Mke wangu alinifanya niwe Mchawi -1

Mke wangu alinifanya niwe Mchawi - 51..........
ILIPOISHIA...
“Kama haya ninayokuambia unaona nakudanganya, nenda kwa mganga yeyote unayeamini ni makini utaambiwa wewe ndiye uliyemuua baba yako na mwanao.
SASA ENDELEA...


“Waganga wengi tumekuwa tunaangalia tatizo bila kuangalia chanzo chake. Matokea yake tunakimbilia kuua tu. Kama ungekuwa umeonewa kweli, ningekufanyia kazi ambayo hakuna yeyote angeingiza mkono, kila mtu asingekuona. Ningekutengeneza ukawa kiza, watu wangekwenda Mashariki na Magharibi wasingekuona.”
“Mzee wangu nimekusikiliza vizuri na nimekuelewa, utanisaidia vipi?”
“Nitakusaidia kuyaondoa maisha ya mama na mkeo katika ndizi kisha nitakupa dawa ya kumtuliza mkeo. Nina imani ukiondoka hapa utatulia na mpenzi wako najua unampenda, basi tatizo litakuwa limekwisha ila jiepushe kupenda kuua, damu ya watu wengine ni nuksi unaweza kuandamwa na matatizo na kila mganga akawa halioni kwa vile aliyetenda ameisha kufa.”
“Mzee wangu nakuapia kwa Mungu sitarudia tena, nikitoka hapa nakuwa kiumbe kipya.”
“Wapo waganga wanaosifika kwa kuua lakini, mimi nasifika kwa kutibu matatizo kama yako.”
“Nashukuru mzee wangu, nimejifunza kitu, naamini nitakuwa mwalimu mwema kwa wengine.”
“Fanya hivyo ili tupunguze mauaji yasiyo na sababu, kazi ya Mungu tumuachie Mungu, tangu nianze uganga sijawahi kuua na sitaua.”
Baada ya makubaliano mganga alituomba tukapumzike nje ili kusubiri muda wa kufanya kazi yangu.
Tulitoka kwenda kukaa sehemu ambayo tuliletewa maziwa na viazi vya kuchemsha.
Kwa vile tulikuwa hatujala tangu asubuhi tulikishambulia chakula chote. Baada ya kula tulioneshwa sehemu ya kupumzika kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana. Kutokana na uchovu wa safari tulilala mpaka siku ya pili.
****
Baada ya kupatiwa kifungua kinywa cha uji wa maziwa na viazi, tuliitwa kilingeni na kukaribishwa kukaa kwenye ngozi ya chui, mzee Ngugude alichukua ungo na kuuweka mbele yake ambapo ndani ulikuwa na ndizi saba. Mbili zilikuwa zimeoza, mbili zilikuwa zimeiva sana na kuanza kubadilika rangi na kuingia weusi kwa mbali na mbili zilikuwa zimeanza kuiva na moja ilikuwa mbichi kabisa.
“Unaziona hizi ndizi?” aliniuliza huku akinisogezea ungo mbele yangu.
“Ndiyo mzee wangu,” nilijibu huku nikizitumbulia macho.
“Umegundua nini?”
“Sijagundua kitu,” nilisema huku nikitikisa kichwa kusisitiza.
“Basi hii ndiyo familia yako.”
“Familia yangu?” nilishtuka kidogo, japokuwa sikumwelewa.
“Ndiyo.”
“Una maanisha nini kusema hii ndiyo familia yangu?”
“Ulipokwenda kwa mganga alikueleza nini kuhusiana na ndizi?”
“Alisema familia yangu imetegewa uhai wake kwenye ndizi.”
“Basi ndizi zenyewe ndizo hizi, nimefanya kazi kubwa kuzivuta, kwa kweli kazi hii ilikuwa ngumu sana. Nimekesha kwa kazi hii lakini nimefanikiwa. Kabla ya kufanya kitu chochote nilitaka uone ili niifanye hii kazi.”
“Kwa hiyo hapa panakuwaje?”
“Kazi iliyopo ni kutoa sumu katika ndizi ili kuyafanya maisha ya familia yako yaondokane na uchawi uliotegwa kwenye ndizi.”
