na shambulio lile lakini alinieleza kwamba hafahamu chochote.Aliniambia niendelee kukaa katika nyumba ile wakati wakiendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio lile la kustusha.” Mathew akainama na kuzama katika mawazo .Alikuwa amekumbuka mbali sana.
“ Kwa takribani siku kumi na nne “ akaendelea Mathew
“ Niliendelea kukaa ndani ya ile nyumba kubwa na nzuri ambayo haikuwa ikikaliwa na mtu mwingine yeyote zaidi yangu.Daktari alifika kila siku na kunitibu jereha.Mkurugenzi pia hakukosa hata siku moja kufika na kuniletea mahitaji mbali mbali ikiwemo chakula.Bado mkurugenzi aliendelea kunisihi nisijaribu kutoka nje kwani hali ya huko haikuwa bado nzuri kwa upande wangu.Alinieleza kwamba nilikuwa natafutwa sana lakini hakunieleza ni akina nani waliokuwa wakinitafuta.Hiki kilikuwa ni kipindi kigumu mno katika maisha yangu.Nililia mno kila siku nikiiililia familia yangu niliyoipenda kupita kitu chochote.Ilifika mahala sikutamani hata kuendelea kuishi kwani sikuona faida ya kuishi bila ya familia yangu iliyoteketezwa kikatili.” Mathew akainama kwa uchungu akikumbuka familia yake halafu akaendelea.
“ Siku moja mkurugenzi alikuja na kunikabidhi nyaraka za kusafiria na kunitaka niondoke nchini haraka sana kwa ajili ya usalama wangu kwani tayari nimekwisha julikana mahala ninakojificha.Niliondoka usiku huo kama mkimbizi nikielekea nchini japan.Tayari mkurugenzi alikuwa amekwisha suka mipango yote na nikafanikiwa kuingia nchini Japan kwa jina la Adrian Kusema nikiwa kama mtafiti wa kilimo ninayekwenda kufanya utafiti wa zao la mpunga.Mwenyeji wangu alikuwa ni mtu mmoja niliyemfahamu kwa jina moja tu la Yamazuka ambaye tayari alikwisha wasiliana na mkurugenzi wangu .Nilipelekwa katika kijiji kimoja cha wakulima wa mpunga ambako nilianza kujifunza kuhusu kilimo cha mpunga.Niliishi katika kijiji kile kwa muda wa miaka mitatu.Nilijifunza maisha ya ukulima.Watu wale walikuwa wakalimu sana.Walinifundisha mambo mengi .Yalikuwa ni maisha mazuri na niliyapenda.Nilijitahidi sana kuyazoea maisha yangu mapya na kuyasahau maisha yangu ya nyuma lakini pamoja na jitihada zote za kutaka kuyasahau maisha ya nyuma,bado picha ya usiku ule iliendelea kunitesa kila uchao.Kila nikifumba macho nilikuwa nikiwaona wenzangu namna walivyokuwa wakiuawa na mbaya zaidi ni ule moto mkubwa niliouona ukiiteketeza familia yangu.Nilishindwa kuiondoa kumbu kumbu ile kichwani kwangu hivyo kunilazimu kuondoka nchini japan nikaelekea Marekani ambako nilikutana na rafiki yangu mmoja aitwaye Jerry Washington ambaye anafanya kazi katika shrikika la ujasusi la marekani C.I.A.Huyu ndiye aliyenisaidia kufahamu kila kitu kuhusiana na kilichotokea siku ile usiku na hata mauaji ya familia yangu.” Mathew akainuka na kuchukua mvinyo akanywa kidogo na kuendelea
”Nchi ya Marekani kwa sasa ndiyo inayoongoza kwa uwekezaji mkubwa sana hapa Tanzania na katika eneo lote la afrika mashariki .Wamewekeza mabilioni ya dola katika sekta ya mafuta na gesi.Kwa sasa wanajenga kituo kikubwa kabisa cha mazoezi ya kijeshi cha wanamaji katika bahari kuu eneo la maji ya Tanzania.Hiki ni kituo kikubwa kabisa kuwahi kujengwa barani afrika.Kutokana na uwekezaji huu mkubwa ,serikali ya Marekani imelazimika kutafuta namna ambayo itayalinda maslahi yake katika eneo hili la ukanda wa afrika mashariki na ndipo walipounda kikosi kiitwacho Team SC41.Kikosi hiki kipo nchini Tanzania na kinaendeshwa kwa usiri mkubwa mno kiasi kwamba si rahisi kufahamu kama kuna kikosi kama hiki hapa nchini.Hata serikali ya Tanzania haifahamu chochote kuhusiana na uwepo wa kikosi hiki ndani ya ardhi yake.Team SC41 ni kikosi kidogo lakini hatari sana na kilichosheheni watu wenye uwezo mkubwa waliopata mafunzo ya hali ya juu nchini Marekani.Kikosi hiki kina uwezo wa kupata taarifa za kila kinachoendelea kila siku serikalini na lengo likiwa kuhakikisha maslahi ya marekani yanalindwa kwani uwekezaji huu mkubwa katika mafuta na gesi unauinua sana uchumi wa Marekani” Akanyamaza kidogo halau akaendelea
“ Makachero wa marekani walikuwa wakimfuatilia Faizat kwa siri toka alipotoka nchini Oman na kuzisoma nyendo zake.Hawakuwa na haraka ya kumkamata japokuwa uwezo huo walikuwa nao.Sisi hatukulifahamu hilo na ndiyo maana baada tu ya kupata taarifa za kuwepo kwa Faizat hapa nchini tulianza mara moja mikakati ya kumkamata bila kuishirikisha serikali ya marekani.Taarifa za mpango wetu ziliwafikia team SC41 hivyo wakawa wamejiandaa kutukabili ili tusiweze kufanikisha mpango wetu wa kumkamata Faizat.Hatukujua kilichokuwa kikiendelea hivyo wakatushambulia na lengo lao likiwa ni kuua kikosi chote kilichokwenda kumkamata Faizat. Hawakutaka siri ivuje kuhusiana kuonekana kwa Faizat hapa nchini.Ni mimi peke yangu niliyefanikiwa kutoka hai katika shambulio lile kwa hiyo ilikuwa lazima wanipate .Waliiteketeza nyumba na familia yangu wakiamini kwamba kwa kufanya vile watakuwa wamenichanganya kwa hiyo itakuwa rahisi kwao kunipata.Namshukuru sana mkurugenzi wangu Dr Wilbert Augustino ambaye alinisaidia nikatoroka nchini vinginevyo nisingekuwa hai mpaka muda huu.Kwa bahati mbaya Dr Wilbert naye alifariki dunia katika ajali tata.Hii yote ikiwa ni kazi ya Team SC41 .Mungu amrehemu sana Yule mzee” akasema Mathew na kunywa mvinyo kidogo halafu akaendelea.
