Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imeanza kutumia Mfumo wa Mashauri wa Mahakama wa Kieletroniki ili kuongeza matumizi ya TEHAMA

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI KUTUMIA MFUMO WA KIELEKTRONIKI WA MASHAURI WA MAHAKAMA KUU

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imeanza kutumia Mfumo wa Mashauri wa Mahakama wa Kieletroniki ili kuongeza matumizi ya TEHAMA, uwazi, uwajibikaji, upatikanaji wa taarifa kwa haraka na imani kwa wananchi kuhusu utendaji kazi wa vyombo vinavyotoa haki kwa wananchi.

Hayo yameelezwa na Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Mark Mulwambo wakati akifungua mafunzo elekezi kuhusu Mfumo wa Kieletroniki wa Mashauri ya Mahakama Kuu ya Tanzania (e-CMS) na utunzaji wa nyaraka za Serikali ambapo ufunguzi huo umefanyika 11/01/2024 mjini Morogoro na kusema kuwa OWMS imeona ni muhimu kwa watumishi wake kupata mafunzo kuhusu Mfumo wa Mahakama wa e-CMS ili waweze kuutumia kwa pamoja na kusomana na mfumo wa usajili wa mashauri wa OWMS (CIMS) kwa lengo la kuboresha utendaji kazi, kuongeza tija na ufanisi katika usajili, matumizi na uendeshaji wa mashauri baina ya Mahakama, OWMS, wadau na wananchi.

Ameongeza kuwa Mfumo wa e-CMS umefanikisha yafuatayo ikiwemo utoaji wa taarifa kwa wahusika wa shauri kuwa shauri lao limesajiliwa na kupangiwa Jaji au Hakimu; umetoa mwanya wa kujumuisha taarifa za taasisi nyingine za Serikali ili ziweze kutumika na kusomana;
utaendana na taratibu za utendaji wa Mahakama; Majaji wanaandika mwenendo wa mashauri kwenye Mfumo badala ya kuandika kwenye majalada; unapanga mashauri kwa kila Jaji badala ya Jaji mmoja kuwa na mashauri mengi au machache.
Pia, Mfumo wa Mahakama wa e-CMS umefanikisha usajili wa namba ya utambuzi wa kesi ambayo haijirudii na kutumiwa na Mahakama nyingine; umesajili taarifa za mashauri ya Mahakama ya Rufaa ambapo hapo awali haikuwepo;

Umetambua na kuruhusu matumizi ya taarifa kutoka NIDA, BRELA, Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na taarifa za taasisi nyingine; umetambua na kubaini usajili wa Mawakili na Waendesha Mashtaka halali kwa kuwatambua kwa namba zao na sio vinginevyo.

Mulwambo amewapongeza Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kujenga Mfumo wa e-CMS kwa kuwa haki itapatikana kwa wakati kwa watu wote bila kujali mahali alipo kwa kutumia TEHAMA na kwa kuzingatia kuwa OWMS ni mdau muhimu hivyo mafunzo kuhusu Mfumo wa e-CMS yanatolewa kwa washiriki 27 kutoka OWMS na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuwawezesha watumishi kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya usajili wa mashauri, utunzaji wa kumbukumbu za kielektroniki na namna nzuri ya kuwahudumia wateja wa ndani na nje.

Aidha, amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kutumia ujuzi watakaoupata na kuyafanyia kazi kwa kuzingatia uadilifu na usiri katika utendaji kazi kwa kuwa Masjala ya Sheria ni Ofisi nyeti katika kutunza nyaraka za Serikali.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masjala ya Sheria wa OWMS, ndugu Dennice Leonard amesema kuwa Mfumo wa Mahakama wa e-CMS utawawezesha wananchi kupata taarifa na kufuatilia mwenendo wa mashauri Mahakamani kwa kupata ujumbe kwenye simu zao za mkononi na barua pepe.

Pia, Katibu Sheria wa OWMS, Bi. Victoria Kawacha ameshukuru ujenzi wa Mfumo wa Mahakama wa e-CMS kwa kuwa utarahisisha utendaji kazi na kupunguza muda wa kuandika taarifa za mashauri na nyaraka mbali mbali kwenye majalada kwa kuwa taarifa zitapatikana kwenye Mfumo huo.

Imetolewa na:

Prisca J. Ulomi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

MAELEZO YA PICHA MAFUNZO YA MFUMO WA MAHAKAMA
PICHA NA.1.jpg

Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Ndg. Mark Mulwambo (aliyeketi kulia) akizungumza na Makatibu Sheria wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati akifungua Mafunzo Elekezi kuhusu Matumizi ya Mfumo Mpya wa Mahakama wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (e-CMS) yaliyofanyika Mkoani Morogoro. Aliyeketi kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masjala ya Sheria Ndg. Dennice Leonard wa Ofisi hiyo.
PICHA NA.2.jpg

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masjala ya Sheria Ndg. Dennice Leonard wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali akichangia mada kuhusu namna Mfumo Mpya wa Mahakama wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (e-CMS) unavyofanya kazi wakati wa mafunzo yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
PICHA NA.3.jpg
PICHA NA.3A.jpg
PICHA NA.3B.jpg
PICHA NA.3C.jpg

Baadhi ya Makatibu Sheria wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wanaoshiriki Mafunzo Elekezi kuhusu Matumizi ya Mfumo Mpya wa Mahakama wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (e-CMS) wakifuatilia mada kuhusu namna mfumo huo unavyofanya kazi katika mafunzo hayo yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
PICHA NA.4.jpg

Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Ndg. Mark Mulwambo (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Makatibu Sheria wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mara baada ya kufungua Mafunzo Elekezi kuhusu Matumizi ya Mfumo Mpya wa Mahakama wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (e-CMS) yaliyofanyika Mkoani Morogoro. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Masjala ya Sheria wa Ofisi hiyo Ndg. Dennice Leonard na wa kwanza kushoto ni Wakili wa Serikali, Bi. Emma Ambonisye.
 
Back
Top Bottom