Mkakati wa Uchaguzi wa Wahafidhina ndani ya CHADEMA 2013

CHADEMA Mpya

Member
Jun 5, 2012
84
22
Dhana ya ugaidi ndani ya vyama vya siasa Tanzania


Michael Sinare
Toleo la 321
16 Oct 2013



UGAIDI ni neno au dhana nzito hasa ukilitamka kwa watu ambao wanaelewa athari zake kwa maana ya matokeo yake katika nchi zao husasan jirani zetu wa Kenya. Ugaidi una tabia zinazofanana katika sababu za kuanza kwake, washiriki au waanzilishi wake kwa maana ya rika na namna ya kuumaliza kwake, sambamba na madhara yake.

Ukifuatilia kwa kina sababu za ugaidi duniani kote ni kuupuzwa kwa madai na haki za kundi fulani la watu kwenye jamii, kundi hili linaweza kuwa kubwa au kubwa kiasi ila ni vigumu kwa kundi dogo sana kwa maana ya uungwaji mkono wake kufanya au kuwa magaidi.

Mara nyingi makundi yenye uungwaji mdogo wa jamii yanapotaka kushika hatamu hutumia njia za vita au uasi kwa watawala walioko madarakani tofauti na wanaoitwa magaidi ambao mara zote hujaribu kufuata njia za kidemokrasia na wanapohujumiwa au kuonewa huamua na wao kuuhujumu utawala au uongozi uliopo ili nao usiishi kwa raha na ukadhani watu wote wana amani na furaha kama ambavyo watawala hao wote hujaribu kufanya propaganda kuwaaminisha watu kuwa wako salama na wawapuuze hao wanaowaita magaidi.

Kwa kifupi ugaidi ni harakati za kufurukuta kuonyesha namna kundi fulani linavyokerwa au kutokukubaliana na wenye nguvu au watawala waliopo madarakani hasa wale wenye maono ya kidikteta. Ufurukutaji huu huwa kwa vitendo vinavyoonekana kuwa ni viovu na ni kwa sababu ustaarabu ama demokrasia huwa inakuwa imebakwa na watawala.

Takwimu zinaonyesha kuwa magaidi wengi ni vijana na hata kama kuna wazee wachache basi walianza harakati zao wakiwa vijana au wamepata msukumo kutoka kwa vijana na wanawatumia vijana tena zaidi wale waliotengwa au kuonewa na utawala uliopo au wanaopingana nao.

Magaidi pia wana tabia nyingine inayofanana ambayo ni kupigania maslahi yao kwa kutumia mgongo wa watu. Pamoja na kwamba wanaweza kuwa wanataka kushika serikali au rasilimali lakini hoja zao wataziunganisha kwenye hisia za watu, mateso ya watu na uonevu wanaofanyiwa watu ili kupata uungwaji mkono.

Ndio maana utasikia Waarabu (Al queda au Talban) na Wamarekani, Al Shabaab na Serikali ya Kenya, Wahutu na Watusi hapa kwetu kuna vuguvugu la Uamsho na watawala. Hii ni kwa sababu vijana wengi ni aggressive…hawana uzoefu wa matunda ya uvumilivu na hawana hofu ya kupoteza, ukilinganisha na wazee.

Kwa hiyo ukiwasikiliza magaidi ni kama wanatetea watu wengi dhidi ya watawala waliopo lakini wakati huo huo wana maslahi yao ndani ya harakati zao. Madai mengi ya magaidi yamejikita katika kukiukwa kwa misingi ya kidemokrasia kama vile chaguzi, kukaliwa au kutawaliwa kimabavu na watu wengine lakini zaidi ni pale wanapoamini kuna hali ya kudhulumiwa au kudharauliwa na kuonekana watu duni wasio na uwezo au kuchaguliwa watu wa kuwaongoza (serikali) hivyo hufurukuta na hii ni ili kuonyesha uwezo wao hasa dhidi ya anayejifanya ana mabavu kwa sababu ya kuwa madarakani, uwezo wa kifedha au kivita.

Ugaidi haukuanza leo hata harakati za uhuru nchini kwetu zilionekana kama ugaidi kwa wakoloni, Mandela alionekana gaidi mbele ya makaburu. Harakati hizi zilionekana kuwa ni ugaidi kwa sababu zilihusisha hujuma mbalimbali dhidi ya wakoloni na makaburu kama watawala. Kwa hiyo, kwa Wakoloni ni ugaidi na usaliti lakini kwa akina Mandela, Malcom X, Steven Biko kwao ilikuwa ni harakati na kufurukuta ili watawala wakae na kutekeleza hoja husika.

Kitu cha muhimu kuhusu magaidi ni kwamba hawajawahi kushindwa kwa njia ya vita. Huwa wanapigana kwa miaka na vita yao hurithiwa na kizazi cha wanaokuja hadi madai yao na hoja zao zinapojibiwa na kukubaliwa (compromise).

Ndio maana kuna mazungumzo kati ya Taliban na Serikali ya Afghanstan yanaendelea baada ya vita kushindwa kumaliza harakati, Libya na Iraq waliowekwa madarakani na watu wa magharibi wameshindwa kuongoza nchi kwa utulivu na amani kwa sababu ya waasi ambao wanaitwa magaidi na watu wa magharibi. Hoja za wanaoitwa magaidi hupaswa kujibiwa au kujadiliwa kwenye meza ya mazungumzo na sio vita.

