Msaidizi wa Kikwete matatani

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
na Mwandishi wetu, Dodoma



BARAZA la Maadili limetoa waraka wa kukamatwa kwa msaidizi wa Rais Jakaya Kikwete wa masuala ya siasa, Rajab Luhwavi, kwa kosa la kukaidi wito uliomtaka kuhudhuria vikao vya kutii maagizo ya baraza hilo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza hilo ambalo limeanza vikao vyake jana jijini Dar es Salaam chini ya Jaji mstaafu Damian Lubuva, Luhwavi analalamikiwa na sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kwa kushindwa kujaza fomu za rasilimali na madeni.

Lubuva alisema waraka huo wamemkabidhi mlalamikaji (sekretarieti) ili wamtafute askari atakayewasaidia kukamkata Luhwavi na kumfikisha kwenye baraza hilo linaloendelea na vikao vyake katika Ukumbi wa Karimjee.

“Tumejiridhisha na maelezo ya mlalamikaji kuwa mlalamikiwa alipelekewa wito wa kuitwa kwenye kikao cha leo, lakini hajatokea na hakuna sababu iliyotolewa, tunaagiza akamatwe aletwe mbele kwa siku tutakayoamua,” alisema Lubuva.

Kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995, kifungu cha 24 (4) baraza hilo lina mamlaka ya kutoa waraka wa kukamatwa kwa mtu anayekaidi wito wa kuitwa kwenye vikao vya baraza hilo.

Alisema baraza hilo lililoundwa mwaka jana lina jukumu kubwa la kusikiliza mashauri ya viongozi waliokiuka sheria ya viongozi ya utumishi wa umma namba 13 ya mwaka 1995.

Alibainisha kuwa sheria hiyo kifungu cha 9(1) inaweka bayana kuwa kiongozi wa umma anatakiwa kuorodhesha rasilimali alizonazo na madeni kila mwaka, siku thelathini baada ya kuchaguliwa, mwisho wa kutumikia wadhifa wake.

Alibainisha kuwa kazi ya baraza hilo ni kusikiliza malalamiko ya ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, walalamikiwa na baadaye hutoa mapendekezo kwa Rais Kikwete juu ya hatua za kuwachukulia wakosaji.

Baraza hilo ambalo litaendesha vikao vyake hadi Aprili 15 mwaka huu, jana lilianza kuwahoji viongozi kadhaa akiwemo Mbunge wa Rorya, Lameck Airo.

Mwingine aliyehojiwa ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Pascal Mabiti, ambaye alikiri kutowasilisha fomu hizo kwa mwaka 2009 kwa bahati mbaya na kuliomba baraza hilo limsamehe huku akiahidi kutorudia kosa hilo.

Baraza hilo linatarajia pia kuwahoji viongozi 24 wakiwemo, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, John Mongela, Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam, Profesa Lwekeza Mkandala, Mhasibu Mkuu wa Ikulu, Joseph Sanga na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani za Ikulu, Hammad Ntungwabona.

Naye Ofisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma, Gertrude Cyriacus, alisema kuwa malalamiko waliyowasilisha katika baraza hilo ni ya watumishi wa umma walioshindwa kujaza fomu za mwaka 2007, 2008 na 2009.

Alisema kabla ya kufikisha malalamiko yao kwenye baraza hilo huwaandikia barua wahusika kuwakumbushia wajibu wao na iwapo jitihada hizo zitashindikana ndiyo hufikia hatua ya kupeleka suala hilo katika baraza la maadili. Leo baraza hilo linatarajia kusikiliza utetezi wa watumishi wafuatao; Said Nguba (mwandishi wa habari wa waziri mkuu), Joseph Sanga (Mhasibu Mkuu Ikulu), Rosemary Lyamuya (Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani Dawasco) na Guido Leshabari (Mkaguzi Mkuu Hesabu za Ndani Taasisi ya Chakula na Lishe, Dar es Salaam).
 
Wote ni wazito au wapo karibu na wazito. Lazima wanafanya kusudi wakijua hata wale waliokabidhi hizo report si za kweli. Huu ni wakati kwa tume kufanya marekebisho ya sheria ili riport ihusishe ndugu wa karibu kama vile mume/mke , watoto, baba, mama maana kuna watu wanaiba wanaandikisha mali kwa wanandugu
 
Tatizo ni Wengi ambao hawaorodheshi Mali zao Mfano Wabunge wengi wote hawafuatilii hayo Maadili

Mtu karibu na Rais hawezi kufanya hivyo as well; Katiba mpya iweke suala hilo kabla mtu yoyote hajagombea cheo chochote Serikalini
 
Mbona wengi tu hawaorodheshi, waanze na Kikwete mwenyewe na baraza lake la mawaziri then wabunge wote na viongozi lukuki wa mashirika ya ummma. Sheria zipo lakini serikali ya CCM kwa makusudi kabisa hawataki kufuata sheria ndio sababu tuna matatizo yasiyoisha.
 
Back
Top Bottom