Muhtasari: Hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha Mwaka 2023/24

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

MUHTASARI WA HOTUBA YA WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA PROF. ADOLF F. MKENDA (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2023/24

DODOMA MEI, 2023

A. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
kufuatia taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo iliyochambua makadirio ya mapato na matumizi ya FUNGU 46 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na FUNGU 18 - Tume ya Taifa ya UNESCO, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako Tukufu, likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 kwa mwaka wa fedha 2022/23. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Tume ya Taifa ya UNESCO kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake thabiti na kutimiza miaka miwili tangu ashike nafasi ya kuongoza nchi yetu. Katika kipindi hicho ametuongoza vyema na kutuwezesha kupata maendeleo na mafanikio makubwa kutokana na miongozo anayotupatia ambayo imetusaidia sana katika kusimamia na kuendeleza Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Aidha, namshukuru kwa kuniamini mimi pamoja na Mheshimiwa Omary Juma Kipanga (Mb) Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuendelea kuongoza Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri katika kuliongoza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb), Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Spika Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) kwa uongozi wenu mahiri wa kuliongoza Bunge letu tukufu. Aidha, natumia nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa jimbo la Babati Vijijini, na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini, kwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa Bunge letu Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, napenda nimshukuru kwa namna ya pekee Mheshimiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko (Mb), Makamu Mwenyekiti na wajumbe wote wa Kamati. Aidha, naomba niwashukuru kwa kupokea, kuchambua na kupitisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2022/23 na kuishauri vema Wizara kuhusu Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2023/24. Natambua na kuthamini sana mchango wa Kamati katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Elimu inachangia katika utekelezaji wa Mpango wa III wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 kwa kuandaa rasilimaliwatu yenye ujuzi, maarifa na stadi zitakowezesha kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kuishukuru familia yangu hasa mke wangu Beatrice kwa kuendelea kuwa karibu yangu na kunitia moyo na kuniwezesha kufanya kazi kwa juhudi na ari kubwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi, naomba sasa nitoe taarifa ya utelekezaji wa majukumu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia FUNGU 46 na FUNGU 18 kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, na Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

B. UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2022/23

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Bunge lako Tukufu liliidhinisha kiasi cha Shilingi 1,555,827,466,796.00 kwa ajili ya FUNGU namba 46 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo Shilingi 533,456,916,000.00 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 1,022,370,550,796.00 zilikuwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Aidha, kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO - FUNGU 18 Wizara iliidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,709,163,000.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambayo yanajumuisha Shilingi 1,176,870,000.00 za mishahara na Shilingi 1,532,293,000.00 za matumizi mengineyo.​

Ukusanyaji wa Maduhuli

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara kupitia FUNGU 46 ilitarajia kukusanya maduhuli yenye thamani ya Shilingi 642,667,620,483.06 ambapo kiasi cha Shilingi 8,680,995,000.00 kilipangwa kukusanywa na idara na vitengo na Shilingi 633,986,625,483.06 zilipangwa kukusanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara. Vyanzo vya maduhuli hayo ni kutokana na ada, malipo ya ushauri elekezi, huduma za Uthibiti Ubora wa Shule na utoaji wa huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2023 Wizara imekusanya Shilingi 400,139,396,734.49 sawa na asilimia 62 ya makadirio ambapo Shilingi 8,116,780,685.14 zimekusanywa na idara na vitengo na Shilingi 392,022,616,049.35 zimekusanywa na taasisi zilizo chini ya Wizara.

Matumizi ya Kawaida

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha 2022/23, Wizara pamoja na taasisi zake iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 533,456,916,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo, Matumizi ya mishahara ni Shilingi 500,196,732,000.00 (idara na vitengo Shilingi 80,090,663,000.00 na Taasisi ni Shilingi 420,106,069,000.00) na Matumizi Mengineyo Shilingi 33,260,184,000.00 (idara na vitengo Shilingi 25,558,821,658.00 na Taasisi Shilingi 7,701,362,342.00).

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2023, Wizara imepokea Jumla ya Shilingi 410,266,920,334.60 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, kupitia Fungu 46, ambazo ni sawa na asilimia 76.91 ya fedha za Matumizi ya Kawaida zilizoidhinishwa. Aidha, kupitia Tume ya UNESCO – Fungu 18 Wizara imepokea jumla ya Shilingi 1,979,133,163.28 sawa na asilimia 73 ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Miradi ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/23, Wizara pamoja na taasisi zake iliidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,022,370,550,796.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo fedha za ndani ni Shilingi 840,906,789,796.00 na fedha za nje ni Shilingi 181,463,761,000.00.

Mheshimiwa Spika
, kwa upande wa miradi ya maendeleo hadi kufikia Aprili 2023, Wizara imepokea jumla ya Shilingi 1,063,782,313,215.36 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo sawa na asilimia 104.05 ya bajeti iliyotengwa. Kati ya Fedha hizo Shilingi 880,846,253,860.91 ni fedha za ndani na Shilingi 182,936,059,354.45 ni fedha za nje.

Mheshimiwa Spika, ongezeko la kiasi cha fedha za ndani kilichopokelewa kinajumuisha: kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ununuzi wa vishikwambi vya walimu, wakufunzi wa vyuo vya ualimu, na wathibiti ubora wa shule; na Fedha kwa ajili ya Bodi ya Mkopo kilichoongezewa ili kukidhi mahitaji ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Aidha, ongezeko la kiasi cha fedha za nje kilichopokelewa kinajumuisha fedha zilizopatikana kutokana na matokeo ya kutekeleza kwa ufanisi kwa viashiria vya miradi ya lipa kulingana na matokeo (Program for Results).

C. TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA

Mheshimiwa Spika, pamoja na mapitio ya sera na mapitio ya mitaala, Mpango na Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2022/23, ulijielekeza katika kutekeleza maeneo ya kimkakati ikiwa ni pamoja na: (i) kuongeza fursa na kuimarisha elimu ya ufundi nchini; (ii) kuhimiza uandishi, uchapishaji na uchapaji wa vitabu hapa nchini; (iii) kuongeza wigo wa shule za ufundi; na (iv) kuimarisha ujifunzaji kwa vitendo katika taasisi za Elimu ya Juu kwa kuanza kujenga kampasi za vyuo zenye kujielekeza katika mafunzo kwa vitendo katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa maeneo hayo ya kimkakati ulieenda sambamba na utekelezaji wa vipaumbele vifuatavyo:

i. Kuhuisha Sera, Mitaala, Sheria na Miongozo ya Utoaji wa Elimu na Mafunzo Nchini

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, Ualimu, Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Juu kwa lengo la kuleta mageuzi ya elimu nchini na kuwapatia wahitimu ujuzi na maarifa stahiki.