“ Nikiwa nchini Marekani ,nilianza kufanya uchunguzi wa kina ili kujaribu kukifahamu kikindi hiki cha Team SC41 lakini juhudi zangu hazikufanikiwa kwa sababu kikundi hiki kinaendeshwa kwa usiri mkubwa mno na ni watu wachache hata ndani ya Pentagon wanaofahamu uwepo wa kikundi hiki hapa nchini kwa hiyo ni vigumu sana kuzipata taarifa zake.Kingine kikubwa nilichofanikiwa kukifahamu ni kwamba hapa nchini kikundi hicho kinaongozwa na mtu aitwaye John Mwaulaya Albert.Baada ya kukosa taarifa zake za kina niliamua kuachana nao na kujitahidi kuyasahau maisha yangu ya awali na ndipo nilipoanza kufanya kazi za kujtegemea.Kwa hiyo ndugu zangu naomba mtambue kwamba Team SC41 ni kikundi chenye nguvu lakini hatari sana.Ni watu wenye mafunzo na uwezo wa hali ya juu mno.” Akasema Mathew.Anitha na Noah walikuwa kimya kabisa wakisikiliza.
“ Kuna mawasli ambayo tunatakiwa tujiulize.Kwanza ni je Peniela ana mahusiano gani na kikundi hiki? Watu wale walioingia ndani mwa Penny walitoka na kuelekea moja kwa moja hospitali alikolazwa John Mwaulaya.Je wana mahusiano naye au wanamuwinda? Lakini je wanamuwinda kwa kitu gani hasa? Kama Peniela ana mahusiano yoyote na Team SC41 basi she is a very very dangerous woman.Na kama kweli ni Team SC41 basi nina hakika kabisa kwamba hata Edson aliuawa na watu hawa na kama ni hivyo basi lazima kuna sababu kubwa na ya msingi iliyopelekea kufanyika kwa mauaji hayo kwani team SC41 huwa inashughulika na masuala mazito yenye maslahi na nchi ya Marekani tu.Tuna kazi kubwa ya kufanya mbele yetu.I can say this is a victory or death.We have to get prepared for a big war” akasema Mathew.Anitha na Noah walikuwa kimya kana kwamba wamemwagiwa maji.Anitha akamtazama Mathew na kuvuta pumzi ndefu akasema
“ I’m scared.Real scared but I have to fight”
“ Me too.Hii ni mara yangu ya kwanza kuisikia Team SC41 “ akasema Noah.
“ Ndugu zangu naomba nisiwafiche hata mimi ninaogopa sana nikiwafikiria Team SC41.Tukio la siku ile usiku halitaweza katu kufutika kichwani kwangu.These people have got no souls.They are monsters.Lakini pamoja na hofu hiyo tuliyonayo sote lazima tupambane nao.Najua ni jambo la hatari kubwa sana kwani unapogusa Team SC41 unagusa taifa lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kijeshi duniani kwa hiyo hawako tayari siri zao zijulikane na kuvuruga uhusiano mzuri ilionao na nchi za afrika mashariki na ndiyo maana nikawaambia kwamba this is a victory or death..” Akasema Mathew.Noah akafuta jasho usoni na kusema
“ Mathew sisi tuko tayari kuingia katika mapambano na Team SC41 ,lakini kuna swali ninajiuliza .Je tunatafuta nini kwa Team SC41.Is this about revenge ?
“ Hata mimi nakubaliana na mawazo yako Noah.Lazima tunapoingia katika mapambano na hawa jamaa tufahamu tunapambana kwa ajili ya kitu gani.” akasema Anitha
Mathew akacheka kidogo na kusema
“ Mapambano haya si kwa ajili ya kulipiza . Msingi mkuu tunaoenda nao ni mauaji ya Edson.Tunatafuta nani alimuua na kwanini.Kadiri uchunguzi wetu unavyoendelea mambo mengi yanazidi kujitokeza likiwamo na hili la Team SC41 na mengine mengi ambayo yatajitokeza mbeleni,lakini naomba tusipoteze msingi mkuu wa kazi yetu yaani kuchunguza kifo cha Edson.Ndani ya mauaji ya edson kutaibuka mambo mengi mazito ndani yake.Kwa hiyo tutachunguza endapo kuna mahusiano yoyote kati ya Peniela na Team SC41,tutachunguza endapo Team SC41 walihusika katika mauaji ya Edson na kama walihusika basi tufahamu ni kwa nini.Endapo tutagundua kwamba Team SC41 walihusika katika mauaji ya Edson basi mapambano yetu na wao yataanzia hapo.” Akasema Mathew
“ Nimekuelewa Mathew lakini nina wazo moja, kwa nini basi tusianze kwanza kumchunguza Peniela na kufahamu uhusiano wake na Team SC41? Hii inaweza ikaturahishia kazi sana” Noah akauliza
“ Not yet Noah.Suala hili ni kubwa na tutalichimba hadi mzizi wake kwa hiyo suala la kumchunguza Peniela lina wakati wake.Kwa sasa tuelekeze nguvu katika suala la kesho.Tuna kazi ngumu sana kesho” akasema Mathew na majadiliano yakaendelea kuhusiana na kazi kubwa waliyokuwa nayo kesho.

