Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Orville Lynn Majors
Wahanga waOrville Lynn Majors
Kila mgonjwa aliyewahi kukutana na muuguzi Orville Lynn Majors, alimuona kama nesi mpole na mwenye upendo wa hali ya juu na anayejua kuwahudumia wagonjwa kwa uadilifu mkubwa. Lakini katika hali kushangaza ikawa kila mgonjwa anaehudumiwa na muuguzi huyu katika Hospitali ya wilaya ya Vermillion iliyopo katika jimbo la Indiana akawa anakufa katika mazingira ya kutatanisha.
Mpaka kufikia mwaka 1995 takwimu za idadi ya vifo vilivyokuwa vikitokea katika Hospitali hiyo iliyokuwa na idadi ya vitanda 60 tu vya kulaza wagonjwa ilikuwa ni ya kutisha na hata wafanyakazi wa hospitali hiyo walipoulizwa hawakuwa na majibu ya kuridhisha. Mnamo March 7 1995 uongozi wa hospitali ya Vermillion ulikuwa na wakati mgumu wa kujibu tuhuma hizo kwani kulikuwa na uwezekano wa hospitali hiyo kushitakiwa kwa uzembe wa kusababisha idadi kubwa ya vifo katika hospitali hiyo ambapo watu walihisi kwamba huenda kuna mchezo mchafu unaochezwa na baadhi ya wauguzi wa hospitali hiyo ambao unahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kipolisi.
Uongozi wa hospitali hiyo ulitoa ripoti yao kwa askari wa upelelezi ambao ulikuwa ukionyesha kwamba vifo vilivyokuwa vikitokea kwenye chumba maalum cha wagonjwa mahututi vilikuwa vimeongezeka ghafla kutoka wastani wa asilimia 20 kwa mwaka hadi asilimia zaidi ya asilimia100, kwani watu wapatao 147 walikuwa wamepoteza maisha katika chumba hicho kuanzia mwaka 1993. Polisi walianza kuangalia rekodi za utendaji kazi wa kila mfanyakazi wa hospitali hiyo.
Karibu ripoti zote za watu waliopoteza maisha katika hospitali hiyo jina la Orville Lynn Majors lilitajwa kama muuguzi aliyekuwa zamu katika chumba cha wagonjwa mahututi wakati kifo kinatokea. Polisi pia waligundua kwamba vifo hivyo vya mfululizo vilianza wiki chache tangu Orville aanze kazi katika hospitali hiyo. Kwa mujibu wa rekodi zilizopatikana katika hospitali hiyo ilionyesha kuwa Orville alikuwa zamu wakati vifo vya wagonjwa 130 kati ya vifo 147 vilivyotokea katika hospitali hiyo.
Ripoti hiyo ilikuwa ni tofauti na muonekano na tabia aliyokuwa nayo, kwani alikuwa akijulikana na uongozi wa hospitali hiyo pamoja na wagonjwa waliowahi kutumia hospitali hiyo kama muuguzi mwenye kujituma na mwenye upendo kwa wagonjwa. Baada Polisi kutilia mashaka utendaji wake, mnamo March 9 1995 ilibidi uongozi wa hospitali hiyo umsimamishe kazi ili polisi wapate fursa ya kufanya upelelezi wao kwa ufanisi.
Kwa mshangao wafanyakazi wengi wa hospitali hiyo hawakuamini kama Orville angeweza kuwa mtu wa kwanza kutuhumiwa kwa kusababisha vifo vya wagonjwa katika hospitali ile. Hata hivyo kitendo cha Orville kusimamishwa kilikuja kuibua makosa mengi ambayo aliyafanya bila ya kujulikana wakati akiwa kazini.