Mheshimiwa Spika, uhuishaji wa Sera unahusisha mabadiliko katika mfumo wa elimu ili kuwawezesha wahitimu kujiamini, kujiajiri na kuajirika katika mazingira ya utandawazi na kukidhi mahitaji ya soko. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 ili kubaini utoshelevu wa sera hiyo na kuandaa taarifa ya mapitio ambayo imewezesha maandalizi ya Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 - Toleo la mwaka 2023 ambalo limejielekeza katika utoaji wa elimu ya amali (Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi) katika ngazi zote za elimu na mafunzo. Vilevile, imefanya mapitio ya mitaala ili kubaini utoshelevu wake na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya mitaala kulingana na maelekezo ya sera.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo Toleo la Mwaka 2023 na Mitaala ya Elimu inapata maoni ya wadau wengi kabla ya uidhinishwaji wake, Wizara imeendesha Kongamano la Kitaifa lililofanyika kuanzia tarehe 12 hadi 14 Mwezi Mei, 2023 Mkoa wa Dodoma. Katika Kongamano hilo, zaidi wa Wadau wa Elimu 1,450 walishiriki (walioshiriki moja kwa moja ukumbini 1,200 na walioshiriki kwa njia ya mtandao 250) wakiwemo wanafunzi, walimu, wahadhiri, wakufunzi, wazazi, wadau wa maendeleo na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini, siasa na kijamii. Vilevile, Wizara inaendelea kupokea maoni hadi tarehe 31 Mei, 2023. Aidha, mwezi Juni, 2023 Wizara itaanza utaratibu za kuomba idhini ili kuwezesha utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Elimu ya Awali, Msingi na Elimu ya Ualimu inatolewa kwa kuzingatia viwango na ubora stahiki, Serikali imeandaa miongozo kama ifuatavyo:​
  • Mwongozo wa Kitaifa wa Uendeshaji na Viwango katika Elimu ya Awali Tanzania Bara kwa lengo la kuimarisha utoaji wa elimu ya awali kwa kuzingatia viwango vya ubora pamoja na kiongozi cha kutekeleza mwongozo husika;​
  • Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji, Usimamizi na Uendeshaji wa Vituo Shikizi vya Shule ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika vituo shikizi nchini; na​
  • Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Utekelezaji wa Shughuli za Ushirikiano wa Wazazi na Walimu katika Elimu ya Awali na Msingi Tanzania Bara kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya wazazi na walimu katika kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi​

ii. Kuongeza Fursa za Elimu kwa Wote

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kuanza shule wanaandikishwa wakiwemo watoto wenye mahitaji maalum. Aidha, inaendelea kuhakikisha kuwa wanafunzi waliopata fursa za masomo wanashiriki kikamilifu katika masomo na kuhitimu. Azma hiyo, imefikiwa kwa kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo:​
  • Usajili wa jumla ya asasi 683 zilizokidhi vigezo kati ya 684 zilizoomba kwa mchanganuo ufuatao: shule za Awali pekee 26 zisizo za Serikali, shule za Awali na Msingi 309 (Serikali 150 na zisizo za Serikali 159) na Sekondari 346 (Serikali 209 na zisizo za Serikali 137) na Vyuo vya Ualimu viwili visivyo vya Serikali ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini;​
  • Imesajili jumla ya wanafunzi 22,802 (Wanawake 11,641 na Wanaume 11,161) katika Vyuo vya Ualimu vya Serikali na visivyo vya Serikali ambapo Astashahada ya Elimu ya Msingi ni 15,177 (Wanawake 8,406 na Wanaume 6,771), Stashahada ya Ualimu 2,787 (Wanawake 1,076 na Wanaume 1,711) na Stashahada maalum ya ualimu wa sayansi sekondari wa miaka mitatu 4,838 (Wanawake 2,159 na Wanaume 2,679); na​
  • Imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu uandikishwaji na umuhimu wa Elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kupitia vyombo ya habari, mitandao ya kijamii na maadhimisho ya Siku ya walemavu duniani, Wiki la Elimu Jumuishi, Siku ya Fimbo nyeupe kwa wasioona, Siku ya Braille duniani, na Siku ya watoto wenye Downsyndrome na Rare Disease.

Mheshimiwa Spika, katika kutoa fursa kwa wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali, Serikali imewezesha kuwarejesha wanafunzi 1,967 (Wanawake 1,046 na Wanaume 86) katika Mfumo Rasmi wa Elimu. Vilevile, imedahili jumla ya wanafunzi 23,263 (Wanawake 15,006 na Wanaume 8,257) katika mikoa 26 ambao wanapata Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (Alternative Education Pathway).

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari. Katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mamlaka ya Elimu Tanzania imetekeleza yafuatayo:​
  • Imewezesha ujenzi wa shule mpya za msingi 40; madarasa 174 katika shule za msingi 70; mabweni manne katika shule za msingi tatu; nyumba za walimu 53 katika shule za msingi 53; mabweni manne katika shule za msingi nne; matundu ya vyoo 6,634 katika shule za msingi 472 na ofisi moja. Aidha, imewezesha ukarabati wa shule kongwe 45 za msingi; na​
  • Imewezesha ukamilishaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari 231 za Kidato cha 1 hadi cha 4 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa kila shule, shule 10 za Kidato cha 5 na 6 kwa wanafunzi wa kike kati ya shule 26 zinazotarajiwa kujengwa kwa kila Mkoa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kila shule. Aidha, imewezesha ujenzi wa madarasa 46 katika shule za sekondari 46; mabweni 72 katika shule za sekondari 54 nyumba za walimu 19 katika shule za sekondari 18; maabara 26 katika shule za sekondari 14, maktaba nne, mabwalo 22, ofisi sita. Vilevile, imewezesha upanuzi wa shule kongwe 18 na ukarabati wa shule kongwe 16 za sekondari.​
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu tarajali kwa kuboresha miundombinu katika Vyuo vya Ualimu nchini kwa kutekeleza yafuatayo:​
  • Imeendelea na ujenzi wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Mhonda na Dakawa ambapo ujenzi upo katika hatua za ukamilishaji. Vilevile, imeendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Vyuo vya Ualimu vitano ambavyo ni; Mamire, Vikindu, Songea, Singachini na Katoke. Ujenzi na ukarabati huo upo katika hatua za ukamilishaji. Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaimarisha mazingira ya utoaji wa elimu ya ualimu na kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Ualimu; na​
  • Imekamilisha ukarabati wa Chuo cha Ualimu Butimba na kuendelea na ukarabati wa maabara za Sayansi na TEHAMA katika vyuo sita vya ualimu ambavyo ni; Chuo cha Ualimu Morogoro, Mpwapwa, Tukuyu, Kasulu, Patandi na Dakawa. Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.​

