Nini matokeo ya mapinduzi ya kijeshi Niger?

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
Na Ahmed Rajab

WIKI imepita kama upepo tangu Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (Ecowas) itangaze kuwa inawapa wapinduzi wa kijeshi wa Niger muda huo wa wiki moja wamrejeshe madarakani Rais waliyempindua, Mohamed Bazoum, na wayazime mapinduzi yao.

Ecowas ikatoa vitisho kwamba lau wapinduzi wasipoyatimiza hayo watakiona cha mtema kuni: majeshi kutoka nchi za Ecowas yataivamia Niger kuyazima kwa nguvu mapinduzi hayo na wakati huohuo Niger ikawekewa vikwazo kadhaa.

Kwa miezi sasa, picha, kama wasemavyo vijana mitaani zilikuwa hazendi baina ya Bazoum na mkuu wa kikosi maalum cha kumlinda Rais, Jenerali Abdourahamane Tchiani, ambaye pia anaitwa Omar Tchiani. Bazoum akatia na kutoa, amuondowe au asimuondowe Tchiani.

Hatimaye, tarehe 24 Julai, Bazoum aliliarifu Baraza la Mawaziri kwamba atampokonya Tchiani wadhifa wake. Habari hizo zilivuja zikamfikia Tchiani na wanajeshi wake. Hali ya kikosi chao ikawa hamkani, haikuwa shuwari tena.

Kwa hakika, hata kabla ya hapo shirika la kijasusi la Marekani, CIA, na lile la Ufaransa la Direction générale de la Sécurité extérieure (DGS) yalishajua kwamba Bazoum atamuondoa Tchiani.

Shirika la DGS liliiarifu serikali ya Ufaransa na likaeleza hatari inayoweza kutokea lau Bazoum atachukua hatua hiyo. Lakini Rais Emmanuel Macron na serikali yake hawakuzitia sana maanani taarifa hizo wala hawakutafuta njia za kumkinga Bazoum.

Macron, ni mtu wa ajabu. Licha ya kuishi na kufanya kazi Nigeria kwa muda, kwa hakika, halielewi bara la Afrika na watu wake. Tangu awe Rais 2017, Macron amekuwa akipelekewa taarifa rasmi za kijasusi kuhusu vuguvugu dhidi ya Ufaransa linalozidi kupata nguvu katika miji mikuu ya nchi ambazo zamani zikitawaliwa na Ufaransa katika ukanda wa Afrika Magharibi.

Kwa hivyo si kwamba alikuwa hajui kwamba kuna wimbi kubwa la uhasama dhidi ya Ufaransa katika eneo hilo. Lakini jeuri na kiburi zimeyafanya macho yake yawe mazito kufunguka na kuuona uhalisia wa mambo ulivyo.

Tchiani na wanajeshi wenye kumuunga mkono walighadhibika waliposikia njama alizokuwa anazipanga Bazoum dhidi yao. Usiku wa tarehe 26 Julai wakaamua kumpindua.

Ilipogonga saa tisa za alfajiri, wakati jiji la Niamey likiwa limelala, wanajeshi hao walipanda kwenye magari ya kivita wakaelekea Ikulu. Walibeba makombora na silaha nyingine nzitonzito. Walipofika kwenye lango la Ikulu, kama walivyotarajia, waliwakuta walinzi wakiwa na bastola na bunduki tu. Waliwapokonya silaha hizo wakaingia ndani. Walitawanyika kwenye bustani ya Ikulu na Tchiani akaingia ndani kwenye makazi ya Bazoum.

Mambo yalipochacha ndani ya Ikulu, Bazoum alitoka ofisini mwake akakimbilia kwenye chumba maalum kwenye ghorofa hiyohiyo ya chini ya Ikulu. Chumba hicho kina lango nene lililotengenezwa kuzuia risasi zisiweze kupenya. Bazoum, mwenye umri wa miaka 63, alijibanza nyuma ya lango hilo.