“Sawa mzee.”
“Unaona ndizi hizi mbili zilizooza?”
“Ndiyo.”
“Basi hizi ndiyo baba yako na mwanao waliofariki, unaziona hizi zilizoiva sana?”
“Ndiyo naziona.”
“Hizi ndiyo mkeo na mama yako, si unaona zilikuwa zikiendelea kuiva.”
“Ndiyo.”
“Basi zingeoza lazima ungepoteza watu wawili kwa mpigo japo ingechukua muda kutokana na kinga uliyopewa mwisho, unaziona hizi zilizoanza kuiva?”
“Ndiyo naziona.”
“Hizi ni za wanao waliobakia, nao walikuwa wakiiva taratibu japo wasingedondoka, lakini wangeoza na kufa kwa mpigo.”
“Mungu wangu!” nilishika kichwa.
“Usishike kichwa hapa nakuonesha ubaya wa kisasi, ungeweza kufanikiwa kuongeza idadi ya vifo vya watu, lakini matokeo yake yalikuwa haya, ungeipoteza familia yako na wewe kuwa chizi.”
“Na hii ndizi mbichi?”
“Hii ndiyo wewe, ukweli walikushindwa na kukubali wameshindwa. Unaiona hii ndizi pembeni?”
“Ndiyo.”
“Unaona nini?”
“Kuna mistari myeusi kama chale.”
“Basi haya ni makombora yaliyotumwa kukuozesha. Lakini mwili wako umekuwa imara, kinga uliyofanyiwa chini ya mti mkuu ndiyo iliyokulinda. Kinga yako ingekuwa ya kawaida ya kuchanjwa tu ungebakia jina.”
“Sasa mzee wangu utanisaidiaje?”
“Nitahamisha sumu kutoka kwenye miili ya familia yako huku ukishuhudia kwa macho yako.”
Alizichukua ndizi mbichi nne na kuziweka kwenye ungo mwingine kisha alichukua dawa ya unga mweupe na kuzimwagia zile ndizi taratibu huku akinuiza maneno anayoyajua. Baada ya muda aliuweka ungo wenye ndizi mbichi pembeni ya ungo wenye ndizi alizosema ndiyo familia yangu.
“Unauona ungo huu?”
“Ndiyo.”
“Una nini?”
“Una ndizi mbichi.”
“Ngapi?”
“Nne.”
“Vizuri,” alisema huku akichukua ndizi zilizooza na kuzitupa pembeni na ndizi mbichi akaziweka kwenye kikapu.
“Sasa nataka hizi ndizi ziwe kama hizi na hizi ziwe kama hizi.”
“Sawa mzee wangu.”
Aliuchukua ungo wenye ndizi mbichi na kuuweka pembeni ya ungo wenye ndizi zilizoiva na kutulia.
“Naomba macho yako yasicheze mbali usijesema nimebadilisha ndizi.”
Nilitumbulia macho kwenye ungo wenye ndizi mbichi, kila dakika nilishindwa kuelewa, ghafla nilijikuta nikichanganyikiwa baada ya kuona ndizi zimebadilika na kuhamia ungo mwingine.
“Umeona nini?” mzee Ngugude aliniuliza.
“Sielewi.”
“Huelewi nini?”
“Naona kama ndizi zimehamia huku.”
“Hapana hazijahama bali sumu nimeitoa na sasa ndizi zilizokuwa kwenye ungo huu zimerudi katika hali ya ubichi.”
“Kwa hiyo.”
“Ubichi huo ni uhai, sasa hivi vifo katika familia yako vitatokea kwa amri ya Mungu na si mkono wa mtu.”
Baada ya kusema vile, alichukua unga mweupe na kunyunyizia, alipomaliza alinieleza niende kuoga maji yaliyokuwa na dawa ili kuondoa mikosi ili nijiandae kwa safari.
Nilifanya kama alivyonielekeza baada ya kumaliza zoezi lile, alinipa unga mweupe akaniambia niubwiye kidogo na mwingine niupulize kama kusafisha njia. Nilifanya kama alivyonielekeza kwa kubwiya unga kidogo, unga ulikuwa na ladha kama ya unga wa ngano. Nilipomaliza tulipewa ruksa ya kurudi nyumbani Tanzania.

