Msaidizi wa Rais Kikwete apelekwa Tume ya Maadili 'msobemsobe'

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
Wednesday, 13 April 2011 20:59

Raymond Kaminyoge
Mwananchi

MSAIDIZI wa Rais Jakaya Kikwete, katika masuala ya Siasa, Rajabu Luhwavi jana alikamatwa na polisi na kufikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma baada ya kukaidi wito uliomtaka kuhudhuria kikao cha baraza hilo Jumatatu iliyopita.

Ilielezwa kwamba Aprili 11, mwaka huu, Luhwavi alitakiwa kufika kwenye Baraza hilo kueleza kwa nini hakujaza fomu kuonyesha mali zake katika kipindi cha mwaka 2009, lakini bila taarifa yoyote, hakufika.

Hatua hiyo ililifanya Baraza hilo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Damian Lubuva akisaidiana na wajumbe, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi na Gidious Tibakweitira, lililazimika kutumia dola kumleta Luhwavi mbele yake.
Katika shauri hilo, Jaji Lubuva alimtaka Msaidizi huyo wa Rais, kueleza sababu zilizofanya ashindwe kufika mbele ya Baraza licha ya kuandikiwa barua na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Katika utetezi wake, Luhwavi alisema hajawahi kupokea barua yoyote ya wito wa kufika mbele ya Baraza hilo: "Sikuwa na taarifa yoyote ya kuitwa mbele ya Baraza lako. Nimesikia kupitia vyombo vya habari kwamba natakiwa kukamatwa na polisi kufikishwa katika Baraza."

Baada ya kutoa jibu hilo, msaidizi wa sekretarieti ya maadili, alionyesha 'dispatch book' iliyoonyesha kwamba barua ya wito kwa Luhwavi ilisainiwa na ofisa wa Ikulu Machi 18, mwaka huu.

Hata hivyo, baada ya kuiangalia sahihi hiyo, Luhwavi alisema haikuwa yake wala ya katibu muhtasi wake... "Hii sahihi siifahamu. Siyo yangu wala katibu muhtasi wangu. Sielewi ni nani aliyesaini. Inawezekana walisaini walinzi wa getini, lakini kwangu, haikufika. Nimekula kiapo cha kuwa mwaminifu. Hii barua haikunifikia. Nafahamu umuhimu wa Baraza hili sikuwa na sababu ya kuacha kufika bila kutoa taarifa."

Mmoja wa wanasheria wa sekretarieti hiyo alidai kwamba barua hiyo ilipelekwa Ikulu na Mwanasheria mwenzao, Hassani Mayunga na kusainiwa na Katibu Muhtasi wa Luhwavi.Jaji Lubuva alihoji iweje maofisa wenzake (Luhwavi) wa Ikulu wapate barua za wito lakini, yeye asipate?
"Hapa inatushangaza, Ikulu maofisa wengine wamefika mbele ya Baraza, ina maana walipata barua za wito lakini wewe peke yako ndiyo hukuipata?" alihoji Jaji Lubuva.

Alimtaka ofisa huyo kutorudia kitendo hicho akisema alitakiwa kuwa mfano kwa wengine kwa kuwa anatoka kwenye ofisi kubwa inayoheshimika."Nisingependa jambo hili kurudiwa siku nyingine. Leo umeletwa na polisi, ukirudia siku nyingine, tutachukua hatua zaidi za kisheria,"alisema Jaji Lubuva.Baada ya maelekezo hayo, Jaji Lubuva aliahirisha shauri hilo hadi Jumatatu ijayo siku ambayo mtuhumiwa huyo atatakiwa kujitetea.

Mbali na Luhwavi, viongozi wengine waliofika mbele ya Baraza hilo jana ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani Ikulu, Alhaji Hamadi Ntungwabona na Diwani wa Viti Maalumu, Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Dorah Kipuyo.

Pamoja na hao, pia yumo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Gabriel Mirumbe na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Endasak-Kateshi, mkoani Manyara.

Akijibu tuhuma zinazomkabili, Ntungwabona alisema alijaza fomu na kuzituma katika Sekretarieti ya Tume ya Maadili lakini anashangaa kwamba hazikufika."Hivi hata kama fomu zangu hazikufika! Kwa nini hamkunijulisha kuhusu hilo wakati Ikulu na ofisi zenu ni jirani?" alihoji. Madai yake hayo yaliwafanya wanasheria wa tume hiyo kumtaka aonyeshe uthibitisho. Hata hivyo, hakuwa nao. Shauri hilo sasa linasubiri uamuzi.

Kwa upande wake, Diwani Kipuyo alisema madiwani wote wa halmashauri hiyo walituma fomu zao kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo."Mkurugenzi Mtendaji ndiye aliyetuletea fomu madiwani wote na tulipozijaza tulizipeleka kwake. Nashangaa kuambiwa kwamba fomu zangu, hazikufika kwenu," alisema.

Baraza hilo leo linatarajiwa kuendelea kusikiliza mashauri ya viongozi kadhaa akiwamo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala.Baada ya kumaliza kusikiliza mashauri hayo, Baraza hilo litatoa mapendekezo yake kwa Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kutoa adhabu.
 
Rais kweli akitaka watu makini wakumsaidia yeye na serikali yake itabidi awe tayari kushugulika hata na mambo madogo madogo kama haya!
Ikilazimu Ikulu ifanye uchunguzi na kufanyia maamuzi uchunguzi huo. Kuna mtu IKULU ameweka sahihi (ya UONGO), asipo tafutwa na kushugulikiwa itakua jambo hatari na la aibu kubwa kwenye OFISI ya JUU na ile.
 
Back
Top Bottom