Vita haimalizi madai ya wanaoitwa magaidi ila huharibu mali za watu, kusaliti harakati za watu kujikomboa na mwishowe hupasua nchi ama taasisi katika makundi au matabaka.

Kwa sababu ugaidi ni dhana; basi gaidi anaweza kuwepo au kutokea sehemu yoyote kwa maana ya taasisi, eneo la utawala au kwenye jamii yoyote. Katika historia ya vyama vya siasa hapa nchi kwetu pia kumekuwepo na watu ambao kama utawauliza au ungeuliza watawala wa vyama hivyo kwa wakati huo wangeweza kuwaita wenzao walioonekana kama waasi au wasaliti kwa kipindi hicho magaidi.

Ugaidi ndani ya vyama vya siasa

Ugaidi umetokea katika vyama vyote vya siasa hapa nchini, vyama ambavyo vimewahi kupata nguvu na huenda ukaendelea kutokea kwa siku za usoni. Msingi wa ugaidi katika vyama ni ule ule ambao umejikita katika dhuluma, dharau na kuviziana kunakofanywa na waliopo madarakani dhidi ya wapinzani wao wa ndani.

Ugaidi NCCR-Mageuzi

Ndani ya NCCR-Mageuzi kulitokea kundi la Mabere Marando (Katibu Mkuu) na Agustino Lytonga Mrema (Mwenyekiti). Akina Marando walikuwa hawaridhishwi na uongozi wa Mrema na kama ungemuuliza Mrema wakati huo, pengine angekuambia akina Marando, Selasini, Anthony Komu, Mwasi na wengineo ni magaidi.

Na kama ungefuatilia nyendo za akina Marando katika harakati zao hizo ungegundua walikuwa wakifanya vitendo vingi vya ‘kigaidi’ dhidi ya utawala wa Mrema. Baada ya Mrema kuchagua njia ya vita kama suluhisho aliishia kuivunja NCCR-Mageuzi na kujeruhi mioyo na nafsi za Watanzania wengi wapenda mabadiliko.

Mrema kama Mmarekani akapeleka vita yake dhidi ya ugaidi unaompinga mpaka Tanzania Labor Party (TLP) nako akaisambaratisha kwani hoja za wanaoitwa magaidi huwa hazifi hata kama magaidi hao watakufa, wengine watarithi hoja hizo. Mrema amebaki peke yake bila wakosoaji na bila umaarufu wake. Alidhani magaidi wanataka kummaliza kisiasa kumbe hoja zao mara nyingi kama zikitekelezwa huwa zinamwongezea umaarufu aliyeko madarakani.

Ugaidi UDP

Chama cha UDP nacho kilishapitia vita dhidi ya ‘ugaidi’ Mzee John Cheyo alitaka kupinduliwa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chama. Labda ungemuuliza Mzee Cheyo wakati ule angekuambia akina Benson Kigaila, Erasto Tumbo, Amani Jidulamabambasi Nzugile, Makanga na wengineo kuwa ni wasaliti, wahuni na magaidi lakini ukweli unabaki pale pale, walikuwa na hoja za msingi kwa manufaa yao binafsi lakini wakiyaunganisha na maslahi ya wengi ndani ya chama chao.

Ni ukweli usiopingika pia kuwa wakati wa harakati hizi za kumpindua Mzee Cheyo vijana hao walifanya mambo mengi yenye mwelekeo na harufu ya usaliti kwa UDP, kama namna ya wao kufurukuta dhidi ya utawala wa Mzee Cheyo.

Mzee Cheyo alipochagua vita kama njia ya kupambana na ugaidi huo matokeo yake amebaki na UDP yake na magaidi wamekimbilia nchi jirani za CHADEMA, CUF na CCM kuendeleza mapambano yao aidha ya walichokiamini au wameamua kuwa wanafiki wa nafsi zao.

Ugaidi ndani ya CUF

Ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) nako matukio ya dhana ya usaliti na ugaidi yametokea kiasi cha kuwafanya watu kama akina Tambwe Hiza, Wilfred Lwakatare, Profesa Abdallah Safari na wengineo kuhama chama hicho baada ya kuzidiwa katika vita dhidi ya utawala wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Naamini ungemuuliza Profesa Lipumba wakati ule angekuambia kuwa wapinzani wake ni wasaliti na magaidi ndani ya chama. Profesa Lipumba naye hakuchagua meza ya mazungumzo kujadili hoja za magaidi wa ‘nchi’ yake ya CUF, matokeo yake akafuata msimamo wa Kagame wa kutaka kulipa kisasi cha matokeo au madhara ya magaidi ambayo ni pamoja na CUF kudumaa kisiasa.

Ugaidi ndani ya CCM

Marehemu Horice Kolimba aliposimama na kusema CCM imepoteza dira naye alionekana gaidi ndani ya CCM na kutakiwa kujieleza na ikawa ndio mwisho wake. Mwaka 2009 aliibuka Samuel Sitta na kijana wake, Nape Nnauye na wengineo na kuanzisha ugaidi ndani ya CCM dhidi ya chama hicho kiasi cha kudaiwa kuanzisha chama wakati akiwa bado ni mwanaCCM.

Tofauti ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete na wenyeviti wenzake wa vyama vingine, hakuchagua vita kama njia ya kutatua ugaidi ule bali alitafuta namna kuuzima kwa mwafaka ndani ya chama chake.

Pamoja na kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni maslahi binafsi ya Sitta na Nape kutaka madaraka, lakini walijionyesha ni wapambanaji wa ufisadi ndani ya CCM. Kikwete akajua hawa shida yao ni madaraka na survival ya kisiasa, akawatunuku vyeo.