*********************

Ni asubuhi nyingine tena,nchi ikiwa inaendelea na maombolezo kufuatiwa msiba mzto wa Dr Flora Johakim mke wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania.Bado hakukuwa na taarifa rasmi zilizotolewa kuhusiana na nini kilichosababisha kifo chake cha ghafla.Salamu za rambi rambi zilimiminika toka kila pembe ya dunia,watu mbali mbali wakimpa pole Dr Joshua rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Jaji Elibariki akiwa miongoni mwa watu waliokuwa katika pilika pilika nyingi siku hii akastushwa na mlio wa simu .Akaitoa na kutazama mpigaji,alikuwa ni Peniela
“ Peniela !!...” akastuka kidogo.Hakuwa ametegemea kama angepigiwa simu na Penny
“Hallo Penny” akasema Jaji Elibariki baada ya kupokea simu ile
“ Jaji Pole sana kwa matatizo yaliyokupata.Nimestushwa sana na msiba wa mama mkwe wako” akasema Penny
“ Ahsante sana Penny.Ni mapenzi ya Mungu,yeye ndiye mwenye kutoa na kutwaa.Vipi unaendeleaje?
“ Ninaendelea vizuri Jaji Elibariki.” Akasema Penny
“ Nimekutafuta kwa siku kadhaa hukuwa ukipatikana kabisa.Nilipatwa na wasi wasi mkubwa kwamba pengine umepatwa na matatizo”
“ Naomba unisamehe sana Jaji Elibariki,nilipatwa na safari ya ghafla ikanilazimu kuondoka bila hata kuaga.”
“ Ok nashukuru kama umerudi salama.Siku nyingine usifanye hivyo.Unatupa wasi wasi sana sisi ambao tunajali usalama wako”
“ Ndiyo Jaji Elibariki.Siku nyingine sintofanya hivyo” akasema Penny halafu kikapita kimya kifupi
“ Jaji Elibariki samahani kwa kukusumbua mida hii lakini nimekupigia simu nina tatizo kidogo na ninahitaji msaada wako”
“ Una tatizo gani Penny?
“ Sintoweza kukueleza katika simu.Unaweza kupata muda sasa hivi tukaonana nikueleze?
“ Uko wapi mida hii? Akauliza Jaji Elibariki
“ kwa sasa niko nyumbani kwangu” akajibu Penny
Jaji Elibariki akafikiri kidogo na kusema
“ Ok ninapafahamu nyumbani kwako nitafika muda si mrefu.” Akasema Jaji Elibariki na kukata simu
“ Penny ana matatizo gani? akajiuliza jaji Elibariki akiwa bado amesimama katika maua
“ Yawezekana akawa na tatizo kubwa ngoja nikamuone” akawaza na bila kuaga mtu yeyote akaingia katika gari lake na kuondoka
“ Nina hakika lazima atakuwa na tatizo kubwa sana ambalo si rahisi kuelezeka simuni.Lazima nikamsikie ana tatizo gani kwani tayari nimekwisha jitolea kwa hali na mali kumsaidia ,kumlinda na kila anayetaka kumdhuru.Peniela tayari amekwisha niingia katika mishipa ya damu .Toka nilipokutana naye kwa chakula cha usiku,kichwa changu hakitulii,kila mara namfikiria yeye “ akawaza .
Penny alikuwa amejilaza kitandani wakati akiongea na jaji Elibariki
“ Mwili wote unaniuma kwa gwaride alilonichezesha Jason jana usiku.Dah ! Jason kweli ni kidume wa shoka.Mziki wake si mdogo.Anajua kuicheza ngoma na hachoki ana mapafu kama ya farasi.” Akawaza Penny halafu akainuka na kwenda kuchukua glasi ya maji ya matunda
“ Kwa kweli jana Jason amenikuna kiswa sawa na kunifikisha ninapopataka.Ni bahati mbaya sana kwamba siwezi kuwa na kijana huyu katika maisha yangu ingawa ninatamani sana kama angekuwa ni mume wangu nikaishi naye mpaka kifo kitutengenishe.Lakini haiwezekani kwa sababu tayari nimekwisha yaharibu maisha yangu na hayawezi kuwa sawa tena.Sintoweza kupata furaha kamwe..” akawaza Penny na kwenda sebuleni akajilaza sofani
