Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,409
- 33,287
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki
Mkoa wa Dar es Salaam unatarajia kuendesha zoezi la kubomoa nyumba zote na sehemu za biashara zilizojengwa chini ya nyaya za umeme wa msongo mkubwa, likiwamo soko la wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama 'Wamachinga' lililopo eneo la Tazara Vetenari.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Meck Sadiki, wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri kusimamia zoezi hilo, ambalo alisema anataka lianze mara moja.
Alisema ni hatari kwa watu kujenga na kuendesha shughuli zao chini ya nyaya za umeme wa msongo mkubwa kwa kuwa kunaweza kuhatarisha maisha yao mali zao.
Mkoa wa Dar es Salaam ni vurugu tupu. Na nawaagiza watendaji wote wa halmashauri tatu za mkoa huu kuhakikisha wavamizi hao wanaondolewa haraka ili sehemu hizo zibaki wazi, alisema.
Alisema amelijulisha Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), kuhusiana na zoezi hilo na kwamba wote waliovamia, hakuna atakayepona.
Ukicheka na nyani utavuna mabua. Hatuwezi kuendelea kuona watu waliovamia maeneo ya chini ya nyaya za umeme wa msongo mkubwa wakiendelea kukaa hapo na kuendesha shughuli zao, alisema.
Alisema hata kama watu hao walipewa maeneo hayo kihalali lazima waondoke kwa kuwa hairuhusiwi kujenga kitu chochote chini ya nyaya za umeme.
Kuhusu wamachinga, Sadiki aliagiza Manispaa ya Ilala kuanza kuwaondoa wale wanaofanya biashara zao jirani na lango la kuingilia ofisini kwake na kama wameshindwa kufanya kazi hiyo waseme ili aifanye yeye mwenyewe.
Nataka wamachinga wote wanaofanya biashara sehemu za watembea kwa miguu waondoke na kuacha maeneo hayo yakiwa wazi. Na hili lazima lisimamiwe na manispaa zote tatu za jiji la Dar es Salaam, alisema.
Aliwataka watendaji mkoani humo kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuvikimbia vyombo vya habari na kwamba kama kila mmoja atatimiza wajibu wake, atawaona waandishi wa habari marafiki zake.
Timizeni wajibu wenu kama mtaona mnafuatwafuatwa na vyombo vya habari. Kinachofanya mfuatwefuatwe ni kutokana na utendaji wenu mbovu na mapungufu mbalimbali mliyonayo, alisema.
Kuhusu fidia kwa wakazi wa mabondeni waliokumbwa na mafuriko mwishoni mwaka jana eneo la Jangwani na Msimbazi ambao walipewa viwanja eneo la Mabwepande Wilaya ya Kinondoni, Sadiki alisema serikali haina mpango wowote wa kuwajengea nyumba wananchi hao.
CHANZO: NIPASHE