Na wale walioitwa mafisadi ukiacha Rostam aliyejiuzulu mwenyewe, siamini kama Kikwete angechagua kundi katika vita ile, CCM ingekuwepo hadi leo. Mafisadi na magaidi wako nyumba moja na wanafanya kazi pamoja na kama itatokea siku wakagombana na kuchagua vita baina yao kama njia ya kumaliza ugaidi wa akina Nape au ufisadi wa akina Lowassa, basi utakuwa ndio mwisho wa CCM kama ilivyokuwa kwa KANU.

Kikwete angeweza kuwaita akina Nape magaidi na kupambana nao kama Mwenyekiti wa chama na isitoshe walikuwa wakipambana na Kikwete kwa namna moja au nyingine kwa sababu walimhusisha na hao waliodai ni mafisadi wakisema ni marafiki zake.

Nasisitiza ugaidi huja baada ya demokrasia kupuuzwa na dhuluma na dharau kushika hatamu katika nchi na taasisi mbalimbali. Magaidi nao wana mapenzi mema kwa maslahi ya kundi fulani ndani ya jamii, tena kundi kubwa tu kwa hiyo mwafaka ni kitu bora zaidi kuliko vita. Pia ungekutana na viongozi wa CCM au Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karatu wa mwaka 1995, ukamuuliza anamzungumziaje Dk. Slaa? Wangekuambia naye ni msaliti na gaidi ndani ya chama. Na walipompuuza aliamua kuhamia CHADEMA ukawa ndio mwisho na kifo cha CCM, wilayani Karatu hadi leo.

Ugaidi ndani ya CHADEMA

Hapa nitazungumza kwa kirefu kwa lengo la kushauri utawala dhalimu wa CHADEMA ambao uko madarakani kwa takribani miaka 10 sasa, chini ya Mwenyekiti Freeman Mbowe, mwenyewe anajiita kamanda wa anga.

Nampongeza Mbowe kwani kwa muda wa miaka kama minane hivi alijitahidi kuzima na kuzungumza na magaidi wake wa ndani, ambao walijaribu kumpinga kwa hila na kwa hoja. Mbowe amekuwa akitumia mbinu za Clinton kwa muda mrefu za intelijensia zaidi kuliko vita kuwadhibiti magaidi ndani ya CHADEMA.

Inasemekana Mbowe pia alitengeneza magaidi wake (mashushu) na kuwapenyeza kwenye ngome za wapinzani wake wa ndani ili kuwadhibiti na alipofanikiwa wengi walihama chama kama njia ya kukwepa aibu ya kushindwa kwa hila zao.

Kuna watu kama akina Aman Kaborou, Shaibu Akwilombe, na Marehemu Chacha Wangwe. Wote hawa kwa nyakati zao wameshawahi kuonekana na hata wao wenyewe kufanya vitendo vya ‘kigaidi’ dhidi ya Mbowe na utawala wake.

Wote walihama Chama na wengine wamekwishaitwa mbele ya haki. Baada ya viongozi hao liliibuka kundi jingine lililopokea hoja zao zile zile ambapo ndani yake kulikuwa na akina David Kafulila, Habibu Mchange, Mtela Mwampamba, Juliana Shonza, Eddo Makata, Kasambala, Kisandu na wengineo.

Wote hawa kwa pamoja wametajwa na gaidi mwingine aitwaye Ben Saanane kuwa walikuwa ni vijana wa Zitto Kabwe, kama gaidi wao mkuu mfano wa Osama vile.

Vijana hao nao wamekwishahama Chama kama njia ya kukubali kushindwa vita na utawala wa Freeman Mbowe na Katibu wake Mkuu, Dk. Wilbrod Slaa, ila Zitto bado yuko ndani ya CHADEMA.

Ninataka tujiulize maswali mawili ya msingi hapa nayo ni –Mosi, utawala wa Mbowe umekuwa ukitengeneza na kuzalisha magaidi ndani ya Chama? Pili, je Zitto ni msaliti na gaidi ndani ya chama? Je, alitengenezwa kuwa hivyo na utawala wa Mbowe au alichagua mwenyewe kuwa gaidi (Tukumbuke maandiko ya Ben Saanane dhidi ya Zitto Kabwe kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii mwishoni mwa mwaka jana).

Tangu kuhama kwa akina Aman Kaborou aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chaderma na mbunge huko Kigoma na kusimamishwa kwa Chacha Wangwe katika nafasi yake ya makamu mwenyekiti, kuliibuka tuhuma mbalimbali dhidi ya Mbowe kuwa ni mbabe, ana ubaguzi, anawatenga viongozi wenzake katika utendaji wa kazi za chama na kuwafanya viongozi wenzake kuwa viongozi alama tu na sio viongozi watendaji.

Tuhuma hizo ziliendelea tena katika awamu hii ya sasa ya Mbowe ambapo makamu wake ni Mzee Said Arfi ambaye miezi michache iliyopita alitishia kujiuzulu nafasi yake ya makamu kwa madai ya kuhujumiwa na uongozi wa Mbowe na kufanywa makamu mwenyekiti asiyejua nini kinaendelea ndani ya Chama.

Inasemekana kuwa Mbowe akipata tatizo leo itamchukua makamu wake Mzee Arfi zaidi ya mwaka kujua mipango mbalimbali inayotekelezwa na chama hasa ile inayoitwa ya kiusalama au siri. Inasemekana Mbowe huwa hampi mrejesho makamu wake kwa mambo mbalimbali yanayoendelea au kutekelezwa na chama chake.

