Mwanaume Maisha ni Mapambano, chagua moja kati ya haya

Infinite_Kiumeni

JF-Expert Member
Jan 23, 2023
382
661
Kupambana sio kutafuta hela tu. Kupambana ni kitendo cha kuwa bora na mwenye thamani zaidi kila siku. Tangu umezaliwa hauna thamani kulinganisha na mtoto wa kike. Usikae kulalamika kuhusu hilo.

Ni juu yako kupambana na kukuza thamani yako. Na utaheshimiwa zaidi kadri unavyozidi kupanda juu kithamani. Japo ni muhimu kuitunza thamani lakini inabidi ukuze thamani yako kila siku. Kwa mwanamke yeye ataangaliwa jinsi alivyoitunza thamani yake. Hasa ile aliyozaliwa nayo.

Mwanaume inabidi upambanie kwa kile unachohitaji. Hakuna mtu anakuja kukusaidia kubeba mzigo wako. Na ukiwa mzigo hakuna akuthaminiye. Unaweza kuwa na hela lakini ukawa mzigo. Matendo yako ndio yanaamua uwe mzigo au wa thamani. Una chaguo moja kati ya haya kila siku unapoamka.

Ukiamka ufikirie na uamue kubweteka.
Utumie muda wako kulaumu wengine.
Kuona huwezi, yaani kuchagua kufeli kwa hiari yako.

Kutukana usiowajua na unaowajua. Uwe mlalamishi na maisha yako yawe vile vile kila siku. Huku ukitegemea ipo siku yatabadilika wakati unarudia matendo yale yale yaliyokufanya uwe katika sehemu uliyopo.

Hauna raha sehemu fulani ya maisha. Lakini badala ya kuipambania furaha, unataka kila mtu awe kama wewe bila furaha.

Hata mwanamke utakayekua naye hatakua wa kukufanya uzidi kupambana, bali naye atakua wa kushusha thamani. Hakuongezei uthamani wowote maishani.

Zaidi ya kwamba anachukua thamani tu toka kwako. Utaishia kusema wanawake wote ni hivyo, lakini ukweli ni kwamba we mwenyewe ndo upo hivyo.
Au.

Ukiamka ufikirie na uamue kupambana.
Kupambana sio kuamka na kwenda kwenye shughuli tu.

Bali ni kupambana na yule wewe wa jana na kuandaa mazingira bora kwa ajili ya wewe wa kesho kuwa bora zaidi katika kila eneo la maisha yako.

Utumie muda wako kusoma vitabu vizuri (ikiwemo vya dini) na kuvifanyia kazi. Kujifunza kwa walio kuzidi kwa lolote badala ya kuwachukia na kujaribu kuwashusha thamani kwa kuwaongelea vibaya.

Kukubaliana na vitu usivyoweza kuvibadili na kubadili unavyoweza. Kubadilika ni ngumu, na inaumiza. Lakini matunda yake siku zote ni matamu kuliko maumivu utakayopitia.

Usijifunge funge kwenye imani ambazo unaona hazikusaidii. Badilika.

Kupata nyumba nzuri, gari zuri, mke mzuri ni kupambana. Na kuna mtu tayari anacho unachokitaka jifunze toka kwake pia.

Usichoke kupambana, hata ukikatishwa tamaa. Wakatisha tamaa wapo kwa ajili ya kukupa motisha zaidi. Wapo kwa ajili ya kukuonesha upande ambao hutaki kuwa. Wapo kwa ajili ya kukukumbusha kwanini hutaki kuwa kama wao. Wao hawaoni wanakukatisha tamaa, wanaona wanafanya kitu sahihi. Wanaona unawaacha katika maisha, hivyo wanataka urudi nyuma ili muwe sawa. Ni nguvu kuwaelewesha, ila achana nao.

Kumbuka.
Mwenye muda wa kubweteka hana muda wa kupambana. Mwenye muda wa kupambana hana muda wa kubweteka.

Mwenye nguvu za kubweteka hana nguvu za kupambana. Mwenye nguvu za kupambana hana nguvu za kubweteka.

Chagua uwe upande upi na ufanyie kazi. Maamuzi ni juu yako utumiaje muda wako na nguvu zako.
 
Back
Top Bottom