Wiki kadhaa kabla, Bazoum aliagiza chumba hicho kifanyiwe ukarabati na hilo lango likazidi kuimarishwa. Sijui kama alioteshwa au moyo wake ulimpa tu afanye hivyo. Chumbani humo pia alikuwamo mkewe, Hadiza Mabrouk Bazoum na mtoto wao wa kiume, Salem.

Bazoum akitumia simu nyerevu aliyo nayo aliwasiliana na baadhi ya washauri wake na Balozi wa Niger, jijini Washington, Kiari Liman Tinguiri, Aliwaeleza kwamba ameshikwa mateka na walinzi wake akawataka washauri wake wapeleke majeshi ya kawaida kwenda kumuokoa na akamwambia Tinguiri aisihi Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati kuinusuru demokrasia ya Niger.

Bazoum aliwahakikishia washirika wake wa Kimarekani na Kifaransa kwamba wasiwe na wasiwasi ataokolewa na wanajeshi wa kawaida. Akizungumza na washauri wake aliwaomba kwa mafumbo wafanye kila njia wayapeleke majeshi ya kawaida kwenda kumuokoa.

Wanajeshi wa kawaida, kwa upande wao, wakisubiri amri za makamanda wao wafanye nini. Makamanda nao wakitazama upepo unavuma upande gani. Hawakuonesha mori na raghba ya kwenda kumuokoa Bazoum aliyekuwa mateka wa akina Tchiani ndani ya Ikulu.

Kwa ufupi, hakujitokeza wanajeshi waliokuwa tayari kupambana na wapinduzi na kumrejesha Bizoum madarakani. Kwa hivyo, mapinduzi yalifanikiwa bila ya mapigano au umwagaji damu. Haya ni mapinduzi yaliyofanywa na kikosi kimoja tu cha majeshi ya Niger — kikosi cha kumlinda Rais.

Kama nilivyogusia kwenye makala yetu ya wiki iliyopita, mapinduzi hayo yamezusha balaa na pia maswali mengi yanayostahiki kuzingatiwa na kujibiwa. Yanahitaji kujibiwa si kwa maslahi ya Niger pekee au hata ya ukanda wa nchi za Sahara/Sahel lakini kwa maslahi ya bara zima la Afrika.

Maswali hayo yamekaa kama donge la uzi wenye mazongezonge. Katika makala haya tutazishika nyuzi za baadhi ya maswali hayo na kujaribu kuzifumua.

Kwanza tukubaliane kwamba tunayoyazungumza hapa ni mapinduzi ya kijeshi, ya wanajeshi kuupindua utawala wa kiraia au wanajeshi kupinduana wenyewe kwa wenyewe. Hatuzungumzii mapinduzi kwa dhana yake asilia ya mapambano ya watu wa tabaka fulani, wenye itikadi fulani ya kisiasa na wanaotaka kuleta mageuzi makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Aghalabu mapinduzi kama hayo huwashirikisha wananchi wanaokuwamo kwenye vuguvugu la kuleta mageuzi. Aghalabu pia wananchi hao hupigana kwa silaha ili wajipatie muradi wao. Mifano ya mapinduzi ya aina hayo ni kama yale yaliyoongozwa na Mao Zedong wa China, Fidel Castro wa Cuba, Amilcar Cabral Guinea-Bissau na Cape Verde na hata ya Samora Machel nchini Msumbiji.

Pamoja na kupigana ili wajikomboe wanamapinduzi hao huwa wanawaamsha wananchi kwa kuwapa masomo ya kiitikadi na ndio maana waliungwa mkono kwa dhati na umma wa nchi zao.

Wapinduzi wa kijeshi, kwa upande wao, huchukua hatua zao, wakiwa juu, wao kwa wao bila ya kuwahusisha au kuwashirikisha wananchi wenzao walio chini. Mara nyingi wanajeshi wanaopindua huwa wa ngazi za juu jeshini, kina Jenerali Ibrahim Babangida wa Nigeria au Jenerali Pervez Musharraf wa Pakistan au Jenerali Augosto Pinochet wa Chile.