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, Serikali imenunua na kusambaza vitimwendo 253 kwa wanafunzi wa shule za msingi 200 na sekondari 53 wenye mahitaji maalum kwa lengo la kuwawezesha kumudu mazingira ya shule na nyumbani.

iii. Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ubora wa elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu kwa kufanya tathmini ya jumla katika asasi 6,317 (Awali na Msingi 5,351, Sekondari 932 na Vyuo vya Ualimu 34) ambapo shule zilipewa ushauri wa kitaalam na kitaaluma kwa ajili ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji. Vilevile, imekamilisha ujenzi wa ofisi tano za Uthibiti Ubora wa Shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Ubungo, Njombe, Bunda na Tarime kwa lengo la kuimarisha mazingira ya utendaji kazi.

Mheshimiwa Spika, katika kujenga umahiri wa walimu na wakufunzi katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuimarisha usimamizi wa shule na vyuo vya ualimu, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imeandaa moduli 12 za Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA) wa Elimu ya Awali na Msingi na imetoa mafunzo kwa walimu 26,657 wanaofundisha elimu ya awali na msingi kupitia vituo vya walimu na shule teule;​
  • Imetoa mafunzo kuhusu Elimu ya Stadi za Maisha zinazolenga afya ya uzazi, VVU na UKIMWI na Jinsia kwa walimu 25,700 kati ya walimu 27,750 wa shule za msingi na sekondari waliolengwa ili kuwajengea uwezo wa kufundisha masuala mtambuka. Vilevile, imetoa mafunzo kuhusu darasa jumuishi kwa walimu 17,800 kati ya walimu 20,000 waliolengwa wanaofundisha Darasa la I – IV. Mafunzo yalilenga kuimarisha utekelezaji wa mitaala; na​
  • Imetoa mafunzo kuhusu mbinu bora ya ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa vitendo kwa walimu wa sekondari 15,282 (Wanawake 3,985 na Wanaume 11,297) kati ya walimu 20,000 waliolengwa. Aidha, mafunzo kwa walimu 4,718 waliobaki yanaendelea kutolewa.​

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha ufundishaji wa masomo ya Amali (Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi stadi) kwa elimu ya msingi na sekondari kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa Sera na Mtaala Mpya, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imeanza maandalizi ya Elimu ya Ualimu wa Ufundi kwa kubainisha vifaa na mashine zinazohitajika katika mafunzo hayo; na​
  • Imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mtaala wa Elimu ya Ualimu wa Ufundi na kubainisha Vyuo vya Ualimu 10 ambavyo vitatekeleza mtaala huo. Vyuo hivyo ni; Kitangali, Ndala, Nachingwea, Kleruu, Mtwara (U), Mpwapwa, Korogwe, Dakawa, Bunda na Kabanga.​

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha upatikanaji wa vitabu kwa mwanafunzi katika elimu ya awali, msingi na sekondari ili kuimarisha uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imeendelea na uchapaji wa vitabu 2,000,000 vya masomo ya Sayansi na Hisabati kwa ajili ya kusambaza katika Halmashauri zenye upungufu mkubwa;​
  • Imechapa na kusambaza nakala 12,307,578 za vitabu kwa mchanganuo ufuatao: nakala 2,535,564 za vitabu vya hadithi vya Elimu ya Awali; nakala 3,885,000 za Vitabu vya Hadithi vya Darasa la I - II; nakala 4,181,226 za vitabu vya Kiada Darasa I na II; nakala 1,687,140 za Vitabu vya Kiada vya Darasa la III, IV na V; nakala 17,104 za Vitabu vya Maandishi yaliyokuzwa Darasa la III, IV na V kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu; nakala 640 za Vitabu vya kiada vya maandishi ya breli kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali wasioona; na nakala 904 za maandishi yaliyokuzwa kwa wenye uoni hafifu; na​
  • Imechapa na kusambaza nakala 525,000 za vitabu vya kiada vya masomo ya Mathematics, Agriculture, English Baseline Orientation course, Biology, Chemistry, Book keeping, Civics, English, Food and Human Nutrition, French, Geography, History, Information and Computer Studies, Kiswahili, Economics, Music, Physics, Textiles and Theatre Arts kwa kidato cha 1 – 6.​

Mheshimiwa Spika, vitabu vyote vilivyochapwa na kusambazwa vinapatikana katika Maktaba Mtandao ambapo wanafunzi na walimu wanaweza kuvipata bila gharama yoyote ya kuunganishwa kwa mtandao (Zero - Rating) na hivyo kurahisisha upatikanaji wake.

Mheshimiwa Spika, imesimamia utoaji wa Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi bunifu ambapo Mgeni Rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Rais Mstaafu wa Msumbiji, Mhe. Joaquim A. Chissano. Tuzo hiyo imehusisha mashindano ya uandishi wa riwaya na mashairi ambapo jumla ya miswada 283 (Riwaya 85, Ushairi 193 na nje ya nyanja za kushindaniwa 5) ilipokelewa.

Mheshimiwa Spika, katika Tuzo hiyo, mshindi wa kwanza kwa kila nyanja alizawadiwa fedha taslimu Shilingi 10,000,000.00, ngao, cheti pamoja na vitabu vyao kuchapwa na kusambazwa kwa gharama ya Serikali. Mshindi wa pili alizawadiwa Shilingi 7,000,000.00 na cheti na mshindi wa tatu Shilingi 5,000,000.00 na cheti kwa kila nyanja. Vilevile, tuzo hiyo itasaidia kuongeza idadi ya vitabu vilivyoandikwa na Watanzania badala ya kutegemea vitabu vinavyotoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, katika kukuza ujuzi wa uandishi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini pamoja na kutambua, kuibua, kukuza vipaji vya uandishi na kuongeza ari ya usomaji nchini, Serikali imeratibu mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi 1,116 wa shule za sekondari ambapo washindi watano walipatikana kwa ajili ya kushiriki katika mashindano ngazi ya Kikanda.

Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kutoa huduma ya maktaba nchini kwa ajili ya kupata maarifa na taarifa mbalimbali, Serikali kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania imesambaza nakala za vitabu 21,200 katika maktaba za mikoa 20.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la upimaji na tathmini ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania imetekeleza yafuatayo:​
  • Imeendesha Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) kwa mwaka 2022 kwa wanafunzi 1,592,600 ambao ni sawa na asilimia 92.65 ya wanafunzi 1,718,896 waliosajiliwa kufanya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne. Katika mtihani huo wanafunzi 1,320,700 sawa na asilimia 82.95 walifaulu;​
  • Imeendesha Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) wa mwaka 2022 kwa watahiniwa 1,350,881 ambao ni sawa na asilimia 97.59 ya watahiniwa 1,384,186 waliosajiliwa. Katika mtihani huo watahiniwa 1,073,402 sawa na asilimia 79.62 walifaulu;​
  • Imeendesha Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili wa mwaka 2022 kwa wanafunzi 635,130 ambao ni sawa na asilimia 92.00 ya wanafunzi 690,341 waliosajiliwa. Katika mtihani huo wanafunzi 539,645 sawa na asilimia 85.18 walifaulu;​
  • Imeendesha Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) wa mwaka 2022 kwa watahiniwa 522,217 ambao ni sawa na asilimia 97.66 ya watahiniwa 534,753 waliosajiliwa. Katika mtihani huo watahiniwa 456,975 sawa na asilimia 87.79 walifaulu;​
  • Imeendesha Mtihani wa Maarifa (QT) kwa watahiniwa 9,557 kati ya watahiniwa 12,110 waliosajiliwa kufanya mtihani ambapo watahiniwa 4,059 sawa na asilimia 42.47 walifaulu; na​
  • Inaendelea na utahini wa Mtihani wa Kidato cha Sita (ACSEE), 2023 kwa watahiniwa 106,946 waliosajiliwa na Mtihani wa Ualimu kwa watahiniwa 8,900 waliosajiliwa. Mitihani hiyo ilianza kufanyika tarehe 2 Mei, 2023.​

iv. Kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Utoaji wa Elimu na Mafunzo katika Ngazi Zote za Elimu Nchini

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa mafunzo kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu (Education Sector Development Plan) na Mpango Mkakati wa Wizara (Strategic Plan) 2021/22 – 2025/26 kwa wadau mbalimbali 1,221 wakiwemo Maafisa Elimu Mkoa na Wilaya; Maafisa Mipango; Wakurugenzi wa Halmashauri; Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya Mkoa na Wilaya; Wathibiti Ubora wa Shule Wakuu na Wakuu wa Vyuo. Mafunzo yalilenga kujenga uelewa kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Elimu Nchini na kujumuisha mpango huo katika mipango na bajeti za elimu kwa ngazi ya Halmashauri na Mkoa.

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji pamoja na kuimarisha usimamizi wa elimu nchini, Wizara imesambaza jumla ya vishikwambi 4,067 kama ifuatavyo: vishikwambi 1,352 kwa wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu; 305 kwa wakufunzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi; 730 kwa wakufunzi wa Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi; na 1,680 kwa Wathibiti Ubora wa Shule Ngazi ya Kanda na Halmashauri. Aidha, imekabidhi vishikwambi 274,812 Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na vishikwambi 6,600 kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ili visambazwe kwa walimu wa shule za msingi na sekondari, maafisa elimu ngazi ya Mkoa, Halmashauri na Kata.

v. Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Mafunzo ya Amali)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza fursa za mafunzo na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imedahili jumla ya wanafunzi 123,352 (Wanawake 65,894 na Wanaume 57,458) katika Ngazi ya Astashahada ya Awali, Astashahada na Stashahada kwa fani mbalimbali; na​
  • Imesajili vyuo 127 katika Bodi za Masomo zifuatazo: Afya na Sayansi Shirikishi vyuo vitatu; Biashara, Utalii na Mipango vyuo vinne; Sayansi na Teknolojia Shirikishi chuo kimoja na vyuo vya ufundi stadi (VET) 119; na kufanya jumla ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuwa 1,329 (Vyuo vya Elimu ya Ufundi -TET 465, Vyuo vya Ufundi Stadi - VET 809 na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi - FDC 55).​
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwajengea uwezo watumishi katika taasisi za Elimu ya ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imetoa mafunzo kuhusu upimaji na ufundishaji wa mitaala inayozingatia umahiri kwa wakufunzi 1,206 wa vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji; na​
  • Imetoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 1,980 wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wadau.​
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza fursa na ubora wa elimu ya ufundi, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika Taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini kwa kutekeleza yafuatayo:​
  • Imekamilisha ujenzi wa jengo lenye madarasa nane yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 880 kwa wakati mmoja, maabara sita zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 270 kwa wakati mmoja, bweni la wanafunzi wa kike lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 428 kwa wakati mmoja na ofisi 26 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 104 katika Chuo cha Ufundi Arusha;​
  • Inaendelea na ujenzi wa hosteli katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar ambapo ujenzi umefikia asilimia 45. Vilevile, inaendelea na ujenzi wa jengo la Maktaba itakayokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,500 na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja katika chuo hicho; na​
  • Inaendelea kukamilisha ujenzi wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Wilaya 25 ambapo ujenzi umefikia asilimia 98. Aidha, Chuo cha Wilaya ya Mbarali na Chuo cha Wilaya ya Kishapu vimeanza kutoa mafunzo.​

vi. Kuongeza Fursa na Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Juu

Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza fursa za Elimu na Mafunzo ya Elimu ya Juu nchini kwa kudahili jumla ya wanafunzi wa Elimu ya Juu 113,383 (Wanawake 49,188 na Wanaume 64,195) sawa na asilimia 88 ya waombaji kwa ngazi ya Shahada ya Kwanza.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeendelea kuimarisha huduma ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa na uhitaji. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetoa jumla ya Shilingi 652,763,079,647.00 kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa wanufaika 202,877 ambapo Shilingi 652,176,491,647.00 zimetolewa kwa wanafunzi wanaosoma ndani ya nchi na Shilingi 586,588,000.00 kwa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, vilevile kupitia SAMIA Scholarship, Serikali imetoa ufadhili wa Shilingi 2,754,370,430.00 kwa wanafunzi 593 wenye ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi katika kidato cha 6 ambao wanaendelea kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati au Afya na Sayansi Shirikishi (Science, Technology, Engineering, Mathematics or Health and Allied Sciences) katika ngazi ya Shahada.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau katika kutoa mikopo ya elimu kwa wanafunzi ambapo Benki ya NMB imezindua huduma hiyo kwa wanafunzi kupitia mzazi au mlezi. Katika mwaka 2022/23 Shilingi bilioni 200 zimetengwa na mkopaji anaweza kukopa kuanzia Shilingi 200,000.00 hadi Shilingi 10,000,000.00 kwa marejesho ya riba nafuu ya asilimia 9.

