Mtutura: Serikali iwalipe wakulima fedha zao

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
Kwa muda mrefu sasa wakulima nchini wanalalamikia ucheleweshaji wa malipo ya fedha za mazao yaliyochukuliwa na Wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA). ACT Wazalendo tumefuatilia kwa karibu mwenendo wa ununuzi wa mazao hayo (mahindi) katika Mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Katavi, Njombe na Mbeya. Tumebaini kuna ucheleweshaji wa malipo kwa takribani miezi mitatu.

Itakumbukwa, ACT Wazalendo tulitoa wito kwa kuitaka Serikali kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha angalau miezi sita ili kujihakikisha usalama wa chakula na kukabiliana na kasi ya kupaa kwa bei za chakula kwa misimu miwili mfululizo. Serikali ilichukua wito wetu na kuahidi kuongeza uwezo wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wa kununua chakula kutoka kwa wakulima kiasi cha tani 500,00. Ingawa ilikuwa bajeti kiduchu kutosha kwa miezi 2, angalau ilitoa matumaini kidogo.

Tumesikitishwa sana kuona utekelezaji wa ahadi hiyo unaenda kinyume badala ya kununua chakula, Serikali kupitia NFRA imeenda kuwakopa wakulima na kuwaacha kwa muda mrefu bila matumaini.
Kitendo cha ucheleweshaji wa malipo kina athiri uwezo wa wakulima kujiandaa na kilimo katika msimu ujuo kwa kuwa hawana fedha za kununua pembejeo za kilimo.

Pili, kimeshusha imani ya wakulima kwa Serikali na kupelekea kukataa kuuza mazao yao kwa NFRA. Hivyo, wafanyabiashara wanatumia mwanya huo kununua kwa bei ndogo na baadae bei zikipanda mzigo wa mfumuko wa bei za vyakula utakuwa mabegani mwa wananchi wa kawaida. Kwa sababu NFRA hawatakuwa na chakula cha kutosha kukiingiza kwenye mzunguko kukabiliana na makali ya bei.

Suala la hifadhi na usalama wa chakula ni muhimu sana kwa usalama na amani ya Taifa. Serikali inapaswa kuacha mzaha au ujanja ujanja. Licha ya kuonyesha tunazalisha chakula cha kutosha, uwezo wetu kama nchi wa kuhifadhi chakula ni mdogo sana kiasi cha kuathiri usambazaji na upatikanaji wa chakula kwenye maeneo yenye mavuno hafifu.

ACT Wazalendo tunaitaka Serikali itoe fedha mara moja kwa NFRA ili iweze kuwalipa wakulima fedha zao zote wanazoidai. Pili, tunarudia wito wetu kwa Serikali kupitia Mamlaka ya Chakula (NFRA) kuongeza nguvu ya kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha miezi sita (6) ili kuwa na akiba ya chakula kama sehemu ya kujiandaa na majanga.

Mwisho, Serikali iweke mazingira bora kwa wakulima wadogo ili kuongeza uzalishaji zaidi; kwa kuendelea kutoa ruzuku katika mbolea na kusimamia usambazaji wake; kuhakikisha usalama wa ardhi kwa wakulima wadogo kwa kushughulikia migogoro ya ardhi.

Imetolewa na;
Ndg. Mtutura Abdallah Mtutura
X: @MtuturaAbdallah
Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika
ACT Wazalendo.
21 Oktoba, 2023
 
Back
Top Bottom