Kama ni kweli, basi hii ndio sababu kubwa inayozalisha magaidi ndani ya vyama vya siasa hasa ikizingatiwa kuwa chama si mali ya mtu au kikundi fulani bali ni mali ya wanachama wote na tena wote wana haki sawa ya kupata taarifa na kushiriki katika ujenzi wa vyama vyao.

Je, Zitto ni msaliti?

Mnamo mwaka 2009 kulikuwa na uchaguzi wa ndani katika CHADEMA. Katika uchaguzi huo walijitokeza watu mbalimbali kugombea nafasi mbalimbali. Desturi ya uchaguzi wowote duniani huwa unakuwa na pande mbili kuu zinazokinzana kimtazamo. Pande hizo huwa zinajitahidi kushinda katika kila ngazi na nafasi inayogombewa katika uchaguzi huo.

Ndani ya CHADEMA kulikuwa na makundi pia. Upande wa Mbowe ambao ulitaka aendelee kuwa mwenyekiti na upande huu ulikuwa na hoja nzito na za msingi kuwa Mbowe amekiimarisha sana chama katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi wake hivyo ni bora apewe kipindi cha pili ili aendeleze na kama sio kukamilisha kazi nzuri aliyokuwa ameifanya na isitoshe alikuwa bado ni kijana mwenye nguvu, ametumikia kipindi kimoja tu na katiba inamruhusu kuendelea hivyo apewe kipindi cha pili.

Kundi hili lililojulikana kama kundi la Mbowe lilikuwa na safu yake ya uongozi ambapo walitamani pia nafasi ya makamu mwenyekiti Bara ichukuliwe na Shambwee Shitambala, ambaye wakati huo alikuwa anavuma sana baada ya kugombea ubunge Mbeya Vijijini lakini alienguliwa kwa uzembe wa kuapa kwa kamishna wa viapo asiyestahili japokuwa alikuwa ni Mwanasheria.

Nafasi ya makamu mwenyekiti Zanzibar ichukuliwe na Said Mzee kutoka Unguja aliyekuwa anamaliza muda wake japo watu Wazanzibar walikuwa hawamtaki kwa madai kuwa hakusaidia chama kukua katika visiwa hivyo kwa hiyo wengi hawakumtaka arejee uongozini.

Nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake walitamani ichukuliwe na Chiku Abwao au Rachel Mashishanga. Nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Vijana walimpendekeza John Heche ambaye alikuwa diwani wa Tarime na aliyefanikiwa kushinda udiwani akiwa bado ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu, jijini Mwanza

Nafasi ya Mwenyekiti wa Baraza la Wazee timu hii ilimpendekeza Mzee Victor Kimesera (Muasisi na Katibu Mkuu wa kwanza wa CHADEMA ambaye wakati huo pia alikuwa mkurugenzi wa wazee) ndio awe Mwenyekiti wa Wazee Taifa.

Ikumbukwe kuwa mabaraza haya ndio kwanza yalikuwa yameanzishwa kwa hiyo uchaguzi huo ulikuwa ni wa kwanza kabisa. Kadhalika katika nafasi za wajumbe wa Kamati Kuu pia kulikuwa na waliopendekezwa.

Kambi ya Zitto nayo ilikuwa na mapendekezo yafuatayo, Zitto awe Mwenyekiti kwa sababu ni kijana na chama kinachoungwa mkono na vijana wengi kwa hiyo vijana watapenda kuongozwa na kijana mwenzao na kujiunga na chama kinachoongozwa na vijana.

Pamoja na hoja hii kusikika vizuri kama ambavyo magaidi wamekuwa wakiweka hoja inayoonyesha kuungwa mkono na kundi kubwa la wananchi lakini nyuma yake kulikuwa na hoja ya kigaidi ya kutaka kumpindua Mwenyekiti Mbowe kwa madai kuwa alikuwa anawaonea baadhi ya watendaji hasa waliokuwa wanaonekana ama ni marafiki wa Zitto au wanatofautiana naye kimawazo.

Kipindi hicho Zitto naye alipata umaarufu kutokana na hoja ya Buzwagi lakini bado umri wake ulikuwa mdogo, hivyo alikuwa mdogo kiupeo na kiuzoefu na pia alikuwa na mihemko (aggressive) mingi. Ndani ya CHADEMA watu wanadai kuwa chanzo cha Zitto kugombea ni ushawishi au shinikizo alilopewa na Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa Chama hicho, Msafiri Mtemelwa.

Msafiri Mtemelwa katika historia ya siasa za Tanzania alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha NCCR-Mageuzi wakati huo kikiongozwa na Mrema na ndio kilikuwa Chama Kikuu cha Upinzani hapa nchini. Wakati Mtemelwa akiwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Mbowe alikuwa ni Mwenyekiti wa vijana wa CHADEMA wakati huo kikiwa ni chama kidogo.

Kujua hali ilivyokuwa wakati huo, ni vema kupima kwa kuangalia hali ya sasa kwa Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA wakati huu yaani John Heche na Mwenyekiti wa vijana wa UDP kwa mfano.

Inadaiwa kuwa wakati wakiwa katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Busanda, Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe alionyesha dharau kwa Mtemelwa kwa kuteua mtu mwingine kuwa kiongozi wa kampeni zile kwa maelezo kuwa Mtemelwa hana uwezo wa kuongoza kampeni zile.