Mheshimiwa Spika,
natumia fursa hii kuushukuru uongozi wa Benki ya NMB na natoa rai kwa taasisi nyingine za kifedha pamoja na wadau mbalimbali wa elimu nchini kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kutoa mikopo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mikopo ya elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wataalamu wetu wanapata uzoefu na ujuzi wenye kuendana na mahitaji ya kikanda na kimataifa. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imeratibu ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 76 wa Kitanzania katika nchi ya Uingereza (Jumuiya ya Madola) wanafunzi watatu, Hangaria 21 na China 52 katika ngazi ya Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamivu; na​
  • Imewezesha mafunzo kwa vitendo katika kilimo kwa wanafunzi 250 nchini Israel kwa kipindi cha miezi 11 kwa lengo la kujifunza kwa vitendo masuala ya kilimo katika nchi hiyo.​
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwezesha mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi kwa watumishi wa Taasisi za Elimu ya Juu kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na utendaji kazi. Katika kufikia azma hiyo Serikali, imetekeleza yafuatayo:​
  • Imetoa mafunzo ya kuandaa mitaala kwa wahadhiri 280 wa Vyuo Vikuu ili kuandaa mitaala kwa kuzingatia miongozo, viwango na mahitaji ya sasa; na​
  • Imewezesha mafunzo kwa wahadhiri na watumishi 2,127 (wahadhiri 192 kuhusu namna bora ya ufundishaji, watumishi 845 mafunzo ya muda mrefu na na watumishi 1,090 muda mfupi) katika Taasisi za Elimu ya Juu.​
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza fursa za mafunzo katika Taasisi za Elimu ya Juu na Sayansi na Teknolojia, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imekamilisha ujenzi wa jengo mtambuka lenye maabara nane na vyumba 11 vya maandalizi, ofisi saba, madarasa nane na stoo saba katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. Aidha, imeanza taratibu za kupata hati miliki kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya chuo hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoa wa Ruvuma; na​
  • Imekamilisha ukarabati wa vyumba vya madarasa 30, mabweni mawili, maabara, ofisi saba, nyumba 10 na miundombinu ya TEHAMA katika Chuo Kikuu Ardhi.​

vii. Kuimarisha Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Maendeleo ya Taifa

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchochea maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu nchini kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imetoa mafunzo kwa wabunifu wachanga 83 na rasilimali fedha kwa wabunifu 27 walioibuliwa katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) mwaka 2022 kwa lengo la kuendeleza bunifu na teknolojia ili zifikie hatua ya ubiasharishaji; na​
  • Imetambua teknolojia mpya 27 zilizozalishwa nchini na hivyo kufanya jumla ya teknolojia zilizotambuliwa nchini hadi sasa kufikia 506. Lengo la utambuzi huo ni kuwa na kanzidata ya kitaifa kwa ajili ya rejea kuhusu taarifa za teknolojia na ubunifu zinazozalishwa nchini​

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kubidhaisha teknolojia na ubunifu kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kuongeza ufanisi katika kuchangia maendeleo ya nchi. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imetekeleza yafuatayo:​
  • Imeendeleza ubunifu wa Prepaid Water Meter kwa kutengeneza na kufunga mita 20 kwa majaribio katika Wilaya 10 za mikoa mitano ambapo kila Wilaya ilipata mita mbili kama ifuatavyo: Tanga (Handeni na Pangani), Morogoro (Morogoro Vijijini na Mvomero), Pwani (Bagamoyo na Mkuranga), Iringa (Iringa Vijijini na Mufindi), na Njombe (Makete na Wanging’ombe). Ubunifu huo utawezesha udhibiti wa matumizi ya maji na ukusanyaji wa mapato; na​
  • Imewezesha kampuni changa mbili za Teknolojia na Ubunifu ambao ni ‘Smart Darasa na Dawa Mkononi’ kushiriki katika shindano la ubunifu ambalo lilifanyika nchini Afrika Kusini lenye lengo la kuendeleza ubunifu. Aidha, shindano hilo lilishirikisha waanzilishi 13 kutoka Namibia, Afrika Kusini, Botswana na Zambia ambapo ubunifu wa ‘Dawa Mkononi’ kutoka Tanzania uliibuka mshindi wa pili.​

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki imeendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya mionzi ya nyuklia nchini kwa kutekeleza yafuatayo:​
  • Imepima sampuli 21,583 za vyakula, mbolea, tumbaku na bidhaa nyingine kati ya 28,000 zilizolengwa kupimwa kutoka mipakani, viwanja vya ndege na bandari ambapo kipimo kilionesha kuwa hakuna uchafuzi wa mionzi;​
  • Imekagua vituo 184 vyenye vyanzo vya mionzi ambapo vituo 168 vilikuwa katika hifadhidata na vituo vipya 16 kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa usalama kwa watumiaji; na​
  • Imetoa jumla ya leseni 314 ambapo leseni 220 za kumiliki na kutumia vyanzo vya mionzi, 62 za uingizaji (import); saba za kupeleka nje ya nchi (export); na leseni 25 kwa ajili ya usafirishaji wa mionzi.​

viii. Kuimarisha na Kuendeleza Tafiti na Matumizi ya Matokeo yake katika Ajenda ya Maendeleo

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa utafiti na matumizi yake katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii na kuchangia maendeleo ya nchi. Katika kufikia azma hiyo, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa ndani wa kufanya utafiti na kutumia matokeo ya utafiti kwa kutoa machapisho 1,836 kupitia Taasisi za Elimu ya Juu katika majarida ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa na kuchangia katika kuvitangaza (Visibility) Vyuo hivyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuanzisha, kuratibu na kusimamia miradi mbalimbali ya utafiti na ubunifu katika taasisi za Elimu ya Juu na Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuongeza maarifa na kutatua changamoto katika jamii. Azma hiyo imefikiwa kwa kufanya miradi ya utafiti 418 katika Vyuo Vikuu, Vyuo Vikuu Vishiriki na Taasisi za Utafiti na Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ili kuhamasisha wataalamu kuandika na kuchapisha kazi za utafiti, Serikali imeandaa Mwongozo wa Utoaji Tuzo kwa Watafiti watakao chapisha utafiti wao katika Majarida yenye hadhi ya Kimataifa ‘High Impact Factor Jounals’ katika Fani za Sayansi Asilia na Tiba.

D. TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA TUME YA TAIFA YA UNESCO (FUNGU 18)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO imetekeleza yafuatayo:​
  • Imetoa mafunzo kwa washiriki 23 kutoka vyombo vya habari, wawakilishi wa Serikali kutoka Idara ya Habari Maelezo na wanachuo kutoka chuo Kikuu cha SUZA kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza utawala wa haki na sheria;​
  • Imeratibu mafunzo dhidi ya mapambano ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu na mbinu haramu michezoni kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo washiriki 230 wakiwemo wakufunzi, viongozi wa michezo, wanamichezo na watunga sera walishiriki; na​
  • Imeendelea kufanya utambuzi wa Taasisi zinazokidhi vigezo vya kujiunga na Mitandao ya Elimu ya UNESCO. Vilevile, imehuisha mikataba minne inayohusiana na Elimu ya Juu.​
Tanbihi: TAARIFA YA KINA YA UTEKELEZAJI YA MAJUKUMU YA WIZARA KWA KINA INAPATIKA KATIKA KITABU CHA HOTUBA UK. 6 - 51

E. MWELEKEO WA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/24, Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu, kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Mheshimiwa Spika, vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni kama vifuatavyo:​
  • Kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu na kuanza utekelezaji;​
  • Kuongeza fursa na ubora wa mafunzo ya amali (Ufundi na Ufundi Stadi) katika elimu ya sekondari na Vyuo vya Mafunzo ya Amali;​
  • Kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari;​
  • Kuongeza fursa na ubora wa Elimu ya Juu; na​
  • Kuimarisha uwezo wa nchi katika Utafiti, Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.​

i. Kukamilisha Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu

Mheshimiwa Spika, Serikali itakamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu pamoja na kuanza utekelezaji wake ili kuimarisha maarifa na ujuzi kwa wahitimu wa ngazi zote za elimu. Aidha, Serikali itafanya mapitio ya sheria ya elimu na sheria mbalimbali za Taasisi za Elimu ili kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.

ii. Kuongeza Fursa na Ubora wa Mafunzo ya Amali (Ufundi na Ufundi Stadi) kwa Sekondari na Vyuo vya Kati vya Amali

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha mafunzo ya Amali (Ufundi na Ufundi Stadi) kwa shule za sekondari na vyuo vya ualimu kwa itawezesha ukarabati wa shule za sekondari za ufundi na kuzipatia vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Aidha, itaboresha vyuo vya ualimu 10 kwa kujenga karakana na kuweka mitambo na vifaa katika vyuo hivyo ambavyo ni: Kitangali, Ndala, Nachingwea, Kleruu, Mtwara (U), Mpwapwa, Korogwe, Dakawa, Bunda na Kabanga kwa lengo la kuimarisha utoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Chuo cha Ualimu Mtwara Kawaida na Mtwara ufundi vitawezesha walimu tarajali kupata mafunzo ya Shahada ya Amali kwa kutumia wahitimu wa Vyuo vya Ufundi (TET) na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET).

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza fursa za elimu ya amali kwa kuendelea kusajili na kudahili wanafunzi katika vyuo vya mafunzo ya amali. Aidha, katika kuongeza idadi ya walimu wa ufundi, Serikali itadahili wanafunzi 660 katika Chuo cha Ualimu wa Mafunzo ya Ufundi Stadi Morogoro – MVTTC.

Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea umahiri walimu wa vyuo vya mafunzo ya amali na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ili kuinua ubora wa mafunzo, Serikali itatoa mafunzo kwa wakufunzi 1,450 kuhusu ufundishaji wa mitaala inayozingatia umahiri (CBET) kwa lengo la kuwa na walimu mahiri watakaotoa mafunzo kwa wanachuo ili waweze kujiajiri na kuajirika.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi 64 katika Wilaya ambazo hazina vyuo hivyo pamoja na ujenzi wa Chuo cha Mkoa wa Songwe na itaanza kutoa mafunzo ya amali katika vyuo 29 vilivyokamilika. Vilevile, itakamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza ya Chuo cha Ufundi Dodoma ambapo kukamilika kwa awamu hiyo kutawezesha kudahili wanafunzi 1,500.

iii. Kuwezesha Ongezeko la Fursa na Ubora wa Elimu ya Msingi na Sekondari

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza fursa za Elimu kwa kutoa ithibati kwa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa kusajili shule za msingi na sekondari takribani 560. Aidha, itaanza kusajili shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mfumo wa kieletroniki.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa fursa za elimu na mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kununua na kusambaza zana na vifaa saidizi kwa walimu tarajali, walimu na wakufunzi wenye mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kubaini na kukuza vipaji vya uandishi unaozingatia ubunifu kwa lengo la kujenga tabia ya kujisomea, kuhifadhi historia, mila na desturi za jamii pamoja na kuimarisha vipaji vya sanaa na michezo. Katika kufikia azma hiyo, Serikali itatekeleza yafuatayo:​
  • Itasimamia utoaji wa Tuzo ya Kitaifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu yenye lengo la kuwatambua na kuwazawadia waandishi mahiri katika nyanja ya riwaya, hadithi fupi na ushairi kwa lengo la kukuza kazi za uandishi bunifu, uchapaji na kuongeza idadi ya machapisho katika shule na maktaba nchini; na​
  • Itaendelea kuratibu mashindano ya uandishi wa insha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ili kukuza stadi za uandishi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini.​

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uthibiti ubora wa elimu kwa ngazi ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu, Serikali itatekeleza yafuatayo:​
  • Itaimarisha Mfumo wa Uthibiti Ubora wa Shule kwa kufanya ugatuaji kutoka ngazi ya kanda kwenda ngazi ya mikoa ili kusogeza huduma karibu na wadau na kuzifikia asasi nyingi; na​
  • Itafanya tathmini ya jumla ya shule na asasi 6,700 katika maeneo yafuatayo: mafanikio ya wanafunzi; ubora wa ufundishaji kwa ujifunzaji na upimaji; ubora wa uongozi na utawala; ubora na mazingira ya shule na matokeo yake katika ustawi, na afya na usalama wa wanafunzi na ushiriki wa jamii. Vilevile, itanunua magari 12 na kuweka samani katika ofisi 195 za uthibiti ubora wa shule kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji wa kazi.​

