Nukuu 6 za kurejesha hamasa na matumaini pale maisha yanapokua tofauti na matarajio

Manyanza

JF-Expert Member
Nov 4, 2010
9,527
14,403
Nukuu hizo 6 ni hizi zifuatazo

1. FURAHA NA HUZUNI
Khahlil Gibran alijibu baada ya kuulizwa kuhusu furaha na huzuni akasema "Furaha yako ipo ndani ya huzuni yako.Kicheko kikubwa na tabasamu pana usoni mwako huwa linakuja kufuatia matukio ya kukutoa machozi.

Ukubwa wa furaha yako unategemea ukubwa wa huzuni yako. Kadiri huzuni yako inakuwa kubwa sana yenye kukutoa machozi huwa ni kiashiria cha furaha kubwa sana ambayo ipo njiani. Furaha yako haipo popote pale uendapo isipokuwa ndani ya huzuni yako.

Kila kitu kizuri chenye kuleta furaha sana machoni kwa watu huwa kimepatikana baada ya màumivu makali katika maandalizi yake.

Umewahi kujiuliza nini kinafanya MWANAMKE kulia machozi ya furaha baada ya kujifungua? Furaha yake imekuja ndani ya huzuni yake ambayo ilikuwa ni màumivu ya kulea ujauzito miezi 9.

Wingi wa maumivu moyoni huwa kiashiria cha wingi wa furaha. Giza ndio mshumaa wako alisema Rumi.

Watu hushangilia sana ushindi mpaka machozi yanatoka baada ya kupitia maumivu makali sana katika mchakato wa mashindano hayo.

Furaha yako ipo ndani ya huzuni yako. Utatoa machozi kwa huzuni na vilevile utatoa machozi ya furaha baada ya huzuni yako kuondoka. Mwanzo wa kila kitu huwa mwisho wa kitu kingine Kila ifikapo mwisho wa safari au tukio fulani huwa mwanzo wa safari au tukio lingine.

Unaweza kuanza upya baada ya mahusiano kuvunjika au kifo cha umpendaye au kupoteza fursa au fedha nyingi sana ambazo kwako ilikuwa msaada mkubwa sana na nguzo ya maisha yako.Zingatia mwisho wa kitu chochote huwa mwanzo wa kitu kingine.

2. HAKUNA CHENYE KUDUMU MILELE
Tabasamu lako au huzuni yako iwe yenye kukufahamisha kwamba hakuna kitu chochote chenye kudumu milele.
Katika maisha yako zingatia kwamba kuna afya na maradhi, kusifiwa na kukosolewa, kupewa pongezi na kuzomewa, kufaulu na kufeli, kupata na kukosa.

Hakuna chenye kudumu milele fedha zinakuja na kuondoka, fursa zinakuja na kuondoka,cheo kinakuja na kuondoka, umaarufu unakuja na kuondoka, mahusiano yanajengwa na kuvunjika,ajali zinatokea, umri unasogea, vitu vyenye thamani vinapoteza thamani kwa vitu vipya kuzalishwa, ujana unakuja na kuondoka, na mwisho kabisa sisi sote tutakufa.

Unapotambua kwamba hakuna kitu chochote chenye kudumu milele utaacha kujitesa sana kama umepata taarifa mbaya sana au nzuri sana.

Unaweza kuwa mwenye furaha sana lakini je furaha yako itadumu kwa muda gani ? Hata ukiwa kwenye huzuni jiulize je huzuni yako itadumu kwa muda gani?

Unaweza kupata taarifa mbaya fikra zako zikakwambia huu ni mwisho wa ulimwengu lakini sio kweli mara ngapi umepokea taarifa mbaya lakini baadaye ikaja kuwa taarifa nzuri tofauti na matarajio yako.

Mara ngapi umekosa nafasi au fursa sehemu lakini baadaye ikawa mwanzo wa fursa nzuri kuliko ya mwanzo. Unaweza kupata taarifa nzuri ukawa na furaha sana lakini baadaye inakuwa tofauti na matarajio yako na unaweza kupata taarifa mbaya lakini baadaye inakuwa taarifa nzuri sana.

3. WEKEZA NGUVU SEHEMU UNAWEZA KUDHIBITI TU
Huwezi kupanga matukio gani yatokee katika maisha yako lakini unaweza kupanga cha kufanya kwa kila tukio lenye kutokea maishani mwako.

Huwezi kuzuia watu wengine kukusema vibaya,huwezi kuzuia ajali kutokea,huwezi kuzuia watu wengine kufanya makosa, huwezi kuzuia watu wengine kufanya maamuzi tofauti na matarajio yako.

Ni hulka ya binadamu kutamani watu wengine kuishi vile anavyotaka lakini kiuhalisia haiwezekani. Kila mtu anaishi kwa kuongozwa na akili yake sio matarajio yako kwake. Kila mtu anaamini yupo sahihi kwa kile ambacho anafanya au kusema.

Ukipata tatizo lolote angalia chanzo cha tatizo husika kama ni maamuzi ya wengine maana yake huwezi kuzuia maamuzi ya wengine ila unaweza kudhibiti maamuzi yako eneo hilo.

Unaweza kufanya kila kitu kwa usahihi lakini hupati matokeo mazuri hiyo ni kawaida kwa sababu huwezi kudhibiti matokeo bali unadhibiti juhudi zako.