Kengele ya getini ndiyo iliyomstua Penny toka katika kijiusingizi kilichoanza kumpitia.Akainuka na kwenda getini.Alikuwa ni Jaji Elibariki
“ Hallo jaji Elibariki.Karibu sana” akasema Penny na kumkaribisha ndani Elibariki kwa furaha
“ Karibu ndani Jaji Elibariki” Penny akamkaribisha sebuleni
“ Penny just call me Elibariki or Eli.Hayo mambo ya Jaji tuyaache mahakamani.” Akasema Jaji Elibariki na kumfanya Penny atabasamu
“ Ok Eli” akasema Penny huku akicheka kidogo
“ Eli unatumia kinywaji gani? akauliza Penny
“ Naomba mvinyo kidogo kama upo.” Akasema Jaji Elibariki.Penny akamtazama na kutabasamu akaenda na kuchukua chupa ya mvinyo akamminia Elibariki katika glasi
“ Pole sana Jaji Elibariki kwa matatizo yaliyowapata.Dr Flora alifariki kwa ugonjwa gani?
“ Mpaka sasa bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa lakini kwa muda mrefu sasa Dr Flora alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na ninaamini hicho ndicho kilichomuua”
“ Pole sana Eli”
“ Nimekwisha poa Penny.Vipi wewe unaendeleaje ?
“ Ninaendelea vizuri sana Eli.Vipi wewe unaendeleaje?
“ Ninaendelea vizuri pia.Wasi wasi wangu ulikuwa ni juu ya usalama wako”
“ Nashukuru sana Eli kwa kunijali.” Akasema Penny na kimya kifupi kikapita
“ Nimestuka sana uliponiambia kwamba una tatizo nikaona nikimbie mara moja nije nikuone.Una tatizo gani Penny? Akauliza Jaji Elibariki
“ Eli nina tatizo ambalo nataka nikueleze lakini kwanza unaonekana umechoka sana.Unaonekana hukupata usingizi wa kutosha usiku.Hii ni hatari kwako Jaji Elibariki kuendesha gari katika hali hii.You need some rest” akasema penny
“ Ni kweli nimechoka Penny.Mambo yalikuwa mengi sana msibani.”
“ Ok Jaji Elibariki,naomba kwanza kabla ya kurejea msibani upate wakati wa kupumzika walau kidogo hapa kwangu .”
“Penny nikitoka hapa nitaelekea moja kwa moja nyumbani kupumzika.”
“ Hapana Elibariki.Huwezi kuendesha gari ukiwa katika hali hii ya uchovu. Utapumzika hapa na utakapoamka utakuwa tayari kuendelea na majukumu mengine.Naomba usiogope Jaji Elibariki.Hapa ni sehemu salama” akasema Penny.Jaji Elibariki hakujibu kitu akatabasamu
“ Kabla ya kupumzika,twende nikupeleke ukaoge kwanza ili uondoe uchovu.Ninayafahamu mambo ya msiba yanavyokuwa,hutapata hata wasaa wa kujimwagia maji”
“ Kweli kabisa Penny.Mambo ya msibani ni mengi mno” akasema jaji Elibariki.Penny akainuka na kumuongoza hadi chumbani kwake akamfungulia bafu ili Jaji Elibariki aweze kujimwagia maji.
“ Dah ! Kweli Penny anajua kuchunguza watu.Ni kweli nimechoka sana na ninahitaji mapumziko.Toka jana sijapata wasaa wa kupumzika.” Akawaza Jaji Elibariki huku akivua nguo akijiandaa kujimwagia maji
“ Penny anataka kunieleza nini? Ana tatizo gani? akajiuliza
“ Sikuwahi hata mara moja kuingia katika nyumba ya Penny.Ni kubwa na nzuri.Dah ! Penny ni mzuri jamani.Ukimuangalia tu hadi unapatwa na msisimko “ akawaza Jaji Elibariki na mara mlango wa bafuni ukafunguliwa.Jaji Elibariki alipatwa na mstuko wa mwaka.Hakuamini kile alichokuwa akikiona.Macho yalimtoka pima.
“ P…pe..Pee..” akataka kusema lakini maneno hayakutoka
Mlangoni alikuwa amesimama Peniela akiwa na tabasamu usoni huku akiwa mtupu kama alivyozaliwa
TUKUTANE SEHEMU IJAYO…………………………………………
Uyu mwanamke ni shetani anawachanganya wote
 