Huu mchomoko wa mapinduzi ya kijeshi ya miaka ya hivi karibuni katika Burkina Faso, Mali, Guinea na sasa Niger ni wa aina yake. Waliopindua ni vijana. Tena ni watu wanaoielewa historia ya nchi zao, hususan uhusiano wao na Ufaransa iliyowatawala zama za ukoloni na inayoendelea kudumisha uhusiano wa kikoloni kati yake na makoloni yake ya zamani.

Wapinduzi hao vijana wanaiangalia mikataba iliyoafikiwa kati ya Ufaransa na viongozi wao wa wakati wa uhuru na wanaona kwamba bado Ufaransa inazidhibiti vilivyo nchi zao. Inazitawala kwa mlango wa nyuma kwa ule mfumo uitwao ukoloni mamboleo. Na wanasema kwamba sababu moja kubwa ya watu wao kuwa mafukara ni namna chumi za nchi zao zinavyokabwa roho na Ufaransa.

Wanakumbuka jinsi Ufaransa ilivyozilazimisha nchi zao zitumie sarafu ya franca ya CFA na wanakumbuka pia kwamba ni hivi karibuni tu Ufaransa iliregeza kamba kidogo na kuziruhusu nchi zao ziweke asilimia ya sarafu zao za kigeni katika hazina ya Benki Kuu ya Ufaransa.

Wanaikumbuka kauli ya Rais wa zamani wa Ufaransa François Mitterrand kwamba katika karne ya ishirini na moja, Ufaransa bila ya Afrika, itaporomoka na kuwa dola ya ulimwengu wa tatu. Kwa ufupi, haitokuwa na lake jambo kwani imekuwa ikijitutumua kwa sababu ya utajiri inaoupora kutoka Afrika.

Kwa hakika, hizi kelele zinazopigwa sasa na Ufaransa, ikisaidiwa na madola mengine makuu ya Magharibi pamoja na umoja wa kijeshi wa NATO dhidi ya wapinduzi wa Niger, zisingepigwa lau nchi hiyo isingekuwa na akiba kubwa ya madini ya urani (uranium). Kwanza ya Niger ni ya aali, ya babu kubwa, na pili ndiyo yanayotegemewa sana na Ufaransa kwa ufuaji wa nguvu zake za kinuklia.

Wapinduzi hao wa kijeshi wanataka kuuvunja uhusiano usio sawa wa kiuchumi na wa kijeshi baina ya nchi zao na Ufaransa kwani Ufaransa imejiingiza vibaya sana kijeshi katika ukanda mzima wa Sahel/Sahara. Ina kambi za kivita, wanajeshi na vituo vingine nyeti vya kiusalama na kijasusi katika eneo zima hilo.

Wapinduzi wa kijeshi wanataka nchi zao zijitoe kwenye udhibiti huo wa Ufaransa, Marekani na NATO na badala yake zifaidike na uhusiano na madola mengine yanayoibuka na kuwa na nguvu za kiuchumi duniani. Miongoni mwayo ni mataifa ya lile kundi la BRICS (Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini) pamoja na Iran.

Kundi la BRICS ambalo litakuwa na mkutano mkuu wa viongozi wake Agosti 22 hadi 24 mwaka huu huko Afrika Kusini, linatazamiwa kutanuka na kuunda mifumo mbadala ya miala mipya ya kifedha na kiuchumi duniani. Hicho ni kitisho kikubwa kwa madola ya Magharibi. Hiyo ni moja ya sababu kwa nini nchi za Magharibi zikawa safu ya mbele kuyalaani mapinduzi ya kijeshi katika baadhi ya nchi za ukanda wa Sahel.

Madola ya Magharibi yamekuwa yakihoji kwamba mapinduzi hayo lazima yazimwe ili kuirejesha demokrasia katika nchi zilizokumbwa na mapinduzi hayo ya kijeshi. Lakini wananchi wa nchi hizo pamoja na wengi wengine katika nchi za Kiafrika wanaiona hoja hiyo kuwa ni kisingizio tu.