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha ujifunzaji na kuongeza ufaulu wa wanafunzi, Serikali itaendelea kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha katika shule za msingi, sekondari pamoja na wathibiti ubora wa shule kwa kutekeleza yafuatayo:​
  • Itatoa mafunzo kwa walimu 10,000 wa masomo ya Sayansi na Hisabati wa shule za sekondari Kidato cha 1 – 4; mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 4,500 wa shule za sekondari 1,300; mafunzo kuhusu programu ya shule salama kwa wakuu wa shule za Sekondari na Wathibiti Ubora wa Shule 1,378; mafunzo kuhusu unasihi na ulinzi wa mtoto kwa walimu 3,370 wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu; mafunzo kuhusu ufundishaji wa moduli za masomo 18 hatua ya I na II kwa walimu 600 kutoka katika vituo 151 vya Elimu kwa Njia Mbadala kwa lengo la kuongeza umahiri na kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji; na​
  • taendelea kuwajengea uwezo walimu 12,000 wa shule za msingi katika upimaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) katika mikoa 10 iliyokuwa na wastani wa chini wa stadi hizo.​

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa vitabu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwa kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada katika maandishi yaliyokuzwa kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la awali, Darasa la I na III, Sekondari Kidato cha 1 na Elimu ya Ualimu kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu na vitabu vya nukta nundu kwa ajili ya wanafunzi wasioona.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza idadi ya vitabu vya ziada na rejea vitakavyosaidia walimu na wanafunzi kukuza uelewa wa mada mbalimbali, Serikali itatathmini vitabu vya ziada na rejea kutoka kwa waandishi binafsi. Aidha, itawezesha uchapaji wa vitabu vya viongozi mbalimbali wa Kitaifa kwa lengo la kukuza uzalendo na maarifa kwa wanafunzi. Vitabu hivyo ni pamoja na: Maisha ya Benjamin William Mkapa; Kitabu cha Maisha ya Ali Hassan Mwinyi; Kitabu cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; na 38 Reflections on Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu na kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na elimu ya ualimu, Serikali kupitia Wizara na Taasisi zake itatekeleza yafuatayo:​
  • Itawezesha ujenzi wa vyumba 90 vya madarasa, matundu ya vyoo 360, mabweni 10 ya wasichana, nyumba 38 za walimu na maabara 20 za sayansi. Vilevile, itawezesha ujenzi wa miundombinu katika shule 10 za wanafunzi wenye mahitaji maalum kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania; na​
  • Itakarabati miundombinu ya maabara za kilimo, sayansi, lugha na sayansi kimu katika Vyuo vya Ualimu saba ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa vitendo. Aidha, itaendelea kuunganisha vyuo vya ualimu 11 katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.​

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na ujenzi wa jengo la maktaba ya Taifa Makao Makuu Dodoma ambalo pia litatumika kuhifadhi nyaraka na machapisho kwa lengo la kutunza historia, maarifa, maadili, na mila na desturi za Mtanzania. Vilevile, itajenga maktaba ya Mkoa wa Singida ambayo itawezesha upatikanaji wa huduma za maktaba.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukuza na kuendeleza kisomo na elimu kwa umma kwa kuanzisha madarasa 1,000 ya kisomo yanayolenga kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Watu Wazima. Aidha, itaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea ujuzi vijana 12,000 kupitia Mpango wa elimu changamani kwa walio nje ya shule awamu ya pili (IPOSA).

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha uongozi na usimamizi wa elimu nchini, Serikali kupitia Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu itatoa mafunzo ya muda mfupi ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa walimu wakuu 6,500 wa shule za msingi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania itaendesha Mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne kwa wanafunzi 1,815,792, Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi kwa watahiniwa 1,537,171, Mtihani wa Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili kwa wanafunzi 691,078, Kidato cha Nne kwa watahiniwa 610,330 na mtihani wa Maarifa kwa watahiniwa 8,500, Mtihani wa Kidato cha Sita kwa watahiniwa 94,920 na Mtihani wa ngazi ya Cheti na Stashada ya Ualimu kwa watahiniwa 8,505.

iv. Kuongeza Fursa na Ubora wa Elimu ya Juu

Mheshimiwa Spika, Serikali itaratibu na kuongeza fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kutekeleza yafuatayo:​
  • Itadahili wanafunzi 135,000 wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kuomba udahili katika vyuo vya Elimu ya Juu kwa ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya Awali na Umahiri​
  • Itatoa nafasi 100 za ufadhili wa masomo kutoka nchi rafiki na mashirika mbalimbali nje ya bara la Afrika kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu;​
  • Itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka 202,877 hadi 210,169; na​
  • Itaendelea kutoa fursa za Elimu ya Juu kwa wanafunzi wenye ufaulu uliojipambanua kutoka wanafunzi 593 hadi 1200 kupitia Samia Skolashipu.​

Mheshimiwa Spika, Serikali itaboresha mafunzo ya udaktari na kuongeza utoaji huduma katika vitengo mbalimbali vya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili ikiwemo shule ya meno na kuendelea na mradi wa ujenzi wa Kliniki ya Uporoto kwa lengo la kuimarisha mazingira ya kufundishia, utafiti na kutoa huduma za tiba kwa jamii. Vilevile, itaimarisha miundombinu ya kufundishia katika kituo cha umahiri cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kampasi ya Mloganzila.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi katika taasisi za Elimu ya Juu nchini, Serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa Wanataaluma na Wataalam 1,197 wa Elimu ya Juu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya Taasisi za Vyuo Vikuu ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga kampasi 14 za Vyuo Vikuu katika mikoa ambayo haina kwa lengo la kuandaa rasilimaliwatu wenye ujuzi watakaowezesha kuleta mageuzi ya kiuchumi. Vilevile, itaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika Taasisi za Elimu ya Juu.

v. Kuimarisha Uwezo wa Nchi katika Utafiti, Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili Kuchochea Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza maarifa na kutatua changamoto mbalimbali katika jamii Serikali itafanya utafiti katika maeneo 177 ya elimu, lugha, kilimo, biashara, uvuvi, mifugo, tiba, haki za binadamu, maendeleo ya watu na mawasiliano, maliasili, sayansi, teknolojia, watu wenye mahitaji maalum, kilimo na chakula, uongozi na biashara. Vilevile, itaendelea kutoa huduma ya ushauri wa kitaalamu katika nyanja mbalimbali. Aidha, itaandaa machapisho 1,806 kwa lengo la kueneza matokeo ya utafiti kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwatambua wabunifu, kuwaendeleza na kubiasharisha ubunifu wao pamoja na kuendeleza miradi mbalimbali ya ubunifu kwa lengo la kukuza utaalamu asilia kwa kuendeleza teknolojia zinazozalishwa na wabunifu nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha matumizi salama ya mionzi ya nyuklia nchini, Serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki itaendelea kudhibiti matumizi ya mionzi nchini kwa kukagua vituo 900 vyenye vyanzo vya mionzi ili kuhakikisha usalama wa wagonjwa, wafanyakazi na jamii. Aidha, itapima na kudhibiti viwango vya mionzi kwa wafanyakazi 2,110 wanaofanya kazi kwenye mazingira yenye vyanzo vya mionzi. Vilevile, itafuatilia hali ya usalama wa hewa katika anga kupitia vituo 1,045.