Katika uchunguzi uliofanywa hospitalini pale ilikuja kugundulika kuwa Orvile alikuwa akifanya kazi za kitabibu kwa wagonjwa wakati alikuwa hana ujuzi nazo, pia ilikuja kugundulika kuwa alikuwa akiwachoma wagonjwa sindano ambazo kitaalamu huchomwa na mtu maalum aliyesomea ujuzi huo. Kutokana na kugundulika kwa makosa hayo mnamo April 1995 Orville alifukuzwa kazi rasmi.
Msemaji wa Bodi ya wauguzi ya Jimbo la Indiana Gerorge Patton Jr. alimzungumzia Orville kama mtu hatari kwa wagonjwa. Kitendo cha Orville kusimamishwa kazi kilikuwa kimeitikisa taaluma ya uuguzi. lakini polisi walikuwa na mtihani mwingine kwani pamoja na kuamini kwamba Orville alihusika na mauaji ya wagonjwa zaidi ya 100 lakini walikuwa na wakati mgumu wa kupata ushahidi wa kumtia hatiani.
Katika ushahidi uliokusanywa katika ripoti ya vifo vingi vya ghafla vilivyotokea katika hospitali hiyo ulionyesha kwamba vilitokana na moyo kushindwa kufanya kazi ghafla au matatizo yatokanayo na mfumo wa kupumua. Wataalam walidai kwamba kama Orville atakuwa ndiye muuaji, basi atakuwa amewauwa kwa kuwachoma sindano yenye kemikali ya Potashiam Kloraid (Potassium Chloride).
Je ni kitu gani kilichosababisha kuwepo na ugumu kuthibitisha madai hayo?
Kwa kawaida sindano yenye kemikali ya Potashiamu Kloraidi hutumika kwa kuwauwa watu walihukumiwa kunyongwa nchini Marekani, ambapo kwa upande wa Orville kulikuwa hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai hayo. Wapelelezi wa Polisi walitumia miezi 15 kutafuta ushahidi wa kumfungulia mashitaka Orville lakini bado walikwama kupata ushahidi madhubuti.
Ingawa walikuwa wamepata hizo kemikali za potashiamu kloraidi nyumbani kwake lakini huo haukuwa ushahidi wa kuthibitisha madai yao. Pamoja na polisi wa upelelezi kuchukuwa miaka 3 katika upelelezi wao dhidi ya Orville ambao uliwagharimu walipa kodi wa jimbo la Indiana kiasi cha dola milioni moja na nusu lakini bado ushahidi wa kumtia Orville hatiani ulikuwa ni wa kimazingira zaidi.
Kwani wapelelezi wa polisi waliamini kwamba, ikiwa ni kweli Orville alihusika na mauaji ya wagonjwa zaidi ya 130 katika kipindi cha miezi 32 aliyofanya kazi katika hospital hiyo, basi ni wazi kuwa hakuacha ushahidi wowote nyuma yake zaidi ya takwimu tu.
Hata hivyo bado polisi walikuwa na tegemeo jingine la ushahidi kutoka kwa mtaalamu kutoka jimbo la Washington ambao waliongozwa na mwanasayansi aliyejulikana kwa jina la Steven Lamm.
Katika uchunguzi wao ambao uligharimu kiasi cha dola laki tatu, wataalamu hao walikiri kwamba kwanza kuna ukweli wa kimazingira wa kumuhusisha Orville na vifo vya wagonjwa 130 kati ya wagonjwa 147 waliopoteza maisha katika Hospitali hiyo, ambavyo vyote vilitokea Orville akiwa kazini.
Katika ripoti yao ilionyesha kwamba wagonjwa wote waliopoteza maisha katika Hospitali wakati Orville akiwa kazini walikuwa wakifa kila baada ya masaa 23 na dakika 1, isipokuwa mgonjwa mmoja ambae alifariki baada ya masaa 551 na dakika 6, ambapo Orville hakuwepo kazini. Mmoja wa wauguzi wanaofanya kazi katika hospitali hiyo alidai kwamba hali ilikuwa mbaya sana kutokana na kushuhudia vifo vya wagonjwa kila Orville awapo kazini.
