Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,346
- 33,183
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Edmund Rice, John Justine (17) mkazi wa Makao Mapya, ambaye anasubiria matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, amejiua kwa kujipiga risasi kifuani, baada ya kudaiwa fedha na baba yake mzazi Justine Kaiza.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1:30 usiku, nyumbani kwa wazazi wa marehemu huko makao mapya.
Alisema kuwa siku ya tukio, mama mzazi wa marehemu, Betty Mushi alikwenda kwenye sherehe na aliporudi muda wa saa 1:00 usiku, alikuta mlango wa geti umefungwa na hapo aliamua kumwomba mtoto wa jirani, ili amsaidie kufungua geti gilo.
Mama huyu baada ya kufunguliwa geti tu, aliingia ndani na alipoingia sebuleni alimkuta mtoto wake amelala chini, huku akihema kwa taabu na damu ikimtoka kwa wingi kifuani, alisema.
Alisema mama wa marehemu alipoona hivyo alitoka nje kuomba msaada wa majirani ambao walifika na kumpeleka hospitali ya Ithna Asher Charitable, maarufu kwa Dk. Mohamed, iliyopo eneo la Tanki la Maji Ilboru.
Kamanda Andengenye aliendelea kueleza kuwa baada ya kumfikisha katika hospitali hiyo, walitakiwa kumpeleka mgonjwa wao Hospitali ya Mkoa Mount Meru na walipofika hospitalini hapo akiwa anapatiwa matibabu alifariki dunia.
Aidha, polisi walipopata taarifa hizo walikwenda eneo la tukio na kukuta bunduki aina ya Shortgun Pump Action na ganda moja la risasi na pembeni yake walikuta ujumbe wa karatasi uliokuwa ukisema kwa maandishi ya herufi kubwa, Ninasikitika kulaumiwa na wazazi wangu, na pia ninawapenda sana.
Pia polisi hao walifaniki wakuona michuliziko ya damu toka ndani ya chumba cha marehemu hadi sehemu alipoangukia sebuleni.
Andengenye alisema kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa awali waligundua baba mzazi wa marehemu alikuwa akimdai fedha kijana wake alizomwibia ambazo ni dola za Marekani 1,500 sawa na fedha za kitanzania zaidi ya Sh. milioni 2.3.
Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na Polisi wanaendelea kumwoji baba mzazi wa marehemu Justine Kaiza kuhusiana na tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ukisubiri uchunguzi zaidi.
CHANZO: NIPASHE