F. TUME YA TAIFA YA UNESCO (FUNGU 18)

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya UNESCO, itaendelea kuratibu, kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa mikataba ya Kimataifa ya UNESCO. Vilevile, itatoa elimu kwa Taasisi na Mamlaka za Serikali kuhusu Mkataba wa 2001 wa Urithi wa Chini ya Bahari (Underwater Heritage) ambao Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo mbioni kuuridhia. Aidha, itafuatilia na kutathmini maeneo mapya ya urithi yaliyopendekezwa na wadau ili kuongeza maeneo zaidi ya urithi wa dunia nchini yanayotambuliwa na UNESCO kwa lengo la kuongeza vivutio vya utalii.

G. SHUKRANI

Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa QS Omary Juma Kipanga (Mb), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ushirikiano anaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu na kufikia malengo ya wizara. Aidha, napenda kumshukuru Katibu Mkuu Profesa Carolyne Ignatius Nombo, Naibu Makatibu Wakuu, Profesa James Epiphan Mdoe na Dkt. Franklin Jasson Rwezimula kwa kunipa ushirikiano. Vilevile, bila kuwasahau Kamishna wa Elimu, Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi na watumishi wote kwa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara na kuwezesha kuandaliwa kwa hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru pia Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, watumishi wa Wizara na Taasisi zake, Walimu, Wanafunzi, na Wadau wote wa Elimu kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wamiliki na Mameneja wa Shule, Vyuo na Taasisi binafsi ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali katika kutoa huduma ya elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru Washirika wa Maendeleo na Wadau wote wa Elimu ambao wamechangia kufanikisha utekelezaji wa Mipango na Miradi ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Naomba kuwatambua baadhi yao kama ifuatavyo: Serikali ya Misri, Msumbiji, Morocco, Namibia, Tunisia, Mauritius, Comoro, Ethiopia, Zimbabwe, Algeria, Afrika Kusini, Malawi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Austria, Brazil, Canada, China, Cuba, Finland, Hungary, India, Indonesia, Italia, Israel, Japan, Korea ya Kusini, Marekani, Malaysia, Netherland, New Zealand, Norway, Palestina, Romania, Saudi Arabia, Sweden, Thailand, Ufaransa, Urusi, Uswisi, Uingereza, Uholanzi, Ujerumani na Venezuela. Aidha, natambua pia mchango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kushukuru Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa yaliyochangia kufanikisha miradi na programu za Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ni pamoja na: Swedish International Development Agency (SIDA), Umoja wa Nchi za Ulaya, Foreign, Commonwealth and Development Office (FCDO), Benki ya Maendeleo ya Afrika, Jumuiya ya Madola, Global Partnership in Education (GPE), United Nations International Children’s Emergency Fund (UNICEF), United Nations Development Programme (UNDP), United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization (UNESCO), United States Agency for International Development (USAID), Benki ya Dunia, Inter University Council for East Africa (IUCEA), Human Development Innovation Fund (HDIF), Deutscher Akademischer Austauschdienst (DAAD), British Council, Campaign for Female Education (CAMFED), Commonwealth Secretariat, Aga Khan Education Services, Japan International Cooperation Agency (JICA), Karibu Tanzania Organization (KTO), Korea International Cooperation Agency (KOICA), Water Aid, Plan International, Tanzania Education Network/Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Mo Foundation, Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Christian Social Services Commission (CSSC).

H. MAOMBI YA FEDHA KWA MWAKA 2023/24

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2023/24, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (Fungu 46) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 1,675,753,327,000.00 kwa mchanganuo ufuatao:​
  • Shilingi 537,880,762,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara ambapo Shilingi 500,957,569,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara na Shilingi 36,923,193,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo; na​
  • Shilingi 1,137,872,565,000.00 zinaombwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 979,083,678,000.00 ni fedha za ndani na Shilingi 158,788,887,000.00 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo.​

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya UNESCO (Fungu 18) inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 2,733,888,000.00 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (Mishahara ni Shilingi 1,124,980,000.00 na Matumizi Mengineyo ni Shilingi 1,608,908,000.00).

Mheshimiwa Spika,
kwa heshima kubwa naomba sasa Bunge lako tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Bajeti ya Fungu 46 na Fungu 18 yenye jumla ya Shilingi 1,678,487,215,000.00.

Mheshimiwa Spika,
napenda kuhitimisha kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza.

Mheshimiwa Spika, Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara http://www.moe.go.tz.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Tanbihi: TAARIFA YA KINA KUHUSU MWELEKEO WA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24 UNAPATIKA KATIKA KITABU CHA HOTUBA UK. 52 - 88
 
SIELEWI KABISA KWA NINI INAITWA WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA,HAKUNA SEHEMU WAMEZUNGUMZIA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KINAGAUBAGA,NA HAKUNA FUNGU LILILOTENGWA KWA AJILI YA MAENDELEO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA,SAYANSI NA TEKNOLOJIA INAMEZWA NA ELIMU.

NASHAURI WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA IVUNJWE,KUWE NA WIAR YA ELIMU NA WIZARA YA MAENDELEO YA SAYANSI,TEKNOLOJIA NA UVUMBUZI.
 
Kwa aina ya watu wa nchi hii wala haitakua na tija bali kuongeza mzigo wa matumizi ya fedha.
 
MAKUBWA YA RAIS SAMIA SEKTA YA ELIMU

Katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Mhe. Rais Dkt. Samia Hassan Suluhu ametenga kiasi cha shilingi Trilioni 1.6 kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya utekelezaji wa Maendeleo na majukumu mbalimbali ya wizara hio
#SautiYaMwenezi
 
Attachments

  • FzOtFxqX0AE4WgJ.jpg
    FzOtFxqX0AE4WgJ.jpg
    109.9 KB · Views: 22
Back
Top Bottom