Muuguzi huyo alikiri kwamba kuna wakati walikuwa wakicheza kamari kwa kuwekeana dau juu ya mgonjwa gani atakufa pindi Orville atakapokuwa kazini, na mara zote mshindi alikuwa akipatikana na kujizolea kitita cha fedha. Pamoja na ushahidi huo ambao ulielemea zaidi kwenye minong'ono na maneno ya mitaani, lakini bado wapelelezi walikuwa na wakati mgumu wa kujenga ushahidi madhubuti wa kumtia Orville hatiani.
Waliopoteza wapendwa wao wahusishwa na upelelezi...!
Ili kupata ushahidi huo ilibidi wapelelezi wa polisi watumie muda mwingi kuwaita watu ambao ndugu zao walipoteza maisha katika hospitali hiyo na wanao ushahidi kwamba kwa njia moja au nyingine Orville alihusika. Mtu wa kwanza kujitokeza alikuwa ni kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Russell Firestone au kwa jina la utani aliitwa "Rusty".
Kijana huyu alimpoteza baba yake aliyekuwa na umri wa miaka 74 wakati huo. Kijana huyo akitoa ushahidi wake mbele ya wapelelezi wa Polisi, Rusty alisema kwamba baba yake alilazwa katika hospitali hiyo mnamo December 12, 1994, kwa wiki kadhaa baada ya kusumbuliwa na tatizo la kuzimia ghafla. Kijana huyo aliendelea kuwaeleza Polisi kwamba baba yake alipewa ruhusa kabla ya kulazwa tena siku sita baadae katika hospitali hiyo hiyo.
Baada ya kupata tarifa kuwa baba yake amelazwa tena, Rusty alikwenda kumuona na alipofika hospitalini hapo alimkuta Orville na muuguzi mwingine wakiwa pembeni ya kitanda cha baba yake, alipowakaribia alimsikia yule muuguzi akisema kwa sauti "mwanae huyo anakuja" Alipofika karibu na kitanda alichokuwa amelala baba yake alimuona baba yake akipepesa macho na mara ghafla akaacha kupepesa macho na kubaki kimya kama vile mtu aliyekata roho. Alipowauliza kwamba baba yake amepata tatizo gani, walimjibu kuwa hajui, hata hivyo Orville alitoa mashine yake ya kupimia mapigo ya moyo na kumpima baba yake, lakini kulikuwa hakuna dalili za mtu kuwa hai. Baadae Orville alichukuwa box lake alilokuwa nalo na kuchukuwa sindano kisha akaijaza dawa asiyoifahamu na kumchoma baba yake na kutoweka.
Rusty alimuuliza yule muuguzi kama ile sindano ilikuwa ni ya dawa gani lakini hakupewa jibu na badala yake yule muuguzi aliendelea na shughuli zake. Baadae Orville alirejea na hapo ndipo yule muuguzi alipomuuliza kwamba Rusty anataka kufahamu kama ile sindano ilikuwa ni ya nini?
Kwa maneno yake mwenyewe Orville alimjibu kwa mkato "baba yako amekwisha fariki, je kuna mtu unahitaji kumuita?" kisha wote wawili wakatoweka na kumuacha pale peke yake. Mtu mwingine liyetoa ushahidi wake alikuwa akijulikana kwa jina la Robert Doran.
Akiongea na wapelelezi wa Polisi, Robert alisema kwamba anakumbuka baba yao John Andrew Doran aliyekuwa na umri wa miaka 76 wakati huo, alilazwa katika Hospital hiyo mnamo October 1994. Akisimulia zaidi Robert alisema kwamba baba yao alianza kupoteza uzito ghafla na kuwa dhaifu kulikoambatana na kizunguzungu, hivyo walipoona hali ya baba yao imebadilika ghafla vile yeye na mkewe aliyemtaja kwa jina la Marjorie waliamua kumpeleka katika katika hospitali ya wilaya ya Vermillion kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Walipofika Hospitalini hapo baba yao alilazwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi. Siku iliyofuata walirejea pale Hospitalini ili kufuatilia vipimo vya baba yao, lakini walipofika walikuta baba yao amehamishiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi. Robert alibainisha kwamba hapo ndio kwa mara ya kwanza alipomuona Orville.