4. TAMBUA KWAMBA MATATIZO YATAKUJA KWAKO

Matatizo yatakuja kwako iwe unatarajia au huna matarajio kabisa. Matatizo hayatazami malengo yako, matatizo hayatazami machozi yako, matatizo hayatazami kama wewe ni mchamungu au mshirikina, matatizo hayatazami kama wewe unasaidia sana watu au huna huruma kabisa, matatizo hayatazami kama wewe ni muongo au mkweli.

Matatizo hayatazami kama wewe ni mlemavu au upo na viungo kamili, matatizo hayatazami kama huna akiba ya fedha au upo nazo.

Matatizo hayatazami kama UMEZALIWA katika familia ya kimaskini kupita kiasi au kitajiri sana, matatizo hayatazami kama umesoma au hujasoma kabisa.

matatizo hayatazami kama huna ndugu wa kukupa faraja au upo nao, matatizo hayatazami kama upo na watoto au huna uzazi, matatizo hayatazami kama umefanya juhudi kubwa sana au hujafanya juhudi zozote.

Matatizo hayatazami kama wewe ni mgonjwa au mzima, matatizo hayatazami kama upo ugenini au nyumbani, matatizo hayatazami kama wewe ni muaminifu sana au msaliti.

Matatizo hayatazami kama wewe ni yatima au upo na wazazi, matatizo hayatazami kama wewe ni kijana au mzee, matatizo hayatazami kama upo kwenye ndoa au ni mjane au umepeana talaka na mwenza wako.

5. HILI NALO LITAPITA
Ni hulka ya binadamu kuchanganyikiwa kama haoni matokeo mazuri baada ya kufanya juhudi kubwa sana kuondokana na maumivu makali sana.

Haijalishi utakuwa unapitia kipindi kigumu sana kifedha,iwe ni kufukuzwa kazi,iwe talaka,iwe msiba,iwe ugonjwa,iwe ni ugomvi na mwenza wako au mwajiri n.k bado hili nalo litapita.

Siku hata ikiwa mbaya kiasi gani bado usiku nyengine itaingia.Maisha lazima yataendelea tu.

Katika maisha yako utapoteza watu wengi sana kama marafiki, ndugu, wafanyakazi wenzako,mwenza wako,watoto wako au wazazi wako kwa njia zifuatazo kifo chake, au kutengana au kuhama makazi au mahusiano kuvunjika.

Hauwezi kuwa binadamu wa kwanza duniani kupitia kipindi kigumu iwe msiba,iwe talaka,iwe ajali,iwe ugonjwa,iwe kufukuzwa kazi, iwe kupata kesi mahakamani,iwe ugomvi na mwenza wako,iwe utovu wa nidhamu wa watoto,iwe kufeli masomo n.k bado utagundua wapo mamilioni ya watu wengine duniani wanapitia kipindi kigumu sana kama cha kwako.

Haijalishi utakuwa unapitia kipindi kigumu sana bado haiwezi kuwa mwisho wa ulimwengu.

Ulimwengu haujafika mwisho wakati wa vita vya dunia, ulimwengu haujafika mwisho wakati wa biashara ya utumwa, ulimwengu haujafika mwisho wakati wa mlipuko wa COVID-19, ulimwengu haujafika mwisho wakati wa mapinduzi ya viwanda, ulimwengu haujafika mwisho kwa sababu ya ajali, mabomu,vita,magonjwa, ukosefu wa ajira n.k.

Yeyote ambaye atakupenda au kuvunja mahusiano na wewe haiwezi kuwa mwisho wa ulimwengu kwa sababu sio tukio jipya hapa ulimwenguni.

6. VIKWAZO NDIO NJIA
Ukipata matatizo ni kawaida kabisa kuona moyo kwenda mbio, kizunguzungu, kuchanganyikiwa, tumbo kuvurugika, kuumwa kichwa na mgongo, uchovu mwili mzima, kubanwa kifua, pumzi kuwa ngumu, kuumia kooni, kutetemeka,kuona aibu,kuona ukungu,kuwa na hasira, kuwa na huzuni, kujichukia, kujiona mpweke, kujiona kituko, kujiona huna thamani,kuanza kulia, kujifungia chumbani kukwepa macho ya wengine.

Hayo ni mabadiliko ya mwili sio mwisho wa ulimwengu. Maumivu hayo yanaweza kukufanya ukaanza kujilaumu, kujikosoa,kulaumu wengine,kukata tamaa ya maisha.

Zingatia kwamba kikwazo kikubwa huwa njia ya mafanikio katika maisha yako. Kitu chochote chenye kuumiza hisia zako huwa kinatoa mafunzo sio mateso.

Makosa yanatupa uzoefu na uzoefu unatupunguzia makosa.
 
Umewahi kujiuliza nini kinafanya MWANAMKE kulia machozi ya furaha baada ya kujifungua? Furaha yake imekuja ndani ya huzuni yake ambayo ilikuwa ni màumivu ya kulea ujauzito miezi 9.
. .
No the tears are from seeing our cute babies after having them stuck at the wrongest of places for hours!!!

Ok ngoja nimalize kusoma
 
Back
Top Bottom