Je, Kazala kakubaliana na mganga Ngugude? Ili kuyajua yote tukutane baadae
 
Mke Wangu Alinifanya Niwe Mchawi - 52...

ILIPOISHIA;
Nilifanya kama alivyonielekeza, baada ya kumaliza zoezi lile alinipa unga mweupe na kuniambia nibwie kidogo na mwingine niupulize kama kusafisha njia. Nilifanya kama alivyonielekeza kwa kubwia unga kidogo, unga ulikuwa na ladha kama unga wa ngano. Nilipomaliza tulipewa ruhusa ya kurudi nyumbani Tanzania.
SASA ENDELEA...


Tulisafiri salama mpaka Mtwara na kuagana na mkalimani wangu ambaye nilimlipa kiasi tulichokubaliana, kutokana na kazi kubwa aliyofanya nilimuongeza kiasi kingine kama asante. Kwa vile tulifika jioni sikutaka kulala pale Namoto nilikwenda kulala Mtwara mjini ili siku ya pili niondoke na mabasi ya asubuhi.

Siku ya pili asubuhi nilipanda basi kurudi Dar ili niunganishe mpaka nyumbani siku ileile. Nikiwa ndani ya basi bado nilikuwa na maswali kuhusiana na maneno ya mzee Ngugude, niliyaona kama yanajichanganya. Kuna wakati aliniambia anaweza kuua na kuna wakati alisema hajawahi kuua kwa kweli maneno yale yalinishtua na kuona kama uwezo wa yule mzee ni mdogo tofauti na sifa zake.

Moyoni niliamini kama ningemkuta bi Nyangunda ningeweza kuwakomesha wabaya wangu. Pamoja na kukubaliana na yule mganga niliamini bado nilitakiwa kwenda ndani zaidi. Nilifika Dar jioni na kuunganisha safari, nikafika nyumbani saa tano usiku. Nilipowasili nyumba ilikuwa kimya kuonesha wamelala. Nilipogonga mlango nilifuatwa na mke wa jirani yetu aliyenieleza kitu cha kushtushwa kwamba watoto wangu wako kwake. Niliulizia mama yao yupo wapi, niliambiwa yupo hospitali pamoja na mama yangu wapo chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

"Mungu wangu tatizo nini?"
"Jana waliugua ghafla, kwa kweli hata hatujui ule ni ugonjwa gani."
"Wapo kwenye hali gani?" niliuliza macho yakiwa yamenitoka pima.
"Tumuombe Mungu tu hata sijui niseme nini toka jana hatujafanikiwa kuwaona," alisema kwa sauti ya huzuni.
Nilibakia nimesimama kwa dakika tano nisijue nifanye nini. Bila kujielewa nilijikuta nimekaa chini huku nikiwa na mawazo mengi kuhusiana na hali ile ya kufikia mke na mzazi wangu kurudiwa tena na tatizo.

Wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa huenda mabadiliko ya mzee Ngugude ya ndizi ndiyo yaliyosababisha yote yale. Bila kuongeza neno nilinyanyuka mzimamzima na kukimbilia hospitali.
Nilikwenda moja kwa moja kwenye wadi ya wagonjwa mahututi nikaelezwa kuwa wametolewa na kurudishwa wadi ya kawaida. Nilipotaka kuwaona nilikatazwa na kuelezwa nirudi kesho yake kwa vile muda ulikuwa umekwenda sana hivyo wagonjwa kwa muda ule hawakutakiwa kuamshwa.