Sipati picha Mathew atakapogundua John Mwaulaya yupo kwenye mission yake
 
Kwani nani ndio stelingi wa hii story ?

Naona Mathew anataka kumzidi steringi Elibariki Ila ipo poa sana hongera nasa LEGE

JE Una STORY NYINGINE VITABU UNAUZA ?

?vipi hukusu hati miliki ya hii story kama wewe ndio mtunzi pamoja na kutuburudisha ila na wewe upate asali ili tuendeleaa kupata story nzuri kipaji unacho
 
Kwani nani ndio stelingi wa hii story ?

Naona Mathew anataka kumzidi steringi Elibariki Ila ipo poa sana hongera nasa LEGE

JE Una STORY NYINGINE VITABU UNAUZA ?

?vipi hukusu hati miliki ya hii story kama wewe ndio mtunzi pamoja na kutuburudisha ila na wewe upate asali ili tuendeleaa kupata story nzuri kipaji unacho

Kutoa ni Moyo Bro
 
Kwani nani ndio stelingi wa hii story ?

Naona Mathew anataka kumzidi steringi Elibariki Ila ipo poa sana hongera nasa LEGE

JE Una STORY NYINGINE VITABU UNAUZA ?

?vipi hukusu hati miliki ya hii story kama wewe ndio mtunzi pamoja na kutuburudisha ila na wewe upate asali ili tuendeleaa kupata story nzuri kipaji unacho
We jamaa ushaaribu utasikia lege anastisha uduma akieleza vitabu vinapopatikana
 
Back
Top Bottom