Uasi dhidi ya Mbowe ukaanzia pale ambapo Mtemelwa atakuwa alikumbuka enzi zake akiwa NCCR-Mageuzi alivyokuwa akimuona Mbowe kuwa naye hana uwezo. Mtemelwa akaamua kuwa gaidi na kuanza mkakati wa kumng’oa Mbowe kwenye Uenyekiti.

Mbowe kwa kulijua hilo akaanza kuwadhibiti vijana wote waliokuwa wanaonekana kuungana na hoja ya Mtemelwa ambapo wahanga wa awali wakawa ni akina David Kafulila, Danda Juju na wengineo ambao mwishowe walihamia NCCR-Mageuzi baada ya kushindwa vita (magaidi wakakimbilia nchi jirani ama kuendeleza vita, kujipanga upya au kukubali kushindwa).

Msafiri Mtemelwa kama gaidi mpya ndani ya CHADEMA wakati huo alibeba hoja zote za magaidi waliomtangulia akina Wangwe, Kaborou na kwa kuwa yeye umaarufu wake haukuwa juu sana akatafuta mtu wa kumtanguliza mbele ili apambane na Mbowe.

Aidha kwa kujua, au ujana wakati huo na au kwa mihemuko, kiu ya madaraka au dhamira nzuri kwa chama Zitto akabeba msalaba huo hasa baada ya kuona utawala wa Mbowe unawadhibiti marafiki zake waishi kwa hofu.

Zitto akajitoa mhanga na inasemekana hata fomu ya kugombea wakati ule Zitto alijaziwa na Msafiri Mtemelwa na picha ilichukuliwa katika moja ya waandishi wa magazeti wakati huo na kubandikwa kwenye fomu.

Inasemekana pia kuwa Zitto alisaini fomu ya kugombea akiwa uwanja wa ndege kuelekea Ujerumani siku ya mwisho ya kurejesha fomu saa nane mchana huku wapambe wakiwa tayari wameshawatangazia Watanzania siku nyingi kupitia magazeti kuwa Zitto atagombea uenyekiti na tayari walishapanga safu yao ya uongozi na pia walishawasiliana na wajumbe wote wa mkutano mkuu na kumchafua sana Mbowe na kumjenga Zitto.

Kwa mujibu wa maandiko yake mbalimbali, Zitto, akiwa na umri wa miaka 16 tu, na mama yake walijiunga na CHADEMA. Kambi ya Zitto nayo ilipanga safu yake kama ifuatavyo. Makamu Mwenyekiti Bara alipendekezwa Arfi. Makamu Mwenyekiti Zanzibar alipendekezwa kijana Said Issa Mohamed kutoka Pemba.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana alipendekezwa David Kafulila ambaye tayari alikuwa ameshaanza kupata misukosuko ya kisiasa kutoka kwa viongozi ama kwa sababu ya tabia yake mbaya au kwa sababu za kiuchaguzi na kisiasa.

Yeye alitaka Uenyekiti wa Vijana na pia alikuwa na ndoto za kugombea ubunge Kigoma Kusini na tayari alikuwa ameshafanya kazi kubwa sana ya ujenzi wa CHADEMA wakati akifanya kazi kwa kujitolea na baadaye Ofisa Habari wa chama hicho. Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake alipendekezwa Mama Leticia Musore ambaye alikuwa Mama kutoka Tarime. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee alipendekezwa Mzee Nyangaki Shilungushela (ambaye ni miongoni wa waasisi pia) kutokea Mkoani Shinyanga.

Matokeo ya Uchaguzi huo wa 2009

Zitto alijitoa kwenye uchaguzi huo inasemekana ni baada ya kushauriwa na Wazee ili kuinusuru CHADEMA na mpasuko wa ndani. Pia kuna watu wanadai ilionekana kama Zitto angeshinda uenyekeiti na Kafulila uenyekiti wa vijana kungeweza kuibuka hoja ya CHADEMA kuwa Chama cha Kigoma badala ya Chama cha Kaskazini kama inavyosemwa toka wakati huo.

Pia zipo hoja kuwa Zitto alienguliwa kwa nguvu baada ya kukataa ushauri wa Wazee kwa madai kuwa Mbowe ameshamuumiza sana yeye na marafiki zake kwa hiyo kufanya hivyo ni kusaliti na kuhatarisha hatma yake kisiasa na washirika wake. Kwa hiyo Zitto akawahamasisha watu wake wapige kura za Hapana kwa Mbowe ili uchaguzi urudiwe.

Kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA iwapo mgombea ni mmoja basi lazima apate zaidi ya nusu ya kura za NDIO. Inasemekana pia kuwa watu hao walifanya kama walivyoagizwa –na Mbowe kwa kujua hila hiyo aliwaweka vijana wake (akina Mnyika, Kigaila, Sabula na wengineo) kuwa wasimamizi wa kura ambapo walimtangaza kuwa mshindi japo haikuwa hivyo.

Hoja hii inapata sana nguvu kwa sababu katika Uchaguzi wa Mabaraza ya CHADEMA pamoja na Makamu wote wa Bara na Visiwani walioshinda ni wale wa timu ya Zitto isipokuwa Baraza la Vijana ambalo uchaguzi ulivurugwa na mambo hayo yaliandikwa sana kwenye mitandao na Zitto akilalamika Kafulila kudhulimiwa ushindi wake.

Hoja nyingine inajengwa hapa kuwa washauri wa Mbowe walijua kuwa nguvu ya CHADEMA ni vijana kwa hiyo ingemuwia vigumu Mbowe kuongoza Chama kama Mwenyekiti wa vijana angetokea upande wa pili yaani Kafulila.