Wao, kwa upande wao, wanahoji kwamba katika Afrika bado hakuna taifa lenye demokrasia halisi. Wanasema hii iitwayo ‘demokrasia’ ni kiigizo bubu kisicho na maana kwa sababu huo mfumo wa demokrasia uliopo hauiani na uhalisia wa demokrasia. Mfumo huo umekuwa ukiruhusu chaguzi zisizo halali, ufisadi na utengwaji wa wananchi katika hatua muhimu za ukataji maamuzi ya kiutawala.

Kwa ufupi, mfumo huo umesababisha utawala mbovu katika takriban nchi zote zenye kuufata Afrika Magharibi na kwengineko katika Afrika. Katika hali hiyo ndio maana wengi wa wazalendo wa Kiafrika wanayaunga mkono mapinduzi hayo ya kijeshi Afrika Magharibi.

Hata hivyo, tunajua kwamba vita dhidi ya ubeberu na ukoloni mamboleo lazima viendane sambamba na ukombozi wa umma kwa kuwapa wananchi nguvu na madaraka halisi.

Kwa muktadha huo, wakati mapinduzi hayo yanaungwa mkono na wapinduzi wanashangiliwa kwa kuzivunja nguvu za nchi kama Ufaransa, lazima wawe wanakumbushwa kwamba hawatolitendea haki bara la Afrika lau watajibadili sura na kuanza kushiriki katika ufisadi na kuwakandamiza wananchi. Ni muhimu kwamba wakawa safu ya mbele kwa kushirikiana na wananchi ili kutafuta mifumo mibadala ya demokrasia shirikishi itayowapa uwezo wananchi wa kawaida kushiriki katika maamuzi yahusuyo mustakbali wao.

Baada ya kushindwa kutumia nguvu za kijeshi kuwatimua wapinduzi wa Niger, kesho jumuiya ya Ecowas itakutana Abuja kuangalia ni hatua gani zichukuwe kutimiza lengo lake la kumrejesha madarakani Bazoum.

Mpaka sasa sijui vipi suluhisho la maafikiano linaweza kupatikana kwa kuwa wapinduzi wa Niger wanakataa kukutana na wajumbe wa Ecowas, wa Umoja wa Mataufana wa Muungano wa Afrika (AU). Ikiwa mashaurino ya kidiplomasia yataendelea kushindikana. Litalobaki litakuwa ni kurudi kule kule tulikoanzia makala haya: matumizi ya nguvu.

Endapo Ecowas itajaribu kuchukua hatua hiyo basi ukanda mzima wa Sahara/Sahel utakwenda arijojo. Kutatokea nakama kubwa tusiyoweza kuitabiri kwa sasa na itayozikumba nchi kadhaa za Afrika Magharibi pamoja na za Afrika ya Kaskazini.

Wataofaidika ni wapiganaji wa itikadi kali za Kiislamu wenye kusema wanapigana vita vya jihadi. Hawa ni wa makundi ya Al Qaeda, Da‘esh (Dola la Kiislamu) na makundi mengine madogo madogo, yakiwa pia ya majambazi na maharamia.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X: @ahmedrajab

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.

Gazeti la Dunia ni Jukwaa Huru la Fikra kwa wasomaji wa lugha ya Kiswahili lenye lengo la kuchapa makala za kichambuzi kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa Tanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. Waandishi wa kwenye jukwaa hili ni maveterani na wabobezi kwenye maeneo watakayokuwa wanaandikia. Kama unajua unachokiandika, hili ni jukwaa lako.

2022 Gazeti La Dunia

Screenshot_20230809-230732_Chrome.jpg
 
Ukiona nguvu za kijeshi zinaanza ndani ya nchi ujue muda muwafaka keki ya taifa inakwenda kuwa na michanga.

Ili linasababishwa na utawala uliochokwa ccm inalakujifunza lakini ni kama wamejiweka pamba masikioni.
 
Back
Top Bottom