Stories of Change - 2022 Competition

lucy mwimbilizye

New Member
Aug 30, 2016
1
0
Ndoa ndoano ni msemo wa muda mrefu sana ukimaanisha kuwa wawili waingiapo kwenye ndoa hawawezi kuachana na wanapaswa kuvumiliana katika hali zote za shida na raha.Ni kama wavuvi wanavyovua Samaki na ndoano. Samaki akinasa kwenye ndoano basi hawezi kuchomoka.Dini zetu pia zinatuongoza kuwa wawili waingiapo kwenye ndoa basi kifo tuh ndio kitawatenganisha. Ndoa ni baraka kutoka kwa mwenyezi MUNGU na ndio maana hata vyombo vya dini,mila na desturi zetu ,Pamoja na serikali inatambua mchakato mzima wa ndoa.Ndoa ni makubaliano ya watu wawili kuwa Pamoja na kuanzisha familia kwa UPENDO,Msingi mkubwa unaoshikilia ndoa ni upendo. Watu wawili wakipendana kwa makubaliano yao wanaweza kuungana na kuwa kitu kimoja kwa njia ya Ndoa.

Upendo unapokosekana baina ya wanandoa huwa ni tatizo kubwa sana,kwani kinachowaunganisha watu hao wawili ni upendo na mengine hufwata. Mimi ninaimani kuwa ukimpenda mtu kwa dhati huwezi ukamdhuru kwa namna yoyote bali utatamani kumlinda na kuhakikisha anafuraha muda wote.Nakubali kuwa watu wawili wanaweza kuwa na tabia tofauti kwa sababu kila mtu amekua kwenye mazingira yake,hivyo hekima na busara ya hali ya juu inatakiwa ili kuweza kuishi Pamoja kwa maelewano mazuri.

Malezi ya Watoto wakike wengi yanatuaminisha kuwa ndoa ni kitu cha thamani sana kwa mwanamke na pale unapofanikiwa kuiipata basi ni lazima kuitunza kwa namna yoyote. Nimewahi kusikia kauli kuwa AMESOMA LAKINI HANA BAHATI YA NDOA, ANAKAZI NZURI LAKINI HAJAOLEWA, amefanya nini sijui lakini hana bahati ya ndoa.Lazima mafanikio yatalinganishwa na ndoa mwishoni,Wazazi wengi huwaambia Watoto wao wa kike pale wanapoolewa kuwa wajitahidi kuvumilia kwa gharama yoyote kuachika ni aibu kubwa kwa wazazi na kwake pia. Mara nyingi ndoa zinapoisha au wanapoachana wanandoa wawili vidole hunyooshewa mwanamke,kuwa ameshindwa kabisa kutunza ndoa yake na ameachika bila hata kujua sababu kubwa ya kuachana watu hao wawili ni nini na jamii inasahau kuwa Ndoa ni makubaliano na kuachana pia ni makubaliano.

Tumesikia hadithi nyingi sana kutoka kwa watu maarafu ambao wamejitokeza wakisema kuwa ndoa zao hazikuwa na furaha na kati ya hao wengi ni wanawake wamejitokeza na kukiri kuwa wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili katika ndoa zao kama vile kupigwa na wengine hadi kupelekea umauti.Haya ni maelezo tunayoyajua kutoka kwa watu maarufu kwa kuwa wamejitokeza na kukiri unyanyasaji wanaopata katika ndoa zao.Wapo wanawake wengi ambao wanapitia changamoto kama hizi na wanashindwa kuongelea au kutoka katika unyayasaji huo kwa kuwa NDOA NDOANO.

Hadi lini tutakariri kuwa ndoai ndoano, Pamoja na kusikia Habari za wanawake wanaopigwa na kunyanyaswa na kuuliwa kwenye ndoa zao?Tumezungukwa na jamii ambayo mwanamke akiacha ndoa yake anaongelewa vibaya na kuonekana ameshindwa kabisa Maisha. Wanawake wengi huogopa kukimbia ndoa za manyanyaso wakiogopa Zaidi mitazamo ya jamii na kuogopa kupoteza kitu pekee cha thamani kwenye Maisha yao kama ambavyo wazazi husema.