Kafulila baada ya matukio hayo aliamua kuhamia NCCR-Mageuzi yeye pamoja na marafiki zake wa timu yake akina Juju, Moses Machali na Felix Mkosamali na wengineo kwa hofu kuwa asingeteuliwa kuwa mgombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini kwa sababu mgombea aliyekuwa amegombea mwaka 2005 alikuwa ni mdhamini wa CHADEMA, Muhsin Hassanali na alikuwa ameonyesha nia ya kugombea tena kwa awamu nyingine.

Walishinda ubunge baada ya kuonekana wamedhulumiwa na CHADEMA na Zitto aliamua kuwaunga mkono kama ilivyosomeka kwenye vyombo mbalimbali vya habari wakati ule; kwa kuwapa magari ya kampeni na misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatosa wagombea wa CHADEMA katika maeneo hayo.

Nilisoma mahali miaka hiyo Zitto akituhumiwa kumuahidi Kafulila kuwa atakuwa Mbunge kabla ya Mnyika ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi Mambo ya Nje na Vijana kabla ya Mabaraza kuanzishwa na kijana mtiifu kwa Mbowe.

Mama Leticia alishinda uenyekiti wa BAWACHA na akapigana kwenye kampeni za uchaguzi mkuu huko Tarime akimsaidia Mwita Waitara lakini hakupewa Ubunge wa Viti Maalumu japo kuwa CHADEMA ilikuwa inatumia sera ya siyefanya kazi na asile kama njia ya kuwateua wabunge hao wa viti maalumu.

Hasira ikampanda akahamia NCCR-Mageuzi baada ya Uchaguzi Mkuu ni kama vile alisita kuhama na akina Kafulila akisikilizia kama atapewa viti maalumu au la. Wapinzani wake yaani Abwao na Mashishanga walipewa ubunge wa viti maalumu.

Baada ya Uchaguzi ili kuzuia mpasuko Mbowe alilazimika kuacha safu yake ile ile ya Katibu Mkuu na manaibu kama ilivyokuwa kabla ya uchaguzi, ambapo alilazimika kumteua Zitto. Viongozi wengine walioshinda nafasi za umakamu pamoja na Zitto waliendelea kubaki kama alama tu kwenye Chama chao wakishirikishwa mambo machache tu kwenye shughuli za chama kwa hofu ya mapinduzi.

Vita hii na majeraha haya yaliendelea mpaka katika Uchaguzi Mkuu wa wabunge na madiwani ambapo kuna maeneo kila kambi ilikuwa na wagombea wake ambapo ilifika mahali wakawa wanafanyiana hujuma wenyewe kwa wenyewe.

Kuna wagombea walikutwa na makosa ya rushwa na uzembe wa kujaza fomu zao walipohojiwa wakadai nimeambiwa na Zitto au Zitto ndie chanzo wengine wakadai hapa Mbowe ndie sababu ya makosa yangu. Haya, yatakuja kuibuka siku si nyingi maana msimu wa uchaguzi ndani ya CHADEMA umekaribia.

Uchaguzi wa Baraza la Vijana ulikuja kurudiwa baadae ambapo ndipo walipotokea akina Habibu Mchange, Mtela Mwampamba, Juliana Shonza kama vijana wanaomuunga mkono Zitto na waliobeba hoja zote za Kafulila na (ambao ni Magaidi au Wasaliti kwa dhana ya upande wa pili) waliowatangulia kama akina Chacha Wangwe, Zitto mwenyewe na wengineo.

Inasemekana kuwa pamoja na uongozi wa Mbowe kuendelea kumuunga Mkono kijana wao John Heche ambaye katika uchaguzi wa awali aliishia kumtukana Zitto matusi ya nguoni pamoja na kwamba ni Naibu Katibu Mkuu kwa madai kuwa alimwibia kura zake.

Zitto, Halima Mdee, na Charles Mwera aliyehamia CUF ndio walikuwa wasimamizi wa uchaguzi ule na alitoa matusi yale pasipo kuchukuliwa hatua yoyote. Pia, walimchomeka kijana Ben Saanane (kama ndio jina lake halisi) awe mgombea aliyejifanya anampinga Heche.

Ben Saanane alijipenyeza kwenye kambi ya akina Mchange kwa kujifanya na yeye yuko kinyume na Heche na kufanikiwa kujua mipango yao yote akijifanya mwenzao. Inasemekana Ben Saanane alipewa vifaa mbalimbali vya kisasa vya kurokodia kama vile radio, saa na kalamu ili kurekodi mienendo ya akina Mchange (Rejea maandiko ya akina Mchange, Mwampamba n.k kwenye mitandao).

Mchange alienguliwa katika Uchaguzi huo kwa madai ya kutoa rushwa na kufanya kampeni kabla ya wakati. Ilichapishwa orodha ya mawasiliano yake pamoja na akauti yake ya M-Pesa na akaenguliwa. Jambo hili lilileta vurumai kubwa kwenye vikao vya CHADEMA huku wengine wakidai zichapishwe orodha na akaunti za wagombea wote lakini jambo hilo lilipingwa vikali na upande wa pili.

Tatizo la Zitto na wenzake kila ulipoinuka uonevu ulioelekea kuvunja CHADEMA inasemekana huwa wanajishusha na kubeba lawama kwa hofu ya kuvunja Chama.