Kwa maneno yake mwenyewe Robert alisema "Huyu kijana mwenye mwili mkubwa(Akimaanisha Orville kwa sababu alikuwa ni mnene) alifika pale tulipo na kutusalimia na kisha alijitambulisha kwetu"
Huku akimnukuu Orville Robert alisema, "Jina langu naitwa Orville Lynn Majors, mimi ndie nitakayekuwa muuguzi wa baba yenu leo, si mlikuwa mkihitaji muuguzi Mahiri?" kwa jinsi alivyokuwa akizungumza alionekana kuwa ni muuguzi mzuri anayeifahamu kazi yake na ambaye aliguswa na ugonjwa wa baba yetu, aliendelea kubainisha Robert.
Baadae majira ya mchana Robert alikiri kumuona Orville akimchoma baba yao sindano ambayo wote hawakuifahamu na baada ya sindano hiyo baba yao alionekana kupua kwa shida na kuonekana kama vile anataka kupoteza fahamu.Akiwa amesimama pembeni Orville alikuwa akimpiga piga begani baba yao huku akimwambia "subiri kidogo nakuandalia dawa nyingine"
Baadae baba yao alifariki kwa kile kilichoelezwa na daktari kwamba amefariki kwa ugonjwa wa shambulio la moyo (Heart Attack). Robert aliendelea kuwaeleza wapelelezi wa Polisi kwamba baada ya habari za hospitali hiyo kutuhumiwa kusababisha vifo vya watu wengi kutoka katika vyombo vya habari, yeye na mkewe Marjorie Doran waligundua kwamba huenda na wao walishuhudia mauaji ya baba yao akiuwawa na Orville mbele ya macho yao. Kwa maneno yake mwenyewe Robert alisema " Tulijiona wote tuwajinga kwa kukaa kimya baada ya tukio lile ambalo lilifanyika mbele ya macho yao"
Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 1997, bado jopo la wapelelezi walijua dhahiri kwamba isingekuwa rahisi kwao kupata ushahidi wa kina wa kumtia hatiani Orville Lynn Majors.
Mtuhumiwa Kizimbani......!
Hata hivyo kesi ya Orville ilianza kusikilizwa rasmi mnamo December 30 1997 katika mahakama ya wilaya ya Clay. Huku akionekana kutokuwa na wasiwasi, Orville alikuwa ametulia wakati Jaji wa mahakama hiyo aliyejlikana kwa jina la Ernest Yelton alimsomea mashitaka ambayo ni ya kuhusika na mauaji ya watu sita, ambapo akipatikana na hatia adhabu yake itakuwa ni kifungo cha miaka isiyopungua 65.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo wakili wa Orville aliyejulikana kwa jina Marshall Pinkus, alikanusha mashtaka yote yaliyosomwa, kwa niaba ya mteja wake.
Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya Orville kusomewa mashitaka, wakili huyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mteja wake amestushwa sana na mashtaka yale.
Wakili yule aliendelea kusema,
"nadhani kuwa baada ya miaka mitatu mingine huenda mtu mwingine akafunguliwa mashtaka yanayofanana na haya kwa sababu vifo vyote vilivyotokea katika Hospitali ya wilaya ya Vermillion kwa jinsi ninavyofahamu vilikuwa ni vifo vya kawaida kabisa. Siamini kabisa kama kuna mtu alihusika na vifo hivyo."