Kauli ile sikukubaliana nayo nilijua kuwa ni ya kunifariji lakini mama na mke wangu walikuwa wamefariki. Nilijikuta nikiangua kilio mbele ya daktari wa zamu na wauguzi kitu kilichowafanya wanishangae.

"Sasa unalia nini wakati tumekueleza uje kesho?" daktari wa zamu aliniuliza huku akionesha kunishangaa.
"Nije kesho kufanya nini ikiwa mama na mke wangu wamesha fariki?"
"Jamani mbona haya makubwa! Tumekwambia wapo salama ila sasa hivi wamelala. Kutokana na hali waliyokuja nayo ya nusu wafu tumewaacha kuangalia afya zao kwanza, bila hivyo ungewakuta nyumbani."
"Si kweli, wamekufa ila mnanificha," niliendelea kulia huku nimekaa chini.
"Kaka hakuna aliyekufa hebu ngoja tukawaamshe uwaone ili uridhike japokuwa si sheria kumuamsha mgonjwa aliyetulia kwa ajili ya mtu kumuona tu."

Kauli ile ilinifanya ninyamaze kidogo, baada ya muda niliitwa na kuingia wadini. Sikuamini nilikutana na mama na mke wangu wapo kwenye hali nzuri kabisa.
"Umeamini?" daktari aliniuliza.
"Hapa nimeamini, mara nyingi mtu akiingia ICU huwa hatoki salama."
"Haya baba waache wagonjwa wapumzike njoo kesho."
Niliagana na wagonjwa wangu na kurudi nyumbani nikiwa na maswali mengi kuhusiana hali iliyowatokea. Nilikumbuka maneno niliyoelezwa na mzee Ngugude kuwa kuna hali itatokea na kuwatisha watu, ni ya kuyabadili mauti kurudi katika uhai.


Itaendelea baadae.....
 
Mke Wangu Alinifanya Niwe Mchawi - 53...

ILIPOISHIA;
NILIAGANA na wagonjwa wangu na kurudi nyumbani nikiwa na maswali mengi kuhusiana na hali iliyowatokea. Nilikumbuka maneno niliyoelezwa na mzee Ngugude kuwa kuna hali itatokea na kuwatisha watu lakini ni ya kawaida katika kuyabadili mauti kurudia uhai.
SASA ENDELEA...


MWANZO sikuelewa kutokana na kuchanganyikiwa, niliamini nilichoelezwa ndicho kilichotokea.
Baada ya siku mbili walitoka hospitali wakiwa wazima wa afya. Kitendo kile kilinifanya nibadili mawazo na kuona hakuna haja ya kuendeleza vita ya kisasi. Niliyakumbuka maneno ya marehemu baba kuwa hakuna mwanadamu mwenye uwezo kama Mungu hivyo tulitakiwa kumuabudu yeye.

Alinieleza kwa dini yake kisasi ni haki lakini kusamehe ni bora zaidi. Niliamini ule ulikuwa wakati wa mimi kujikabidhi kwa muumba ili nizaliwe upya. Niliendelea na shughuli zangu kama kawaida huku nikiwa nimejifunza vitu vingi katika maisha yangu.

Niliamini hakuna vita ndogo pia moto hauzimwi na mafuta. Siku zote tulihusiwa kusamehe ili kurudisha amani, pia unapolipa jema kwa baya, ubaya hukosa nafasi lakini ukilipa baya kwa baya vita yake haina mwisho. Nilijifunza kitu kimoja kikubwa kuhusu mwanadamu kuingilia kazi ya Mungu, kuua ni kazi ya Mungu kuingilia kazi hiyo ni kujiingiza kwenye dhambi ya kujitakia. Uwezo wa kuumba na kuua ni wake yeye peke yake. Hata unayemuua ukimwacha lazima atakufa tu kwa nini umuue?