Uchaguzi ule ulipita ambapo timu ya Zitto ilifanikiwa kumpata Shonza kama Makamu Bara na Makamu wa BAVICHA Zanzibar kwasababu mgombea wao wa uenyekiti alienguliwa tayari. Kwa ujanja mkubwa, ili kuhalalisha vitendo vyao, baadae wakamuengua Saanane na Mwampamba ili kumzuia Mtela pia ambae wajumbe wa kambi ya Zitto walishaamua kumpa kura zote baada ya Mchange kuenguliwa.

Saanane alipewa coverage kubwa kwenye vyombo vya habari japokuwa hajui hata tawi lake la chama liko wapi ili kupunguza kura za Mchange na kambi ya Zitto na walipofanikiwa kumuengua Mchange mapema kwa kosa la rushwa kazi ya Saanane kwa maana ya uchaguzi ikawa imeisha kwa wakati ule ila akapewa kazi nyingine ya kumchafua Zitto ili kumdhibiti kwenye uchaguzi ujao ndani ya CHADEMA.

Katika BAVICHA pia mchezo ukawa ni ule ule. Upande wa Zitto ukaanza kutengwa (kumbukeni malalamiko ya Shonza kuhusu sms za Dk. Slaa kwamba hatakaa afanye kazi katika utawala wa Mbowe ) kama ambavyo hata makao makuu ya CHADEMA mambo yaliendelea na yanaendelea hadi sasa.

Kwa matukio hayo unaweza kuona kuwa uongozi wa Mbowe pamoja na kufanikiwa kuikuza CHADEMA bado umeendelea kutengeneza magaidi wa ndani ya chama na sasa zipo taarifa kuwa washauri wote wa Mbowe ni wale waliokuwa waasi, wasaliti na magaidi au wanamapinduzi wa vyama nilivyovitaja hapo juu ambao wote kwa nyakati zao walikuwa wakipigania madaraka kwenye vyama vyao wakakosa na kuamua kuhamia CHADEMA.

Viongozi hawa walioonekana magaidi kwenye vyama vyao yaani akina Dk.Slaa (CCM), Benson Kigaila (UDP), Wilfred Lwakatare (CUF), Erasto Tumbo (UDP) na wengineo kwa maana ya mtazamo wa viongozi wao wakati ule, ndio washauri wakubwa wa Mbowe kwa sasa ambaye hajawahi kuonja wala kushiriki ladha ya mapinduzi katika chama chake au chama kingine chochote kwani yeye amekulia CHADEMA kwa amani.

Wanamapinduzi wana kauli yao mashuhuri sana duniani kuwa “Wanamapinduzi hawastaafu”. Ndivyo alivyokuwa akisema Gadafi, Hugo Chavez na ndivyo anavyosema Museveni, Kagame, Mugabe na wengineo. Msingi wa kauli hii ni hofu ya kulipiziwa uovu wao waliowafanyia wapinzani wao na hofu ya kudhalilishwa kwasababu tu ya misingi ya chuki, visasi na fitina walizopandikiza kwa waliowapindua dhidi ya raia wao.

Ni dhahiri kabisa Dk. Slaa, Kigaila, Lwakatare wanao uwezo mkubwa sana wa kumpindua kiongozi kwa fitina kubwa na hata kujitahidi kuubakiza utawala unaowapa usalama na amani dhidi ya fitina kwa gharama yoyote ile.

Hii ni kwasababu wana uzoefu na mapinduzi katika maisha yao ya siasa. Kuwashinda watu kama hawa (wanamapinduzi) falsafa ni ile ile tu Mahakama Kubwa kuliko zote ni Wananchi kwa kusaidiwa na Nguvu ya Ukweli.

Wanamapinduzi duniani kote ni waoga na hawapendi umma wanaouongoza ujue ukweli kuhusu wao. (Wana CHADEMA kazi kwenu kulinda chama chenu).

Hivyo basi upo uwezekano mkubwa sana na umeshaanza kusemwasemwa kwenye mitandao na vyombo mbalimbali vya habari wa wanamapinduzi hawa kutaka kubaki madarakani (na kwa tabia yao huwa wanamshikilia kiongozi yule aliyepo madarakani kwa nguvu zao zote ili abaki kuwalinda). Hili tunaliona kwa Mugabe, Kagame na tumeliona kwa Kibaki na wengineo. Watakuwa wameshaanza kumshawishi Mbowe agombee tena kwa msingi ule ule wa hofu ya kulipiziwa madhalimu na fitina zao walizofanyia wengine.

Na hata wale ambao hajafanya fitina tayari wanajikuta tu wameshazoea kuishi kimapinduzi pinduzi tu kwa hiyo dalili zikionekana tu wanatafuta upande.

Pamoja na tabia hii mbaya ya kuwatenga wapinzani wao katika uongozi, watawala wanaojifanya wanapambana na magaidi ni wazuri wa propaganda hasa za fitina na kujenga mitandao ili kujaza nafasi nafasi iliyo wazi mioyoni mwao inayotokana na hofu.

Duniani kote wako, walikuwa na wataendelea kuwa hivyo. Pia kazi yao ni kuvizia wapinzani wao wafanye makosa au kuwatengenezea makosa ili wapate mada za kufanyia propaganda. Mara nyingi hutafuta faili na kuvizia mapato, mikutano, kazi na marafiki wa mpinzani wao kuzalisha propaganda hasa wakati wa karibia na chaguzi. Inasemekana haya yanaendelea ndani ya CHADEMA .

