Tuache siasa, bandarini tunaua uchumi
Mwandishi wetu
WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe sasa ametangaza kupokea ripoti ya tume aliyoiunda kuchunguza tuhuma ambazo zimekuwa zikidaiwa kuwa chanzo cha kuzorota kwa huduma za bandari zetu na hasa Bandari ya Dar es Salaam.
Tuhuma za Dk. Mwakyembe wakati akiunda tume yake na hata sasa, zinaelekezwa tu kwa uongozi wa Mamlaka ya Bandari Tanzani (TPA) na zaidi viongozi maalumu anaowalenga yeye tu na mfumo mzima katika sekta husika.
Kwa kuwa waziri hana taaluma katika maswala ya usafiri kwa njia ya majini bandari nikiwa kama mmoja wa wadau kwenye sekta hiyo naamini sasa atakuwa amepata ufahamu wa kuifahamu vema sekta nzima ikiwa ni pamoja na mfumo mzima wa kupokea, kuhifadhi na kusafirisha mizigo ipitayo kwenye bandari zetu zikiwamo zile za maziwa.
Kwa wadau waliobobea kwenye eneo hili na ambao biashara zao za kila siku hutegemea ufanisi endelevu wa kila mdau kwenye eneo hili wanategemea kuona ripoti yenye weledi na muonekano wa kitaaluma kuliko ya kutafuta makosa ndani ya mdau mmoja.
Kwa maelezo ya Dk. Mwakyembe na wanaoungana naye, kwa sasa inaonekana tuhuma zinaelekezwa TPA ili kuhalalisha mbele ya umma kwamba Bandari ya Dar es Salaam kuna uozo, wizi, rushwa na kila aina ya uovu unaofahamika duniani.
Baadhi ya wadau wanaona matamshi kama haya na ambayo hayajahusisha wadau wote kwa kina yanatoa taswira ambayo inaweza kuwapoteza wateja kabisa hata wateja wachache tulionao Tanzania.
Waziri anadiriki kusema eti amehakikishiwa na mawaziri wenzake wa uchukuzi wa nchi jirani kwamba nchi hizo zitaendelea kuzitumia bandari zetu hasa ya Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau na wafanyabiashara wanasema kwamba mawaziri siyo wanaofanya biashara ila kazi yao ni kuweka na kusimamia sera ya biashara husika.
Tunafahau na waziri lazima afahamu kwamba bandari haiwezi kufanya kazi zake bila kuhusisha kwa umakini sekta nyinginezo na mfanyabiashara mmoja anayemiliki meli kubwa duniani ameliambia gazeti hili wazi kwa kusema, "Bandari haiwezi kufanya kazi kivyakevyake kama kitu kilichojitenga bila vifaa, watu au taasisi na mitandao inayopaswa kufanya nayo kazi!"
Hali kadhalika bandari haiwezi kufanya kazi ikawa na ufanisi bila kuwa na viunganishi thabiti kwa maana ya barabara, reli na mabomba ya mafuta.
Pia bandari haiwezi kuwa na ufanisi wa kupokea mizigo mingi kwa wakati mmoja kama haina miondombinu ya kutosha na ya kisasa kama gati za kutosha na zenye kina kinachoweza kuegesha meli kubwakubwa ambazo zinaweza kutia nanga hapa kama zilivyo kwenye bandari zinazoshindana na Bandari ya Dar es Salaam.
Ikumbukwe baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 wa Kenya kugubikwa na vurugu, wafanyabiashara wa Uganda walipata shida kutokana na mizigo yao kukwama kwenye Bandari ya Mombasa kwa zaidi ya miezi mitatu mpaka hali ilipotengemaa.
Ni wakati huo ujumbe mzito ulikuja kutoka Uganda ukiongozwa na Waziri wa Uchukuzi, kuja kuona uwezekano wa kutumia Bandari ya Dar es Salaam na kuahidi kwamba Uganda ingetumia kupitisha asilimia 30 ya mizigo yake hapa kama mbadala wa Bandari ya Mombasa.
TPA ilibidi iweke wakala kule Uganda kama njia ya kuwavutia Waganda lakini wafanyabiashara wamekuwa wanasita kutokana na ukweli kwamba miundombinu yetu bado ni hafifu.
Kukosekana kwa reli kumefanya Waganda waghairi kutokana na gharama kubwa kwa njia ya barabara wakilinganisha na umbali wa kutoka Mombasa mpaka Kampala.
Hoja hapa ni kwamba pamoja na kuhakikishiwa na Waziri wa Uchukuzi wa Uganda wa kutoa ahadi ya asilimia 30 ya mizigo ya Uganda kupitia hapa imekuwa ni kitendawili kutokana na changamoto za mapungufu katika mtandao wetu wa njia za usafirishaji mpaka mzigo ufike Uganda au utoke Uganda mpaka bandarini Dar es Salaam.
Kama wadau, tunaona changamoto za uendeshaji bandari ziangaliwe kitaaluma zaidi kuliko kuchukua mrengo wa kisiasa.
Inashangaza kuona inachukua zaidi ya miaka mitano kuamua namna ya kuongeza gati mbili kwa nia ya kuongeza ufanisi kwenye sekta nzima kwa njia ya bahari ambayo faida yake yake ni kuongeza pato la taifa kwa kuwa kila mdau kwenye biashara inayohusiana na Bandari ya Dar es Salaam atakuwa anachangia kwa kiasi kikubwa kwenye GDP!
Mombasa wanaongeza gati nne kwenye katika bandari yao na mkandarasi yuko kazini mwaka wa pili sasa.
Pia wanajenga bandari mpya ya Lamu ambayo pia mkandarasi yuko kazini; hapa tunalumbana wakati wenzetu wanashangilia kwa ujinga wetu.
Waziri anahusisha vipi TPA peke yake na wizi wa makontena?! Mizigo hutolewa bandarini kwa njia ya nyaraka ambazo zina mlolongo mrefu.
Je, kama nyaraka za mzigo husika zimeghushiwa wakati mzigo unapotolewa bandarini au toka kwenye eneo linalomilikiwa TICTS, bandari au mkaguzi mkuu wa bandari atajuaje?
Tumeona kwenye vyombo vya habari kwamba kuna makontena yameshikwa huko Hongkong yakiwa na pembe za ndovu zikitokea Dar na Mombasa.
Je, hapa TPA inahusika vipi wakati anayetakiwa kufungua na kukagua makontena kabla hayajapelekwa kwenye meli kupakiwa ni ofisa forodha?
Ni vema wanasiasa wakajifunza kwanza jinsi bandari inavyofanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ndani ya mfumo kabla ya kufanya maamuzi ambayo kwa kiasi kikubwa yatakuwa hayajengi zaidi ni kuuvuruga mfumo wote wa usafirishaji kwa njia ya majini na kuua uchumi wetu kwa maslahi ya kisiasa.
Source: www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=41830
Hili Gazeti huwa kwa kila siku linanichukulia Hela Yangu ila kwa hii story, Naona kuna Msukumo Wa kisirisiri wa kifisadi!! Mwandishi wamekununua kwa TZS Ngapi?