Nina imani wengi mmesoma mkasa wangu tokea mwanzo mpaka leo nilipofikia tamati, napenda kuwaomba wote tusikimbilie kuua au kumroga mtu kwa ajili ya mwanamke kwa vile mke au mume bora hutoka kwa Mungu si kwa mapenzi ya mwanadamu.
Kama mwanamke si muaminifu mkanye kama ukishindwa mwache au mtenge, lakini usiue kwa ajili yake. Japo wengi tunaamini waganga wa asili ni wabaya, lakini kama watatokea waganga kama mzee Ngugude dunia itakuwa salama.

Namalizia kwa waganga wa asili, jina lenu linaweza kuwa baya kwa watu kutokana na kuonekana nyie ndiyo chanzo cha matatizo kati ya mtu na jirani yake hata familia kwa familia.

Mganga siku zote anatibu, anayeua au kumroga mtu huyo ni mchawi ni makosa kumwita mganga. Basi chagueni moja kuwa wachawi au waganga. Namalizia kwa kumuomba Mungu anisamehe kwa yote niliyoyafanya kwa ajili ya mke wangu, kwani niliishia kuwa mchawi kamili nilifikia hatua mbaya ya kuroga na kuua pia nilikuwa radhi hata kula nyama ya mtu kwa ajili ya mke wangu.

Najua hukumu yake kwangu ni kubwa lakini kupitia ukurasa huu najutia kila nilichokifanya. Nakuombeni katika mkasa huu chukueni mazuri na mabaya muyaache kwa vile kusudio la kuutua mzigo mzito uliokaa moyoni mwangu ilikuwa kuhakikisha makosa yangu hayarudiwi na mtu mwingine.

Namalizia kwa kuwashukuru wote mliokuwa nami mwanzo hadi mwisho wa mkasa huu Mungu awabariki, asanteni.

''MWISHO.''
 
Tunasubiri kwani kazala nae matata hakubali mkewe kugegedwa,akirudi home atakuta kuna mtu anamgegeda mkewe,kesi nyingine hio
 
Kila nafsi itaonja mauti... Hata mganga na mchawi wana siku zao za kuishi duniani. Unanikumbusha usemi wa "ukila nyama ya mtu huwezi acha utataka ule tena na tena" Ukianza kwenda Kwa waganga huwezi acha kila siku utaenda tuu. Kwa sisi wakristo Biblia inatuonya kuwa" Ole wake mtu yule amtegemeaye mwanadamu"
 
stori nzuri sna na inafundisha kuwa kisas hakina maana na haitakiwi kuumiza kichwa kwa mwanamke aloshindikana, dawa ni kuachana nae maana hata Ndoa ya Kikristo inaweza kuvunjwa iwapo mmoja wao amekamatwa akizini. Kwaio Bwna Kazala alikuwa na uhalali wa kuvunja ndoa yake na kuoa mwanamke mwingne na bado angekuwa hajavunja shreria ya dini ya kikkristo japo yeye hakuwa mkristo.

Tunasubir stori nyingne Mzizimkavu maana nimeshakuwa Addict wa story zako ila nasubr uimalizie ile ya Wakala wa Shetani pia.
 
Ni kweli hakuna haja ya kuendelea na mwanamke mzinzi ndio maana hata nelson mandela alipiga chini mzigo
 
Nimejeksha nikiisoma hii Simulizi. Ngoma hii haijaisha! Bado mbichi. Inapaswa iendelezwe. Baada ya wagonjwa kupona na Kazala kurudi nyumbani na kuendelea na maisha ya kawaida nini kilifuata? Na ile dawa ya kumfanya mwanamke aache uzinzi ilifanya kazi?
 
Back
Top Bottom