Ushauri wangu kwa wazazi wa sasa,tunapaswa kulea Watoto katika njia iliyo bora Zaidi cha kwanza ni kupandikiza Watoto wetu na HOFU YA MUNGU,mtu mwenye hofu ya MUNGU kamwe hawezi kufikiria kumdhuru binadamu mwenzake.Wazazi wanatakiwa kuwa mifano bora kwa Watoto , wajifunze wakiona hakuna mapigano kati ya wazazi.Jambo muhimu ni kuwafundisha Watoto wa kiume namna ya kuheshimu wanawake toka wakiwa wadogo na pia kuwafundisha Watoto wetu wa kike kuwa ndoa ni kitu muhimu lakini sio kitu muhimu kuliko chochote duniani.

Wanaume wenye tabia ya kupiga na kudharirisha wanawake ndani ya ndoa au mahusiano huo ni USHAMBA na sio ujanja.Ndoa ni makubaliano na sio kummiliki mtu kwa kumfanya chochote unachotaka,Unaona umekosewa tumia Zaidi mdomo kuelezana kwa hekima na sio ngumi wala silaha.Mara nyingi wanasema tenda yale unayopenda utendewe,hakuna mtu anapenda kupigwa au kuumizwa na kudhalilishwa.Ikishindikana kabisa kutatua chagamoto kwa maongezi basi haina budi kila mtu Kwenda kwa njia zake kuliko kutumia nguvu na kuumizana.

GBV.PNG

picha kutoka Cartoon: 16 days of activism to fight gender-based violence: Let’s defend the vulnerable and fight impunity | This is Africa

Wanawake NDOA SI NDOANO,utavumilia vipigo hadi lini?Utavumilia udhalilishaji hadi lini?Inuka na ufanye maamuzi sahihi kabla hujapoteza Maisha yako.Wewe sio ngoma ya mtu kuipiga pale anapotaka,unapaswa kuishi kwa furaha kama wanawake wengine.Tafuta chanzo chako cha kipato ili uweze kutatua changamoto zako kuliko kumtegemea mwanaume kila kitu,ataona anakumilika na hata akikupiga ataona ni sawa kwake. Wengi tunaishia kusema ATABADILIKA TU,Hadi lini atabadilika?Nafikiri ni pale ambapo atakapokatisha uhai wako ndipo atakapobadilika.Vyombo vya sheria ni rafiki sana kwetu na madawati ya kijinsia yapo kwa ajili ya kutatua changamoto.

Leo ninaandika kwa ujasiri bila uwoga kuwa NDOA SIO NDOANO huu msemo wa ndoa ndoana ulitungwa na mtu na haimaanishi kuwa ni sahihi endapo ndoa itakosa UPENDO na kugeuka Zaidi sehemu ya unyanyasaji na matendo ya ukatili.Mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika kuwadhihaki wanawake walioacha ndoa zao na kuwapa picha mbaya sana kama WANAWAKE WALIOACHIKA.

Leo ninatumia mtandao huu wa kijamii kuwapongeza wanawake wote waliokimbia ukatili kwenye ndoa zao,watambue kuwa wao ni mfano wa kuigwa kwa wanawake wengi ambao wanashindwa kutoka kwneye hiyo changamoto.Sipingani na vyombo vya kidini ila napingana na vitendo vya ukatili vinavoendelea chini ya mwamvuli wa NDOA NDOANO.

Nina imani hakuna dini inayachochea unyayasaji na ukatili wa aina yoyote,hivyo swala hili linapaswa kupewa kipaumbele hata na viongozi wa dini zetu. Tutambue kuwa linapofika suala la usalama na amani yako haina budi kufanya maamuzi magumu yatakayobadilisha Maisha yako na kukupa furaha Zaidi.
 
Back
Top Bottom