Hitimisho

Nilisoma kwenye mitandao kuwa Saanane baada ya kazi ile nzuri ameajiriwa Makao Mkuu ya CHADEMA na sasa ni mtumishi wa makao makuu.

Ushauri wangu kwa Mbowe. Kila mtu anathamini na anapongeza juhudi zake za kuifanya CHADEMA kuwa taasisi na amefanikiwa sana hata mimi nampongeza sana.

Ila naamini kwa kushauriwa na wanamapinduzi waliomzunguka (magaidi wa siasa) huenda wameanza kumshawishi kuwa mroho wa madaraka kwasababu tu ya hofu walizo nazo za kulipiziwa fitina zao na ubaya wao kwa wengine.

Mbowe hapo ulipofika na kufikisha Chama chako cha CHADEMA kwa uongozi wako makini na pia kama Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mpaka sasa karibia utawawezesha Watanzania kupata Katiba Mpya ya Nguvu ya Umma tena kwa kuwaunganisha Wapinzani na Makundi mbalimbali ya jamii yaliyokuwa yametengwa na mchakato wa Katiba mimi nafikiri panatosha sana kwa wewe kuingia kwenye vitabu vya historia ya nchi hii.

Mimi naamini ukigombea tena hata kama utashinda kwa haki au kwa hila utapoteza thamani ya historia yako kwa nchi hii. Ilimchukua Nyerere miaka 23 kuligundua hili hadi leo tunamtaja kwa heshima wenzake akina Mugabe wanamaliza kwa kushinikizwa.

Umefanya makubwa, acha historia ikulinde na kukutukuza mpe mtu kijiti hicho. Na mimi nafikiri mtu pekee anayejua misingi ya kuanzishwa kwa CHADEMA na ameiishi kwa muda mrefu hata kama ana mapungufu ya kibinadamu ni Zitto Kabwe labda atokee mwingine ila mpaka sasa sijaona mwingine ndani ya CHADEMA.

Zitto akizungukwa na washauri wazuri anaweza kuivusha CHADEMA na kuingiza katika enzi nyingine. Washauri hawa wawe na kazi ya kudhibiti kauli zake tu na uzuri wa Zitto ni msikivu na ndio maana amemudu kuhudumu katika kamati kubwa za Bunge letu na hata kupokea ushauri mbalimbali wa vikao vya Chama chake.

Kwa mtazamo wangu kauli nyingi za Zitto zilijikita katika dhana ya ama tukose wote, au kukata tama dhidi ya ukandamizwaji na frustrations za kutengenezewa au kusababishiwa hasa na Wanachama, Viongozi na wabunge wenzake ndani ya chama wanaousaka umaarufu kama wake au hata kuota kumzidi huku wakisahau kuwa kabla hawajawa wabunge walikuwa wakitaka Ubunge ili wawe kama Zitto na walipoupata wanamuona mnoko wao ndio wanajua sana.

Wabunge wanaotajwa kumuwazia Zitto mawazo ya aina hii ukiangalia historia zao nao ni walewale magaidi toka vyama vilivyokuwa na nguvu miaka ya nyuma, wamekulia kwenye mapinduzi na vita vya ndani vya kisiasa kwenye vyama vyao.

Mh. Mbowe nakupa ushauri kama ule wa JK aliompa Kagame.

Zungumza na gaidi wako huyo (Zitto) hata kama ameleta madhara kama ya Genocide ndani ya nchi yenu (CHADEMA) na ikibidi sasa mwachie nchi aongoze yeye maana kama umemshirikisha kwenye serikali yako kwa miaka 10 na mmefanya kazi vizuri ni obvious kwamba kijana huyu ni mstahimilivu na ana ngozi ngumu ya kisiasa na atakuwa ameshakomaa kimawazo na kiuzoefu.

Ukichagua kuendelea, kuendeleza au kuanzisha vita basi ni dhahiri vita yenu haiwezi kuisha sana sana mtaathiri wananchi wa nchi yenu bila kujali ni wa kundi gani namaanisha wanaCHADEMA na mwisho wa siku vita hiyo itarithiwa na wengine wajao.

Zitto nawe anza kujiandaa kisaikolojia kusamehe majeraha yote ya kisiasa uliyoyapata katika umri mdogo na yaliyokuwa na lengo la kukumaliza kisiasa kwa sababu ya hofu tu ya wenye mamlaka. Usiweke visasi wala kufuata mfumo wa utawala wa Wanamapinduzi hao ndani ya Chama chako.TUJISAHIHISHE

Ukweli hauui ila unauma. Ukweli haupendi kupuuzwa.

Source Raia Mwema
 
Mboyoyo miiingi but nothing at all!!!Kwa Chadema hatuhitaji chadema mpya bali twahitaji TANZANIA MPYA ili kuikomboa nchi kutoka kwenye mzamo tunaozamishwa na ccm,umeharibu kwa kutaka Kamanda Mbowe amwachie kijiti Mnafki Zito ambaye tumeshamgundua uhusiano wake na mabaradhuli wahafidhina wa ccm-magamba.
 
kinachoendelea ndani ya chama chetu ni maendeleo ya kukuza demokrasia.Ni Mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina,waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa dhidi ya watukuzao siasa majitaka.Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi safi kuikabili.Nitasimama daima upande wa demokrasia-ZITTO ZUBERI KABWE,Mb.WITO NAOMBA TUJADILI KAULI HII BILA HASIRA WALA UCHAMA KWA KUANGALIA NA KILE KINACHOENDELEA NDANI YA CHADEMA
 
Back
Top Bottom