Akiendelea kufafanua kauli yake wakili yule alisema kwamba kilichotokea ni kuwa kulikuwa na wagonjwa ambao wengi walikuwa wazee ambao walifikishwa katika hospitali hiyo kwa matibabu na kama inavyojulikana kuwa mji wa Vermillion ni mji wa pili kwa ongezeko la watu katika jimbo la Indiana hivyo hospitali hiyo ilishuhudia ongezeko hilo la wagonjwa wengi wazee huku kukiwa hakuna maandalizi yoyote ya kuongeza wataalamu. Wakili huyo aliendelea kubainisha kwamba kimsingi Hospitali ya Vermillion haina wataalam wa kutosha ambao wangekwenda sambamba na ongezeko hilo la wagonjwa ambao hasa wengi walikuwa ni wazee, ambapo kama wangekuwepo vifo hivyo visingetokea.
Naye mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo aliyejulikana kwa jina la Mark Greenwall akionekana kujiamini aliwaambia waandishi wa habari kuwa anayo kesi nzito dhidi ya Orville na kesi hiyo inategemea zaidi ushahidi kutoka kwenye jopo lake la wapelelezi wakishirikiana na wataalamu wa kitabibu ambao ndio waliopewa jukumu la kuchunguza vifo 160 vilivyotokea katika hospitali hiyo kati ya mwaka 1993 na mwaka 1995, ambapo asilimia 50 ya vifo hivyo vilionekana kutokea katika mazingira ya kutatanisha.
Akizungumzia kitendo cha Orville kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya watu 6 tu badala ya watu 160 ambao ndio aliokuwa akituhumiwa kuwauwa awali, Greenwall alisema kwamba kitendo cha Orville kufunguliwa mashtaka ya watu sita tu hakimaanishi kuwa kulikuwa na vifo vya watu sita tu, bali walichukuwa kesi za watu sita ambazo walikuwa na uhakika wa kupata ushahidi wa kutosha ambao ungemtia Orville hatiani bila ya kutia shaka yoyote. Baada ya Orville kusomewa mashtaka, nje ya mahakama ile ambayo ilifurika umati wa watu ambao walikuwa wakiifuatilia kesi ile ambayo ilivuta hisia za watu wengi, miongoni mwao wapo waliokuwa wakimtetea Orville.
Akizungumza nje ya mahakama mdogo wake na Orville aitwae Debbie McClelland alisema kuwa kaka yake hana hatia kwa sababu hakuhusika na mauaji ya yale. Kwa maneno yake mwenyewe Debbie alisema "tangu uchunguzi wa kesi hii uanze na mpaka kufikia sasa hivi ambapo kesi ipo mahakamani wazazi wetu wamekuwa na wakati mgumu sana na hii imevuruga kwa kiasi kikubwa maisha yao lakini mungu anatupa nguvu na kuendelea na maisha yetu kama kawaida, japokuwa tunatiwa moyo na majirani zetu lakini hali si ya kuridhisha pale nyumbani"
Naye mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina la Ida Harris ambaye aliwahi kuwa muhudumu wa wazazi wa Orville pale nyumbani kwao wakati fulani alisema kuwa kwa jinsi anavyomfahamu Orville haamini kwamba alihusika na mauaji yale, na anaona kabisa kwamba hawamtendei haki. Kesi ile ambayo iliahirishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi mwaka 1999, ilipangwa kuhamishiwa katika mji mwingine uitwao Brazil ambao upo maili kadhaa kutoka katika mji wa Vermillion kusini mwa mji mwingine wa Terre Haute, na hii ilitokana na kwamba mji huo ndipo idadi ya watu waliopoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha katika Hospitali ya Vermillion County ni kubwa.
Mashahidi wapatao 79 walijitokeza kutoa ushahidi wao ambapo wengi walikiri kumuona Orville akiwachoma sindano ambazo zilipelekea vifo vya wapendwa wao, ambapo kimsingi alikuwa haruhusiwi kuwachoma wagonjwa sindano hizo. Mnamo October 17, 1999 Orville alipatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya watu sita na hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani, bila uwezekano wa kifungo cha nje (Parole).